RIWAYA; NGOMA NGUMU.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SIMU; 0758573660/0624155629.
SEHEMU YA PILI..
“Zuki Gadu!?” Amolo aliuliza kwa mshangao.
“Yes, huyohuyo. Huyo ndiye anaeweza kuifanya kazi hii. Mwenyewe hupenda kuijiita Miguu ya kuku, akipita haachi nyayo, wala sauti ya vishindo vyake, haisikiki” Kamonga alisema huku akisimama na kuzungusha shingo yake, mbele ya kaka zake.
“Wewe ulimjuaje huyu jamaa?” Atumba alimuuliza.
“Miguu ya kuku aliwahi kuwa mlinzi wa Baba, hivyo anatufahamu vema, pia anauwezo mkubwa sana wa kufanikisha mambo yake. Anafaa kwa kazi hii” Kamonga alijibu kwa uhakika.
“Sasa mlinzi binafsi ataweza kweli kashikashi za serikali? Unatushangaza bwana mdogo” Mhisani aliongea bila kuficha wasiwasi wake.
Ulikuwa mtihani mkubwa, majina matatu mezani, lakini lilihitajika jina moja tu ili kazi ifanyike. Kazi nzito na ya hatari. Ilihitajika plate namba tano kutoka Benki ya Umoja, Benki yenye ulinzi kuliko Benki zote ndani ya jiji la Nairobi.
“Awezaye kuifanya kazi hii ni Miguu ya kuku, achaneni na Sajenti Nyau na huyo jamaa mwingine.” Kamonga aliendelea kuwashawishi wenzake.
“OK! Tuamue kwa kusema, wote ni wazuri. Je, tutampa vipi mzuri zaidi?” Amolo aliamua kufupisha mjadala.
“Nadhani tuyachambue maongezi yao. Mtu makini hupimwa kwa weledi wa ulimi wake.” Tindo alishauri.
“Inaweza kuwa njia nzuri, lakini ni kama tunacheza kamari tu.” Amolo alionesha wasiwasi wa njia iliyoshauriwa.
“Ndugu zangu, kama tunautaka utajiri, ni vema tukamtumia Miguu ya kuku. Hawa wengine nadhani wanafahamika vema kabisa, sioni umuhimu wa kuwapigia simu. Tunaweza kuwapigia, ikawa ni njia moja wapo ya kufanya tukafuatiliwa tunachopanga kufanya hapa Nairobi. Hili jambo libaki kuwa siri ya familia tu.” Kamonga aliongea kwa sauti, huku akipigapiga meza kuonesha msisitizo wake.
Ukimya ukashika hatamu, kila mmoja aliwaza lake. Ilikuwa ni ngumu kumwamini mtu mmoja, kufanya kazi ngumu na ya hatari namna ile. Ilikuwa ni vema waifanye wenyewe, kwa sababu walikuwa na; pesa, nguvu kazi ya vijana wao watiifu pia, walikuwa na vifaa vyote ambavyo vingelihitajika kukamilisha kazi yao.
Hili jambo la mpango wao uliyowagarimu muda na pesa nyingi, kufanywa na mtu mmoja, huku wao wakiwa washuhudiaji, lilikuwa linawaungurumisha matumbo
“Anyway, tumpe kazi Miguu ya kuku. Akifeli ni rahisi sisi kumkataa na kwa nguvu tulionayo, ni rahisi kumkataa na tukaendelea na mpango wetu kwa njia nyingine” Mhisani aliamua kumaliza mjadala kwa kukubaliana na matakwa ya mdogo wake wa mwisho, ambae alipendekeza namna ya kukamilisha wizi ndani ya benki ya umoja.
“Lete namba zake za simu tumpigie” Amolo alisema huku akitoa simu yake mfukoni.
“Huyu jamaa mambo ya kazi huwa anatumia email ama Threema, simu ni kwa maongezi ya kawaida tu.” Kamonga alimwelekeza kaka yake.
“Duh!” Amolo aliguna huku akifungua viboksi vya simu yake, kisha alitafuta kikasha cha email na kukifungua na kuingiza anuani aliyotajiwa, kisha akatuma ujumbe mfupi uliyosomeka; ‘NEEDED!’
Alitulia kidogo na kupokea ujumbe kutoka kwa Miguu ya kuku. Ulisomeka; ‘SYMPATHY or ELSE?’
Amolo alimgeukia Kamonga na kumwonesha ule ujumbe.
“Mjibu Sympathy” Kamonga alimwelekeza.
Haraka Amolo alituma majibu kama alivyoelekezwa. Sekunde chache ujumbe ulijibiwa kwa swali.
‘5W?’ Ujumbe ulisomwa kwa sauti. Wote hawakuelewa alimaanisha nini, isipokuwa Kamonga pekee ndiye aliyetambua ilikuwa na maana gani, haraka aliamua kuwaelekeza wenzake kwa namna alivyoelewa.
“Hiyo inatumiwa na wanausalama kumhoji mtuhumiwa ama shahidi, pia ni somo kwa waandishi wa habari, linalowaongoza kupembua habari zao.” Alinyamaza kidogo na kisha aliendelea.
“….5W hutumika kuhoji, yaani husimama badala ya maneno; When, Where, Why… Hivyo nadhani anahitaji kujua sisi ni nani, tuko wapi, kwa nini tunamhitaji.”
“Kwa hiyo tumjibu vipi sasa!”
“Jitambulishe!”
Amolo aliingia kikashani na kumwandikia ujumbe uliyosomeka hivi; ‘SADON BROTHERS!’
Sekunde chache baadae, ujumbe wao ulijibiwa kwa maneno machache tu.
‘THREEMA,UXC!’ Amolo aliusoma tena kwa sauti, ni kama alihitaji kufafanuliwa ulivyomaanishwa ujumbe ule.
“Anahitaji kupigiwa kupitia threema!” Kamonga alisema huku akichukua simu yake na kuingunisha na runinga kubwa iliyokuwa ukutani, kisha alipekua kikasha cha Threema kwenye simu yake na kupiga kwa njia ya mtandao. Iliita kidogo na kupokelewa upande wa pili na sura ya mtu aliyekuwa amekaa sofani, ilijaa kwenye runinga kubwa iliyokuwa kwenye kile chumba kilichokuwa kimebeba ndugu watano.
Walikuwa wanaonana mubashara na Zuki Gadu p.a.k Miguu ya Kuku.
“Kuna kazi ya kufanya ndani ya siku tatu zijazo.” Mhisani alianza kuzungumza.
“Kazi hiyo ni nyepesi, lakini ni ngumu vilevile, kwa sababu inahitajika kumwaga damu ikibidi, ama kutumia akili nyingi ili kuweza kuifanikisha.” Alimeza mate na kuendelea.
“Ndani ya Benki ya Umoja, kuna plate za kutengeneza pesa. Zipo plate tisa, ila sisi tunahitaji plate moja tu, ambayo ni plate namba tano.”
“Umoja Bank, plate namba tano!” Miguu ya kuku alisema huku akichezea kompyuta yake, iliyokuwa mapajani. Punde akageuka na kusema.
“Nitahitaji kiasi cha milioni mia nne, kukamilisha kazi hii!”
Sadon Brothers walitazamana kwa mshangao, hawakuwa wametarajia kutajiwa kiasi kikubwa cha pesa kwa wizi pekee.
“Mbona pesa nyingi sana bwana!” Tido alisema kwa kuhamaki.
“Ni kawaida yangu kutoza pesa hiyo kulingana na uzito wa kazi, hivyo ni juu yako; kukubali ama kukataa na kuzima dili”
“Duh! Hii kiboko!!”
“Ninazo dakika mbili za kuzungumza na nyinyi, hivyo ni vema mkajielekeza kwenye mada.” Aliwambia bila kupepesa macho yake.
“Lakini unahakika utaweza kufanya kazi hiyo!?” Mhisani alimuuliza.
“Nipe kazi, nikishindwa itafahamika. Unachotakiwa kufanya ni, kuniwekea nusu ya malipo, kisha nusu utamalizia nikikamilisha kazi yako”
“Ok! Unakaribishwa Nairobi!”
“Ahsanteni! Lakini nina ombi moja!”
“Tunakusikiliza bwana Zuki!”
“Naomba nusu ya mpango wenu, muuvujishe bila kusema mnapotaka kutenda tukio na tukio la aina gani.”
“Heh!!” Jamaa walipigwa na mshangao. Wao walitegemea kufanya kwa siri, lakini sasa wanaambiwa wavujishe mpango huo.
Mtihani!!
“Mbona kama unataka tufanye kile ambacho hatukufikiria? Pia unataka kufanya kazi hii ionekane ngumu kupindukia!” Amolo alisema huku akijikuna kichwa chake kwa hofu ya kilichosemwa na Miguu ya kuku.
“Hakuna namna! Itabidi iwe hivyo ndugu zangu. Wizi wa benki ni tofauti na wizi mwingine. Akili yako ndiyo ushindi wako!” Zuki Gadu p.a.k Miguu ya kuku, aliendelea kushawishi.
“Kwa nini unataka mpango uvuje?” Mhisani alimuuliza.
“Nataka vyombo vya ulinzi na usalama, vikae chonjo nchi nzima, kisha nitumie makosa yao kutekeleza ninalowaza.”
“Mimi nadhani tukupe mikakati ya namna ya kutekeleza jambo letu. Tutakupa ramani na baadhi ya maelekezo kuhusu benki ya Umoja, kisha fanya kazi kwa urahisi zaidi.”
“Hapana! Mmenipa kazi, acheni nifanye kazi nitakavyo, msiniongoze. Mkakati wenu bakini nao, fanyeni mkakati wangu.”
“Kwa hiyo huo mkakati wako ni kututaka tuuvujishe mpango wetu?”
“Hivyo ndivyo itakiwavyo!”
“Tusipotekeleza itaathiri vipi mpango wako?”
“Inaweza kuniondolea ufanisi wangu, pia inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kukamilika, kuliko ambavyo ingevuja!”
“Hii kali aisee!” Mhisani alisema huku akiwageukia wenzake, ambao nao walikuwa wamesimama wakishangaa maelekezo ya mtu wao.
“Sawa, tutakutafuta dakika tatu zijazo.” Amolo alisema huku akikata mawasiliano na kumpa simu Kamonga.
Baada ya kuachana na Miguu ya kuku, Sadon brothers, walibaki peke yao ndani ya chumba cha mikutano, ndani ya jumba lao la kifahari. Walitazamana bila kusemeshana, huku kila mmoja akiwaza lake kichwani.
Ilikuwa ni ngumu kumwamini Miguu ya kuku, lakini haikuwa rahisi pia kufanya ile kazi peke yao. Vichwa viliwauma; mpango walouhitaji, pia walihitaji kufanya kazi na mtu wa nje ya kundi lao.
“Tufanye nini ndugu zangu!” Mhisani aliwauliza wadogo zake.
“Nadhani tumempata mtu sahihi, hatuna haja ya kujiuliza mara mbilimbili. Zuki Gadu, ni sahihi kuifanya kazi hii.” Kamonga aliendelea kuwashawishi wenzake.
“Hapa tatizo siyo Zuki, hapa tatizo ni kuvujisha mpango serikalini. Ni ngumu kulitekeleza hilo jambo!”Tindo aliongea kwa msisitizo.
“Kwanza tunakubaliana na gharama anazozihitaji?” Amolo aliwauliza wenzake.
“Hiyo ni pesa ndogo sana aliyoihitaji. Tatizo bado lipo kwenye kuvujisha mpango.” Mhisani alijibu.
“Tumpe pesa, ila tusivujishe mpango wetu uliyotugharimu pesa nyingi kukamilika. Hatuwezi kuuza gharama zetu kirahisi namna hiyo.” Amolo nae aliongezea.
“Naona tuuvujishe mpango kwa kumruhusu yeye mwenyewe auvujishe awezavyo, lakini tusivujishe mikakati yetu hata chembe!” Kamonga alishauri. Wenzake walimtizama.
“Upo sahihi! Tumpe hiyo kazi peke yake!” Tindo aliafiki.
“Na iwe hivyo!” Amolo nae alikubali, huku akimtizama Mhisani, ambae nae alitikisa kichwa chake kukubali kilichozungumzwa.
Haraka walimuunganisha Miguu ya kuku kwa njia ya mtandao.
“Kila ulichohitaji kitafanyiwa kazi, lakini kwa shariti moja tu!” Mhisani alimwambia Zuki Gadu p.a.k Miguu ya kuku.
“Nawasikilizeni!” Miguu ya kuku aliitikia.
“Tutaomba uvujishe mpango huo kwa njia zako.”
“Itabidi muongeze dau la pesa!”
“Eeh!!”
“Yes! Kwa sababu sijui mkakati wenu ulivyo, zaidi najua mnataka plate namba tano. Sijui mlivyokuwa mmejipanga kufanikisha hilo”
“Kwa hiyo tukiongeza dau, utavujisha mpango wako na si wetu?”
“Ndivyo ilivyo!”
Sadon Brother’s, walitazamana, kisha wakaafiki kuongeza dau. Ilikuwa rahisi kuafiki kwa sababu, mpango wao ulikuwa salama kuvuja.
“Sawa, ujapohitaji usaidizi, tuko tayari wakati wowote!”
Miguu ya kuku alifikiria kidogo, kisha akasema..
“ Haina ubaya! Lakini acheni nifanye kazi yangu kadri niwezavyo. Nyie mkae kimya na angalieni yatakayokuwa yanajiri. Msiingilie lolote.”
“Haina neno! Unakaribishwa Nairobi!” Mhisani alijibu na kumkaribisha Miguu ya kuku.
“Great!” Miguu ya kuku alijibu na kutoka hewani.
Baada ya Miguu ya kuku kutoka hewani, ndugu watano walibaki peke yao. Walijadili mambo machache, kisha walisambaratika na kila mmoja, alienda kuendelea na majukumu yake ya kujimaarisha zaidi kwenye kitengo chake.
ITAENDELEA.
