FRANKENSTEIN EPISODE 1

JABA PLANET.
FRANKENSTEIN
SURA YA KWANZA: UUMBAJI
EPISODE 1
      Ulikuwa usiku wa kiza kinene,usiku wa giza totoro,kiza cha 'mgunguna' ,usiku wa dhoruba kali mwishoni mwa mwezi wa Novemba.Kwenye maabara yake iliyoko chumba cha juu cha mnara wa Ingolstadt,huko Ujerumani,Dr. Victor Frankenstein alikuwa kainama mbele ya dude kubwa  mfano wa binadamu na lisilokuwa na uhai.

Lilikuwa karibu kuisha,ama kweli ni kiumbe aliyeiteka akili yake kwa asilimia kubwa mno,limeivuruga akili na roho yake Dr.Victor kwa takriban miaka miwili.Kwa msisimko ulioashiria uchovu,aliichunguza kazi ya mikono yake hatimaye akapata kila kitu kilikuwa sawa na alikwisha maliza uumbaji wake.Kilichobakia nikuwekelea vyombo vya umeme na kufanya uumbaji wake kupata uhai.

Frankenstein alifanya kazi yake ya mwisho na kusubiria,macho yake yaliangalia mahali pamoja tu,kwenye lile jitu aliloliuamba,mmh hakuwa hata na nafasi ya kupepesa macho yake.

Ilikuwa tayari imefika  saa moja asubuhi ,mvua ilikuwa ikinyesha na matone yake yalikuwa  yakigongagonga kupitia dirisha la maabara yake Dr.Victor Frankenstein.Kidogo mshumaa wake uzimike,kupitia mwangaza wake hafifu,aliyaona macho ya rangi ya njano nyepesi ya jitu lile aliloliumba yakifunguka,lilipumua kwaa nguvu kisha kwa  mtetemeko wa kutisha miguu ilitingika.

Kwa uoga wa hali ya juu,Dr.Victor Frankenstein aliliangalia janga hilo,lililomugarimu  sana nguvu,akili na maumivu kuliumba jitu hilo.

Ama kweli lilikuwa jitu kubwa lililokuwa na viungo sawia...

mmh  ngozi ya jitu lililoumbwa na Dr.Victor  ilikuwa ya njano na ilikuwa imeziba misuli na mishipa yenye nguvu  ndani yake.Nywele zake zilikuwa kama kichaka na weusi wa kumetameta,meno yake yalikuwa meupe yaliyomemetuka kama theluji mbele ya miale ya jua.

"Mungu wangu! alijisemea Dr.Victor .." Nimefanya kazi ngumu kwa takriban miaka miwili ilimradi niweze kurudisha uhai kwa mwili usio kuwa na uhai...Ndoto yangu ilikuwa ni kuhakikisha nimegundua siri ya maisha ama uhai ili niumbe race nyengine ya wanadamu...Ona sasa nimemaliza kuliumba jitu ambalo hata kuliangalia ni shida !"

Ndoto yake yote aliyokuwa nayo ilipotea.Baada ya kuliangalia jitu hilo kwa mara ya mwisho tena kwa uoga zaidi..alitoka mbio kwenye maabara na kuenda moja kwa moja hadi chumba chake cha malazi na kujirusha samadarini mwake akiwa na mavazi yake.Alitamani angalau apate lepe la usingizi...hatimaye baada ya kujisahau na kusahau kidogo kilichokuwa kikiendelea..usingizi ulimvamia vuum! Ila ulikuja na ndoto za kuogofya na kutisha ajabu.

Kwa mara ya kwanza alijipata yeye ni kijana mdogo ...akiwa na familia yake kwao nyumbani huko Swiss,Geneva alikozaliwa Frankenstein.Alimuona babake jamaa muhimu na wa kuheshimika sana na wote wanaomtambua,mamake mzazi iwapo kawa marehemu,kaka zake wadogo  wawili,Ernest na William, na Elizabeth pia alikuwa kama kiokote hakuwa mmoja wa familia ila walimpenda sana.

Hata alivyokuwa mdogo Victor Frankenstein alikuwa na hamu kubwa mno  ya kusoma  na kupata elimu.

...Akiwa kwenye chumba chake  cha malazi  kilichogubikwa na giza aliendelea kuota...mmh ndoto za kutisha kweli kweli...mara kaota mamake mzazi kaiaga dunia ..
Ghafla kajipata makaburini akiendelea na ndoto yake ya kujuwa chanzo cha uhai na uumbaji wake.Maono yake mahali pale kwenye giza na penye utulivu wa kutisha...shahidi pekee ulikuwa mwezi.

Mara Frankenstein aliinama mbele ya kaburi lililokuwa wazi...alifunguwa jeneza lililokuwa ndani mle na kuwacha mwili wazi...minyoo na mabuu yalikuwa yaking'ong'ona na kutambaa huku na kule.Frankenstein aliinama karibu zaidi..kwenye ubaridi..ni usiku ..kaona kivuli akadhania kamuona mamake..

...Frankenstein aligutuka kwenye lepe zito la usingizi akiwa kajawa na uoga...kavamiwa na wasiwasi mwili mzima.Kijasho chembamba kilimtiririka kwenye paji lake la uso.Meno yake yaligongana na miguu yake yote miwili ilitetemeka HALAFU sasa kupitia mwangaza hafifu wa mbalamwezi uliojilazimisha kupita chumbani mle kupitia kidirisha cha chumba  kile...aliliona lile jitu 'Monster' .

Jitu hilo lilitembea kwa mwendo wa kujivuta chumbani mle likimfuata Frankenstein...hili ni lile lile jitu la kutisha aliloliumba mwenyewe.

Kwa uoga zaidi aliokuwa nao Frankenstein...alisubiri pale pale.Jitu hilo lilizifungua pazia za kitanda.Macho yake...kama yanaweza kuitwa macho yalikuwa yakimkodolea Frankenstein.Lilifungua kinywa chake na kuonyesha taya zake na kutoa mlio wa kutisha kama cheko fulani vile lililoachia mikunjo kwenye mishavu yake.

Labda lingeongea lakini Frankenstein hakungojea kipindi hicho wala hakutaka kusikia.

Lilinyoosha mkono likijaribu kumzuia muumbaji wake lakini juhudi ziliambulia patupu,Frankenstein alihepa kwenye tundu la sindano,aliruka kutoka kitandani mle na kwa haraka zaidi aliteremka vigazi na kuelekea chini.Alijificha kwenye ua wa nyumba ile na kusikiliza kila hatua kwa umakini zaidi.Alikuwa akiogopa sana,kila mlio ulikuwa ukitangaza makaribio ya Pepo ama maiti yule aliyempea uhai.

Hakuna mwanaadamu yeyote yule anayeweza kuvumilia kuiona sura ile ya kutisha.Maiti kurudishwa uhai sio hali rahisi ya kuvumilia.Mwanzoni kabla halijamalizwa kuumbwa,Frankenstein alikuwa akiliangalia na halikupendeza kamwe.Lakini mishipa,misuli na viungo vilipopata uwezo wa kutembea Jitu hilo la kuogofya lilizidi kutisha.Na ule ukubwa wake,ukubwa  alioupanga Frankenstein ulizidisha ujitu wake.

...Kwenye ua ule uliojaa ubaridi,Dr.Frankenstein aliweza kuyasikia mapigo yake ya moyo yaliyopiga haraka na mfululizo hali iliyomfanya aweze kutambua kila ateri yake  mwilini mwake.Ijapokuwa kile kimvua kilikuwa kimeisha yale mawe mawe yaliyokuwa uani yalikuwa bado yakizizima kwa ubaridi uliokuwapo.Dr.Frankenstein aliegemea ukuta ulikuwa na unyevu unyevu na mikwaruzo.

Alikuwa kachoka kwelikweli kutokana na kazi  ngumu iliyochukuwa  miezi na vilevile kutokana  na usiku huo  wa kutisha.Kusema kweli alikuwa kachanganyikiwa,aliuhisi uchungu wa tamaa yake.Ndoto zake,matamanio yake ya kuumba race yake ya binadamu na  mambo yote aliyotarajia,yote yamegeuka kuwa tishio  kubwa ajabu Mabadiliko  yalikuwa haraka mno.

...Akiwa mgonjwa wa uoga,Frankenstein  alibaki uani mle usiku mzima...

   baada ya usiku mrefu na wakutisha hatimaye kulipambazuka.Asubuhi iliyojaa unyevu unyevu wa mvua iliyokuwa kanyesha tena usiku uliopita.

Ilikuwa saa kumi na mbili asubuhi hiyo ...Frankenstein alibumburuka alipokuwa na kuingia mtaani.Alitembea kwa mwendo na hatua za haraka haraka kama ambaye hilo ndilo lilikuwa suluhisho kamili la kulihepa Jitu lililokuwa likimuandama.Kusema kweli Frankenstein aliogopa sana kwa kila kona aliyopiga mtaani alidhania kama atakutana nalo.

Aliapa hatorudi kamwe kwenye jumba alilokuwa akiishi...alihisi kama anahitaji kuongeza mwendo ila alikuwa ametota kwa mvua iliyomnyeshea.Alihisi miguu yote haiwezi mbeba kwa sababu ilikuwa ikimuuma kwelikweli.

Aliendelea kutembea masafa marefu na kwa muda mrefu akijaribu kupunguzia akili mzigo  kwa kufanya mazoezi ya mwili.Alitembea vichochoro vya Ingolstadt hatimaye akafika kwenye kituo cha mabasi.Frankenstein alitulia kiasi  huku macho yake yakiangalia basi lililokuwa likikaribia...lilipokaribia zaidi ndipo aligundua lilikuwa basi la Swiss stagecoach.lilisimama alipokuwa akingojea.

Mlango ulipofunguliwa ...Frankenstein alimuona Henry Clerval rafiki yake wa dhati...rafiki wa kitambo na wakaribu zaidi..wawili hao walizungumza mengi.Frankenstein alifurahia uwepo wa rafikiy yake.Alimshika Cleval mkono na kwa muda kidogo akasahau uoga na vitisho .Kwa mara ya kwanza kwa muda wa miezi mingingi iliyopita alihisi amefurahia.

Wawili hao walitembea mtaani  mwa mji wa Ingolstadt wakielekea chuoni mwa kina Frankenstein.Njiani humo walikuwa wakiongeleeia  marafiki,familia  na habari njema za Clerval.

"Nimefaulu kumbembeleza babangu aniruhusu nisome  hapa chuoni Ingolstadt na wewe...Clerval alisema....

           
"Hakuna jambo linalonifurahisha kushinda uwepo wako," Frankenstein alimjibu rafiki yake Clerval.

"Lakini rafiki yangu nakuomba unipee habari kuhusu familia yangu...baba,kaka zangu na Elizabeth."Je,ni wazima kweli?"  Ulikuwa unapata muda mrefu...zaidi ya miaka minne  tangia awaone.

"Ni buheri wa afya na wote wanaendelea vizuri ila kwa kiasi fulani wako na wasiwasi...kwa sababu ni muda mrefu  hawajakuona wala kusikia habari kutoka kwako angalau hata kwa waraka." "Lakini rafiki yangu Victor ,"Clerval aliendelea..akimuangalia Frankenstein kwa uso.."Nimegundua kitu,nahisi wewe rafiki yangu ni mgonjwa kwa jinsi muonekano wako ulivyo...umekuwa mwembamba mno,umekonda,ni kama una siku kadhaa haujalala."

"Wala hujakosea rafiki yangu,umegonga ndipo,"Frankenstein alijibu akiwa mwingi wa uchovu.
"Nimefanya kazi ngumu..kazi iliyonifanya nilale kuchelewa kila siku,ilikuwa majaribio fulani yaliyoninyima hata nafasi ya kupumzika kama unavyoona.Lakini niko na matumaini tena makubwa zaidi kuwa kazi yenyewe imeisha na sai niko huru."

Frankenstein alitetemeka kwa uoga,hakutaka kufikiria wala kuelezea zaidi yaliyotokea usiku uliopita .Alitembea haraka haraka,hatimaye waliwasili chuoni.Aliangalia juu ya mnara  kulipokuwa na nyumba yake.Na kama lile jitu aliloliacha chumbani mwake litakuwa bado liko mle ndani,labda likiwa bado liko hai likitembea tembea pale ndani atafanyaje ? Aliingiwa na baridi,aliogopa zaidi huenda rafiki yake Clerval  akagundua jinsi alivyokuwa na wasiwasi.

Frankenstein alimsihi rafiki yake amngojee pale chini kwa dakika kidogo yeye akapanda vigazi hadi juu kabisa.Pole pole akaingia kwenye vigazi vidogo vilivyokuwa vikilenga kwenye mnara.
Alisimama tisti huku mkono wake kwenye kitasa cha mlango.Kijasho chembamba kilichoongozana na ubaridi fulani kilianza kumtoka.Alitetemeka kwa uoga kisha akaamua liwe liwalo...aliusukuma mlango kwa nguvu,kama mtoto mdogo akitarajia atakutana na jini vile upande wa ndani,lakini hakuna kitu chochote kilichotokea.

Kisha kwa uoga akajitosa ndani mle,chumba kilichokuwa kama cha maombi pia vile vile sebuleni kilikuwa kitupu.Chumba chake cha malazi pia kilikuwa kitupu hapakuwa na dalili yoyote hata ya mgeni wake wa kutisha.

Alianza kutafuta kila mahali,nyuma ya mapazia yote,ndani ya kabati,chumba chake cha kazi,chini ya meza na hata nyuma ya milango.Ndani mle mna vitu  kadhaa vilikuwa  vimetawanyika vkiwemo nguo,vitabu na vipande vya vioo.Ni kama vilikuwa vimetupwatupwa na mtu aliyekuwa kajawa na gadhabu.
Frankenstein alipohakikisha jitu halikuwa ndani mle hakuamini macho yake,alijawa na furaha ya ajabu.Alicheka kwa furaha na kwa haraka akateremka vigazi kuelekea alikokuwa kamuacha Clerval.

Frankenstein na Clerval walipanda tena hadi chumbani wakiwa pamoja na mtumishi akawaletea kiamsha kinywa.Frankenstein kwa raha aliyokuwa nayo hakuweza kujizuia.Sio raha tu iliyomvaa  bali alihisi  kama maelfu ya vipini  vikimtekenya mwilini  na mapigo ya moyo yalipiga haraka haraka.

Hakuweza kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu,mara karuka juu ya kiti,mara alipiga makofi  na kujichekea chekea.

Kwa mara ya kwanza Clerval  alidhania  mwenzake alikuwa akifurahikia ujio wake, lakini alipomchunguza kwa ukaribu na kwa  makini zaidi machoni mwa rafikiye aligundua kuna jambo lisilokuwa la  kawaida na hakuweza kuelewa  ni  nini.
Clerval aliendelea kusikiliza kicheko kilichomuogopesha na kumzidishia  mshangao.

"Mungu wangu! Hivi Victor uko na tatizo gani rafiki yangu?" Clerval aliongea kwa  sauti ya juu  na iliyojaa uoga.
"Usijichekee kiasi hicho! Wewe  waugua kwa  kiasi fulani! Ni  nini kilicho sababisha yote haya jamani?"

"Usiniulize maswali,"Frankenstein  aliongea huku akiziba macho yake asiweze kuona alichodhania  kiko mbele yao.Alichodhania kakiona lilikuwa lile jitu la  kutisha aliloliumba ,Monster,lilikuwa likiingia chumbani mle huku  mikono yake likiwa  limeinyosha.

"Muulize huyu,"alilia Frankestein  huku akinyosha kidole kilichotetemeka.
"Anaweza kukueleza.Ooh,niokoe mimi! Niokoe!"akifikiria lile  jitu limemkamata na  kumzuia.Frankenstein aling'ang'ana kwa  nguvu mwishowe  akaanguka chini.....

....ITAENDELEA....usikose sehemu ijayo...Mungu akulinde popote ulipo.

Simulizi za Mike  Gonard 

Hadithi & Simulizi Za Kijasusi 

jabaplanet.blogspot.com

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.