HADITHI: MALAIKA MWEUSI
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500.
EPISODE 4
ILIPOISHIA: 3
Nilimshika na kumgeuza ambapo alipiga kelele kutokana na maumivu. Maskini mama yangu aliteseka..sijui wanadamu wengine kwa nini Mungu aliwaumba katika hali ya ubinadamu kwa nini asiwaumbe wanyama nilimchukia sana baba sijui nimfananishe na kitu gani,” Malaika alisema kwa uchungu mkubwa japo jambo lile lilitokea muda mrefu.
SASA ENDELEA...
Aliendelea kuhadithi kisa kilichokuwa sawa na kuchubua ndonda lilipona. Baada kumgeuza huku moyo wangu ukiwa katika maumivu makali nilimpa moyo mama yangu.
''Ooh pole sana mama yangu taratibu.”
Nilimgeuza mama alilalia mgongo kisha akaniita tena
“Mwanangu Tereza.”
''Abee mama''
“Kila nikikuangalia moyo wangu unaniuma.''
''Una maana gani mama?’
“ Mwanangu najua utapata shida utaishi maisha ya tabu hata ile dhamira yako siamini kama itatimia''
“ Mama...mbona leo sikuelewi, una maanisha nini?”
''Ni vigumu kunielewa kwa vile bado mdogo akili yako ni changa ndiyo maana nakuonea huruma”
“ Unanionea huruma kwa lipi?”
“Mwanangu nakuacha kama kinda la ndege ambalo mama yake amekufa kutokana na mvua kubwa yenye upepo mkali iliyozoa kiota chake na kuua wazazi wote na kubaki kinda lisilojua lolote.”
“ Mama unataka kwenda wapi kama mateso ya baba yamekushinda basi tuondoke wote sitakubali kubaki kuendelea kupigwa na baba. “
Kauli yangu ilimfanya mama acheke kicheko ambacho sikukielewa kilikuwa ni kicheko cha mtu aliye jikatia tamaa ya kuendelea kuishi.
''Tereza mwanangu.''
''Abee mama.”
“Leo nataka kukupa siri moja sipendi kufa nayo moyoni nina imani Mungu atanihukumu.”
''Siri gani mama yangu?”
Mama aliushika mkono wangu na kuunyanyua kisha alianza kunisimulia.
“Miaka 15 iliyopita mimi mama yako nilikuwa mtawa kwenye kanisa kuu mjini nimekuwa pale kwa zaidi ya miaka mitano nikimtumikia Mungu.
Siku moja niliporudi nyumbani kumjulia hali bibi yako ambaye ni mama yangu, kwa kuwa vijijini kuna shida ya maji niliamua kufuata maji kisimani. Kisima hikihiki tulichokitumia miaka ya nyuma kabla ya kujengwa baadhi ya nyumba kulikuwa na pori.
Wakati natoka kisimani kuchota maji ile navuka tu lile pori walitokea wanaume watatu ambao ni vijana wa pale kijijini ambao nilikuwa nimesoma nao na kucheza nao lakini siku hiyo walikuwa na roho ya kishetani kwa kunivamia na kunivuta kichakani ambapo walinibaka kwa zamu.”
“Aah! Mamaa!” Nilishtuka sana kusikia habari ile japo moyo uliniuma nilitulia nijue mwisho wake.
“Kitendo kile kwa kweli kilinidhalilisha sana na kunitia dosari katika maisha yangu ya utawa lakini sikutaka kumweleza mtu na wale wote walionitendea kitendo kile niliwasamehe, kwani sisi tumefundishwa kusamehe saba mara sabini kwa kuwa walionibaka hawakujua walitendalo.
“Nilirudi hadi nyumbani nikiwa na siri yangu moyoni niliogopa kumwambia mtu kwani niliona aibu. Baada ya kumaliza mapumziko yangu nilirudi Parokiani kuendelea na huduma na siri yangu moyoni. Siku zilibadilika na hali yangu ya kimaumbile nayo ilibadilika ilibidi nipelekwe hospitali ambapo nilipopimwa niligundulika ni mjamzito.
“Hapakuwa na jinsi, kanisa ilibidi linitenge na kuondolewa baada ya kuonekana nilivunja masharti kufanya ngono nje ya utaratibu za utawa. Nirudi tena kijijini kuanza maisha mapya, hiyo mimba ndio uliyozaliwa wewe,” habari hizi zilinishitua sana na kujua kumbe sina baba ujauzito wangu uliingia baada ya mama yangu kubakwa.
“Waliokubaka kwani bado wapo hapa kijijini?” nilimuuliza mama.
'"'Eehe wapo mbona huwa naongea nao walishakuja kuniomba msamaha nami niliwasamehe.”
“Aah! Mama hao si watu wa kuwasamehe ningekuwa na uwezo ningewaulia mbali,” nilisema kwa hasira japo nilikuwa binti mdogo.
”Aah, mwanangu jifunze kusamehe ili hata bwana Mungu naye akusamehe usipende kulipiza kisasi.”
“'Ni ngumu, ni akina nani hao?”
Mama alinitajia kwa majina, kumbe ni watu ambao nilikuwa nawaheshimu sana kumbe ni mashetani ipo siku yao,” nilijikuta nikisema kwa hasira.
“Mama kwa nini mungu aliumba wanaume si bora angeumba dunia na jinsia moja. Mama wanaume wote angewageuza wanyama kama nyati, kiboko na hata fisi.” ''Hapana sio wote wanaume wana roho mbaya wapo wenye roho nzuri na pia wapo wanawake wenye roho mbaya kuliko hata wanaume.”
''Hapana...hapana...hakuna mwanaume mwenye roho nzuri yaani mama naapa sitawapenda wanaume mpaka nimeingia makaburini nina imani ni kundi la mashetani yaliyohasi ingekuwa amri yangu ingekuwa dunia ya jinsia moja...na huyo shetani mwingine alikujuaje?”
“Mwanangu lekebishe kauli yako, baba yako usimwite shetani,” mama alinionya.
“Tena mkubwa wa mashetani binadamu gani asiyekuwa na huruma ndio maana nilikuwa najiuliza muda mrefu baba gani asiyekuwa na mapenzi ya familia yake?”
''Yule baba yako tulikutana nae hapahapa kijijini kwa kweli katika siku za mwanzo alikuwa ni mtu mzuri sana, lakini kumbe upole wake ulikuwa wa kuniteka kimawazo kumbe ni chui aliyevaa ngozi ya kondoo...alianza kubadilika na kunipiga hasa baada ya bibi yako kufariki, ulevi ukawa ndio sehemu ya maisha yake.”
“Alizidi kubadilika na kunipiga, yeye ndio aliyenitia ubovu huu wa mwili kwa kipigo hata meno yeye ndiye aliyeningoa kutokana na kipigo.”
“Sasa mama bado mtu huyo unamtetea labda sio mimi nitakapokua mkubwa nimkute amekufa la sivyo lazima nitalipa kisasi,” nilisema kwa uchungu.
“'Hapana mwanangu usifanye hivyo, la muhimu ni kuomba kwa Mungu usome kwa bidii kwani huo ndio mtaji wako utaokutoa kwenye dimbwi la umaskini.”
“Mama ninakuahidi nitasoma kwa bidii ili siku moja niwe hakimu au polisi ili niwashikishe adabu wote wenye tabia ya kuwanyanyasa wanawake'.”
“Mungu atasikia maombi yako lakini chonde usilipe kisasi,” mama alizidi kunionya, alitulia kidogo kisha alianza kuhema kama mwenye pumu, kitu kilichonitisha.” ''Tereza...mwanangu nipe...maji,” mama alisema kwa shida, nilimletea maji wakati huo alikuwa akiongea kwa sauti iliyoanza kufifia.
''Maskini mwanangu...Mungu nilindie mwanangu,” hakuendelea tena alinyamaza kimya,nilimuita:
''Mama...mama.” hakunijibu zaidi ya kunitazama, alitabasamu lakini tabasamu lake liliishia kati alitulia tuli, nilimuita lakini hakunijibu.
Ile hali ilinitisha ilinibidi nitoke nje niombe msaada wa majirani, nilishangaa wakati natoka nje baada ya muda ndipo nilipotambua mama yangu alikuwa amekufa. Siku hiyo nililia sana hadi nikapoteza fahamu. Sio siri mama yangu nilikuwa nampenda sana lilikuwa pigo zito maishani mwangu.
Baada ya mazishi ya mama niliendelea kukaa na baba ambaye nilifahamu kuwa si baba yangu mzazi ila ni wakufikia, nilikuwa sina jinsi lakini ukweli nilimchukia sijui nimfananishe na kitu gani. Si yeye tu hata wanaume wote duniani niliwachukia sana licha ya mama kunikataza nisilipe kisasi. Kisasi changu ni kusoma kwa bidii ili siku moja niwe askari wa cheo cha juu au hakimu ambaye nitawashikisha adabu wote wanaonyanyasa wanawake.
Baada ya msiba wa mama kidogo nyumbani alirudi katika hali ya utulivu, niliendelea kusoma kwa bidii na darasani nilifanya vizuri mtihani wangu wa darasa la tano. Nikiwa darasa la tano mwaka mmoja baada ya kifo cha mama alikuja mama mmoja hivi.
Nilimsikia baba yangu akisema:
“Tena huyo ndio anarudi,” nilipofika niliwasalimia na kisha kuingia ndani, nikiwa nabadili nguo baba aliniita.
"Thereza."
”Abee baba, nabadili nguo."
"Fanya haraka kidogo.”
Baada ya kubadili nguo nilitoka nje.
"Abee baba."
"Thereza mwangu huyu mama hapa anataka akuchukue akupeleke mjini.”
“Na shule baba?”
“Aah! Utasomea huko huko.”
Nilishindwa kukataa hata nguo za kubadili sikubeba niliingia ndani ya gari na kuletwa jijini kwa mara ya kwanza. Mawazo yangu nilijua nakuja kusoma kumbe kufanywa mfanyakazi wa ndani nilipomuuliza mama alinijibu kuhusu kusoma jibu alilonipa ndio lilinimaliza kabisa ndoto yangu ya kuwa afisa wa jeshi au hakimu ilizimika.
Alijibu kuwa yule baba wangu wa kambo amemuuzia kwani alipofika pale kijijni kutafuta mtumishi wa ndani alinitoa mimi, roho iliniuma nilipojua nimeuzwa kama mbuzi.
Kuanzi hapo nikawa mtumishi wa ndani ya nyumba hiyo kwa kweli nilifanyishwa kazi kama mbwa sikuwa na mapumziko. Kitu kilichonifanya nimshangae mama huyu ambaye hakuonyesha hata huruma kwanza umri wangu haukuwa wa kufanya kazi pili kazi zilikuwa nzito ambazo zilinizidi uwezo.
Miaka miwili ilikatika nami nikazoea kazi za sulubu siku moja nilivamiwa chumbani kwangu na baba ambaye alinibaka na kunitishia endapo nitasema nitajuta kuzaliwa. Japo aliniumiza ilibidi niwe mpole sikumweleza mtu nilikumbuka yale yote ambayo yalimtokea mama yangu.
Roho iliniuma nilimkumbuka mama yangu siku hiyo nililia sana kitu kilichomshtua mama mwenye nyumba. Usiku wa siku iliyofuata ilikuwa kama wameambizana mtoto wa mwenye nyumba naye alinibaka, Mchezo ule ukawa wa kila siku kunibaka. Mwisho hali ile niliizoea nikawa sigomi tena akifika baba sawa au mtoto wa mwenye nyumba walinikuta tayari nawasubiri.
Nafikiri walikuwa hawajuani siku zote penzi halina siri siku moja tulifumaniwa na mama mwenye nyumba mbona siku hiyo ilikuwa kasheshe. Pamoja na kujitetea kuwa nililazimishwa lakini hawakunielewa siku hiyo alichonifanya mama yule nina imani akitanitoka akilini mwangu.
Alinifunga kwa kamba na kunichoma katika mapaja yangu kwa pasi na kunipaka pili pili sehemu za siri kisha kunipa kipigo cha mbwa.
******
Baada ya mateso makali nilifukuzwa pale nyumbani tena ukiwa ni usiku huku mvua kubwa ikinyesha. Yaani ulikuwa ukatili wa hali ya juu, kubakwa nibakwe niteswe na kipigo juu.
Nililala kwenye jumba moja bovu hadi asubuhi ambapo niliokotwa na wasamali wema na kupelekwa hospital ambapo sehemu zangu za siri zilikuwa hazitamaniki, mapaja na ngozi yote ilikuwa imebanduka. Kabla ya matibabu kwanza nilipelekwa kituo cha polisi na kupewa PF3 ndipo nilipopata matibabu.
Nilimshukuru Mungu nilipata msamalia mwema mmoja ambaye alisema atanisimamia kuhakikisha wahusika wote wanatiwa hatihani. Katika muda wote niliokuwa pale hospitali alinihudumia kama mdogo wake na baada ya kupata nafuu alinichukua hadi nyumbani kwake.
Kisha aliifungulia mashtaka ile familia kwa unyanyasaji wa kijinsia na ubakaiji. Siku moja wakati anarudi nyumbani yule dada ambaye kitaaluma alikuwa mwanasheria wa kujitegemea alinieleza kuwa ameamua kujitoa katika kesi yangu kwa kuhofia usalama wa maisha yake.
Alinipa nauli ili nirudi nyumbani kwetu iringa katika wilaya ya Makete kwani kama ningeendelea kukaa pale basi maisha yake yangekuwa hatarini. Kutokana na vitisho ilibidi niondoke siku ileile usiku na kulala kwenye nyumba ya wageni karibu na stendi ya mabasi Ubungo.
Kama kawaida asubuhi nilidamkia kituo cha basi, lakini mwaka wa mkosi ni mkosi tu nikiwa nataka kukata tiketi nilipogundua pesa yangu ya nauli ilikuwa nimeibiwa. Niliangua kilio pale kituo cha basi lakini hakuna mtu hata mtu mmoja aliyenijali.
Wapo walionisaidia pesa ya chakula tu na hata jioni ilipoingia ilibidi nilale palepale kituoni hadi asubuhi. Nilijifikiria sana nirudi tena kwa yule dada ili nimweleze masahibu yaliyonikuta, lakini aliyonieleza jana yake yaliniogopesha kuhofia usalama wa maisha yake.
Niliamua kuingia mjini na kuomba msaada kwa wasamalia wema, siku hiyo Mungu aliniangazia kwani mpaka jioni nilikuwa nimepata laki moja na arobaini elfu. Hapo tamaa ikanipata nikaona nisifanye haraka kuondoka niendelee kuombaomba hata nikirudi nyumbani niwe na pesa nyingi za kufungulia miradi ya kujiendeleza kimaisha.
Jioni ile nilipanga chumba cha gesti moja ya uswahilini na kulipokucha nikaendelea kuchangisha mchango wa hiyari. Siku hiyo mambo hayakuwa mazuri sana nilipata elfu sitini. Kama kawaida yangu jioni nilirudi kwenye chumba changu na kulala hadi asubuhi.
Kulipo pambazuka kama kawaida yangu kiguu na njia, nakumbuka siku moja nilikutana na mtu mmoja ambaye nilimuomba pesa zaidi ya mara tatu. Hapo sasa niliona naanza kuchanganya mambo niliamua kukaa kona moja sehemu ya Mtaa ya barabarani maeneo ya Faya nakufanya hapo ni makazi yangu ya kudumu.
Niliamua kutafuta nguo zilizochakaa ili nionekane kweli ni chokoraa na shukuru kipindi kile cha mzee ruksa watu walikuwa wakitoa pesa zao bila ya ubahiri. Ndani ya mwezi mmoja nilipata pesa nyingi kiasi cha kufuta wazo la kurudi nyumbani sikuwa na neno niliamua kupanga chumba na kununua vitu vya ndani.
Kuanzia hapo ikawa ni kawaida yangu ifikapo jioni kujichanganya katika majumba ya starehe ilikuwa ni vigumu kunitambua kwani mchana nilikuwa chokoraa niliyenyoa upara wenye kuonyesha kidonda kikubwa lakini usiku hubadili nguo na kuvaa nguo nusu uchi za kichangudoa na kichwani nilivaa wigi la nguvu. Nashukuru Mungu aliniumba nikiwa na umbo la kuvutia ndio maana hata baba na mtoto wake walishindwa kujizuia na kuamua kunibaka.
Nikiwa viwanjani nilipata marafiki waliosifia figa yangu kuwa endapo nitafuatana nao lazima wazungu wajichanganye siwezi kukosa dola mia tano mpaka elfu kwa mara moja. Kutokana na malengo yangu nilikubali kuifanya kazi ile kwa muda kisha niachane nayo.
Kuanzia hapo nikawa na kazi mbili asubuhi nakuwa ombaomba na usiku naruka viwanjani kama kawaida. Utafikiri nilikuwa nimejifukiza dawa wanaume walikuwa wakinifuata kama malkia wa nyuki hoteli zangu zilikuwa za kitalii tu sio za uswahilini.
Kutokana na kitendo cha mimi kuwazidi kete baadhi ya rafiki zangu kiliwaudhi na walifanya kunifanyia njama. Shoga yangu mmoja alinipeleka kwa rafiki yake mmoja anayekuwa akisoma chuo kikuu ili tukamtembelee kumbe walikuwa wamepanga nibakwe na wanafunzi zaidi ya kumi ili wanikomoe .
Bila ya kujua niliongozana na rafiki yangu yule tulipofika chuo kikuuu niliingia katika chumba kimoja cha yule shoga yake mara aliniomba nimsubiri kumbe walikuwa wamewafuata wale wanafunzi wa kiume mara waliingia vijana wa kiume kama kumi walinishika kwa nguvu na kunibaka. Kutokana kuwa sijawahi kufanya mapenzi zaidi ya mwanume mmoja nilizidiwa nguvu na kupoteza fahamu nilipozinduka nilijikuta nipo hospitali nikiwa katika hali mbaya.
Wanieleza kuwa walinikuta ufukweni nikiwa mtupu kama nilivyozaliwa baada ya kuokotwa na askari wa doria ambao walinileta hospitali. Kila nilivyowaeleza hawakukubali walidai kuwa mimi ni changudoa uliyataka mwenyewe. Niliruhusiwa kutoka hospital baada ya wiki tatu.
Nilipotoka hospitali hali yangu haikuwa nzuri sehemu zangu za siri zilikuwa zimeharibika vibaya na zilikuwa zikitoa harufu mbaya kama mzoga uliokufa kwa ajali.
Kwa vile nilikuwa na pesa za kutosha nilikwenda kwenye hospitali ya Mjerumani ambaye huduma zake zinasifika.
Hospitali yenyewe ipo Kibaha, Pwani, nilikutana na yule mzungu ambaye alinichukua vipimo baada ya muda alinijulisha kuwa vipimo tayari nakuniita kwenye chumba ambacho kilikuwa na mitambo ya kisasa.
Alinilaza kitandani ambapo aliniambia nipanue miguu yangu, alikuwa amevaa gloves na kunichunguza sehemu zangu za siri na kisha aliandika kwenye karatasi kabla hajaniruhusu kuvaa nguo zangu. Tulirudi hadi ofisini kwake na kunihoji sababu zilipelekea nipate ugonjwa huo.
Nilimweleza yote bila ya kumficha kitu, alitikisa kichwa na kusema:
“Ugonjwa huu auhusiani na kubakwa bali ni vimelea ambavyo vimepandikizwa. Katika hospitali za kawaida usingepona kwani sehemu zako za siri zingeoza kabisa na hatimaye utumbo pia mwisho wake ungekufa.”
“Walinipandikizia kivipi?"
" Hii ni dawa hatari sana sijui aliyekupaka sehemu za siri ameitoa wapi pia inaonekana aliyefanya hivi alikuwa amedhamiria kukuua."
Kusikia vile moyo wangu ulinilipuka na kujiuliza hivi hawa nimewakosea nini hasa mpaka wafike hatua ya kutaka kuniua.
“je, gharama zake utaziweza?" aliniuliza.
‘Kwani ni shilingi ngapi?"
"Mmh! Sijui kama utaiweza hasa kutokana na kazi yako ya uchangudoa."
'We nieleze nikishindwa si basi siyo kazi yangu.”
"Milioni mmoja na laki saba tena nimekupunguzia kutokana na hali yako ya ugonjwa huu, dawa zake ni lazima uchanganye na dawa zaidi ya saba na matibabu yake halisi ni shilingi milioni mbili na laki mbili."
Baada ya kuniambia vile nilishusha pumzi japokuwa hela nilikuwa nayo lakini matibabu ni bora zaidi ya pesa ambazo zinatafutwa.
“Ndiyo nitalipa.”
“Sasa lini utaanza matibabu?"
"Hata sasa hivi niko tayari."
"Pesa unayo hapa?"
“Hapa nina laki tano nyingine nitaleta."
"Sasa sikiliza binti nataka nikusaidie na wewe unisaidie," alisema daktari.
"Unisaidie kivipi na mimi nikusaidie kivipi?"
"Nitakutibu bure tena ndani ya wiki moja hali yako itakuwa nzuri."
"Eeh na wewe nikusaidie nini?" Wazo langu kunitaka kimapenzi japokuwa sikuamini sana kwa vile sehemu zangu za siri zilikuwa hazitamaniki.
“ Kuna kazi moja ndogo ambayo nitakupa nina imani haitakuwa nzito kwako lakini yenye ujira mkubwa."
“Kazi! Kazi ipi hiyo?”
“ Kutokana na maelezo yako utanifaa sana tena sana kwani ulipokuwa ukikutana na mwanaume ulilipwa kiasi gani?"
“Kwa wazungu ilikuwa dola mia hamsini mpaka mia mbili kwa waswahili ilikuwa elfu hamsini mpaka laki na nusu lakini mimi nilikuwa siwataki waswahili."
"Basi kuna kazi yangu nitakulipa dola elfu mmoja kwa kila kichwa."
"Kwa kichwa una maana gani?"
"Utajua subiri upone kwanza, mbona hii kazi imewanufaisha wasichana wengi kama tungejuana mapema wala usingekumbwa na matatizo yote haya."
Nilianza matibabu mara moja kwa kweli nilipata matibabu ya hali ya juu ndani ya siku mbili hali ilianza kuwa vizuri na ndani ya wiki mbili nilipona kabisa. Baada ya kupona nilikutana rasmi na Mr Rymond au kama anavyopenda kuitwa Mr Ray ndani ya ile hospital yake ambavyo tulikutana under ground kulikuwa na sebule kubwa yenye samani za kifahari.
Aliniuliza natumia kinywaji gani, nilimweleza kuwa natumia pombe kali ambazo nilizoea kuzitumia .Alileta chupa kubwa kama mtungi aina ya whiski ikiwa kwenye kitololi kidogo alimimina kwenye glasi mbili kisha alinipa ya kwangu na yeye akabaki na yake.
" Karibu sana," Dk Rey alinikaribisha.
"Ahsante.”
Tuligonganisha glasi zetu ili kuonesha upendo na kutakiana baraka ya kinywaji chetu.
"Ndiyo binti kwa umbile lako na uzoefu wako kuna kazi mmoja nitakupa, nina imani itakupa pesa nyingi kwa muda mfupi itategemea bidii yako."
"Kazi ipi hiyo?"
Kabla ya kunijibu kililia kitu kama alama ya kuashiria kuna jambo.
"Samahani nakuja," alinitaka radhi na kuelekea chini ambapo aliniacha peke yangu nikiwa na mawazo mengi juu ya hiyo kazi aliyotaka kunipa.
Malipo manono kiasi kile na ule usemi wa kila kichwa kimoja dola 1000 alikuwa na maana gani. Nilitulia huku nikikata maji taratibu kama mamba mzee . Baada ya dakika kama tano alirudi na kunitaka radhi tena.
"Ooh ,samahani kwa kukatisha mazungumzo."
"Bila ya samahani najua una majukumu mengi."
"Ni hivi kwa kuwa unauzoefu mkubwa na kazi yako ya uchangudoa na ni msichana mwenye mvuto wa sumaku nina imani kazi yangu utaifanya vizuri."
"Ni kazi ipi hiyo?"
"Ni hivi, kazi mpya haina utofauti na kazi ya uchangudoa lakini tofauti yake hautokuwa ukifanya mapenzi."
"Unafikiri kuna mwanaume atakaye kubali kukulipa pesaa yake bila ya tendo la ndoa?"
'Swali lako ni zuri, shida yangu ni yule mtu ukishapatana naye usikubali akupeleke anapopataka yeye mwambie gharama ya chumba utalipa wewe kwa hiyo yeye ataona amepata mchekea, chakufanya utaenda naye hadi chumbani na kumuacha. Utamuachaje? Mkishaingia usipokee kwanza pesa yake mweleze akusubiri na wewe toka nje wala usirudi.
Ndani ya gari utamkuta mtu atakulipa pesa yako muda uleule kazi itakuwa imemalizika kwako sasa itakuwa ni juu yako kutafuta mtu mwingine."
"Sasa huyo mwanume atabaki huko chumbani akiwa anfanya nini?" nilitaka kujua.
"Ndio maana nikakueleza kuwa utakuwa milionea kwa muda mfupi sana, maswali mengi hayana umuhimu nia imani tumeelewana sawa?"
"Kwa kuwa una maadui sipendi upate matatizo kama yale unajua vizuri akumulikae mchana usiku atakuchoma nitakufanyia plastic surgery ili kutengeneza uso wako vizuri uvutie mara dufu ."
Sikuwa na kipingamizi nilifanyiwa utengenezaji wa uso ndani ya miezi miwili nilikuwa mtu tofauti sana sikuwa tena yule Thereza unayemjua nilitengenezwa umbo la kimalaika kweli.
Pua yangu ya asili ilikuwa ni pana lakini ilipunguzwa na kuwa nyembamba ya kisomali hata mama yangu mzazi kama angefufuka asingenitambua uso wangu ulichongoka. Baada ya kuwa sawa mara moja nilingia viwanja na safari hii sio kusimama barabarani bali kuagiza kinywaji cha gharama ni kwenye mahoteli makubwa .
Haikuchukua muda mtu mmoja mwenye wadhifa alijipendekeza masharti yalikuwa yaleyale ya kumpeleka nitakapo mimi alikubali bila pingamizi niliongozana naye.
Sharti nililompa atangulie nje nikiwa na sababu asijulikane ametoka na mimi ni moja ya masharti niliyopewa na Dokta Ray.
Yule kibopa alitangulia nje baada ya dakika kama tano hivi nilimfuata na kumweleza aingie kwenye yeksi iliyokuwa nje kwa ajili ya kazi maalumu. Nilikwenda naye moja kwa moja hadi kwenye ile nyumba ya wageni ya Royal Light. Nilikodisha chumba na kupewa funguo niliongozana na kibopa yule hadi chumbani.
Tulikaa wote kitandani akiniangalia kwa macho ya mahaba, nilimuomba radhi anisubiri nakuja baada ya muda si mrefu.
"Basi usichelewe bibie."
"Ondoa shaka mpenzi."
Nilimuacha ndani na kutoka zangu nje, nilirudi ndani na ile teksi iliyotuleta ambayo ilikuwa bado inaningojea nje. Dereva alinipa dola 1000 kisha akaniuliza anipeleke wapi kwa vile muda ulikuwa bado unaruhusu. Alinihamishia katika hoteli ya Sea Cliff napo hata robo saa haikufika nilichukuliwa na kijana wa kiarabu akajipendekeza nikaondoka naye japo mwanzo aling’ang’ania sana tutumie gari yake lakini
nilimdanganya kwamba nisingependa watu wajue nimeongozana naye alikubali kilimpeleka katika hoteli nyingine tofauti ambayo ipo karibu na maeneo ya White Cruse.
Mpaka saa saba za usiku nilikuwa tayari nimelamba watu wanne nilirudishwa nyumbani kulala wakati huo nilikuwa nimepanga maeneo ya Magomeni Chemchem kwa walima mchicha.
Niliona kama maajabu vile yaani kazi ya saa tano nilikuwa nimeingiza dola za Kimarekani elfu nne. Kazi ile nilipangiwa kuifanya mara tatu kwa wiki, ijumaa, jumamosi na jumapili. Siku nyingine nilishinda nyumbani kujipumzisha.
Nilipewa maelekezo kuwa nisijihusishe na kazi ya aina yoyote zaidi ya kupumzika lakini kila jioni ilikuwa ni lazima tukutane.
Tulikuwa zaidi ya wasichana kumi hapo ndipo nilipojuana na mkeo mama Gift ambaye alitokea kuwa rafiki yangu mkubwa. Kwa kweli kazi yetu ilikuwa ni nzuri ndani ya miezi sita nilikuwa na pesa nyingi lakini hata hivyo siku zote nilikuwa najiuliza maswali yasiyokuwa na majibu juu ya wale wanaume tuliokuwa tukiwapeleka kwenye nyumba za wageni walikuwa wanafanya nini?
Siku moja nilimdodosa Dokta Ray juu ya wale watu ndipo aliponipa siri hiyo lakini mwanzoni nilijua ni kweli kumbe ni uongo eti wao wanadili na wauzaji wa madawa ya kulevya hivyo wale wanaowapeleka ni wateja wao wanatujua wanakuja kwa njia ya kututongoza na tunapowapeleka kwenye nyumba za wageni na kuwaacha kuna watu ambao wakwenda kuwauzia yale madawa ya kulevya.
Pesa nyingi nilizozipata nilijenga nyumba kubwa maeneo ya Kunduchi na kununua magari mawili ya kutembelea na pesa nyingine niliweka benki. Siku moja nilipita katika maeneo ya kijiweni kwangu kwa zamani niliwakuta washirika wangu hakuna hata mmoja aliyenitambua.
Sio siri roho iliniuma kwa jinsi nilivyowakuta niliwapa pesa za kutosha na niliporudi nyumbani nilichukua nusu ya pesa zangu na kununua maeneo sehemu mbal mbali na kuamua kujenga vituo kwa ajili ya watoto wa mitaani . Ndoto yangu ilikuwa mara wamalizapo masomo yao wakute nimeshajenga viwanda ili wafanye kazi.
Wakati huo nilikuwa naendelea kazi yangu ya kusaka wateja wa madawa ya kulevya kwa muda mfupi jina langu lilikuwa kubwa ndani na nje ya nchi kutokana na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto wa mitaani. Nilipata wageni wengi kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali ya nchi za nje na kutaka kujua shughuli zangu naziendeshaje.
Niliwaeleza na hapo misaada mingi ilipofumuka na ndipo nilipozidi kujiendeleza ikiwa pamoja na kupata mikopo iliyonisaidi kujenga viwanda vidogo vidogo. Kwa mwaka mmoja NGO'S za nje zilikuwa zikinitumia dolla za kimarekani laki tano hizi zilinisaidia kuboresha miradi yangu na kupanua shughuli zangu.
Wakati huo rafiki yangu mama Gift alikuwa na mpenzi wake ambaye walifikia
hatua ya kutaka kuoana lakini mara ilitokea kutoelewana na yule mpenzi wake ilionesha mkeo alikuwa amepunguza mapenzi.
Kwa kuwa tulikuwa mashoga ilibidi anitumie mimi ili nimueleze tatizo linalofanya mpaka penzi lao kuyumba nilijitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuwapatanisha lakini mkeo alinieleza kuwa niachane nae.
Nilikuwa namuonea huruma sana yule kijana nilijaribu kumliwaza, alinieleza nimweleze nini anachotaka chochote kile atampatia ili tu arudishe penzi lao kama zamani.
Nilipomweleza mkeo mama Gift kwa kuwa alikuwa shoga yangu mkubwa, ilibidi anieleze kuwa yeye ni mchumba wa mtu na mchumba wake ni ofisa wa jeshi la polisi upande wa upelelezi ambaye alikuwa msomoni Russia amerudi.
Alinieleza hata hii kazi ya kukusanya wateja itamuwia vigumu kwani wakati wowote atakuwa mke wa mtu. Kuwa ule urafiki wake na yule kijana anayeitwa Mac Donald alikuwa anafanya nae kwa wizi tu lakini mhusika mwenyewe alikuwa nje ya nchi.
Ilibidi nimweleze ukweli Mac Donald juu ya penzi lao kulega, nilishangaa aliponiuliza kama nina mpenzi nilimjibu kuwa sina.
Basi yule kijana akaniahidi vitu vingi endapo nitamkubalia kuolewa naye ili kumuonesha mama Gift. Kwa kuwa mimi nilijali msirahi nilimkubalia ndipo aliponinunulia lile gari langu la Lexus pamoja na kuniporomeshea jumba hii la kifahari.
Mipango ya harusi iliendelea kama kawaida, siku mmoja nilikutana na mkeo mama Gift sikumficha nilimweleza ukweli juu ya uamuzi wangu na Mc Donald wa kunioa pia nilimweleza vitu alivyonipa ambapo nilimuona akionyesha hali ya unyonge fulani niliaga nae.
Ndoa yangu iliwahi kufanyika kuliko ya kwao nilimtumia kadi ya harusi .Usiku wa siku ile nilipokea simu kutoka kwa mkeo ambapo niliongea naye
"Ted vipi?"
"Safi tu lete stori shemu hajambo?"
"Hakuhusu."
" Mmh! Unasemaje?"
"Sikiliza Ted, elewa wazi Mac Donald ni mpenzi wangu na tulikuwa hatujaachana hivyo shoga kwa usalama wako achana naye."
"Mbona sikuelewi? "
"Huwezi kunielewa, umalaya tu, ina maana wanaume wameisha hadi umfuate bwana wangu?"
"Wewe si mke wa mtu mtarajiwa?"
"Kama hivyo? “
"Subiri ndoa yako."
"Ted huu si wakati wa mzaha, ama sivyo utajuta kuzaliwa hiyo ndoa yenu mtaifunga kwa Mungu .
"Usinitishe.”
''Tutaona.'.
''Tutaona.'' alikata simu.
Siku nne kabla ya kufunga ndoa nilitekwa kutoka nyumbani na watu wasiojulikana niliteremshwa kwenye gari na kufungwa kitambaa cheusi usoni.
Nilipelekwa sehemu nisiyojulikana na kuteremshwa garini niliingizwa kwenye jumba moja na kufunguliwa kitambaa usoni, mbele yangu kulikuwa wanamume wenye miili iliyoshiba.
Nilishangaa kuwepo sehemu ile nilijiuliza nimepelekwa pale kwa kosa gani kabla ya kupata jibu nilikatishwa na makofi yaliyotoka nyuma yangu.
''Shoga kiko wapi sasa tusilaumiane nilikueleza ukafikiri ni utani sasa ndoa yako utaifungia kwa Mungu,” ilikuwa ni sauti ya mkeo mama Gift aliyekuwa amevalia trak sut nyekundu na raba nyeupe.
''Kwani shoga tatizo ni nini kama ni Mac Donald mchukue na mimi uniachie uhai wangu,” mwanzo nilidhani utani lakini mpaka kufikia pale niliona kuna dalili mbaya mbele yangu.
''Mmh! Ndio unalijua hilo, ushachelewa.”
Aliwaamuru wale vijana wa kazi wanivue nguo zote na kulazwa chali juu ya meza.Waliniweka kama vile mtu anayetaka kujifungua japokuwa sijawahi kujifungua.
Wakiwa wamenishika barabara mama Gift alikuja hadi karibu yangu akiwa ameshika kisu kikubwa chenye ukali wa kutisha nilimsikia akisema huku akinishika sehemu zangu za siri.
''Hizi ndio sehemu zinazo kutia kiburi'', mara nilianza kusikia maumivu ya kuchokonolewa na kitu chenye ncha kali maumivu yalizidi kwani kisu kilizidi kuingizwa ndani zaidi katika sehemu zangu za siri, maumivu yalikuwa ni makali sana na sehemu zangu za mapaja nazo walizichanachana na kisu. Baada ya kumaliza unyama wake walichukua kipande cha mti na kunishindilia nacho damu zilinitoka kama ng`ombe aliyechinjwa.
Maumivu yalikuwa makali nilimsikia mama Gift akiwaamuru wale vijana wake wanipige hadi niage dunia. Kipigo kiliendelea mpaka nikapoteza fahamu sikujua kilichokuwa kinaendelea.
Your Thoughts