NYUMA YA PAZIA (MAISHA YA ROMAN ABRAMOVICH)
SEHEMU YA 1
Roman Arkadyevich Abramovich ni yatima aliyelelewa katikika umasikini wa kupitiliza na baadae kufanikiwa kuwa moja ya matajiri wakubwa zaidi kuwahi kutokea duniani. Historia yake ni mwanana kabisa kumtia mtu moyo namna ambavyo unaweza ‘kuinuka kutoka mavumbini na siku moja kuketi na wafalme.’ Wazazi wake walifariki angali bado akiwa mdogo kabisa kabisa na hivyo kupelekea yeye kulelewa na nduguze waliokuwa wanaishi kaskazini mwa Urusi kwenye eneo la Komi.
Japokuwa wazazi wake na yeye mwenyewe wameishi maisha yao karibia yote nchini Russia lakini asili yao hasa ni Israel. Babu yake mzaa baba, mzee Nahim Abramovich alikuwa ni mfanyabiashara ambaye aliishi pamoja na mkewe (bibi mzaa baba) Tauba Berkover waliishi wote huko jamuhuri ya Lithuania kwenye jimbo la Taurage. Baba yake Abramovich, Arkady Abramovich alikuwa ni afisa wa serikali katika jamuhuri ya Lithuania. Mama yake Abramovich aliyeitwa Irina Michaleno wazazi wake (babu mzaa mama) Vassili Michalenko na mama yake (bibi mzaa mama) Faina Grutman nao wote waliishi jamuhuri ya Lithuania. Wazazi wake (Arkady na Irina) walifariki akiwa mdogo kabisa… mama yake Abramovich, Irina alifariki Roman akiwa bado mchanga kabisa na baba yake Arkady alifariki kwa ajali ya gari miaka michache baadae. Na ndio hii ilisababisha Abramovich kwa mara ya kwanza kabisa kwenda kuishi Komi kwa nduguze, kaskazini mwa Urusi na baadae Uktah eneo lenye baridi kweli kweli na umasikini uliokithiri.
Katika ujana wake Abramovich aliwahi kujiunga na jeshi kwa muda mfupi sana kabla ya kuacha na kuanza kufukuzia ndoto zake. Kama ilivyo ndoto ya vijana wengi Tanzania miaka ya nyuma “kwenda Dar es salaam kutafuta maisha” ndicho hicho pia kinawakumba vijana wengi duniani kote kutaka kwenda kwenye miji mikubwa ya nchi zao husika, ndicho hiki pia alikifanya Roman… aliondoka Uktah na kwenda Moscow ‘kutafuta maisha’. Akiwa Moscow alifanya akili ya kujiunga na kozi ya masuala ya mafuta na gesi katika taasisi ya Gubkin Institute of Oil and Gas ambako alikuwa anasoma huku akiuza matairi chakavu ya gari ili kuweza kujikimu kimaisha. Akiwa bado anapambana kutafuta nafuu ya maisha hapa Moscow ndipo pia alikutana na mkewe wa kwanza, Olga na kumuoa.
Maisha hayakuwa mepesi sana kwa Abramovich… kipindi hiki ni kipindi ambacho Urusi ilikuwa inapitia kipindi cha mpito mgumu sana wa kiuchumi na kifalsafa. Ni kipindi ambacho ujamaa ulikuwa unadondoka na ubepari kushamiri nchini Urusi. Ni kipindi ambacho Urusi ilikuwa moja ya sehemu hatari zaidi kuishi kutokana na uhuni na ubabe ambao ulikuwa unatokea Urusi na nchi nyingi za Ulaya ya Mashariki. Ni kipindi hiki ambacho nchi za ulaya mashariki zilibatizwa jina la “Wild East”. Abramovich alifanya kila aina ya kazi ya hali ya chini, kuanzia kuuza bidhaa ndogo ndogo mitaani mpaka kuwa makenika kwenye viwanda na hata kuwa ‘bodyguard’.
Waswahili tunasema kwamba “anayejua, anajua tu”, kwamba kuna watu unaweza kuwapa ndimu ukidhani unawakomoa lakini atakushangaza kwa kuikamua na kutengeneza ‘juisi ya lemonade’ na kuinywa kwa raha mustarehe. Ndicho ambacho Roman alikifanya, kuanguka kwa ujamaa na kuibuka kwa ubepari, tena ubepari wa kihuni na ubabe aliona yaweza kuwa fursa adhimu kabisa kwake… akaanza kufanya biashara ya kila namna. Roman akaanzisha biashara ya kuuza midoli… ile biashara ya kuuza tairi chakavu akaikuza zaidi na kuifanya kwa upana na mpaka kuwa wakala rasmi wa tairi mpya kutoka viwandani.
Lakini moja ya biashara ambayo ilimsaidia kumpa ‘connections’ ilikuwa ni pale alipofungua biashara ya kutoa ulinzi binafsi (bodyguards). Pale juu nilieleza kwamba kipindi anaanza maisha Moscow Roman aliwahi kufanya kazi ya u-bodyguard, lakini safari hii sio yeye alikuwa bodyguard bali alikusanya vijana wake kadhaa na kufungua kama kampuni ya kutoa ulinzi kwa wadosi.
Nimesema kwamba hiki ni kipindi ambahi Urusi ilikuwa ni ‘Wild West’, kipindi ambacho uhuni na ubabe ulikuwa ndio namna ya maisha. Kipindi ambacho ujamaa unandoka, serikali ikibinafsisha nyenzo zake za kiuchumi kwa watu wachache. Hapa kwetu Tanzania tumepita pia kwenye kipindi kama hiki hiki na wazee wetu wanajua shurba waliyopitia… anguko la ujamaa na kuibuka kwa ubepari. Kipindi ambacho tulibinafsisha kila kitu na kuacha wake zetu tu. Tofauti ni kwamba hapa kwetu wajanja ambao walibinafsishiwa mali za nchi walikuwa wanashindana ni yupi ambaye atatoa rushwa kubwa zaidi… lakini kule ‘Wild East’ haikuwa rushwa tu pekee… naam, ilikuwa lazima utoe rushwa kubwa kumzidi mwenzako lakini aliyekuwa mtemi na muhuni zaidi ndiye ambaye angeweza kujihakikishia umiliki wa kiwanda au rasilimali husika. ilikuwa ni kula au uliwe. Jifunze kula ‘nyma ya mtu’ au subiri ufanywe kitoweo.
Katika biashara za makampuni makubwa kuna kitu kinaitwa ‘hostile take-over’. Yaani kwa mfano bwana Mo Dewji na kampuni zake za MeTL waanze kuuza hisa za kampuni zake za MeTL Group kwa umma… anakuja mtu ambaye kwa muda mrefu alikuwa anatamani aiweke MeTL mikononi mwake… tumuite mtu huyu Paul (mfano tu). Ananunua hisa nyingi zaidi kumuwezesha kupata ujumbe wa bodi ya wakurugenzi wa MeTL. Kisha anaanza kukaa kwa siri na wanabodi mmoja mmoja na kuwashawishi kumuondoa Dewji kama MD na Mwenyekiti wa bodi … kikao kinaitwa, kura zinapigwa… bodi inamuondoa Dewji kuwa MD na mwenyekiti wa bodi na kumfanya Paul kuwa MD na mwenyekiti mpya wa bodi. Dewji anabakia kuwa mwanahisa tu wa kawaida kama wengine bila uwezo wowote wa kimaamuzi juu ya kampuni yake ambayo aliinzisha. Hii inaitwa ‘hostile take-over’. Lakini kipindi hicho huko ‘Wild East’, Urusi ya miaka hiyo walikuwa na namna ya tofauti ya ‘Hostile Take-over’. Tajiri mwenzako anakuvizia, anakuteka… anakutesa mpaka unasaini makaratasi. Kisha anakutandika risasi na kesho yake inatangzwa kuwa kampuni/kiwanda chako ni chake na mliuziana kwa maandishi na nyaraka anazo. Wiki moja baadae mwili wako unaokotwa jalalani and nobody cares, maisha yanaendelea… Wild wild East.!!
Katika mazingira kama haya ambapo miili ya matajiri, waandishi wa habari na hata viongozi wa kisiasa ilikuwa inaokotwa kila siku imetupwa mitaani unaweza kupata picha ni kwa namna gani ambavyo biashara ya u-bodyguard iliweza kushamiri. Matajiri walikuwa na hofa na maisha yao muda wote, kwa hiyo walihitaji ulinzi muda wote. Biashara ya Roman ikashamiri.
‘Dili’ hizi za kulinda matajiri na bishara zake za hapa na pale zilimpa ‘connection’ na kusaidia kujuana na watu muhimu ndani ya Moscow. Moja ya watu hawa muhimu ambaye baadae alikuja kuwa kama ‘mentor’ wake alikuwa ni Boris Berezovsky Mwanamahesabu nguli na mhadhiri wa chuo kikuu ambaye alikacha kufundisha chuo na kugeukia biashara ili asipitwe na upepo wa utajiri uliokuwa unavuma Urusi kipindi hicho.
Berezovsky alikuwa ni moja ya ma-Olygarch wa kwanza kabisa ndani ya Urusi. Nimeeleza pale mwanzoni Oligarchy ni watu wa namna gani. Borozevsky alikuwa ni moja ya matajiri wakubwa zaidi Urusi kipindi hicho ambaye alinufaika sana na ubinafsishaji wa mali za umma. Oligarch Boris Berezovsky hakuwa tu Oligarch bali alikuwa ni sehemu ya ma-Oligarch wachache ndani ya Urusi ambao waliojulikana kama ‘The Family’.
The Family ilikuwa ni ‘inner circle’ ya watu wachache sana ambao walikuwa karibu na Rais wa Urusi kipindi hicho Boris Yeltsin. Watu hawa walikuwa ni wanafamilia wa Yeltsin pamoja na matajiri wachache sana akiwemo Berezovsky. Kikundi hiki cha matajiri wachache pamoja na familia ya Rais ndio kiuhalisia ndio walikuwa wanaendesha nchi.
Kwa hiyo kitendo cha Abramovich kujiweka karibu na Berezovsky ilimaanisha kwamba alikuwa amefanikiwa kujenga urafiki na moja ya watu muhimu zaidi ndani ya Urusi na mwenye ushawishi ndani ya inner cirle ya Rais.
Watu wenye asili ya uyahudi twaweza kuwachukia na kuwasema tutakavyo kwa uonevu ambao labda wanaufanya… lakini jambo moja ambalo hatuwezi kubisha ni uwezo wao wa asili kiakili na kimkakati. Japokuwa Abramovich kwa kipindi hicho alikuwa ni mrusi tu lakini kuna damu ya kiyahudi ilikuwa ndani yake na ni wakati huu ambao alidhihirisha umahiri wake kimkakati.
Baada ya urafiki wao Abramovich na Berezovsky kukomaa na kushibana, Abaramovich alimuomba Berezovsky amsaidie kumtambulisha kwa watu muhimu Kremlin. Moja kwa moja Berezovsky akahisi labda Abramovich anataka kutambulishwa kwa Rais au mawaziri na akamjibu bado hajafikia ngazi ya kutambulishwa kwa watu hao… lakini Abramovich akamwambia hapana haitaji kutambulishwa kwa Rais au mawaziri… anahitaji kutambulishwa kwa mtu anaitwa Valetin Yumachev ambaye kipindi hicho alikuwa ni afisa wa kawaida tu wa Ikulu kitengo cha habari na maelezo na hukuwa na ushawishi kwa Rais Yeltsin. Berezovsky alishangaa maana Yumachev hakuwa na ushawishi wowote ule pale Kremlin.
http://pseudepigraphas.blogspot.com/
Ndio hapa ambapo nasema kuna watu ni ‘born tacticians’… akili yao inawaza kimkakati kwa kila hatua na moja wapo ni huyu Abramovich. Abramovich alielewa wazi kabisa hawezi kutambulishwa kwa Rais na japo alikuwa na tuhela tudogo twa kubadili gari na nyumba lakini ukilinganisha na ma-Oligarch kipindi hicho yeye alikuwa ni kidagaa tu, ‘hohe hahe’ ambaye hawezi hata kukaa meza moja na rais. Lakini anaitaka hiyo connecvtion kuliko kitu chochote kile ili afike pale anapopataka kimafanikio. Ndipo hapa ambako aliona kitu ambacho wengine hawakukiona… Valentin Yumachev, afisa habari mdogo wa Ikulu. Abramovich aligundua kwamba Yumachev alikuwa na mahusiano ya siri ya kimapenzi na binti wa Yeltsin aliyeitwa Tatyana. Binti huyu wa Rais pia alikuwa anapendwa mno na baba yake na alikuwa moja ya watu anaowasikiliza sana na kuwaamini.
Abaramovich akapiga hesabu zake… kama akiweza kujenga urafiki wa kushibana na Yumachev, na kisha kufanya uhusisano wa Yumachev na Tatyana ukue na hatimaye labda kuoana. Maana yake ni kwamba atakuwa ni rafiki wa mkwe wa Rais wa Urusi. Na kutokea hapo kujiweka karibu na Rais kupitia mgongo wa ‘best friend’ wake itakuwa ni rahisi kama kusaga maini.
Berezovsky akamtambulisha Abramovich kwa Yumachev. Hata Yumachev mwenyewe akashangaa… ‘mtoto wa mjini’ Abramovich ambaye ni rafiki wa ma-Oligarch kutambulishwa kwake. Kwa hiyo hata urafiki ukakua kwa haraka sana Yumachev kuona ni heshima kubwa kwake kwa mtoto wa mjini kama Abramovich kumthamini na kumuona ana umuhimu.
Lakini Abramovich alikuwa anaiona ‘potential’ ndani ya Yumachev ambayo hata mwenyewe alikuwa haioni… Abramovich alikuwa anaona miaka mitano mbele ambayo wengine walikuwa hawaioni…
Kipindi hiki ambacho nimeeleza kwamba Abramovich aliomba kutambulishwa kwa Yumachev, Abramovich alikuwa ni kijana mdogo tu wa umri wa miaka 28. Kutokana na urafiki wao wa kushibana na Berezovsky, Berezovsky alimtambulisha Abramovich kwa Yumachev bila kusita. Nimeeleza kwamba kipindi hicho Yumachev alikuwa ni afisa habari tu wa Ikulu lakini hakuwa na ushawishi wowote kwa Rais Boris Yeltsin.
Lakini baada ya urafiki wa Yumachev na Abramovich kukolea… Abramovich akaanza ‘kumuazima akili’ Yumachev. Kumuonyesha ni kwa namna gani uhusiano wake wa kimapenzi na mtoto wa Rais wa nchi kama akichanga karata zake vyema uhusiano huo unaweza kumuinua kutoka mavumbini kwenye uafisa habari wa ikulu na pengine kumfanya kuwa moja ya watu muhimu zaidi kwenye ‘inner circle’ ya Rais Yeltsin.
Yule binti wa Rais ambaye Yumachev ana uhusiano naye wa kimapenzi hakuwa binti tu legelege wa kula mkate kwa siagi mezani… binti huyu alikuwa ni moja ya washauri wakuu wa Rais Yeltsin. Alikuwa ni moja ya watu wenye kuaminiwa zaidi na Rais. Sasa ambacho Abramovich alikuwa anakifanya ni kumpa mikakati ya Yumachev na kisha Yumachev anakwenda kushauriana na Tatyana na kisha wanaenda kumshauri Rais. Kadiri muda ulivyokuwa unakwenda Yumachev akaanza kuonekana kwamba naye ni mtu mwenye bongo makini na mwenye kujua mikakati. Si miezi mingi, Yeltsin akamapandisha cheo Yumachev akamfanya kuwa ‘Head of Adminstration’ wa Ikulu, cheo ambacho kwa kipindi hicho nchini Urusi kilikuwa adhimu mno. Si hapo tu kwa ushauri wa Abramovich Yumachev akamuoa kabisa Tatyana. Hapo ndipo hasa pale ambapo Abramovich alikuwa anapataka.
Kwa pamoja Abramovich, Yumachev na safari hii pamoja na Tatyana urafiki wao ukaota mizizi haswa. Kutokana na ukaribu huu wa Abramovich na Afisa mkuu wa masuala ya utumishi Ikulu na nchi pamoja na ukaribu na binti wa rais ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais moja kwa moja Abramovich akatambulishwa na ‘marafiki’ zake hao wawili kwa Rais Yeltsin na kutokana na uwezo wake wa hali ya juu wa kimikakati na kufikiri, Abramovich hakuchukua muda sana akawa sehemu ya ‘The Family’.
Nilieleza pale mwanzoni kuhusu ‘The Family’, ile inner circle ya Rais Yeltsin ambayo ilikuwa inaundwa na wanafamilia ya Rais pamoja na ma-Oligarch wa Urusi. Hii ‘The Family’ ndio hasa ilikuwa inaendesha nchi ya Urusi kipindi kile. Sasa baada ya Abramovich kuwa sehemu ya ‘The Family’ kukaibuka inner circle ndani ya Inner circle. Yaani kwamba kwenye wale watu wachache ambao walikuwa wanaaminiwa mno na Rais Yeltsin (The Family) kukaibuka kikundi cha watu wachache zaidi kati yao The Family ambao walikuwa wanaaminiwa zaidi na Rais uzidi wengine wote, ndio hapa nasema inner circle ndani ya inner circle. Watu hawa walibatizwa jina la “Utatu Mtakatifu” na utatu huu mtakatifu walikuwa Abramovich, Yumachev na Tatyana.
Kijana yule yatima, aliyekimbia umasikini kutoka kwenye maisha ya kulelewa na ndugu zake jimboni Komi, ati leo hii akiwa na miaka ishirini na nane tu anaketi meza moja na moja ya binadamu mwenye ushawishi na nguvu zaidi duniani, Rais wa Urusi na tena anaketi akiwa moja ya watu ambao Rais anawaamini sana na kuwasikiliza sana.
Ndani ya hii ‘The Family’ Abramovich alipachikwa jina la ‘Family Wallet’. Hii ni kutokana na kutumiwa sana na Rais Yeltsin na familia yake kwenye usimamizi wa masuala yao ya fedha na utajiri wao.
Nimeeleza, wakati huu ndipo ambapo Ujamaa ulikuwa umedondoka na Ubepari kuanza kushamiri… kwa hiyo kwa wanasiasa na wazee ambao wamekuwa kwenye maisha ya kijamaa hawakuwa na uelewa mpana sana wa namna ambavyo mizania ya kibepari inavyofanyakazi. Lakini Abramovich alikuwa ni mfanyabiashara japo hata kama alikuwa akiuza midoli na matairi, amekulia mtaani akijua ni namna gani kanuni za ‘natural selection’ zinafanyakazi… vyenye nguvu vinakula dhaifu… na zaidi ya yote Roman alikuwa na uwezo wa kuzaliwa wa kiakili, mikakati na ‘kujiongeza’. Kwa hiyo akatumia ujuzi wake huu kushauri familia ya Rais namna bora zaidi ambavyo wanaweza kutunza utajiri wao… akaanza kuwafundisha na kuwezesha familia ya Rais Yeltsin kufungua offshore accounts, uwekezaji kwenye masoko ya hisa, kufungua offshore companies ambazo wamiliki wanafichwa kwenye mifumo ‘complex’ kujua nani hasa ni mmiliki na mambo mengine mengi ya kibepari. Kwa maneno mengine Abramovich alikuwa anawafungua macho namna ya ‘kuiba’ na kuficha fedha za umma kisasa katika namna ambayo ni ngumu kujulikana na namna za uhakika zaidi kwa fedha hizo kuwa salama.
Urusi ilikuwa inabadilika haraka mno… kutoka kuwa mpigia chapuo mkuu wa Ujamaa duniani na kuwa nchi ya kibepari tena ubepari wa kihuni kabisa. Japo suala la ubinafsishaji wa makampuni ya umma kwenda kwenye umiliki wa watu binafsi lilipongezwa sana na nchi za magharibi wakiona kama hatua nzuri ya nchi hiyo kuhama kutoka kwenye uchumi unaoshikiliwa na dola na kuanza kwa ‘soko huru’ la kiuchumi ndani ya Urusi lakini wananchi wa Urusi hawakuona kile ambacho wadosi hawa wa magharibi walikuwa wanakiona. Wananchi walikuwa na hasira wakihisi kwamba nchi yao na uchumi unaganywa kwa kikundi cha watu wachache huku wao wakiendelea kuteseka na hali duni za kimaisha.
Kipindi cha ubinafsishaji wa makampuni ya umma kuna jambo mojaambalo mwanzoni lilikuwa jema lilikuwa limefanyika kabla ya kugeuka shubiri mbeleni.
Kila mwananchi alipewa ‘voucher’ yenye thamani ya fedha ya Urusi rouble 10,000. Lengo la vocha hii ilikuwa ni kuwapa nafasi kila mwananchi wa urusi kumiliki hisa kwenye kampuni za serikali ambazo zilikuwa zinabinafsishwa. Kivipi? Yaani kwamba kampuni ya serikali ikiwa inauzwa na ikatangazwa kwamba kampuni hiyo ina thamani ya kiasi fulani cha fedha… ni kweli watajitokeza matajiri ambao watanunua hisa nyingi zaidi lakini bado mwananchi wa kawaida alikuwa anaweza kupeleka vocha ile ya rouble elfu kumi na akanunua hisa zenye thamani ya vocha hiyo.
Lakini kwenye miti hapana wajenzi na mtu aishiye mwituni ambaye hajui thamani ya almasi siku akiishika hawezi kuona tofauti yake na kokoto, aweza kuipiga kwenye manati kama jiwe ili aue ndege chiriku akafanye kitoweo. Ndicho ambacho kilitokea Urusi. Nchi ilikuwa ndio kwanza ilikuwa imetoka kwenye ujamaa… wananchi hawakuwa wanajua namna gani hasa ubepari unafanyakazi. Nini kilichotokea? Wajanja wachache wakawa wanatuma mawakala wao vijijini na mijini kwa wananchi… wanawashawishi wananchi wawape vocha na wao wanawapa fedha tasilimu. Karibia kila mwananchi alikuwa anakubali. Anatoa vocha yenye thamani ya rouble 10,000 alafu yule ajenti anampa labda rouble 200 cash. Unaweza kujiuliza wananchi hawa walikuwa vichaa au?? Hapana… maarifa… maarifa… fikiri mwananchi huyu amezaliwa na kukulia kwenye ujamaa. Leo hii ati unampa kipande cha karatasi unamwambia kina thamani ya pesa (wakati yeye anaona ni karatasi tu) alafu unamwambia atumie karatasi hiyo kwenda kununua hisa za kampuni (hajui hata hisa ina maana gani zaidi ya kusikia tu kwenye rediio inatajwa tajwa)… alafu unamueleza akiwa na hisa kwenye kampuni fulani siku moja inawezekana labda (hakuna uhakika) kama kampuni hiyo husika ikianza kutengeneza faida atalipwa ‘dividends’ (dividends ndio ‘mdudu’ gani). Unaweza kuona mnyumbuliko wa mawazo ya mtu huyu aliyekulia kwenye ujamaa? Yawezekana hata sisi tungekuwa kwenye nafasi zao tungeuza vocha ya thamani ya rouble elfu kumi kwa rouble 200 cash tukale wali na nyama tushibe, tulale, tuamke tuanze kuhangaika tena kesho.
Na hii imetokea hata hapa kwetu nchini tena juzi juzi tu hapa… unakumbuka kipindi cha ruzuku ya pembejeo za kilimo za serikali katika utawala wa Mzee Kikwete? Watu walikuwa wanauza vocha kwa shilingi elfu kumi tu alafu wale mawakala wanapeleka NMB wanalipwa laki na sitini kwa kila vocha au zaidi.!! Yale yae, almasi kuiona kokote…
Sasa pale Urusi wajanja wachache sana walinunua hizi vocha na na kuzitumia kununua hisa za makampuni yaliyokuwa yanabinafsishwa… makampuni ya mafuta, gesi asilia na kadhalika. Ndipo hapa kukaibuka matajiri wale ambao nilisema wakabatizwa jina ma-Oligarch. Mbaya zaidi Yeltsin akawaweka karibu mno ma-Oligarch akishirikiana nao kuendesha nchi.
Wananchi walikuwa na hasira kweli kweli na Yeltsin
Umaarufu wa kisiasa wa Rais Yeltsin ulikuwa umeshuka mno kupitiliza. Ukichangiwa pia kwa sehemu nyingine kutokana na matatizo ya moyo mara kwa mara akipatwa na mshituko na kufanyiwa upasuaji na kumfanya asionekane sana kwa umma.
Ukafika mwaka 1996… mwaka wa uchaguzi mkuu wa Urais. Kila mtu alikuwa anasubiri kusikia Yeltsin atamtangaza nani kama mgombea kwenye chama chake maana hakuna ambaye alikuwa anadhani kwamba Yeltsin atagombea tena maana umaarufu ulikuwa umeporomoka mno, wananchi wanamchukia na afya yake ilikuwa mgogoro.
Ajabu ni kwamba mwezi February mwaka huo 1996 Yeltsin akatangaza kwamba atawania muhula mwingine wa uonngozi. Vyama vya upinzani vilishangilia maana walijua kwamba ushindi wa kishindo uko barazani kwao.
Kabla ya kupiga kura mwezi Desemba, katikati ya mwezi July yalitolewa matokea ya kura za maoni na mgombea wa chama cha Upinzania cha Kikomunisti Bw. Gennady Zyuganov alikuwa anaongoza kwa asilimia nyingi akimuacha mbali kabisa Rais Boris Yeltsin.
Kambi ya Rais presha ikawapanda… paniki ikiwatawala. Kila mti unateleza. Hakuna mwenye kujua wafanyeje… waliona kabisa wanaelekea kuupoteza ‘mnofu’ wao. Nani awaokoe?
Pale mwanzoni niliandika kwamba… a born tactician, haijalishi ni mazingira gani utamuwekea lazima apate namna ya ‘ku-survive’, lazima aone upenyo mwembamba wa shaba kwenye giza totoro. Mpe limao ukidhani unamkomoa, ukirudi baadae utakuta amelikamua na kutengeneza juisi ya ‘lemonade’ akinywa kwa starehe kabisa. Hivi ndivyo ambavyo Roman Abramovich akili yake inanyumbulika… wakati ambapo timu nzima ya Rais Yeltsin imepaniki hawajui nini cha kufanya yeye aliona hiyo ndio fursa kwake kumdhihirishia Boris Yeltsin kwamba kichwa chake kimebeba mbongo ambayo sio ya mchezo mchezo…
Uchaguzi ulikuwa unakaribia, wananchi walionekana dhahiri wanaegemea upande wa mkomunisti Zyuganov. Taarifa hii si kwamba ilikuwa mbaya kwa Rais Boris Yeltsin pekee bali pia na genge lake lote la “The Family” kwa sababu ilikuwa dhahiri kwamba kama ikitokea mkomunisti Zyaganov akichukua nchi kitu cha kwanza ambacho angekifanya ni kurejesha serikalini viwanda na makampuni yote ambayo yalikuwa yamebinafsishwa na Rais Yeltsin kwa watu binafsi.Hakuna ambaye alikuwa na jawabu kichwani wa nini hasa wakifanye kunusuru kile ambacho kilikuwa kinaelekea kutokea… baadhi ya watu kwenye inner circle wakamshauri Rais Yeltsin afute uchaguzi na atawale nchi kidikteta. Lakini hili lilikuwa ni wazo la kipuuzi kabisa labda kutokana na maji kuwafika shingoni maana mfumo huu ulikuwepo Russia huko mwanzoni miongo kadhaa nyuma na ukafeli na kudondoka.
Wakati ambapo kila mtu akiwa amechanganyikiwa na kutoa mawazo yasiyo na mbele wala nyuma kuleta auheni yoyote ndipo ambapo Abramovich akaingilia kati. Akakaa mstari wa mbele na kushika usukani wa mikakati ya uchaguzi kambi ya Rais Yeltsin. Russia ilikuwa imetoka kwenye ujamaa na ubaya ni kwamba ile akili ya kijamaa bado ilikuwa haijawaisha. Kama wasemavyo, unaweza kumtoa kijana kutoka ‘nanjilinji’ kuja mjini lakini kamwe huwezi kuitoa ‘nanjilinji’ akilini mwa huyo kijana. Nchi ilikuwa imeingia kwenye ubepari lakini wazee bado walikuwa wanawaza na kufanya mambo yao kama wajamaa. Abramovich akataka kuwaonyesha namna ambavyo chaguzi zinafanyika kwenye nchi za kibepari.
Kwanza akamshawishi Rais Yeltsin amfute kazi meneja kampeni wake. Kisha nafasi hiyo akashauri apewe mtoto wa Rais Tatyana. Kwa nini? Kwanza kwasababu Tatyana atakuwa na uchungu zaidi na kampeni hiyo kwa kuwa ‘ana kitu cha kupoteza’ kama wasiposhinda. Lakini pia kama ambavyo nilieleza kuwa Tatyana hakuwa binti legelege wa kula mkate kwa siagi tu, bali alikuwa ni mpambanaji haswa. Lakini tatu Abramovich alitaka Tatyana ashike wadhifa wa meneja kampeni kwa kuwa alikuwa rafiki yake na walau alikuwa kwa mbali Tatyana alikuwa ameanza kuwaza nama ambavyo yeye Abramovich anawaza. Wanasema ukikaa karibu na waridi lazima unukie.
Kisha Abramivich akafanya kitu ambacho kwa kipindi kile nchini Rusia hakikuwa kimezoeleka sana japo kwa nyakati zetu hizi twaweza kuona ni cha kawaida. Abramovich akatengeneza mkakati wa namna ya ‘kucheza’ na media
Jambo moja ambalo tunapaswa kulifahamu ni kwamba katika kipindi hiki kutokana na udhaifu mkubwa wa mbinu za uongozi za Yeltsin, uchumi wa Russia ulikuwa umeyumba sana kiasi kwamba mpaka serikali ilikuwa imechacha kweli kweli. Serikali kwa kipindi hicho ilikuwa inajiendesha kwa kutumia fedha za mkopo dola bilioni kumi ambazo serikali ilikuwa imekopeshwa kutoka IMF.
Sasa basi, vituo vya televisheni vyote ambavyo awali vilimilikiwa na serikali vilikuwa navyo vimebinafsishwa. Kwa hiyo hata serikali ikitaka kurusha matangazo walikuwa wanapaswa kulipia. Lakini serikali ilikuwa imechacha.
Abramovich akaitisha kikao maalumu na watu ambao walikuwa wamebinafsishiwa vituo vya habari nchini Russia na hata wale ambao wamejitutumua kuanzisha vya kwao wenyewe. Abramovich alikuwa na ombi moja tu kwao… waache kurusha habari yoyote kumuhusu Zyuganov, mpinzani mkuu wa Yeltsin ambaye alikuwa anaongoza kwenye kura za maoni na badala yake vyombo vyote vya habari virushe habari kuhusu kampeni za Rais Yeltsn.
Abramovich akawaeleza kwamba atafanya kila namna mpaka Rais Yeltsin ashinde kiti cha Urais na akishashinda ‘atawakumbuka’ wamiliki hao wa vyombo vya habari kwa hicho walichokifanya.
Hakuna mmliki yeyote wa chombo cha habari ambaye alikataa ‘ofa’ hiyo. Hakuna ambaye hakutaka ‘kukumbukwa’ pindi ambapo Yeltsin akishika muhula mwingine.
L
Katika kundi hili la wamiliki wa vyombo vya habari ambao Abramovich alikuwa anamlenga hasa alikuwa ni swahiba wake wa zamani Berezovsky. Yule Oligarch ambaye alimtambulishaga kwa Yumachev. Berezovsky alikuwa anamiliki ‘media house’ ambayo ndiyo ilikuwa ina ushawishi kuliko vyombo vingine vyote. Sio tu kwamba alikuwa amemlenga kwa kuwa alikuwa na media house yenye nguvu zaidi, Abramovich alikuwa na wazo lingine la siri zaidi, wazo mwanana kabisa ambalo kama likitimia basi laweza kumfanya ghafla kuwa moja ya watu matajiri zaidi nchini Russia na duniani. Nitaeleza baadae…
Kampeni ikaendelea… kufumba na kufumbua, kila televisheni, kila redio, kila gazeti kila siku kukicha kulikuwa na habari moja tu, Boris Yeltsin, Boris Yeltsin, Boris Yeltsin. Tofauti na ambavyo Yeltsin alikuwa amezoeleka kwamba sio ‘mtu wa watu’ lakini ghafla Yeltsin alionekana akiwa na haiba nyingine mpya kabisa. Kila siku yuko mahala fulani… leo ametembelea shule fulani ya upili Moscow, kesho yuko sokoni akisikiliza shida za wachuuzi, kesho kutwa yuko kiwanda fulani akila chakula cha mchana na wafanyakazi. Warusi walishuhudia Yeltsin mpya ambaye hawakuwahi kumuona. Yeltsin akaongeza ruzuku kwa wanafunzi, akatoa fedha nyingi kutoka serikalini mabilioni kwa ajili ya kuwalipa pensheni wazee. Na kila hatua, kila kitu haijalishi ni kikubwa au kidogo ndogo kiasi gani kiliripotiwa na kila chombo cha habari nchini Russia
Vyombo vya habari vilimpamba kwa kila namna ambayo waliweza huku wakiwaeleza wananchi kwamba wakimchagua Zyuganov kutokana na sera zake zinaweza kuifanya Urusi kuingia kwenye vita
Mara moja mikutano ya kampeni ya Yeltsin ikaanza kujaa watu kwa mafuriko. Yeltsin akageuka kuwa ‘sweetheart’ wa Warusi wote. Katika mikutano Yeltsin aliongea kama mtu muungwana tofauti na kawaida yake ya kufokafoka kama jendaheka. Aliongea kwa ustaarabu na kumwaga ahadi kedekede.
Siku ya uchaguzi ikawadia, December 5, 1996. Kura zikapigwa. Siku moja mbele matokeo yakatangazwa… Boris Yeltsin alikuwa ameshinda kti cha Urais kwa kupata 52% ya kura zote zilizopigwa. Yaani kama mtu alikuwa amelala usingizi miezi mine nyuma na kuamka siku hiyo umwambie Yeltsin alikuwa amemshinda Zyuganov angeweza kukuona ni mwendawazimu.
Yaani ndani ya miezi mine tu, ‘adacadabra’ za mikakati ya Abramovich zilikuwa zimebadili mioyo ya warusi kumchukia Yeltsin na sasa kuwa ‘sweetheart’. Ilikuwa nikitu ambacho hata Yeltsin mwenyewe hakutegemea.
Baada ya Yeltsin kuapishwa kushika muhula mwingine wa uongozi watu wa kwanza kuhakikisha wanapata ‘mnofu’ mnono zaidi walikuwa ni ule Utatu Mtakatifu. Tatyana, Yumachev na Abramovich. Tatyana akateuliwa na baba yake kuwa rasmi mshauri wake mkuu. Yumachev akateuliwa kuwa katibu Mku Kiongozi… na Abramovich… naam Abramovich akateuliwa kuwa nani? Waziri Mkuu? Hapana… Waziri wa Mambo ya Nje? Hapana… Waziri wa Ulinzi? Hapana… aliteuliwa kuwa nani?
Abramovich alikataa kupewa nafasi yoyote ile ndani ya serikali. Uwendawazimu? No… Abramovich, a born tactician… anaona kile ambacho wengine hawakioni.
Alimweleza tu Yeltsin kwamba ameshiriki namna ile katika uchaguzi na kuhakikisha anashinda kwa kuwa anampenda Yeltsin kama baba yake kabisa na anadhani ndiye mtu sahihi zaidi kuingoza Russia.
Moyo wa Yeltsin ukamomonyoka na kububujikwa kabisa… hakika huu ni upendo wa kuzidi kipimo, mtu anakupigania kwa jasho na damu ushinde kiti cha Urais alafu hataki umlipe kwa kumpa cheo chochote? Yeltisn akajihisi kama amepata mtoto wa kiume ukubwani… tena mtoto mtiifu na mwenye kumpenda baba yake.
Japokuwa kipindi hiki Abramovich hakuwa tajiri kabisa hata kidogo kama tumjuavyo sasa, lakini Abramovich alikuwa anajua ni nini anakitaka… hakutaka papara ya kurukia vyeo vya serikali… alijua lengo lake hasa liko wapi. Kila kitu sasa kilikuwa kiko sawa, mkakati wake umeenda vile ambavyo alikuwa amepanga. Kitu pekee alichohitaji sasa ilikuwa ni subira… naam, subira… subira ni ‘necessary ingredient of genius’.
Akasubiri serikali iundwe. Wagawane vyeo. Walioukwaa uwaziri na ukuu wa maidara washerehekee na kupongezana, kisha aingie ‘kazini’.
Miezi kadhaa ikapita… serikali mpya ikiwa imeshaundwa na imetengemaa na inafanyakazi zake kama kawaida. Huu sasa ulikuwa ni wakati muafaka aliokuwa anausubiri.
Siku hiyo miezi ya mwanzoni kabisa mwa mwaka 1997 akampigia simu yule swahiba wake wa zamani, Bw. Berezovsky. Yule jamaa mwenye media house yenye nguvu zaidi kipindi kile nchini Urusi, ambaye pamoja na wamiliki wengine wa vyombo vya habari kipindi kile cha kampeni Abramovich aliwaomba wamsaidie Yeltsin kushinda kiti cha Urais na kuwaahidi Yeltsin atawakumbuka kwenye utawala wake.
Alipompigia simu na Berezovsky kumuuliza wanakutana kwa lengo gani…. Akamjibu jibu moja tu kwamba, “muda wa Rais kuwakumbuka umewadia.!”
Boris hakujua na hakuna ambaye angeweza kujua zaidi ya Abramovich mwenyewe kwamba, ndani ya wiki chache baada ya simu hiyo Abramovich alikuwa anaelekea kuwa moja ya binadamu mwenye utajiri mkubwa zaidi juu ya uso wa dunia.
Baada ya kikao hicho muhimu kati ya Berezovsky na Abramovich kufanyika na mambo ya siri kukubaliana… hatimaye ukasubiriwa utekelezaji.
ITAENDELEA...
Your Thoughts