Ngoma Ngumu 06

RIWAYA; NGOMA NGUMU



NA; BAHATI K MWAMBA.

SIMU; 0758573660/0624155629.


 SEHEMU YA SITA..


“Mbona kama roho yangu inakataa kumwamini huyu jamaa, halafu anaonekana kuwa mjanjamjanja sana.”, Sajini Aliwaza huku akiendelea kufuatilia nyendo za mshukiwa wake.


“Kwa nini hili litokee na huyu jamaa awepo hili eneo?” Alijiuliza tena huku akimwona mshukiwa wake akipanda pikipiki na kutomea. Haraka alimfuata ofisa mmoja na kumwagiza mafuatilie hadi atakapoishia. Alipomaliza kutoa maagizo, alirejea kuendelea na kazi nyingine.


   Zuki Gadu hakuwa mjinga kiasi hicho, wakati anatoka ndani ya benki alikuwa makini kuwatizama watu ambao walikuwa kwenye lile eneo. Macho yake yalikutana na sura ya ofisa aliyemfahamu vema. Ofisa ambae ni mla rushwa kuliko udhaniavyo. Baada ya kumuona pale na namna walivyotazamana, moja kwa moja alihisi kuna jambo yule bwana atakuwa analifikiria. 


“Huyu bwege anaweza kuharibu kila kitu. Ananitilia shaka ingali mapema sana.” Aliwaza huku akipanda pikipiki na kwa pembe ya jicho lake, aliweza kumuona alivyokuwa anatoa maelekezo huku akimnyooshea kidole.


“Kumekucha!”Aliwaza huku akiwaza jambo la kufanya ili Sajini Nyau asiendelee kumfuata. Alifika kwenye hoteli aliyofikia na kumlipa dereva aliyempeleka. Baada ya kulipa hakuingia ndani bali alisimama nje ya lango akiangalia kule alikotokea. 


   Dakika mbili baadae, alitokea ofisa mmoja akiwa kwenye pikipiki. Ofisa yule alishituka baada ya kumuona Miguu ya kuku akitizama kule alikokuwa akitokea. Polisi hakusimama, alipitiliza kama vile hakuwa na lengo la kumfuatilia mtu.


 “Nilijua ni lazima huyu bwege atatuma mtu anifuate!” Aliwaza huku akipita getini na kuingia ndani ya hoteli aliyofikia jijini Nairobi.


  Alipoingia ndani, alienda kujibwaga kitandani kama mtu aliyekoswa kufumaniwa. Aliwaza mawili matatu, kisha akainuka na kuchukua simu yake, akazitafuta namba za simu za Bob Rando.


   “Niko Nairobi!” Alimwabia Bob.


“Safi sana, umefika wakati mwafaka, unatakiwa kwenye usaili kesho. Nenda upate kazi kwenye hiyo kampuni.” 


“Tuahirishe huo mpango, tayari nishaharibu huku.” 


“Oh! Una haraka sana mzee, ile ni Benki ya taifa. Usipokuwa makini utaozea gerezani!” 


“Nitatema ndoano kabla sijafikia huko, lakini tusiombeane hayo kwa sasa!” 


“Ok! Kuna jambo gani tena?”


“Nitafutie mwanamke mzuri sana Nairobi Nzima. Nataka kufanya nae kitu.”


“Wewe na wanawake wapi na wapi?” 


“Siyo ulivyowaza, nina mahitaji nae mengine ya msingi sana. Kama utampata sasa hivi, itakuwa vema zaidi na umlete nilipo.” 


“Sawa!” Bob alijibu na kukata simu. 


Baada ya kukata simu, Miguu ya kuku alimkumbuka Kaimu Meneja wa benki ya Umoja, bwana Mensa Munga. Haraka alikimbilia simu yake na kuwasha data, ambapo aliingiza lile jina na kuanza kufuatilia taarifa muhimu kuhusu yule bwana. 


  “Taarifa zake si za wazi sana. Hili si jambo la kawaida kwa watu wakubwa kama yeye!” Aliwaza huku akiendelea kuperuzi na kudadisi baadhi ya mambo ambayo alihisi yatamrahisishia mambo yake. Hadi anamaliza kusoma taarifa za bwana Mensa Munga, hakuwa ameambulia chochote cha maana. 


“Naona ugumu wa hii kazi!” Alisema huku akikuna kichwa chake kwa kidole chake cha shahada.


“Sikuwa na haja sana na huyu Kaimu Meneja, shida yangu ilikuwa ni Meneja mwenyewe. Je, atakuwa wapi? Ni ngumu sana kwa tukio kama lile kutokea kwenye benki yake na asitokee hadharani. Pia ofisi ikikaimiwa, ina maana mwenye ofisi atakuwa hayupo. Sasa yu wapi bwana huyo?” Alijiuliza huku akikaa kitandani. 


 “Bila kumpata Meneja, kazi yangu itakuwa ngumu mara dufu.” Aliwaza huku akitaka kujilaza kitandani. Ghafla alikurupuka kama aliyetekenywa. 


  Alisimama wima akifikiria jambo.


“Kama chini ya jengo kuna ofisi za usalama wa nchi, wanaingilia wapi? Naamini kuna mafundi ambao huwa wanaenda kurekebisha mitambo, huwa wanapitia wapi? Kule ndani sijaona kambarau ya kwenda juu au kushuka chini.” Aliwaza huku akizunguka ndani ya chumba.


“Hapa ndipo ilipotuzo ya ushindi wangu. Lazima kuna mlango ambao unapitisha wafanyakazi wa usalama na mlango unaopitisha watunza Kuba.” Aliendelea kufikiria. 


“Naamini mlango huo hauko ndani ya benki. Sijaona kabisa dalili ya ile benki kuwa sehemu ya kushushia watu kwenda ground na sijaona watu wakiingia ndani ya lile jengo kwa nia ya kushuka chini. Labda tuseme wanaingilia kwenye kambarau ya jengo zima, hapana. Hawawezi kushiriki hilo jambo na raia wa kawaida.” Alijiuliza maswali na kujijibu mwenyewe.


     Wakati akiwa kwenye lindi la mawazo, mara simu yake ikaunguruma. Haraka aliidaka na kubofya kipokea.


“Nimempata mwanamke uliyemuhitaji. Anaitwa Susa Mchachuko. Ni mrembo wa viwango vyote unavyohitaji.” Rando alimwambia baada ya simu kuunganishwa.


“Anaweza kufika hapa ndani ya muda gani?” Zuki aliuliza.


“Mpe nusu saa tu!” 


“Sawa, mpe mawasiliano yangu. Mwambie atumie Threema au Jabba. Jumbe ziwe secured!” 


“Anajua kila kitu. Nitafute ukiishiwa mbinu.” Bob Rando alisema na kukata simu. 


  Miguu ya kuku alibaki akiwa ameshika simu yake bila kuamua lolote. Kuna jambo alikuwa anawaza kuhusu mwanamke uliyemuhitaji. Nafsi yake ilikuwa inakinzana na maamuzi yake aliyoyafanya. 


“Lakini kuna wakati mambo magumu yanahitaji njia rahisi kuyatatua. Namuamini Rando, hawezi niletea garasa.” Aliwaza huku akiwasha data kwenye simu yake, ili iwe rahisi kupokea ujumbe wa Susa.


    Wakati akijipa muda kumngoja Susa Mchachuko, aliamua kuendelea kufanya jambo lingine ambalo lingempa mwanga wa mtego wake. Alivua saa yake aliyokuwa ameivaa, kisha akachomoa ufunguo wake. Simu ilitoa mlio fulani wa bip mara tatu, na kioo cha saa kikajaa wino mweusi ambao ulikuwa umepitia na msitari mwembamba wenye rangi nyeupe. Mwishoni mwa msitari huo kulikuwa na namba mbili. 


 Lengo lake lilikuwa ni hizo namba, haraka alichukua kalamu na kuandika zile namba kwenye kiganja chake, kisha akaitupa ile saa kitandani huku macho yake yakiwa yameganda kiganjani mwake. 

0.9 ndizo namba alizokuwa amezikodelea macho huku akili yake ikizunguka zaidi ya pangaboi. 


 “Sekunde tisa!” Aliwaza huku akigeukia kitandani ilipokuwa saa yake, aliitizama kwa sekunde chache kisha alirejea kuzitizama zile namba. Ni kama hakuridhika na kile alichokuwa amekiona. Taratibu alichomoa kalamu aliyokuwa ameipachika kwenye mfuko wa shati lake. Alielekea ukutani na kuwasha taa kisha aliinua mkono wenye kalamu hadi ilipovuka usawa wa kimo chake, kisha aliinua uso wake na kufanya aitazame kalamu huku akiwa ameinua macho yake bila kujali ukali wa taa iliyokuwa ikiwaka mchana ule. Alifanya vile kwa kuwa alihitaji kuona kitu fulani ambacho alihitaji kukiona ndani ya kalamu. 


 0.92, hicho ndicho alikiona ndani ya kalamu. Alishusha kalamu yake huku uso ukiwa umajikunja kwa tafakuri. Licha ya kuonekana hakubaliani na kile alichokiona, lakini ukweli ni kuwa hakuwa amedanganywa na vifaa vyake vile ambavyo vilikuwa maalumu kupima mjongeo wowote wa kieletroniki, kisha hupiga hesabu ya mwendo huo na kutoa majibu ndani ya dakika moja baada ya upimaji. Lengo la kwenda na vifaa hivyo ndani ya benki, ni kujaribu kujua Kuba itakuwa umbali gani kutoka ilipokuwa mashine ya kutolea pesa. Miguu ya kuku aliamini Kuba hiyo itakuwa haiko mbali na Kuba kubwa ambayo huhifadhi pesa zote za benki. Ikiwa Kuba ndogo ambayo huwekwa kiwango maalumu cha pesa ili kuhudumia watumia kadi, basi Kuba kubwa haitakuwa mbali na hapo na hata zile Kuba zenye plate nazo zitakuwa maeneo hayohayo. 


   Kile kitendo cha kujua kutoka ilipo Kuba hadi pesa kufika kwenye ATM huchukua sekunde tisa, ilimaanisha kulikuwa na umbali wa kawaida ambao haukuwa umbali mrefu. Hiyo imaanisha Kuba hazikuwa chini kama alivyodhani. 


“Hii inatokeaje kirahisi namna hiyo?” Aliwaza huku akiitupa kalamu juu ya kitanda na yeye kujibweteka kivivu. 


“Hapa naamini kuna Kuba mbili zenye kazi tofauti. Hii Kuba ya pesa ipo upande wa juu wa hilo jengo, ila Kuba yenye plate itakuwa inalindwa ndani ya jengo la usalama wa nchi.” Aliwaza huku akijikuna kidevu chake. Licha ya kuwaza hivyo lakini aliamini usimamizi wa plate hizo utakuwa chini ya mamlaka ya benki na mtu pekee ambae angeliweza kumfukisha huko ni Meneja wa Benki ambae hadi wakati huo hakuwa amejua alipo. 


“Itakuwa bahati mbaya sana kama Meneja atakuwa nje ya nchi, lakini akiwa ndani ya nchi ni hakika atakuwa anajua njia ya kuingilia ndani ya jengo la usalama. Na ndiye atakaenifikisha kwenye kilele cha mafanikio. Lakini nitampataje?” Alijiuliza swali la muhimu sana kwenye mpango wake.


 Akiwa kwenye lindi la mawazo, masikio yake yalisikia mlio wa ujumbe kwenye simu yake. Haraka aliikwapua na kuusoma.


“Niko nje ya Pama, nielekeze chumba chako. Susa.” Ujumbe ulisomeka hivyo, haraka aliujibu..


“Twiga room!” Kisha haraka alianza kuondoa baadhi ya vitu ambavyo hakutaka mtu mwingine avione. Alivihifadhi chini ya godoro na kwenda kufungua mlango, baada ya kusikia ukigongwa mara kadhaa. 


ITAENDELEA.

Jaba Zulma

Siyumbi

Your Thoughts

Previous Post Next Post

Contact Form