Ngoma Ngumu 03



RIWAYA; NGOMA NGUMU.

NA; BAHATI K MWAMBA.

SIMU; 0758573660/0624155629.

SEHEMU YA TATU..

DAR ES LAAM….


Miguu ya kuku aliweka simu yake pembeni, kisha aliegemea kwenye sofa na kutazama juu. Mawazo mengi yalipita kichwani mwake. Wazo moja lilikuwa zito zaidi kuliko mawazo mengine. Lilikuwa ni wazo ambalo lilimtia hofu kubwa.


“Nimefanya kazi nyingi, lakini sijawahi kuiba benki. Na kinachonitisha zaidi ni ulinzi ulioko kwenye mabenki, hasa ndani ya benki.” Alijisemea taratibu huku akijaribu kujenga picha kichwani mwake, kwenye baadhi ya mabenki makubwa nchini Tanzania.


“Hii ni kazi ngumu sana aisee!” Alisema huku akiishika laptop yake iliyokuwa mbele yake, juu ya meza. Aliparaza kidogo na ukatokea mchoro(picha) wa jengo refu lenye ghorofa zaidi ya kumi nane. Jengo lile lilinakishiwa kwa vioo, kuanzia chini hadi juu.


“Kazi ipo duh!” Alijisemea huku mkono mmoja ukiwa kidevuni na macho yake yakiwa yametulia kulitizama jengo lile. Aliendelea kulichunguza kwa umakini sana, huku akili yake ikifanya kazi kubwa kutafakari.


“Mara zote benki huwa zinakuwa chini kabisa ya majengo marefu namna hii!” Alijisemea huku akichezesha mshale wa kuongoza, kuelekea upande wa chini wa lile jengo.


“Kama ipo huku chini, ina maana, wanamiliki basement yote na huko ndiko iliko vault ya kuhifadhia pesa na vault ya kuhifadhia hizo plate!” Alijisemea tena huku akiendelea kuizungusha picha ya jengo refu, lililopewa jina la Patrice Lumumba, huku likiwa chini ya umiliki wa Nssf.


  Wakati alipokuwa akiendelea kupitia picha kadhaa za jengo lile, kuna kitu kingine aligundua na kitu kile kilimtia woga wa wazi kabisa na aliwaza kutema ndoano, endapo alichokuwa amegundua kingelikuwa sahihi. 


Haraka alianza kutafuta picha za satellite ili aweze kujiridhisha na kile alichokuwa amekigundua na kukitilia wasiwasi. 

 Jengo la Patrice Lumumba lilikuwa ni jengo refu sana na lenye uwekezaji mkubwa jijini Nairobi. Lilikuwa ni jengo ambalo lilijengwa kwa upekee sana. Lilikuwa ni jengo refu pekee maeneo ya Upper hill, huku kukiwa hakuna jengo lingine lau lenye ghorofa moja kwenye ule mtaa.


“Kwa nini ipo hivi?” Alijiuliza huku akizidi kumakinika na picha alizokuwa anazishuhudia kupitia kompyuta mpakato iliyokuwa mbele yake. Alizidi kuyatalii kwa macho maeneo jirani na jengo la Patrice Lumumba. Hapo ndipo mwili ulimsisimka zaidi.


Kwa nini!


Kwa sababu, jengo lile lilizungukwa na maeneo nyeti sana, ambayo si rahisi mtu kuyagundua, japokuwa mengine yalifahamika kirahisi. Jengo lile lilikuwa lipo katikati ya vikosi vya jeshi na vile vya usalama wa raia.

 

 Mashariki mwake kulikuwa na makao makuu ya jeshi la kujitegemea, huku Magharibi kwake kukiwa na kituo kikuu cha polisi cha Nairobi. Upande wa kaskazini kulikuwa na kambi ya kikosi cha anga(Moi air base), na upande wa kusini kukiwa na makao makuu ya chama tawala. 


“Sasa nimeelewa ni kwa nini jengo hili limeota peke yake bila kuruhusu majengo mengine ya aina hiyo! Huu utakuwa ni mtaa wa kimkakati hapo nchini Kenya!” Alijisemea huku akijishika kichwani kwa kujikwarua. Nywele ziliwasha kwa hofu ya kile alichokuwa anakiwaza.


“Mbona hii kazi inataka kunionjesha umauti?” Aliwaza huku akianza kutafuta umuhimu wa benki ya Umoja ndani ya nchi ya Kenya. 


Kulikuwa na maelezo mengi sana kuhusu benki hiyo, lakini hayakumuingia akilini, yalikuwa ni maelezo mepesi kuliko alivyotarajia.


“Maelezo haya, hayawezi kufanya nchi iweke hapo zile plate za fedha!” Alisema huku akitikisa kichwa na kuchukua simu iliyokuwa pembeni yake. Alitafuta jina alilohitaji, kisha alipiga na kuzungumza kile alichotaka kuzungumza. Lakini alichojibiwa, kilimfanya afikirie kuwapigia Sadon Brothers, na kuitema kazi aliyopewa.


Yalikuwa ni maelezo ya kuogofya kwa binadamu mwenye moyo wa nyama, ilihitaji kiumbe kisicho na damu kuvumilia na kuendelea kushikilia dili gumu namna ile. Dili lenye kuuza roho.


    Miguu ya kuku alikuwa amempigia simu mtu wake wa karibu, mtu ambae hufanya nae kazi kila inapotakiwa kufanya kazi. Huyu mtu alikuwa ni kiongozi wa kanisa ndani ya jiji la Nairobi. Mtu huyo aliitwa Mchungaji Emmanuel, alikuwa na jina lake la kazi za siri alizokuwa anafanya. Alikuwa ni muuzaji wa silaha, huku akitumia mgongo wa kanisa, kama kivuli cha kuifanya biashara yake hiyo, iliyokuwa imeshamiri sana nchini Congo na sasa alikuwa Nairobi kama sehemu ya kupanua mtandao wake. 


   Wengi walimfahamu kwa jina la Mchungaji Emmanuel, lakini Miguu ya kuku alimfahamu na pia alipenda kumuita Bob Rando. Mtu mwenye taarifa nyeti za kila nchi anayoitembelea. Mtu ambae alikuwa ni mfanikishaji mkubwa wa mipango yake.


“Nambie Zuki!” Mchungaji Emmanuel p.a.k Bob Rando, alianza kuongea baada ya kupokea simu.


“Safi Bob!” Miguu ya kuku alijibu.


“Najua umenipigia utakuwa upo mzigoni kama kawaida yako!”


“Hakika hujakosea Bob! Niko hapo Nairobi, lakini roho inasita kuendelea na jambo langu!”


“Mh! Leo hiyo!? Kama roho inasita, achia dili. Uhai ni muhimu zaidi kwa sasa” 


“Tatizo jamaa wameshafanya malipo ya awali, kitu ambacho kitanibana ni kanuni zangu, nikipokea huwa sirudishi hadi nikamilishe kazi”


“Kanuni zipo ili zivunjwe komredi” 


“Hujakosea! Lakini kanuni zangu hazina kipengele cha kuvunjwa!”


“Basi, fanya hiyo kazi kama huwezi kuivunja. Vaa mabomu, ingia mzigoni!”


“Ngoja nione hadi mwisho itakuwaje”


“Naamini akili yako bado haijachoka kuvunja mitego yote! Upo wewe ni zaidi ya mwanajeshi Zuki!”


“Sawa kwa kunipa nguvu upya, naomba unipe msaada kidogo kabla sijaja Nairobi”


“Kila siku nipo kwa ajili yako! Wewe ni zaidi ya ndugu. Wakati wote nipo kwa ajili yako, hadi siku nitakapoiaga Dunia!”


“Maneno mazito sana unaongea Bob! Naomba unisaidie kudukua jengo la Patrice Lumumba na ikibidi, unipe na unyeti wa Benki ya Umoja.”


“Taarifa zake unazihitaji lini?” 


“Hata kama unazo sasa hivi, nipe.”


“Nipe nusu saa!” Bob Rando alisema na kukata simu. 


  Miguu ya kuku alipumua peke yake, huku akiigeukia laptop yake. Kisha akaanza kusoma mikakati ya kifedha kutoka wizara ya fedha ya Kenya. Aliamua kusoma mikakati hiyo, kwa kuwa alijua kuna kitu kitakuwa kimepangwa na nchi ya Kenya kuhusu mipango fedha. 


“Plate namba tano, haiwezi kuwa na umuhimu kiasi hicho kama ingelikuwa haina jambo nyuma yake. Lazima kuna kitu kinachowasukuma hawa jamaa kuiba hii plate!” Alijisemea huku vidole vyake vikicheza kwa kasi kubwa na macho yake yakiwa makini, kutizama kilichokuwa kinapita kwenye kompyuta yake.


   Wakati alipokuwa akizipita ripoti kadhaa, hatimae alikutana na ripoti ambayo iliamsha hisia fulani kichwani kwake. Ripoti ilitolewa na katibu wa wizara, ripoti ilihusu mpango wa serikali kuchapa shilingi mpya, ambayo itaziba mianya ya wahujumu uchumi ambao wameondoa pesa kwenye mzunguko na kupelekea kuwe na hali ngumu ya uchumi. Ripoti ile iliendelea kubainisha kuwa; lengo la kufanya vile ni, kuwafanya watu walioondoa pesa kwenye mzunguko, kurejesha pesa hizo ili kuendana na matumizi mapya ya shilingi mpya. 


“Sasa hiyo plate na hili jambo vinaingilianaje?” Alijiuliza huku akiwa ameganda na asijue la kufanya.


“Hawa jamaa wanataka kuihujumu nchi yao bila shaka!” Alijisemea huku akiendelea kuperuzi habari nyingine.


“Nchi za wenzetu huko, haya makundi ya kihuni huwa yanamiliki uchumi wa nchi, yawezekana na hawa wanataka kulitenda hilo hilo nchini mwao!” Alijiwazia.


“Lakini hainihusu! Kazi yangu ni kutekeleza tu!” Alisema kwa sauti huku akiichukua simu yake iliyokuwa inaita pembeni yake.


ITAENDELEA.

Jaba Zulma

Siyumbi

Your Thoughts

Previous Post Next Post

Contact Form