MALAIKA MWEUSI EPISODE 8

Emmanuel Lee
By -
0

 HADITHI: MALAIKA MWEUSI

EPISODE 8

MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’

SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA: EPISODE 7

"Thereza usifanye hivyo basi sema unataka kiasi gani zaidi ya Bilioni 100 sema tupo tayari kukupa."

“Father Gin nielewe, ukitaka tuongelee habari ya kazi uondoe unafiki ndani ya kundi lako hapo tutakuwa tayari kuifanya kazi yako."

"S...sa....asa..."

"Hakuna cha sasa fanyia kazi niliyo kueleza kwaheri."

Nilinyanyuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Wote walibakia midomo wazi, nilitoka hadi ofisini kwa Dk Ray.

SASA ENDELEA...


"Vipi mmemalizana?"

 "Sifanyi kazi ya kitoto."

 "Mbona sikuelewi?"

 ''Unajua hao sijui mabosi wako wanathamini masirahi yao kuliko uhai wa mtu ambaye ndio muhimu kuliko kitu chochote.”

 "Teddy mbona unazidi kunichanganya."

“Sikuchanganyi bali ninyi ndio mnataka kunichanganya.”

"Kivipi?"

"Kinachotokea kwenye kundi kama sio kugeukana ni nini iweje mtu auawe kabla ya kazi ni nani aliye toa siri kama sio ninyi kwa ninyi, mnataka mnimtoe sadaka?”

"Wacha woga nina imani mafunzo yaliyokutoa woga."

"Sio kwa mtindo huu."

"Kwa hiyo?"

 "Kazi siifanyi na gharama zenu zote nijulisheni ni kiasi gani ili niwalipe," nilisema kwa jeuri.

"Thereza ni kweli usemayo lakini ni mapema sana fikiria mara mbili"

 "Kwanza  Ray wale vijana mliowaandaa kwa ajili ya kuvuna damu na ngozi wapo wapi?"

"Wapo kijiji cha Farijika."

"Mnawavuna toka vijijini?"

"Kapana."

''Mnawatoa wapi?"

“Sasa hivi tuna muundo mpya wa kupita vituo vyote vya kulelea watoto wa mitaani na kukusanya wale wakubwa kwa kisingizio kuna chuo tumeanzisha kwa ajili ya stadi za kazi.  Tukiwachukua baada ya muda huvuna damu na ngozi."

"Ooh vizuri wacha niende."

“Sasa vipi kuhusu hiyo kazi?"

"Tafuteni mtu mwingine."

"Thereza usicheze na Father Gin utakufa kifo kibaya."

"Hiyo itakuwa kesi nyingine.''

Nilimuacha Dk Ray macho yamemtoka pima, niliingia kwenye gari langu na safari ya mjini ilianza. Nikiwa njiani nilikuwa na mawazo mengi juu ya miradi haramu ya Father Gin na kikundi chake mtu niliyekuwa namheshimu kutokana na tabia yake ya upole ukarimu anayejali watu kumbe ni subiani mkubwa mnyonya damu za watu.

Roho iliuma kuona kumbe vijana wadogo wanakusanywa wakidhani wanapewa misaada kumbe ni mavuno yao ya damu na ngozi. Suala la kuwakusanya vijana ili kutengeneza vuno la damu na ngozi toka kwenye vituo vya kuletea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu liliniumiza kichwa.

Lilifanya mwili usisike na kuona hata katika vituo vyangu vya kulelea watoto wa mtaani wameisha nyofoa baadhi ya vijana wangu kwa kisingizio cha kuwapa stadi za kazi. Mwili ulinisisimka nikaona kuna umuhimu kuwaita wakuu wote wa vituo vyote vilio chini yangu niwaulize ni watoto wangapi wamechukuliwa.

Najua utajiuliza nini hatima yangu ya kukataa kuifanya ile kazi na kulikataa donge nono la bilioni 100. Wasiwasi wangu ulikuwa ni uamuzi wa Father Gin juu yangu. Kukataa kule nilikuwa na maana yangu tulia utaijua sasa hivi.

  Mafunzo ya mwaka mzima yalinijenga kimwili na akili,  niliamua kurudi nyumbani

kwangu kupumzisha akili.  Nilipofika nyumbani nilioga kula na kulala ili kujipumzisha akili. Simu ya getini alilia nilinyanyuka na kuipokea.

"Unasemaje Joe?" nilimuuliza mlinzi wangu mtiifu.

"Kuna wageni."

"Waulize ni kina nani," nilimsikia akiwauliza:

"Madamu ni Father Gin na Doctor Ray." 

Kusikia vile nilishtuka kidogo, baada ya kushusha pumzi nilimjibu:

 "Waruhusu,” nilijinyanyua kitandani na kuelekea bafuni kuondoa uchovu kisha  nilirudi chumbani na kujifunga koti langu jepesi la kulalia na kuteremka chini kuonana na wageni wangu. Niliwakuta sebuleni, nilipo waona niliwakaribisha kwa tabasamu pana.

"Karibuni sana."

"Asante sana." walijibu kwa pamoja.

  "Sijui wageni wangu mnatumia vinywaji gani?" niliwauliza. 

"Mimi hapana," alijibu Father Gin.

"Hata mimi nashukuru."

  "Haya kama hamtaki leteni habari najua mna mengi nyuso

zenu zinajionyesha,” niliwauliza swali kwa vile nilijua lazima kile kitu kitatokea.  

"Ni kweli, uamuzi wako sikuutegemea umenichanganya sana," alisema father Gin.

 "Wa kuchanganyikiwa ni wewe au mimi ambaye ndiye unaye ninadi uhai wangu kwa bei nafuu."

“Sema chochote utakavyo ili tu kazi yangu ifanyike."

 "Sio kwamba kazi sitaifanya.”

"Ila?"

 "Pale nimeikataa makusudi lazima uelewe wenzio wanakuzunguruka we hujiulizi kwa nini siri inavuja?" nilimpa siri ya kukataa mbele ya wenzake.

“Kwa hiyo unataka kusemaje?"

"Kazi ipo palepale, ilibidi nilikatae ili kama kuna msaliti ajue sitaifanya japo najua bado nitafuatiliwa ili nitolewe uhai."

"Kazi nitaifanya ila nataka maelezo kamili ya adui zangu picha zao na wanaishi wapi ili kazi ianze mara moja."

 "Ooh! Siamini maneno yako kweli wewe umetuzidi akili kwa kulijua tusilo lijua, vipi kuhusu mkataba?" aniuliza Father Gin.

"Kesho kama kawaida nitapofuata maelezo ya kazi kama ulivyo nieleza mambo yote anayo Dk Ray."

 "Hamna taabu, siku njema."

"Nanyi pia," niliagana nao nami  nilirudi   ndani kujipumzisha.

Asubuhi siku ya pili niliamka na kwenda kibaha. Nilipofika bila kuchelewa nilipewa maelezo ya adui zangu picha zao na ramani  ya  miji wanayokaa. Niliingia mkataba wa shilingi bilioni 100 pale nililipwa bilioni 60 taslimu. Nilipotaka kuondoka Dk Ray alinieleza mengine mapya.

 "Thereza kutokana na mapenzi mazito juu yako imebidi niuweke rehani uhai wangu."

“Una maana gani?"

"Kuna siri moja ambayo kila nikikuangalia moyo unaniuma hivyo nipo tayari kufa kwa ajili hivyo, nipo tayari kufa kwa ajili yako....najua nitahatarisha maisha yangu sina budi

kukupa siri hii."

Kauli na Dk Ray ilinishtua na kujiuliza ni siri gani itayo hatarisha maisha yake.

''Dk Ray ni siri gani hiyo mbona unanitisha?”

"Thereza hapo si sehemu yake nitakuja kwako usiku ili nikupe siri ambayo nina imani

inaweza kuchukuwa uhai wangu."

“Hakuna taabu nitakusubiri kwa hamu.” 

Niliagana na Dk Ray na kurudi Dar. Nilipita vituo vyote kuchukua  taarifa ya watoto walioingia na waliotoka. Baada ya kufika nyumbani nilipitia taarifa zote za vituo vilivyo chini yangu. Moyo ulinipasuka kukuta watoto zaidi ya watoto tisini wamechukuliwa na Father Gin kwa ajili ya kuvuna damu na ngozi.

Nilijiapiza kuwa si watoto wangu tu hata hao wa vituo vingine nitahakikisha

hawanyonywi damu na kuchunwa ngozi. Nilijua mimi ndiye mwenye dhamana ya 

kuokoa uhai wao.  Nilipanga kabla ya kuondoka nitamdanganya Father Gin

tuwatembelee watoto ili niwaone vilevile kujua mandhari yake iko vipi ili nijue

jinsi ya kuwakomboa.

Siku ile saa nne na nusu usiku Dk Ray alifika nyumbani kwangu.  Nilimkaribisha sebuleni, nilimkaribisha kinywaji kikali ambacho nilikiandaa kwa ajili yake.

"Karibu sana Dk Ray.”

"Asante sana mrembo."

Tukiwa tunapata vinywaji yeye vinywaji vikali mimi nilikuwa na malta guiness.

"Dk Ray nina imani una siri nzito moyoni mwako ambayo unaonyesha wazi imekunyima raha toka ulipotamka suala la siri bado uso wako unaonyesha hofu fulani moyoni mwako."

''Ni kweli Thereza."

"Ni siri gani hiyo?"

"Thereza,"aliniita jina langu kwa sauti ya chini huku akifuta mdomo yake kwa mkono.

 "Abee."

 Baada ya kushusha pumzi na kunywa nusu glasi ya whisky kwa mpigo alisema.

"Thereza kwanza elewa nakupenda zaidi ya kupenda nataka kwanza uelewe hilo."

"Nashukuru kwa kunipenda,"  nilimjubu kwa sauti ya upole. 

"Thereza wala si utani ni mapenzi yangu ya chini ya moyo wangu."

“Nashukuru nami nakupenda pia.”

 "Sasa Thereza upo tayari kuwa na mimi?"

“Si tatizo ni suala la maamuzi tu hilo usihofu."

"Thereza japo nina imani penzi langu kwako sitalifaidi."  

 "Kwa nini?”

"Kifo kipo mbele yangu."

"Una maana gani kusema hivyo?"

Wakati huo Mr Ray alikuwa akibugia whisky kwa pupa hata sauti yake ilionyesha ameanza kulewa.

"Si unakumbuka vizuri kiapo ulicho kula kwenye mkutano?"

''Ndiyo."

 "Walisema  hawatasita kumuua mtu yoyote atayetoa siri ya kikundi?"

"Sasa mimi si mwanachama wa kikundi siri itakuwa ndani ya kikundi."

 "Thereza hiki kikundi nakijua mimi vizuri, zipo siri zinazojulikana na zipo siri sirini

ambazo tunazijua sisi tu."

"Mmh, siri sirini?"

"Ndiyo Thereza, kama nikikueleza na wakijua  lazima wataniua.”

"Basi  haina haja ya kunieleza siri itayohatarisha maisha yako."

"Kama nitakaa kimya itahatarisha maisha yako."

''Maisha yangu! Kivipi?”"

"Eeh, ndiyo."

  "Mungu wangu ni siri gani hiyo unayofanya mwili wangu kusisimka na kujawa na hofu kubwa?"

"Thereza bila mapenzi yangu ya dhati juu yako nisingekueleza siri hii vilevile wewe unanihusu mimi sana kuliko mtu yoyote. Pia nina imani ukivuka salama nami nikavuka mtihani ulio mbele yangu tutafunga ndoa, “ alimimina mdomoni whisky iliyokuwa imebakia kwenye glasi na kuniita jina langu kwa sauti ya kilevi:

 "Thereza."

 "Abee."

''Najua undi hili unalielewa juujuu siku zote jasusi hana rafiki, siku zote anajali masilahi yake..anachojali kazi yake unapoimaliza lazima apoteze ushahidi."

"Kupoteza ushahidi una maana gani?"

"Swali zuri Thereza, siku zote jasusi huwa hajiingizi kwenye kazi zenye ushahidi, humtumia mtu.  Ili kufanyiwa kazi hutangaza malipo mazuri yatayomshawishi

mtu aifanye kazi lakini mwisho wa kazi unapowajulisha kazi imekwisha hapo ndipo hukuua ili kupoteza shahidi."

"Eti kufanya nini?" nilishtuka.

"Kukuua ili kupoteza ushahidi ikiwa pamoja na kuchukua pesa zao zote walizokupa kupitia watumishi wa benki ambao ni mawakala wao ambao huwalipa asilimia fulani ya pesa zile."

Habari zile zilinishtua sana zilikuwa mpya kabisa maishani mwangu ambazo sikutarajia kuzisikia. Nakubaliana na usemi wa Dr Ray Jasusi hana rafiki pia jasusi hafanyi biashara ya hasara. Macho na masikio yalifunguka.

"Dr Ray una ushahidi na unayosema?" Nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.

"Ndiyo, wengi wameuawa baada ya kufanya kazi na kudhulumiwa malipo yao. Japo

wamekupeleka mafunzoni nia yao ni kufanikisha kazi yao ukiimaliza ujue na we ndio mwisho wa maisha yako."

"Hivi wale watu mnaowachuna ngozi na kuwanyonya damu mnawazika wapi?" nilibadili mada kwa faida yangu.

"Kuna tanuru kwa ajili ya kuchoma miili yao na ikisha kuwa jivu tunaitupa baharini.

"Dr Ray unaweza kunisaidia vipi maana hata sijui nifanye nini hata najuta kuingia

mkataba, ningeyajua haya mapema nisingekubali, bora ningeendeleza msimamo wangu," niliingiwa wasiwasi na taarifa ile.

"Bora umekubali wangekuua."

"Na kuhusu pesa nitazilindaje?"

"Ni rahisi zibadili kwenye  akaunti ubadili na jina ukiwezakana weka mafungu hata kumi benki tofauti hapo utakuwa umewaweza tena kwa majina tofauti."

"Nini kingine cha muhimu hiki ni muhimu 'pass word' zitakusaidia sana hasa hii ya

Father Gin yule si Father bali Jasusi Gin anayepaka matope dini za watu yule ni shetani sijui kwa Mungu atajibu nini juu ya roho za watu alizozipoteza”

Dr Ray alinipa pass word zaidi ya tano za shirika lile la ujasusi ambalo halikuwa  la dini kama linavyojulikana. Ndiyo maana hata Bwana Yesu kabla ya kuondoka alitutaadharisha na watu wataojinadi kwa jina lake hao tusiwaamini na ndio wanaochafua watu wa kweli walio wasafi mbele ya bwana.

Nilikumbuka kile kikao watu wanaonekana wasafi mbele ya dini zao kumbe wanyonya damu ukiwakuta mbele ya waumini wao wanavyo mtukuza Mungu kumbe mashetani.

Lakini kwa Mungu kila kitu kitalipwa kulingana na matendo yao, Mungu si mwongo wala si mtani wa mtu, ipo siku kweli itadhihiri hata ufanye gizani.   

"Dr Ray ulijuana vipi na Father Gin?"

"Of course yule Father Gin alinichukua kutoka chuo cha ujasusi kazi yangu kubwa

ilikuwa kuwatibu watu wote walio chini yake, hasa kuzingatia kazi ya ujasusi ni ya

hatari yenye majeraha na makovu mengi.

"Ili kupoteza lengo tulijenga  hospitali kubwa Kibaha na kuwahudumia watu wote lakini ni  kituo cha ujasusi,”  Dr Ray akionekana pombe zimemkolea aliongea kwa sauti ya huzuni.

 "Thereza."

"Unasemaje?"

"Naomba uniahidi kama utakuwa tayari kufa kwa ajili yangu kwani na mimi nimejitoa kwa ajili yako."

"Dr Ray makuahidi."

"Basi kama nitakufa atayeniua si mwingine ila Father Gin na kuomba umuue kwa mkono wako."

 "Nakuahidi nitafanya hivyo."

“Thereza naomba penzi lako kwa usiku huu japo sina uhakika kama nitauona usiku

wa kesho,” Dk Ray alizungumza kwa sauti iliyokata tamaa.

"Usihofu mpenzi leo mwili wangu utakuwa mali yako na tukivuka mtihani uliopo mbele yangu na yako ruksa kunivisha pete." 

"Mpaka hapo hata kama nitakufa basi nitakufa moyo wangu ukiwa shwali nina imani

penzi lako lina thamani kwangu kuliko uhai wangu."

Nilimshika mkono na kupanda naye juu, baada ya kuongea tulioga pamoja na kujilaza

Kilichofuata nilimpa alichokitaka. Asubuhi baada ya supu zito na kuzimua na whisky Dk Ray aliniaga akiwa na furaha moyoni nina imani unajua nini kilichomfurahisha.

Baada ya kuondoka nami nilioga na kujiandaa kukabiliana na kilicho mbele yangu nilijiona nimo ndani ya kinywa cha mauti na uwezekano wa kutoka ni mdogo sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano kwani vifo vilikuwa nyuma na mbele sidhani kama vyote nitaweza kuvikwepa.

Penzi langu kwa Mr Ray si penzi la moyoni, kwangu kama shukurani ya kunifungua 

macho. Yeye alikuwa na mapenzi ya kweli moyoni mwake na kuwa tayari kufa juu yangu.

Sikuwa na budi kuonyesha mapenzi ya dhati juu yake japo siyo moyoni bali ya kuunda kwa kipindi kile yeye alikuwa mtu  muhimu sana ambaye alinisaidia kuyajua

mengi . Lakini mwanzo alinisaidia kwa ajili ya kuwafanyia kazi zao.

Japo Mungu kanijalia uzuri wa shani unaowazuzua wanaume wengi, nilishangaa

kwa kauli yake kuwa anipenda mtu aliyezichezea sehemu zangu za siri mara nyingi  sikujua nini kilichomvutia kwangu.

Niliingia chumba changu nilicho kiteua kwa kazi zangu za kijasusi, chumba ambacho

nilikifunga mitambo ya mawasiliano.  Nilizichukua zile picha tano za watu wanaotakiwa kuuawa.

Niliwaangalia kati ya hao watano walikuwa wazungu mmoja ndiye alikuwa mweusi kama mimi. Wote walionekana watu wa makamo kasoro msichana Marry White alikuwa umri kama wangu kama kunizidi ni miaka miwili. Baada ya kuzihifadhi picha zote kichwani nilianza kuangalia ramani na mitaa.

Walikuwa wanaoishi maelezo yaliyonionyesha nitateremka katika uwanja wa ndege wa London na kufikia hotel ya Browns Hotel London. Ofisi za wabaya zangu zilikuwa jirani mtaa wa Regent.

Na Italy nishukie uwanje wa ndege wa Rome na kupanga kwenye Hotel iliyo jirani na

uwanja huo wa ARZEMIDE. Na Ujerumani ilionyesha nishukie uwanja wa ndege wa 

Pusseldorf ulio katika mji wa Dusseldorf. Na kupanga hotel ya karibu ya RADISSON SAS HOTEL DUSSELDORF. Iliyopo kwenye mtaa wa Kaiserwerther.

Baada ya kuihifadhi ile ramani kwenye kumbukumbu za ubongo wangu. Nilipata 

kifungua kinywa  nikiwa napata kifungua kinywa wazo moja lilinijia ni muhimu kujua

mazingira  watoto wale waliotunzwa kwa ajili ya kuvunwa damuna ngozi hapo baadaye.  Niliona haina haja ya kumshirikisha tena Father Gin juu ya safari yangu

kuwatembelea wale watoto.   

Nilimuona Dk Ray anafaa sana ni muhimu anaweza kunisaidia zaidi,  nilimpigia

simu.

 "Vipi honey mzima?"

"Wa afya sijui wewe ua la moyo wangu."

 "Mimi mzima ni hivi upo kazini?” 

"Ndiyo"

"Nakuja sasa hivi nina shida na wewe." 

 "Nipo nimejaa tele kama pishi la mchele," kidogo nicheke Mzungu ana maneno kama

Mswahili.

Basi nakuja mpenzi."

"Ila usije moja kwa moja ofisini teremkia mbali na uje kwa kupitia mlango wa nyuma."

"Sawa," nilikata simu.

Sikuwa na muda wa kupoteza nilikodi gari, sikuwa na haja ya kwenda na gari

langu nilijiona kama nimeishaianza kazi, nilianza kwenda mwendo wa  machale, kama nilivyo elekezwa na Dk Ray.

Niliwasiri Kibaha baada ya nusu saa niliteremkia mbali na kutembea kwa miguu hadi pale hospitali tena nilipitia kwa nyuma. Nilipofika ofisini nilikutana na pigo la mwaka mwili wa Dk Ray ulikuwa umelazwa juu ya meza ukiwa umetenganishwa na kichwa matumbo yakiwa nje.

Kengele ya hatari ililia kichwani kuonesha shughuli imeshaanza, nikiwa bado nimepigwa na bumbuwazi mara nilisikia sauti za watu wakiongea nje ya chumba.

"Hivi huyu malaya wake atakuja saa ngapi? Unajua sister tumemuahidi kazi itakuwa ya saa moja." mmoja alimuuliza mwenzake.

"Atakuwa amepitia wapi au tumfuate kwake?" Mwingine alichangia.

"Tunaweza kuchengana naye tumsubiri namba yake ya simu si unayo tumpigie tukijifanya Doctor Ray we nakuamini kwa kuigiza sauti za watu."

Kusikia vile moyo ulinipasuka nilijua nitajulikana, niliitoa simu haraka

na kuizima nilijua kwa mtindo huo wamenikosa. Nilimsikia mmoja akisema:

"Unajua Marc sio siri inavyoonekana huyu msichana ni mtu hatari sana, kwani hata

sister Marry White alionyesha jinsi anavyomuhofia.”

"Inawezekana machale yamemcheza hata simu yake haipatikani."

"Ingia ndani ukaangalie namba kwenye simu ya Doctor Ray kama zinalingana."

 "Nilijua shughuli rasmi imeanza nilijibanza nyuma ya mlango, sauti za nyayo za viatu nilizisikia zikisogelea mlango wa ofisi, mara mlango ulifunguliwa  aliingia kijana aliyeonyesha mwili wa mazoezi alikwenda kwenye meza ili achukue simu iliyokuwepo juu ya meza pembeni na mwili wa Dr Ray.

Niliurudisha mlango kwa mguu, nilimsogelea kidogo nikijua sehemu ile teke la

kuzunguka litampata vizuri. Nilikohoa ili ageuke na kuweka vizuri kisogo chake.

Alipogeuka kabla hajashangaa niligeuka na teke mzunguko lililompata kwenye kisogo. Hakuwahi kupiga hata kelele alikuwa mgeni wa kuzimu. Nilimlaza pembeni na kumsubiri wa pili niliyemsikia akimwita mwenzake:

"Marc vipi mwaka mzima?"

"Tunapoteza muda kama vipi tumfuate kwake."

Alipoona kimya aliingia mwenyewe  alionyesha hakujiandaa, aliingia kizembe

ilionyesha alijiamini sana. Alipoingia alishangaa kutomuona mwenzake

alimwita.

"Marc," ilimwita kwa sauti ya juu kidogo. 

"Unasemaje?"  niliitikia, alipogeuka nusra azirai kwa mshtuko alikuwa kama ananifananisha.

 "Wewe ni  Thereza?"

"Ndiyo mimi."

"Marc yupo wapi?"

"Wanaongea lugha moja na Doctor Ray."

"Yaa..ani umemuua?" Aliniuliza macho yamemtoka pima.

"Sijui muulize mwenyewe,"nilimjibu kwa dharau.

"Sikubalii," alichomoa kisu.

"Aaah... Aibu mwanaume mzima  uliyekamilika unanibebea kisu mtoto wa kike."

Kauli yangu ilimfanya aone aibu na kukitupa kisu pembeni alivua fulana

iliyo kuwa imembana na kuuonyesha mwili wake uliojengeka kimazoezi.

Nilijua lazima atapigana kwa pupa alinifuata kama mbogo na kutupa ngumi nzito iliyotoa mlio wa kukata upepo iliponikosa. Niliinama na kumpiga kiwiko cha kuzunguka kwenye mbavu changa alizozinyoosha wakati wa kupiga ngumi. Nilimsikia akiguna kwa maumivu.

Alipopiga ngumi nyingine niliiongezea na teke kwenye maungio aliongeza kilio

Kingine. Mkono ulipoteremka ulikuwa umelegea nilijua nimeshauvunja.

Nilimalizia na teke la kuzunguka la chini lililomrusha juu na kuanguka chini kama mzigo. Nilimfuata na kumuongeza ngumi mfurulizo zilizomlegeza. Nilimfuata na kumuuliza:

"Marry White yupo wapi?" nilimuuliza kwa sauti ya ukali kidogo, lakini hakujibu alionesha kiburi.

"Aaah unajifanya nunda siyo?"

Wakati huo hasira zilikuwa zimenipanda nilitamani kunywa damu ya mtu, mauaji ya Dk Ray yaliniongezea hasira.

"Utanijibu hunijibu?"

Aliendelea kuwa kimya, niligeuka kufuata kisu, akili yangu ilicheza na yeye siku zote

jasusi yoyote hakubali kufa kikondoo.  Nilipogeuza uso nilikuta ndio anapeleka mkono wa kulia mdomoni kwa vile wa kushoto nilikwisha uvunja, Niliruka kama mkizi na kufanikiwa kuupiga pembeni alichotaka kukimeza ili ajiue. Nilimshikia kile kisu na kumuuliza.

"Nakuuliza kwa mara ya mwisho Marry White yupo wapi?"

"We niue tu mi sijui," alionesha kiburi cha hali ya juu.

"Aah unafanya utani siyo?"

Niliingiza kisu katika jereha lake la jichoni, maumivu yalipozidi alipiga kelele:

"Utaniua bure, we niue kabisa kuliko kunitesa hivi mi’ sijui lolote."

"Nitalitoa jicho kama utaleta kitu kujua," wakati huo nilikuwa nakandamiza kisu kwenye jeraha. Yule mtu alipiga kelele za maumivu makali.

 "Ooh!Niache nitakueleza."

Nilikichomoa kile kisu kilichokuwa kimeingia robo tatu, wakati  huo damu zilikuwa zikizidi kutoka kwenye jeraha.

"Haya ongea."

"Nimeamini kweli wewe mtu hatari sifa na hofu alizoonyesha sister Marry White nilifikiria ni uongo kweli dada unatisha,"alisema yule jamaa huku anauma meno kwa maumivu makali.

"Sikuja kusifiwa hapa nieleze Marry White yupo wapi?”

"Yupo Nairobi."

"Nairobi anafanya nini?"

"Sijui ila alisema mpaka jioni atakuwa Arusha." 

“Yupo sehemu gani pale Nairobi?"

"Huwezi kumuwahi ila jioni ya leo wana kikao kingine Arusha."

"Vikao vyao vinahusu nini?"

"Ukweli mimi sijui, sisi kazi yetu kubwa ni kutumwa kufanya mauaji."

"Ooh, vizuri, mmeshaua watu wangapi?"

"Sisi kama tungekuua wewe ungekuwa wa sita."

"Ina maana wapo wengine?"

"Tupo wengi."

"Kwa nini mlitumwa kuniua mimi?"

"Ujuzi tunatofautiana hivyo sisi ndio tulioonekana tupo juu kutumia silaha hata mapigano ya mikono."

"Mbona unaonekana cha mtoto hata hujui kupigana?" Nilimdhihaki.

"Wewe unatisha ningejua uwezo wako uko hivi wala nisingedhubutu kuja kunadi uhai wangu kwa bei ya bure."

"Nieleze hapa mjini mpo wangapi?"

"Tupo sita."

"Wengine wapo wapi?"

"Wanafuatilia biashara za bosi."  

"Biashara gani hiyo?"

"Ya kukusanya vijana" kusikia vile nilishtuka.

"Hao vijana mnawakusanya ili iweje?"

"Kwa kweli hapo mimi sijui." 

"Acha kuniudhi nieleze ukweli."

"Ukweli sijui ila baada ya kuwakusanya huwapeleka nje kidogo ya mji wa Arusha  sehemu hiyo nilishafika mara moja kupeleka watoto. Lakini zaidi ya hapo sielewe mara nyingi tulishawakusanya huwapeleka na tukiwafikisha sisi tunarudi."

"Umesema biashara una maana gani?"

"Mara nyingi hutumia pesa kupewa vijana waliopo kwenye vituo vya kulelea vijana."

"Hii biashara mmeianza lini?"

"Ni mwezi wa sita sasa."

"Mungu wangu!"

 "Dada mbona umeshtuka kwani hii biashara ina nini?" Yule mkora aliniuliza.

"Aaah, wacha tu," nilificha ninachokijua.

"Umenieleza wenzio wapo hoteli gani?"

“Wote tupo New African Hoteli."

"Pale mmetumia majina gani?"

"Pale nilipanga chumba kimoja na Marc"

"Wewe unaitwa nani?"

"Zone."

"Ehe na wengine?"

"Yupo Cathy ambaye yupo chumba kimoja na Puchu na Kallo yupo na John."

 "Ok, vizuri, umenieleza Arusha sehemu gani?"

 "Nje ya Arusha mimi si mwenyeji sana."

"We raia wa wapi?"

 "Kenya"

 "Umesema mkishakusanya  vijana mnarudi lini Arusha?"

"Leo usiku."

"Asante kwa msaada wako."

"Naomba na mimi unikimbize hospitali."

 Sikumjibu nilikuwa kama nataka kuondoka niligeuka na teke kali iliyomvunja shingo na kumuwahisha kuzimu. Nilipitia mlango wa nyuma na kutokomea zangu, nilimkuta dereva wangu usingizi umempitia.

"Kaka  vipi? Niwahishe Dar."

 "Ooh, dada umeisharudi, umesema?" Dereva alikurupuka katika usingizi wa mang'amung'amu.

Dereva aling'oa gari kwa mwendo wa kasi kurudi Dar, njiani nlikuwa na mawazo mengi juu ya vita iliyo mbele yangu nilijua kazi imeisha anza. Kwa maana moja au nyingine niliona kazi yangu huenda ikawa nyepesi hatua za awali baada ya kujua kumbe kundi la Marry White lipo hapahapa Tanzania na shughuli zake anazifanya Arusha.


 Nilipofika nyumbani nilibadili mavazi na kuvaa kama sister na msalaba mkubwa nilipotoka hata dereva alinishangaa.

“Vipi sister unataka usafiri?’

“Acha kujichanganya nipeleke New Africa Hotel.”

“Aah kumbe ni sister.”

“Nani alikuambia mimi ni brother?"

“Sina maana hiyo yaani mtumishi wa kanisa.”  

“Utayajua yote we niwahishe.” 

Alisimamisha gari kwenye  maegesho ya Hotel, niliteremka na kuingia ndani, nilikwenda moja kwa moja hadi mapokezi nilimkuta muhudumu wa kike.

“Habari yako dada,” nilimsalimia.

“Nzuri tu sister.” 

“Kuna wageni wangu nimeelezwa wapo hapa.” 

“Wapo chumba namba gani?”

“Sikumbuki ila tarehe waliyoingia naikumbukai ilikuwa tarehe...” nilimtajia alipekua kitabu cha wageni.

“Sister majina yanaanzia hapa angalia jina la mgeni wako,” niliinama na kuanza kuangalia majina ya wale wakora niliyaona na kuangalia namba za vyumba vyao. wakati narudisha kitabu nilimsikia yule muhudumu: 

“Sister tena unabahati wageni wako hao.” nilipogeuka nilikutana na kijana mmoja aliyejengeka mwili kimazoezi alikuwa amevaa fulana nyeusi ya kubana na msichana mwembamba. Walipotukaribia yule msichana muhudumu alitaka kuwaita, Nilimzuia na kumtaka akae kimya.

“Waache wapite, pale yupo nani na nani?”

“Ina maana huwajui wageni wako?” mhudumu wa mapokezi alinishangaa.

“Ukweli hawa siwajui ila ninao wafahamu ni Marc na Puchu.”

“Wacha wapumzike ili nikawaulize Marc na Zone wapo wapi,” nilitengeneza uongo.

 Nilitulia kwenye makochi mapokezi kama dakika tano, nilipoona ule  ni muda muafaka nilikwenda moja kwa moja hadi chumba walicho ingia. Sikugonga nilikizusha kitasa ambacho kilikubali na kuusukuma  taratibu lakini yenye kasi.

Ajabu chumbani  hapakuwepo na mtu zaidi ya nguo kuzikuta ovyo kitandani. Niliurudisha mlango na kukaa tayari kwa lolote. Mara walitoka  bafuni kuoga wakiwa amekumbatiana waliponiona walishtuka kidogo yule msichana alisema: 

“Sister Marry White umekuja si ulituambia muda huu utakuwa Nairobi?”

Lakini  mwanaume alishtuka na kusema:

“Hapana si Sister Marry White, huyu humuoni maji ya kunde?”

“Mimi si Sister Marry White naitwa Thereza yule mliyetumwa na sister Marry White mje mniue,” mo;owajibu huku nikiondoa kilemba kichwani.

 Kusikia vile walitaharuki kama ukuta ungekuwa una upenyo wangejipenyeza ili kukimbilia.

“Mungu wangu!” walisema kwa pamoja.

“Msishangae, kwanza hebu nielezeni kabla ya maswali yangu. Mpaka sasa mmeshakusanya watu wangapi ambao mnawapeleka Arusha kwa ajili ya kuwanyonya damu na kuwachuna ngozi?” 

 Swali langu lilizidi kuwachanganya macho yalinitoka pima. Mara nilisikia mlango ukigongwa nilimwonyesha yule msichana kwa ishara afungue. Msichana aliyekuwa  amejifunga taulo lililoziba matiti na chini kuishia chini ya makalio alisogea hadi mlangoni. 

Wakati huo nilikuwa nimeshikilia bastola mkononi huku nikifunga kibambo cha kuzuia sauti. Alikuja akitetemeka nilimwambia kwa ishara kwa ukali kidogo afungue.

Aliufungua mlango aliingia msichana mmoja mwenye umbile la kati kama langu alipoingia tu alimrukia shoga yake huku akisema mambo yote tumekamilisha hesabu imetimia jioni safari.

Wakati huo shoga yake taulo lilikuwa limemdondoka kwa woga na kumwacha mtupu kitu kilicho mshtua yule msichana aliyeingia  ambaye nilikuwa na uhakika ndiye  Kallo  

Kallo alipotizama pembeni alishtuka nusra atimue mbio kurudi nje kwa woga. Niliwahi kuusukuma mlango kwa mguu alijibamiza nao na kuanguka chini damu zikimtoka puani na mdomoni. 

Aliponyanyuka aliangalia damu mikononi mwake inavyotoka puani na mdomoni nilimwita karibu yangu na kumueleza akae chini.

“Kallo ukweli  ndio yataowaokoeni na adhabu ya kifo ila ukifanya kiburi utasafiri kwenda ahera.”

''Kwanza umejuaje jina langu?''

"Kaniambia Sister Marry White."

"Ati?" alishtuka.

'Huu si muda wa kushangaa, kwanza John yupo wapi?" swali lile lilizidi kumchanganya na kujiuliza nimewajuaje.

"Sijui," alijibu kwa mkato.

“Hujui wakati ndiye mwanaume wako mlie kuwa nae kwenye upumbavu wenu.. hivi na ninyi mkinyonywa damu na kuchunwa ngozi mngefurahi au mngekubali?" swali lingine lilizidi kuwachanganya zaidi.

"Au umtoe mdogo wako au mwanao akachunwe ngozi na kunyonywa  damu mngekubali?"

“ Eti kaka Puchu?” mtoto wa kiume mdomo ulikuwa mzito nilimgeukia Kallo aliye kuwa karibu yangu.

'En’he, Kallo naomba jibu zuri John yupo wapi?"

"Nimesha kujibu sijui," alijbu kwa kiburi cha kike.

"Hujui eeh, hebu simama."

Alisimama nilijifanya kama nampa mgongo huku  nikiongea kwa sauti ya chini"

"Nimeisha...”  kabla hajamalizia sentesi niligeuka na kelbu iliyompata sawasawa kwenye shavu la kulia na kumpeleka chini na kuzidi kumtoa damu kwa wingi mdomoni na puani

Ile kelbu ilimfanya alegee, nilimfuata pale chini na kumkwida na kumuuliza kwa hasira zilizokuwa zimeshapanda vibaya, Nilimtikisa huku nikimuuliza kwa ukali.

"John yupo wapi?"

"Yupo n.. n.. nje." 

Nilishtushwa na teke zito la Puchu lililonipeleka chini kabla sijasimama aliniongeza mateke ya mfululizo kama manne lakini lililoniingia lilikuwa moja.  Niliufyatua mguu wake mmoja na kwenda chini. Hapo chini tulishikana mwenzangu alikuwa na ubavu alininyanyua  na kunitupa upande wa pili na kuidondosha bastola niliyo kuwa nimeichomeka kiunoni  

 Puchu alinirukia na kunipelekea mashambulizi mazito. Siyo  siri mwanamume yule alikuwa na mshipa japo ngumi zake nyingi nilizipangua lakini mikono iliwaka moto.

Sikubahatika  kujibu mashambulizi zaidi ya kurudi nyuma. Nilipofika ukutani Puchu alidhamilia animalize pale pale. 

Ngumi za mbavu za mfululizo zilinilegeza nilimwona akivuta ngumi nzito usawa wa shavu, kwenye masumbwi wanaita krosi ili animalize. Ngumi ile niliiona na kuinama mkono wake ulipiga ukutani nilimsikia akiguna. Nilimpiga teke la nyuma lililomfanya ajigonge uso ukutani, kabla hajageuka nilipitisha teke kwa chini na kumpiga sehemu za siri kwenye hashua. 

Alipiga kelele za maumivu na kupiga magoti nilimfuata na kumshika nywele zake na kugeuza shingo yake alionekana amelegea nilimuongeza ngumi kama kumi za mfululizo zilizomtepetesha kabisa, wakati nageuka nilikuta ndio kwanza cathy alikuwa bado yupo uchi wa mnyama akiwa ameshilia bastola yangu akitaka kunipiga risasi.

Nilijirusha pembeni risasi  zaidi ya nne zilimpata Puchu na kummaliza wakati najirusha kwa kujiviringisha hewani sikumpa nafasi Cathy ya kunipiga risasi nyingine nilichomoa kisu na kumrushia Cathy kilichompata sehemu ya moyo na kumuua pale pale. 

Ndani kulikuwa na maiti mbili ya Puchu na Cathy, nilijinyanyua mwili ukiwa unaniuma na damu zilikuwa zikinitoka puani na mdomoni. Niliokota bastola yangu na kisu changu. 

Nilichukua shuka kitandani na kujifutia damu na kumfuata kallo aliyekuwa bado amejilaza chini.  Nilimshika na kumketisha ili ajibu maswali yangu, Mara nilisikia mlango ukifunguliwa nilinyanyuka haraka na kujibanza nyuma ya mlango.

Kiliingia kipisi cha mtu kilichonyoa upara na mwili mkubwa uliojengeka vyema kimazoezi uliofichwa na fulani nyeusi ya mikono mirefu iliyo mbana na kuonyesha umbile lake vizuri. 

Nilijua ni John tu, aliponiona alishtuka nusra akimbie lakini niliwahi kufunga mlango kwa mguu kitu kilichozidi kumchanganya. Nilimweleza kwa ishara asogee mbele mbali kidogo na mimi. Lakini bila kutarajia teke lake la nyuma liliipiga bastola yangu pembeni.

Kabla sijatulia nipange mashambulizi alikuwa ameshanifikia, mikono liliwaka moto nusu saa nzima hakuna aliyempata mwenzake, kila mtu alikuwa akishambulia na kuzui. John alibadili staili na kunivamia mzima mzima na kunikaba shingoni japo ngumi  zangu zilimpata puani na mdomoni na kumtoa damu hakuniachia alinisukumia ukutani. 

Alinibana ukutani japo nilijitahidi kujitoa mikononi mwake alinizidi nguvu alinipigiza ukutani mara tatu mpaka nikaanza kuona kizunguzungu.  Alininyanyua juu akiwa amenishikilia shingoni huku akiendelea kuniminya shingo huku akisema:

“Mrembo utakufa kifo cha raha wewe hufai kuuliwa kwa risasi au kisu bali utakufa kwa busu."

Alikuwa akininyonya damu zangu zilizokuwa zikitoka mdomoni,  huku akizidi kuiminya shingo, nilijua shingo si muda mrefu itavunjika. Nilikumbuka mafunzo ya kupambana na mtu mwenye nguvu pale anapokuwa amekubana.  Nilipepesa mikono yangu kama mfamaji na kufanikiwa kushika sehemu za macho hapo niliingiza vidole vyangu na kucha zangu ndefu zilimuingia barabara.  

Alipiga kelele za maumivu na kuniachia, nilianguka chini.  Alishika macho yake niliyoyatia makucha, nilitumia nafasi ile kupeleka mashambulizi mfululizo sehemu za siri.  Alipiga kelele huku akipiga magoti nilimaliza kazi kwa teke la kuzunguka lililompata chini ya kisogo na kuvunja sehemu ya nyuma, alianguka kama mzigo na kukata roho. 

 Nilikaa chini kuvuta pumzi mwili wote haukuwa na nguvu kama angetokea adui mwingine angeniua bila taabu. Nilijunyanyua hadi mlangoni nikipepesuka na kufunga mlango kwa ndani ili asiingie mtu mwingine. Kallo alikuwa bado amekaa ilionekana Kallo hakuwa mzoefu wa shughuli zile  kelbu moja tu ndio imemfanya vile, nilimnyanyua hadi bafuni na kumwagia maji. Hapo alipata nafuu aliweza hata kutembea peke yake.  Nilimkalisha kwenye kitanda mikono nimemfunga na kamba na kuanza kumuhoji:

“Nina imani umeona malipo ya kiburi cha wenzako nadhani hutapenda nawe kuwafuata nataka uniambie ukweli Dar mmekuja wangapi?” 

"Sita."

"Nitajie majina?"

"Mimi,Cathy, John, Puchu, Marc na Zone.”

“Marc na Zone wapo wapi?"

"Walitumwa waje kukuue wewe."

"Wapi?"

"Kwako au Kibaha."

"Kibaha wangenipataje nami si makazi yangu?"

"Ilikuwa kubahatisha kwani Doctor Ray inaaminika ndiye anayejua habari zako zote inasemekana ndiye aliyekutafuta.”

"Vizuri, Mary Wahite alijuaje habari zangu?”

"Hapo sijui."

''Mmevuna damu na ngozi kwa muda gani?”

"Ni mwezi wa sita sasa."

"Hadi sasa mmeshauza damu kiasi gani?"

"Bado ndio tupo kwenye makusanyo vile vile mitambo ya kunyonya damu na kuisafisha inamaliziwa kufungwa, wiki hii hivyo kazi inaanza wiki ijayo.”

“Hadi saa mmeisha kusanya vijana wangapi?"

"Elfu sita."

"Elfu sita! Wote hao? Mmewahifadhi kambi moja?"

"Hapana wengi tumewaacha kwenye vituo vyao kwa udogo wa kambi yetu."

"Kambini wapo wangapi?''

''Elfu mbili na mia tatu na leo tumekusanya mia mbili hivyo watakuwa elfu

mbili na mia tano, ila mtambo ukianza ndani ya wiki mbili tutakuwa tumewamaliza wote kwani damu inatakiwa haraka."

Habari zile zilizidi kuusisimua mwili wangu mpaka nywele zilinisisimka. Nilijikuta nikipata matumaini ya kuokoa damu za watu wasio na hatia japo sikujua nzito ulikuwepo mbele yangu.

Lakini kwa uwezo wa Mungu niliamini nitashinda japo nilikuwa kwenye

kundi la uovu la Father Gin. Niliamini  uwezo wa Mungu kwani yeye ndiye mwenye aliyefanya majabu kuniingiza kundini niokoe walio taabuni katika mateso mazito.

Niliamini kwa nguvu za Bwana ningeshinda uovu na kulisafisha jina la Kristo kwa

wale wanaotumia kuvuli chake kuichafua dini yake na  na manufaa yao kwa kuwatendea watu uovu.

"En’he umeniambia leo umekusanya watu mia mbili?” nilimuuliza swali.

"Eeh ndiyo."

"Wako wapi?"

"Wako vituoni mwao tutawapitia jioni."

"Kambi yenu ipo wapi?"

"Nje ya mji wa Arusha ukivuka Kijenge unakata kushoto kuna barabara ya vumbi ukiifuata utafika kambini kwetu."

"We raia wa wapi?"

"Tanzania."

"Mtanzania halafu unatenda unyama kama huu?"

''Dada yangu mimi nilikuwa mhudumu wa kambi moja hapa Dar ya watoto wanaishi kwenye mazingira magumu tulichukuliwa sita kutoka vituo tofauti. Tukiwa tunawahudumia wale watoto hapo ndipo tulipopewa semina ya madhumuni ya kile kituo kuwa si kulea watoto bali kuvuna damu na ngozi na tulielezwa kuwa atayetoa siri ile atauawa

“Kwa kweli dada yangu tuliishi katika mazingira magumu sana, mmoja wa wenzetu alitoroka kwenda polisi kutoa taarifa juu ya kile kituo.  Huwezi kuamini kumbe Marry White  anashirikiana na polisi.  Mkuu wa polisi alimpigia simu mkuu wa kituo mR Cosmas alipokwenda ndipo alipomkuta  mwenzetu pale polisi na kuelezwa alichokipeleka pale.

 "Tukiwa hatuna hili na lile kilipigwa king'ora  tukakusanywa tulipokusanyika tulikuta Mr Cosmas akiwa amemshika mwenzetu mtupu kama alivyozaliwa na kuelezwa alichokifanya na adhabu yake alichunwa ngozi adharani akiwa hai na mwili wake kutupiwa mamba, Ooh! Maskini Devota alikufa kifo kibaya," sauti ya Kallo ilibadilika na kuwa ya kilio chenye majonzi, habari ile hata mimi ilionyesha napambana na watu wa aina gani.

  Kallo aliendelea kuongea kwa sauti ya majonzi na kilio kuonyesha  jinsi gani kifo cha shoga yake Devota kilivyomuuma.

“Huwezi kuamini dada kuna watu wana roho mbaya sijui  nifananishe na nini nina imani wamemzidi shetani. Devota alichunwa ngozi mbele ya macho yetu kilio alicholia nilisikia maumivu moyoni. Moyo uliniuma kama vile mtu kaupasua kwa kisu butu bila ganzi vipande mbili.

“Yaani kuna watu pale kambini wameandaliwa kwa kazi mbili yupo anayejiita Zimwi shetani yeye kazi yake kuchuna ngozi za watu wote wanaopewe adhabu. Pia yupo mtu mwingine mwenye mwili mkubwa hana tofauti na mzee Ole wa gazeti la Sani yeye huyu anajiita Roho ya chuma kazi yake kuua watu kwa kuwapasua na shoka katikati ya utosi au kukucharanga shoka kama vile wauza bucha. Kuna gogo maalum lililoandaliwa kwa kazi hiyo.

“Umeshashuhudia mauaji mangapi zaidi ya Devota?”

“Mmh, ni mengi...we acha tu dada yangu yanatisha si ya kusimulia.”

“Unataka kuniambia wengine wote kosa lao ni hilohilo la kutokuwa waaminifu wa kikundi?”

“ Hapana ..wapo waliokula njama ya kuua vitendea kazi, wengine kuuza silaha na mwingine aliyeuawa wiki iliyopita alitaka kumbaka mhuduma wa kambi.”

“Vizuri unataka kunieleza mauaji ya Doctor Ray mmeyafanya kwa sababu gani?” 

“Ni hivi dada hili kundi tulielezwa ni watu waliojitenga kutoka kwenye kundi moja kubwa linaloongozwa na mzungu mmoja anayefahamika kwa jina la Father Gin, lakini si Father hasa bali ni mkuu wa majasusi.”

ITAENDELEA

Post a Comment

0Comments

Your Thoughts

Post a Comment (0)