Ngoma Ngumu 05



RIWAYA; NGOMA NGUMU.

NA; BAHATI K MWAMBA.

SIMU; 0758573660/0624155629.


 SEHEMU YA TANO..


****


   Alipofika chumbani alichukua kadi aliyokuwa ameiweka kitandani, kisha alichukua kiberiti cha gesi alichokuwa amekihifadhi kwenye begi lake. Aliuwasha mshumaa, kisha aliuchukua kadi ya benki na kuigeuza na kufanya kibati cha kadi kionekane sawia. Alipohakikisha kibati kimeonakana kama alivyotaka, alianza kudondosha tone za mshumaa kwenye kibati cha kadi yake ya benki. Alidondosha tone kadhaa kisha aliuzima mshumaa na kuuweka kwenye meza iliyokuwa ndani ya chumba. 


   Alipohakikisha mshumaa umezima, aliuchukua kadi ya benki na kufuta tone za mshumaa zilizokuwa zimeanza kuganda. Alifuta vema kabisa na kuhakikisha hakuna mabaki yanayoonekana. Alipomaliza zoezi hilo, alibadilisha nguo alizokuwa amevaa na kuvaa mavazi yenye heshima. Alivalia shati la mikono mirefu na suruali ya kitambaa na viatu vya mchomoko. 


 Alipokwisha kuvaa, alienda kujitizama kwenye kioo na aliporidhika na umaridadi wake, alichukua kadi yake ya benki na kutoka nje. 


 Alipofika nje, aliita moja wa madereva pikipiki waliokuwa wanapaki nje ya ile hoteli. 


“Nipeleke hapo umoja benki tafadhali” Alimwambia dereva. 


“Mh!” Dereva aliguna huku akimtizama kwa mshangao.


“Vipi, mbona wanishangaa?” Alimuuliza dereva.


“Nashangaa umbali mfupi kutoka hapa, unaitisha vipi usafiri?” 


“Wewe usijali, nipeleke tu!” 


“ Lakini si ni hapo kaka!” Dereva alisema huku akinyoosha mkono upande ambao ilikuwepo benki.


“Nadhani ufanye biashara kaka, kama huhitaji pesa yangu nitaita mtu mwingine!” 


“Ooh, basi twende ndugu!” Dereva alisema huku akikaa vema kwenye pikipiki yake. 


 Miguu ya kuku alidandia na kukaa na safari ya mita sabini, ilianza. 


  Walipokuwa wanakaribia kuingia kwenye maegesho ya magari na pikipiki, alichukua kalamu ya wino na kuipachika kwenye mfuko wa shati lake, kisha aliangalia saa yake ya mkononi na kuisimamisha majira yake.


  Alipokwisha kushuka kwenye pikipiki, alimlipa dereva na kumruhusu aondoke. Alipobaki peke yake kwenye maegesho, aliangaza huku na huko kama anaeyafananisha mazingira. Aliporidhika kuyatalii mandhari, alipiga hatua zake taratibu kuelekea upande wenye mashine ya kufyatulia pesa kwa haraka(ATM). Alipofika kwenye kibanda cha mashine hiyo, alipanga foleni kulingana na kukuta foleni ya watu sita wakingojea huduma. 


  Muda wote aliokuwa kwenye foleni, alikuwa anatizama saa yake mara kwa mara mithili ya mtu anaeiwahi usaili wa kazi. Wakati waliposalia watu wawili ili zamu yake ifike, alibonyeza saa yake na kutulia kama vile alifanya jambo la kawaida tu. 


   Baada ya kusuburi kwa muda mrefu, hatimae zamu yake ilifika. Taratibu alipiga hatua zake bila papara, huku jicho lake likizunguka mithili ya jicho la kinyonga lililoona sherehe ya nzi. Alikuwa anajaribu kuzitizama kamera za siri zilizofichwa ili kuchukua matukio yaliyokuwa yanaendelea kwenye kile kibanda cha mashine ya kutolea pesa. 


  Jicho lake kali lilifanikiwa kukutana na kamera zaidi ya tatu ambazo zilifungwa kwa siri na kulikuwa na kamera mbili ambazo zilikuwa wazi, kiasi kila mtu angeliweza kuziona. 


 ‘Bila shaka hizi kamera za siri ndizo zinazopeleka taarifa kwenye ofisi za usalama wa nchi na hizi zinazoonekana ni za ofisi za ulinzi kwenye hii benki' Alijiwazia huku akiweka kadi yake ya kutolea pesa, kisha alibofya hapa na pale na kuandika kiasi cha pesa alichotaka kutoa kwenye mashine. Alipomaliza, alisimama na kusubiri kwa sekunde kadhaa.


  Wakati mashine ilipoanza kuunguruma ili kupokea pesa kutoka kwenye Kuba(vault), yeye alikuwa anavuta pumzi nyingi na kutulia bila kuzitoa, akiwa na maana ya kuruhusu masikio yake yapokee kile alichokuwa anatarajia kukisikia kwenye ile mashine. 


   Alikuja kuzishusha pumzi zake, wakati pesa zilipoanza kutoka na yeye alitulia kusubiri kiasi alichoomba kikamilike. Wakati akingoja kiasi cha pesa kimalike ili aweze kumpa nafasi mtu aliyekuwa nyuma yake, ni wakati huohuo akili yake ilikuwa ikipiga hesabu za kujitetea na jambo alilokuwa analisubiria kwa hamu kubwa litokee kwenye ile mashine ya kutolea pesa. 


  Wahenga walisema; subira yavuta heri, hatimae kile alichokuwa anakingojea kwenye mashine, kilitokea kama alivyokuwa amefikiria. Mashine ilikuwa imepitiliza kutoa kiasi cha pesa alichohitaji. Pesa nyingi zilitoka kwa wakati mmoja huku mashine ikipiga kelele za kutoa tahadhari. 

Jambo lile lilimfanya aruke pembeni huku akitoa sauti ya hamaniko. Wale waliokuwa nyuma yake nao walisogea pembeni huku wakitaka kujua kulikoni.


  Miguu ya kuku hakuwajali, badala yake alisimama pembeni akishangaa kile kilichokuwa kinatokea pale kwenye mashine, huku akiishika saa yake kwa umakini mkubwa ambao si wa kutilia shaka. 

Alizima majira ya saa yake.


  Mlio wa tahadhari na sauti ya kuhesabu pesa bila kukoma uliwashitua walinzi waliokuwa eneo lile, ambapo walisogea haraka ili kujua kilichokuwa kinaendelea pale. Walipofika waliwaondoa watu wote, huku wakijaribu kuwasiliana na watu wa ulinzi wa pesa ndani ya benki, waweze kuzima mfumo wa utoaji pesa kwa mashine ya nje. 


 Wafanyakazi wa benki wengi walitoka nje baada ya tukio lile huku kila mmoja akijaribu kuuliza kilichotokea. Jitihada za kuiondoa kadi iliyokuwa imeng'ang'ania zilifanikiwa baada ya dakika saba. 

Miguu ya kuku alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamesimama pembeni wakitizama hekaheka za wafanyakazi ambao walikuwa wanafanya jitihada za kunusuru hali iliyotokea. Macho yake yalikuwa makini kumtizama kila manyakazi, huku umakini wake huo akiuelekeza kwenye vibanio vilivyokuwa juu ya mifuko ya sare zao. Alisoma majina na nyadhifa zao. Lakini hadi anawamaliza wafanyakazi wale waliokuwa wametoka nje, hakuwa amefanikiwa kusoma kile alichokuwa anakitegemea.


“Inawezekana kweli asiwepo?” Alijiuliza huku akiongeza umakini ili kuhakikisha kile alichokitaka kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi hao.


 “Nani mwenye kadi hii?” Ofisa mmoja wa ulinzi aliuwauliza watu waliokuwa wamekusanywa pembeni na kuzingirwa na moafisa wengine, kwa nia ya kuhakikisha hakutatokea hujuma yoyote kutoka kwa raia hao.


 “Ni yangu!” Miguu ya kuku alisema huku akiwa amenyoosha kidole juu na kuigiza sura yenye kutia simanzi.


 “Fuatana nami!” Mlinzi alimwambia huku akipiga hatua kuelekea ndani ya benki. Miguu ya kuku nae alifuata huku akijipongeza kwa kufanikisha hatua yake ya kwanza kwa mafanikio, japo hatua muhimu hakuwa na hakika kama itafanikiwa.

  Aliongozwa kuingia ndani ya benki, kisha akaelekezwa kuingia kwenye ofisi ya meneja wa benki ile maarufu jijini Nairobi. Baada ya kuingia, alikutana na sura ya mzee wa makamo, ambae alikuwa amesimama kwa kuegemea meza, huku miguu yake akiwa ameibebanisha na mikono akiwa ameifumbata kifuani. Kibanio kwenye mfuko wake kilimtambulisha kama Kaimu Meneja wa benki, na mezani kulikuwa na kibao kikubwa kikiwa kimelazwa na alipokisoma, kilikuwa na jina la kaimu Meneja, Mensa Munga. 


 “Karibu ukae hapo!” Meneja huyo alimwambia huku akimuonesha pahali pa kukaa. Miguu ya kuku alikaa huku akimtizama usoni.


 “Mchezo gani umeufanya kwenye mashine ya pesa?” Aliulizwa.


“Hakuna mchezo wowote nilioufanya. Hata mimi sielewi kimetokea kitu gani kwa kweli!” Alijibu Kinyonge.


“Kwa sasa tunaomba uache hapa vitambulisho vyako muhimu, ikiwemo hati ya kusafiria. Kisha wewe nenda kaendeleee na majukumu yako na sisi tutakutafuta baada ya kukamilisha uchunguzi wetu.” 


“Lakini nahitajika kwenye usaili wa kazi kesho. Natakiwa niwe na kila kitu unachohitaji nikiache hapa!” 


“Ilitakiwa uwe chini ya ulinzi hadi wakati huu, lakini tunaamua kukuacha kwa sababu za kidiplomasia. Hatuwezi kushikilia raia wa kigeni, bila kujiridhisha na tuhuma dhidi yake. Lakini pia haimaanishi kuwa tunakutuhumu kwa jaribio la wizi wa pesa, bali tutasema yote baada ya kujiridhisha na uchunguzi wa kilichotokea.” 


  Ukapita ukimya wa sekunde kadhaa, kisha Mensa Munga alisema..


“Nakuruhusu uendelee na majukumu yako mengine. Lakini karibu Nairobi, jisikie huru” 


“Ahsante!” Miguu ya kuku alijibu huku akitoa vitambulisho vyake na kuviweka juu ya meza ya Meneja, kisha akauvuta mlango na kutoka nje, ambapo alikutana na mlinzi aliyekuwa amemsindikiza. Walitoka kwa pamoja.


  Nje kulikuwa na umati wa maofisa wengi wa jeshi la polisi, wakiwa wamejizatiti na silaha nzito. Walikuwa wanaongeza ulinzi baada ya kupewa taarifa na uongozi wa benki, kuhusu tukio la mashine kumwaga pesa bila kikomo. Mafundi wa mifumo ya benki nao walikuwa wameongezeka, ili kubaini chanzo cha hitilafu hiyo.


  Miongoni mwa maofisa waliokuwa wameongezeka ni Sajini Nyau, ambae alikuwa ameongozana na Inspector mmoja aliyekuwa kiongozi wa msafara ulioenda kuongeza nguvu za ulinzi kwenye eneo lile.


   Mwanzo alikuwa kama anamfananisha Miguu ya kuku, lakini kadri Miguu ya kuku alivyokuwa anasogea ndivyo alivyoweza kumtambua bila uficho. Sajini Nyau alishangaa kumuona mtu yule eneo lile, alimfahamu vema kabisa na alizifahamu kazi zake. Ijapokuwa, hakuwahi kujua anafanya umamluki. Alimfahamu kwa kuwa aliwahi kuwa mlinzi binafsi wa kiongozi wa kwanza wa kundi la Sadon. Uwepo wake mazingira yale, ulimfanya ahisi kuna jambo haliko sawa ndani ya Nairobi, ijapokuwa hakuwa anajua ni jambo gani. 


ITAENDELEA.

Jaba Zulma

Siyumbi

Your Thoughts

Previous Post Next Post

Contact Form