HADITHI: MALAIKA MWEUSI
EPISODE 3
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500.
ILIPOISHIA: EPISODE 2
Kauli ile ilimzidi kumuongezea hasira Anderson alimtikisa kwa nguvu na kumsukumia ukutani Malaika Mweusi alijigonga kichwani na kupasuka.
Damu nyingi zilimtoka akiwa mtupu na kumlaza kwenye zulia wakati huo alikuwa amelegea na kuhema kwa mbali.
Aliwapigia simu vijana wake waje kumchukua, mara ghafla umeme ulikatika kwa dakika moja na uliporudi Malaika Mweusi hakuwepo.
SASA ENDELEA...
Hali ile ilimshtua Anderson na kuhofia kuwa watu wanamfuatilia hata kumuua wangeweza. Mara vijana wake walitokea.
“Vipi mzee hata bado ulikuwa hujabadili hata nguo?”
“Aaa… basi endeleeni na shughuli zenu ila vijana watatu wabaki kwa ajili ya kulinda nyumba yangu,” Anderson alianza kuingiwa na woga.
Lakini alilala salama mpaka asubuhi bila ya hatari yoyote aliyofikilia kumtokea. Asubuhi kama kawaida alishughulikia mazishi ya baba yake na baada ya mazishi alirejea nyumbani. Ndugu na jamaa walienda nyumbani kwake kumpa pole kwa misiba ya mfululizo iliyomuandama.
***
Baada ya msiba alianzisha operesheni ya kuichunguza miradi yote ya Malaika Mweusi. Wakurugenzi wake wote waliwekwa ndani ili waeleze Malaika Mweusi amekwenda wapi.
Jambo lile ilikuwa ni geni kwao, walikuwa hawajui taarifa zozote za Malaika pia walikuwa wameonana naye mara moja tangu waajiriwe na wengine ni mara chache sana. Alikuwa akifika mara mojamoja tena bila taarifa na kuangalia shughuli zinaendaje na kisha kuondoka zake zaidi ya hapo huwasiliana kwa simu.
Kutokana na ukali wake kwenye kazi zake kila aliyepewa jukumu lake alitekeleze kwa umakini mkubwa aliisha watishia atakayefanya mchezo katika kazi zake atamuua hadharani. Ile ilisababisha kila moja kuwa makini hata kama yeye hayupo.
Siku zote kazi zake zilikwenda vizuri hivyo hakuna mtu yoyote aliyejua nyendo zake kwa vile hakuwa na ukaribu na mtu. Pamoja na kujitetea waliendelea kuwekwa ndani ili kumshinikiza Malaika Mweusi ajitokeze la sivyo wakuruenzi wote wangeendelea kusota mahabusu. Wiki zilikatika bila kujitokeza .
Anderson aliendelea na msako mkali kuhakikisha anamtia mkononi bila ya kuogopa hatari yoyote kwa vile hakuna alichokuwa akikiogopa tena hasa baada ya familia yake yote kupotea.
Akiwa ofisini akisubiri ripoti za vijana wake kuhusu Malaika Mweusi mara alijulishwa na sekretari wake kuwa kuna kikongwe kimoja kinataka kumuona. Alimruhusu aingie ndani mara aliingia bibi kizee mmoja mwenye mvi kichwa kizima akiwa anatembea kwa kuinama akitumia mkongojo wake, alipomuona alimkaribisha huku akiwa amesimama.
“Ooh, karibu sana bibi.”
“Ahsante mjukuu wangu .”
“Shikamoo, sijui nikusaidie nini?”
Ghafla bibi alibadili sauti toka ya kizee na kuwa ya kijana iliyokuwa tofauti na umri wake.
“Anderson,” yule bibi alimwita.
Akiwa bado anashangaa kubadilika kwa sauti ya yule bibi, ghafla mgeni wake alinyanyuka na na kuondoa zile nywele nyeupe na plastiki yenye uso wa bibi kizee. Hakuwa mwingine ila Malaika Mweusi aliyekuwa mbele yake.
Anderson akiwa kwenye mshangao mkubwa alishtuliwa na sauti ya Malaika Mweusi.
“Anderson nasikia unanitafuta kwa udi na uvumba mpaka umewaweka ndani watu wasio na hatia, sasa nimekuja sijui ulikuwa unasemaje?”
Kabla Anderson hajajibu kitu Malaika Mweusi akatoa kitabu na kumtupia juu ya meza:
“Nina imani kilichofanya unipige na kutaka kuniua ni hiki kitabu nimekuletea ukisome halafu niulize swali ambalo nitakujibu leo nipo tayari kwa lolote utakalo,” Malaika alizungumza kwa sauti ya upole aliyoizoea Anderson.
Anderson alikichukua kitabu huku mikono ikitetemeka alikirudia kukisoma kilikuwa vilevile kilikuwa hakijaongezwa kitu wala kufutwa.Baada ya kukisoma jasho jembamba lilimtoka lakini alijikaza kiume na kumuuliza swali kwa sauti ya kitetemeshi.
“ Haya majina ni ya nani?”
“Ni ya wafu kasoro jina moja tu la father Gin.”
“ Nani aliyewauwa?”
“ Mimi.”
“Ooh! Mungu wangu, “ Anderson alishika kichwa.
“ Uliza swali jingine nina muda mfupi wa kuendelea kukaa hapa,” Malaika alimwambia huku akiangalia saa yake ya mkononi.
“Wapo walionimulika mimi nikawachoma siku zote akuanzae mmalize.”
“Hapana ….hapana…..siamini kama wewe ni muuaji ila muuaji unamjua tafadhali mtaje ili tumtie hatiani ili afunguliwe mashitaka na kupata adhabu kubwa.“
“Ni mimi.”
“ Kama ni wewe siamini sijawahi kukuona unaua siamini.”
“Ni kweli siwezi kuua hata sisimizi ukiona hivyo ujue kuna sababu.”
“Ni kweli ulimuua mama?”
“Ndiyo .”
“Kwa sababu gani?”
“ Ipo sababu.”
‘ Ina maana mke wangu na mwanangu uliwaua wewe?”
“Ndiyo.”
“Malaika acha utani huu si wakati wa utani nieleze ukweli muuaji ni nani?”
“Muuaji ni mimi,” bado alishikilia kauli yake.
“kama ni wewe kwa nini umewauwa watu wote hawa?”
“Hii si sehemu ya kuujua ukweli, sasa hivi utaongozana na mimi usiulize nakupeleka wapi? Upole wako ndio utakaokusaidi usifanye ujanja wowote kwa usalama wako.“
Anderson alikubali, Malaika Mweusi aliuvaa ule ubibi kizee na kuongozana na Anderson hadi nje. Wote waliwaona walijua ameongozana na kikongwe, wakiwa wameelekea barabarani mara gari aina ya Land Cruiser V8 yenye vioo vyeusi ilisimama mbele yao aliamliwa kuingia ndani ya gari naye alifanya vile bila ubishi liling’oa nanga.
*****
Gari lilipoondoka, Malaika Mweusi alijirudisha akiwa katika hali yake ya kawaida.
Anderson alitulia tuli kama mtu aliyefungwa akitafakari Malaika ni mwanamke wa aina gani? Alikumbuka tabia ya kubadilika mara kwa mara aliyoelezwa na vijana wake pale walipokuwa wakimfuatilia.
Ndani ya gari kulikuwa na vijana wanne waliokuwa wamevalia fulana nyeusi za kubana huku miili yao ikionekana wazi kuwa ni watu wa mazoezi, walioonekana ni walinzi wa Malaika Mweusi.
Kwenye gari watu wote walikuwa kimya isipokuwa Malaika mweusi aliyekuwa akijiangalia kwenye kioo kidogo akiutengeneza vizuri mwili wake. Gari liliingia kwenye moja ya makampuni yake ambayo haikuwa ngeni machoni kwa Anderson kwani alishawahi kufika alipotembezwa na Malaika Mweusi.
Gari ilikwenda moja kwa moja hadi kwenye chumba kimoja ambapo gari liliteremshwa kwa kutumia 'lift' hadi chini na mara baada ya kufika chini aliamuliwa ateremke.
"Samahani mzee tafadhali teremka."
Anderson alitii amri na kuteremka, aliamuliwa aingie kwenye gari jingine aina ya Range Rover Sports Car jeusi, alitii amri na kuteremka kwenye gari moja na kuhamia jingine aliloelezwa,
Ndani ya gari lile ilikuea ni vigumu kuona nje, vioo vyake vilikuwa ni vyeusi tii visivyo ruhusu aliye nje kuona ndani hata wa ndani kuona nje. Gari liliondoka kupitia njia nyingine. Anderson hakujua anapelekwa wapi alitualia tuli kusubiri nini alichokusudia kikukifanya Maliaika Mweusi alikuwa tayari kwa lolote hata kufa.
Baada ya mwendo wa dakika ishirini gari lilipiga honi kwenye geti la mlango wa jumba kubwa la kifahari.
Baada ya gari kusimama wale vijana wanne waliteremka pamoja na Malaika Mweusi na kisha Malaika alimkaribisha Anderson ambaye muda wote alikuwa kimya.
"Karibu mheshimiwa karibu ujisikie kuwa mtu huru,” Malaika alisema kwa sauti tamu.
Jumba lililokuwa mbele yake hakuwahi kuliona kwa macho zaidi ya kuliona kwenye TV.
Akiwa bado ameshangaa Malaika alimshika mkono na kumkaribisha ndani kwenye sebule la kifahari.
"Karibu ujisikie kuwa upo kwako..ooh sorry si kama vile uko ugenini, hapa ni kwako japo makaribisho yenyewe hayakuwa mazuri lakini kutokana na kazi yako hutashangaa."
Anderson hakujibu kitu zaidi ya kuzidi kushangaa alikuwa akijiuliza kuwa lile jumba la nani, alitembeza macho yake kwa chati kulisanifu lile jengo lenye thamani mule ndani. Macho yake yalitua kwenye picha kubwa iliyomuonyesha yeye akiwa amekumbatiana na Malaika Mweusi na picha yake na nyingine ya Malaika kubwa ya paspoti zikiwa zimepamba sebule ile.
Kitu kilichozidi kumchanganya kilikuwa ukubwa wa jumba lile la Malaika Mweusi, akiwa katikati ya mawazo alishtushwa na sauti ya Malaika alipokuwa akiwaamuru walinzi wake watoke nje.
"Haya jamani endeleeni na shughuli zenu."
Walinzi bila ya kujibu waligeuka na kuondoka, Malaika alimgeukia Anderson ambaye bado alikuwa amesimama kama sanamu.
"Ooh, mpenzi karibu sana, japo najua moyo wako umejaa kisasi juu ya yote nina imani moyoni mwako mimi si Malaika wako Mweusi tena bali ni shetani Mweusi. Muda si mrefu utanielewa tafadhali ondoa hofu hakuna baya lolote litakalokupata," alimtoa hofu.
Wakati huo Malaika Mweusi alikuwa amejisogeza karibu kabisa na Anderson na kumshika begani.
"Mbona umegeuka kuwa bubu? Onyesha angalau furaha bila woga."
"Lakini kwa nini umefanya hivi?” Anderson aliuliza swali la kukurupuka.
"Utanielewa maadamu tupo pamoja na sehemu yenye usalama na utulivu wa hali ya juu hapa hata wanajeshi wa Bush waliomshika Sadamu hawawezi kufika."
"Yaani siamini..siamini tena naona kama njozi akili yangu haikubali kama muuaji ni wewe, kwa nini usimseme au ndiye aliyetaka kukuua ili usitoe siri..nakuhakikishia ukimtaja utapata ulinzi kama wa rais.
"Basi ondoa hofu mpenzi utamjua sasa hivi..."
Malaika Mweusi alisema yale huku akimpapasa mgongoni kwa mikono yake laini.
"Sasa mpenzi twende kwanza ukaoge ili utoe uchovu maana naona kila muda nikikuona unatoka jasho."
"Sasa mpenzi twende kwanza ukaoge ili utoe uchovu maana naona kila muda nikikuona unatoka jasho."
"Usiwe na hofu taarifa za muuaji ni muhimu kuliko hata huko kuoga".
"Sasa mpenzi unataka kuniudhi umetaka nikueleze muuaji wa kweli nimekubali sasa haraka ya nini habari zake si za kubabaisha inahitaji muda na utulivu, naomba unisikilize twende."
"Sawa,” Anderson kama kawaida yake hakuwa na ubishi mbele ya kauli ya Malaika mweusi.
Waliongozana hadi ghorofa ya juu katika jumba lile lililokuwa na ghorofa moja, Malaika Mweusi alimuingiza hadi kwenye chumba cha kulala chenye kitanda kipana sana na sofa za nguvu za kukalia kilikuwa ni chumba cha gharama sana.
Anderson alikaa kwenye sofa na Malaika Mweusi alikwenda hadi kwenye kabati alivua nguo alizokuwa amevaa na kuvaa upande mmoja wa kanga nyepesi bila ya kitu chochote ndani.
Alichukua taulo hadi kwenye kiti alichokuwa amekaa Anderson na kumvua zile nguo alizokuwa amevaa na kumfunga taulo, waliongozana wote hadi bafuni kuonga. Walipotoka kuoga Malaika Mweusi alimpa bukta Mr Anderson ambayo ilionekana ni mpya na fulana ya mikanda ambayo iliuweka mwili wazi ili upate baridi.
Akiwa amevalia kigauni chepesi cha kulalia alimuongoza hadi kwenye chumba kimoja kilichokuwa na computer na makochi madogo mawili. Alimuacha Anderson akiwa amekaa kwenye kiti alitoka na baada ya muda alirudi na chupa kubwa ya pombe na glasi mbili zenye shingo ndefu.
Aliziweka kwenye stuli aliyoichukua sebuleni alimimina whisky katika glasi zote mbili na kumkaribisha Anderson aliipokea na kuigonganisha na ile ya Malaika Mweusi kwa lengo la kutakiana heri kinywaji chao.
Wakiwa wamekaa kila mtu na kiti chake wakitazamana, muda wote akili ya Anderson haikuwa sawa kwani alitaka kumjua muuaji halisi.
"Thereza nakusikiliza," Anderson alivunja ukimya.
Anderson kwa mara ya pili alimuita jina lake halisi ambalo lilimganda kichwani mwake kwa muda mrefu.
"Hakuna tatizo nitakueleze."
"Thereza.”
"Abee".
"Nani muuaji?"
"Mimi".
"Thereza huu si muda wa utani wewe si muuaji, muuaji yupo nieleze ukweli nani muuaji?"
"Anderson shida yako ni kumjua muuaji au unataka nini kingine?"
"Nataka kumjua muuaji wa kweli."
"Mimi ndiye muuaji."
"Kwani ukimtaja kuna nini?"
"Wewe umegunguaje kuwa mimi namjua muuaji?"
"Kwenye kitabu."
"Ule mwandiko ni wa nani?"
"Wako."
"Sasa kwa nini hutaki kuniamini au kuuliza nini chanzo cha mauaji, nafikiri hili ni muhimu kuliko kung'ang'ania kitu kisicho kuwepo."
"Sawa, kama ni wewe kwanini umefanya mauaji yale na ulifanya kwa kushirikiana na nani?"
"Kwa kweli mauaji yote niliyofanya ni kisasi yaani ni malipizo ya yote niliyotendewa ila kwenye kitabu changu kila jina lililokuwepo kwenye kile kitabu nimemuua kwa mkono wangu."
"Sawa hao wakubwa walikukosea na Gift alikukosea nini?"
"Kwa wepesi hivyo huwezi kuelewa tulia utalewa vizuri kisha ruksa kunifikisha kwenye vyombo vya sheria. Nipo radhi kwa hukumu yoyote itakayotolewa juu yangu tena safari hii sitapotea kama nilivyofanya awali."
Malaika alipiga funda moja la whiski na kuendelea kuzungumza, aliinama kama dakika mbili bila ya kuongea kitu alipoinuka tayari macho yake yalikuwa yamebadilika kuwa mekunduna kamasi nyembamba zilimtoka huku mishipa ya kichwa ikiwa imesimama kitu kilichomshtua Anderson.
Alijawa na mawazo na kujiuliza maswali yaliyokosa majibu kwani alimuona ni kiumbe kilichobadilika kila wakati, alizungumza kwa sauti yenye kitetemeshi iliyojaa machungu iliyochanganyika na kilio kitu kilichomfanya Anderson kuhoji:
"Thereza mbona unaniangulia kilio badala ya kunieleza sababu za wewe kutoa roho za watu ambao mimi nina imani hawana hatia."
"Anderson inaniuma sana lakini sijui nilichokifanya ni kwa sababu ya kufanya hivyo japokuwa marehemu mama alinikataza nisilipe kisasi. Ni historia ili unielewe lazima nianze kutoka chimbuko langu.
"Nikiwa na umri wa miaka sita akili yangu ilipembua zuri na baya nilishuhudia maisha ya manyanyaso na mateso aliyopata mama kutoka kwa baba ambaye kila siku alikuwa akimpa kipigo kila akirudi kutoka kwenye pombe.
Mpaka napata akili yangu nilimkuta mama akiwa hana baadhi ya meno mdomoni lakini baba hakujali hilo zaidi ya kuendelea kumpa kipigo cha mbwa mwezi. Kila nilipomwa mama amshitaki baba lakini alikataa na kusema anamuachia Mungu kila nikimuangalia mama roho iliniuma sana nilikuwa sina jinsi.
Kuna wakati nilishindwa kuvumilia manyanyaso ya baba nilikwenda kwa wazee ambao ni jirani lakini nao waliogopa kutokana na ukirofi wa baba. Maisha ya manyanyaso na kipigo yaliendelea na hali ile mama aliizoea siku ikipita bila ya mzozo wowote au mama kupigwa ilikuwa kwa bahati mbaya.
Nikiwa darasa la nne siku moja nilirudi nyumbani na kumkuta mama yangu akiwa mwenye wasiwasi mwingi kitu kilichonitia hofu ilibidi nimuulize mama.
"Mama vipi mbona haupo katika hali yako ya kawaida kulikoni?"
"Mwangu leo mbona kasheshe ," alinijibu.
"Kasheshe ya nini tena mama?".
"Sijui kama leo nitalala baba yako alitaka nimpikie bata lakini wakati nimefuata maji kisimani huku nyuma sijui kaja mbwa au paka amechukua baadhi ya nyama."
"Sasa mama si umueleze ukweli," nilimshauri mama.
"Wewe si unamjua vizuri baba yako anaelewa neno?".
"Mmh! Sasa utafanyaje?"
"Nasubiri kipigo sina kingine."
Kauli ya mama iliniumiza roho na kujiapia siku hiyo nisingelala, nitakaa macho mpaka baba atakaporudi."
Usiku ulipoingia niliingia chumbani kwangu na kujilaza lakini masikio yote niliyaelekeza chumbani kwa wazazi wangu, majiri ya saa tano baba alirudi kwa bahati nzuri nilimsikia mlango ukifunguliwa na mama.
Niliwasikia wakizungumza japo maneno yao sikuyasikia vizuri, baada ya muda kidogo nilisikia kilio cha mama hapo nikajua shughuli imeanza. Nilikurupuka kutoka chumbani kwangu na kwenda chumbani kwa wazazi wangu, nilimkuta mama amelala chini huku baba akimshindilia miguu ya kichwa.
Mama alimuomba msamaha huku akimweleza baba kuwa anamuua lakini baba hakusikia kilio cha mama kilichochanganyika na maumivu makali...masikini mama yangu alikuwa kwenye mateso makali. Kufika hapo Malaika Mweusi alianza kulia. Alifuta machozi yake kwa kutumia lile gauni lake, kisha aliendelea.
Kuona vile ilibidi niingilie kati kwa kumvamia baba japo kwa nguvu wala mwili simuwezi lakini nguvu niliyoingia nayo ilimfanya baba apepesuke na kuangukia upande wa pili kwa ukali alinifokea.
"Wewe mtoto unaweza kuingilia ugomvi wetu huna adabu eeeh."
"We Thereza hebu ondoka," mama alisema kwa sauti ya chini iliyoonesha kuwa ana maumivu makali ya kipigo, sikukubali nilipomfuata baba aliyekuwa anamrudia mama kutaka kumpiga, alinisukuma hadi ukutani ambako niligonga kichwa na kupasuka wakati huo baba aliendelea kumsurubu mama. Nami sikukubali nilijitupa juu ya mama ili atuue wote wakati huo mama alikuwa amekata kauli.
Baba aliendeleza kipigo pale aliponikanyaga mgongoni na kunipiga kwa mateke ya mbavuni mpaka nikapoteza fahamu. Nilizunduliwa na maji yaliyokuwa yakinidondokea kwani nyumba yetu ilikuwa ya miti kutokana hali yetu ya umaskini tuliyokuwa nayo.
Nilizinduka na kujizoa pale chini huku mwili wangu wote ukiwa unaniuma kwa maumivu ya kipigo cha baba. Mama alikuwa amejilaza pembeni yangu huku akikoroma nilimgeukia na kumuita.
"Mama..mama..”
" Mwanangu Tereza nichemshie maji ya moto unikande mwili," aliitikia kwa tabu sana wakati huo baba alikuwa ameondoka. Niliwasha moto wa kuni kwa shida na kumchemshia maji ya moto mama. Maji yalipopata moto nilimkanda mwili mzima kidogo alianza kujisikia nafuu.
Siku hiyo baba alirudi mapema ambapo alimletea mama dawa za maumivu aina ya panadol na kisha kuondoka. Kwa kweli hali ya mama haikua nzuri muda wote alishinda amelala hata kujigeuza kwake ilikua ni shida ilikuwa lazima akipiga kelele za maumivu hata mimi pia mwili wangu ulikuwa na maumivu hasa nyonga na sehemu za mbavu nilizokanyagwa na baba na jeraha la kichwani lililopasuka.
lakini kutokana na hali ya mama ilibidi maumivu yangu niyaweke kando ili nimhudumie hata shule ilinibidi nisitishe kwa muda kwa ajili ya mama yangu, siyo siri mama yangu nilimpenda sana.
Baada ya siku chache za kumhudumia kidogo mama alipopata nafuu ilibidi nianze kwenda shule lakini hata hivyo ilinilazimu niwahi kurudi nyumbani kumjulia hali kwa kuwa alikuwa hawezi kufanya kazi yeyote.
Siku moja niliporudi nyumbani kumjulia mama hali yake nilimkuta katika hali mbaya sana akiugulia maumivu nilimkimbilia chumbani kwake ambapo alikuwa amelala kwenye kitanda na kumuita.
''Mama...mama.''
''Ooh...ooh Mungu wangu..nakufa mie..''
''Mama..nini tena mama yangu..mbona unanitisha?”
''Aaha..nani..mwanangu Thereza?” mama aliniuliza.
''Abee mama, ndio mimi.''
''Ooh, vizuri njoo unigeuze upande huu.”
Nilimshika na kumgeuza ambapo alipiga kelele kutokana na maumivu. Maskini mama yangu aliteseka..sijui wanadamu wengine kwa nini Mungu aliwaumba katika hali ya ubinadamu kwa nini asiwaumbe wanyama nilimchukia sana baba sijui nimfananishe na kitu gani,” Malaika alisema kwa uchungu mkubwa huku machozi na makamasi yakimtoka japo jambo lile lilitokea muda mrefu.
ITAENDELEA
Your Thoughts