ACETAMIN-220...(12)
MTUNZI:BARAKA GEOFREY
+255652089642
TAHADHARI:Majina na matukio yote kwenye simulizi hii ni ya kutungwa tu kwa ajili ya kufikisha ujumbe.
ILIPOISHIA..........
Helikopta ilipasua anga kwa dakika kadhaa mpaka bandari ya Dammam iliyopo mashariki kabisa mwa mji wa Riyadh kwenye ghuba ya Persia.....bwana mdogo alishushwa na kupandishwa kwenye nyambizi moja ndogo ya kisasa humo aliwakuta vijana wengine kama kumi tofauti kabisa na alitoka nao Pakistan safari ya yule mwanaume mjapan iliishia pale, nyambizi iliyakata maji kwa kasi na kuibuka kwenye pwani ya India jiji la Mumbai...Aaron alisafirishwa mpaka jiji la New Delhi kwa ndege na kisha alipandishwa ndege mpaka jiji la New York Marekani
ENDELEA..........
Jijini New York Aaron alikutanishwa na mrusi mmoja mmoja wa kompyuta na teknolojia aliyeitwa Dimitri Adrian huyo alimpa mafunzo makali kuhusu udukuzi (hacking), kutengeneza programme mbalimbali na ujanja mwingi wa kimtandao pia alifundishwa mambo mengi sana ya kiteknolojia kwa miaka mitatu
Aaron akiwa na miaka 14 alipelekwa nchini Iraq ilipo kambi ya siri ya bwana Abd al-Uzza inayotoa mafunzo makali ya kikomandoo na huko alipata mafunzo hayo mazito kwa miaka mitatu na kuhitimu akiwa ni mmoja kati ya vijana wadogo wachache waliofanikiwa kuhitimu mafunzo hayo ya kutisha kwani wengi walikufa katikati ya mafunzo hayo magumu....pamoja na ugumu huo lakini Aaron alionyesha uhodari mkubwa kuwapita hata wengine waliomwacha mbali kiumri
****************
SAUDI ARABIA - 2010
Aaron alikuwa ametulia ndani ya ndege ya shirika la Qatar airways inayoelekea Saudi Arabia kipindi hicho alikuwa ametimiza miaka 17, alikuwa anarejea tena kwa bwana Abd al-Uzza kupewa maelekezo zaidi kwani aliwaahidi kuwapa kazi maalum baada ya mafunzo hayo......
Majira ya saa 8 mchana ndege ilitua uwanjani jiji la Riyadh na Aaron alishuka kama kawaida alimuona mtu akiwa na bango lenye jina lake na alimfuata, alipelekwa kwenye jumba la kifahari la bwana Abd na alipewa maelekezo ya kumsubiri kwenye chumba cha mkutano baada ya kupata chakula cha maana na kinywaji haikuchukua mda mrefu bwana Abd aliingia ndani ya chumba hicho mara hii alikuwa yeye peke yake...
"Naona umekua sasa kijana wangu.....karibu tena nyumbani" alisema bwana Abd akitabasamu
"Asante" alijibu Aaron
"Hongera kwa kupita kwenye mafunzo hayo magumu wengi huwa wanaishia njiani.."
"Asante mkuu"
"Sasa nadhani twende kwenye kazi ya msingi niliyokuitia" alitulia kwa mda kidogo kuuvuta umakini wa Aaron
"Nadhani umepitia mafunzo ya kutosha na pia umefanya misheni nyingi hivyo una uzoefu wa kutosha licha ya umri wako....toka siku ya kwanza nilivyokuona nilikuona kuwa ni kijana mpambanaji na mwenye uwezo mkubwa hivyo nikuambie kuwa nakuamini sana kuwa utaifanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa" bwana Abd aliweka kituo kidogo
"Nadhani unaifahamu Afrika Mashariki"
"Ndiyo ni asili yangu" alisema Aaron
"Vizuri sana....baada ya kuuona uwezo wako nimekuteua kuwa kiongozi wa oparesheni maalum huko" aliweka kituo kifupi na kisha kuendelea
"Kama nilivyowaambia mwanzoni ili kuileta haki ya kweli duniani tunaihitaji kushika maeneo yote duniani, tayari tumefanikiwa kuanzisha kikundi cha wapambanaji cha Al Shabaab nchini Somalia mwaka 2004 ambacho kitakuwa msaada wenu mkubwa katika harakati hizo pia tumeanzisha vikundi vingi tu vya wapambanaji kama Boko Haram, Abdullah Azzam brigades na Ansal al-sharia
na lengo letu hasa ni kusambaa Afrika na dunia yote" bwana Abd aliweka kituo tena kwa wakati huo akili ya Aaron ilisafiri maili nyingi na kukumbuka tukio baya sana ambalo lilianza kusahaulika kwenye maisha yake, picha ya mama yake akimiminiwa risasi ilikuja ghafla kichwani mwake
"Tuko pamoja kijana?" sauti ya bwana Abd ilimshtua kutoka kwenye mawazo
"Ndiyo mkuu" alijibu kama mtu aliyeshtuka kutoka usingizini
"Sawa kuanzia sasa wewe utakuwa kiongozi wa oparesheni hiyo na mtaanzia nchini Kenya kutoka hapa utapelekwa kwenye ofisi yako na huko utaanza majukumu yako rasmi, maelekezo mengine utayakuta huko, nitahitaji ripoti kila baada ya miezi sita na ukumbuke kazi hi ni ya umuhimu na usiri mkubwa hivyo umakini mkubwa unahitajika" alikamilisha bwana Abd na kuinuka kisha kutoka ndani ya chumba hicho hakuhitaji maswali, maoni wala ushauri kikao ndiyo kilikuwa kimefungwa rasmi
****Mwaka 1959 serikali ya kikoloni ilihisi uwepo wa mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika mashariki na kuanza rasmi utafiti lakini kabla hawajafika mwisho wa utafiti wao walitimuliwa katika ukanda huo na nchi zote Afrika Mashariki zilijipatia uhuru wake mpaka mwaka 1963 Kenya ikiwa nchi ya mwisho kupata uhuru wake ambao iliupata tarehe 12/12/1963
Utafiti huo ulicheleweshwa mpaka miaka ya 2000 mwanzoni ambapo hazina kubwa ya mafuta na gesi iligunduliwa Afrika Mashariki...nchi zilizoendelea na wawekezaji mbalimbali walidondosha mate kwa tamaa ya hazina hiyo kubwa sana
Bwana Abd al-Uzza pia alipata fununu za ugunduzi huo na alihakikisha kwamba ni kweli hivyo yeye pia alisuka mikakati madhubuti ya kuikwapua hazina hiyo adhimu kutoka kwa nchi hizi zinazoendelea****
Mwanamke mmoja aliingia kwenye chumba hicho na kumwongoza mpaka nje kwenye gari nyeusi ya kifahari aina ya Bugatti Veyron
"Bosi amesema nikukabidhi hili gari" alisema mwanamke yule, Aaron alishangaa tu kwani hakujua kama amepewa lile gari na bwana Abd alipogeuka alimuona yule mwanamke akiishia zake ndani ya lile jumba, aliingia ndani ya gari na kukaa kwenye kiti cha dereva
"Karibu Ayman al-Zawahiri kiongozi wa oparesheni maalum mimi nitakuwa msaidizi wako" sauti nyororo ilisikika kwenye spika za gari hilo, Aaron hakushtuka sana kwani teknolojia kama hizo alijifunza alipokuwa nchini Marekani
"Weka mkono wako hapo" sauti ile ilimuelekeza na kioo chenye umbo la mkono kikaanza kuwaka mwanga mwekundu, Aaron aliweka mkono na 'fingerprints recorded successively' kioo cha kwenye dashboard kilionesha maneno hayo...kisha ramani ya jiji la Riyadh ikatokea kwenye kioo na hapo kidoti chekundu kilikua kikiwaka waka eneo mojawapo
"Endesha mpaka kwenye eneo hilo hapo ndiyo ofisini unapotakiwa kufika" sauti ilimuelekeza tena
Aaron aliwasha gari na kuondoka kuelekea eneo hilo alijikuta mbele ya jumba kubwa la kifahari na hapo geti lilifunguka mbele yake walikuwepo walinzi kama watano walioshika silaha zao na wote kwa pamoja walipiga saluti ya heshima gari yake ilipoingia na kisha alielekezwa sehemu ya kupaki.... Aaron alishangaa mapokezi hayo anayopewa kama mtu mkubwa, mdada mrembo alimpokea na kumpeleka mpaka chumba kimoja ambako ilikuwepo ofisi yake
"Karibu bosi" mdada yule alimkaribisha kwa heshima
"Naitwa Chloe ni katibu wako" alijitambulisha mwanadada yule
"Asante" alijibu Aaron kifupi kisha mdada yule alitoka nje na mara simu iliyokuwepo mezani iliita, alinyanyua mkonga wa simu na kuipokea
"Natumaini umeshafika ofisini kwako.... Baada ya masaa mawili jiandae utakuwa na kikao na watu waliopo chini yako watakaokusaidia katika oparesheni yako" sauti ya bwana Abd al-Uzza ilisikika na kisha simu ilikatika
Aaron alishususha pumzi na kutulia kitini akitafakari juu ya jukumu alilopewa lakini pia kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kupita alianza kuikumbuka familia yake aliwaza sana kama kaka yake yuko hai au aliuawa kwenye shambulio lile
'Hapana mimi ni mpambanaji sitakiwi kuwaza juu ya yaliyopita' kwa kiasi fulani nafsi ilimwambia kuwa hayupo upande sahihi na amejiunga na watu wakatili walioua familia yake
'Hapana hawakufanya ukatili bali walikuwa kwenye harakati za kupambana na madhalimu wanaounyanyasa ulimwengu' mgogoro uliendelea nafsini mwake, akiwa bado amezama kwenye mawazo kengele ya ofisini kwake ililia na alimruhusu aliyeko nje aingie
"Mkuu wageni wote wapo chumba cha mkutano wanakusubiri" alikuwa ni Chloe katibu wake aliyemletea ujumbe
"Sawa" alijibu na kisha kuinuka alimfuata mdada yule mpaka chumba cha mikutano kisha yeye aliishia nje, Aaron aliingia ndani na kukuta watu takribani kumi mle ndani na wote walisimama kwa heshima, bado Aaron aliwaza inakuwaje aheshimiwe hivyo na watu hao ambao walionekana wakubwa na wenye cheo kuliko yeye, baada ya Aaron kukaa kwenye kiti na wote walikaa na kutulia kimya
Aaron hakujua aanzie wapi kwani hakujipanga hata na kikao hicho ni kama mtu mmoja alimsoma mawazo yake na alijikoholesha kidogo kuashiria anataka azungumze
"Karibu sana bosi mimi naitwa Faheed nilitumwa na mkuu mwaka mmoja uliopita kufanya utafiti wa eneo lote la Afrika Mashariki na kuandaa mazingira kwa ajili ya oparesheni yetu maalum" alikaa kimya kupisha utambulisho wa wenzake
"Naitwa Rashid ni mjumbe kutoka Al Shabaab nipo hapa kufanikisha oparesheni inakamilika" alijitambulisha mtu mwingine
"Naitwa Akram ni mtu wa mahusiano na serikali za Afrika Mashariki"
Utambulisho uliendelea na hatimaye kila mmoja alijitambulisha na kisha bwana Faheed alisimama na kisha alianza kuongea tena
"Naomba nitoe ripoti ya tulipoanzia mpaka hapa" alisema Faheed
"Sawa" Aaron alimjibu
"Oparesheni ilianza mwaka 2007 baada ya mkuu kutupa maelekezo juu ya oparesheni hiyo hivyo utafiti ulifanyika eneo lote la Afrika Mashariki na pia watu muhimu kwenye oparesheni hii tulijumuishwa kwa pamoja kwenye timu hii ambao tupo hapa mbele yako....mpaka sasa tumefanikiwa kuanzisha kambi ndogo pembeni mwa msitu wa Arbedare Kenya ambayo ipo chini ya ndugu Rashid pia tumeweza kwa kiasi kujenga mtandao ndani ya serikali ya Kenya na pia kwa kiasi kidogo sana nchini Tanzania na Uganda kwa msaada wa ndugu Akram" Faheed aliweka kituo na kuendelea
"Hiyo ni ripoti kwa ufupi mengi zaidi yapo ndani ya mafaili unaweza kupitia ukipata mda.....mkuu Abd al-Uzza alituambia tuishie hapo tulipofikia mpaka mkuu wa oparesheni atakapofika rasmi ndiye atatoa jina la kundi hilo linaloanza Afrika mashariki pamoja na kupanga mikakati kwa ajili ya oparesheni hiyo" Faheed alimaliza na kuketi chini
Ukimya mfupi ulipita kisha Aaron alianza kuongea
"Niwapongeze kwa kazi kubwa mliyofanya na jitihada kubwa za kupambania haki ulimwenguni" kisha aliweka kituo na mara wazo lilipita kichwani mwake 'freedom fighters' maneno yale yalipita kwenye akili zake na kisha akaendelea kuzungumza
"Nianze kwa kulitambua rasmi kundi letu la kupambania haki na uhuru wa wanadamu wote dhidi ya madhalimu, litaitwa 'maharib alhuriya' (wapambania uhuru)" alisema Aaron na kisha wote walipiga makofi na kutulia
"Ndugu Rashid utaendelea kuisimamia kambi hiyo ambayo nimeshaitambulisha rasmi na wengine tunaendelea kupeana majukumu kadri mda unavyozidi kwenda.....nafunga kikao hiki mpaka nitakapowaita tena kwa kupanga mikakati yetu"
"Sawa mkuu" wote walikubali na kuanza kuondoka mahali hapo baada ya Aaron kuondoka
"Hivi mkuu siku zote aliwaza nini kutuletea katoto katuongoze kwenye oparesheni muhimu kama hii?" Alikuwa ni Faheed akimuuliza mwenzake mmoja
"Hata sijui, sisi sote tuna uzoefu wa kutosha wa mambo haya kwanini basi asiteue mmoja wetu mpaka afuate hichi kitoto ambacho bado kinanuka maziwa?" mwenzake na yeye aliuliza kwa mshangao, kiuhalisia hakuna aliyejua maana ya jambo hilo isipokuwa bwana Abd al-Uzza mwenyewe
Kila mmoja aliingia kwenye gari yake na kuondoka kwenye jumba hilo ambalo lilikuwa ni makazi ya Aaron na ofisi yake pia aliyopewa na bwana Abd kwa oparesheni hiyo maalum
ITAENDELEA USIKOSE SEHEMU IJAYO.............
