Acetamin 220 (08)



ACETAMIN-220...(08)
MTUNZI:BARAKA GEOFREY
0652089642

TAHADHARI:Majina na matukio yote kwenye simulizi hii ni ya kutungwa tu kwa ajili ya kufikisha ujumbe.

ILIPOISHIA..........
"Hivi mkuu siku zote aliwaza nini kutuletea katoto katuongoze kwenye oparesheni muhimu kama hii?" Alikuwa ni Faheed akimuuliza mwenzake mmoja
"Hata sijui, sisi sote tuna uzoefu wa kutosha wa mambo haya kwanini basi asiteue mmoja wetu mpaka afuate hichi kitoto ambacho bado kinanuka maziwa?" mwenzake na yeye aliuliza kwa mshangao, kiuhalisia hakuna aliyejua maana ya jambo hilo isipokuwa bwana Abd al-Uzza mwenyewe
Kila mmoja aliingia kwenye gari yake na kuondoka kwenye jumba hilo ambalo lilikuwa ni makazi ya Aaron na ofisi yake pia aliyopewa na bwana Abd kwa oparesheni hiyo maalum
ENDELEA............
Siku chache zilizofuata kikao kingine kati ya waanzilishi wa kundi la maharib alhuriya kilichukua nafasi na hapo mikakati mizito juu ya kujiimarisha katika ukanda wa Afrika Mashariki ilipangwa Rashid alipewa jukumu lile lile la kuwa msimamizi mkuu Afrika Mashariki na Faheed aliwekwa kuwa msaidizi wa karibu wa Aaron
Baada ya kikao utekelezwaji ulikuwa ni wa kasi sana na umakini mkubwa kwani Aaron hakutaka mchezo kabisa, ndani ya miezi sita tayari aliua watu kumi kwa mikono yake mwenyewe, ambao walifanya uzembe au kujaribu kuleta usaliti...kila mtu alimuogopa Aaron

Ndani ya miaka miwili mafanikio makubwa yalionekana; nchini Kenya kambi ilizidi kuwa kubwa na walifanikiwa kujiingiza katika sekta zote muhimu nchini humo kama uwanja wa ndege, ulinzi na usalama, nishati na madini na vigogo wengi walikuwa upande wao kwani pesa iliyotolewa na bwana Abd ilifanya kazi nzuri ya kuwahadaa watu hao ambao matumbo yao yalikuwa na njaa na dhiki kali wakiweka uzalendo na utu wa wananchi pembeni
Pia walifanikiwa kuanzisha misingi yao nchini Tanzania kwa kuwahadaa baadhi ya viongozi wa juu serikalini na kuanzisha kambi ndogo pembezoni mwa mlima Meru Arusha, nchini Uganda pia kambi ya Mujarib alhuriya ilianzishwa ndani ya msitu wa Mabira...

Aaron alikuwa ofisini kwake akiipitia ripoti anayopokea kila mwezi kutoka kwa Rashid mara simu mezani kwake ikaanza kuita kwa fujo...alinyanyua mkonga wa simu na kuiweka sikioni
"Natumaini u mzima kijana wangu" sauti ya bwana Abd al-Uzza ilisikika kwa utulivu upande wa pili hakumpa nafasi ya kujibu aliendelea kuongea
"Nikupongeze kwa kazi nzuri unayoifanya sikutegemea kuwa ungepiga hatua kubwa kiasi hicho kwa mda mfupi
"Asante mkuu" Aaron alijibu
"Sasa kesho saa mbili na dakika 13 usiku tukutane Vivienda hotel Villas granada kuna kikao cha msingi sana"
"Sawa mkuu"

                     **************
VIVIENDA HOTEL VILLAS GRANADA (SAA 2 NA ROBO USIKU)
Aaron alikuwa ameketi kwenye mojawapo ya viti katika ukumbi mdogo wa mikutano kwenye hoteli hiyo ya nyota tano, ndani ya ukumbi huo alikuwepo bwana Abd al-Uzza na wenzake watatu hivyo jumla chumba hicho kilikuwa na watu watano

"Ndugu zangu huyu ndiye kijana wetu Ayman al-Zawahiri anayesimamia oparesheni yetu kule Afrika Mashariki" alianza kuongea bwana Abd al-Uzza, na mshangao wa wazi ulionekana kwa wenzake kwani hawakutegemea kwamba kijana mdogo kama huyo anaweza kuimudu vizuri kazi hiyo
"Najua mnamwona ni kijana mdogo ila sote hapa tunajua kinachoendelea kule Afrika Mashariki na hii yote ni kazi ya huyu kijana wetu" bwana Abd aliongea mwa msisitizo na hapo wenzake wakatikisa vichwa kuonyesha kuridhika

"Ayman atatupa ripoti fupi na kisha tutamweleza tulichomuitia hapa" bwana Abd alisema na kisha kutulia kumwacha Aaron atoe maelezo yake, kwa mda mfupi Aaron alitoa ripoti fupi na kumaliza
"Naona kazi kubwa imefanyika nikupongeze kijana" mzee mmoja wa kiarabu mwenye ndevu nyingi aliongea na kisha kuendelea

"Tumekuita hapa kukupa maelekezo muhimu.....kusudi kubwa la kuanzisha kundi ambalo lipo chini yetu kule Afrika Mashariki ni kushika serikali zote za kule ambazo kwa sasa zimeshikiliwa na vibaraka wa mataifa dhalimu, katika tafiti zilizofanyika huko ni rahisi kuingiza watu wetu kwenye nchi zote kidemokrasia kasoro nchi ya Tanzania ambayo ni ngumu sana kuingilika, hivyo njia rahisi ya kuishika nchi hiyo ni kupitia mapinduzi ya kijeshi" aliweka kituo mzee huyo

"Kwahiyo wewe na wenzako mpange kila aina ya mikakati ya kutimiza kazi hii, kisha ndugu Abd al-Uzza atakufahamisha kwa kina watu ambao tumewaandaa kushika nyadhifa ya juu kabisa kwenye kila nchi....niwatakie kazi njema" alihitimisha mzee huyo na wenzake kutikisa vichwa ishara ya kukubaliana naye.... kikao hicho kiliendelea kwa saa moja na kiliisha saa tatu na nusu usiku kila mmoja aliondoka kuelekea anakokujua

                     ****************
CHUO KIKUU CHA HAVARD MAREKANI JANUARY,2011
Austin Meyer alikuwa ametoka kwenye mtihani wake, kichwa kilikuwa kimechoka na alirudi chumbani kwake kupumzika, alipoingia chumbani alitupa begi lake lenye laptop kwa hasira kitandani kichwa kilikuwa kizito kweli kweli
'Dah bora nimalizie mwaka wa mwisho' aliwaza kichwani na kisha kutabasamu akivuta picha namna atakavyotunukiwa kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya ini miezi mitano ijayo aliwaza pia namna atakavyoisaidia nchi yake iliyokosa wataalam kama yeye, usingizi ulikuwa umeanza kumchukua taratibu na mlio wa simu yake ulimshtua alikunja sura kwa hasira ya kukatishiwa usingizi wake na aliichukua simu yake akimuonea huruma mtu aliyempigia kwa shombo atakazojibiwa, Olivia lilisomeka jina kwenye kioo chake na hapo alijikuta akitabasamu na hasira zake zikiyeyuka ghafla kama theluji iliyosogezwa kwenye moto mkali, aliivuta simu yake na kuipokea kivivu
"Hello baby" sauti nyororo ya kipenzi chake ilisikika
"Hello kipenzi nimekumiss" alijibu kiuchovu Austin
"Mh mbona kama umechoka sana mpenzi wangu" Olivia aliongea kwa sauti ya kubembeleza
"Nimetoka mwenye mtihani"
"Ooh sawa nitakupigia baadae basi pumzika sasa hivi pumzika mme wangu"
"Asante love you" 
"Love you too dear"
Austin hakukaukiwa na tabasamu kila alipoongea na Olivia barafu wa moyo wake, kausingizi kalianza kumpitia kwa mbali na mara simu yake iliita tena, Austin alijikuta akitoa tusi zito la nguoni kwa mpigaji kwani alimharibia starehe yake aliamua kuiacha tu mpaka ilipokatika, alifyonza kwa hasira na kuanza kuutafuta usingizi tena kwa mara nyingine simu ilianza kuita kwa hasira aliichukua amwone ni nani anayemsumbua, Sister Magreth jina lilionekana kwenye simu,
Alihisi amepigwa na ubaridi ghafla na kuganda kwa sekunde chache hakuamini kuwa amemtukana mmama huyo aliyemlea toka akiwa mtoto mdogo na aliyemheshimu sana japokuwa hakusikia tusi alilomtukana ila alijisikia hatia sana, kwa adabu zote aliipokea simu
"Tumsifu Yesu Kristo" sauti ya unyenyekevu ya sister Magreth ilisikika
"Milele amina" alijibu Austin kwa unyenyekevu kama sio yeye aliyetukana dakika chache zilizopita
"Pole na masomo mwanangu"
"Asante mama"
"Unaendeleaje?"
"Vizuri tu sijui huko mnaendeleaje"
"Sisi pia tunamshukuru Mungu tunaendelea vizuri sasa nisipoteze mda wako mwingi mwanangu..... siku nyingi ulitamani ukutane na mfadhili wako lakini alibanwa na majukumu na safari za mara kwa mara asubuhi ya leo alinipigia ameniambia kuwa yupo huko Marekani na kesho ana safari ya kuelekea Italia mwa hiyo anataka akutane na wewe, usiku huu atakuwa maeneo ya hapo chuo hivyo ameniambia umtafute kwani namba yako ilikuwa haipatikani"
"Nilkuwa kwenye mtihani mama ndiyo maana sikupatikana...ila nimefurahi sana kwamba leo nitakutana naye"
"Sawa basi jiandae umsalimie sana"
"Asante mama" alijibu Austin na simu ilikatika

Austin alijikuta hapati usingizi tena kwa siku nyingi alitamani sana kukutana na mfadhili wake aliyemsomesha kuanzia kidato cha tano mpaka hapo alipo ila alikuwa ni mtu wa safari nyingi hivyo alimuona mara chache tu alipowasiliana naye kwa 'video call' hamu yake ilikuwa kubwa sana mpaka akajikuta kitanda hakilaliki tena na akianza kuzunguka zunguka humo chumbani akimshukuru Mungu kwa mtu mwenye roho nzuri kama huyo
Ngo ngo ngo!
Mlango wa chumba chake uligongwa, safari hii hakukasirika kwani usingizi ulishapaa mda mrefu hivyo alienda kuufungua na kumwona rafiki yake mwenye asili ya Israel aliyeitwa Ilan
"Ooh Dr. Ilan" alimkaribisha kwa bashasha
"Asante Dr Austin" alimjibu na kisha wote wakacheka kwani toka wanajuana mwaka wa kwanza hapo chuoni walianza kuitana 'doctor'
"Nikajua upo na mtoto humu chumbani maana sio kwa namna ulivyochelewa kufungua" Ilan alianza utani
"Aah wapi kaka si unajua sina hayo mambo" alijibu Austin
"Ah wapi wewe mwaka juzi si yule mchumba wako Olivia alikuja kukutembelea hapa haki ya Mungu yule mtoto ni hatari"
"Hebu acha basi" Austin alimjibu kwa namna ya sitaki nataka kwani alipenda mchumba wake asifiwe
"Hahaha bichwa linavimba mwenyewe, ila nakwambia kaka lazima nioe Tanzania"
"Karibu uchunwe mpaka mifupa aisee" alijibu Austin na wote walicheka

"Sasa Austin kuna jambo la msingi limenileta wewe ukiwa kama ndugu yangu wa karibu" alizungumza Ilan
"Eheee niambie" alizungumza Austin kwa hamu ya kujua
"Sikia ndugu yangu kuna dili la hela nyingi limepatikana ni hela nyingi sana kaka ambazo zitatuchukua hata tukifanya kazi kwa miaka 50 hatuzipati" alizungumza Ilan
"Hebu niambie ni dili gani ndugu yangu" alizungumza Austin kwa hamu iliyozidi kipimo
"Hahaha mbona una haraka ndugu yangu.....ni hivi dili lenyewe amenishirikisha rafiki yangu anayetoka nchini kwenu Tanzania anaitwa Jacob yeye anachukua PhD ya pharmacy sasa baadae usiku nitakuja na Josh tuongee vizuri"
"Baadae kuna mtu wa muhimu natakiwa kukutana naye"
"Hamna shida tufanye kesho usiku basi"
"Si uniambie tu sasa hivi"
"Tulia wewe.....jipange kesho tutakutana najua hautaniangusha" Ilan na alisema na kisha kuondoka akimwacha Austin kwenye mawazo akiwaza ni dili gani hilo lenye pesa nyingi hivyo
'Atakuwa anatania tu huyu mjinga' Austin aliwaza na kisha kulala ili apunguze uchovu kidogo

                     ***************
Mida ya saa mbili kasoro usiku Austin alikuwa ndani ya Havard square hotel mahali ambapo aliahidiana na mdhamini wake kwamba wakutane aliingia kwenye sehemu ya chakula na kuangaza macho huku na huko akiitafuta sehemu moja yenye utulivu, alienda kwenye meza iliyoko kwenye kona kisha alikaa kwenye kiti, alinyanyua mkono wake na kisha kuangalia saa yake nzuri aliyopewa na mchumba wake Olivia iliasoma saa mbili kasoro dakika tano
'bora nimewahi hawa wazungu wanapenda sana kutunza mda' aliwaza Austin kisha aliichukua simu yake mfukoni na kumtumia mfadhili wake ujumbe mfupi kuashiria kuwa ameshafika na kumuelekeza mahali alipokaa
Aliinua uso wake ili aendelee kuyafurahia mazingira ya pale
Loh! mzee mmoja mzungu aliyevaa suti safi nyeusi alikuwa amekaa kwenye kiti cha upande wa pili wa meza akimtizama Austin kana kwamba alikuwepo hapo kitambo, mzee huyu alikuwa na mvi kiasi na uso usiokaukiwa na tabasamu
Austin alipatwa na mshtuko kidogo kwani hakujua mtu huyo amefika mda gani, sura ya mzee huyo aliitambua haswa kuwa ndiye mfadhili wake, aliinuka na kumsalimu kwa heshima...
"Nimefurahi kukuona ukiwa mzima kabisa kijana wangu Austin" mzee yule alianza mazungumzo kwa kiswahili fasaha kabisa
"Nimefurahi kukuona pia baba karibu sana Havard....ni miaka mingi sana nilitamani sana kukutana na wewe" Austin aliongea
"Asante sana walezi wako waliniambia namna ulivyotamani kuniona na leo tumepata nafasi.....nadhani unanifahamu vyema naitwa Mr. McDonald"
"Nakufahamu vizuri sana mzee" alijibu Austin akitabasamu
"Hahahahahaha hunifahamu vizuri kijana.....kesho utakuwa na ratiba gani?" Alimuuliza mzee huyo
"Tumemaliza mitihani leo hivyo kesho nitakuwa na mapumziko" 
"Sawa jiandae kesho utaenda na mimi kwenye mapumziko" alisema mzee huyo na bila kusubiri jibu alinyanyuka na kuanza kuondoka
Austin hakumuelewa kabisa alijua labda mzee huyo ameenda maliwato lakini dakika zaidi ya 20 zilipita na hakumuona
'Heee ameondoka?' alijiuliza Austin, alijua kabisa wangekuwa na mengi ya kuzungumza lakini hakuelewa kwanini mzee huyo aondoke mapema namna hiyo tena bila hata kuaga alisubiri kwa dakika kumi zingine kisha alichoka na kuamua kuondoka hotelini hapo akiwa na mawazo tele
'Sijui huyu mzee mzimu maana mambo yake hayaeleweki' aliwaza Austin akiwa amejilaza chumbani kwake na kisha alianza kujicheka kwa wazo lake la kipuuzi
'Labda alikuwa anamuwahi demu wake maana hivi vizee vya kizungu vinapenda sana watoto' aliendelea kuwaza pumba na usingizi ulimchukua taratibu
      
                     *****************
Austin alishtuka asubuhi baada ya kuhisi kuna mtu anamwamsha alikurupuka kwa hasira akijua ni Ilan anamwamsha kwa kweli hakuna kitu Austin alikipenda kama kulala ilikuwa ni heri umnyime chakula kuliko umsumbue usingizini
Alikutana na sura ya mtu asiyemjua akimwamsha, aliamka kwa taharuki hakujua mtu yule amefikaje ndani ya chumba chake wakati alikifunga usiku
Hakuwa mtu mmoja bali wawili mwingine alikuwa nyuma kidogo na wote walivaa suti nyeusi za gharama
"Nyie ni kina nani?" Aliuliza kwa tahamaki
"Tumetumwa na mkuu tukuchukue anakusubiri kwahiyo amka na ujiandae haraka"
"Mkuu gani?" Aliuliza Austin akionyesha wasiwasi
"Mr McDonald" alijibu mmojawao
"Sina ratiba nae mimi" 
"Ametuambia alishakwambia kwahiyo jiandae tunaondoka baada ya nusu saa" alijibu mtu huyo akianza kuondoka na mwenzake
"Subiri kwanza mmefikaje hapa" aliuliza Austin, mtu yule aligeuka tu kisha kupuuza swali
"Tunza mda tafadhali tuna dakika ishirini tu" alisema na kutoka nje kabisa pamoja na mwenzake
'Huyu mzee mpuuzi nini ananitumia watu kunichukua kwani lazima?' aliwaza Austin kwa hasira
'kama sio kumheshimu kwa kunisomesha nisingeenda' aliwaza, alisonya kisha akavuta taulo lake na kuelekea bafu lililopo ndani ya chumba chake
ITAENDELEA USIKOSE SEHEMU IJAYO...........

Please ukisoma like share na ucomment tukutane kesho

Jaba Zulma

Siyumbi

Your Thoughts

Previous Post Next Post

Contact Form