RIWAYA; NGOMA NGUMU.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SIMU; 0758573660/0624155629.
SEHEMU YA NANE..
Hakutegemea kusikia yeye ni miongoni mwa windo la Miguu ya kuku. Mwili uliingiwa na ubaridi na akili ikisimama kufanya kazi kwa sekunde kadhaa.
“Susa, una hakika na unachokisema?”
“Uhakika ninao na amenipa kazi ya kukufuatilia. Kaahidi kunilipa pesa nyingi sana endapo nikifanikiwa kunasa nyendo zako zote.” Susa alimfafanulia.
“Kakwambia ananiwinda kwa sababu gani?”
“Hajasema ila kanambia nikifanikiwa kukuingiza mtegoni, atanielekeza cha kufanya juu yako.”
“Mh! Sajini aliguna huku akizunguka ndani ya chumba bila kujua kilichomzungusha.
“Sasa hapo unahisi utajiri upo wapi?” Hatimae alisimama na kumuuliza Susa.
“Ninahisi kuna jambo kubwa anataka kulifanya hivyo ameona ni bora ajue mizunguko yako, usije kumharibia mambo yake. Sasa hilo analopanga, ndilo ninalohitaji lituingizie pesa kutoka kwake au aliyemtuma.”
“Lakini mbona kuna maofisa wengi sana tena wenye vyeo vikubwa, why me?”
“Waswahili mwajuana kwa vilemba. Anajua kazi zako nyeusi, hivyo anaweza kuwa anahofu utamharibia mipango yake.”
Sajini hakuongeza neno, badala yake aliishia kumkodolea macho Susa ambae alikuwa amekaa kitandani akichati na simu.
“Banki ya umoja!” Sajini aliongea taratibu kama vile hakuhitaji mwingine asikie.
“Benki? Kuna nini huko Benki?” Susa aliuliza maswali mfululizo huku akinyanyuka kitandani.
“Leo kuna tukio limefanyika benki na hakuna ambae alijua lilitokeaje na alielifanya ni huyohuyo jamaa.”
“Tukio gani?”
“Jamaa alipoingiza kadi yake ya benki, mfumo wa pesa ukaharibika na kuanza kumwaga pesa bila mpangilio. Kadi yake ilipokaguliwa ilikutwa na kiasi kikubwa cha pesa, jambo ambalo limewafanya polisi waanze kupuzia uchunguzi kwa kuwa hawakuona dalili za wizi kwa mtu huyo.. Akaunti yake inasoma zaidi ya Milioni mia tano za Kenya. Sasa huyo atawezaje kuiba kwenye ATM?”
“Kwa hiyo na wewe uliamini hawezi kuiba?”
“Siyo rahisi kihivyo. Kwanza nilipomuona tu, roho yangu ikashindwa kutulia na palepale nilifanikiwa kujua anapoishi. Ni karibu na hapo Benki. Hilo haliwezi kuwa jambo la bahati mbaya ni lazima kutakuwa na kitu anakipanga.”
“Hebu nipe muda nijue anachopanga, kisha nitakujuza na sisi tupa…..”
“No! Siwezi kuondoka hapa bila kujua anachopanga. Hebu mpigie simu.” Sajini alimwambia Susa. Na bila kuchelewa, simu ikawa hewani na waliiweka kwenye sauti kubwa.
“Yes Susa!” Miguu ya kuku aliitika punde tu alipopokea simu.
“Kazi ya kwanza nimeshaifanya. Tayari nina namba zake na tumekubaliana kukutana baadae kidogo.”
“Good! Umefanya kazi nzuri sana. Endelea hadi nitakapokupa maelekezo mengine zaidi.”
“Sawa. Lakini si vibaya ukinishirikisha sasa ili nijue najiweka vipi kwake.”
“Vyovyote utakavyojiweka kwangu ni hatua. Kikubwa kuwa makini. Watch your step!”
“Ok!” Susa alijibu kinyonge na kukata simu kisha alimgeukia Sajini Nyau.
“Nadhani umesikia. Sasa jiandae muda wowote tutajua kinachoendelea.”
“Duh! Lakini bado najiuliza kwa nini mimi niwe windo lake? Na baada ya hapo atanifanya nini?”
“Kuwa makini kwa siku hizi chache. Nitakujuza kila kitu tutachopanga na huyo bwege. Akiwa mzigo sana tunamchapa za uso tumtupe msitu wa Kibera awe chakula ya fisi.” Susa alisema huku akichukua mkoba wake na kuuweka begani kwa nia ya kuondoka.
“Hebu nipe kwanza dawa ya kichwa, kisha niingie kumwinda huyu jamaa. Lazima nijue anakutana na nani na wanapanga nini juu yangu.” Sajini alisema huku akimshika mkono mwenyeji wake.
“Mh jamani, husahau tu. Haya nifanye utakavyo mpenzi.” Susa alisema huku akiachia mkoba wake uende chini bila kizuizi na taratibu aliinua mikono yake na kuiweka juu ya mabega ya sajini Nyau ambae nae alimpokea kwa bashasha huku akili yake ikiwaza jambo moja tu, ngono.
****
Wakati wao wakiwa wanaingia kwenye ulimwengu wa wazinifu, Miguu ya kuku alikuwa anashuka kwenye gari na kurejea ndani ya hoteli. Kuna pahali alikuwa anataka kwenda kwa kutumia gari aliloachiwa na Susa, lakini alisita kulitumia baada ya kuongea na Susa. Aliingiwa na mashaka na maongezi walioongea, kuna kitu alihisi hakiko sawa. Kwanza ni namna ambavyo Susa alitumia muda mfupi kukutana na Nyau, lakini cha kushangaza zaidi ni namna ambavyo alifanikiwa kuaminiwa na huyo jamaa.
“Yaani mtu akutongoze dakika moja na dakika inayofuata ukubali?” Aliwaza wakati akisukuma mlango wa chumba chake na kuingia.
“Hata kama kuna wanaume malaya, haiwezi kuwa haraka hivyo. Yaani uone mtu dakika moja na dakika inayofuata umtongoze? Umpe namba zako? Haiingii akilini kirahisi namna hiyo.” Alizidi kuwaza lakini mashaka yake yalithibitishwa na jambo moja; wakati walipokuwa wakiongea, alikuwa anasikia mwangwi wa sauti yake kila alipokuwa akiongea. Hiyo ilimaanisha aliwekwa kwenye sauti kubwa. Na kama ndivyo ilivyo, ilimaanisha kulikuwa na mtu mwingine pembeni ambae alikuwa anasikia maongezi yao. Ni nani mtu huyo? Hakuwa na jibu.
“Huyu binti kacheza karata mbaya sana kwangu.” Alijisemea huku akitabasamu na kuutupa ufunguo kitandani, kisha alifunga mlango na kutoka nje, ambapo alitembea kuelekea sehemu ambayo angelipata usafiri wa haraka.
Mbele yake kulikuwa na pikipiki mbili, ambapo aliita moja na kupanda na kuomba kupelekwa mtaa wa pili. Walikubaliana bei kisha safari ilianza. Dakika chache walifika sehemu fulani ambayo aliona inafaa kuachwa. Alishuka na kumlipa dereva pikipiki na kisha alianza kutembea kwa miguu akiwa na lengo la kumpoteza yule dereva ili asijue alipokuwa akielekea, endapo kama kungelitokea mtu wa kuuliza kuhusu safari yake hiyo.
Alipohakikisha dereva ameondoka, nae alichepuka kwenye uchochoro fulani na kuufuata kwa hatua ndefundefu hadi macho yake yalipoweza kuona bango kubwa lililokuwa limeandikwa ‘Tujibambe Bar.’ Aliangaza huku na huko hadi alipofanikiwa kuona sehemu iliyokuwa imeegeshwa magari ya wateja wa bar ile maarufu. Macho yake yalikuwa makini na kutizama vibati vya magari. Alifanya hivyo kwa kila gari aliloona lipo hapo, hadi pale alipofanikiwa kuona namba za gari alilokuwa analitafuta. Alipiga hatua na kwenda kuingia ndani yake ambapo alikuta funguo zake zikiwa zipo sehemu husika, aliwasha lile gari na kuondoka bila kuulizwa na mlinzi ambae alikuwa maeneo yale. Kulikuwa ni gari la mmoja wa marafiki zake ambao walikuwa Nairobi, alikuwa ameliomba baada ya kushindwa kuamini kulitumia gari la Susa ambae hadi wakati huo alikuwa ameshindwa kumwamini tena.
“Wanawake wajinga sana!” Alijisemea huku akiiingiza gari kwenye barabara kuu na kumbukumbu mbaya zikipita kichwani mwake, kumbukumbu ambazo zilitokana madhira ya wanawake juu yake, kiasi kilichomfanya kutokumuamini mwanamke yeyote Duniani ijapokuwa, kuna wakati alikuwa anawatumia kufanikisha mambo yake. Lakini hata kuwatumia huko ni kwa sababu aliamini ni kutokuwa waaminifu kwa watu aliowatuma kwao. Kifupi aliamini mwanamke si lolote mbele ya neno la mwanaume, hasa mwanaume mwenye pesa.
“Mwanamke si lolote mbele ya pesa na si lolote mbele ya sauti ya mwanaume.” Alijisemea huku akisindikiza na sonyo refu ambalo hakujua kama angeliweza kulitoa kwa kuwa lilikuwa ni sonyo la kunyali. Lakini kwa sababu ya chuki zake, alijikuta akiweza kulitoa kwa usahihi kabisa.
Miguu ya kuku aliendesha gari hadi alipofika karibu na Benki ya Umoja. Alisimamisha gari kwa mbali kidogo sehemu ambayo aliweza kuona upande wa mbele wa ile benki. Alisimama bila kuzima gari lake, kisha alikaa vema kumtizama kila aliyeingia na kutoka ndani ya benki ile.
Alikaa kwenye gari zaidi ya saa mbili na wakati wote huo, hakuwa amebandua macho yake upande wa benki. Kukaa kwake pale kulimfanikishia mambo mawili makubwa, kwanza; alifanikiwa kuliona gari la kampuni ya Jatu, ambapo kwa harakaharaka alipolitafuta mtandaoni, aligundua ni kampuni la usalama wa vifaa vya kieletroni na mifumo ya kompyuta. Lakini jambo la pili alifanikiwa kuona aina ya gari ambalo Kaimu Meneja alilitumia. Alitambua gari hilo kwa kuwa alimuona zaidi ya mbili akilipanda na kuondoka, kisha kurejea baada ya muda mfupi na mara ya mwisho alifanikiwa kumuona akirejea akiwa ameongozana na lile gari la kampuni ya Jatu ambapo, lilishusha watu watatu walioongozana na Meneja Mensa Munga kuelekea ndani ya benki. Kwake huo ulikuwa ni ushindi wa awali kabisa.
Kile kilichokuwa kimempeleka pale hatimae kiliwadia. Macho yake yakiwa makini kutizama mbele, aliondoa gari pale alipokuwa na kuingia barabarani huku macho yake yakiwa makini kabisa kutizama gari lililokuwa mbele yake. Lilikuwa ni gari la Kaimu Meneja Mensa Munga.
Aliendesha gari kwa umakini ili dereva wa gari la Meneja, asigundue kama anafuatiliwa kwa nyuma. Lakini hata yeye alikuwa akiendesha kwa umakini ili asije kuingia kwenye mtego wa maofisa usalama ambao pengine walikuwa wanafuatilia nyendo zake.
ITAENDELEA.
