RIWAYA; NGOMA NGUMU.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SIMU; 0758573660/0624155629.
SEHEMU YA NNE..
“Unauhakika, unataka kufanya hili jambo?” Bob alianza kwa swali baada ya mwenzake kupokea simu.
“Ni lazima nilifanye komredi!”
“Sasa sikia; ile Benki ya Umoja ni benki ya biashara, lakini ipo kwenye mikono ya serikali kwa asilimia zote. Yaani ile pale ni tawi la benki kuu, japo wananchi hawajui lolote, zaidi wanajua ni benki ya kibiashara tu. Lakini kikubwa zaidi, ile benki ndiyo yenye hazina yote ya nchi. Ina maana kwamba; hata vipande vya madini vimehifadhiwa pale ina maana, ile ndiyo roho ya nchi. Na kulithibitisha hilo, lile jengo limejengwa kwenda chini ghorofa mbili, na huko ndiko mzigo unaoutaka umehifadhiwa. Lakini…”
“Lakini nini Bob!”
“Huko chini, kuna ofisi za Usalama wa nchi na ina maana, kunalindwa saa ishirini na nne tena ulinzi mkali kuliko unavyodhani.
“Duh! Una maanisha, vault ipo kwenye hizo ghorofa za chini?”
“Exactly! Mzigo upo huko.”
“Duh!”
“Lakini ngoja nikusaidie jambo moja.”
“Lipi hilo?”
“Lile ni jengo la kibiashara na huwa kunapangishwa kwa mtu yeyote mwenye kampuni kubwa. Ukishapanga, utaelekezwa kuitumia benki ya umoja kufanya kila muamala wako. Ikiwa na maana, unakuwa chini ya uangalizi bila wewe kujua.”
“Kwa hiyo una maana nipange huko juu, kisha nifanye uhuni wangu kirahisi?”
“Hakika umewaza vema!”
“Mimi naona haijakaa sawa! Unaonaje nikitafuta ajira kwenye moja ya kampuni zilizopanga humo?”
“Yes!” Bob aliitikia kwa furaha, jambo lililomshangaza Zuki p.a.k Miguu ya kuku.
“Sikia Zuki, kwenye ghorofa ya tatu, kuna kampuni ya ulinzi ya Dop. Kampuni ile huajiri watu mbalimbali wenye uzoefu na wenye ujuzi mbalimbali. Kampuni ile ndiyo inayosafirisha pesa zote za Umoja benki, lakini pia ni kampuni ambayo huajiri mafundi umeme na watu wa huduma ya kwanza. Hivyo ni wewe na uamuzi wako, uwe fundi umeme, au uwe mtoa huduma ya kwanza na uokozi kwa dharura!”
“Naweza kuwa yeyote kati ya hivyo, lakini nafasi ya kupata kazi ipo? Maana kwa harakaharaka naona hiyo ni kampuni ya wanausalama wenyewe”
“Wewe usiwaze, mathalani wamekubali kupokea mtu yeyote ili wafiche ukweli wao, utapata kazi kupitia mimi. Mimi ndiye Mchungaji Emmanuel bwana!” Bob Rando alimalizia kwa kucheka kwa sauti kubwa.
“Haya poa bwana Pastor!” Miguu ya kuku alisema na kukata simu huku akitabasamu.
“Huwa sipendi sana kuzunguka na kazi moja, kwa muda mrefu, ila hii inaonekana itanilia wakati wangu kuliko nilivyodhani” Alijisemea huku akinyanyuka na kuelekea chumbani kwake.
NAIROBI, KENYA.
Zilikuwa zimepita siku tatu tangu Zuki Gadu p.a.k Miguu ya kuku, aingie jijini Nairobi. Alifikia kwenye hoteli ya Pama. Hoteli ambayo ilikuwa umbali mfupi kutoka lilipokuwa jengo la Patrice Lumumba. Katika siku zote hizo ambazo alikuwa kwenye hiyo hoteli, alikuwa ametumia muda mrefu kulichunguza vizuri jengo lile refu. Alizingatia zaidi ulinzi uliyokuwa upande wa chini ‘Basement’.
Kwa haraka aligundua kulikuwa na walinzi saba ambao walikuwa wanalinda pale benki. Walinzi wawili kati ya hao saba, walikuwa wanalinda eneo la kuegesha magari, walinzi wengine wawili, walikuwa wanalinda upande wa nje ambao ulikuwa na ngazi za kuelekea kwenye ghorofa za juu, bila kupita basement, ambako kulimilikiwa na umoja benki. Walinzi wengine wawili, walikuwa wanalinda eneo la mlango na mlinzi mmoja, alikuwa ndani ya benki.
“Ulinzi wa hapa si mchezo aisee!” Alijisemea huku akivuta kiti na kukaa kwenye meza iliyokuwa ndani ya mgahawa, uliyokuwa mita chache kutoka lilipokuwa jengo la Patrice Lumumba.
Dakika moja baadae, mhudumu alimfuata na kumpa orodha ya vyakula vilivyokuwa vinapatikana wakati huo.
Miguu ya kuku alichagua supu ya samaki na chapati tano. Mhudumu aliondoka kwenda upande wa jikoni, kuleta alichoagizwa.
Wakati mhudumu anaondoka, Miguu ya kuku yeye, aliamua kuendelea kufanya jambo lililokuwa limempeleka pale. Alizungusha macho yake ndani ya ule mgahawa, mithili ya mtu aliyekuwa anamtafuta mgoni wake.
Watu wengi waliokuwa pale ndani, walikuwa bize kushugulikia vyakula vyao huku baadhi wakionekana kuzama kwenye mazungumzo na wengine wakiperuzi kwenye simu janja zao. Lengo lake halikuwa kuwatizama watu hao, bali, alihitaji kuwaona watu ambao walikuwa ni zaidi ya wateja kwenye ule mgahawa.
Licha ya jicho lake kumfikia kila mmoja lakini hakuweza kumtilia shaka yeyote.
“Haiwezi kuwa rahisi namna hiyo. Hapa ni lazima kutakuwa watu wanaotizama nyendo za wapita njia.” Alijiwazia huku akiendelea kuzungusha kichwa chake kila pande ya ule mgahawa.
Wakati akiwa kwenye upelelezi; mhudumu alirejea akiwa na sinia la kiamsha kinywa alichoagizwa.
“Karibu!” Mhudumu alimwambia huku tabasamu la kheri likiwa limeupamba uso wake.
“Ahsante sana mrembo!” Miguu ya kuku alimjibu huku akiinuka na kwenda kunawa.
Alipomaliaza, alirejea kwenye na kuanza kufakamia chakula kilichokuwa mezani. Hakuhitaji kutumia dakika nyingi kulijaza tumbo, alihitaji kuwahi kufanya jambo moja zaidi ili kufanikisha kile kilichikuwa kimempeleka pale.
Dakika tano zilimtosha kumaliza supu na chapati zake tano, kisha alienda kunawa na kurejea alipokuwa. Baada ya kuketi, alizungusha macho yake pale mgahawani. Aliporidhika na utulivu uliokuwepo, alitoa mkebe kwenye mfuko wa suruali yake. Mkebe ule ulikuwa umehifadhi paketi mbili za sigara, aina ya safari.
Alitoa paketi moja na kuifungua, kisha alichomoa pisi moja ya sigara na kuibana kwenye vidole vyake vya mkono wa kulia na kurejea kuifunga paketi kisha, aliirejesha kwenye mkebe na kurudisha mfukoni. Tofauti na mawazo ya wengi kuhisi alitoa sigara pekee, yeye alikuwa ametoa na kitu kingine cha ziada. Alikuwa ametoa kitu chenye ufanano na mdudu vule.
Alichukua sigara na kuiweka kwenye mfuko wa shati, huku macho ya watu waliokuwa wamechukizwa na utoaji wa sigara eneo kama lile, wakimpotezea baada ya kuona hana mpango wa kuivuta. Lakini jambo moja hawakuelewa; wakati alipokuwa akiweka sigara kwenye mfuko, ni wakati huohuo alipodondosha kile alichokuwa amekichukua kwenye paketi ya sigara, kwa uficho.
Baada ya kuhakikisha kimetua chini kwa namna aliyokuwa ameikusudia, alitoa simu yake mfukoni na kuanza kuperuzi taratibu, huku mkono wake mmoja ukitoa pesa na kumpa mhudumu aliyekuwa amesimama kando yake, akingoja malipo ya huduma aliyotoa.
Alilipa pesa iliyohitaji, kisha alirejesha macho yake kwenye simu yake huku masikio yake yakizisikia hatua za mhudumu akiondoka mbali nae.
Dakika moja baada ya kuwa bize na simu yake, kile alichokidondosha chini kilipata uhai na kuanza kujongea ndani ya mgahawa. Kilitembea kila sehemu iliyokusudiwa kisha kilirejea pale alipokuwa Miguu ya kuku. Aliinama na kukiokota kisha alikiweka mfukoni mwake na kunyanyuka kuelekea kwenye hoteli aliyofikia.
Alipofika ndani ya chumba alicholipia, alitoa simu yake kisha alimalizia kwa kukitoa kile kidubwasha chenye umbo ufanano na mdudu vule. Alibofya simu yake mara kadhaa na kile kidubwasha, kilianza kumweka. Kilimweka mara saba na kuzima kabisa.
Miguu ya kuku alipumua kwa nguvu, huku akikuna kidevu chake bila kutarajia.
“Aisee! Hapo mgahawani pekee, kuna watu saba wenye silaha! Hii ni zaidi ya Benki kwa kweli!” Alijisemea kwa sauti huku macho yake akiwa ameyaelekeza kwenye kile kidubwasha kilichokuwa kitandani. Kilikuwa ni kifaa maalumu cha kuhisi silaha iliyofichwa, huhesabu idadi ya silaha na pia kilikuwa na uwezo wa kutoa taarifa endapo kungelikuwa na mlipuko maeneo ya karibu. Miguu ya kuku alipewa kifaa kile wakati alipokodiwa kufanya misheni huko South Afrika. Misheni ambayo ilimkutanisha na jasusi wa Israel aliyemzawadia kifaa kile na vingine vingi vya aina ile.
“Kuiba ndani ya hii Benki kunahitaji umakini sana, la sivyo nitaingia kaburini kabla ya wakati wangu.” Alijisemea huku akikunjua laptop yake na kuiwasha, kisha alianza kusoma vitu kadhaa kuhusu majengo ya Benki na namna yanavyohifadhi mali zake.
Katika pekuapekua zake, aligundua mara nyingi kila benki huwa inakuwa na sehemu maalumu za kuhifadhia ambazo huitwa ‘Vault',sehemu hizi huwa zinakuwa na ulinzi wa kieletroniki. Ukiachilia mbali ulinzi wa aina hiyo, pia huwa kuna ulinzi shirikishi ambapo; kuna kamera na pia huwa kuna sensors maalumu ambazo husaidia kuhisi mitetemo, mjongeo ama joto lisilokawaida.
“Ulinzi wote unaweza kuwa umezingatiwa? Na vipi hii Kabu, inaweza kuwa ipo kwenye hizo ofisi za usalama?” Alijiuliza huku akiendelea kuperuzi taarifa kadhaa zinazohusu mabenki mbalimbali Duniani.
“Kazi ipo!” Aliwaza huku akifunga kompyuta yake na kukaa kitandani na kujaribu kuwaza hili na lile kuhusu kazi iliyokuwa mbele yake.
Dhahiri aliona ugumu uliokuwa mbele yake hasa kwa kuzingatia namna ambavyo ulinzi Mkubwa uliimarishwa ndani ya umoja benki.
Alikuna kichwa chake kwa kutafakari baadhi ya mambo ambayo alihisi yatamkwamisha kwenye mpango wake huo. Akiwa amezama mawazoni, mara kuna kitu kilipita kichwani kwake.
Alisimama wima ndani ya chumba chake, kisha alianza kutembea bila utaratibu maalumu.
Ghafla alisimama na kuelekeza macho yake upande lilipokuwa begi lake la nguo. Akifikiri kidogo, alipiga hatua kulifuata. Alilifungua na kutoa kadi ya benki. Aliitizama kwa umakini mkubwa, aliigeuza pande zote bila kupepesa macho yake.
Ilikuwa ni kadi ambayo inaweza kutoa pesa kwenye benki yoyote ile kwenye nchi yoyote.
Aliporidhika na kile alichikuwa anafikiria kuhusu kadi ile, aliitupa kitandani na kutoka nje ya chumba. Alipofika nje, alielekea kwenye mtaa ambao ulikuwa na maduka.
Alitembea kwa dakika kadhaa hadi alipoufikia mtaa wenye maduka, alienda hadi kwenye duka aliloona anaweza kupata alichokihitaji. Alipofika alitoa salamu kwa mhudumu kisha aliomba kuuziwa mshumaa. Alitajiwa bei na alilipa kaisi kilichotosha kuuziwa mshumaa mmoja.
Alipewa mshumaa wake na kurejea ndani ya chumba cha hoteli aliyofikia jijini Nairobi.
ITAENDELEA.
