MAUWAJI YA HALAIKI
EPISODE 3
Taarifa bado zilikuwa zikiendelea kutolewa katika vyomba mbalimbali vya habari juu ya kutafutwa kwa Benedict. Kiasi cha shilingi milioni ishirini ambacho kilikuwa kimetolewa kilionekana kutokutosha kabisa hali iliyofanywa kuongezwa hadi milioni ishirini. Benedict akaonekana kuwa mtaji hali iliyowafanya watu kuzidi kumtafuta zaidi na zaidi.
Benedict akaonekana kuchoka kukaa sebuleni pale kutokana na macho yake kuwa mazito.Hapo hapo Benedict akainuka na kuelekea chumbani kulala. Hamidu alibaki peke yake pale sebuleni akiangalia televisheni. Moyo wala haukutulia, mvutano mkubwa ukaanza kuvutana ndani ya moyo wake. Upande mmoja ulimtaka aelekee katika kituo cha polisi na kutoa taarifa juu ya uwepo wa Benedict ndani ya nyumba ile lakini upande mwingine ulimkataza kufanya hivyo.
Hamidu hakujua afanye nini, alibaki kimya sebuleni pale huku macho yake yakiendelea kuangalia televisheni. Hamidu hakuendelea kubaki katika hali ile, nae akainuka na kuanza kuelekea chumbani kulala.
“Siwezi kuusaliti urafiki kwa milioni ishirini” Hamidu alijisemea huku akijitupa kitandani na kulala, hakuchukua muda mrefu, usingizi ukampitia.
Hamidu aliamka mara baada ya masaa matatu kupita. Moja kwa moja akayapeleka macho yake katika saa kubwa ya ukutani, tayari ilikuwa imetimia saa tisa alasiri. Hamidu hakutaka kuendelea kubaki sebuleni pale hali ambayo ilimfanya kuelekea sebuleni huku akimwacha Benedict kitandani.
Hamidu akaiwasaha televisheni, macho yake yakatua katika picha ya Benedict ambayo ilikuwa ikionyeshwa mara kwa mara katika televisheni tofauti tofauti. Kiasi kile cha shilingi milioni ishirini kikatangazwa tena kuwa kama zawadi kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa Benedict. Matatizo mbalimbali ya kifedha yakaanza kumiminika kichwani mwake.
Alimkumbuka mama yake ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa moyo, zilihitajika fedha kwa ajili ya matibabu. Mawazo ya matatizo yake hayakuishia hapo, akaanza kumkumbuka mpenzi wake, Salama ambaye alikuwa mjauzito. Salama alikuwa akihitaji matunzo na aliamini kama angekuwa na kiasi kie cha fedha basi mambo yangekuwa rahisi zaidi. Kila kitu katika kipindi hicho ambacho alikuwa akikifikiria kilikuwa kikihitaji fedha.
Hadi kufikia hatua hiyo, moyo wake haukutaka kufikiria urafiki tena, kwa haraka haraka akainuka kochini na kuanza kuelekea chumbani kwake. Akafungua droo ya kitanda na kutoa funguo zote za milango ya nyumba ile. Akatoka chumbani mule na kuanza kufuata mlango wa jikoni na kisha kuufunga. Hakuishia hapo, pia akaufuata mlango wa sebuleni na kisha kuufunga.
Akaanza kupiga hatua za haraka haraka kuelekea getini. Akili yake haikuwa ikifikiria kitu chochote zaidi ya fedha, tena kiasi ambacho kingemaliza matatizo yote ambayo alikuwa nayo. Hakutaka kumwambia mlinzi kitu chochote kile ka kuhofia kwamba nae angehitaji kiasi fulani cha fedha.
“Mbona unaonekana una haraka namna hiyo?” Mlinzi alimuuliza Hamidu.
“Narudi saa hivi”
“Unaelekea wapi?”
“Narudi sasa hivi” Hamidu alilirudia jibu lake.
Mlinzi akabaki kutokuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kinaendelea. Alitamani kuuliza swali jingine lakini hakupata nafasi hiyo kwani tayari Hamidu akawa amekwishapotea machoni mwake.
Hatua zake zilikuwa za haraka haraka, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka hali iliyomfanya kuchukua kitambaa chake na kuanza kujifuta. Katika kipindi hicho alikuwa akipiga hatua kuelekea katika kituo cha polisi cha Tandale huku kichwa chake kikiwa kinafikiria fedha kiasi cha shilingi milioni ishirini. Moyo wake ulikuwana furaha kwani hakuamini kama katika kipindi kichache kijacho angekuwa na kiasi kikubwa cha fedha. Moyo wake ulikuwana furaha kwani hakuamini kama katika kipindi kichache kijacho angekuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Ingawa alikuwa akitembea kwa hatua za haraka haraka lakini bado alijiona akitembea kwa mwendo wa taratibu. Moyoni alitamani apate mbawa katika kipindi hicho ili apae na kutua katika kituo cha polisi cha Tandale. Akili yake wala haikuukumbuka urafiki kati yake na Benedict, kitu ambacho alikuwa akikikumbuka ni milioni ishirini ambazo aliziona zikiwa mlangoni.
Hamidu akaanza kukimbia, kila mtu njiani alibaki akimshangaa lakini hilo wala hakuonekana kujali chochote kile. Kadri alivyozidi kupiga hatua kuelekea mbele na ndivyo ambavyo furaha ndani ya moyo wake ilivyozidi kuongezeka zaidi. Mara baada ya kutumia dakika kadhaa, akafika katika kituo cha polisi cha hapo Tandale.
“Vipi kijana?” Polisi mmoja alimuuliza Hamidu.
“Yu…po..nyu..mban..i” Hamidu alijibu huku akihema.
“Yupo nyumbani? Nani?”
“Benedi…ct…” Hamidu alijibu.
Kila polisi akaonekana kushtuka, jina ambalo alilitaja Hamidu ndilo ambalo lilionekana kuwashtua. Wote wakaanza kumwangalia Hamidu huku wakionekana kutokuamini kile ambacho kilitoka mdomoni mwa Hamidu.
“Unasemaje?”
“Benedict”
“Yupo wapi?”
“Nyumbani” Hamidu alijibu.
Kila polisi akaonekana kuchanganyikiwa kwa furaha, gari aina ya Defender likasogezwa karibu, polisi watano waliokuwa na bunduki mikononi mwao wakaingia pamoja na Hamidu. Gari likaanza kuendeshwa kwa mwendo wa kasi. Kila polisi akashikilia vizuri bunduki aliyokuwa nayo mkononi. Wananchi wakabaki wakishangaa, mwendo wa kasi wa gari lile uliwafanya kujua kwamba kuna kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
“Una uhakika kijana kwamba mtu huyo ni Benedict?” Polisi mmoja alimuuliza Hamidu.
“Asilimia mia tatu” Hamidu alijibu.
Gari likafunga breki katika eneo la Mafyoso Camp. Wahuni wote ambao walikuwa wakipita njia karibu na eneo la Camp hiyo wakaanza kukimbia. Polisi wote wakaruka chini kama makomandoo, wakaanza kupiga hatua kuelekea katika vichochoro huku wakimfuata Hamidu. Wananchi hawakuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kinaendelea mahali hapo, kila kitu kilichokuwa kikitokea kilionekana kuwa kama filamu.
Mlinzi akabaki kuwa na mshtuko mara baada ya kuwaona polisi waliokuwa na bunduki wakifika katika eneo hilo huku wakiwa na bunduki mikononi mwao. Moja kwa moja wakaingia ndani ya eneo la nyumba hiyo, polisi watatu wakaanza kuzungu zunguka katika eneo hilo huku polisi wawili wakiingia ndani pamoja na Hamidu.
Moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea chumbani. Mikono yao ilishikilia vizuri bunduki zao. Mara baada ya kuufikia mlango wa chumba kile, wakaufungua na kuingia ndani. Kitanda kilionekana kuwa kitupu, hakukuwa na mtu yeyote yule. Wakaanza kuangalia uvunguni mwa kitanda, kabatini na kila sehemu chumbani mule lakini hakukuwa na mtu yeyote.
Wakatoka chumbani na kuanza kuangalia katika kila sehemu ndani ya nyumba ile lakini napo hakukuwa na mtu yeyote yule. Kila mmoja akabaki kimya akimwangalia mwenzake. Hamidu alibaki akishagaa tu, hakuamini macho yake kama Benedict hakuwepo ndani ya nyumba hiyo na wakati milango ilikuwa imefungwa na funguo alikuwa nazo yeye mwenyewe.
“Vipi?” Polisi mmoja aliyeonekana kuwa kiongozi aliuliza.
“Hayupo”
“Mmeangalia vizuri?”
“Ndio mkuu”
“Hadi stoo na chooni?”
“Kila sehemu. Hakuna mtu”
Kila mmoja akakaa kimya huku wakimwangalia Hamidu ambaye alionekana kama kujifikira kitu. Hamidu akakaa katika hali hiyo kwa sekunde kadhaa, akaanza kupiga hatua kuelekea katika korido ndani ya nyumba hiyo. Moja kwa moja akayapeleka macho yake katika mlango wa kuingilia darini, mlango ulionekana kukaa upande tofauti na siku nyingine hali iliyoonyesha kuwa kuna mtu alikuwa ameufungua.
“Benedict….” Hamidu alisema kwa sauti ya chini huku macho yake yakiangalia mlango ule wa dari.
“Unasemaje?” Polisi mmoja aliuliza.
“Nafikiri atakuwa darini” Hamidu alijibu.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, hapo hapo polisi mmoja akaanza kupanda darini kwa msaada wa polisi wengine. Darini kulikuwa na giza kitu ambacho kilimfanya yule polisi kutokuona kitu chochote kile. Akaomba tochi, kwa haraka haraka Hamidu akaelekea chumbani kuleta tochi.
“Kuna dalili za kuwepo huko?” Polisi mmoja aliuliza.
“Ndio. Nasikia harufu ya pafyum huku” Polisi yule aliyekuwa darini alijibu. Hamidu wala hakuchelewa kurudi, ni ndani ya sekunde kadhaa akarudi mahali pale na kumgawia tochi polisi aliyekuwa darini.
Bado msako wa kumtafuta Benedict ulikuwa ukiendelea kama kawaida mitaani. Kila polisi alionekana kuchanganyikiwa kutokana na kutokupatikana kwa Benedict. Kamanda mkuu wa polisi, Bwana Idrisa alionekana kuchanganyikiwa zaidi. Ofisini hakukukalika kabisa, akili yake ilikuwa ikimfikiria Benedict tu. Kila alipokuwa akiziangalia picha za Benedict ofisini pale, alikuwa akipiga meza kwa hasira.
Kamanda Idrisa akaunyanua mkonga wa simu na kupiga namba fulani ambapo baada ya muda simu ikapokelewa na kuanza kuongea na mtu wa upande wa pili. Aliongea nae kwa takribani dakika tano, akakata simu. Bwana Idrisa alionekana kuwa na mawazo, hakuamini kama kweli mpaka muda huo Benedict hakuwa amepatikana japokuwa walikuwa wametangaza kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa Benedict.
Alikaa katika hali hiyo ya mawazo kwa takribani dakika thelathini, mara akashtushwa na sauti ya mlango ambao ulikuwa ukigongwa. Akatoa kauli ya kumtaka mgongaji kuingia ndani. Vijana watatu, wavulana wawili na msichana mmoja wakaingia ndani ya ofisi ile na kutoa salamu kwa kupiga saluti na kisha kukaa katika viti vilivyokuwa ndani ya ofisi hiyo.
Kamanda Idrisa hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya kwa muda huku akiwaangalia vijana wale ambao walikuwa mule ofisini mwake. Kwa kuwaangalia tu, vijana wale walionekana kuwa shupavu sana kutokana na miili yao kujengeka vizuri kutokana na mazoezi ambayo walikuwa wakiyafanya. Aliporidhika, akachukua moja ya faili ambalo lilikuwa pale mezani, akalifungua na kutoa picha za Benedict na kuziweka mezani.
“Mnamuona huyu?” Kamanda Idrisa aliwauliza.
“Ndio” Wote waliitikia kwa pamoja mara baada ya kuziangalia picha zile.
“Masaa kumi na moja yamepita tangu aiumize mioyo ya Watanzania” Kamanda Idrisa alisema na kuendelea.
“Kwa masaa hayo yote wananchi wameshindwa kumkamata kabisa na sidhani kama wataweza kumkamata. Kazi hii nawaachieni ninyi, fanyeni kazi hii kwa nguvu zote, tunamhitaji mtu huyu” Kamanda Idrisa aliwaambia vijana wale ambao walikuwa wapelelezi.
“Martin, Moody na Sabrina, tunamtaka mtu huyu ndani ya masaa sabini na mbili” Kamanda Idrisa aliwaambia.
“Usihofu mkuu. Ndani ya masaa hayo tutakuwa tumefanikisha zoezi hilo” Moody alimwambia kamanda Idrisa.
Mara baada ya kupewa maelekezo yote, wapelelezi wale wakatoka ndani ya ofisi ile huku wakiwa na picha tatu za Benedict. Wakalifuata gari lao ambalo walikuwa wamelipaki katika eneo la ofisi ile ya makao makuu ya polisi na kisha kuondoka mahali hapo.
Kila mmoja ndani ya gari alikuwa akifikiria lake, kazi ambayo ilikuwa mbele yao ilikuwa ngumu lakini kutokana na uzoefu mkubwa waliokuwa nao kazi ile ikaanza kuonekana kuwa nyepesi tofauti na kazi mbalimbali ambazo walikuwa wamezifanya kabla. Mafanikio makubwa ya kipelelezi ambayo walikuwa wameyapata katika kazi nyingi zilizopita ziliwapa nguvu za kuona kwamba walikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kufanikisha kile ambacho kilikuwa mbele yao.
“Hii ni kazi ndogo sana, yaani ni kama kumsukuma mlevi mlimani” Marini aliwaambia wenzake.
“Tuliwapata watu ambao waliisumbua serikali kwa kipindi kirefu sana, huyu hawezi kutusumbua hata mara moja” Moody alichangia.
“Nafikiri masaa tuliyopewa ni mengi sana, yaani naona tungepewa masaa matano tu” Sabrina alisema maneno ambayo yaliwafanya wote kuanza kucheka kwa uhakika wa kufanikisha kumkamata Benedict.
Mara baada ya kukabidhiwa tochi moja kwa moja polisi yule akaanza kumulika mule darini. Alimulika katika kila sehemu ndani ya dari lile lakini hakukuwa na mtu yeyote yule ni mabomba ya nyaya za umeme pamoja na mbao ndivyo ambavyo vilikuwa vikionekana mbele yake. Kadri ambavyo polisi yule alivyozidi kumilika darini mule na ndivyo ambavyo jasho lilivyozidi kumtoka kutokana na joto kali ambalo lilikuwa mule darini.
“Vipi tena? Mbona hausemi chochote?”
“Hakuna mtu. Mungu wangu!”
“Kuna nini tena?”
“Siamini!”
“Huamini nini?”
“Njooni muone” Polisi yule alisema.
“Acha hizo. Tuambie kuna nini?”
“Ametoroka. Bati limeachia, nafikiri alitoa baadhi ya misumali”
“Lakini si umesema kuna harufu ya pafyumu?”
“Harufu bado ipo ila yeye hayupo” Polisi yule alijibu.
Jibu lile lilionekana kumchanganya kila mtu aliyelisikia. Hawakuonekana kuamini kama kile walichokisikia kilikuwa sahihi au walikuwa wamesikia vibaya. Polisi yule akateremka, Mwili wake ulikuwa umejaa jasho huku shati lake likionekana kuchafuka. Hawakutaka kuendelea kubaki ndani ya nyumba ile, wote wakaanza kutoka nje na kumfuata mlinzi ili kutaka kufahamu mahali alipokuwa Benedict.
“Mgeni wangu yupo wapi?” Hamidu alimuuliza mlinzi ambaye alionekana kutetemeka.
“Sijui yupo wapi”
“Hakutoka hapa?”
“Hakuna aliyeingia wala kutoka” Mlinzi alijibu.
Kila mmoja akaonekana kuchoka. Walimwangalia mlinzi mara mbili mbili huku wakionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akiwaambia. Milioni ishirini zilizokuwa kichwani mwa Hamidu zikaanza kupotea, matatizo ambayo alikuwa nayo aliyaona kuendelea kama jinsi ambavyo yalivyokuwa. Machozi yakaanza kumlenga kwani hakuamini kama Benedict angeweza kutoroka ndani ya nyumba ile na kumfanya kukosa kiasi cha shilingi milioni ishirini ambacho kilitangazwa kuwa kama zawadi kwa yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.
Joto lilikuwa kali darini kutokana na jua ambalo lilikuwa likiendelea kumulika na kulifanya bati la nyumba ile kupata joto. Darini kulikuwa na giza kitu ambacho kilimfanya kutokuona kitu chochote kile. Benedict hakutaka kufanya kitu chochote kile, alitulia kwa muda huku akiyapa nafasi macho yake kulizoea giza lililokuwa kule darini. Ni ndani ya dakika mbili tu, macho yake yakaanza kuona kila kitu.
Ni mbao zilizoshikilia bati na mabomba yaliyokuwa na nyaya za umeme ndivyo vitu ambavyo vilikuwa vikionekana mule darini. Benedict akaingia ndani zaidi, jasho likaanza kumtoka huku kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo joto lilivyozidi kuongezeka. Hakukuonekana kuwa na njia yoyote ile ambayo ingemfanya kutoka salama ndani ya nyumba ile.
Kitu alichokifanya ni kuanza kutembea chini chini hadi kufika katika sehemu ambayo ilikuwa karibu na nje. Akajilaza chali juu ya kenchi na kisha miguu kuipeleka kwenye bati. Kwa kutumia nguvu zote ambazo alikuwa nazo, akaanza kulisukuma bati lile kwa juu huku wakati mwingine akiligongagonga. Akaendelea kupiga zaidi na zaidi tena kwa nguvu zote, mara bati likaanza kwenda juu huku misumali ile ambayo iliishikilia bati lile ikianza kuachia.
Nguvu alizokuwa nazo zikaongezeka zaidi kwani alitumaini kwamba kazi ile wala haikuwa ngumu kama alivyofikiria kabla, aliendelea zaidi na zaidi. Nguo zake zote ambazo alikuwa amezivaa zilikuwa zimeloana kana kwamba alikuwa amemwamgiwa ndoo ya maji. Kadri alivyokuwa akifikiria jinsi alivyokuwa akitafutwa na polisi na ndivyo ambavyo alipta nguvu zaidi ya kufanya kile ambacho alikuwa akikifanya kwa wakati ule. Akili yake haikutaka kukubali kabisa kama Hamidu alikuwa ameelekea sehemu nyingine zaidi ya kituo cha polisi.
Taratibu misumali ikapanda zaidi hadi kuachia mbao. Benedict akalisogeza bati kwa nguvu zote na kuliinua upande ule aliokuwa na kisha kuanza kupitisha kichwa. Hali ilionekana kuwa ngumu sana kwake lakini aling’ang’ania mpaka akafanikiwa huku akiwa amejichuna vya kutosha. Akafanikiwa kutoka, akajirusha mpaka chini, akaangalia katika kila upande, hakumuona mtu yeyote yule.
Sauti za watu zikaanza kusikika masikioni mwake, akajisogeza pembezoni mwa ukuta na kuanza kuchungulia kule kulipokuwa na geti. Akapigwa na mshtuko mara baada ya kumuona Hamidu akiwa na polisi watano huku wakiingia ndani ya eneo la nyumba ile. Hakutaka kubaki mahali hapo ili kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea, alichokifanya ni kuuparamia ukuta na kutokea upande wa pili na kuondoka zake huku akimshukuru Mungu kwa kumtoa salama ndani ya nyumba ile.
Wapelelezi, Martin, Moody na Sabrina hawakutaka kupoteza muda. Moja kwa moja wakajiweka tayari na kuanza kazi ya kumtafuta Benedict kwa masaa sabini na mbili tu. Kitu walichokifanya ni kuanza kuelekea Mwenge alipokuwa akiishi Benedict huku lengo lao likiwa ni kutaka kupata kila kitu walichokihitaji kuhusu Benedict.
Mara baada ya kufika nje ya geti, dereva akaanza kupiga honi ambako baada ya muda mchache, Angelina akafika getini na kufungua geti. Gari likaingizwa ndani hadi katika sehemu ya maegesho. Wapelelezi wakateremka, wakaongea kidogo na Angelina na kisha kuanza kuelekea ndani huku dhumuni lao likiwa kutaka kuongea na Bi Meriana.
Wakajiweka kochini, Angelina akaondoka mahali hapo kuelekea chumbani na baada ya muda akarudi sebuleni hapo akiongozana na mama yake, Bi Meriana. Uso wa Bi Meriana ulionekana kuwa na majonzi, macho yake yalikuwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba katika kipindi kichache kilichopita alikuwa akilia. Huku akionekana kuwa na uchovu, akajiweka kochini na kuanza kuangaliana na wapelelezi wale.
Wakabaki wakiangaliana kwa muda fulani. Kitu walichokifanya wapelelezi wale ni kutoa vitambulisho vyao na kumgawia Bi Meriana ambaye akaanza kuviangalia. Aliviangalia kwa sekunde kadhaa, aliporidhika, akawarudishia.
“Tunahitaji kufahamu baadhi ya vitu kuhusu Benedict” Martin alimwambia Bi Meriana.
“Vitu gani?”
“Vitu vyote ambavyo tutaviulizia” Martin alijibu.
Wote wakaanza kutoa karatasi pamoja na kalamu walizokuwa nazo tayari kwa kuandika maelezo ambayo walitarajia kuyapata kutoka kwa Bi Meriana na Angelina. Ukimya ukatawala mahali hapo kwa dakika kadhaa na baada ya muda maongezi yakaendelea.
“Hupendelea kwenda sehemu gani baada ya mapumziko ya muda mrefu nyumbani?” Martin aliuliza huku mkono wake ukijiandaa kuandika.
“Kwa marafiki zake mbalimbali” Angelina alijibu.
“Marafiki hao wanaishi maeneo gani”
“Maeneo tofauti tofauti, Magomeni, Ilala, Tandale, Mbag…….”
“Na vipi kuhusu kumbi za starehe?” Moody alidakia kwa kuuliza swali.
“Shindwa. Mwanangu ni Mkristo safi hawezi kwenda sehemu kama hizo” Bi Meriana alijibu huku akionekana kukasirishwa na swali lile.
“Samahani. Vipi kuhusu ufukweni?”
“Ni mara chache sana huenda huko”
“Nyakati gani?”
“Jioni” Angelina alijibu.
Maswali hayakuendelea tena, wakaweka makaratasi yao ndani ya vitabu vyao, wakainuka, wakaaga na kuondoka mahali hapo. Vichwa vyao tayari vikaanza kupata picha fulani, kutokana na ujuzi mkubwa waliokuwa nao katika kazi ile, tayari walionekana kufahamu baadhi yavitu ambavyo waliviona vingewasaidia. Wakaingia ndani ya gari lao, nyuso zao zilikuwa zikionyesha tabasamu ya mafanikio. Gari likawashwa na kuondoshwa ndani ya eneo la nyumba hiyo.
“Umepata picha gani?” Sabrina aliuliza.
“Kuna asilimia kubwa atakuwa ufukweni” Martin alijibu.
“Kwa nini?”
“Hawezi kwenda sehemu nyingine tofauti na hiyo kwani anajua kwamba anatafutwa”
“Ok! Unafikiri fukwe gani? Coco au?”
“Haiwezekani kuwa huko”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu ya idadi kubwa ya watu” Martin alijibu.
Benedict hakutaka kuendelea kupoteza muda katika upande wa pili wa nyumba ile ambayo ilikuwa ikikaliwa na Hamidu. Akaanza kukimbia huku akipita katika vichochoro tofauti. Sauti kubwa ya muziki wa taarabu ikaanza kusikika masikioni mwake, Benedict akapunguza kasi, akaanza kutembea kwa mwendo wa kawaida kuelekea kule ilipokuwa ikitokea muziki wa taarabu.
Benedict akaiweka vizuri kofia yake kwa kuishusha zaidi ili kuuziba uso wake. Akaendelea mbele zaidi hadi alipokimaliza kichochoro kile. Akatokea katika sehemu iliyokuwa na eneo kubwa. Idadi kubwa ya watu wasiopungua sabini walikuwa katika eneo hilo, maspika makubwa zaidi ya matano yalikuwepo katika eneo hilo.
Benedict hakutaka kupoteza muda mahali hapo, akaanza kutembea kuelekea katika upande mwingine kwa kupita katikati ya watu waliokuwa wakicheza muziki ule wa taarabu. Hakukuwa na mtu yeyote abaye alikuwa akifahamu kwamba mtu yule ambaye alikuwa akipita katikati yao alikuwa Benedict, muuaji ambaye alikuwa akitafutwa na Watanzania katika kipindi hicho.
Mara baada ya kutoka katika eneo lile lililokuwa na ‘rusha roho’ moja kwa moja Benedict akaendelea na safari yake. Maswali kibao bado yalikuwa yakiendelea kumiminika kichwani mwake juu ya usaliti ambao aliufanya rafiki yake, Hamidu dhidi yake. Moyo wake haukuamini hata kidogo kama Hamidu angeweza kufanya kile alichokifanya cha kumletea polisi ili wamkamate.
Hakutaka kumuamini mtu mwingine yeyote, Hamidu alionekana kumpa picha halisi juu ya marafiki zake wengine ambao alikuwa nao. Mara baada ya kufika katika barabara ya vumbi, akaanza kunyoosha moja kwa moja huku lengo lake likiwa ni kutaka kufika katika kituo cha mabasi cha Argentina kwa kupitia katika soko kuu la Tandale.
Alitumia dakika kumi mpaka kufika katika kituo cha daladala cha Argentina, akapanda daladala iendayo Kariakoo. Stori kuhusu yeye ndizo ambazo zilikuwa zimetawala ndani ya daladala ile. Benedict hakuonekana kushtuka, akabaki katika hali ile ile ya kawaida. Gari lilipofika katika kituo cha Usalama, Magomeni, akateremka na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea katika kituo cha Magomeni Hospitali.
Picha zake zilikuwa zimezagaa katika kila sehemu alizokuwa akipita. Kofia yake bado ilikuwa kichwani mwake, uso wake alikuwa ameuinamisha chini kwa kuhofia kujulikana na watu ambao alikuwa akipishana nao. Kutoka Usalama hadi Magomeni Hospitalini alitumia dakika tano tu akawa amekwishafika katika katika kituo hicho ambapo akachukua daladala iliyokuwa ikielekea Kawe.
“Yaani siku ya pili hii, hata dalili za kukamatwa kwake hazijajionyesha” Mzee mmoja aliongea kwa sauti huku mkononi akiwa na gazeti la Ze Utamu. Kila abiria aliyekuwa ndani ya daladala ile akageuka na kumwangalia mzee yule.
“Yaani hata tetesi kuwa alionekana Mwenge” Kijana mmoja alimwambia mzee yule.
“Kama alionekana kwa nini sasa wasimkamate? Huo ni uongo” Mzee yule alisema.
Benedict akazidi kuuficha uso wake vizuri kwa kutumia kofia ile kwani hali ilivyoonekana ndani ya daladala ile, ni lazima angepigwa hata kabla ya kupelekwa polisi kama tu angegundulika. Safari bado iliendelea mbele, abiria wengine walikuwa wakiteremka na kupanda lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye aligundua kama Benedict alikuwepo ndani ya daladala ile.
Mara baada ya kufika katika kituo cha Sanaa, Benedict akateremka, akavuka barabara na kuanza kupiga hatua kuelekea ufukweni. Benedict hakuonekana kujiamini, mara kwa mara macho yake yalikuwa yakiangalia nyuma kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akimfuatilia. Alitumia mwendo wa dakika kumi hadi kufika ufukweni. Benedict akaendelea kupiga hatua hadi katika sehemu ambayo ilionekana kufaa machoni mwake.
Macho yake yalikuwa yakiangalia jinsi ambavyo mawimbi yalikuwa yakipiga nchi kavu. Furaha ya kulichoma kanisa na kuua watu zaidi ya mia mbili na hamsini bado iliendelea kuwepo ndani ya moyo wake. Aliporidhika kuangalia mawimbi yale, akayapeleka macho yake katika kioo cha saa yake na kugundua kuwa ni saa kumi na mbili na nusu jioni.
Benedict akayaamisha macho yake kutoka katika kioo cha saa yake na kuyapeleka pembeni. Benedict akapigwa na mshtuko mkubwa mara baada ya kuyagonganisha macho yake na ya mwanamke ambaye alikuwa amekaa mchangani. Msichana yule akashtuka kupita kiasi, akamwangalia vizuri Benedict huku akionekana kuamini kile ambacho alikuwa akikiona mbele yake.
Kwa mbali msichana yule akaanza kutetemeka kwa woga, kwa haraka haraka akainuka kutoka pale alipokuwa na kuanza kuondoka huku akianza kugeuka geuka nyuma kumwangalia Benedict. Mara baada ya msichana yule kupotea machoni mwake, hapo hapo akainuka na kuanza kuelekea sehemu nyingine ambapo kulikuwa na mawe mengi. Wala hazikupita dakika nyingi, mara akamuona yule msichana akirudi pale ufukweni akiongozana na polisi aliyeonekana mlinzi ambaye alikuwa na bunduki mkononi.
MAUWAJI YA HALAIKI
NO :24
Safari ya kuelekea katika ufukwe wa Msasani bado ilikuwa ikiendelea. Mara baada ya kufika Sanaa, Moody akalikata gari kona ya upande wa kulia na kuanza kuelekea katika ufukwe huo. Njia nzima, wapelelezi walikuwa makini kuwaangalia watu ambao walikuwa wakipishana nao. Walichukua dakika tatu wakafika katika ufukwe huo ambako kulikuwa na idadi ndogo ya watu.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye aliteremka garini, walibaki humo huku wakiyapeleka macho yao katika kila kona ufukweni hapo. Dalili za uwepo wa Benedict hazikuwepo kabisa ufukweni hapo. Huku Moody akianza kuingiza gia tayari kwa kuliondosha gari ufukweni hapo, ghafla macho yake yakatua kwa msichana ambaye alikuwa akitembea kwa mwendo wa haraka haraka huku akiangalia nyuma.
“Nafikiri kuna kitu kinaendelea” Moody aliwaambia wapelelezi wenzake.
“Sabrina, mfuatilie msichana yule” Moody alimwambia Sabrina.
Kwa haraka sana pasipo kupoteza muda, Sabrina akateremka garini na kuanza kumfuatilia msichana yule. Yule msichana hakuonekana kujiamini, muda wote alikuwa akiangalia angalia nyuma. Sabrina hakutaka kumuacha msichana yule mbali, alimuacha umbali wa hatua kumi tu. Safari ya msichana yule iliishia mbele ya geti kubwa ambako kulikuwa na mlinzi mmoja aliyekuwa na bunduki kubwa.
“Yupo kuleeee….” Yule msichana alimwambia mlinzi yule.
“Nani?”
“Benedict…..Benedict Matimya” Msichana yule alijibu.
Mlinzi yule akaonekana kushtuka, alimwangalia msichana yule mara mbili mbili huku akioenekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kinywani mwake. Akaishika vizuri bunduki ile na kuanza kuondoka na msichana yule kuelekea kule ufukweni. Kichwa cha mlinzi yule kikaanza kufikiria fedha, milioni ishirini ambazo kila siku zilikuwa zikitangazwa zikaonekana kumchanganya na kujiona akiwa tajiri.
Sabrina akaanza kupiga hatua kuelekea kule ambako alikuwa amewaacha wenzake ndani ya gari. Macho yake hayakuacha kumwangalia mwanamke yule na askari yule ambao walikuwa wakizidi kuondoka kuelekea ufukweni. Mara baada ya kulifikia gari lile, akaufungua mlango na kuingia ndani.
“Vipi?” Martin aliuliza
“Endesha gari kuelekea kule, wafuate wale. Yupo kule” Sabrina alimwambia Moody.
Hakukuwa na cha kuuliza tena, Moody akawasha gari na kuanza kuelekea kule walipokuwa wakielekea askari yule na mwanamke yule. Waliendelea mbele kwa mwendo fulani, Moody akasimamisha gari na wote kuteremka. Wakaanza kutembea kwa mwendo wa haraka haraka kule ambapo mwanamke yule na askari walipokwa wakielekea. Wakaziandaa bunduki zao vilivyo kwani kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Benedict alikuwa kule.
“Yuko wapi sasa?” Waliisikia sauti ya askari yule ikiuliza.
“Alikuwa hapa. Nilimwacha hapa. Alikuwa amevaa kofia kubwa” Mwanamke yule alijibu.
Martin na wapelelezi wenzake wakajifanya kutokujishughulisha na kitu chochote kile, wakaanza kuyapeleka macho yao katika kila kona ufukweni pale. Hakukuwa na uwepo wa Benedict mahali pale. Waliendelea kuangalia angalia katika kila kona mahali pale huku giza likiendelea kuingia lakini wala Benedict hakuonekana ufukweni pale hali iliyowafanya kuanza kukata tamaa.
“Martin……Moody…” Sabrina aliwaaita. Kwa haraka haraka Martin na Moody wakaanza kumfuata Sabrina ambaye alikuwa amesimama karibu na ukuta uliozunguka hoteli ya Casanova.
“Angalieni ukuta huu” Sabrina aliwaambia.
“Mbona sijakupata. Unamaanisha nini?” Moody aliuliza.
“Hauoni alama za viatu? Atakuwa ameruka kuingia katika eneo la hoteli hii” Sabrina aliwaambia.
Hawakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika sehemu walipokuwa wamelipaki gari lao, wakaingia ndani na kuanza kuelekea mbele ya hoteli ile. Ndani ya gari, kila mmoja alikuwa kimya huku bunduki zao zikiwa viunoni mwao, kila mmoja aliona kwamba Benedict atakuwa amechukua chumba ndani ya hoteli ile. Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamekishafika ndani ya eneo la geti lile na kuteremka garini.
“Kuna mtu yeyote aliyetoka?” Martin alimuuliza mlinzi mara baada ya kumuonyeshea vitambulisho vyao.
“Muda gani?”
“Ndani ya dakika tano zilizopita”
“Hapana”
Hawakutaka kupoteza muda, walichokifanya ni kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu ya mapokezi hotelini hapo. Mara baada ya kufika mapokezini pale, wakatoa vitambulisho vyao na kumuonyeshea dada yule aliyekuwepo pale mapokezini. Macho yao wala hayakutulia, walikuwa wakiangalia katika kila kona mahali pale ili Benedict asiweze kuwatoroka tena.
Wapelelezi wakapewa ruhusa ya kumtafuta Benedict katika maeneo ya hoteli ile. Walimtafuta katika kila kona ndani ya maeneo ya hoteli ile lakini hawakuweza kumpata. Kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa, hawakuelewa sehemu ambayo Benedict alipokuwa amejificha. Wapelelezi hawakutaka kuridhika, moja kwa moja wakarudi mapokezini na kuomba ruhusa ya kumtafuta Benedict katika vyumba ndani ya hoteli ile.
“Hawezi kuwa huko jamani. Hawezi kuwa huko” Dada wa mapokezi aliwaambia.
“Kwa nini isiwezekane?”
“Ataingia chumba gani? Atatumia funguo zipi?”
Hakukuwa na mtu ambaye aliyajibu maswali yale ambayo yalikuwa yameulizwa na dada yule, walibaki wakiangaliana tu. Ingawa dada yule wa mapokezi alikuwa amewaambia kwamba Benedict hakuwa kaika chumba chochote ndani ya hoteli ile lakini wakaonekana kabisa kutokukubaliana nae.
“Acha tufanye upekuzi tu. Bado hatujaridhika” Martin alimwambia dada yule.
Dada wa mapokezi hakutaka kuendelea kuweka mgomo, alichokifanya kwa wakati huo ni kumpigia simu mmiliki wa hoteli ile, Bwana Matemba. Zilipita dakika kumi, gari moja la kifahari likaanza kuingia ndani ya hoteli ile na kisha mzee mmoja ambaye alikuwa na ndevu zilizojaa mvi kuteremka na kuanza kuelekea mapokezini.
“Kuna nini Shannia?”
“Kuna watu kutoka katika makao makuu ya polisi” Shannia alijibu.
Wapelelezi wakatoa vitambulisho vyao na kisha kumgawia mzee Matemba ambaye alivichukua na kuanza kuviangalia. Aliviangalia kwa sekunde kadhaa, aliporidhika, akawarudishia.
“Na vipi kibali cha kufanya upekuzi?” Bwana Matemba aliwauliza
“Hicho hatuna kwa sababu kitu chenyewe kimetokea ghafla” Martin alijibu.
Mzee Matemba hakuwa na kipingamizi, akawaruhusu wapelelezi waanze kufanya msako ndani ya vyumba vilivyokuwa katika hoteli ile ingawa vyumba vingine vilikuwa na wageni. Msako ukaanza kufanyika kutoka katika chumba kimoja hadi kingine. Kila mmoja alikuwa makini, walimtafuta katika kila vyumba, bafu na vyoo lakini Benedict hakuwepo huko hali iliyoonekana kuwachanganya.
“Vipi?” Mzee Matemba aliwauliza.
“Hayupo” Moody alijibu.
Wapelelezi hawakutaka kubaki mahal hapo, walichokifanya ni kuanza kutoka nje. Wakaangalia saa zao, ilikuwa imekwishaingia saa moja na dakika kumi usiku huku sauti ya muziki ikisikika kutoka katika ukumbi ambao ulikuwa jirani na hoteli ile. Wakaingia katika gari lao lakini hata kabla hawajaondoka, Martin akateremka hali iliyowafanya Moody na Sabrina kushtuka.
“Nina machale. Nisubirini” Martin aliwaambia.
Martin akaanza kupiga hatua za haraka haraka kumfuata mlinzi, alipomfikia, akaanza kuongea nae maongezi ambayo yalichukua dakika moja tu. Hapo hapo Martin akaanza kupiga hatua kuelekea nyuma ya hoteli ile huku akiongozana na mlinzi yule. Walipofika nyuma ya hoteli ile, Martin akauparamia ukuta.
“Huku kuna nini?”
“Ukumbi wa starehe. Kuna bendi ya Twanga Pepeta itapiga hapo usiku wa leo baadae” Mlinzi alijibu.
Martin akaendelea kuchungulia zaidi na zaidi ndani ya ukumbi ule. Baadhi ya watu wachache walikuwa wametulia vitini huku wengine wakilishughulikia jukwaa ambalo lilitarajiwa kutumika katika usiku huo. Macho ya Martin yakaendelea zaidi na zaidi kuchungulia. Mara moyo wake ukamlipuka kupita kawaida mara alipomuona mtu ambaye alikuwa na uhakika kwamba alikuwa Benedict japokuwa alikuwa amevalia kofia kubwa.
“Benedict….Benedict…” Martin alikuwa akijisemea huku macho yake yakimwangalia mwanaume yule ambaye aligeuka nyuma na kuyafanya macho yao kugongana.
“Ndiye yeye. Ndiye yeye” Martin alisema kwa mshtuko huku akionekana kutokuamini.
Mara baada ya Benedict kuuparamia ukuta ule akafanikiwa kuingia katika eneo la hoteli ya Casanova. Benedict akaanza kupiga hatua kuelekea katika upande uliokuwa na geti la kutokea hotelini pale. Hata kabla hajafika, akapigwa na mshtuko mara baada ya kuliona gari moja likiingia ndani ya hoteli ile jambo ambalo likaonekana kumtia wasiwasi.
Akajificha, vijana watatu wakateremka na kuanza kuongea na mlinzi. Tayari Benedict alikuwa ameshikwa na wasiwasi zaidi, alichokifanya ni kuyapeleka macho yake katika ukuta ambao ulikuwa umetenganisha ukumbi mmoja wa muziki na hoteli ile na kisha kuuparamia.
Akayapeleka macho yake upande wa pili, akawaona watu zaidi ya ishirini wakiwa wamekaa katika viti ukumbini pale huku wakiwa wamempa mgongo na wengine wakiandaa jukwaa. Benedict hakuonekana kujali uwepo wa seng’enge zilizokuwa na ncha kali, akajipenyeza na kisha kushukia upande wa pili huku mwili wake ukiwa umetobolewa na seng’enge zile.
Benedict akaanza kupiga hatua kukifuata kiti kimoja kilichokuwa mahali pale ndani ya ukumbi ule na kisha kutulia huku kofia yake aina ya Malboro ikiwa vizuri kichwani mwake. Benedict hakutaka kuondoka mahali pale kwani kulionekana kuwa na ulinzi mkubwa kwake, Muda uliendelea kusonga mbele, mara baada ya nusu saa kupita, akayageuza macho yake na kuangalia pale ukutani aliporukia.
Benedict akapigwa na mshtuko mara baada ya macho yake kugongana na macho ya mtu ambaye alionekana kumtilia mashaka. Walahazikupita hata sekunde tano, yule mtu akaacha kuchungulia. Wasiwasi ukaanza kumshika Benedict. Akajiona kuwa karibu kukamatwa.
MAUWAJI YA HALAIKI
NO :25
Mara baada ya Benedict kuuparamia ukuta ule akafanikiwa kuingia katika eneo la hoteli ile ya Casanova. Akaanza kupiga hatua kuelekea katika upade mwingine ambao ulikuwa na geti. Hata kabla hajapiga hatua zaidi kuelekea kule getini, akapigwa na mshtuko mara baada ya kuliona gari moja likiingia ndani ya eneo la hoteli ile.
Benedict akajificha huku wasiwasi ukianza kumkamata. Milango ya gari lile ikafunguliwa na vijana watatu kuteremka na kisha kuanza kuongea na mlinzi. Wasiwasi zaidi ukaonekana kumshika, alichokifanya ni kuanza kuuangalia ukuta ambao ulikuwa ukitenganisha hoteli ile na ukumbi na kisha kuuparamia huku akionekana kutokuziogopa seng’enge zilizokuwa ukutani pale.
Akayapeleka macho yake katika upande ule wa ukumbi, watu zaidi ya ishirini walikuwa wamekaa vitini huku wengine wakitengeneza jukwaa la burudani. Hakuonekana kujali ncha za seng’enge zile, akarukia upande wa pili. Mwili wake ulichomwachomwa na ncha za seng’enge zile, damu zikaanza kumtoka.
Benedict akaanza kupiga hatua kukifuata kiti kimoja kilichokuwa ndani ya ukumbi ule huku kofia yake aina ya Malboro bado ikiwa kichwani mwake. Sehemu ile ikaanza kuonekana kuwa ulinzi mkubwa kwake. Baada ya dakika thelathini kupita, akageuka nyuma na kuanza kuangalia pale ukutani alipokuwa amepandia kuingilia ukumbini hapo.
Benedict akapigwa na mshtuko hasa mara baada ya macho yake kugongana na macho ya mtu ambaye alionekana kumtilia mashaka. Wala hazikupita hata sekunde kumi, yule mtu akaacha kuchungulia. Wasiwasi ukamshika Benedict, akajiona kuwa karibu kukamatwa, alijua ni lazima mtu yule angezunguka upande wa pili na kuingilia kupitia mlango wa mbele. Akili yake haikufikiri kitu kingine zaidi ya kitu kimoja tu ambacho kingemfanya kutoka salama mahali pale.
Kwa haraka haraka Martin akashuka ukutani na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea kule wenzake walipokuwa. Mlinzi hakuonekana kuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kinaendelea, alichokifanya ni kuanza kumfuata Martin mpaka kule lilipokuwa gari walilokuja nalo mahali hapo.
“Mbona haraka hivyo?” Sabrina aliuliza huku akionekana kumshangaa Martin
“Shukeni……Twendeni”
“Wapi?”
“Kule. Benedict yupo kule” Martin alijibu.
“Unasemaje?”
“Twendeni”
Martin hakutaka kupoteza muda mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kuelekea nje ya hoteli ile huku akiwa kwenye mwendo wa kasi. Sabrina na Moody hawakutaka kubaki mahali pale, walichokifanya ni kuanza kumfuata Martin
Mara baada ya kufika katika geti la kuingilia katika eneo la ukumbi ule, wakajitambulisha kwa mlinzi huku wakimuonyeshea vitambulisho vyao. Mlinzi hakuonekana kuamini kabisa, moyo wake ulikuwa mgumu kuamini kama kweli mpelelezi kama mpelelezi angeweza kujitangaza wa mtu kwamba alikuwa akifanya kazi hiyo.
“Kuna mtu tumekuja kumchukua” Martin alimwambia mlinzi.
“Sitowaruhusu hadi mtoe viingilio” Mlinzi aliwaambia.
Kila mmoja akaonekana kumshangaa mlinzi, maneno ambayo aliongea yalionekana kuwashangaza. Hawakutegemewa kudaiwa viingilio katika geti lile kwani walijua fika kwamba viingilio vilikuwa vikichukuliwa katika mlango wa mwisho kuingilia ukumbini mule kwani baadhi a magari yalikuwa yamepaki katika eneo kubwa la ukumbi ule.
“Lakini sisi ni map……” Martin alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, mlinzi akaingilia.
“Sogeeni kwanza nifungue geti” Mlinzi aliwaambia.
Geti likafunguliwa na teksi iliyokuwa na vioo vilivyokuwa na tinted kutoka. Wapelelezi wakazidi kuchanganyikiwa zaidi, walichokifanya ni kuacha kuongea kwa kauli za kulazimisha, wakaanza kuongea na mlinzi kinyenyekevu. Walimbembeleza mlinzi kwa dakika tatu na ndipo akawaruhusu kuingia.
Wakaanza kupiga hatua za haraka haraka kuufuata mlango mkuu wa kuingilia ndani ya ukumbi ule. Mlangoni wala hakukuwa na mtu yeyote yule jambo lililowafanya kuingia hadi ndani. Bado watu walikuwa wakiendelea kulipamba jukwaa ukumbini mule kwa ajili ya muziki ambao ulitarajiwa kupigwa na bendi ya Twanga Pepeta usiku wa saa nne.
Walichokifanya ni kuanza kumtafuta Benedict ndani ya ukumbi ule, kitu cha kushangaza, Benedict hakuonekana. Hawakutaka kuridhika, walichokifanya ni kuelekea mpaka chooni lakini napo huko wala Benedict hakuonekana hali ambayo ilianza kuwachanganya.
“Lakini si ulisema ulimuona! Mbona hayupo?” Moody alimuuliza Martin.
“Hata mimi mwenyewe na shangaa. Nilipochungulia mwanzao, alikuwa amekaa hapa” Martin alijibu.
“Ulipomuona alikuona?”
“Ndio”
“Basi atakuwa ametoroka” Moody alisema.
Hawakutaka kuendelea kubaki ndani ya ukumbi ule, walichokifanya ni kuanza kuelekea nje ya ukumbi ule hali iliyowafanya watu waliokuwa mule ukimbini kuanza kuwashangaa. Walichokifanya ni kuanza kumtafuta katika kila eneo ndani ya eneo la ukumbi ule lakini napo Benedict hakuonekana. Hawakuwa na jinsi tena, walichokifanya ni kuanza kupiga hatua kumfuata baunsa ambaye alikuwa akiongea na rafiki yake.
“Tunamtafuta Benedict Matimya. Mmemuona maeneo haya?” Martin aliuliza.
“Benedict!”
“Ndio”
“Yule anayetafutwa?”
“Ndio”
“Acheni utani bwana. Mnajua kwamba mnazizungumzia milioni ishirini hapo?”
“Tunalijua hilo. Nilimuona hapa muda mchache uliopita. Alikuwa amevaa kofia ya Malboro yeye rangi nyekundu” Martin aliwaambia.
Maneno aliyoongea Martin yakaonekana kuwashtua, mtu ambaye alikuwa amevaa kofia aina ya Malboro ambayo ilikuwa na rangi nyekundu wala hakuwa mgeni machoni mwao, walimuona kipindi kichache kilichopita. Baunsa alibaki akiwaangalia mara mbili mbili walinzi wale huku akinekana kutokuamini kile ambacho kilikuwa kikizungumziwa.
“Kumbe yule alikuwa Benedict?”
“Ndio”
“Mna uhakika?”
“Ndio”
“Nendeni Blue Diamond hoteli pale Magomeni. Alichukua teksi hapa” Baunsa aliwaambia.
Unamaanisha ile teksi ambayo iliondoka muda mchache uliopita”
“Ndio hiyo hiyo. Yeye ndiye aliyeikodi kumpeleka hotelini” Baunsa aliwaambia.
Martin na wenzake wakaanza kupiga hatua kulifuata gari lao huku kila mmoja akionekana kuzidi kuchanganyikiwa. Tayari Benedict kwao akaonekana kuwa mgumu kupatikana tofauti na jinsi ya walivyokuwa wakidhani mwanzoni. Moody akashikilia usukani kama kawaida yake na safari ya kuelekea katika hoteli ya Blue Diamond kuanza.
“Ni lazima tumkamate” Martin alisema huku akionekana kukasirika.
Benedict hakutaka tena kuendelea kubaki mahali pale, mtu ambaye alikuwa amechunglia juu ya ukuta ule tayari alikwishaanza kumtia wasiwasi. Alichokifanya muda huo ni kusimama na kuanza kuufuata mlango mkuu wa kuingilia ukumbini pale. Macho yake yakapigwa na mshtuko mara baada ya kuliona gari dogo likiwa limesimama pembeni huku vijana watatu wakiongea na mlinzi.
Benedict hakuona uwezekano wa kutoka ndani ya ukumbi ule. Macho yake yakapigwa na mshtuko wa furaha mara baada ya kuiona teksi ya biashara ikiwa katika eneo la ukumbi ule. Kwa haraka haraka akaanza kuisogelea taksi ile, alipoifikia, kijana mmoja akafika mahali hapo huku akiwa ameongozana na baunsa wa ukumbi ule.
“Karibu” Dereva alimwambia Benedict bila kumtambua huku akimfungulia mlango.
“Nipelekee Blue Diamond Hotel”
“Elfu saba”
“Haina tatizo” Benedict alijibu.
Dereva akawasha gari na kumuaga baunsa. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akifahamu kwamba kijana yule ambaye alikodi teksi ile alikuwa ni Benedict ambaye alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba nchini Tanzania. Dereva akaanza kuliondoa gari lile mahali pale.
Mlinzi akafungua geti, gari likatoka. Macho ya Benedict yalikuwa yakiwaangalia vijana watatu ambao bado walikuwa wakiendelea kuongea na mlinzi. Moyo wa Benedict ukamlipuka kwa furaha hasa mara baada ya kujiona ametoka salama katika ukumbi ule. Mara baada ya teksi kufika maeneo ya Kijitonyama, akamtaka dereva asimamishe gari pembeni, akateremka na kwenda katika mashine ya ATM. Akatoa kadi yake, akachukua kiasi chote cha fedha kilichobaki na kurudi garini.
Safari iliendelea. Gari lilichukua dakika arobaini likafika katika eneo la hoteli ya Blue Diamond. Akateremka, akamgawia dereva kiasi cha fedha alichokuwa akidaiwa na moja kwa moja kuanza kuelekea katika sehemu ya mapokezi. Alipojiandikisha, akapewa ufunguona kuanza kwenda katika chumba namba themanini kilichokuwa katika ghorofa ya tatu.
Benedict alitulia kwa dakika hamsini, ghafla akashtukia kitasa cha mlango wa chumba kile kikianza kutekenywa. Kwa haraka akainuka pale kitandani, akaanza kupiga hatua kuufuata mlango ule. Alipoufikia, akachungulia kupitia kitundu kidogo cha mlangoni. Jicho lake likatua katika uso wa kijana ambaye alichungulia katika ukuta uliotenganisha hoteli ya Casanova na ukumbi wa muziki wa Hill Top.
Foleni ndefu ya magari ilikuwepo barabarani. Magari yalikuwa yakitumia muda mwingi kusimama kuliko kutembea. Kila mmoja akaonekana kukasirika kutokana na foleni ile kuwakera kupita kiasi. Kila mmoja aliona ilikuwa ni afadhali kushuka garini na kuanza kutembea kutokana na foleni ile kuwachelewesha kupita kiasi.
Walitumia dakika arobaini hadi kufika maeneo ya Morocco. Foleni bado ilionekana kuwakera. Walikaa katika foleni hiyo ya mataa ya Morocco kwa muda wa dakika saba na ndipo wakaruhusiwa. Moody hakutaka kuendesha gari kwa kasi ndogo tena, akaingiza gia na kuanza kuendesha kwa mwendo wa kasi.
Watu walibaki wakilishanga gari lile ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kiasi ambacho kila mmoja akaona kwamba lilikuwa limeibwa na hivyo lilikuwa likikimbizwa na polisi. Walitumia dakika mbili mpaka kufika katika maeneo ya Magomeni hospitalini, hapo wakakutana na foleni nyingine ambayo iliwaweka hapo kwa muda wa dakika tano.
Waliporuhusiwa, walitumia muda wa dakika mbili tu wakawa wamekwishafika katika eneo la hoteli kubwa ya Blue Diamond ambayo ilikuwa imezungushwa ukuta mkubwa. Walipoingia ndani ya eneo la hoteli hiyo, wakateremka na moja kwa moja kuanza kuelekea mapokezini huku macho yao yakiangalia kila upande.
“Tunahitaji kumuona Benedict” Martin alimwambia dada wa mapokezi.
“Benedict nani?”
“Matimya” Martin alitoa jibu lililoonekana kumshtua dada wa mapokezini.
“Umesema nani? Benedict Matimya?”
“Ndiye huyo huyo”
“Hapana. Sijawahi kumuona uso kwa uso toka nizaliwe zaidi ya kuziona picha zake tu” Dada yule alijibu.
“Kuna mtu yeyote kachukua chumba katika hoteli hii dakika kadhaa zilizopita ambaye alivalia kofia aina ya Malboro iliyokuwa na rangi nyekundu?” Martin aliuliza.
“Ndio”
“Ulimpa chumba?”
“Ndio”
“Namba ngapi?”
“Themanini”
Hawakuwa na sababu ya kuendelea kuchelewa mahali hapo, walichokifanya ni kutoa vitambulisho vyao na kumuonyeshea yule dada ambaye akaonekana kugundua kwamba wale walikuwa polisi waliotoka katika kitengo cha upelelezi, alichokifanya ni kuanza kwenda nao katika chumba hicho kilichokuwa katika ghorofa ya tatu.
Wakapandisha ngazi mpaka kuifikia ghorofa ya tatu ambapo moja kwa moja wakaanza kuziangalia namba zilizokuwa katika milango kadhaa, walipoufikia mlango uliokuwa na namba themanini, Martin akaanza kukitekenya kitasa cha mlango ule ambao ulionekana kufungwa.
“Naomba funguo za akiba za mlango huu” Martin alimwambia yule dada.
“Nimeziacha kaunta. Subiri nikakuletee”
Kwa haraka haraka dada yule, Mariamu akaanza kuelekea kaunta kuzichukua funguo zile huku wapelelezi wakiwa wamebaki mlangoni pale. Mwendo wake ulikuwa wa haraka haraka huku moyoni akijilaumu kwa kutokujua kwamba mtu ambaye alichukua chumba alikuwa Benedict ambaye alikuwa akitafutwa na polisi. Alipofika kaunta, akazichukua funguo zile za akiba na kuanza kurudi ghorofani.
“Hizi hapa” Mariamu alisema huku akimkabidhi funguo zile Martin.
Martin akaingiza ufunguo katika kitasa kile, bahati ilionekana kuwa yake kutokana na kutokuwa na ufunguo wowote kwa ndani. Wakaufungua mlango na kuingia ndani. Chumba kilikuwa kitupu, wakaanza kumtafuta Benedict katika kila kona ndani ya chumba kile lakini wala hakuweza kuonekana.
“Yupo wapi?” Martin aliuliza.
“Hatujui. Chumba kitupu”
“Hadi chooni kutupu?”
“Nd…….” Sabrina alijibu lakini hata kabla hajamalizia jibu lake, wakasikia Mariamu akianza kupiga kelele kutoka chooni. Kwa haraka haraka wakaanza kumfuata.
“Kuna nini?”
“Angalieniiiiii…….”
“Mungu wangu! Twendeni chini” Martin aliwaambia wenzake na kuanza kuelekea chini huku wakiamini kwamba Benedict alikuwa ameshuka chini kwa kutumia bomba kubwa la chooni.
Benedict alitulia kwa muda na kuyapeleka macho yake kila kona ndani ya chumba kile. Hakuona kama kulikuwa na dalili zozote za kuondoka ndani ya chumba kile bila kupitia mlangoni. Kwa haraka haraka akaanza kulifuata dirisha la chumba kile na kufungua kioo, hakukuonekana kuwa na bomba lolote ambalo lingemuwezesha kushukia chini.
Benedict hakutaka kupoteza muda, kwa haraka haraka akaanza kuelekea chooni ambako akaufungua mlango na kisha kulifuata dirisha la choo kile na kuchungulia. Moyo wake ukamlipuka kwa furaha mara baada ya kuliona bomba kubwa likiwa limeelekea chini.
Kwa haraka haraka Benedict akatoka nje ya choo kile kwa kupitia dirishani, akalidandia bomba lile na kuanza kuteremka chini. Moyo wake haukuwa na wasiwasi wowote kwani alijua ni vigumu kuonekana na mtu yeyote kutokana na upande ule kuwa nyuma ya hoteli ile. Kutokana na haraka aliyokuwa nayo wala hakuchukua muda mrefu kufika chini, ni ndani ya dakika mbili tu, akawa amekwishafika chini.
Akaanza kupiga hatua kuelekea mbele ya hoteli ile, lakini hata kabla hajafika, akajibanza pembezoni mwa ukuta na kuanza kuchungulia kule mbele ya hoteli ile. Macho yake yakatua kwa mlinzi ambaye alikuwa makini kuangalia kila upande kitu ambacho kilionekana kumpa wasiwasi mkubwa Benedict. Akayatoa macho yake kutoka kwa mlinzi na kuyapeleka katika ghorofa ya tatu hasa katika dirisha la chumba alichokuwa amepanga.
Macho yake yakatua kwa mtu ambaye alikuwa akichungulia nje kupitia katika dirisha la chumba kile na baada ya sekunde chache, watu watatu wakaongezeka dirishani pale. Wasiwasi ukaongezeka zaidi hasa mara baada ya kuwaona watu wale wakichomoka kwa haraka kutoka pale dirishani.
Benedict akaangaza macho yake huku na kule, macho yake yakatua katika choo kidogo kilichojengwa nyuma ya hoteli ile. Benedict hakutaka kujiuliza, hapo hapo akaanza kupiga hatua kukifuata choo kile. Alipokifikia, akaufungua mlango na kuingia ndani. Macho yake yakaanza kuangalia katika kila kona ndani ya choo kile.
Hakukuwa na sehemu yoyote iliyokuwa wazi zaidi ya dirisha dogo lililokuwa katika upande uliokuwa na nyaya nyingi za umeme. Akapanda kwa kukanyaga bomba la maji chooni mule, akaanza kuliangalia dirisha lile.
“Ni lazima niling’oe” Benedict alijisemea.
Martin, wapelelezi wenzake pamoja na Mariam wakaanza kuteremka ngazi kwa haraka haraka kuelekea chini. Kichwa cha kila mtu katika kipindi hicho kilikuwa kikimfikiria Benedict. Kila mtu alikuwa na uhakika kwamba Benedict alikuwa ameteremkia chini kwa kutumia bomba la choo ambalo lilikuwepo nyuma ya hoteli ile.
Mara baada ya kufika chini, moja kwa moja wakaanza kuangalia katika kila eneo la hoteli ile. Wakaelekea hadi katika eneo lililokuwa na bomba lile kubwa la choo, wakaangalia katika maeneo ya karibu na bomba lile lakini napo hakukuwa na mtu yeyote. Hawakutaka kuendelea kubaki kule nyuma ya hoteli, wakaanza kupiga hatua kumfuata mlinzi huku kila mmoja akionekana kuchanganyikiwa.
“Vipi?” Martin alimuuliza mlinzi.
“Sijamuona hapa”
“Na hakuna mtu aliyetoka?”
“Hakuna kabisa”
“Acha utani”
“Huo ndio ukweli”
Wakazidi kuchanganyikiwa zaidi, Benedict akaonekana kuwazidi ujanja kwa mara nyingine tena. Kila mmoja akaonekana kuchoka, wakabaki kimya huku wakiwa hawajui ni kitu gani ambacho walitakiwa kukifanya katika kipindi kile. Martin ndiye ambaye alionekana kuchanganyikiwa zaidi, alibaki katika hali hiyo kwa sekunde kadhaa, akamsogelea mlinzi.
“Hauna wasiwasi na sehemu yoyote nyuma ya hoteli hii” Martin alimuuliza mlinzi.
Swali lile likaonekana kuwa gumu kujibika, mlinzi akabaki kimya kwa muda huku akionekana kufikiria kitu. Kwa haraka haraka katika hali ambayo ilimshangaza kila mtu, mlinzi akachomoka kutoka mahali hapo huku akikimbia kuelekea nyuma ya hoteli ile. Wapelelezi hawakutaka kubaki mahali pale, nao wakachomoka mahali pale kumfuata mlinzi kule nyuma ya hoteli alipokuwa akielekea.
“Kuna nini?” Moody alimuuliza mlinzi mara baada ya kumfikia.
“Mmeangalia chooni?” Mlinzi aliuliza.
“Chooni! Choo gani?” Martin aliuliza.
“Kile pale” Mlinzi aliwaonyeshea.
Kwa haraka haraka wakaanza kukifuata choo kile. Mara baada ya kuufikia mlango wa choo kile, Moody akashika komeo la mlango wa choo kile na kujaribu kuufungua. Mlango ukaonekana kufungwa, Moody akajaribu zaidi na zaidi lakini mlango haukufunguka kitu ambacho kiliwafanya kuona kuwa Benedict alikuwa ndani ya choo kile.
“Nani hutumia choo hiki?” Martin aliuliza huku akilishika komeo la mlango na kujaribu kuufungua.
“Mimi, mlinzi”
“Unaweza kuturuhusu kuuvunja mlango huu?” Martin alimuuliza mlinzi. Mlinzi akabaki kimya kwa muda huku akiyapitisha macho yake kwa kila mpelelezi ambaye alikuwepo mahali pale.
“Sawa. Uvunjeni”
Martin na Moody hawakutakakupotza muda, hapo hapo wakaanza kuuvunja mlango ule. Kutokana na mlango ule kutokuwa imara, wakafanikiwa kuuvunja. Wakaingia chooni, macho yao yakatua katika dirisha dogo la choo kile. Nyavu ilikuwa chini, Martin akapanda juu ya ndoo iliyokuwa ndani ya choo kile na kuanza kuchungulia kupitia katika kidirisha kile.
“Huyu atakuwa ametuacha kwa mara nyingine tena” Martin aliwaambia wenzake huku akiendela kuchungulia katka kidirisha kile.
“Unaona nini huko?” Moody aliuliza.
“Mitambo kadhaa ya umeme. Nafikiri itakuwa mitambo ya kuendeshea umeme ndani ya hoteli hii” Martin alijibu.
Your Thoughts