Type Here to Get Search Results !

BANGUZI 2

 RIWAYA: BANGUZI

NA: HASSAN O MAMBOSASA


SEHEMU YA PILI



Kuagana kwa Heriety na Spora haukuwa mwisho wa mazungunzo kwa wanadamu wote, bali ni kwao tu. Upande mwingine ndani ya dunia hii, nchi hiyohiyo waliyopo. Mwanamke mmoja alikuwa amesimama nje ya nyumba kuukuu, akiwa anatazama mkabala na mwanamama mwingine ambaye amevaa vilivyo kuliko yeye. Upande mwingine wa nyumba hiyo kulionekana turubai kubwa, kukiwa wanaume kadhaa waliyopo hapo wakiwa wametulia huku minong'ono ikiwa inasikika kwa mbali. Umbali uliyopo kutoka hapo walipo, hadi ambapo wanaume wamekaa. Hakukuwazuia kuweza kufanya mazungumzo yao, waliamua kuwa huru nayo.


"Shoga mimi ndiyo ninaingia hivi sasa tangu siku nilivyoondoka niambie kunani hivi sasa hapa?", Mwanamke aliyefana kimavazi alisaili.


"Yaani shoga mara moja hii ushasahau, hujui kama siku kama ya leo ndiyo ambayo Jamal alitutoka (machozi yakimlenga). Mwaka wa pili huu bila mwanangu, Mungu ndiyo anajua kwanini amenitenganisha naye. Alimpa maradhi hadi akaja kumchukua Jamal wangu"


"Nimeshasahau mwenzangu, ila pole kwa hilo. Kazi ya Mola haina makosa. Wajua wote duniani tumezaliwa na siku moja tutatoweka, shukuru Mungu kwa kila hali shoga kidonda cha miaka miwili iliyopita usikitoneshe tena mwenzangu"


"Sawa, niambie za huko utokapo?"


"Kwema tu Shoga, nimepita hapa nikwambie mzigo unaenda vizuri huko. Kariakoo wateja ni wengi siku hizi yaani mambo ni safi. Mgao wako ni huu hapa" Mwanamke yule aliposema hivyo, alitoa burungutu la pesa na kumpatia mwenzake ambaye alilifunga kwa haraka kwenye pindo la nguo.


"Mwenzangu safari tuongeze mzigo na twende wote, tusaidane maana naona siku hizi mambo ni supa kama kabisa. Wateja wengi hadi mzigo wote umeisha haraka hivyo"


"Fanya hivyo Fatuma, kazi iishe haraka maana tukiwa wawili mambo yatakuwa rahisi tu"


"Haya shoga, wacha mimi nikaendelee na mengine huko ndani si unajua kuna ugeni leo"

"Haya mimi nawahi nyumbani"


Wanawake hao waliagana, mmoja alirejea ndani na mwingine akashika njia yake. Eneo hilo haikupita muda mrefu kulianza kunukia harufu ya ubani huku dua zikisomwa. Muda huo Kiongozi wa dini wa eneo hilo aliitwa kuongoza dua hiyo, yeye bila ya kusita aliisoma hapo huku akisaidiwa na baadhi ya wasaidizi wake. Hakukuwa na uchangamfu wowote ule, shughuli yenyewe ni kumbukumbu kwa marehemu haikuhitajika kuwekwa kikolombwezo chochote. Dua na ulaji wa chakula ndiyo ulifanyika, majira ya mchana kila kitu kilitimia. Wenyeji walitoa shukrani za dhati kwa wote waliyowasaidia hadi kukamilika kwa kumbukumbu hiyo, baada ya hapo wageni walitawanyika wakabaki wenye nyumba hiyo tu.


****


"You know what? I'm so happy today, sikutegemea kama ningeweza kufika na kukipata hiki nilichonacho hivi sasa. Mungu ndiyo muweza wa yote" Sauti ya Kijana mmoja ilisikika ikiwaambia wenzake waliyovaa majoho ambao wapo kwenye viti vya plastiki vilivyozunguka meza

"Jeta si wewe tu hadi hapa wote tuna furaha ya hayo hebu muulize hapo Bibie Lui, uone kama hana furaha", Msichana mwingine alisema huku akicheka na kupelekea Jeta na Binti mwenye kujulikana kwa jina la Lui watazamane kwa bashasha kisha wakapigana mabusu mbele ya wenzao wote. Makofi yalifuatia huku wengine wakishangilia hali hiyo.


Wapenzi hao walionesha mapenzi ya dhati kwao, pamoja na furaha kuu waliyo nayo kwenye siku muhimu katika maisha yao. Majoho waliyoyavaa ambayo yalisheheni mataji mbalimbali yaliashiria ni namna gani walivyo na furaha katika maisha yao. Kwa pamoja waliinua bilauri za vinywaji vyao na kuzigonganisha, mlio wa mgongano huo unapelekea kusikika mvumo wa ving'ora vya gari la wagonjwa pamoja na sauti ya mwanamke akilia kwa uchungu. Hii inamfanya Gina agutuke kwa nguvu kutoka mahali ambapo anaziona bilauri za vinywaji za nyumbani, alirudi nyuma kwa mshtuko na kuanza kuhema huku machozi yakimtoka hata ashindwe kuongea chochote kile. Majira hayo alikaa kwenye kochi sebuleni, aliinuka na kukimbia chumbani kwake kwa uoga huku akiwaacha wadogo na mama yake wasielewe nini kinachoendelea.


"Hebu Eliza kimbia haraka kamwangalie dada yake asije kujidhuru bure", Mama yao alisema na binti yake akatii, alipoondoka aliweka mikono kichwani huku akisema, "Mungu wee! Sijui mwanangu anakumbuka nini au anaona kitu gani kila akiona vitu hivyo. Picha zake zote tumezificha, sasa mara kioo kinamfanya awe kivingine mara glass hizi nazo dah!"


"Mama cool down, everything will be okay", Spora alisema.


"Okay, ila haya anayoyafanya yananishangaza sana yaani nafikiri hata kwenda kwa Sangoma nikidhani ni jambo la giza linamtesa"


"Mama tusifikie huko, hebu tusubiri baada ya jumamosi ndiyo tutajua nini cha kufanya. Nampenda sana dada yangu nipo radhi arejee kwenye hali ya kawaida, ila si kwa imani hizo ambazo hapo awali ulizipinga kwani nyumba ya ibada alishaingia na kufanyiwa maombezi ila hakukuwa na nafuu yeyote"


****


_FIJI_

Mlio wa feni uliendelea kusumbua ingawa ulitoa vitu viwili kwa wakati, navyo ni faraja pamoja na kero kutoka ukuukuu wake na kuendelea kufanya kazi pasipo kufanyiwa marekebisho. Ufariji wake ulimfanya Mtumiaji asiweze kuhisi kama ni karaha zaidi ya kuendelea kufanya kazi zake kwa muda mrefu, liliendelea kufanya kazi yake huku aliyepo kwenye ofisi yenye samani za kisasa pamoja na kiyoyozi ambacho kilizimwa kutokana na hali ya hewa ilivyo kiasi cha kuruhusu madirisha kuwa wazi. Ofisi hii ilipambwa na kuta zenye rangi nyeupe, huku aliyepo hapo ndani akiwa na suti pamoja na koti jeupe likiwa limezungushwa nyuma ya kiti. Haikuhitaji elimu ya ziada kuweza kung'amua kuwa hapo ni hospitali, na huyo aliyepo ni Tabibu.


Daktari huyo akiwa na kifaa chake cha kufanya kazi shingoni alionekana akiandika faili fulani, mara akasikia mlango ukifunguliwa kisha akaingia Muuguzi mwenye asili ya kihindi akiwa na faili mkononi mwake. Huyu alimfanya aachie tabasamu kumwona kwake, naye alipokea bashasha kutoka kwa nesi huyu.


"Naam Ladhika, karibu", Alimlaki.


"Asante Dokta Aesop naona unaendelea kuwajibika, tangu uje huku Fiji sijakuona walau ukiwa ni mwenye kutembea tu zaidi ya kufanya kazi tu na kutulia nyumbani kwako ukiendelea na majukumu ya kitabibu"


"Nimejifunga kwenye kifungo cha kuokoa maisha ya wanadamu wenye matatizo ya aina hii, wacha nitumie muda wangu mwingi katika kutafuta mbinu mbalimbali za kusaidia wanadamu. Wengi ni wenye kuhitaji msaada kila kukicha, nimezunguka nchi kadhaa nikisaidia watu wa namna hii na nakutana na matatizo ya aina tofauti hivyo lazima nitumie muda wangu mwingi kuwasaidia" Dokta Aesop akisema hayo Ladhika aliweka faili mezani kwake kisha akaanza kutalii mandhari ya humo ndani kama ndiyo anayaona, alizungusha macho kutoka pande moja hadi nyingine. Hatimaye akaja kuyatuliza kwenye picha mbili ziliyopo ukutani humo ndani, alizitazama kisha akarejesha macho kwa Tabibu.


"Dokta umekuwa mwingi wa kazi na wala hukuwahi kuniambia watu wale waliyopo pale ukutani ni kina nani. Nakutambua wazi wewe ni Mgiriki na umezaliwa nchini Ugiriki, na familia yako ipo Ugiriki. Nitazamapo watu weusi kama wale ambao unasema ni muhimu kubaki na kumbukumbu zao kichwani mwako, huwa hunifafanulii"


"Ladhika, nina kila umuhimu kwa mmojawapo kati ya wale wawili. Huku nikibaki kujivunia sikuwahi kumwona mtu jasiri kama yeye. Wingi wangu wa kazi ndiyo unanifanya nishindwe hata walau kukosa nafasi ya kukueleza hilo, ila naamini siku ya jumapili asubuhi ndiyo wasaa mzuri wa kuweza kukufunulia kila kitu. Ukajua kwanini nimependa kuongozana na picha za vijana hawa wawili, ninawahusudu sana"


"Sawa utunze ahadi yako tu Dokta..... faili la mgonjwa ulilolihitaji hilo hapo mezani wacha nikaendelea na kazi zangu nyingine"


"Majira hayo napenda sana kufanya mazoezi angalau ya kukimbia, huwa sina ratiba ya kikazi labda itokee kuna mgonjwa wa dharura. Vinginevyo nitakuwa ninaendelea na kuuweka mwili wangu sawa. Nashukuru kwa kuniletea faili hilo, nahitaji nipange cha kufanya juu yake huyu kijana"


"Sawa Dokta, hata siku hiyo nipo mapumziko nafikiri itakuwa muda mzuri haswa kujua kuhusu hilo. Nikuache ufanye kazi kwa hivi sasa"


Ladhika alitoka na kumwacha Dokta Aesop akiendelea kufanya kazi yake, kwa jinsi alivyojitolea maisha yake kwa ajili ya kushughulikia maradhi ya watu wengine. Kwa jina kamili anaitwa Dokta Achillios Aesop, tabibu mwenye shahada ya uzamivu kuhusu masuala ya moyo wa mwanadamu. Ametumia muda wake mwingi kusema taaluma hiyo pamoja na kufanyia kazi kwenye nchi mbalimbali. Ni mwenye familia na alishawahi kuoa ila walitofautiana na mke wake hivyo walitalikiana, ana watoto wakubwa na wote ni matabibu wakubwa nchini Ugiriki.


Daktari huyu hupenda haswa kufanya tafiti na kujua kila tatizo jipya ambalo linahusu taaluma yake na kuweza kulitatua. Hili lilipelekea agundue aina mpya ya matibabu ya maradhi kadhaa ya moyo ambayo yalishindikana. Ilimpelekea kutunukiwa uprofessa ila hapendi kutumia zaidi ya kubaki kujiita Dokta, nchini kwao tu ndiyo wanamtambua kama Professa Achillios Aesop. Huyu bwana kwa kubobea zaidi kwenye taaluma hii, suala la maslahi katika matibabu mara nyingi huliweka kando. Zipo mara nyingi alizoweza kufanya kazi kwa kujitolea kwa nchi mbalimbali, ili aweze kuokoa maisha ya watu ambao hawana kipato cha kukidhi matibabu hayo. Hupenda sana kusafiri na kikosi chake cha matibabu kutoka nchi moja hadi nyingine, kutafuta mahali ambapo kuna wenye shida. Wale waliyo na kipato walitozwa pesa, ila wasiyo na uwezo walisaidiwa na gharama zake alizibeba yeye mwenyewe ikiwemo kuwalipa watu wake.


Alipendwa sana kila nchi anayofika kutokana na moyo wake wa kujitolea kwa watu wasiyojiweza, alizunguka mabara kadhaa na hatimaye akaingia barani Afrika. Huko ndipo alitembelea nchi zote akishughulika na tatizo hilo, hatimaye akaja Tanzania ikawa nchi ya mwisho kupita akiwa na matabibu wake. Nchi hiyo aliipenda mno kiasi cha cha kuweka makazi kwa mdua mrefu, huku akiwalipa madaktari wake wasaidizi gharama nyingine baada ya kumaliza kutibu warejee nchini Ugiriki. Yeye akawa mkazi wa nchini humo, hata watoto wake wakawa wanafika kumwona na kurejea. Huko ndipo alipoweza kuweka historia ya kipekee na kujionea mengi akiwa huko. Hadi pale alipofikiria ni muda mwafaka wa kuhama na kwenda kuishi sehemu nyingine za duniani na kupelekea aangukie nchi ya mashariki ya mbali iitwayo Fiji.


****


Toka aingie ndani kutokana na kumbukumbu zile zilizomnga kwa ghafla na kisha kupotea, hakula chochote na hata alipohimizwa kula ikawa kazi bure. Usiku ulimkuta namna hiyo na hata akapitiwa na usingizi pasipo kutia kitu tumboni mwake. Asubuhi ya siku ya jumamosi ndipo alipoamka, aliogeshwa na kusafishwa kinywa kisha akawekwa kitandani. Siku hii hakuleta mgomo wa kutia chakula, alilishwa na kutii amri hadi alipomaliza akaachwa apumzike.


Ikawa ni ahueni kwa ndugu zake, alitulia na utulivu ambao kidogo uliwafanya wawe na amani. Pamoja na kuchanganyikiwa kwake, Gina hakuwa na fujo kuu kama ilivyo wengine, labda akumbuke kitu halafu kimtoke kichwani na kuanza kumvuruga akili yake ndiyo angefanya mambo ya ajabu. Vinginevyo utulivu ndiyo kawaida yake daima, hadi majira hayo yakawa ni hayohayo akiwa ni mkimya kupitiliza na wala hakuongea lolote lile. Si Bubu ila msongo wa mawazo ndiyo umemfanya awe namna hiyo, ndugu wamehangaika mno kwa madaktari wa kawaida ambao wamewashauri kutumia vindonge tu vya kuweza kutuliza hali hiyo. Ndiyo wanafuata ushauri huo, ikawa akionekana kuleta jambo jingine geni kabisa basi hufanya hivyo na aendelee kukaa kwenye hali ya utulivu. Dawa zikiisha Tabibu aliyekuwa akimpatia tiba, ndiye aliyewashauri wafike na kuchukua zingine na si kuzitafuta madukani.


Watu wengi husema sana kuwa maisha ya dawa si mazuri, ila kwa familia hii ni bora wangeendelee na dawa kama walivyoshauriwa na daktari ambaye huwa anamtibu mara nyingi. Kanuni ile ya kufuata ushauri wa mganga wa kisasa waliiona ni ahueni, ingawa hadi kufikia majira hayo hawakuwa wameona tumaini lolote ile.


****


Siku hii ya jumamosi ni siku mapumziko, ambapo sehemu zingine wafanyakazi huwa hawafiki kabisa. Huku wengine wakifanya kazi hadi saa sita mchana kisha hurejea makwao kupata mapumziko. Mmoja wa watu wasiyogusa ofisi zao siku za mapumziko, alionekana akiwa ameketi eneo la nje la nyumba ya kifahari huku akibarizi upepo mwana utokao ufukwe wa bahari ambao haukuwa mbali kutoka hapo alipo.


Pembeni yake alisimama kijana aliyevaa fulana nyeusi pamoja na suruali aina ya 'jeans' akiwa mtulivu tu. Mtu huyo alionesha ni namna gani mwenye kupenda ukwasi, alivaa madini ya gharama kubwa shingoni akiwa na ameketi eneo ambalo jirani kuna chupa ya mvinyo wa bei ghali. Pembezoni ilionekana bilauri imejazwa kimiminika chekundu.


"Leo hivi huu mpango wa kuendelea kuwepo nchini Tanzania utauendeleza hadi lini?", Kijana aliyevaa nguo nyeusi aliuliza.


"Hadi nisikie Kaka yangu amefariki dunia ndiyo nitaondoka mahali hapa, hii kwa dunia nzima iweze kuishi. Nimefoji taaluma kwa ili tu niweze kuwaokoa wanadamu", Leo alijibu.


"Naelewa hilo, ila vipi Jus akijua kama upo huku, unafikiri itakuwaje wakati anajua kabisa ulimpiga vita muda mrefu tangu upo nchini kwetu kule. Unafikiri hawezi kuhisi kuna mkono wako katika hili"


"Ndiyo maana sitaki anione katika hili, nimechagua nijifanye mwenye taaluma hii makusudi ili nisiweze kukutana naye tena mara nyingi kazi zangu nafanya kwa usiri mkubwa. Najua siku zake zitahesabika, niko radhi kuondoka na kurejea nchini kwangu hadi pale tu nitakaposhuhudia kifo chake na si vinginevyo"


"Vizuri kwa kusimamia maisha ya wengi, ila aliyemfanya vile hana huruma hata thumni nakwambia"


"Ukimfanyia kazi ukatili jua, ukikosea kufanya kazi yake lazima akufanyie ukatili. Leo ratiba vipi mbali na mapumziko?"


"Supervisor kashauri tupumzike ndani tu tusitoke si unajua huyo jamaa yako anayekaribia kuanza kutumia Kitimaguru anazunguka jijini sana siku hizi"


"Ok hakuna shaka ilimradi kazi isiweze kuharibika"


****


_JUMAPILI_,

_ SAA KUMI NA MBILI_, 

_FIJI_ 


Tofauti ya masaa nchini Tanzania na jamhuri ya Fiji, ni masaa tisa, ambapo nchi ya bara la Afrika ipo nyuma kimasaa. Majira hayo ni saa tatu usiku, kule ni saa kumi na mbili asubuhi. Muda huo Dokta Aesop alionekana akikimbia taratibu akikatisha mitaa kadhaa ya eneo analoishi nchini humo. Akiwa pembezoni mwa barabara alikimbia huku akipishana na magari machache tu asubuhi, jasho likimvuja aliendelea kukatiza mitaa hadi akafika eneo ambalo kuna kituo cha mabasi ya kukusanya abiria nchini humo. Hapo akamkuta Ladhika akiwa amevaa nguo za mazoezi ameketi, akiwa bado mwili una moto alisimama huku akirusha miguu akihema kwa kutoa pumzi puani.


"Dokta ndiyo maana umri umeenda sana ila bado unaonekana ni mwenye miaka hamsini tu", Ladhika alisema huku akitabasamu.


"Mazoezi ndiyo kila kitu ndani ya dunia hii, sitaki nije kutembelea fimbo mapema yote hii. Hata kama nimegusa miaka sabini", Dokta Aesop alisema huku akihema kwa kuchangamsha mwili kwa muda mrefu.


"Hongera, naona leo umetunza ahadi yako ile. Karibia hapa subira yangu mahali hapa ni kwa ajili ya kusikia tu kuhusu hao"


Dokta Aesop aliposikia hivyo aliketi jirani na Ladhika halafu akasema, "Kwakuwa umeonesha nia ya kutaka kutambua kwanini ninatembea na picha za watu weusi wale, sina budi kukueleza. Ila unapaswa utambue kuna sababu kuu mbili, ya kwanza ni upendo na nyingine ni ujasiri na kujitoa kwa lolote"


"Ndiyo Dokta"


Tabibu wa siku nyingi akaanza kusimulia, "niliwahi kuzunguka nchi mbalimbali duniani, ila Tanzania nakumbuka ni ardhi iliyonivutia. Ni nchi isiyokuwa na maendeleo makubwa sana, ila aina ya watu wake wanaoishi huko ndiyo walinivutia haswa na kutamani kuendelea kukaa hapo. Niliwasili na jopo la madaktari wasaidizi wapatao kumi na tano nchini humo, ambapo tuliweka kambi yetu ya kwanza eneo la mnazi mmoja na baadaye tukahamishia hospitali ya taifa ya nchi ile. Tulihudumia watanzania wengi kwa kujitolea tu huku nikipoteza kiasi kikubwa kwangu kuona wanadamu wengine wanasalia kuishi duniani. Kusikika kwetu kulipelekea watu mbalimbali kuanza kumiminika jijini Dar wakidhani ni sehemu moja tu tungefikia, siku za kuwepo jijini humo zilipokatika tuliondoka moja na kusogea mkoa wa Pwani. Tukaweka kambi hospitali iitwayo Tumbi, huko tuliendelea na tiba yetu vilevile. Tulimaliza huko kote na hatimaye tukafika mikoa mingine, hadi tukaja kuangukia mkoa ule ambao umenifanya niweze kubaki na picha ya bini uliyeiona kule ofisini kwangu. 

ITAENDELEA...

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.