WAKILI WA MOYO 05


HADITHI: WAKILI WA MOYO 05

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

SIMU: +255713 646500


ILIPOISHIA:

“Siamini maumivu ninayosikia juu ya mpenzi wangu kuwekwa ndani na kubambikiwa kesi nzito halafu familia yake inasema eti nimefurahi! Mimi Mage nifurahi kufungwa kwa mpenzi wangu?” Mage alimuuliza mama yake huku akibubujikwa na machozi ya uchungu.

SASA ENDELEA...


“Nani amekuambia hivyo?”

“Mama Hans.”

“Unaona mwanangu ile siyo familia badala ya kukuonea huruma ndiyo kwanza wanakulaumu, ufanye vile ili iweje ungeweza kuvuruga ndio yako kama mtu humpendi.”

“Mama nakuapia Hans akinioa sitaki kuwaona ndugu wa mume.”

“Mage mwanangu hayo siyo maneno, bado tunataka kuonesha upendo kwa wenzetu kipindi hiki kigumu.”

“Mama wakati Hans yupo ndani nataka kuzungumza na Colin naamini ananipenda sana.”

“Ukiisha zungumza naye?”

“Ili nikamate huku na huku kama Hans atafungwa basi niwe na Colin.”

“Na Hans akitoka gerezani na kukuta umeolewa?”

“Nitajua, nina imani Colin nammudu, nitamweleza ukweli kuwa kwake nilikuwa najiegesha na nimpendaye karudi. Mbona anajua kuwa kwa Hans nimekufa nimeoza.”

“Mage kumbuka ukianzisha uhusiano na Colin mpaka kufikia kufunga ndoa lazima watu watasema umehusika kumfunga mpenzi wako hapo ndipo utaongeza uhasama na familia ya kina Hans.”

“Nitafanya kwa siri.”

“Colin akitaka kukuoa?”

“Nitamvuta kwa muda ili kumsubiri Hans, kama anafungwa maisha sina jinsi kama miaka saba nitajishikiza kwa Colin.”

“Ulivyomuacha atakukubali kweli, ha..ha..lafu leo kaingia na msichana mrembo ni nani yake?”

“Mpenzi wa rafiki yake,” Mage aliongopa.

“Mmh! Ili kutengeneza mazingira mazuri unatakiwa kujipendekeza kwa mama Colin.”

“Nitafanya hivyo, najua yule mama ananipenda sana nikimfuata na kumweleza nimerudi kwa mwanaye nina imani atapiga vigelegele.”

“Mmh! Haya.”

Mage aliachana na mama yake na kwenda chumbani huku mawazo yake yote yakiwa kwa Colin kutokana na kuujua ukweli wa kesi ya Hans kwa kuamini kutoka kutakuwa muujiza. Alipanga kuanza kujipendekeza kwa familia ya kina Colin wakati akisubiri hukumu ya mpenzi wake.

                                                            ****

Colin alimpeleka Cecy chuo cha urembo ambako alisoma kwa miezi mitatu, muda wote walikuwa kama kumbikumbi kila mmoja alionesha mahaba mazito. Taarifa ya kukamatwa mchumba wa Mage iliwafikia na kushagaa taarifa ya kukamatwa kwake kuwa alihusika na kifo cha mkewe na mwanaye ili tu amuoe Mage.

“Colin yaani naomba kama mama yako atasababisha tutengane usifanye kama mpenzi wa Mage alivyofanya. Heshimu uhai wa mtu, kama ipoipo tu, Mungu ana maajabu yake ameweza kutukutanisha pamoja bila sisi wenyewe kujua. Kwa hivyo ni makosa kulazimisha kitu.”

“Cecy kila dakika nakuwa mwanafunzi wako, wewe ni zaidi ya mwanamke pamoja na umri mdogo lakini Mungu amekupa busara na hekima.”

“Kama ni kweli mpenzi wa Mage anahusika kutenda unyama ule  kwa ajili ya Mage atakuwa ametenda dhambi kubwa sana.”

“Mi’ siamini mtu anaweza kumuua mke na mwanaye kwa ajili ya mpenzi wake.”

“Kwa hiyo ungemuoa Mage, mimi ningekuwa na nafasi gani moyoni mwako?” Cecy alimuuliza swali la kizushi.

“Cecy tuachane na hayo, unakumbuka wiki ijayo ndiyo onesho lako la kwanza la mavazi, mazoezi yako yamenipa matumaini ya kuishtua dunia.”

“Mmh! Nitafunikaje maana nguo zote nilizojipima hadi mwenyewe najione wivu, si vibaya kujisifia mi’ mzuri bwana.”

”Siyo mzuri bali  mrembo,” Colin alimrekebisha.

“Bwana eeh, urembo unatengenezwa lakini uzuri ni wa asili.”

“Sawa mama umeshinda.”

Wiki moja baadaye liliandaliwa onesho la kwanza la mavazi la kampuni ya Colin litakalo ongozwa na Cecy. Matangazo yalirushwa mwezi mzima katika vyombo vyote vya habari na kufanya watu wengi wavutike na kuapa kutolikosa. Miongoni mwa watu walipanga kwenda kwenye onesho hilo la kwanza la kimataifa alikuwa ni Mage na shoga yake Brenda.

Washiriki walikuwa wengi kutoka ndani na nje ya nchi na kufanya onesho lile lizidi kuvutia watu wengi. Siku ya onesho ilipowadia Mage na shoga yake Brenda walikuwa miongoni ma watu waliohudhulia onesho hilo lililojaza watu wengi. Muda ulipofika maonesho yalianza  kwa kuanza kupita wageni ambao walionesha mavazi ya kigeni na kuwafanya watu walipuke mayowe.

Baada ya kumaliza wageni lilianza vazi la Kitanzania kuanzia vazi la vitenge,  khanga na vikoi.Walianza kutangulia mabinti ambao nao walikuwa katika kampuni hiyo. Baada ya kupita wote ikafika kipindi akatokea Cecy katika vazi la kitenge chenye kilemba kirefu na kufanya ukumbi ulipuke mayowe.

Alipita na mavai zaidi ya kumi ya ubunifu na kuacha historia kwenye onesho lile.

 “Mage huyu si yule msichana aliyeingia na Colin siku ya Send of yako?” Brenda aliuliza baada ya kumfananisha Cecy.

“Ndiye yeye.”

“Mage tuache utani msichana huyu mzuri tena ana uzuri wa asili,” Brenda alimsifia Cecy.

“Hana lolote uzuri upo wapi?” Mage aliponda.

”Wivu huo, kwenye ukweli uongo hujitenga, yule msichana mzuri.”

“Brenda tutakorofishana tumekuja kuangalia mavazi au kuja kumsifia mtu, kwanza mavazi aliyovaa ya kishamba nani sasa hivi anavaa mavazi ya khanga na kitenge. Angejua wala hakupendeza lolote,’ Mage alimbeza Cecy.

“Mageee! Siamini kama una nafasi katika moyo wa Colin, kitu kama hiki hata mimi nikimuona yupo  na mpenzi wangu lazima nipate presha,” Brenda alizidi kumuumiza roho shoga yake. 

“Brenda naona umetumwa kuja kuniumiza roho, kosa langu kuja na wewe pamoja?” Mage alikuja juu.

“Lakini Mage kwani nikimsifia yule mwanamke kuna ubaya gani ikiwa wewe ni mchumba wa mtu na Colin si mtu wako?”

“Unajuaje kama nitarudiana na Colin.”

“Mrudiane kivipi ikiwa wewe utaolewa na Hans na Colin anaweza kumuoa huyo msichana.”

Wakiwa katikati ya onesho Colin ambaye alifahamika kama mkurugenzi wa kampuni ile ya urembo na mavazi alifuatwa na watu wenye majarida ya urembo kumtaka Cecy kwa ajili ya kuyapamba majarida yao kwa sura yake kwa mkataba mnono. Pia makampuni mengine ya Afrika ya kusini na Ufaransa ambao walikuwa wageni waalikwa walivutiwa Cecy na kuomba kufanya naye kazi kwa mkataba mnono.

Nyota ya Cecy ilizidi kung’aa, Colin aliwakubalia lakini walitakiwa waonane kesho kwa ajili ya mazungumzo zaidi, walikubaliana. Siku ile pia ilikuwa maalumu kwa Colin. Wakati burudani ikiendelea Mc alisimamisha kwa ili mkurugenzi aseme neno.

Colin alichukua kipaza sauti na kuwasalimia wote kisha alisema:

“Ndugu zangu kwanza nashukuru kwa muitikio katika onesho la leo ambalo limekuwa na mafanikio makubwa tofauti na nilivyofikiria. Mpaka sasa tumepata naombi ya kumtaka Malkia Cecy kupamba majarida na pia kwenda kufanya maonesho Afrika ya kusini Marekani na Ufaransa,” kauli ile ilifanya ukumbi ulipuke kwa mayowe. 

“Lakini hilo silo lililonifanya nimnyang’anye kipaza sauti Mc, nia yangu nilikuwa nimeweka ahadi  moyoni mwangu siku ya leo nifanye kitu gani. Naomba nimwite malkia wa usiku wa leo Cecilia hapa mbele.”

Cecy alitoka chumba maalumu akiwa na gauni refu jekundu lililokuwa likiburuza kwa nyuma, lililokuwa limempendeza sana kama bi harusi.

“Ndugu zangu, wazazi wangu na wageni waalikwa katika onesho hili la kwanza la kimataifa. Leo ndiyo namtambulisha kwenu wakili wa moyo wangu binti mrembo Cecy kuwa ndiye mke wangu mtarajiwa,” ukumbi ulilipuka tena kwa mayowe.

Colin aliendelea kwa kujipapasa na kutoa mkebe mdogo na kusema:

“Cecy mpenzi fumba macho,” Cecy alifanya vile.

Colin alitoka pete ya tanzanite iliyochanganywa na almasi na kukishika kidole cha Cecy na kumvisha na kufanya ukumbi wote kulipuka kwa mayowe kila mtu akisema kuwa kila mmoja kampata mwenzake.

Lile lilikuwa pigo mujarabu kwa Mage aliyekuwa na ndoto za kurudi kwa Colin kama Hans atafungwa.

Mapigo ya moyo yalianza kumwenda mbio na jasho kumtoka kwa wingi, kizungumzungu kikali kilimshika na kiza kinene kilitanda mbele yake na kumfanya adondoke alipokuwa amekaa. 

Alichukuliwa haraka kwenda kupewa huduma ya kwanza kwa vile pale ukumbuni kulikuwa na kila kitu.

Shughuli ilendelea kwa Mc kulitangaza vazi jipya la wachumba siku ya kuvishana pete lililompendeza vilivyo Cecy. Baada ya onesho yale Colin alijiandaa kuingia mkataba mnono wa Cecy na hayo makampuni. 

                                                  ***

Cecy aliingia mkataba wa mamilioni ya fedha ya miaka miwili  kwa  makampuni mawili ya majarida makubwa Marekani moja la Vibe  na Ebony kwa ajili ya kupamba ukurasa wa mbele pia aliingia mkataba mnono wa kampuni ya maonesho ya mavazi ya Ufaransa ambayo yabadili maisha ya Cecy toka umaskini wa kutupa mpaka msichana bilionea.

Baada ya kuingia mkataba mnono uliomtaka aanze kazi hiyo mwezi mmoja baadaye kwa ajili ya mazoezi ya mwezi mmoja na kujifunza lugha vizuri kabla ya kuianza kazi hiyo mara moja. Cecy aliomba kuzungumza kwanza na familia yake pamoja na mpenzi wake Colin ili ajue ataanza lini kazi yake, walikubalia na kumpa siku mbili za kutoa jibu ili wakiondoka wajipange vipi.

Ilikuwa tofauti na mapokeo ya Cecy baada ya kulala maskini na kuamka tajiri mkubwa. Ndoto yake ilikuwa kuolewa na Colin na si kufanya kazi ya mabilioni, alijiuliza kukaa miaka mwili nje ya nchi lazima Colin atatafuta mwanamke mwingine na yeye kupoteza kitu muhimu maisha zaidi ya fedha atakazolipwa katika kazi yake.

  Kwake alichokitafuta kilikuwa kuwa karibu na Colin na kufanikiwa kuwa naye karibu na kubakia kitu kimoja ndoa ambayo aliiota siku zote. Baada ya kuachana wa wenye makampuni toka nchini za nje. Cecy alionekana mtu mwenye mawazo tofauti na kitu alichokipata cha kugeuka bilionea kwa kufanya  onesho lake  moja na kuonekana.

Baada ya kufika nyumbani ilibidi amuulize:

“Vipi mpenzi wangu  mbona kama hauna furaha wakati leo umeuaga umaskini?”

“Mi kwangu naona kama ndiyo unataka kuniongezea umaskini,” Cecy alijibu kinyonge.

“Kivipi?”

“Hivi nikiwa huko tutakuwa pamoja?”

“Hapana ila tutaonana mara chache kwa vile utakuwa bize na kazi yako ya kuizunguka dunia kufanya maonesho.”

“Uoni kama nitakuwa nimepata fedha zisizo na faida kwangu.”

“Kivipi?”

“Colin wewe ni kila kitu kwangu, niliapa kuwa mbali na wewe ni pale mmoja wetu akichukuliwa na umauti na si  vinginevyo.”

“Hilo tu, nitakuwa naonana na wewe kila mara wala usihofu.”

“Colin nina wasiwasi nikiwa mbali kuna vipanga watu watakunyakuwa na mimi kuichukia dunia, kukupata nimetoka jasho la damu. Furaha yangu ni kuwa karibu yako na si kuingiza mamilio ya fedha.”

“Najua mpenzi unanipenda lakini hili dili ni zaidi ya mapenzi kwa vile litayabadilisha maisha yako sasa hivi una uwezo wa kujenga gharofa Masaki au Kunduchi.”

“Colin mimi huko siendi na hizo hela zao sizitaki.”

“Usifanye hivyo, ukilipoteza hutakuja kujuta maisha yako yote.”

“Moyo wangu naujua hauna shida ya mabilioni ya watu bali upendo toka kwako, pia naona umekwenda kinyume na makubaliano yetu.”

“Kivipi mpenzi?”

“Ulisema unataka kunifungulia kampuni ili niwe nafanya maonesho na si kwenda kufanya kazi nje ya nchi.”

“Mpenzi, yaani dili ulilopata fedha utakayoipata kwa miaka yote hiyo  unaweza kukaa bila kufanya kazi na kuishi maisha ya juu.”

“Sina maana hiyo, uliniahidi baada ya kumaliza masomo unanioa sasa ahadi yetu ipo wapi? Au ndiyo unanitoa kijanja urudiane na Mage baada ya mpenzi wake kufungwa?” Cecy alilia wivu.

“Ahadi yetu ipo palepale, we fanya kazi mwaka mmoja kisha tunafunga ndoa ndipo nitajua nitafanya nini.”

“Cecy mpenzi hujui tu kiasi gani cha fedha utakacholipwa, ni wasichana wachache dunia wenye bahati hii. Tukitaka tufanye harusi itachukua muda wakati mwezi ujao unatakiwa Afrika ya Kusini kwa mazoezi ya wiki mbili kabla ya kwenda Ufaransa. Kutokana na makubaliano picha za jarida la Ebony watatumia za kwenye onesho na zile walizokupiga siku ile. Malipo yako ya kwanza yataingia mwezi ujao ya dola elfu  mia mbili arobaini(408,000,000)  kwa mwaka. Baada ya mwaka malipo yataongezeka na kuwa dola elfu mia tatu (510,000,000). Pia utapata bonas ya asilimia tano kutokana na mauzo huoni kwa miaka miwili utakuwa mbali mpenzi wangu kwa kutengeneza dola elfu mia tano arobaini (918,000,000).

Bado kampuni ya maonesho itakulipa dola elfu mia tatu (510,000,000)  kwa mwaka na bonasi kila onesho la nchi kubwa barani Ulaya na Amerika. Unataka nini tena mpenzi wangu, kipindi hiki hebu ndoa iweke pembeni tupige pesa.”

“Colin nakuona kama unampigia mbuzi gitaa, nakueleza kwa mara ya mwisho pesa inaweza kununua kitu chochote chini ya jua lakini si furaha ya moyo wa mtu dawa ya mtu ni mtu si kitu.”

“Mmh! Sasa wewe ulikuiwa unatakaje?”

“Kwanza tuoane kisha tutajua kama kwenda au kufanyia kazi hapa lakini si kukaa mbali na wewe.”

Ulikuwa mtihani mzito kwa Colin kutokana na msimamno wa mpenzi na kuliona kama dili lile litapeperuka kwani walikuwa wapo wapo nchini wakisubiri kauli yao ataanza lini kufanya kazi. Lakini kwa Cecy alikuwa haelewi kitu bado ya kutetea ndoa yake pia kuwa karibu na mpenzi wake kwa kuogopa vibaka vya wapenzi wa watu.



Jioni ya siku ile Colin alikutana na mama Cecy na kumuelezea hatua waliyofikia na uamuzi wa Cecy.

“Mama nilikuwa naomba umweleze mwenzangu akubali kwanza kwenda kufanya kazi ndoa itafuata baadaye.”

“Mmh! Nitajaribu kumweleza, nina imani atanielewa.”

“Yaani nitashukuru sana, sijawahi kuona mwanamke mwenye msimamo kama Cecy.”

Kwa vile Cecy alikuwa amekwenda kuoga aliporudi alikaa pembeni ya mama yake na kumuacha Colin aliyekuwa amekaa kochi la peke yake. Baada ya ukimya mfupi mama Cecy aliuvunja ukimya ule.

“Cecy mama.”

“Abee mama.”

“Nina imani leo Mungu atuangazia maisha yetu?”

“Ni kweli mama, lakini maisha hayatakuwa na furaha bila kutimiza ndoto yangu.”

“Najua una hamu ya kutimiza ndoto yako, lakini kilichotokea ni muhimu kwa wakati huu ndoa yako ipo palepale.”

“Hilo nalijua, siku zote fimbo ya mbali haiuwi nyoka, kama nitaanza kazi naweza kukaa hata miezi mitatu bila kumuona Colin na wakati penzi langu limenitoa jasho la damu. Naweza kupata fedha lakini nikapata jeraha lisilopona mpaka nakufa na pengine likawa ndio sababu ya kifo changu.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Mama kama unavyojua mchumba wa Mage yupo ndani na kesi yake ni nzito, kwa habari za juujuu kweli anahusika katika vifo vya mkewe na mwanaye ili arudiane na Mage. Kwa hiyo uwezekano wa kutoka ni mdogo huoni muda huo nikiwa mbali na Colin penzi linaweza kuzaliwa upya na nafasi yangu kupotea.

“Kama nilijitoa kwa ajili ya Colin ifike wakati nimkose hizo fedha zitakuwa na faida gani kwangu. Nipo tayari kupoteza hata fedha zilizojaa bahari lakini si kumpoteza Colin, moyo wangu ndiyo unaojua thamani yake si yeyote. Mama hujui kiasi gani niliumia niliposikia Colin akioa lakini machozi yangu hayakwenda bure, Mungu alisikia kilio changu na kunirudishia mpenzi wangu mikononi mwangu na kuamini haki ya mtu huwa haipotei bali hucheleweshwa.”

“Sasa kama unafahamu hivyo kwa nini una wasiwasi na  Mage?”

“Mama, Golden chance never came twise.”

“Hapo umeniacha feri una maanisha nini?” 

“Kwangu hii ni nafasi ya dhahabu kamwe haijirudii mara mbili.”

“Cecy nakuahidi wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu, nilivyofahamu thamani yako ndani ya moyo wangu upengo wangu uliongezeka mara dufu. Cecy wewe ndiye wakili wa moyo wangu uliyenitetea wakati wa matatizo hakuahidi sitamfungulia mwanamke mwingine moyo wangu nilipokufungia moyoni mwangu ufunguo niliutupa baharini,” Colin alimuhakikishia  mapenzi yake ya dhati kwake.

“Colin ufunguo kuutupa baharini ni usemi tu lakini mnasahau ufunguo unaweza kumezwa na samaki na kuurudisha watu wakauokota na kuufunguo moyo wako na mimi ukanitoa moyoni mwako. Colin unanipenda?” Cecy alimuuliza Colin huku amemkazia macho.

“Zaidi ya sana na kama kuna kauli nyingine zaidi ya hiyo ungeijua ningeisema mbele yako.”

“Naomba unioe.”

“Nitakuoa kwa vile wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu.”

“Si kwa wakati mnaotaka ninyi bali kabla ya kuanza kazi  yangu nataka nikisimama sehemu nijulikane kama mrs Colin na si miss Cecy.”

“Muda tuliopewa ni mdogo sana wa maandalizi ya harusi, hivyo ungekwenda kufanya kwanza kazi  kisha ukirudi tutafunga ndoa utakuta maandalizi tayari ukifika tunafunga ndoa na kuondoka.”

“Kwani kazi si naanza mwezi unaokuja huu muda hatuwezi kufunga ndoa?”

“Cecy wewe sasa si Cecy muuza ndizi bali wa kimataifa kwani wiki ijayo sura yako inaruka dunia nzima kwenye Jariba la Ebony harusi yako haitakiwi ya kulipua bali iendane na wewe mwenyewe.”

“Mimi Cecy hata niwe vipi bado nitabakia Cecy muuza ndizi, kwa hiyo kama mna nia nifanye kazi tufunge ndoa ya kawaida ila sherehe nikirudi zaidi ya hapo kazi yenyewe siitaki na msiambie kitu kinachohusu hiyo kazi. Fedha inatafutwa kwa njia yoyote lakini upendo kwa kweli ni adimu kama maji jangwani.

“Naweza kumsifu Mage kwa kuvunja uchumba wetu si kwanza nimepata nafasi bali amezieleza hisia zake za kweli toka moyoni kwake kuwa kuna mtu aliyekuwa akipenda kwa dhati. Kosa walilofanya kuua viumbe wasio na hatia lakini walikuwa wapo sahihi kabisa. Kama mliona Mage yupo radhi kulaaniwa na dunia kwa ajili ya mapenzi basi na mimi nipo tayari kufa maskini kwa ajili ya mapenzi,” Cecy alisema kwa sauti kavu isiyo na mzaha hata kidogo.

“Mmh! Mwanangu Colin mpaka hapo mimi sina neno siku zote mwenye kujua maumivu ya moyo ni mhusika, wengine ni washauri na mwisho wa siku ana uamuzi wa kukubali au kukataa anabakia nao mwenyewe na mwenzio amekataa,” mama Cecy hakuwa na kuongeza baada ya kauli ya mwanaye.

“Mama nimesikia yote nitayafanyia kazi, najua kabisa Cecy ananipenda na ameteseka juu yangu. Nimemuhakikishia yeye ndiye chaguo la moyo wangu na mwanamke wa maisha yangu kwa vile moyo wake imeingia wasiwasi basi nitafanya anavyotaka mpenzi wangu ili aamini mbegu yake ya upendo imemea kwangu na kuzaa matunda.”

“Hilo ndilo neno nililokuwa nikilisubiri usiku na mchana, najua hukupenda maamuzi yangu lakini utaamini siku moja kwa nini nimeharakisha harusi.”

Baada ya makubaliano ya kufunga ndoa kabla ya kwenda kuanza kazi, Colin alikwenda kwa mama yake kumweleza taarifa ya Cecy kupata mkataba mnono na kutakiwa kwenda kufanya kazi nje na alivyong’ang’ania kuolewa kuliko kufanya kazi. Alipofika nyumbani alimkuta mama yake amekaa sebuleni, alimsalimia na kukaa pembeni yake.

“Vipi baba, una jambo?” mama yake alimuuliza kwa vile alifahamu vizuri mwanaye.

“Ndiyo mama.”

“Ehe,” mama yake aliweka vitu vyake chini na kugeuka amsikilize vizuri mwanaye kwa vile kila kukicha alikuwa na jakamoyo. Hasa baada ya ndoa ya mwanaye na Mage kuvunjika katika hatua za mwisho.

Colin alimweleza mkataba alioingia Cecy na makampuni yote ambayo yalimuacha mama yake kinywa wazi kufikia hatua ya kusema.

“Yaani Cecy muuza ndizi alipwe mamilio ya fedha kwa kazi ya kupamba jarida na kuonesha mavazi huoni atakutana na watu wengi wenye fedha na wewe kumkuacha. Kwa nini umemtafutia kazi kama hiyo wakati shida yako ilikuwa awe mkeo kwa vile hatuna shida katika maisha yetu.”

“Mama, yote hayo tisa kuna kitu Cecy kanichanganya sana yaani mpaka kichwa kinaniuma,” Colin alisema kwa sauti ya unyonge.

“Kitu gani? Nilijua lazima uhusiano wenu utaingia dosari pesa atakazolipwa ni nyingi sana hasa akizingatiwa alikuwa hohehahe,” mama Colin alichangia bila kujua anataka kuambiwa nini.

“Sivyo unavyofikiria, mama Cecy anataka ndoa kabla ya kwenda kuanza kazi.”

“He! Si umesema mwezi ujao anatakiwa kuondoka?”

“Ndiyo, lakini yeye amesema bila ndoa na kazi hataki.”

“Mbona sikuelewi hataki kazi kwa ajili ya ndoa?”

“Ndiyo mama, anataka akiondoka hapa awe tayari mke wangu.”

“Kwa nini anafanya haraka hivyo, kwa nini asiende kwanza kisha arudi kufunga ndoa wakati huo maandalizi yatakuwa yamekamiliksa anaolewa na kuondoka.”

“Amekataa, amesema nikimlazimisha kwenda na kazi yenyewe hataki.” 

“Kweli elimu ni muhimu. Yaani anataka kuyakataa mamilioni kwa ajili ya ndoa tu?” mama Colin alishangaa.

“Mama Cecy ni tofauti na wanawake wengi, mimi kwake ni kila kitu hasikii wala haoni anasema anaweza kuondoka huku nyuma Hans akafungwa hivyo naweza kurudiana na Mage na yeye kupoteza alichokitafuta muda mrefu. Yupo radhi kuendelea kuuza ndizi lakini si kunikosa mimi.”

“Mmh! Kazi ipo, sasa utafanyaje?”

“Nilikuwa naomba ushauri wako japo nilimkubalia kufunga naye ndoa kabla ya kuanza kazi.”

“Ninafikiri wazo lako zuri, japokuwa sikupenda harusi ya aina hiyo, lakini kwa vile naujua msimamo wa yule msichana sina budi kukubaliana nawe. Sijawahi kuona mwanamke msimamo mkali kama yule binti. Anajiamini katika kitu anachokitafuta hasa akiwa na haki nacho.”

 Walikubaliana kufanya maandalizi ya harusi kwa kuandaa vikao vya wiki tatu, wiki ya nne inakuwa harusi.

                                                       ***

Baada ya upelelezi wa kesi ya Hans kupanga njama za kifo cha mkewe na mwanaye kukamilika ilisomwa hukumu katika mahakama kuu. Siku hiyo walijaa watu pomoni kutaka kusikiliza nini kitakacho amuliwa juu ya tuhuma za Hans kumuua mkewe. Baada ya jaji kukaa kwenye kiti chake na watu wote kukaa chini alitulia kupanga kalatasi zake vizuri  kisha alikohoa kidogo kuwafanya watu wote wakae tayari kumsikiliza wakiwemo Mage, mama yake shoga yake Brenda, familia nzima ya Hans pia alikuwepo mama Colin, Colin na mchumba wake Cecy. 

Watu wote walitulia kumsikiliza jaji huku mioyo ikiwadunda wakiomba utokee muujiza utakao badili damu kuwa maji meupe. Kwa sauti yenye kusikika alisema:

Nina imani wote uliopo hapa mnajua tupo hapa kwa sababu gani, leo ndiyo siku tunayo hitimisha kesi  inayomkabiri Hans  Simgao ambaye anakabiriwa na kesi ya mauaji iliyochukua takribani mwezi mzima  na leo ndiyo siku ya hukumu yake.

Kama kawaida kesi hii ilianza kusikiliza mahakama ya mwanzo ambayo haikuwa na uwezo wa kuhukumu na kuamuliwa kuletwa huku mahakama mkuu yenye uwezo wa kutoa hukumu kwa kesi yoyote nzito. 

Baada ya hukumu kama mtuhumiwa hata ridhika na hukumu hii bado ana nafasi ya kwenda mbele zaidi kwenye mahakama ya rufaa.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote za mashtaka na utetezi na mahakama kuridhika utetezi wa pande zote. Kutokana na maelezo upande mashtaka unaosema kuwa mtuhumiwa aliwatuma watu kumuua mkewe ili arudiane na mpenzi wake wa zamani ambaye wakati huo alikuwa kwenye maandalizi ya kuolewa na mwanaume mwingine.

Baada ya mashahidi wote waliopanda kizimbani akiwemo mchumba wa marehemu kutoa ushahidi wao ambao ulifanyiwa kazi na hatimaye kujiridhisha na ushahidi upande wa mashtaka ambao unatia hatiani moja kwa moja mtuhumiwa kwa hiyo mahakana inamuhukumu  Hans Simgao kifungo cha maisha gerezani na kazi ngumu. Narudia tena kusema kuwa kama hamjalidhika na hukumu hii mna nafasi ya kukata rufaa mahakama ya rufaa,” hakimu alimaliza hukumu yake.

Hakimu baada ya kutoa hukumu ile iliamsha vilio mahakamani huku mama mzazi na Mage kuanguka chini na kupoteza fahamu. Ilibidi huduma ya kwanza ifanye kazi yake ya ziada kutoa huduma ya kwanza kutokana na watu wengi walipoteza fahamu baada ya hukumu nzito iliyompoteza Hans uraiani.

Baba yake hakukubaliana na huku ile na kuapa kukata rufaa kuhakikisha mwanaye anachiwa huku kwa vile makosa yalionekana ya kutengeneza lakini aliamini mwanaye hawezi kumuua mkewe kwa ajili ya mwanamke. Wakili aliyewekwa kutetea kesi ile aliomba nakala ya hukumu ili waweze kukata rufaa.

                                                                 ***

Mage alizinduka na kujikuta amelala kwenye kitanda cha hospitali akiongezwa maji, pembeni alikuwa mama yake na shoga yake Brenda. Alipowaona aliangua kilio upya  huku akisema:

“Mama mkosi gani nimekosa Bara na Pwani, hivi nitaweka wapi uso wangu mbele ya jamii wakijua mimi ndiye niliyesababisha kifo cha mke wa Hans huku wengine wakiniona mimi ndiye sababu ya Hans kufungwa maisha.”

“Mage aliyoyafanya Hans hukumtuma kafanya kwa matakwa yake siamini kama angekushirikisha ungemkubalie afanye unyama kama ule. Ni heri angempa talaka kuliko alichokifanya,” alisema Brenda.

“Brenda naamini nuksi ndiyo nyota yangu haiwezekani Hans afungwe maisha Colin naye awe na mpenzi. Nina imani sina faida ya kuendelea kuishi.”

“Mage unataka kufanya nini?” Brenda alishtuka.

“Mwanangu hayo ni mawazo gani, Hans kufungwa si mwisho wa maisha bado una nafasi ya kuitafuta furaha,” mama yake alimtia moyo.

“Sasa mama hiyo furaha nitaipata wapi ikiwa hata aliyemweka kama spare tyre ana mwanamke mwingine ambaye ni mzuri kuliko mimi.”

“Brenda yote umeyataka mwenyewe ungenisikiliza sasa hivi ungekuwa kwa mumeo.”

“Mama sikubali nitalipiganie penzi la Colin  kwa gharama yoyote.”

“Sasa Mage unataka kuchanganyikiwa, juzi tu Colin kamtangaza mchumba wake mbele za watu tena mtu maarufu utaanzia wapi?” Brenda alimuuliza.

“Kama mnataka niendelee kuishi naomba hili ninalotaka kuamua mniachie mimi mwenyewe zaidi ya hapo mtaokota mzoga wangu,” Mage alitoa vitisho.

“Lakini Mage wanaume wameisha? Mbona kuna wavulana wazuri kuliko huyo Colin na Hans?” Brenda alimuuliza.

“Ni kweli wapo wanaume wazuri lakini si kila mbegu humea kwenye udongo wowote. Mapenzi yangu kwa Hans na Colin ni kama mtende kwenye jangwa si rahisi mti mwingine kumea sehemu ile basi ndivyo mapenzi ya Hans na Colin walikuwa kama mapacha ndani ya moyo wangu.”

“Basi ndivyo hivyo mtaka pupa hadiliki kula tamu.”

“Jamani nimewaeleza naomba mniache ni uwamuzi wangu mtu atakayeingilia uamuzi wangu ajue ndiye atakayehusika na kifo changu.”

“Mmh! Fanya mchezo utakwenda kufunga ndoa na Hans gerezani,” mama Mage alitoa taadhari kwa mwanaye aliyetaka kuingilia mapenzi ya watu.

                                                                          ***

Kufungwa kwa Hans kuliongeza umakini kwa Cecy kuhakikisha kila kona aliyokuwepo Colin na yeye yupo huku moyo wake ukimpa tahadhari ya yeye kuwa mbali na Colin lazima kuna kitu kitatendeka. Wazo lake lilikuwa kuachana na kazi ya kufanya maonesho ya mavazi ili kumlinda mumewe na Mage msichana aliyebakia kama genda heka ambalo linaweza kuvamia mume wa mtu bila aibu.

Baada ya kutoka gym wakati wa kurudi nyumbani Cecy alionekana mtu mwenye mawazo mengi kitu kilichomfanya apoteze mchangamfu wake wa kawaida.

“Bebi.”

“Abee, Cecy alitikia huku akichukua chupa ya juisi.

“Vipi mazoezi ya leo yamekuchosha?” alimuuliza huku akimtazama.

“Hapana kawaida tu,” Cecy alimjibu bila kumtazama.

“Mbona huna uchangamfu wako wa kawaida.”

“Kuna kitu kinaniumiza kichwa nafikiria kubadili uamuzi.”

“He! Uamuzi tena mpenzi wangu?” Colin alishtuka kidogo agongane uso kwa uso na  gari lililokuwa likija kwa mbele yao lakini alijitahidi kulirudisha sehemu yake.

“Ndiyo mpenzi kuna jinamizi linataka kuivamia furaha ya moyo wangu.”

“Jinamizi gani tena  mpenzi wangu?” Colin aliipaki gari pembeni ya barabara ili amsikilize vizuri mpenzi wake.

“Colin naomba unisikilize vizuri.”

“Sawa mpenzi.”

“Nimeamua kuvunja mkataba wa kwenda kufanya maonyesho nje ya nchi.”

“He! Kwa nini jamani? Si nimekubali kufunga nawe ndoa ndipo uondoke,” Colin alishtuka.

“Hukumu ya Hans imeondoa kabisa amani ya moyo wangu.”

“Kivipi mpenzi?”

“Najua nikiondoka utarudiana na Mage.”

“Siwezi...siwezi mpenzi, yule ni matapishi sitayarudisha mdomoni mwangu.”

“Hapana Colin, yule mwanamke nikiondoka lazima atatumia hila za kike kukurudisha mikononi mwako na mimi kutoka kapa. Kwa hiyo mimi siendi popote wapigie simu waeleze nimevunja mkataba yote.”

“Mpenzi utafungwa, una hela za kuwalipa ili kuvunja mkataba?”

“Kwani kazi nimeanza?”

“Hakuna kitu kama hicho, ukitaka fanya hata mwaka mmoja ndipo uvunje.”

“Basi kama hivyo tutaondoka wote kwenda huko nitakapokuwa.”

“Sawa hakuna tatizo lakini usiache kazi.”

“Hapo tutaelewana kidogo na sitaki kumuona Mage kwenu wala kukupigia simu.”

“Yote yanatekelezeka mpenzi wangu.”

Kauli ya Colin ilirudisha furaha ya Cecy na kujikuta akitabasamu na kumnywesha juisi mpenzi wake aliyekuwa amezima gari kwa mshtuko. Aliwasha gari na safari ya kurudi nyumbani iliendelea. Wakiwa njiani simuya Colin iliita Cecy aliichukua  na kuangalia na kukuta haina jina alimpa Colin.

“Mpenzi pokea simu.”

“Kapiga nani?”

“Haina jina.”

“Achana naye.”

“Hapana pokea hujui nani anakupigia.”

Colin aliichukua siku na kupokea:

“Haloo.”

“Ooh! Mpenzi wa maisha yangu, za toka jana mahakamani nina imani unajua kabisa sasa ndiyo nafasi yetu ya kufunga ndoa na kuwa mke na mume.”

“We! Nani?” Colin pamoja na kujua aliyepiga simu ni Mage alijifanya hamjui aliyepiga ili Cecy asijue kitu.

“Colin mpenzi kipi kilichokufanya usahau sauti ya malkia wa moyo wako au sababu ya hicho kinyago?”

“Jitambulishe au siyo nakata simu,” Colin alijifanya kuja juu.

Cecy alishtuka majibu ya mpenzi wake lakini alitulia amalize kuzungumza ndipo amuulize.

“Ni mimi Mage mwanamke pekee uliyeshushiwa na Mungu, amini kufungwa kwa Hans Mungu ametenda ili ile ndoa yetu ya ahadi itimie.”

“Umekosea namba,” Colin alisema huku akikata simu.

“Nani?” Cecy alimuuliza.

“Kuna mtu anaonekana amekosea namba.”

“Basi unakuta mtu anapiga simu na kuanza kutoa maagizo mengi bila kujua anazungumza na nani,” Cecy alimuunga mkono mpenzi wake.

“Umeona eeh, mpenzi nawe yamekukuta?”

“Mara chache.”

“Mara nyingi watu huwa wanachanganya namba badala ya sita wanaandika tisa basi akipiga inakwenda kwa mwingine,” Colin alizidi kuficha kilichopita.

Wakiwa katika ya mazungumzo ujumbe  uliingia kwenye simu ya Colin, aliichukua simu haraka kwa kuamini unatoka kwa Mage. Kabla hajafungua upande wa ujumbe Cecy alidaka na kusema:

“Nipo kwa ajili yako nitasoma na kukueleza kimeandikwa nini.”

Colin alipoangalia namba ya ujumbe ule ilikuwa iliyopigwa muda mfupi na Mage, alijikuta njia panda kumuachia simu Cecy asome ujumbe ule ambao aliamini si mzuri kusomwa naye. Lakini hakuwa na jinsi huku akiomba usiwe ujumbe mbaya ambao utamchanganya mpenzi wake na kulizua jipya pengine kukataa hata kazi yenyewe.. 

Cecy alichukua simu na kufungua upande wa ujumbe na kuanza kusoma, ghafla macho yalimtoka pima na mapigo ya moyo yalianza kumwenda mbio  huku jasho likitanda kwenye maji la uso.

Ujumbe ulikuwa umeandikwa:

Colin wewe ndiye mpenzi wangu wa maisha, kumbuka ahadi yetu tuliyoahidiana kuwa mume na mke ipo palepale. Huu ndiyo wakati wangu hicho kinyago chako hakina nafasi mimi  na wewe tunajulikana kwa wazazi wetu na mbele ya Mungu. Colin nakupenda zaidi ya kupenda, kufungwa kwa Hans Mungu ametenda ili ahadi yetu itimie. Mimi ndiye mkeo uliyechangulia na Mungu. I love you my husband to be Colin forever and ever mmmmwaaa.  

Colin aliyekuwa akifuatilia uso wa Cecy  alishtuka kuona macho ya Cecy yakikodolewa pima kisha kuanza kutoka machozi, alijua kimenuka, kwa mchecheto bila kujielewa kama yupo barabarani  gari lilihama njia na kwenda kujingonga kwenye nguzo ya umeme na kufanya utokee mlipuko mkubwa baada ya waya za umeme kugusana.



Msichana mmoja shoga wa Brenda rafiki wa Mage ambaye alikuwa akimfahamu  Colin  kutokana na kuwepo siku Colin alipomvisha pete Mage. Alikuwepo kwenye ajali ile kutokana na kutemka kwenye daladala na kukuta watu wakitolewa kwenye gari lililokuwa likiwaka moto.

 Kwa vile hakuijua namba ya simu ya mama Colin aliamua kumpigia simu Brenda  amweleze Mage ili ampigie mama Colin kumjulisha ajali ile. Baada ya kupigiwa simu Brenda alipokea upande wa pili:

“Haloo Loveness, niambie shoga!”

“Aisee kuna tatizo,” alisema kwa sauti iliyojaa wasiwasi.

“Mbona unanitisha kuna nini?” Brenda alishtuka.

“Colin kapata ajali mbaya sana.”

“Colin! Yupi?”

“Aliyekuwa mchumba wa Mage.”

“Wewe! Ajali ya nini tena Mungu wangu?”

“Gari alililokuwa akiendesha nimepata ajali  mbaya barabara ya Sam Nujoma jirani na Mlimani City kwa kugonga nguzo ya umeme.”

“Mungu wangu, vipi hali yake?”

“Mmh! Kwa kweli kuna taarifa nyingi japo si rasmi.”

“Mungu wangu nisaidie mja wako, taarifa gani tena Love?”

“Wapo wanaosema wamekufa papohapo.”

“Jamaniii! Kwani alikuwa na nani?”

“Na msichana mmoja ambaye anaonekana alikuwa na nguo za mazoezi.”

“He! Yaani nimechoka, siamini kama Colin amekufa kirahisi namna hiyo.”

“Sasa shoga nina imani Mage ana namba ya mama yake, mpigie ili awajulishe nina imani hawana taarifa.”

“Poa, lakini siamini mpaka niuone mwili wa Colin kwenye jeneza.”

Brenda akiwa amechanganyikiwa alimpigia simu Mage aliyekuwa amekaa kwao huku akichezea simu yake. Baada ya kumtumia ujumbe Colin alipiga simu ambayo iliita bila kupokelewa na mwisho ilizimwa kabisa.

Baada ya kuzimwa alijikuta akijiapiza:

“Lazima nimpate Colin kwa hiyari kwa nguvu, nitahakikisha nampoteza kinyago wake ili niipate nafasi yangu bila hiyo sina maisha heri ninywe sumu.”

Akiwa katikati ya mawazo simu yake iliita, wazo lake alijua Colin alikuwa akitafuta sehemu nzuri ili ampigie. Alipoangalia alikuta inatoka kwa shoga yake Brenda, aliipokea.

“Niambie shoga.”

“Mage kuna taarifa siyo nzuri.”

“Taarifa gani?”

“Zinamhusu zilipendwa wako.”

“Nani, Hans?”

“Hapana, Colin.”

“He! Colin kakupigia simu?”

“Siyo kunipigia simu bali kapata ajali mbaya.”

“Acha utani, acha kunirusha roho unione kama nampenda, sio siri Colin ndiye aliyebeba uhai wangu.”

“Mage hebu tuliza akili unisilize.”

“Haya niambie mpenzi.”

“Colin amepata ajali mbaya barabara ya Sam Nujoma jirani na Mlimani City na haijulikani kama mzima au amekufa.”

“Brenda sipendi utani wa kujinga, nimetoka kuzungumza na Colin hata robo saa haijapita.”

“Sasa wewe fanya utani naomba umpigie simu mama yake sasa hivi, mweleze Colin amepata ajali na amekimbizwa Muhimbili. Naomba usiongeze lingine usije muua mama wa watu kwa mshtuko. Najua anampenda sana mwanaye ndiye kama mboni ya macho yake.”

“Japo siamini nitampigia tu.”

“Fanya haraka, unaambiwa hata gari alilokuwa akiendesha limeteketea lote.”

“Mungu wangu ! Brenda unasema kweli?” Mage aliuliza kwa sauti ya kilio.

“Kweli, siwezi kukutania kwa jambo zito kama hili.”

“Mungu wangu hii nuksi gani? Kama Colin akifa nitakuwa na faida gani ya kuendelea kuishi,” Mage alizungumza peke yake huku macho yamejaa machozi na mikono kumtetemeka wakati wa kutafuta namba ya mama Colin.

Kila alivyokuwa akilitafuta machozi yalizidi kuyafunika macho yake hata alipoyafuta kwa mkono yalijaa tena. Alitoka chumbani na simu mkononi hadi sebuleni na kumkuta mama yake. 

“Mage nini?” mama yake alishtuka na hali ya mwanaye.

“Colin, mama,” alisema huku akilia na kumpa simu mama yake.

“Colin! Kafanya nini?”

“Ajali.”

“He! Lini?”

“Sasa hivi.”

“Taarifa umezitoa wapi?”

“Kanipigia Brenda sasa hivi?”

“Dah! Vipi hali yake.”

“Na..na..sikia a..a..meku..”

“Wewe mtoto ushia hapohapo,” mama Mage alimkata kauli mwanaye hakutaka kulisikia neno la mwisho kwa vile aliamini litamuumiza moyo wake.

“Mama mpigie simu mama yake hana habari.”

“Mmh!” 

Mama Mage alichukua simu yake kutafuta namba ya mama Colin huku naye mikono ikimtetemeka. Baada ya kuipata alipiga simu ambayo ilipokelewa upande upande wa pili.

“Haloo dada vipi?”

“Kwema, una habari gani?”

“Za nini?”

“Kuhusu Colin.”

“Mmh! Sina habari zozote.”

“Kuna taarifa kapata ajali.”

“Ajali!?” mama Colin alishtuka.

“Eeh, ndiyo, kuna mtu kampigia simu Mage na kutaka tukujulishe kwa vile hakuwa na namba yako ya simu.”

“Mungu wangu wee, yupo katika hali gani?”

“Hebu subiri,” alisema na kuziba sehemu ya kuzungumzia na kumgeukia Mage.

“Eti Mage mwili wa Colin umepelekwa hospitali gani?”

“Mama sijasema amekufa ila watu wanafikiria hivyo,” Mage alimgeuka mama yake.

“Sasa kapelekwa wapi?” 

“Mama mwambie amekimbizwa muhimbili, ila usimwambie yupo kwenye hali gani mengine atayajua hukohuko mwenyewe. ”  Baada ya kuzungumza na mwanaye aliachia sehemu ya kuzungumzia na kuzungumza na mama Colin.

“Anasema baada ya ajali wasamalia wema wamewapeleka Muhimbili.”

“Wanasema hali yake ipo vipi?”

“Hawajajua kwa vile amebebwa na kuingizwa kwenye gari na kuwahishwa hospitali.”

“Na..na.. Cecy?”

“Sijajua hebu subiri...Eti Cecy alikuwepo? Alimuuliza mwanaye. 

“Ndiyo.”

‘Ndiyo walikuwa pamoja.” 

“Na..nashukuru dada.”

“Nami nakuja huko.”

“Sawa tutakutana.”

Baada ya kukata mama Mage alinyanyuka kuelekea chumbani kuchukua funguo ya gari, baada ya kuchukua alitoka nje na Mage alitoka kumfuata mama yake waliingia kwenye gari na kutoka kuelekea Muhimbili. Muda wote Mage alikuwa akilia kitu kilichomfanya mama yake kuingilia kati. 

“Unasema hajafa unalia nini mbona unamchulia mwenzio.”

“Mama inauma Colin ndiye lilikuwa tumaini langu mwisho.”

“Muombee basi apone.”

“Yaani Mungu asikie dua langu, Colin apone lakini mchumba wake afe.”

“Wee mtoto roho gani hiyo?”

“Mama wakipona wote sina changu.”

“Hebu achana na mawazo hayo,” mama Mage alisema huku kanyaga mafuta kuwahi hospitali.  

Mama Colin baada ya kuzipata taarifa zile alimpitia mama Cecy aliyekuwa hana taarifa zozote kwa kujua mwanaye alikwenda mazoezi asubuhi na mpenzi wake. Naye alishtuka lakini mama Colin alimpa moyo wafike hospitali ili wajue kipi kinaendelea japokuwa hakujua watoto wao wapo kwenye hali gani.

Walijikuta wakifika pamoja na Mage na mama yake, waliongozana wote mapokezi kuulizia taarifa za wagonjwa wao. Waliambiwa wote wamekimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi kwa vile hali zao si nzuri. Walikwenda kuonana na mganga mkuu, aliwakaribisha ofisini kwake.

“Ndiyo wazazi wangu kwanza poleni sana.”

“Mmh! Hatujapoa kwani hatujui hali za watoto wetu,” alijibu mama Colin.

Dokta Bukos kwanza alitulia kama anasoma taarifa kwenye kalatasi kutafuta neno la kuwaeleza ili wasipagawe kutokana na hali za wagonjwa wao. Baada ya kutulia kwa muda alinyanyua uso wake na kusema kwa sauti ya upole.

“Wazazi wangu hali za wagonjwa si mbaya wala nzuri sana lakini bado tunapigania maisha yao.”

“Lakini baba mtu mpaka kuletwa chumba cha wagonjwa mahututi lazima hali yake ni mbaya sana?” aliuliza mama Colin.

“Ni kweli, chumba hicho ni kwa ajili ya uangalizi wa karibu kwa mgojwa.”

“Kwani hali zao zikoje?” aliuliza mama Cecy.

“Bado kwa vile wameletwa hawajitambui hivyo kwanza tunashughulika na suala la kurudisha ufahamu kisha tutajua tufanye kitu gani.”

“Mbona nilisikia wamekufa?” Mage aliropoka.

“Si kweli, kama wangekuwa wamekufa wodini tumewapeleka kufanya nini?” daktari alijibu kwa ukali kidogo.

“Wee Mage acha kuropoka,” mama yake alimkanya.

“Jamani naomba kuzungumza na wahusika wa wagonjwa wengine msubiri nje,” daktari alisema.

Mage na mama yake walitoka nje na kubakia mama Colin na Cecy, baada ya kubakia wawili dokta alitaka kujua uhusiano ya waliobakia na wagonjwa. Wote walijitambulisha.

“Basi wazazi wangu ajali waliyopata ilikuwa mbaya sana, majeraha si makubwa sana lakini inaonesha wamejigonga kwenye kitu kigumu wakati gari likipata ajali hivyo kusababisha mtikisiko wa ubongo uliopelekea kupoteza fahamu. Lakini tunahangaika ili kurudisha fahamu zao.”




“Zitachukua muda gani kurudi?” mama Cecy aliuliza.

“Hatuwezi kujua ubongo umecheza kiasi gani, lakini msiwe na wasiwasi hii ni hali ya kawaida kwenye ajali za namna hii,” dokta aliwapa moyo.

“Tunaweza kwenda kuwaona?” aliuliza mama Cecy.

“Kwa leo bado kuna baadhi ya mambo tunashughulika nayo kuanzia kesho mna nafasi ya kuja kuwaona.”

“Sawa.”

Mama Colin na mama Cecy walitoka ofisini kwa mganga mkuu na kukutana na Mage na mama yake wakiwasubiri, walipotoka waliwauliza.

“Vipi wanasemaje?” Mage alikuwa wa kwanza kuuliza.

“Bado wapo chini ya uangalizi maalumu,” alijibu mama Colin.

“Hatuwezi kuwaona?” mama Mage aliuliza.

“Kwa leo haiwezekani.”

“Mmh! Basi watakuwa wana hali mbaya sana,” Mage alisema.

“Anayejua ni dokta, sisi hatujui kwa vile hatujawaona,” alijibu mama Colin ambaye alionesha kuchoshwa na maswali ya Mage.

“Jamani hatuna cha kufanya maombi yetu yote yawe kwa watoto wetu ili Mungu awaepushe na matatizo yaliyo mbele yao,” alisema mama Mage.

“Ni kweli dada yangu,” alisema mama Cecy ambaye muda wote alikuwa kimya kutokana na mshtuko alioupaka kwa ajali ya watoto wao.

Walikubaliana kurudi nyumbani mpaka kesho ambayo wangerudi kuwaona, mama Mage aliwashauri wote waongozane nyumbani kwa mama Colin kufanya maombi ya pamoja ili Mungu awaepushe na matatizo yale. Waliongozana wote hadi nyumbani kwa mama Colin ambako walifanya maombi ya pamoja yaliyoongozwa na mama Mage.

Walipiga magoti na kushikana mikono kisha mama Mage alishusha maombi.

“Baba Mungu tumepiga magoti mbele yako tunajua hakuna chochote chini na juu ya jua kiwezacho kufanyika bali kwa idhini yako. Baba Mungu lisilowezekana kwa mwanadamu kwake linawezekana, lililo zito kwa mwadamu wako ni jepesi. Eeh, Baba tunaomba uwaepushe watoto wetu na matatizo mazito kama ulivyoweza kumuepusha mwanao mpendwa pale msalabani.

Kama ulivyoweza kumponya Ayubu na maradhi ya ajabu ambayo alipona kupitia kwa uweza wako. Baba Mungu unaweza kumponya aliye mahututi unaweza kumfufua aliyekufa kwako wewe hakuna kinachoshindikana  baba waponye wenetu ambao hatujui hali zao ni wewe pekee mwenye kuugeuza usiku ukawa mchana basi yaondoe maradhi miilini mwao wape afya njema.

Baba vunja pepo wa maumivu vunja pepo wa mauti  vunja pepo wa  maradhi kwa jina la mwanao Yesu Kristo aliyehai Amen.”

“Ameni,” waliitikia pamoja.

Baada ya maombi walinyanyuka na kukaa kwenye makochi, kwa vile hawakuwa na la kuzungumza mpaka siku ya pili watakapokwenda kuwaona wagonjwa wao. Mama Mage na mwanaye waliaga na kuondoka kurudi nyumbani na kuwaacha mama Colin na Cecy wakiwa wamekaa kila mmoja akiwaza lake.

                                                                 ***

Siku ya pili alfajiri walikutana wote hospitali ya Muhimbili , kwa vile daktari alikuwa hajafika ilibidi wamsubiri mpaka saa moja asubuhi alipofika, alipowaona aliwaeleza wasubiri ili afike wodini kwanza.  Dokta Bukos baada ya kuwazungukia wagonjwa wote na kuchukuwa taarifa kutoka kwa daktari wa zamu aliwafuata kwenda kuwaona wagonjwa wao.

Waliingia mmojammoja kutokana na taratibu za kuingia chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Colin alikuwa akipumulia mashine akiwa amelala bila kutikisika. Lakini dokta Bukos aliwaeleza kuwa kidogo ameanza kupata fahamu kwa misuli ya mwili kuanza kufanya kazi taratibu japo hakuonesha mabadiliko yoyote zaidi ya kulala vilevile walivyomkuta.

Katika chumba kingine Cecy naye alikuwa vilevile amejilaza akitumia mashine kupumua, yeye alionekana ufahamu bado kabisa japokuwa mapigo ya moyo dokta alisema yapo mbali sana. Lakini aliwaomba wazidishe kumuomba Mungu na si kulia. 

                                                          WIKI MOJA BAADAYE  

Baada ya wiki moja hali ya Colin ilimalika kidogo kwa kuweza kutambua watu japo bado alikuwa hawezi kuzungumza kwa haraka kwa kutafuta maneno. Cecy hali yake ilikuwa bado mbaya pamoja na mwili kuanza kurudisha hisia bado alikuwa akiendelea kutumia mashine za kumsaidia kupumua.

Walijikuta katika wakati mgumu baada ya hali ya Cecy kuonekana kuchelewa kuimalika. Mganga mkuu aliomba kama wana uwezo basi Cecy apelekwe India kwa ajili ya matubabu zaidi  baada ya kuamini uwezo wa madaktari wa Tanzania uliishia pale kuweza kuuamsha mwili lakini hali ilikuwa bado tofauti na Colin ambaye aliweza kula hata kufanyishwa mazoezi japokuwa alikuwa akizungumza kwa shida. 

Madaktari waliwahakikisha ndani ya wiki nyingine hali itaimalika zaidi na kuweza kuanza mazoezi ya peke yake. Fedha iliyokuwa ikitakiwa kwa ajili ya matibabu na nauri ya Cecy na msaidizi wake ilikuwa kubwa ambayo mama Cecy hakuwa nayo. Kwa hali  ya mgonjwa ilivyokuwa ikionekana  mama Colin aliamini kabisa Cecy hawezi kupona hivyo kutoa kiasi hicho cha fedha ni sawa na kuzitupa.

Mama Cecy alikuwa radhi kuuza nyumba ili tu mwanaye akatibiwe, lakini mama Colin alimshauri asisumbuke kwa vile wagonjwa wa aina ile huwa hawaponi heri asiipoteze nyumba kwani Cecy akifa atakuwa na sehemu ya kukaa.

Mama Cecy alikuwa radhi kulala nje lakini ajue hatima ya hali ya mwanaye, ili kujitoa kwenye lawama alichangia milioni tano katika milioni ishrini na tano zilizotakiwa. Mama Cecy alitafuta dalali wa kuiuza nyumba kwa bei ya kutupa ili tu mwanaye akatibiwe India kama kufa basi afe akijua alikuwa akipigania maisha yake.

Wiki ile ndiyo ilikuwa wiki ya malipo ya Cecy kutoka katika kampuni ya jarida la Ebony ambayo iliijngiza kwenye akaunti ya Cecy pia walifunga safari mpaka Tanzania kuonana na Cecy kwa ajili ya kumpiga picha zingine kwa ajili ya matoleo mengine. Jarida lililotoka na picha ya Cecy ilivunja rekodi ya mauzo ya kampuni ile toka ianzishwe. 

Uongozi wa kampuni ile ulipanga kumpa mkataba mnono wa muda mrefu zaidi pia kumfunga asitumike kwenye majarida mengine. Walipofika walitaka kuonana na meneja wake ambaye ni mchumba wake Colin mmiliki wa kampuni ya Urembo. Taarifa walizopata ziliwashtuka kusikia Cecy na mchumba wake walipata ajali mbaya sana. Walikwenda mpaka hospitali na kuwaona wagonjwa.

Colin alionekana hajambo lakini Cecy bado hali yake ilikuwa tata, walionana na mganga mkuu na kutaka kujua nini hatma ya mgonjwa kwa siku alizokaa hospitali. Aliwaeleza hatua walizochukua tokea mwanzo kwa wagonjwa wote na kufanikiwa kwa  mmoja na sehemu walipokwama na kuhitaji msaada wa matibabu zaidi nje ya nchi.

Waliulizia kama kuna uwezekana wa mgonjwa kupona, walijibu upo wa hamsini kwa hamsini. Waliuliza gharama ya matibabu yote walielezwa milioni ishirini na tano kwa awali kama itazidi watajulishwa kwa vile mgonjwa hakuwa wa kutoka mapema. Walikubali kugharamia matibabu ya Cecy mpaka hatua ya mwisho. Baada ya makubaliano zilifanywa taratibu zote za kumsafirisha mgonjwa na mtu wake wa karibu.

Siku ya tatu Cecy alisafirishwa pamoja na mama yake kwenda India kwa matibabu ambayo wengi waliamini madaktari wa Tanzania waliona aibu kusema ukweli kuwa Cecy ameisha kufa anachosubiri kupoa tu. Baada ya safari ya angani Cecy alitua katika jiji la Mumbay na kupelekwa katika hospitali ya Apolo.

Alipokelewa mara moja alianza kupatiwa matibabu kwa kuchukuliwa vipimo vyote ili kuangalia tatizo lipo wapi. Baada kurudi majibu ya vipimo ilionesha Cecy atapona lakini itachukua muda kurudi katika hali ya kawaida kutokana na kupoteza kumbukumbu na ubongo wake kucheza kidogo, lakini  alikuwa na bahari nzuri ubongo haukuvia damu.

                                                                         TANZANIA

Hali ya Colin iliendelea vizuri kwa kuimalika kwa kasi kubwa tofauti na walivyotegemea. Baada ya wiki aliweza kuzungumza vizuri na kuanza kumkumbuka mpenzi wake Cecy. Wakiwa wamekaa kitandani  Colin alimuuliza mama yake.

“Mama mbona simuoni Cecy wala mama yake leo siku ya tatu?”

“Cecy alisafiri walifiwa na bibi yao kabla hujapata ajali.”

“Mama ina maana nilipata ajali peke yangu?”

Swali lile lilimchanganya sana mama yake aliyeamini mwanaye baada ya ajali alipoteza kumbukumbu na hakutaka kumshtua kutokana na hali na mchumba wake ambaye aliamini aliondoka mfu kwa asilimia tisini na tano.

“Kwani unakumbuka nini?”

“Unajua mama nakumbuka  wakati napata ajali nilikuwa na Cecy tukitoka mazoezini  na sababu ya ajali ni Mage.”

“Mage?” mama yake alishtuka.

“Ndiyo mama.”

“Mage kasababisha kivipi?”

Colin alimweleza tukio zima la ajali ilivyotokea mpaka kupata ajali, baada ya kumsikiliza aliguna na kusema:

“Kwani Mage aliandika ujumbe gani?”

“Kwa kweli sikuuona bali usomaji wa Cecy ulionesha ujumbe siyo mzuri.”

“Sasa wewe nini kilikupelekea kupata ajali.”

“Mama baada ya kumwangalia Cecy usoni moyo ulishtuka na kujua hakuna tena usalama kwa vile aliisha mshutumu Mage mapema baada ya hukumu ya mchumba wake kabla ya simu na kutishia kusitisha mkataba. Mage alinipigia simu na kuzungumza maneno ambayo ni uchokonozi kwa vile anajua kabisa nipo na nani.”

“Inaonekana alikuacha bado anakupenda ulikuwa una hiyari kukubali au kukataa au hata kumfanya spea taili.”

“Mama Cecy ni kila kitu kwangu ndiye mwanamke wa pekee moyoni mwangu sina nafasi nyingine.”

“Lakini ulitakiwa kujua ameandika ujumbe gani kabla ya kupagawa na kusababisha ajali mbaya.”

“Kwani gari limeharibika sana?”

“Limeungua lote na moto.” 

“Mungu wangu na..na Cecy?”

“Naye alipata majeraha kama yako.”

“Yupo hapa hospitali?”

“Hapana yeye inaonekana alipata matatizo makubwa na kukimbizwa India.”

“Maskini mpenzi wangu,” Colin alishika kichwa kwa mshtuko.

“Lakini taarifa zinasema anaendelea vizuri,” mama yake alimpa moyo.

“Hospitali natoka lini?”

“Wiki hii lakini utatakiwa kuja kila siku asubuhi kufanya mazoezi ya viungo ili kuurudisha mwili katika hali ya kawaida.”

“Nikijisikia vizuri kidogo nakwenda India kumwona mpenzi wangu.”

“Hakuna tatizo tutakwenda wote,” mama Colin alimkubalia mwanaye kumpa moyo lakini aliamini kabisa Cecy hakuna kitu siku zake zilikuwa zikihesabika walichosubiri taarifa za msiba wake.



                                                          ***

Mama Mage na mwanaye walikuwa wakizungumza kuhusiana na hali ya Colin na mchumba wake.

“Mama unafikiri mchumba wa Colin anaweza kupona?”

“Mmh! Kwa kweli ni Mungu tu mwenye uwezo wa kumponya, taarifa nilizopata kutoka kwenye hospitali aliyokuwa anatibiwa kupona ni asilimia ndogo na hata akipona bado hata kuwa sawa.”

“Kwa hiyo mama nina imani hii ni nafasi yangu ya kurudi kwa Colin?”

“Ni nafasi yako kama ukiifanyia kazi bila hivyo itakupita huku unaiona.”

“Sasa mama niifanyie kazi ipi au  niende wa Karumanzila?”

“Si kwenda kwa Karumanzila bali kujipendekeza muda huu wa matatizo kuonesha unamjali sana Colin kwa kwenda asubuhi unarudi usiku ikiwezekana ulale hukohuko.”

“Mama tena naondoka muda huu.”

“Mwanangu kijua ndicho hiki lazima uuanike sasa, huenda Mungu alikuwa na kusudio lake la kuirudisha ndoa yetu iliyoyeyuka kwa kifungo cha Hans na kufa kwa Cecy.”

“Umeona eeh, mama utakuwa nabii kwa kuiona hilo, japo siwezi kufurahi kwa matatizo ya Cecy lakini kila kitu hupangwa na Mungu.”

“Halafu nimeambiwa Colin atatakiwa kila siku asubuhi  apelekwe hospitali kwa mazoezi, nataka kazi hiyo uifanye wewe tena utachukua gari la kifahari la kumpelekea hospitali.”

“Mama hilo si la kusema mbona kikohozi kimepata mkohoaji nitahakikisha mahaba ninayo mpa anamsahau marehemu wake(Cecy).”

Baada ya mazungumzo Mage alimuaga mama yake kwenda kumwona Colin nyumbani kwao ili aurudishe ukaribu wao kutokana na matatizo ya mchumba wake Cecy. Mage maombi yake alitaka Cecy afie India, Tanzania urudi mwili tu usio na uhai, aliendesha gari hadi nyumbani.

Mama Colin alimpokea Mage aliyejionesha mwenye huzuni kutokana ugonjwa Colin.

“Karibu mkwe.”

“Asante mama, mume wangu anaendeleaje?”

“Mmh! Kiasi hajambo vipi nyumbani hamjambo.”

“Hatujambo kiasi.”

“Kuna anayeumwa?”

“Hapana ila huwezi kuamini toka Colin apate matatizo nimekuwa sili wala silali vizuri utafikiri naumwa mimi.”

“Pole, la muhimu kumuomba atapona tu.”

“Mama maombi yangu yote kila dakika ni kwa Colin.”

“Mama yako hajambo?”

“Hajambo, mume wangu yupo wapi?” Mage alijifanya ana shauku ya kumuona Colin.

“Yupo chumbani kwake amepumzika.”

Kwa vile chumba cha Colin alikuwa akikijua alikwenda moja kwa moja na kuingia ndani bila hodi. Alimkuta amesinzia aliinama na kumpiga busu la shavu lililomfanya Colin afumbue macho. Alishtuka kukutana na Mage aliyekuwa amemchanulia tabasamu pana amesimama pembeni ya kitanda.

“Colin mpenzi wangu pole sana,” Mage alisema huku akikaa kitandani, lakini Colin hakumjibu alikuwa kama anamshangaa.

“Vipi inaendeleaje mpenzi?” alimuuliza tena.

“Mage unatafuta nini hapa?” Colin alimuuliza akiwa amemkunjia uso.

“Colin mpenzi wangu maswali gani hayo wakati unajua wewe ni mgonjwa?”

“Hata kama mgonjwa sikukuita uje unione labda ungekuja kuona jeneza langu na si mwili wangu.”

“Kwa nini unasema hivyo mpenzi wangu?” majibu la Colin yalimshtua Mage.

“Kwanza naomba jina la mpenzi lifutike mdomoni na moyoni mpenzi wako, mpenzi wangu ni mmoja tu Cecy.”

“Kumbuka kabla ya Cecy nilikuwepo miye.”

“Kuna mtu aliye mpenzi wa moyo wako si mwingine bali Hans si Colin.”

“Colin, Hans amefungwa si mpenzi wangu mwenye nafasi hiyo ulibakia wewe peke yako.”

“Mimi ulinipenda lakini Hans ulimpenda zaidi kwa hiyo ndiye chaguo sahihi la moyo wako si mimi. Nami wewe nilikupenda lakini Cecy nilimpenda zaidi naye ndiye aliyenipenda kuliko kiumbe chochote kilichopo chini ya jua. Malaika sijawaona nina amini hata wao ningewaona wasingeuzidi uzuri wa Cecy.”

“Wewe Colin acha kukufuru Cecy ana uzuri gani kumshinda malaika?”

“Malaika uliisha muona?”

“Sijamuona lakini nasikia mzuri sana.”

“Basi uzuri wao haufiki kwa Cecy, kwa vile ulichokitaka kimefanikiwa naomba uachane na mimi.”

“Colin nimefanya nini?” Mage aliuliza huku akilia.

“Unajua umeniumiza mara ya kwanza hukutosheka umeniumiza kwa mara ya pili bado hujaridhika naona kimebakia roho yangu tu.”

“Colin usiseme hivyo unaniumiza?”

“Ulitaka tufe sote lakini nakuhakikishia Cecy atapona na atarudi tufunge ndoa hata kama Cecy atakufa nitafunga ndoa na maiti ya Cecy si mwanamke mwingine.”

“Colin usiseme hivyo, Cecy akifariki siyo mwisho wa dunia maisha yataendelea, nina imani hakutakuwa na mwanamke mwingine atakayechukua nafasi ya Cecy bali mimi.”

“Ninacho kisema hakitafutika moyoni mwangu Cecy ndiye mwanamke wangu wa maisha nawe msubiri Hans mfunge ndoa au nenda mkafungie ndoa gerezani.”

“Kwa nini Colin unanichukia hivyo?”

“Sitakusamehe mpaka nakufa naomba utoke nje,” Colin alisema kwa sauti ya juu.

“Colin ukikataa najiua.”

“Kajiue kwani ukifa mimi napungukiwa nini labda muuaji mwezio Hans.”

Maneno yale yaliuchoma moyo wa Mage ambaye alikuwa na matumaini ya kuchukua nafasi ya Cecy ambaye aliamini kupona kwake ni asilimia ndogo sana na hata kipona hataweza kuwa sawa. Kutokana na maelezo ya kidaktari aliyemfuata baada ya Cecy kupelekwa India. 

Alimweleza kuwa kama atapona angeweza kuwa na tatizo la kusahau au kupoteza kumbukumbu ambacho huwa sawa na kichaa cha kipindi kama maji kupwa maji kujaa kuna wakati inakaa sawa kuna wakati inahama.

Baada ya kuumizwa na maneno ya Colin yaliyomkatisha tamaa alitoka nje akilia kilio cha kwikwi kitu kilichomshtua mama Colin aliyekuwa amekaa sebuleni akisoma Biblia.

“We, Mage unalia nini, Colin kazidiwa?”

“Ha..ha..pana mama, Colin kanifukuza eti hataki kunioa.”

“He! Kwa sababu gani?”

“Hata sijui, yaani anasema yupo radhi kufunga ndoa na maiti ya Cecy kuliko kunioa mimi. Eti mama, siombi ila kwa bahati mbaya Cecy amekufa mwanamke wa kuolewa na Colin kuna mwingine zaidi yangu?”

“Hakuna.”

“Sasa kwa nini ananidhalilisha kwa maneno makali?”

“Labda umemkuta leo hayupo vizuri.”

“Mama naomba kama Cecy atakufa basi nafasi yake nipewe mimi kwa vile tunajuana vizuri, inawezekana kufungwa kwa Hans na hii ajali ilikuwa mpango wa Mungu kuirudisha harusi yetu iliyofungwa mbinguni.”

“Mmh! Makubwa,” mama Colin aliguna maneno ya Mage.

“Mama naomba ukazungumze na Colin, si ulisema anatakiwa kupelekwa hospitali kila asubuhi, kazi hiyo nitaifanya mimi hata kumpikia chakula kumfulia  kipindi chote nitafanya nini. Nipo tayari kuhamia hapa kuhakikisha Colin hapati tatizo lolote.”

“Basi tulia nitazungumza na Colin.”

Mama Colin alikwenda chumbani kwa Colin ili ajue kimetokea nini mpaka apishane kauli na mpenzi wake wa zamani.  Alimkuta Colin amejilaza macho kaangalia juu, mlango ulipofunguliwa aligeuza shingo kuangalia  nani anayeingia alimkuta ni mama yake.

“Vipi baba?” mama yake alimuuliza.

“Safi tu,” alijibu akiwa bado ameangalia juu.

“Upo sawa baba?”

“Sipo sawa,” alijibu akiwa bado macho yake yakiangalia darini.

“Kwa nini tena mwanangu?”

“Nani kampa ruhusa huyu shetani kuingia ndani?” aliuliza huku akigeuka kumtazama mama yake.

“Colin! Shetani nani?”

“Mage, sitaki kumuona machoni mwangu,” alisema kwa sauti ya juu kidogo.

“Kwa nini baba?”

“Aliyonifanyia madogo, leo ni Mungu tu nipo hai lakini kifo changu angechangia yeye hata mateso ya mpenzi wangu chanzo ni yeye. Kaniumiza mara ya kwanza hajafurahi karudia mara ya pili kaniumiza na mpenzi wangu bado tu ananifuata anataka nini kama siyo uhai wangu?”

“Lakini kwa nini unamhukumu bila kujua ujumbe alioandika umeandikwaje?”

“Mama, ulikuwa mbaya, Cecy hawezi kulia kwa ujumbe wa kawaida.”

“Colin bado hutakiwi kumhukumu kwa kitu usichojua, inawezekana ulikuwa wa kawaida lakini kwa vile mpenzi wako aliisha jenga chuki kwa Mage huenda hakufurahia ujumbe ule.”

“Lakini mama hata kama, ni haki mtu kutuma ujumbe au kupiga simu akijua kabisa mimi ni mchumba wa mtu na tupo katika hatua gani?”

“Hapo anaweza kuwa amefanya makosa lakini hakuna adui wa maisha, adui wa leo rafiki wa kesho, msamehe mwenzio nimemwacha analia kwa maneno yako makali.”

“Mama nitamsamehe Mage labda Cecy apone asipopona sitamsamehe mpaka nakufa.”

“Sikiliza mwanangu, ni wazi Mage anakupenda sana hujui tu, kama Mungu anapitisha uamuzi wake, Cecy anafariki Mage ndiye mwenye nafasi ya kuwa mkeo.”

“Mama kwa nini unakimbilia kufa mpenzi wangu, nataka nikuambie kitu. Cecy akifanya nitafunga naye ndoa kabla ya kuzikwa.”

“We’ Colin umerogwa yaani ufungwe ndoa na maiti ili iwe nini?”

“Kutimiza ahadi niliyomuahidi Cecy ambayo ndiyo ndoto yake kubwa kwangu ya kuwa mke na mume. Mama Cecy nampenda lakini yeye ni mwalimu wangu wa mapenzi ndiye wakili wa moyo wangu kanipigania wakati wote kuonesha ana mapenzi ya kweli kwangu Cecy hanipendei kitu bali mimi kama mimi.”

“Mmh! Na ukiisha muoa?”

“Nitaendelea kuwa muaminifu katika ndoa yangu mpaka mauti yatakaponichukua.”

“Kwa hiyo huoi tena?”

“Mama ndoa ipo moja tu dunia ikiisha fungwa duniani mpaka mbinguni haitafunguliwa.”

“Sasa kama amekufa si ndiyo mwisho wa ndoa yenu.”

“Kwangu itakuwa mwanzo kwa vile sijaitumikia ndoa yetu.”

“Colin mwanangu upo sawa?”

“Tena akili zangu zipo timamu.”

“Hebu pumzika naona kama haupo sawa.”

“Mama wala usisumbuke kufikiria unavyotaka kufikiria sina jibu zaidi hilo nililokupa.”

“Kwa mfano Cecy atarudi hayupo sawa na ugonjwa wake hauponi au amepooza utafanya nini?”

“Kama nitaweza kufunga ndoa na mwili wake usio na pumzi sitabadilika nitafunga ndoa na Cecy katika hali yoyote.”

”Mmh! Sawa.”

Mama Colin alitoka bila kuongeza neno huku akijiuliza Mage kamfanya nini Colin mpaka kufikia uamuzi mzito kama ule. Lakini aliamini zile ni hasira za kumwona Mage lakini baadaye zitashuka  na kuelewana. Aliamini kabisa ugonjwa wa Cecy si wa kupona na kama akipona hata kuwa sawa hivyo mwanamke aliyeona anamfaa mwanaye ni Mage kwa vile tayari waliisha kuwa wapenzi kabla ya hapo. 

Mage baada ya kutokeza mama Colin alikaa mkao wa kutaka kujua amezungumza nini na mwanaye.

“Vipi mama, Colin kasemaje?”

“Hii kazi niachie mimi, najua bado ana hasira zikipoa atanielewa tu.”

“Yaani mama siamini maneno anataka kuoa maiti ya Cecy kwani wanawake wamekwisha? Hata kama hanitaki mimi lakini bado wapo wazuri na wenye tabia nzuri kuliko Cecy.”

“Hilo lisikutie presha, nammudu kwa vile ni mwanangu na wala hataoa mwanamke mwingine zaidi yako. Ninyi mnafahamiana na vile mlikuwa mnapendana hivyo mtaendelea uliposimamia.”

“Umeona eeh mama, yaani Colin namshangaa kweli.”

“Sasa sikiliza kesho anatakiwa kupelekwa hospitali kwa mazoezi njoo asubuhi umpeleke.”

“Mamaa! Kwa hali hii atakubali?” Mage aliishangaa kauli ya mama Colin.

“Mage we njoo mimi nitajua nitafanya nini, nakuhakikishia lazima ataolewa na mwanangu.”

“Mmh! Mama nitafurahi, bado naona kama nipo ndotoni.”

“Wala si ndotoni, amini Colin wewe ndiye mkewe.”

“Nashukuru sana mama, basi nikuache niwahi nyumbani.”

“Hakuna tatizo msalimie mama yako.”

“Salamu zimefika.”

Mage aliagana na mama Colin na kurudi nyumbani kwao huku dua lake likiwa kwa Cecy asirudi hai ili aichukue nafasi ambayo aliamini ilikuwa yake hapo awali. Hakutaka kuyajutia maamuzi yake ya kuachana na Colin na kurudiana na Hans kwani kwake ulikuwa uamuzi sahihi ilitokea bahati mbaya ya kufungwa maisha.

Moyoni mwake alikuwa tayari kumsubiri Hans hata miaka kumi ili waoane lakini kifungo cha maisha kilimvunja nguvu na kuamini mtu sahihi kwake alikuwa Colin. Aliapa kumpigania Colin kwa nguvu zote kumrudisha mikononi mwake hata kwa kutoa uhai wa mtu. Alipofika nyumbani kwao alimweleza mama yake kilichotokea na kumshtua sana.


ITAENDELEA...




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.