Taifa la Mungu; Vitendo vya Kishetani
Ni jambo la kusikitisha na la kushtua kwamba Israel, taifa linalojulikana kwa jina la nchi teule la Mungu, limeendelea kuyatumbukiza macho ya dunia katika maovu ya kutisha. Kwa jina la kujilinda, taifa hili limegeuza ardhi ya Palestina, hasa Gaza, kuwa kaburi la watoto, wanawake na wazee wasiokuwa na hatia. Mabomu yanaporomoshwa bila huruma, hospitali zikibomolewa, na chakula pamoja na dawa zikikatwa, dunia inashuhudia dhihirisho la vitendo visivyo na utu ambavyo haviwezi kuelezwa kwa neno jingine ila kishetani.
Lakini cha kusikitisha zaidi ni unyonge wa jumuiya ya kimataifa. Umoja wa Mataifa, chombo kilichoundwa kwa dhima ya kuilinda dunia dhidi ya ukatili wa namna hii, kimeendelea kushindwa kwa aibu. Vikao visivyo na matokeo, maazimio yasiyo na nguvu, na kauli zisizotekelezwa vimegeuza UN kuwa kivuli cha kile kilichokusudiwa kuwa. Ni ishara ya ulimwengu uliolemewa na hofu, usio na ujasiri wa kukemea kwa nguvu kile ambacho ni dhahiri kuwa ni uhalifu wa kibinadamu.
Na kisha kuna Marekani – taifa linalojiita nguzo ya demokrasia na haki za binadamu. Kwa unafiki wa hali ya juu, limekuwa mstari wa mbele kusukuma ajenda zisizo na mashiko kama haki za ushoga na mijadala ya kipuuzi, huku likiwafumbia macho mamilioni wanaoangamizwa kwa mabomu yanayonunuliwa na kodi ya wananchi wake. Marekani inabeba bendera ya kulinda haki, lakini mkononi mwake imeshikilia upanga wa kulinda unyama wa Israel. Ni kichekesho cha kikatili kinachodhihirisha upendeleo na ubaguzi wa waziwazi dhidi ya mataifa dhaifu.
Leo dunia inapaswa kusema wazi: inatosha. Hakuna jina la utakatifu linaloweza kuhalalisha mauaji ya halaiki. Hakuna historia ya kiimani inayoweza kufunika damu ya watoto isiyo na hatia. Taifa linalodai kuwa la Mungu linapotekeleza vitendo vya kishetani, ni wajibu wa binadamu wote kukemea kwa sauti kubwa, bila hofu na bila unafiki. Amani ya kweli haitapatikana kwa mazungumzo ya kinafiki, bali kwa kusimama imara dhidi ya uhalifu, bila kujali ni nani anayefanya.