Kenya ilianza kama cheche ndogo lakini ikaonyesha dunia nzima kwamba vijana wa kizazi cha Gen Z hawawezi tena kufungwa midomo. Mnakumbuka zile maandamano za kupinga gharama ya juu ya maisha mwaka wa 2023? Ilikuwa kama movie. Vijana walijipanga bila uoga, wakajaza mitaa Nairobi, Kisumu, Mombasa na miji mingine. Mitandao ya kijamii ikawa silaha yao kubwa; memes zikazaliwa, hashtags zikavuma, na kila video ya polisi ikitembea mitaani ilifika TikTok, Instagram na X ndani ya dakika chache.
Kwa mara ya kwanza, serikali iliona wazi kwamba kizazi kipya kina nguvu zaidi kuliko risasi au mabomu ya machozi. Na dunia ikashuhudia: vijana wa Kenya hawataki tena kuishi kwa ahadi tupu, hawataki kulipia gharama kubwa ya maisha huku wakikosa kazi. Walitaka uwajibikaji, na sauti yao ilisikika.
Lakini Kenya haikubaki peke yake. Hii movement ya vijana ikawa kama moto wa nyika. Nigeria waliendeleza presha kupitia #EndSARS; wakisema basi tena na ukatili wa polisi. DRC vijana wakaingia barabarani kupinga uonevu wa kisiasa na mizozo isiyoisha. Afrika Kusini, wanafunzi na vijana walidai kazi na elimu bora, wakisema maisha ya mateso si future yao. Ulikuwa kama Gen Z wote duniani walikuwa wamekubaliana kimya kimya: “enough is enough.”
Sasa basi, story ikafika mbali zaidi, Nepal. Serikali yao iliamua kufunga mitandao ya kijamii Facebook, Instagram, YouTube, WhatsApp, X, wakifikiri vijana wangenyamaza. Lakini walijipiga bao. Vijana wa Nepal waliona hii sio tu kuhusu apps, bali jaribio la kukandamiza sauti ya kizazi kizima. Ndipo wakajimwaga mitaani kwa nguvu ambazo hazikuwahi kuonekana.
Maandamano yakaanza peaceful lakini yakageuka kuwa makali. Majengo ya serikali, ofisi za media na mali zinazohusishwa na wanasiasa zikachomewa moto. Huu ulikuwa ujumbe wa moja kwa moja: “tumekasirika, tumeshachoka.” Polisi wakajibu kwa nguvu mabomu ya machozi, maji ya kuwasha, hadi risasi za moto. Watu walijeruhiwa, wengine wakapoteza maisha, lakini Gen Z haikurudi nyuma.
Shinikizo lilipozidi, serikali ya Nepal ikalazimika kubadilisha msimamo. Marufuku ya mitandao ikaondolewa, baadhi ya mawaziri wakajiuzulu, na wengine walihama miji wakihofia hasira ya wananchi. Ilikuwa kama system yote imetikiswa. Na dunia ikapata fundisho lingine: youth power sio theory, ni reality.
Kwa sisi huku Kenya na Afrika, hii ni ishara kubwa. Vijana ndio wengi zaidi katika bara hili, na changamoto zinazowakumba ni zile zile ukosefu wa ajira, gharama kubwa ya maisha, ufisadi na wanasiasa wanaotaka kushikilia madaraka milele. Lakini Gen Z imeonyesha kuwa hawako tayari kukaa kimya. Wameonyesha kuwa kutoka barabara hadi kwenye mitandao, kutoka memes hadi maandamano, sauti ya vijana inaweza kubadilisha historia.
Gen Z sio “keyboard warriors” kama wengi walivyokuwa wanadhani. Ni kizazi kinachojua kupiga kelele, kupanga, na kusimama kidete. Ni kizazi kinachochoka kuona wazazi wao wakiteseka huku wanasiasa wachache wakila maisha. Ni kizazi kinachojua kuwa future ni yao, na hawatakubali kuibiwa tena.
Kutoka Nairobi hadi Kathmandu, hii ni story moja: kizazi kipya hakina hofu, hakina uvumilivu wa ahadi tupu, na kiko tayari kupigania kesho iliyo bora. Na kama historia imetuonyesha, hakuna kitu hatari zaidi kwa system yenye ufisadi kuliko vijana walioungana.