GAZA: HISTORIA YA DAMU

GAZA: HISTORIA YA DAMU

Mgogoro wa Gaza umeendelea kuwa kitovu cha mjadala duniani, ukivuta hisia na mijadala mikali kuhusu haki za binadamu, usalama wa kitaifa na mustakabali wa amani ya Mashariki ya Kati. Huu si mgogoro uliyoibuka ghafla, bali ni simulizi ya karne nzima iliyochanganyika na historia ya ukoloni, vita na ndoto za taifa ambazo hadi leo hazijawahi kutimia.

Mwanzo wa Mgogoro: Enzi za Kikoloni

Mwanzoni mwa karne ya 20, Palestina ilikuwa chini ya Dola ya Kiosmani. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Uingereza iliwekwa kusimamia eneo hilo kupitia British Mandate. Katika kipindi hiki, mnamo 1917, Uingereza ilitoa Balfour Declaration, ikiahidi kuunga mkono kuanzishwa kwa "makao ya kitaifa ya Wayahudi" Palestina.

Wakati huohuo, Waarabu waliokuwa wakikaa Palestina walikuwa na matarajio ya kujitawala. Hivyo basi, mvutano ukawa umeanza kabla hata ya taifa la Israel kuundwa.

Kuundwa kwa Israel na Nakba ya Palestina

Mwaka 1947, Umoja wa Mataifa ulipitisha mpango wa kugawa Palestina kati ya Wayahudi na Waarabu. Wayahudi walikubali, lakini Waarabu walikataa wakihisi mpango huo ulikuwa wa upendeleo.

Mnamo Mei 1948, Wayahudi wakatangaza taifa lao jipya la Israel. Hatua hii ikaleta Vita vya Kwanza vya Kiarabu na Israel ambapo mataifa jirani ya Kiarabu yaliingia vitani. Katika mzozo huo, mamia ya maelfu ya Wapalestina walikimbia makazi yao au walifukuzwa, tukio linalojulikana kama Nakba (yaani "janga"). Wengi wa wakimbizi hao walihamia Gaza na Ukingo wa Magharibi, wakibeba hadithi za maumivu na mateso ambayo yameendelea hadi vizazi vya sasa.

Vita vya 1967 na Ukaliaji wa Israel

Mwaka 1967, katika Vita vya Siku Sita, Israel iliishinda Misri, Jordan na Syria. Matokeo yake, Israel ilichukua maeneo makubwa ikiwemo Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Jerusalem Mashariki. Hapo ndipo Palestina ikaanza rasmi kuishi chini ya ukaliaji wa Israel.

Kutokana na hatua hiyo, hamasa ya mapambano ya ukombozi ilikua, na makundi kama Palestine Liberation Organization (PLO) yalianzishwa kupigania taifa huru la Palestina.

Juhudi za Amani Zilizoshindikana

Mwaka 1993, kupitia Mkataba wa Oslo, PLO na Israel walikubaliana juu ya kuunda Mamlaka ya Palestina (PA), ambayo ingesimamia baadhi ya maeneo ya Palestina. Wapalestina walitarajia hili lingekuwa mwanzo wa uhuru wao, lakini makazi ya walowezi wa Kiyahudi (settlements) yaliendelea kujengwa katika ardhi ya Palestina, jambo lililovunja imani ya wengi.

Kuingia kwa Hamas na Mgawanyiko wa Kisiasa

Mwaka 2006, chama cha Hamas kilishinda uchaguzi wa Palestina. Mwaka uliofuata, kikachukua udhibiti wa Gaza kwa nguvu baada ya mivutano na Fatah. Tangu hapo, Gaza imekuwa ikitawaliwa na Hamas, huku Ukingo wa Magharibi ukibaki chini ya Mamlaka ya Palestina inayoongozwa na Fatah.

Matokeo yake, Israel na Misri wakaweka vikwazo vikali (blockade) vya ardhini, baharini na angani. Gaza ikawa eneo lenye msongamano mkubwa wa watu, ambapo karibu kila nyanja ya maisha – kuanzia afya, elimu, hadi ajira – ilikumbwa na mateso makali.

Migogoro ya Mara kwa Mara

Kuanzia mwaka 2008, Israel na Hamas wameingia vitani mara kadhaa (2008, 2012, 2014, 2021). Kila vita ilileta maafa makubwa Gaza, ikiharibu miundombinu, kuua maelfu ya raia na kusababisha dunia kushuhudia taswira za kusikitisha za wakimbizi na watoto waliokatwa tamaa.


Israel mara zote imesema inalinda usalama wake kutokana na makombora ya Hamas, huku Hamas ikisisitiza inajibu dhidi ya ukaliaji na kunyimwa taifa lao.

Shambulio la Oktoba 7, 2023

Hali ilifikia kilele kipya mnamo 7 Oktoba 2023, wakati Hamas ilipoanzisha shambulio kubwa ndani ya Israel. Mamia ya wanamgambo walivamia maeneo ya mipaka, kuua zaidi ya Waisraeli 1,000 na kuwateka wengine.

Israel ikajibu kwa operesheni kubwa ya kijeshi Gaza, ikitangaza lengo la "kuangamiza Hamas kabisa." Mashambulizi ya anga, mizinga na mashambulizi ya ardhini yakaacha Gaza katika kifusi, na raia ndiyo wakawa wahanga wakuu.

Mgogoro wa Kibinadamu

Kuanzia mwishoni mwa 2023 hadi sasa (2025), Gaza imekuwa katika hali mbaya zaidi ya kibinadamu. Hospitali zimeharibiwa, dawa zimekwisha, maji safi na umeme ni nadra, na maelfu ya familia zimepoteza makazi.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameeleza hali hiyo kama janga la kibinadamu lisilokuwa na kifani, huku ripoti zikionyesha kuwa watoto ndiyo waathiriwa wakuu

Dunia Yagawanyika

Mgogoro huu umeigawa dunia:

Nchi za Magharibi nyingi zimekuwa zikiiunga mkono Israel kwa hoja ya usalama wake.

Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya mataifa ya Kusini mwa dunia yamekuwa yakitetea haki za Wapalestina.

Mashirika ya kimataifa na wanaharakati wamesisitiza suluhisho la kudumu kupitia kuundwa kwa taifa huru la Palestina kando na Israel.

Mustakabali Uliojaa Mashaka

Licha ya mashinikizo ya kimataifa ya kuanzisha mazungumzo ya amani na kutoa misaada, vita bado vinaendelea. Gaza imekuwa mfano wa mateso yasiyoisha, na swali kuu linasalia: Je, dunia itapata ujasiri wa kuleta suluhisho la kweli kwa watu wa Palestina na Israel?

Kwa sasa, Gaza inasalia kuwa kioo cha dunia kinachoonesha gharama ya kutokuwepo kwa amani na mshikikiano.


Comments