Ngoma Ngumu 09

RIWAYA; NGOMA NGUMU.

NA; BAHATI K MWAMBA.

SIMU; 0758573660/0624155629.




 SEHEMU YA TISA..

Safari ilichukua zaidi ya dakika kumi na tano hadi walipofika mitaa ya Riverside. Mitaa ambayo ilikuwa imezingirwa na ukimya mkubwa huku nyumba za wenyeji zikiwa zimezungukwa kwa kuta na mageti mazito, yasiyotoa nafasi kwa watu wengine kujua kinachoendelea ndani ya nyumba zao. 

Gari la Mensa Munga ambae alikuwa ni Kaimu Meneja wa benki ya umoja, liliingia kwenye nyumba moja, ambayo ilikuwa imezungukwa na miti mingi huku ukuta mrefu ukiwa umemeza mwonekano wa nyumba yake. Geti lilifunguliwa na mlinzi mwenye bunduki alitokeza. Alitizama ndani ya gari kisha aliruhusu gari kuingia na yeye akifunga geti na kufanya iwe siri kuona kilichokuwa kinaendelea huko ndani.

Miguu ya kuku aliyaona yote akiwa anatembeza gari kwa mwendo wa taratibu kwenye barabara pweke, isiyo na hekaheka nyingi. Alipitiliza kama vile hakuwa anashida na maeneo hayo. Aliongeza mwendo kidogo na alipofika umbali kutoka ilipokuwa nyumba ya Mensa, aliamua kugeuza na kurudi alipotokea. 

Wakati gari yake ikikaribia kufika usawa nyumba ya Kaimu Meneja ambayo ilikuwa pembezoni mwa barabara, aliweza kuona gari dogo likienda kusimama getini na mtu aliyekuwa upande wa dereva alishuka na kwenda getini. Kilichonvutia kwa mtu yule ni kuwa akimfahamu na uwepo wake pale, ilikuwa ni ishara kwamba kuna kitu kilikuwa kinaendelea. 

Miguu ya kuku alimuona Sajini Nyau, getini kwa Mensa Munga.

“Huyu bwege amefuata nini hapa?” Alijiuliza huku akiongeza kasi kutoka kwenye eneo lile, kuna sehemu alikuwa anawahi kabla ya giza kuingia. Hivyo hakuhitaji kupotezewa muda wake na Sajini Nyau.

“Ngoja nivujishe mpango wangu!” Alisema huku akichukua simu yake na kumpigia Susa. 

“Upo wapi saivi?” Aliuliza baada ya simu yake kupokelewa.

“Niko Kisii, najiandaa kwenda kuonana na Sajini.”

“Good! Sasa nataka unisikilize kwa umakini mkubwa.” Alisema huku akipunguza mwendo wa gari ili azungumze kwa uhuru.

“Huyo mtu nataka tumtumie kuiba Benki!

“Benki? How!” Susa aliuliza kwa mshangao mkubwa.

“Nitakwambia baadae. Kwa sasa ni hivyo kwa hiyo kama utaweza, naomba uanze kumdodosa kuhusu namna wanavyopanga ulinzi wa mabenki kila ahsubuhi.”

“Kwani unataka kupiga tukio benki gani?”

“Nitakwambia wakati mwingine, kwa sasa nichukulie hizo taarifa.”

“Lakini yeye ni ofisa wa kawaida na benki huwa wanalinda KFFU. Hapo itakuwaje?

“Hivi wewe si mwanamke?” Zuki alimuuliza.

“Ndiyo!”

“Na mara nyingi vigogo hukutumia kama chambo kuwapata wabaya wao siyo?” 

“Ndiyo!”

“Basi hushindwi kumfanya Nyau akavuna taarifa za KFFU na kukupa wewe. Nakulipa utumike kwa akili na mwili. Kama pesa haitoshi, sema niongeze!”

“Hapana usinielewe vibaya. Huwa nimekuuliza nikiwa na sababu zangu, ila usijali kila kitu kitakuwa sawia kabisa.” 

“Nafurahi kusikia hivyo!” Miguu ya kuku alisema na kukata simu, huku akitabasamu kivivu.

“Yaani huyu mtoto ananiona mi bwege sana? Ngoja ainjoi shoo!” Alijisemea huku akikamata vema usukukani wa kuongeza mwenda. Alitaka kuwahi kwenye ofisi za Jatu kabla ya saa moja jioni, kuna kitu alihitaji kufanya. Wakati huo zilikuwa zimesalia dakika ishirini kabla ya kufika saa moja kamili na kwa kupitia maelekezo aliyokuwa amesoma kuhusu ofisi za Jatu, alijua itamchukua dakika kumi na tano kufika hapo ofisini.

                       ****

 Alipokaribia ofisi za Jatu, alijipapasa kwenye mfuko wake wa suruali na kuushika mkasi mdogo. Alipohakikisha mkasi wake umekaa vema mfukoni, alitafuta sehemu na kuegesha gari lake kisha alianza kutembea kwa miguu kuelekea zilipo ofisi hizo.

 Alitumia dakika tano kufika zilipo ofisi, alitizama getini na kuona zilikuwa wazi na kulikuwa na mlinzi mmoja akirandaranda huku na huko na bunduki yake mkononi. Taratibu alijongea getini na kukutana na mlinzi mmoja wa mapokezi.

“Nina shida na maneja wa hapa.” Alijibu baada ya kuulizwa shida yake.

“Anajua uwepo wako hapa?” Mlinzi aliuliza.

“Hapana, imekuwa ghafla sana. Sijatoa taarifa ya ujio wangu.” 

“Sawa, saini hapa na utapewa maelekezo yote pale mapokezi.”

“Ahsante sana.” Zuki alisema huku akisaini kwenye kitabu cha wageni, akiwa amejitambulisha kwa jina la Somba Bhaku. 

 Alipomaliza kusaini aliruhusiwa kuingia ndani ya ofisi. Alipofika mapokezi alieleza shida yake, ambapo aliambiwa kwa shida yake si lazima kuonana na meneja, bali anatakiwa kulipia mapokezi na kisha ataongozana na fundi mkuu ili kutatua changamoto yake, kupitia mifumo ya kompyuta iliyoko pale ofisini na kama tatizo litakuwa kubwa zaidi, basi atatakiwa kuongozana na mafundi watatu ili kutatua changamoto yake huko ofisini kwake. Yaani waende ofisini kwa Zuki Gadu, ambae alijitambulisha kama Somba Bhaku.

Baada ya kujaza taarifa fulani kwenye fomu ya malipo, alitoa kadi ya benki na kufanya malipo. Kisha alipewa risiti na kuelekezwa kwenye ofisi za fundi mkuu wa mifumo ya kompyuta. 

 Kitu kimoja ambacho mtu wa mapokezi hakuwa na umakini nacho, ni jina la kadi iliyotumika kufanya malipo. Kadi ile haikuwa na jina la Somba, bali ilikuwa na jina la Fransis Mkorofi, ambae alikuwa ni raia wa Malawi. Na kadi hiyo ilimilikiwa kihalali kabisa na Miguu ya kuku na nyingi huitumia nyakati kama hizo, huku silaha yake kubwa ikiwa ni ulimi wake na namna ya kuwafanya wahudumu wapoteze umakini hasa wahudumu wa kike. 

Kadi hiyo ni miongoni mwa kadi nyingi anazomiliki kwa kutumia majina tofautitofauti na uraia tofauti. Lakini namna alivyopata kadi hizo, ilibaki kuwa siri yake na kamwe hajawahi kujisahau na kumsimulia mtu namna anavyofanikishaga ulaghai wake.

Miguu ya kuku aliongozwa kuingia ndani ya ofisi za fundi mkuu. Aliingia ndani akiwa hana wasiwasi wowote ule. 

Ofisini alikutana na sura ambayo alitoka kuiona saa chache zilizopita, ikiingia ndani ya Benki ya umoja. Alijipongeza kwa kuwaza kuingia kwenye ile ofisi na lengo lake lilikuwa ni kukutana na mmoja wa mafundi waliotembelea ile benki jioni hiyo, baada ya yeye kuacha kizaazaa.

Alikaribishwa kwa ukarimu na yule fundi, ambae macho yake yalionesha ujanjaujanja mwingi.

“Hii ofisi ni ya wana usalama.” Aliwaza huku akimtizama yule jamaa kwa jicho la udadisi mkubwa.

banner

Alihisi ile ni ofisi ya kimkakati ya usalama wa nchi, ili kujua ofisi nyingi zinajiendeshaje kwa kupitia kwenye mifumo ya kompyuta zao. Na aliamini hivyo baada ya kuwaona wao ndiyo waliopewa kazi ya kurekebisha mfumo wa benki ya Umoja. 

“Hii ni zaidi ya ofisi!” Aliwaza huku akijiweka sawa kwenye kiti alichokuwa amekalia. Hakutaka kuendelea kupoteza muda huku akijua yupo sehemu ambayo si salama kwake.  

“Nakusikiliza ndugu Somba Bhaku!” Jamaa aliongea huku akifumbata mikono yake na kumtazama kwa udadisi mkubwa.

Hila za macho ya fundi zilijaa vema kwenye ubongo wa Zuki Gadu, lakini alitaka kutumia udhaifu mdogo kumteka yule jamaa na kumtapisha kile alichokuwa anakihitaji.

“Aah, jioni hii ni kama nimekuona pale Umoja Benki. Ama mwafanana tu.” Zuki alianza kumjaza umakini yule bwana. Aliamini wakati mtu akiwa kwenye udadisi mkubwa, ni wakati huo ambao hupoteza nguvu ya uamuzi wa haraka. Hivyo alitaka yule bwana azame kumdadisi kisha yeye apasue yai kwa kidole kimoja.

“Wewe hapo Benki ulinionaje bwana Somba?” Yule jamaa aliuliza huku akikaa vema kwenye kiti chake na kumkazia macho mgeni wake.

“Aah nilikuwa nina shida zangu pale, tukaambiwa mashine ya fedha ni mbovu, sasa wakati unatoka ndipo niliona ukiwa umeongozana na Meneja.” Zuki alijibu huku akijichekesha.

“Wewe ulijuaje yule ni Meneja? Kwani unafahamiana nae?” Fundi aliendelea kuuliza maswali ya msingi sana ambayo hakujua alitegwa kuyauliza, bila yeye kujua na hiyo ilikuwa inampa majibu Zuki Gadu ya kuwa ile ni zaidi ya ofisi ya kawaida.

“Kwani Meneja huwa anajificha?” Zuki nae aliamua kuuliza huku akianza kupiga hesabu namna ya kumvamia yule jamaa.

“Hajifichi, lakini si lazima kila mteja amfahamu.” Jamaa alijibu huku macho yake yakiwa hayabanduki usoni mwa Zuki Gadu.

“Ooh basi tuachane na Meneja, naomba unitatulie shida yangu.” 

“Ooh! Lakini si vibaya tukijadili kilichokuwa kinaendelea pale Benki, unajua kimeathiri sana shughuli za leo!” Fundi alijitia kutaka kuendeleza ile mada huku akijiweka tayari kwenye kiti.

“Athari zipo, ikiwemo mimi kukosa pesa na kumuona Meneja!” Zuki alisema huku akiinuka kwenye kiti kitendo kilichomfanya fundi aondoe umakini na kumtazama huku akiwa hajaelewa vema kilichokuwa kimesemwa na mgeni wake. 

“Mbona unasimama bwana Somba!” Fundi alisema huku akijaribu kumtazama mgeni wake ambae alikuwa amesimama na kuanza kusogea mlangoni, jambo lililomfanya fundi ainuke kwa lengo la kumzuia mgeni wake wa ajabu. Mgeni ambae amelipia huduma lakini, anaondoka bila kueleza shida yake. 

 Fundi hakujua kama anajiingiza mtegoni. Na laiti kama angeligundua hila za mgeni wake, hakika angelibaki amekaa au angelitumia njia nyingine na si ile ya kunyanyuka na kutaka kutoka kwenye kiti ili awahi kumzuia mgeni wake. 


ITAENDELEA.

Jaba Zulma

Siyumbi

Your Thoughts

Previous Post Next Post

Contact Form