HADITHI: WAKILI WA MOYO 06
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: +255713 646500
ILIPOISHIA:
Moyoni mwake alikuwa tayari kumsubiri Hans hata miaka kumi ili waoane lakini kifungo cha maisha kilimvunja nguvu na kuamini mtu sahihi kwake alikuwa Colin. Aliapa kumpigania Colin kwa nguvu zote kumrudisha mikononi mwake hata kwa kutoa uhai wa mtu. Alipofika nyumbani kwao alimweleza mama yake kilichotokea na kumshtua sana.
SASA ENDELEA...
“Mmh! Yamekuwa hayo unafikiri utafanyaje naona kila kitu kimevurugika.”
“Lakini mama Colin kasema kesho niende nikampeleke Colin hospitali.”
“Utampeleka vipi ikiwa hataki hata kukuona?”
“Mama yake kasema yeye anajua kila kitu kinachotakiwa kufanyika na ameniahidi lazima nitaolewa na mwanaye.”
“Mmh! Sawa kwa vile kasema mama yake lakini maneno ya Colin yamenitisha kusema, eti yupo tayari kufunga ndoa na maiti ya Cecy kuliko kuoa mwanamke mwingine.”
“Mama au akili ya Colin imepata tatizo baada ya kujigonga kwenye ajali?”
“Inawezekana maana ajali haikuwa ya kawaida.”
“Mmh! Inawezekana maana alivyonigeuka si kawaida yake, mama naamini Colin ananipenda.”
“Au yule mtoto alimwendea Colin kwa Karumanzila?”
“Inawezekana kabisa si bure ana urembo gani wa kumfanya Colin atake kufunga ndoa na maiti yake.”
“Hata mimi naona, lazima nasi tuhangaike ili kuhakikisha nafasi hiyo unaipata wewe.”
“Yaani huwezi kuamini sara zangu zote namuomba Ziraili amtokee Cecy na kummaliza kabisa tufikirie mambo mengine.”
“Duh! Kweli wewe kiboko, wenzio dua zao wanaomba amani wewe shari.”
“Siku zote adui yako muombee matatizo.”
“Mmh! Haya.”
MUMBAY INDIA
Katika hospitali ya Apolo katika mji wa Mumbay nchini India madaktari waliendelea kuumiza kichwa kutokana na ugonjwa wa Cecy ambao uliwachanganya akili baada ya kuweza kufumbua macho lakini mwili bado haukuwa na mawasiliano kwa asilimia zote.
Waliufanyia vipimo vyote na kukaa jopo la madaktari mabingwa kuchunguza Cecy ana tatizo gani lililopelekea kuwa katika hali ile. Hali iliyojitokeza ilikuwa tofauti na maelezo ya ajali yake, walijikuta wakifikia uamuzi wa kumrudisha Tanzania kwani waliamini hakutaka na mabadiliko yoyote kwa muda mfupi.
Matumaini ya kupata nafuu yalikuwa asilimia ndogo sana kuliko kupoteza maisha. Uhai wake waliamini hautachukua muda mrefu kwa vile mawasiliano hayakuwepo zaidi ya mapigo ya moyo yalienda kawaida pia hata mapafu yalifanya kazi vizuri.
Kilichowashangaza kuweza kupita kwa chakula laini na kufanyiwa kazi na kutoka kinyesi chepesi ambacho alisaidia bila habari. Mama yake alikuwa na kazi ya kumgeuza na kumsafisha anapojisaidia pia kumbadili ubavu ili kutoweka vidonda kwa kulalia upande mmoja kwa muda mrefu.
Mama Cecy naye alikata tamaa ya mwanaye kupona kutokana na kutotokea mabadiliko yoyote makubwa zaidi ya kuweza kutazama na kula kitu kilichokuwa kikitia matumaini kidogo.
Baada ya jopo la madaktari kukubaliana kumrudisha Tanzania, kwa kuamini kwa kuwa Tanzania ataweza kupata vitu viwili, moja kulikava taratibu akiwa nyumbani hivyo kupunguza gharama. Pili hata akifa wasipate gharama za kuusafirisha mwili wa marehemu.
Walimwita mama Cecy kumpa taarifa zile walizokubaliana kuhusu mwanaye kurudishwa Tanzania. Baada ya kuingia kwenye ofisi ya madaktari bingwa alikaa kitini huku akiwa na mkalimani daktari aliyeongozana naye.
“Mama Cecy, tumekuita hapa ili kukujulisha hatua tuliyofikia, inaonesha ugonjwa wa mwanao utachukua muda mrefu kupona. Hivyo tumeamua kumrudisha Tanzania ili uweze kumhudumia nyumbani pia kupata msaada wa matibabu ya kusaidia kuusisimua mwili.”
“Mmh! Sasa itakuwaje ikiwa hospitali inayotegemewa mmeshindwa, mwanangu si ndiyo anakwenda kufa?”
“Hapana si kufa bali huduma za muhimu tumejitahidi kadri ya uwezo wetu, hatuwezi kuendelea kumweka hospitali na kuongeza gharama wakati huduma zingine anaweza kuzipata akiwa hukohuko Tanzania. Sisi kazi yetu kubwa tumemaliza kilichobakia na kazi ya Mungu.”
“Mmh! Sawa.”
Mama Cecy alikubali kwa sauti ya kukata tamaa kwani siku zote watu waliokwenda India hurudi wamepona na ikishindikana basi mtu huyo huwa wa kumzika. Aliamini ile ilikuwa kauli ya kumpa moyo lakini siku za kuishi mwanaye zilikuwa zinahesabika.
Iliandaliwa mipango yote ikiwa pamoja na tiketi ya kurudi Tanzania na kupangiwa siku ya kurudi. Habari zile zilikuwa pigo mujarabu moyoni kwa mama Cecy mwanaye mmoja kama mboni ya jicho lake alimuona akitoweka katika sura ya dunia. Lakini yote alimuachi Mungu kwa vile muweza wa kila kitu.
Taarifa za kurudishwa Tanzania Cecy baada ya ugonjwa wake kuonekana utachukua muda mrefu kupata nafuu. Zilimfikia mama Colin na kuamini ile ndiyo nafasi ya pekee kwa Mage kuichukua nafasi ile baada ya kupata uhakika hali ile inaweza kuchukua muda mrefu kupata nafuu au maisha yake yote yawe ya kitandani alijua ilikuwa kuwapa moyo lakini Cecy alikuwa maiti mtalajiwa.
Kwa taarifa ile aliamini mwanaye pamoja na msimamo lazima atabadilika na kukubali kumuoa Mage huku akijitolea kumsaidia Cecy kwa kumwekea mtu wa kumhudumia na kumlipa kwa maisha yake yote ili tu kumfurahisha mwanaye.
Alitamani siku moja aitwe bibi na hakuwa na mtoto mwingine zaidi ya Colin ambaye ndiye aliyemtegemea kumleta mjukuu. Ugonjwa wa Cecy ulionesha hakukuwa na dalili zozote kuweza kubeba ujauzito na yeye kupata mjukuu. Moyoni alijikuta akipata mawazo mabaya ya kumuua Cecy kama mwanaye atasimamia msimamo wake wa kutotaka kuoa mwanamke mwingine.
Lakini kuna kitu kilimtisha baada ya kukumbuka kauli ya mwanaye kufunga ndoa hata na maiti ya Cecy. Hiyo ilimpa wakati mgumu. Lakini alipanga kumtumia Mage kuyabadili mawazo yake na kukubali kumuoa. Siku ya pili Mage alifika kama alivyoelekezwa na mama Colin lakini hakutakiwa kuonana na Colin mpaka mpango wake autekeleze.
Baada ya Mage kufika alifikia chumba cha msichana wa kazi na mama Colin alikwenda chumbani kwa Colin kumwamsha ili ajiandae kwenda hospitali.
“Jiandae basi ukafanye mazoezi.”
“Sawa mama.”
Colin aliingia bafuni kuoga baada ya kuoga alibadili nguo na kutoka chumbani kwake na kwenda kukaa sebuleni kumsubiri mama yake ili waende kwenye mazoezi ya viungo (Physiotherapy). Mama Colin alitoka chumbani kwake akiwa tayari kwa safari begi lake begani. Colin alipomuona mama yake alinyanyuka ili waondoke.
Lakini ghafla alishtuka kumwona mama yake akiweka mkono kichwani katika paji la uso huku amekunja uso.
“Nini mama?” Colin alishtuka.
“Kichwa,” mama alisema kwa sauti ya kujilazimisha.
“Mungu wangu! Kimefanya nini tena mama yangu?” Colin alishtuka na kujitahidi kumfuata mama yake ili amshike.
“Hapana baba , niache nitakaa mwenyewe,” mama Colin alisema huku akisogea kwenye kochi na kukaa.
“Nipe maji,” alisema akiwa ameinama mkono kichwani.
Colin alipotaka kwenda kumchukulia maji alimkataza na kutaka amwambie msichana wa kazi. Baada ya kuitwa alileta maji kwenye glasi na kumpa mama Colin aliyeyanywa yote na kupumua pumzi nyingi kisha alisema.
“Duh! Afadhali kidogo.”
“Sasa itakuwaje maana kwa hali hiyo huwezi kuendesha gari?”
“Na kweli siwezi kuendesha gari, nimekumbuka Mage alisema atakuja kukuona asubuhi.”
“Mage gani?”
“Si aliyekuwa mchumba wako.”
“Mama niseme mara ngapi kuwa sitaki kumuona yule shetani wa kike,” Colin alisema kwa hasira kidogo.
“Mwanangu wewe ndiye uliyekuwa ukinieleza siku zote nisikae na jambo baya moyoni muda mrefu naweza kupata matatizo. Kwa nini unamchukia hivyo Mage? Hata kama alifanya kosa lililosababisha ajali bado alitakiwa kusamehewa. Humtaki kuwa mpenzi wako lakini bado ni mwanadamu anayetakiwa kusamehewa na kumwona rafiki, hujui adui wa leo ni rafiki wa kesho.”
“Ni kweli mama, najitahidi kumsamehe lakini moyo wangu umekuwa mzito.”
“Huyo ni pepo mchafu tunatakiwa kumkemea.”
“Sawa mama nitajitahidi.”
“Kwa vile siwezi kuendesha gari leo basi naomba Mage atatupeleka hospitali.”
“Sawa mama,” Colin hakutaka kukataa kwani angemuudhi mama yake.
“Ngoja nimpigie simu.”
Mama Colin alijifanya kipiga simu na kujizungumzisha peke yake:
“Eeh! Umekaribia... tena umefanya vizuri... wahi basi utupeleke hospitali...haya tunakusubiri... Umekaribia... sawa... hakuna tatizo tupo tayari,” mama Colin alijifanya kukata simu.
“Kwani kafika wapi?” Colin aliuliza.
“Yupo nje ya geti.”
“Sawa.”
Mama Colin alijifanya kuelekea upande wa vyumbani na kwenda chumba cha msichana wa kazi na kwenda kuzungumza Mage.
“Mambo yamekwenda vizuri japokuwa imenibidi nilazimishe kwa cheo cha umama, sasa pitia mlango wa nyuma kisha ingilia mlango wa mbele kujifanya ndiyo unaingia.”
“Sawa mama.”
Mage alitokea mlango wa nyuma na kwenda kulichua gari alilokuwa amelipaki nje na kuingia nalo. Aliteremka kwenye gari na kuingia ndani.
“Karibu mama.”
“Asante, za hapa?”
“Nzuri.”
Mage alisogea kwa Colin na kumsalimia:
“Umeamkaje?”
“Namshukuru Mungu.”
“Nina imani hali yako itatengemaa muda si mrefu ili urudi katika majukumu yako, sara zangu zote hukutanguliza mbele nina imani Mungu ataipokea.”
“Amina.”
“Mage tunaweza kwenda.”
Mage alimshika mkono Colin na kunyanyua, alitoka naye hadi nje na kuingia kwenye gari la Mage ambalo aliomba walitumie kwa siku ile. Colin muda wote alikuwa kimya hakutaka kutia neno kwa kuhofia kumuudhi mama yake ambaye muda huo aliamini kabisa hali yake siyo nzuri hakutaka kuharibu kote kwani bado hali ya mpenzi wake Cecy ilibakia kitandawili.
Walikwenda mpaka kwenye kitengo cha mazoezi ya viungo (Physiotherapy), walipofika mama Colin alikaa pembeni na Mage alimsaidia Colin kufanya mazoezi kwa kumshikilia sehemu zingine ambazo alihitaji msaada. Kila dakika Mage alikuwa akitokwa na machozi kitu kilichomshtua Colin.
“Mage unalia nini?”
“Sijui moyoni mwako una hasira kiasi gani juu yangu.”
“Sina hasira yoyote.”
“Hapana Colin una kitu kizito juu yangu kutokana na yaliyotokea, ile ni mipango ya Mungu tu, naomba Colin unisamehe najutia kilichotokea ni mapenzi ndiyo yaliyonisukuma kufanya vile. Hata kama hutaki kuwa na mimi naomba unione rafiki na si adui.”
“Mage ningekuwa sijakusamehe tusingekuwa karibu hivi na kuweza kukusikiliza.”
“Nashukuru Colin kwa kunisamehe, naamini wewe ni mume mwema hakika Cecy kapata lulu kwenye chaza.”
“Nashukuru.”
“Vipi hali ya Cecy?”
“Kwa kweli mpaka sasa sijajua, mama amekuwa akinificha japo walinieleza inaendelea vizuri.”
“Mungu atamsaidi siku moja atasimama na kufanikisha mlichokipanga,” Mage alimpa moyo kinafiki.
“Amina.”
“Colin.”
“Naam.”
“Baada ya Cecy moyoni mwako yupo nani?”
“Bado sijamuona labda mwenetu atakaye zaliwa.”
“Basi naomba baada ya mwenenu nafasi inayofuata nipe mimi, naomba usiniweke mbali na mawazo yako.”
“Hakuna tatizo.”
“Naomba niwasiliane na wewe wakati Cecy yupo mbali.”
“Mage, suala la mawasiliano naomba tuliweke pembeni kwanza.”
“Kwa nini Colin, kukujulia hali tu.”
“Ukitaka kuwasiliana na mimi tumia simu ya mama lakini kwa sasa sitatumia simu kwa vile ndiyo iliyoleta yote haya.”
“Colin basi hujanisamehe.”
“Kukusamehe si kunilazimisha kufanya vitu nisivyo vitaka, nimekueleza sitaki kutumia simu unanilazimisha kwa kisingizio cha kutokusame. Kumbuka ubishi huo ndiyo uliosababisha yote haya.”
“Nimekuelewa Colin, nisamehe sana, nitajitahidi kukuelewa ili tusije kosana tena.”
“Itakuwa vizuri.”
“Colin nashukuru kunisamehe moyo wangu sasa mwepesi nilikuwa kama nimebeba mawe.”
“Kawaida katika maisha kuna kukosana na kupatana.”
“Nashukuru sana.”
Mama Colin aliyekuwa mbali kidogo mazungumzo yale yalimtia moyo na kuamini mpango wake umeweza kufanikiwa kwa kuamini Mage ndiye chaguo lake la awali kabla Cecy kuingilia penzi lile. Taarifa ya kurudishwa Cecy kutoka India hakutaka kumweleza haraka mwanaye mpaka akapotua nchini kwani kwa taarifa siku inayofuata ndiyo aliyokuwa akiwasilia nchini.
Alipanga kuonesha ushirikiano mkubwa lakini alibakia na siri yake juu ya Cecy na ugonjwa wake ambao kama ulishindikana India basi Tanzania ilikuwa ni kusubiri kifo. Kumweka Mage karibu na Colin kungemsaidia kumweka karibu kimapenzi hata akifa Cecy basi Mage achukue nafasi ile.
Baada ya mazoezi walirudi nyumbani huku kila mmoja akiwa na furaha moyoni mwake japokuwa furaha ya Colin ilikuwa usoni na mdomoni lakini moyoni bado halikosa raha kushindwa kupata mawasiliano ya kujua hali ya mpenzi wake Cecy. Lakini aliamini baada ya muda hali yake itatengemaa na yeye mwenyewe kwenda India kumuona Cecy.
Siku ile Mage alishinda pale na kufanya kila kitu kwa ajili ya Colin, kuanzia usafi wa chumba chakula cha mchana vyote alifanya yeye na muda mwingi alikuwa karibu yake ili kuhakikisha anairudisha nafasi iliyoipoteza kupitia matatizo ya Cecy. Kitu kile kilimfurahisha sana mama Colin na kuuona mpango wake taratibu utafanikiwa.
Siku ile taarifa ilifika kwa Cecy anawasili toka India, mama Colin hakutaka kumwambia mwanaye ila saa sita usiku alikwenda kuwapokea pekle yake. Baada ya ndege tukutua abiria waliteremka na kutoka nje.
Alisimama macho yakiwa ndani huku akijiuliza Cecy atarudi katika hali gani, akiwa mapokezi alikiona kitanda kikisukumwa nyuma yake alikuwepo daktari aliyeondoka naye na nyuma ya daktari alikuwepo mama Cecy ambaye alionekana amepururuka mwili kutokana na matatizo ya mwanaye.
Mama Colin alijitokeza kuwapokea kwa kumkumbatia mama Cecy.
“Jamani dada karibuni, poleni na safari.”
“Mungu ni mwema.”
“Karibuni,” alikwenda kitandani kumwangalia Cecy ambaye muda huo alikuwa amepitiwa usingizi.
“Vipi anaendeleaje?”
“Tutazungumza nyumbani, vipi Colin naye anaendeleaje?”
“Kweli Mungu ni mwema anaendelea vizuri.”
Kwa vile alikuwa amekuja na gari aina ya Toyota Noah aliyeelezwa ndiyo inayotakiwa kumpokelea mgonjwa, walimweka kwenye gari na kuelekea nyumbani kwa mama Cecy ambako siku ile kulifanyika usafi na kuiweka nyumba katika hali nzuri. Hivyo walikuta nyumba ipo vizuri pamoja na msichana wa kazi aliyeachwa kwa ajili ya kuangali nyumba kwa muda wote ambao hakuwepo.
Baada ya kufikishwa nyumbani aliingizwa chumbani na kulazwa kitandani, muda wote mama Colin alimfuatilia Cecy na kuonesha hakuwa na dalili zozote za kupona. Pamoja na huruma kumjia lakini bado aliamini kama Cecy atakufa basi Mage ndiye mbadala wake.
Baada ya kumlaza kitandani daktari aliyekwenda na Cecy India alikaa na wazazi wawili na kuwaeleza:
“Jamani nina imani maelezo tulipewa India unayakumbuka, lakini kwa kuongezea ninataka kuwaeleza, mgonjwa hali yake bado japo kuna mabadiliko makubwa sana tofauti na alivyokwenda. Ugonjwa wa Cecy umekuwa tofauti na ugonjwa mwingine ambao madaktari bingwa wamekutana nayo huu kidogo umewala akili.
“Inaonekana mwili wa Cecy anajenga mawasiliano taratibu sana inaweza chukua muda mrefu sana kunyanyuka kitandani. Hivyo anatakiwa uangalizi wa karibu sana, kama kuna uwezekano aajiliwe mtu kwa kazi hii ili kumpumzisha mama yangu hapa kwani namhurumia amefanya kazi kubwa usiku na mchana kwa ajili ya kumwangalia mwanaye japo nilimsaidia bado muda wote alikuwa halali.
“Mgonjwa ataendelea kupata huduma ya kuchuliwa kila siku mwili mzima ili kusisimua misuli ya mwili. Nina imani kwa uwezo wa Mungu anaweza kupata nafuu upesi kwa vile mwisho wa akili ya mwanadamu ndipo uwezo wa Mungu huchukua nafasi yake,” dakta Mariamu Shaka aliwapa moyo kwa maneno ya hekima.
“Nina imani mpaka leo yupo hivi lazima turudishe shukrani zangu kwa Mungu wetu,”mama Colin alisema.
“Kingine mama, huoni maajabu pamoja na mwili kukosa mawasiliano lakini vitu vyote vya ndani vinafanya kazi hata kuweza kula japo chakula laini kitu ambacho kimewashangaza hata madaktari bingwa.”
“Ni kweli tuna kila sababu ya kumshukuru alichotupa si haba, kama leo katupa kidogo na kurudisha shukurani kwake basi hatasita kutupa kikubwa nina imani mwanangu siku moja atasimama,” alisema mama Cecy kwa hisia kali.
“Amina, Mungu wetu ni msikivu,” alijibu dokta Mariamu.
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda mama Colin aliaga kurudi nyumbani na kumwacha mama Cecy mgonjwa na daktari ambaye alilala pale ili kesho yake baada ya kumpatia mgonjwa huduma arudi nyumbani kwake.
Kutokana na hali aliyomuona nayo Cecy hakutaka kumweleza mwanaye kwa kujua atamshtua hata kukosa raha na kumuongezea matatizo kwa vile alimpenda sana mchumba wake. Lakini alijiuliza mwanaye akijua lazima atamweleza vibaya, alipanga kumwambia baadaye kuwa Cecy amerudi.
Aliamua kukaa kimya huku wiki ilikatika bila kumweleza kitu chochote mwanaye juu ya Cecy kurudi toka India. Siku zote alitoka peke yake kwenda kumwona Cecy na kuonesha kugushwa na hali ile huku akimlipa daktari aliyekwenda naye India pesa nyingi ili kumpatia huduma ya kumchua na kumwangalia kila siku baada ya kazi.
Wema wake ulikuwa wa mamba wa kutoka machozi lakini alikuwa na siri moyoni mwake kujionesha anamjali mgonjwa. Lakini aliamini kupona kwa Cecy ni ndoto, kila alipoulizwa na mama Cecy kuhusu hali ya Colin alisema hajambo kiasi.
“Hawezi kutembea?”
“Mmh! Kwa sasa amekatazwa kutembea.”
“Kwa nini basi usimlete aje amwone mchumba wake?”
“Atakuja hali yake ikitulia.”
“Kwa hiyo hali yake inaonekana bado.”
“Ni kweli.”
“Mmh! Mpe pole isingekuwa hali ya Cecy ningekuja kumwona mkwe wangu.”
“Mungu atawapa afya na kuweza kunyanyuka.”
“Mungu atasikia dua zetu, kila jambo la heri Mungu ulishika mkono nina imani Cecy na Colin watasimama na siku moja kusherehekea harusi yao.”
“Amen,” mama Colin aliitikia huku moyoni akijisemea “Labda harusi aliyosema mwanaye ya kufunga ndoa na maiti ya Cecy, lakini harusi ya sherehe ukumbuni itakuwa muujiza.”
Mama Cecy aliamini hali ya Colin ni mbaya ila mama yake anampa moyo, alipanga siku akipata nafasi afike kumwona kwani haikuwa vizuri mzazi mwenzie kuja kumuona mwanaye na yeye kutokwenda kumuona Colin. Kwa vile hali ya mwanaye alijua alipanga siku moja baada ya kumpatia chakula akilala atoke mara moja kwenda kumwona Colin na kuwahi kurudi.
Siku ya tatu ambayo mama Colin alipiga simu kuwa hatakwenda kwa vile kuna sehemu ambapo angerudi usiku. Siku hiyo mama Cecy aliitumia kumwandaa Cecy ambaye alishangaa kuona mabadiliko madogo baadhi ya sehemu kupata joto kama miguuni ambako kulikuwa na ubalidi kwa muda mrefu.
Baada ya kumpatia chakula chepesi na dawa alimwacha apumzike na yeye kukodi gari mpaka kwa mama Colin kumjulia hali mgonjwa. Wakati huo Mage alikuwa akiendelea kuwa karibu na Colin ili kujivuta karibu kwa kuamini baada ya kifo cha Cecy basi nafasi ile ni yake.
“Colin nina imani sasa hivi afya yako ni nzuri unaweza hata kuendesha gari.”
“Namshukuru Mungu, pia nashukuru kwa msaada wako kwangu kwa muda wote wa kuniangalia.”
”Usijali nipo kwa ajili yako, nitapigania afya yako hata kwa gharama yoyote.”
“Usiwe na wasi nina imani sasa hivi sijambo na wiki ijayo nitakwenda India kumwangalia Cecy.”
“Lakini hali yako si bado kwa nini usisubiri upone kabisa.”
“Mage, mimi sijambo sasa hivi naweza kufanya lolote, lakini afya ya mpenzi wangu siijui. Mpaka leo bado yupo hospitali huenda yupo kwenye hali mbaya lazima niende nikajue hali yake.”
“Mmh! Sawa,” Mage aliogopa kutia neno kwa kuhofia kukorofishana na Colin ambaye alionekana bado ana mapenzi mazito na Cecy. Alijua msimamo wake ni kwa vile hajamwona lakini akimwona hali yake aliamini lazima angebadili mawazo na nafasi ile kumpa yeye.
Wakiwa katika ya mazungumzo walishtuliwa na hodi, waliponyanyua macho Colin hakuamini kumwona mama Cecy aliyejua yupo India na mpenzi wake, lakini afya yake ilioneka imedhoofu sana.
“Ha! Mama ni wewe?” Colin alisema huku akinyanyuka na kwenda kumpokea mama mkwe.
“Ni mimi mwanangu, unaendeleaje na wewe?”
“Namshukuru Mungu, hali yangu sijambo. Sasa hivi nilikuwa nasema wiki ijayo nakuja India kumwona mchumba wangu. Ha..ha..lafu mbona uko huku Cecy umemwacha na nani hospitali?”
“Kwani mama yako hajakwambia?”
“Kuhusu nini?”
“Kurudi kwetu, nimemuulizia ameniambia hali yako bado si nzuri, hivyo nikaona nije nikujulie hali baba yangu na kumwacha mchumba wako na msichana wa kazi.”
“Mama unataka kuniambia Cecy yupo Tanzania?” Colin alishtuka huku macho yamemtoka pima.
“Colin unauliza ukweli au unatania?”
“Mama mimi na wewe hutujawahi kutaniana, hata muulize Mage muda si mrefu nilikuwa namwambia lazima nije India kumjulia mchumba wangu hali yake baada ya mimi kuamini nimepona.”
“Siamini unachokisema najua unaumwa hivyo hukuwa na uwezo wa kuja kumpokea mchumba wako, lakini sikubali kauli yako kuwa huna taarifa yoyote kuwa mimi na Cecy tupo nchini kwa wiki sasa.”
“Wiki!?” Colin alishtuka.
“Colin hebu acha kujitoa akili, ina maana mama yako hajakwambia?”
“Hajaniambia, ina maana mama anajua?”
“Mbona ndiye aliyetupokea na kila siku lazima afike kumuona mgonjwa kasoro leo.”
“Mmh! Una maanisha mama yangu, mama Colin?”
“Ndiye huyohuyo, ina maana hajakwambia?”
“Haki ya Mungu sijui kitu, sikuwa ugonjwa wa kushindwa kuja kumpokea mpenzi wangu, kwa nini mama kanificha hivi, Cecy mpenzi wangu atanielewa vipi?” Colin alisema kwa uchungu.
“Sijui, labda muda wake wa kukueleza bado, lakini namshukuru sana amejitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha afya ya mpenzi wako inatengemaa.”
“Vipi hali ya mpenzi wangu?”
“Bado, lakini ana afadhali kwa mbali sana.”
Colin alinyanyuka na kumwomba mama Cecy aende akamwone mpenzi wake.
“Mama naomba nikamwone mpenzi wangu.”
“Colin pumzika kwanza hujapona vizuri, nilikuja kukuona tu.”
“Hapana...kama Cecy ana wiki hapa mama kanitendea unyama mkubwa sana,” Colin alisema huku akionekana kuchanganywa na taarifa zile ambazo hakutegemea kusikia kwa kuamini Cecy bado yupo India.
Colin hakusema kitu alikwenda ndani na kuchukua ufunguo wa gari na kutoka.
“Mama naomba twende,” Colin alipagawa na kusahau muda mfupi alikuwa na Mage alitoka bila hata kumuaga na kumfanya Mage aumie moyoni kuona ana kazi kubwa ya kuubadili moyo wa Colin. Lakini aliamini kifo cha Cecy ndiyo tiketi yake ya kuwa na Colin, aliendeleza dua za kuomba kifo cha Cecy.
Colin japo alikuwa hajaruhusiwa kuendesha gari alikwenda kuchukua gari na kumwomba mama Cecy waondoke. Waliongozana hadi kwenye gari na kuondoka kuelekea kwa Cecy. Wakiwa ndani ya gari Colin alimdodosa mama Cecy.
“Mama kwanza vipi hali ya mchumba wangu?”
“Hajambo, lakini bado.”
“Bado nini kinamsubua?”
“Siwezi kukueleza kwa vile unakwenda mwenyewe kila kitu utakiona.”
“Mmh! Sawa.”
Colin aliendesha gari huku akiwa na mawazo mengi juu ya mama yake kukaa kimya huku kila siku anakwenda kumwona mgonjwa bila kumwambia aljiuliza alikuwa na maana gani na mchumba wake angemwelewa vipi kama amerudi bila kwenda kumwona.
Walipofika walikwenda hadi ndani, Colin alionekana mwenye kimuhemuhe cha kumwona mpenzi wake. Kwa vile alikuwa akikijua chumba cha Cecy aliingia moja kwa moja. Lakini chumbani kwake hakuwemo alitoka na kukutana na mama Cecy.
“Mama mpenzi wangu yupo wapi?” Colin aliuliza macho yamemtoka pima na presha juu.
“Colin taratibu umefika utamuona, subiri,” mama Colin alisema huku akielekea chumba alicholazwa Cecy.
Alipakaribia alipogusa mlango alishtuka kusikia Cecy akimwita sauti ambayo ilipotea toka alipopata ajali iliyokuwa ikimwita.
“Ma..a..ma...ma..a..ma.”
Alisogea haraka kitandani na kuitikia.
“Abee mwanangu.”
“Nigeuze nimechoka kulala hivi?”
Mama Cecy aliona ule ni muujiza mkubwa kwake kwa vile siku zote mgonjwa alikuwa wa kulala bila kujitikisa wala kusema neno zaidi ya kutumbua macho tu bila kuyapepesa. Alimgeuza na kumlaza vizuri.
“Niwekee mto chini.”
Mama yake haraka alichukua mtu na kumwekea mwanaye.
“Mama ulikuwa wapi?”
“Nilikuwepo nje.”
“Mbona dada alisema ulitoka?”
“Nilifika dukani.”
“Mume wangu Colin yupo wapi?”
“Yupo sebuleni.”
“Ana fanya nini?”
“Ndiyo amefika sasa hivi.”
“Alikuwa wapi?”
“Kwao.”
Cecy kusikia Colin yupo sebuleni alitaka kunyanyuka na kuishia kukaa kitako na kurudi tena chini. Kitendo cha kujinyanyua peke yake yalikuwa maajabu mengine kwa mama Cecy ambaye alipiga ishara ya msalaba na kumsukuru Mungu kwa kile alichokionesha muda ule mbele yake.
“Asante Mungu... Asante baba... Asante kwa kila akifanyacho mbele ya macho yangu.”
“Mama,” Cecy alimwita mama yake.
“Abee.”
“Naomba niende kwa Colin.”
“Subiri.”
Mama Colin alitoka hadi sebuleni ambapo Colin alikuwa akizungumza na dada wa kazi juu ya hali ya Cecy. Alimdodosa na kuelezwa yote toka akipofika na hali aliyokuwa nayo na maajabu ya siku ile alipokuwa akimtengeneza kitandani na kushtuka kumsikilia akiiita jina la Colini na baadaye aliita mama yake.
Dada wa kazi alimweleza ametoka, ndipo alipoanza kumuuliza maswali ambayo alimjibu kwa vile mambo mengi alikuwa akiyaelewa. Baada ya mazungumzo na dakika ishirini Cecy aliomba kugeuzwa tofauti na siku za nyuma alikuwa wa kulala tu na kugeuzwa kwa kipindi.
“Kwa hiyo toka apate ajali ndiyo kazungumza leo?”
“Ndiyo najua hata mama ataona muujiza.”
“Mmh!” Colin aliguna na kujiuliza nini hatima ya mpenzi wake ikiwa sehemu inayotegemewa na watu wote imeshindwa. Ile kwake ilikuwa picha mbaya sana kwake na kukiona kifo cha Cecy kipo mbele. Aliamini yote aliyasababisha yeye alijikuta akitokwa na machozi ya uchungu.
“Colin baba,” Colin alishtuliwa na mama Cecy.
“Naam mama,” Colin aliitikia huku akinyanyua kichwa.
“Ha! Unalia nini tena?” mama Cecy alishtushwa na machozi ya Colin.
“Inauma.”
“Cecy anakuita.”
Colin bila kujibu alinyanyuka na kuelekea chumbani ambako alimkuta Cecy amelala kitandani mwili ukiwa umepururuka kwa ugonjwa.
“Cecy,” aliita kwa sauti huku akisogea kitandani na kumkumbatia mpenzi wake.
“Colin mume wangu,” Cecy alisema huku akijitahidi kumkumbatia mpenzi wake.
Ilikuwa ajabu nyingine Cecy kuweza kumkumbatia Colin kwa mwili uliobakia mifupa mitupu.
“Ni mimi Cecy mke wa maisha yangu.”
“Colin nifurahi kukuona mpenzi wangu japokuwa nina muda mrefu nilikuwa siwezi kuzungumza wala kujigeuza. Lakini kuja kwako kumekuwa dawa ya kupona kwangu. Hata nikifa sasa hivi moyo wangu utakuwa na furaha kwa vile nimekuona chakula cha nafsi yangu,” Cecy alisema kwa sauti ya chini.
“Ni kweli naamini Mungu alituumba kwa ajili yetu, siamini niliyoyasikia na niliyo kutana nayo leo,” Colin bado alikuwa kama yupo ndotoni.
“Ni Mungu tu mpenzi wangu.”
Siku ile Colin alishinda pale mpaka jioni pembeni ya Cecy, pamoja na yeye hali yake kuwa katika uangalizi lakini hali aliyomkuta nayo mpenzi wake aliamini amepona kabisa. Jioni daktari aliyempeleka India alipopitia kuangalia hali mgonjwa wake alishikwa na mshangao baada ya kukuta hali ya Cecy ina mabadiko makubwa.
“Mungu mkubwa siamini ninachokiona leo,” mama Cecy alisema huku akifuta machozi kwa kiganja cha mkono.
“Ni kweli Mungu katenda muujiza wake,”Colin alisema huku naye akifuta machozi.
“Jamani msinililie tena, kama nilikuwa nusu mfu kwa muda mrefu na leo nipo hivi, basi aminini nimepona,” Cecy alisema kwa kujiamini.
Siku ile kazi ya masaji aliifanya Colin huku akimpa moyo mpenzi wake kuwa atapona.
“Kweli nitaweza kutembea? Maana kwa hali ya kulala kitandani kama nyoka nimechoka.”
“Utapona tena na kusimama, nakuahidi baada ya kupona nakufanyia bonge la surprise.”
“Colin nawe kwa kunipa moyo, je nisipopona?”
“Ugonjwa utakuwa wetu sote.”
“Hutafuti mwanamke mwingine?”
“Cecy baada ya kukufungia moyoini mwangu ufunguo niliutupia baharini, mimi ni kipofu mbele yako. Wewe ndiye uliyekuwa mwanamke wa mwisho kuonwa na macho yangu. Siamini kama nitapenda tena katika maisha yangu kama tutatengana. “Nakupenda Cecy zaidi ya kupenda. Amini usiamini muda si mrefu utasimama na kutimiza ndoto yetu ya kuwa mke na mume.”
“Colin sikuwahi kumwamini mtu katika maisha yangu lakini wewe kwangu sina la kuongeza nakuamini mpenzi wangu. Mungu ana maajabu yake amani kila litendekalo lina makusudio yake.”
“Cecy Mungu waajabu wewe ni yule wa jana leo na kesho, Mungu alikupa azina ya busara na hekima ni mtaji mkubwa katika maisha yetu.”
“Asante kwa kulitambua hilo.”
Pamoja na Cecy kuwa mgonjwa aliweza kuzungumza mengi mpenzi wake mpaka ulipofika muda wa kumwacha apumzike. Colin hakutoka alilala pembeni ya mpenzi wake. Daktari Mariam alishangazwa na hali aliyomkuta nayo Cecy ulikuwa muujiza mkubwa maishani mwake.
“Kweli Mungu mkubwa hutenda pasipo mtu kutegemea, siamini... siamini kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu wetu,” dokta Mariam Shaka alichanganyiwa na hali aliyomkuta nayo Cecy.
Dokta Mariam alisema baada ya kumwona Cecy akijigeuza kitandani na kumwita mpenzi wake.
“Colin.”
“Naam mpenzi.”
“Nataka kwenda msalani.”
Colin alimnyanyua na kumkalisha kisha aliomba chombo cha kujisaidia na kupewa, kazi yote ya kumhudumia mpenzi wake alifanya mwenyewe. Baada ya kumwogesha alimrudisha kitandani. Baada ya huduma zote dokta Mariam alimchunguza ilionesha kila kiungo kimepata ufahamu.
Kila alipomminywa kwa nguvu alipiga kelele, ile ilikuwa dalili nzuri kuonesha mwili mzima umeisharudisha mawasiliano. Baada ya kufanyiwa uchunguzi alikalishwa kitako na kuelezwa aliyekuwepo mbele yake ni dokta Mariam Shaka dokta aliyekwenda naye India kwa siku zote alizokuwa naye huko katika kukuchua mwili.
“Asante dada yangu Mungu atakulipa,” Cecy alisema huku machozi yakimtoka.
“Usijali, Mungu mkubwa naamini muda si mrefu utasimama tena, hatua ya leo ni kubwa kweli kila lililo zito kwa mwanadamu kwa Mungu ni jepesi.”
“Hakika,” alisema mama Cecy.
Colin alikuwa karibu muda wote kuonesha jinsi gani anavyomjali mpenzi wake ambaye aliamini ni mwanamke wa maisha yake. Siku hiyo kila kitu Colin aliomba amfanyie mpenzi wake. Ilikuwa faraja kubwa kwa Cecy ambaye pamoja na kuwa bado mgonjwa lakini ukaribu wa kipenzi chake uliongeza faraja moyoni mwake.
***
Upande wa pili baada ya Colin kuondoka na mama Cecy, Mage hakuondoka alibakia kumsubiri Colin kwa kuamini kutokana na maelezo ya mama yake Cecy alikuwa nusu mfu mtu wa kulala tu. Hivyo asingekaa muda mrefu angerudi mapema na kumkuta, alitumia muda mwingi kuangalia mikanda ya video.
Mama Colin alirudi saa mbili kasoro usiku na kumkuta Mage peke yake amejaa tele sebuleni. Mage alipomwona mama mkwe zilipendwa alinyanyuka na kumpokea.
“Wawooo, karibu mama.”
“Asante mwangu, za kushinda?”
“Mmh! Nzuri.”
“Mbona kwanza umeguna kabla ya kujibu.”
“Hamna mama.”
“Mwenzio yupo wapi?”
“Ametoka.”
“Ametoka! Kaenda wapi?”
“Kumwona mgonjwa.”
“Mgonjwa! Mgongwa gani?”
“Cecy.”
“Cecy! Nani kamwambia kama Cecy yupo?” mama Colin alishtuka kusikia habari zile.
Alipomuona anaingia alihamisha macho kwenye runinga na kumtazama mlangoni alikuta ni mama Colin. Alinyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda kumpokea.
“Karibu dada.”
“Asante,” mama Colin alijibu kwa sauti ya chini huku akificha hasira zake juu ya kitendo cha mzazi mwenzie kwenda kwake na kufanya mwanaye amchukie kwa kumficha kuwemo kwa mpenzi wake nchini.
“Karibu, Vipi hujafika nyumbani?” Mama Cecy alimshangaa usiku ule wakati alisema siku ile hawataonana.
“Colin yupo wapi?” mama Colin aliuliza kwa sauti kali kidogo.
“Dada hata salamu unakimbilia kumuulizia Colin?”
“Salamu si muhimu kama kujua hali ya mwanangu.”
“Mwanao hajambo.”
“Sitaki kusikia hajambo bali kumwona yupo au ameondoka?”
“Yupo chumbani na mchumba wake.”
“Chumbani? Anafanya nini?”
“Mama Colin ni swali gani hilo, ina maana chumbani kwangu kuna mzoga?” mama Cecy alijibu kwa hasira.
“Siyo hivyo dada, si unajua Colin bado mgonjwa mpaka sasa sijui yupo wapi.”
“Colin na Cecy nani mgonjwa na ugonjwa mwanangu kautoa wapi, mbona tumekwenda vizuri tunataka kuharibu mwisho?”
“Basi samahani dada najua Cecy anaumwa, lakini sijui Colin yupo wapi maana nilimwacha nyumbani amesikia amekuja kumwona mchumba wake.”
“Nimekujibu nini?”
“Sawa ngoja nikamwone.”
Mama Colin alielekea chumbani kwa mgonjwa akiamini atamkuta mwanaye pembeni ya kitanda huku akiumizwa na hali ya mpenzi wake aliye katika hali unusu mfu. Alipofika alipigwa na butwaa kumkuta Colin akimlisha Cecy matunda.
“Ha!” mama Colin alijikuta akipiga ukelele wa mshtuko.
“Aah! Mama karibu, Mungu mkubwa kuja leo mpenzi wangu kanyanyuka kama ningekuja mapema sasa hivi angekuwa hajambo kabisa,” japo yalionekana maneno ya kawaida lakini yalikuwa kama mkuki moyoni mwa mama Colin.
“Ha! Kweli Mungu mkubwa Cecy umenyanyuka mama!” mama Colin hakuamini alichokiona mbele yake.
“Karibu mama mkwe, sina cha kukulipa ina namuomba Mungu anipe afya niweze kukulea mama yangu katika maisha yangu yote. Umeweza kupigania maisha yangu kwa hali na mali. Naamini kabisa kwa Mungu hakuna kinachoshindikana, karibu mkwe,” Cecy alisema huku akijiweka vizuri.
“Asante mkwe wangu, Mungu ni muujiza ninachokiona mbele yangu ni kazi ya Bwana aliyotenda.”
Mama Colin alikwenda kumkumbatia Cecy ambaye alikuwa amepururuka na kubaki mifupa mitupu. Mama Cecy naye alikuwa amefika hakutia neno zaidi ya kukaa kimya akimwangalia mzazi mwenzie.
“Jamani leo ni katika siku ambazo nimepata furaha ya ajabu, nakuahidi kuipigania afya ya Cecy kwa gharama yoyote ili kuhakikisha anarudi katika hali yake ya zamani,” alisema mama Colin.
“Asante mkwe sina cha kukulipa bali kukuonesha mapenzi ya dhati yasiyo na chembe ya unafiki.”
“Asante mkwe wangu,” mama Colin alijikuta akitokwa na machozi kwa maneno mazito ya Cecy ambaye alipoteza kauli na viungo vya mwili kufanya kazi kwa zaidi ya miezi sita.
“Jamani nina imani Mungu ni mkubwa ameweza kutusimamia kwa hiyo tumshukuru kwa pamoja kwa kuweza kutenda juu yangu,” Cecy alisema huku akitaka kuteremka kitandani.
“Baki kitandani tutaomba ukiwa hapahapa kitandani,” Colin alimzuia mpenzi wake.
“Naomba niteremke ili nipige magoti pia kwa kauli yangu kufunguka naomba niongoze maombi kumshukuru Mungu.”
Baada ya wote kupiga magoti na kufumba macho Cecy alianza kuomba:
“Asante baba Mungu kwa wema na utukufu wako, umekuwa nami muda wote wa maradhi na mateso yangu mazito ambayo kila mwanadamu alikata tamaa lakini baba ulikuwa nami muda wote.
“Baba sina cha kukulipa zaidi ya kukuabudu kwa kufuata yote unayotaka tuyafanye na kuyaacha yote uliotukataza. Baba rudisha furaha mioyoni mwa wote waliopoteza matumaini na kuwafanyia wasiyo yategemea rudisha furaha kati nyumba yetu iliyopotea kwa muda mrefu tupe afya njema.
“Baba kila aliyetokwa na machozi kwa mayeso yetu mfute na umpe furaha kama kuna aliyefurahia matatizo yetu baba msamehe kwa vile hajui atendalo. Umetuumba wanadamu kwa udongo ulio safi basi tupe mioyo yetu upendo tupendani tuoneane huruma na kuombeana mazuri.
“Asante Baba kwa kuninyanyua leo, asante kwa kurudisha furaha iliyitoweka kwa muda mrefu katika familia zetu.Walipe mara mia wote waliotoa kwa ajili ya matatizo yetu. Baba yaliyotokea ni majaribu tupe imani ya kusimama upande wako na usimpe nafasi adui shetani kutupotosha.
“Baba timiza ndoto yetu ya mimi kuwa mke halali wa Colin, Baba Mungu nashukuru kwa kunichagulia mume mwema mwenye mapenzi ya dhati, nami namwahidi kuwa mke mwema katika siku za pumzi zangu. Simamia ndoa yetu ondoa kila jicho la hasada roho chafu za chuki, uongo na uadui kwa jina la mwanao Yesu Kristo aliye hai, Ameni.”
“Ameni,” waliitikia pamoja huku kila mmoja akifuta machozi kutokana na maombi mazito aliyoporomoshwa na Cecy.
“Naombeni maji,” Cecy aliomba maji baada ya kuomba kwa muda mrefu na kuvunjwa jasho kama maji, kutokwa na jasho jingi ulikuwa muujiza mwingine kwa mama Cecy baada ya kutotoka jasho jingi kwa zaidi ya miezi sita.
Alipatiwa maji na kuomba kupumzika, Colin alimpandisha kitandani na kumfunika shuka.
“Colin mpenzi napumzika kidogo ila usiondoke wewe ndiyo furaha yangu.”
“Sawa mpenzi.”
Walimwacha Cecy amelala na kutoka nje kwa ajili ya mazungumzo.
“Jamani kuna nini kimefanyika ambacho mimi sikijui?” mama Colin aliuliza.
“Hakuna kilichofanyika na muujiza wa Mungu, wakati narudi nilisikia Cecy ananiita nilipoingia nilishtuka kumwona akiniita. Nilipomsogelea sikiamini kumwona mwanangu katika hali ile kwani niliisha kata tamaa.”
“Kweli nimeamini muujiza wa Mungu upo,” alisema mama Colin.
“Ni kweli.”
“Sasa kwa vile nilikuwa nimekuja ghafla wacha nikapumzike pia tumwache mgonjwa apumzike ili kesho tujue tutafanya nini.”
“Dokta Mariam amesema lazima tumpeleke hospitali akafanyiwe vipimo.”
“Hakuna tatizo, Colin baba,” alimgeukia mwanaye.
“Naam mama”
”Itaidi tuondoke ili ukapumzike kwa vile nawe hali yako haijatengemaa vizuri.”
“Mama mimi nimepona kabisa mgonjwa ni Cecy na nipo hapa kwa ajili ya kuhudumia kwa kila kitu.”
“Sawa, lakini twende nyumbani tutakuja kesho.”
“Mama naomba unisamehe, leo siondoki nitalala na mpenzi wangu.”
“Mmh! Sawa.”
“Nikutakie usiku mwema.”
Mama Colin alimkumbatia mwanaye kisha alimuaga kuelekea alipopaki gari. Alimkuta Mage amesinzia baada ya kumsibiri kwa muda mrefu, alipofika alimwamsha.
“Mage pole kwa kukuweka.”
“Isijali mama mkwe, vipi mbona umechelewa Colin ameisha ondoka?”
“Yupo.”
“Mbona umemwacha?”
Mama Colin alimweleza Mage yote aliyoyakuta na kumfanya asindwe kuamini na kujikuta akiuliza:
“Mama unayosema ni kweli?” Mage hakuamini.
“Kweli kabisa, yaani nilichokiona mbele yangu ni muujiza Cecy amenyanyuka tena anaonekana kama mtu aliyepata nafuu wiki nzima.”
“Mmh! Nimekwisha!” Mage alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Kwa nini unasema hivyo?” mama Colin alishtuka.
“Mama kweli Colin atanioa?”
“Sikudanganyi, Colin anampenda sana Cecy, hakuna kiumbe kitakacho mbadili mawazo, yaani nimemkuta kama mwenda wazimu sijui Cecy angekufa mwanangu angekuwaje.”
“Mmh! Sawa,” Mage alisema huku nguvu zikimwisha na kujikuta akijilaza kwenye usukani badala ya kuondoa gari.
“Vipi mbona hivyo?”
“Mama kupona kwa Cecy ni pigo zito moyoni mwangu, hapa nilipo sina hata nguvu za kuendesha gari. Naomba mama yangu uendeshe naweza kugonga.”
“Hakuna tatizo.”
Mama Colin alizunguka upande wa pili ili kuendesha gari baada ya Mage kupatwa na mshtuko kutokana na Cecy kupona. Mama Colin alishangazwa na hali ya Mage kubadilika ghafla baada ya kupata taarifa ya kupata nafuu kwa Cecy.
“Mbona umekuwa hivyo?”
“Mama basi tena.”
“Lakini Mage hukutakiwa kununua pilipili kwa shughuli ya mwenzio ile ilikuwa pata potea. Nafasi uliichezea mwenyewe huna wa kumlaumu.”
“Mmh! Sawa.”
Kutokana na kutokuwa kwenye hali nzuri Mage alilala palepale ili kuitafuta siku ya pili, mama Colin naye alikuwa na maswali yasiyo na majibu juu ya hali ya Cecy kubadilika kabisa wakati alikuwa nusu mfu. Lakini upande mwingine alimshukuru Cecy kupona kama angekufa mwanaye angekuwa chzi kwa jinsi alivyopagawa kwa mpenzi wake kupona.
***
Siku ya pili Cecy alichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake, majibu yalionesha kila kitu kimo sawa. Majibu yale yalikuwa faraja tele kwa Colin na kwa mama Cecy ambao ndiyo walioteseka kipindi chote cha ugonjwa wa Cecy.
Alitakiwa kufanya mazoezi kutokana na viungo kukaa muda mrefu bila kufanya kazi, afya ya Colin ilikuwa imetengemaa aliomba kwenda kupumzika na mchumba wake Afrika ya kusini kwa miezi miwili.
Wazazi hawakuwa na jinsi walikubali watoto wao waende Afrika ya kusini kupumzika na kuendelea kupata huduma za kiafya. Baada ya siku mbili Colin na Cecy walielekea Afrika ya kusini katika mji Port Elizabeth katika hotel ya The Beach Hotel kwa ajili ya mapumziko baada ya mateso ya muda mrefu.
Colin alichukua muda ule kuhakikisha anafuta machungu yote aliyoyapata mpenzi wake kutokana na ajali mbaya iliyowapata ili kurudisha imani kwake kwa vile Mage alionekana bado yupo karibu na familia yao hasa mama yake hivyo kutia doa upendo wake.
Muda mwingi walitumia kukaa wawili chumbani kila asububi na jioni walifanya mazoezi madogo madogo katika Gim iliyowa katika hoteli waliyofika na majira ya saa moja walitembeatembea pembezoni mwa ufukwe. Lilikuwa penzi lililozaliwa upya kwa wapendao baada ya kupoteana kwa kipindi kirefu.
Baada ya wiki mbili Cecy naye kimwili kilianza kurudi wakiwa wamejipumzisha chumbani kwao, Cecy alimuuliza mpenzi wake ambaye aliamini alikuwa na ufahamu tofauti na yeye alikuwa nusu mfu.
“Colin nina imani wakati naumwa ulikuwa karibu na Mage.”
“Si kweli, huwezi kuamini toka ile ajali sina ukaribu na mtu nilikuwa sitoki ndani hata simu kuanzia siku ile situmii. Najua Cecy huniamini lakini nakuhakikishia niliapa mbele ya mama yangu na mama Mage walipokuja kuniona hospitali kuwa sitaoa mwanamke mwingine kama wewe ungekufa.
“Niliwaeleza kama utakufa nitatimiza ahadi niliyokuahidi kwa kufunga ndoa na maiti yako na nisingeoa tena mpaka nakufa.”
“He! Kwa nini ufanye hivyo, ningekufa mimi si ingekuwa nafasi ya mwingine. Heri tungekuwa tumezaa ulikuwa na sababu ya kufanya hivyo.”
“Cecy kuoa mwanamke mwingine wakati ajali nimesababisha mimi ningekuwa nimeshiriki kwenye kifo chako. Wewe ndiye wakili wa moyo wangu umenitetea wakati wote wa matatizo yangu. Bila wewe kitendo alichonifanyia Mage ningeweza kuwa chizi.”
“Asante kwa kunipenda kwa kipindi chote cha mateso yangu, Colin nimeamini wewe ni mume wa maisha yangu naomba Mungu adumishe penzi letu ufe nikuzike nife unizike.”
“Asante mpenzi wangu nitakupenda siku zote za maisha yangu.”
“Hata mimi, Colin,” Cecy alimwita mpenzi wake akimtazama usoni.
“Naam.”
“Siku ya kuondoka ulikataa kubeba simu sasa tutawasiliana vipi na nyumbani?”
“Nimeapa sitatumia tena simu katika maisha yangu kwani ndiyo sababu yakutaka kuyachukua maisha yetu. Pia wazazi nimewajulisha tupo hoteli gani wakitutaka watupata tukiwataka tutawapata kwa njia ya simu ya hotelini.”
“Colin, naweza kusema wivu wangu wa kijinga umetufikisha hapa, sikutakiwa kukosa imani kiasi kile cha kutaka kila kitu katika simu yako nikione. Naweza kusema nilijitakia mwenyewe. Nimejifunza kitu sikutakiwa kukubana kiasi kile kwa vile mapenzi ya kweli yako moyoni na wala si kwenye simu.
“Colin nilikupenda kupitiliza na kujikuta nakuwa kichaa wa mapenzi kwa ajili yako, lakini umenidhilishia kwa vitendo kuwa unanipenda mapenzi ya dhati kwa vile hukuyumba wakati wa matatizo yangu. Angekuwa mwanaume mwingine angekwisha kuwa na mchumba mwingine au ameisha funga ndoa.
“Colin mpenzi wangu nakuomba kuanzia leo hii tumia simu, mimi si limbukeni tena wa simu. Upendo na uaminifu wako ameufanya moyo wangu uwe huru na kukuamini kwa asilimika mia. Colin najivunia kuwa na mwanaume kama wewe nimekutafuta kwa udi na uvumba japo mama yako alifanya utani kuniita mkwe lakini niliamini nami nina haki ya kuwa na mwanaume nimtakaye aliye katika hali yoyote.
“Asante Colin kugeuza mazoea ya maskini hana haki ya kupenda, nipende Colin nikupende, Colin unajua wewe ndiye mwanaume wangu wa mwanzo na wa mwisho. Nakupenda Colin zaidi ya kupenda.”
“Cecy najua thamani yako moyoni mwangu ni zaidi ya madini yote unayoyajua na usiyo yajua. Niliapa moyoni mwangu sitakupoteza mtetezi wa moyo wangu. Cecy mpenzi wewe ni zaidi ya mwanamke ni malaika wangu.”
“Asante mpenzi, ila hujanihakikishia utatumia simu?”
“Cecy nilitaka kuacha kutumia simu kwa ajili yako, lakini kwa vile umeniruhusu nitatumia.”
“Colin.”
“Naam.”
“Nina ombi moja naomba ukikubalie kwani toka nimefika hapa kuna kitu kimekuwa kikinisumbua jibu lako ni faraja ya moyo wangu.”
“Cecy malkia wangu, sema chochote nitakitekeleza.”
“Kuna kitu nimejifunza kwako kila unapotaka kufunga ndoa kuna tokea matatizo umeisha lingudua hilo?”
“Dah! Kweli kabisa mpenzi hilo jambo hutokea.”
“Sasa nitaka tufanye kitu tofauti katika safari yetu hii.”
“Kitu gani?”
“Tufunge ndoa kabisa hukuhuku tukurudi tuwe mke na mume.”
“Mmh! Lakini ndoa yenye baraka lazima wazazi wawepo.”
“Wazazi tutawaita huku tukirudi Tanzania tunafanya sherehe tu.”
“Sawa hakuna tatizo.”
Walikumbatiana kwa furaha walizima taa ya mwanga mkali na kuwasha ya mwanga hafifu kila mmoja aliyasikia mapigo ya moyo wa mwenzake.
***
Mage alionekana kuchanganyikiwa kutokana na taarifa za kupona kwa Cecy mwanamke aliyejua ni wa kufa siku yoyote. Kilichomchanganya zaidi ni kugeuka kwa mama Colin kusimama upande wa Cecy wakati mwanzo alimpa moyo wa kumpata mwanaye.
Akiwa bado hajajua atafanya nini alipata taarifa iliyomkata maini ya Colin kwenda Afrika ya Kusini na mchumba wake kwa ajili ya mapumziko ya muda mrefu. Lakini hakutaka kukata tamaa alianini njia ya kumpata Colin ni ni kumuua Cecy au kumtia kilema ambacho kitamfanya asiolewe na Colin.
Wazo la kuua aliliweka kando kwa muda kwa kuamini lile lingekuwa la mwisho kabisa baada ya mipango ya awali kuferi. Aliamini anaweza kutumia njia nyingi kuhakikisha Cecy aolewi na Colin. Mpango ulikuwa kumwagia tindi kali au kutuma vijana kubaka na picha zake kusambazwa kitu ambacho aliamini Colin na familia yake wasingekivumilia lazima angempiga chini Cecy.
Mpango wake alipanga kuupanga kabla ya Colin na mpenzi wake kurudi kutoka Afrika ya kusini. Alijua ndoa ingechukua muda ili kusubiri afya ya Cecy iimalike naye angetumia nafasi ile kumtia doa Cecy na yeye kuichukua nafasi aliyokuwa akiitafuta usiku na mchana kama wokovu baada ya mwenyewe kuichezea shilingi kwenye tundu la choo.
Aliapa kutumia kiasi chochote cha fedha kuhakikisha anampoteza Cecy na kulimiliki penzi la Colin. Walijipanga kutafuta watu ambao angewalipa kiasi cha pesa watakachokubaliana ili wamfanyie kazi yake kwa uhakika bila mtu yeyote kujua kitu.
Wakati akiwaza hayo taarifa ya kuitwa Afrika ya kusini iliwafikia wazazi wa Colin na Cecy kuwa wanatakiwa mara moja. Japokuwa hawakujua wanaitiwa nini, walikubaliana kuondoka kwenda kuwasikiliza watoto wao wana lipi. Baada ya siku nne Colin na Cecy waliwapokea uwanja wa ndege wa Port Elizabeth na kuwapeleka katika hoteli ya The Beach waliyofikia wao.
Wote walifarijika kukuta afya ya Cecy imeimalika haraka na nuru yake ya awali ikianza kuonekana kwa mbali. Ilikuwa furaha kwa familia kukutana wote wakiwa katika hali ya furaha. Usiku wa siku ile baada ya chakula walikaa pamoja kwa ajili ya mazungumzo.
Mzungumzaji mkuu alikuwa Cecy ambaye ndiye aliyemuomba Colin aseme yeye.
“Wazazi wetu najua mmeshtuka na wito wetu wa ghafla, lakini wito huu una maana kubwa katika maisha yetu watoto wenu. Wito huu ni kwa ajili ya kuja kusimamia harusi ya watoto wenu.”
“Watoto wetu kina nani?” mama Colin aliuliza.
“Ya mimi na mume wangu Colin ambayo tumepanga kuifunga wiki ijayo.”
“He! Mbona haraka sana kwa nini mnataka kufungia huku?” aliuliza mama Cecy.
“Mama kuna kitu kiliniijia haraka akilini mwangu ambacho nilikiamini kabisa na nilipomwambia mwenzangu ambaye alikubaliana na nilichokiona na kukubaliana kufunga ndoa huku.”
“Kitu gani?” mama Colin aliendelea kuuliza.
“Nilifuatilia hatua zote za harusi za mpenzi wangu ambazo huvurugika mwishoni, mfano wa kwanza muda mfupi kabla ya kumuoa Mage lilitokea tatizo lililomjeruhi moyo mpenzi wangu. Mfano wa pili muda mfupi kabla ya ndoa yetu likatokea la kutokea, hivyo imeonesha kuna tatizo.
“Nilichokiwaza mimi ni kuhusiana matukio yote hivyo naamini huku tutafunga ndoa isiyo na starehe ambayo itakuwa na baraka ya wazazi wa pande zote. Kwa hiyo wazazi wetu tunaomba mkubali ombi letu ili tukirudi Tanzani tuwe tayari mke na mume. Kuhusu sherehe tutaifanya tukijipanga.”
“Mmh! Colin we ulikuwa unasemaje?” mama Colin alimuuliza mwanaye.
“Mi namuunga mkono mpenzi wangu amekuwa na jicho la tatu ambalo wote tulikuwa hatuna.”
ITAENDELEA
Your Thoughts