Ngoma Ngumu 10

RIWAYA; NGOMA NGUMU.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SIMU; 0758573660/0624155629.

 SEHEMU YA KUMI..



Miguu ya kuku alimuona vema mwenyeji wake namna alivyokuwa akipaparika kuwahi mlangoni. Kwake hiyo ilikuwa ni turufu adhimu kabisa ambayo aliingoja kwa muda mrefu sana. Aligeuka kwa kasi ya upepo, kisha alijifyatua mzimamzima na kwenda kumkumba mwenyeji wake. Kitendo kile kilifanya wapige mweleka bila kutarajia, lakini muonguko wao haukumzuia Miguu ya kuku kuwahi kujinyanyua na kumtandika mwenzake kiwiko cha pua na kumpasua mwamba wa pua. Fundi alitaka kupiga kelele, lakini alijikuta akishindwa baada ya ngumi nzito kujaa chini ya kidevu na kumfanya ang'ate ulimi wake bila kupenda. 

Fundi alipigwa mapigo ya harakaharaka ambayo hakujua yalipigwa kwa mtindo gani, bali alijikuta akichakaa huku akiwa hajapewa nafasi ya kuinuka chini. Lakini kikubwa hakujua anapigwa kwa sababu gani. 

  Miguu ya kuku baada ya kumlainisha mwenyeji wake, haraka alimnyanyua na kumkaliza kwenye kiti na kumtazama kwa sekunde kadhaa, kisha akasema…

“Nitakuacha endapo ukinipa ushirikiano wa kile ninachokihitaji.” Alinyamaza na kumtazama Fundi ambae alikuwa anapumua kwa tabu huku mawasiliano ya ubongo wake, yakiwa hayapo sawasawa.

“Leo ulienda kufanya nini kwenye benki ya Umoja?” Alimuuliza.
Fundi alikaa kimya huku akipeleka macho yake kushoto kwake, akimaanisha hahitaji kuulizwa lolote. 
Alifanya hivyo akiwa hajui alikuwa anakabiliana na mtu wa aina gani na laiti angelijua, asingehangaika kuficha lolote.

  Miguu ya kuku hakutaka kupoteza muda alitoa mkasi wake na kuinua juu, kisha aliushusha pajani mwa Fundi bila huruma. Fundi alitaka kupita kelele, lakini alitandikwa kofi zito lililomtoa kwenye mstari wa upigaji kelele. Alibaki akiwa amezubaa na asielewe alichokuwa anafanyiwa na yule jamaa.

“Nakuuliza tena kwa mara ya mwisho. Ulienda kufanya nini?”
. Fundi alichagua kukaa kimya. Lakini uchaguzi wake haukudumu, alijikuta akiropoka bila kupenda kile alichoulizwa baada ya mkasi uliokuwa umesimama kwenye nyama za upaja wake, kuchezeshwa mara kadhaa kitendo kilichomfanya ahisi ubongo wake unataka kuchomwa moto.

“Nilienda kurekebesha Kuba.” 

Miguu ya kuku alimtizama kwa sekunde kadhaa, kisha akamuuliza…

“Kuna Kuba ngapi kwenye hicho chumba ulichoingia?”

“Ipo moja tu!”

“Ulinzi wake upoje?”

“Ni wa kisasa sana.”

“Mifumo ya ulinzi wa kibenki unayo kwenye kompyuta zako?”

“Ndiyo ipo.”

Haraka aliruka ilipokuwa kompyuta na kuanza kubofya hapa na pale, huku akimuuliza fundi baadhi ya vitu alivyoshindwa kuvielewa. Alifanikiwa kupata kile alichokihitaji, haraka alisoma kwa umakini na kukariri kila alichoona kwake in muhimu, kisha alifunga kompyuta na kumgeukia yule jamaa.

“Hiyo Kuba ina nini zaidi ya pesa?”

“Ina pesa tu. Haina cha ziada.”
Baada ya kupewa hilo jibu, alimnyanyua yule jamaa na kumtwanga kichwa kizito kilichomtoa ufahamu, kisha alimwacha aende chini kama kiroba cha mzigo. Alichukua mkasi wake na kuutia mfukoni, kisha alijiweka sawa na kuondoka ndani ya ofisi. Alienda hadi mapokezi na kuaga kama hakuwa yeye aliyetoka kuadhibu mtu. 
Alitoka nje ya ofisi za Jatu na kuelekea alilokuwa ameacha gari alilokuwa anatumia.

 Alipofika ndani ya gari alichukua simu yake na kumpigia Susa.

“Umefanikiwa kuonana nae?” Alimuuliza.

“Ndiyo!” Susa alijibu.

“Umemwambia kuhusu fununu za wizi wa benki?”

“Ndiyo. Na amepagawa sana hapa anapiga simu hovyo kwa wakubwa zake.”

“Ok! Sasa naomba ufanye jambo moja hivi..” Alinyamaza kidogo baada ya kuhisi tena amewekwa kwenye sauti kubwa. Alitasamu na kuendelea..

“Mwambie akupe taarifa za ulinzi pale benki, pia mwambie achukue vitambulisho na kadi zangu za benki kwa kaimu Meneja wa benki. Fanya uwezavyo umshawishi avichukue hivyo vitu. Akishachukua nambie nikupe mpango wa mwisho anaotakiwa kutusaidia huyo boya.” 

“Sawa boss!” Susa alisema na simu ilikatwa.

 Miguu ya kuku baada ya kukata simu, alibaki akitabasamu peke yake. Alikuwa ameamua kumlisha taarifa butu Sajini Nyau, kisha alitaka taarifa hizo zimkombolee vitambulisho vyake kwa Kaimu Meneja. Hakutaka kukutana na Kaimu Meneja pale benki, kwa kuwa alijua hadi kufikia ahsubuhi atakuwa Wanted ndani ya jiji la Nairobi. Aliamini hivyo kwa sababu ya kitendo alichokifanya kwenye ofisi za Jatu. Alijua ni lazima mamlaka husika zianze kumwinda usiku na mchana.
 Jambo la kwanza alilohitaji kufanya ni kwenda hadi Kama hoteli, kisha achukue mizigo yake yote na kutokomea anakokujua huku akijipanga kuingia ndani ya ofisi za usalama wa nchi kuiba plate namba tano. Kwa haraka alishagundua hakukuwa na hizo plate kwenye Kuba za benki, bali zitakuwa zinalindwa kwenye Kuba zilizoko chini ya jengo lile.

 Yeye alihitaji kujua mlango wa kuingilia huko tu na wa kumwonesha mlango ulipo, atakuwa ni Meneja wa benki ya Umoja, ambae hakuwa akimfahamu hadi wakati huo. 

“Wa kunifikisha kwa Meneja ni huyo Kaimu Meneja.”Alijisemea wakati akiingia kwenye maegesho yaliyokuwa kando kidogo ya hoteli aliyofikia.

 Alishuka haraka na kuangaza huku na huko alipohakikisha kila kitu kipo sawa, alipiga hatua kuelekea ndani ya hoteli. Alipita mapokezi na kuchukua funguo kisha alielekea ndani ya chumba chake. 
Alipotokeza ndani ya chumba chake, aligundua kuna kiumbe alikuwa ameingia pale ndani na kukagua baadhi ya sehemu. Alitabasamu na kuanza kukusanya vifaa vyake vyote. Alipomaliza, aliviweka kwenye begi lake na kuanza kutoka ndani ya chumba. Lakini hakufanikiwa kufika mlangoni. Kwa kasi ya ajabu alijikuta akivamiwa na mtu aliyeingia ndani kwa kasi bila kubisha hodi, kitendo kilichofanya asambaratike chini kama kiroba cha ngano. Lakini haraka alifanikiwa kusimama na kuacha begi lake likiwa chini.

 Macho yake yaliganda kwa mtu aliyekuwa mbele yake. 

Naam! Alikuwa ni Sajini Nyau aliyevamia nyumba ya nyegere bila taarifa, lakini hakujua aliyemvamia huwa anapenda kukabiliana na watu kama yeye ambao huwa wa kiherehere.
 Miguu ya kuku aliingiza mkono kwenye mfuko wake wa suruali na alitoka na vipande sita vya karanga. Akabugia kipisi kimoja na kubaki na vipande vitano kwenye mkono wake wa kushoto. Kisha akachora mchoro. Akawa tayari kwa makabiliano. 

Sajini Nyau alienda kumvamia kwa kuwa alihitaji taarifa za wizi wa benki, kisha aziuze kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kumtumia Susa. Hivyo aliona ni kama anachelewa kungoja kusikia mipango nusunusu kupitia kwa Susa. Alihitaji kupata taarifa kinagaubaga kutoka kwa mhusika na kisha alipanga kumteka mhusika ili akishavujisha taarifa, kisha ajipe ujiko wa kumkamata mpanga mipango ya wizi. Sajini alishakichoka hicho cheo, alihitaji kupanda cheo nae awe lau na maamuzi ya kuwatuma watu wengi waliochini yake. Usajini kwake aliona umamnyima baadhi ya fursa hasa zile za kuaminiwa na vibopa ambao hupenda kudhulumu haki za wanyonge. Nyau alihitaji cheo kikubwa zaidi na kulikuwa hakuna njia nyingine zaidi ya kujitoa kwa hila ili afanikiwe kupata alichohitaji.

Lakini tatizo alijiamini na kumdharau Miguu ya kuku. Alijiamini kwa sababu alikuwa ni miongoni mwa maofisa ambao hutegemewa kwenye mapambano ya ana kwa ana. Ila ni kwa kuwa hakujua aina ya mtu aliyekutana nae wakati huo.

 Miguu ya kuku alimchokoza mvamizi wake kwa kumfuata kwa pigo moja la judo, kisha akarudi nyuma na kutulia huku akimuacha Sajini akipaparika kama Kasa alietupwa nchi kavu. 

Sajini kwa kasi alirusha ngumi mbili mfululizo huku akikema kama Bruce Lee, lakini mapigo yake yote yalienda bila kumfikia mlengwa. Miguu ya kuku alisogea nyuma na kutupia kipande kingine mdomoni mwake, na mkononi alibaki na vipande vinne.

  Mchezo ukaendelea huku yeye akiwa makini asimuumize Sajini, kwa sababu alihitaji kumtumia hapo mbeleni. Hivyo hakuona kama kuna haja ya kumchakaza, wakati bado hajapata vitambulisho vyake.

 Kila mara alikwepa ngumi zaidi kuliko alivyoshambulia yeye na mkononi alibaki na vipande vitatu tu, huku vitatu vikiwa vimeishia mdomoni. Kwa kawaida akiishia vipande vitatu, huwa anatoa nafasi kwa hasimu wake kuendelea kuishi, lakini vikibaki viwili au kimoja, ni lazima mpinzani wake ajute kuingia kwenye anga zake. 

Miguu ya kuku hakutaka kumdhuru Sajini, hivyo alipobakiza vipande vitatu akajipanga kimapigano, kisha akamfuata Sajini kwa mapigo ya haraka haraka ambayo yalimpa tabu kuyapungua. Sajini aliruhusu kushambuliwa na bila kupenda alijikuta akienda chini huku macho yake yakianza kupoteza nuru na sikio lake la upande wa kushoto likitoa milio isiyo na utamu wa kusikilizwa. Alipojaribu kuinuka, alijikuta akirudi chini huku macho yake nayo yakizidi kupoteza nuru yake. 

Sajini Nyau alipoteza fahamu bila kujua amepigwa sehemu gani iliyompotezea fahamu zake.

ITAENDELEA.

Jaba Zulma

Siyumbi

Your Thoughts

Previous Post Next Post

Contact Form