A Reject Kayumba 09

Comments ...
banner

A REJECT KAYUMBA 2024.
​NA: Emmanuel Charo.
WhatsApp: +254796273110
​SEHEMU YA 9
​"Niko tayari kufanya lolote, Mheshimiwa Gahag," Abdul alijibu.
​Wakati Abdul akiingia rasmi kwenye mikono ya Gahag, chini ya ardhi kule Kerugoya, Manu alikuwa akikamilisha msimbo wake wa udukuzi huku akiitazama picha ya Nuru kwenye skrini. Vita kati ya rafiki hawa wawili wa zamani haikuwa tena ya kugombania msichana mmoja wa Kiyemeni; ilikuwa imekuwa vita ya kudhibiti nchi. Na Manu alijua, njia pekee ya kumwangusha Romeo, ilikuwa ni kumtafuta Nuru na kumwambia ukweli wote aliouweka kwenye kompyuta yake.
​Endelea...
​Siku ziligeuka kuwa wiki, na wiki zikayeyuka na kuwa miezi. Kule jijini Mombasa, hali ilikuwa ya majonzi mazito. Habari za 'kifo' cha Abdul kwenye ule mlipuko wa gari zilikuwa zimeisambaratisha familia yake na kumuacha Almas akiwa nusu mfu. Kwa kuwa mwili uliokutwa kwenye lami ulikuwa umeteketea kiasi cha kutotambulika, serikali ilitoa majivu na mabaki machache kwa familia ili wayahifadhi. Hakuna aliyejua kuwa mwili ule haukuwa wa Abdul, bali ulikuwa wa mmoja wa wale makomandoo wa Idara ya Usalama aliyeuawa wakati Abdul akitoroka usiku ule, kabla ya Abdul mwenyewe kukamatwa na kupelekwa Kambi ya Romeo.
​Mvua nyepesi ilikuwa ikinyesha kwenye makaburi ya Waislamu eneo la Kikowani. Almas alikuwa amepiga magoti mbele ya kaburi dogo lililokuwa na kibao chenye jina la Abdul Razak. Alikuwa amevalia baibui jeusi, uso wake ukiwa umepauka kwa kilio cha siku nyingi. Macho yake makubwa ya Kiyemeni, ambayo zamani yalikuwa yakimulika kwa furaha na aibu, sasa yalikuwa yamejaa kiza na uchungu usioelezeka.
​"Kwa nini uliniacha, Abdul?" Almas alinong'ona huku akishika mchanga mbichi wa kaburi lile. "Uliniahidi maisha mazuri... uliniahidi ndoa. Nani alikufanyia unyama huu?"
​Ghafla, sauti ya nyayo zikikanyaga majani makavu ilisikika nyuma yake. Mwamvuli mweusi mkubwa ulifunguliwa na kufunika mvua iliyokuwa ikimdondokea Almas. Almas aligeuka taratibu. Alisimama mbele yake mwanamke wa makamo, aliyevalia koti refu la ngozi na miwani myeusi. Hakuwa mwingine bali Mama Yusra, mwanamke aliyesuka mtego uliosababisha Abdul aingie kwenye mikono ya serikali, ingawa Almas hakujua hilo.
​"Machozi hayarudishi waliolala, binti," Mama Yusra alisema kwa sauti ya kishujaa, sauti iliyokosa chembe ya huruma.
​"Wewe ni nani? Na unataka nini hapa?" Almas aliuliza, akisimama na kujifuta machozi.
​"Mimi ni mtu anayejua ukweli," Yusra alijibu, akiinua miwani yake kidogo kumtazama Almas. "Mpenzi wako hakufa kwa ajali. Aliuawa. Alijiingiza kwenye mambo makubwa ya kiusalama ambayo yalimzidi umri. Aliuawa na mfumo uliokosa huruma."
​Maneno yale yalichoma kama mshale kwenye moyo wa Almas. Kifua chake kilianza kuhema kwa kasi. "Nani? Nani aliyemuua Abdul wangu?"
​"Watu wenye nguvu. Watu ambao huwezi kuwapiga ukiwa unalia kwenye makaburi," Yusra alisogea hatua moja mbele, sauti yake ikibadilika kuwa ya ushawishi mzito. "Nimekutazama kwa muda mrefu, Almas. Wewe ni chotara wa Kiyemeni na Kimijikenda. Ndani ya damu yako kuna asili ya ukakamavu wa kivita na uvumilivu. Unataka kulia maisha yako yote, au unataka nguvu ya kulipiza kisasi kwa wale waliomchukua Abdul wako?"
​Almas alimtazama yule mwanamke kwa muda mrefu. Ule moyo wake wa upole uliokuwa ukimpenda Manu na baadaye kumpenda Abdul, ulikuwa umekufa siku aliposikia habari za msiba ule. Ndani ya nafsi yake, alihisi shimo kubwa ambalo lingeweza kufunikwa tu na damu ya wale waliomuumiza.
​"Nipe hiyo nguvu," Almas alijibu kwa sauti ya chini lakini iliyojaa msisitizo. "Niko tayari kufanya chochote."
​Mama Yusra alitabasamu kwa uovu. "Twende zetu."
​Siku hiyo, Almas alipotea rasmi katika mitaa ya Mombasa. Hakuna aliyejua alikokwenda, hata familia yake. Alipelekwa kwenye kambi ya siri ya ujasusi inayomilikiwa na mrengo wa Mama Yusra, mradi ulioitwa Project Wendo. Kambi hii ilikuwa Nairobi, mbali kabisa na macho ya watu.
​Huko, maisha ya Almas yalibadilishwa kwa asilimia mia moja. Alivuliwa baibui lake na kuvalishwa sare za kijeshi. Nywele zake ndefu alizozipenda sana zikakatwa na kubaki fupi. Alipitishwa kwenye tanuru la mateso ya kimwili na kisaikolojia. Alifundishwa jinsi ya kutumia silaha za kila aina, kuanzia visu vya kimyakimya hadi bunduki nzito za masafa marefu (Sniper rifles). Alifundishwa jinsi ya kupigana kwa mikono mitupu, kuvunja mbavu na shingo za maadui bila kutumia nguvu nyingi.
​Lakini funzo kubwa zaidi alilopewa, lilikuwa ni kuua hisia zake.
​Miezi nane baadaye, kwenye chumba cha giza cha mafunzo, Mama Yusra alikuwa amesimama akimtazama binti mmoja akipigana na wanaume watatu waliokuwa na miili mikubwa. Binti huyo alikuwa mwepesi kama paka, akitumia miguu yake kuruka na kuangusha mateke mazito yaliyowavunja taya wale wanaume ndani ya sekunde chache. Alipomaliza, alisimama wima, akihema kidogo, macho yake yakiwa hayana chembe ya huruma wala hofu.
​Yule binti alikuwa ni Almas. Lakini hakuwa tena yule binti mwenye aibu wa Mombasa. Uso wake ulikuwa mkavu, mwili wake ukiwa umekakamaa kimazoezi, na macho yake yalikuwa ni ya muuaji.
​Mama Yusra alipiga makofi taratibu. "Safi sana. Umefaulu mtihani wako wa mwisho. Umegeuka kuwa silaha kamili. Lakini silaha nzuri haiitwi kwa jina la asili. Kuanzia leo, wewe sio Almas. Jina hilo limezikwa pale Kikowani Mombasa. Wewe utajulikana kwa msimbo wako mpya."
​Almas aligeuka na kumtazama Mama Yusra. Sauti yake ilipotoka, ilikuwa ya ubaridi usio wa kawaida. "Msimbo gani?"
​"Wewe ni Malaika wa kifo. Wewe ni Angel," Yusra alijibu, akimkabidhi faili jekundu. "Hii ni misheni yako ya kwanza, Angel. Na baada ya hapa, nitakutuma nchini Urusi, ambako utajificha na kuwa jasusi wetu mkuu chini ya ulinzi wa genge la Henessa. Utasubiri maelekezo yangu ya kutikisa mifumo ya dunia."
​Almas—ambaye sasa alikuwa ni Angel—alichukua lile faili bila kutabasamu. Hakujua kuwa mpenzi wake Abdul alikuwa hai na anafanya kazi kama muuaji wa serikali chini ya Gahag. Hakujua pia kuwa Manu, kijana aliyewahi kumweleza hisia zake za dhati, sasa alikuwa ni mdukuzi hatari anayeitwa Reject Kayumba. Hatima ilikuwa imeanza kuwasuka hawa vijana watatu kwenye kamba moja hatari ambayo ingekuja kuleta maafa makubwa pindi watakapokutana tena.
... views
Advertisement

Comments ()