USA Aingia Mchezoni

0

USA Aingia Mchezoni: Ushirikiano Mpya na Israel Dhidi ya Iran


Katika kile kinachoonekana kama ukurasa mpya wa mivutano ya Mashariki ya Kati, Marekani imejiunga rasmi na Israel katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran. Hatua hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia leo imezua taharuki kubwa katika duru za kimataifa huku dunia ikitazama kwa wasiwasi hatma ya usalama wa kikanda.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi, mashambulizi hayo yamelenga maeneo muhimu ya nyuklia nchini Iran kama vile Fordow, Natanz na Esfahan. Vikosi vya anga vya Marekani viliripotiwa kushambulia kwa usahihi mkubwa, kwa kushirikiana na majeshi ya Israel, katika kile walichokiita “jibu la lazima dhidi ya tishio la Iran kwa amani ya kimataifa.”

Mashambulizi haya yanakuja baada ya kipindi kirefu cha mvutano kati ya Israel na Iran, ambao sasa umechukua mkondo mpya kwa ushirikiano wa wazi kutoka kwa Marekani. Viongozi wa Marekani wamesema hatua hiyo inalenga “kupunguza uwezo wa Iran kutengeneza silaha za nyuklia na kuimarisha ulinzi wa washirika wa Marekani katika eneo hilo.”

Baada ya mashambulizi hayo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alitoa hotuba ya moja kwa moja, akimsifu Rais wa Marekani kwa hatua aliyochukua. Katika hotuba hiyo, alisema:

 “Rais Trump na mimi huwa tunasema: ‘Amani hupatikana kwa njia ya nguvu.’ Kwanza huja nguvu, ndipo amani hufuata. Usiku huu, Donald Trump na Marekani wameonesha nguvu ya kweli na ya haki. Hongera Rais Trump. Uamuzi wako wa kishujaa wa kulenga vinu vya nyuklia vya Iran kwa kutumia nguvu kubwa na ya haki ya Marekani utabadilisha historia.”

Na akahitimisha kwa maneno haya

“Mungu ibariki Marekani. Mungu ibariki Israeli. Mungu aibariki miungano yetu isiyotikisika na imani yetu isiyovunjika.”

Kwa upande wake, Iran imelaani mashambulizi hayo ikiyaita uvamizi wa wazi wa kinyume na sheria za kimataifa. Viongozi wake wameapa kulipiza kisasi, huku taarifa kutoka Tehran zikieleza kuwa majeshi ya Iran sasa yamewekwa katika hali ya tahadhari ya juu.

Ripoti pia zinaonyesha kuwa baadhi ya makombora ya Iran yalirushwa kuelekea Israel kama sehemu ya mashambulizi ya kulipiza, ingawa idadi kamili ya madhara bado haijathibitishwa.


Jumuiya ya Kimataifa Yatoa Kauli

Mataifa kadhaa yameeleza wasiwasi mkubwa juu ya hali hii. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, China, Urusi na mataifa mengine wameitaka Israel, Iran na Marekani kurejea kwenye meza ya mazungumzo na kujizuia dhidi ya kuchochea mzozo mkubwa zaidi.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaonya kuwa hatua hii ya Marekani inaweza kuchochea vita vya eneo au hata kuzua machafuko ya kimataifa, hasa ikizingatiwa umuhimu wa eneo la Ghuba kwa soko la mafuta duniani.

Kwa kuingia kwa Marekani mzozoni, mwelekeo wa mzozo wa Mashariki ya Kati umechukua sura mpya. Kwa sasa, dunia inatazama kwa tahadhari, ikiomba busara, diplomasia, na maamuzi ya hekima yazidi silaha. Lakini kama alivyosema Netanyahu, “Kwanza huja nguvu, ndipo amani hufuata” – je, huu ndio mwanzo wa amani au moto mpya wa vita?

Jaba Planet itaendelea kukujuza kila hatua ya mzozo huu kwa undani na kwa wakati.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.