PENDO LANGU KWAKO

Emmanuel Lee
By -
0

 

PENDO LANGU KWAKO



Uketi chini mpenzi,ya moyoni nikwambie,
Daima nitakuenzi, uhai uniishie,
Hutoipata simanzi, nataka ufurahie,
Pendo langu kwako wewe, halipimwi Kwa mizani,


Halipimwi Kwa mizani, uzitowe wazidia,
Pendo linayo thamani, hakuna cha kufikia,
Hata Kwa mizani gani, huwezi kulipimia,
Pendo langu kwako wewe, hutolikuta dukani,


Hutolikuta dukani, ati labda lauzwa,
Pendo li ndani moyoni, kwalo pendo nimemezwa,
Kwani halina kifani, Kwa kitu likaigizwa,
Pendo langu kwako wewe, Kwa mwingine hulikuti,


Kwa mwingine hulikuti, pendo akakupatia,
Nina pendo lenye dhati, la moyo uloridhia,
Pendo liso na wakati, daima kufurahia,
Pendo langu kwako wewe, linang’aa kama nyota,


Linang’aa kama nyota, maishani Kwa nuru,
Pendo Raha kulipata, kufaidi Kwa Uhuru,
Pendo chozi kunifuta, Kwa nini nisishukuru,
Pendo langu kwako wewe, liishi zote dawamu,


Waache waone wivu, Kwa pendo ninalokupa,
Sisi tule zetu mbivu, Kwa pendo ninalokupa,
Kwako niwe msikivu, sitoweza kukutupa,
Pendo langu kwako wewe, lizidi shamiri.


NA: Emmanuel Charo

©2018


 

 

 

 

Post a Comment

0Comments

Your Thoughts

Post a Comment (0)