WAKILI WA MOYO 01


Hadithi: WAKILI WA MOYO

SEHEMU: 01

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

SIMU: +255713 646500

                                     

Maumivu ya moyo hayana msaidizi na  moyo wa kupenda hauna subira, kilichojificha moyoni huwa sawa na mfungwa asiye na kosa lakini hajui kujitetea. Siku zote anayependa  kama mhusika hajui kama anapendwa huwa mateso ya kujitakia.  Cecilia  msichana alinayetoka katika familia ya  maskini  anampenda Colin mvulana  aliye katika familia ya kitajiri mwenye  mchumba anayetaka kufunga naye ndoa. Anajikuta akiumia kila akimuona, pamoja na kuonekana jambo hilo kama  maji kupanda mlima lakini msichana Cecy  anauapia moyo wake kuwa  atauwekea wakili  na kuweza kushinda kesi ya maumivu ya mapenzi. 

Je, atafanikiwa? Kuyajua yote ungana tena na mtunzi mahiri  katika hadithi tamu ya mapenzi ili upate uhondo mwanzo mwisho.

TWENDE KAZI.....     

Mama Cecy  alishangaa kumuona mwanaye amerudi mapema huku sinia likiwa limejaa ndizi, alimalizia kupuliza moto wa kuni kisha alitoka jikoni huku akifuta machozi kwa upande wa khanga kutokana na moshi wa kuni kumuingia machoni. Alimtazama  binti yake aliyekuwa amekaa chini huku ameshika tamaa na machozi kumtoka.

“Cecy  nini tena  mama?” alimuuliza huku akimsogelea.

“Mama  hata nashindwa kujielewa sijui ni kwa nini inakuwa hivi?” alisema huku akiondoka mkono shavuni bila kufuta machozi. 

“Una lingine au ni lilelile za siku zote?”

“Kuna lingine lipi mama yangu! Hata sijui kwa nini nimejiingiza kwenye mateso ya kumpenda Colin mtu ambaye  hayajui mapenzi yangu kwake.”

“Lakini kwa nini mwanangu unapenda kuota ndoto za mchana, wewe na Colin wapi na wapi  kama mbigu na ardhi.”

“Najua mama utasema hivyo lakini katika mapenzi hakuna kitu kama hivyo, nakuapia kwa Mungu Colin  atakuwa mume wangu wa ndoa.”

“Cecy mwanangu hebu achana na kujishugulisha na masuala ya mapenzi, hebu jiangalie ulivyo na alivyo Colin. Kwanza mwenzako hand same.”

“Hata mimi beutiful girl,” Cecy alijibu kwa kujiamini huku akinyanyuka na kujishika mkono kiunoni kujionesha kuwa ni mrembo.

“Mwenzio ana elimu ya chuo kikuu wewe darasa la saba la kufeli, mwenzako  anatoka  kwenye familia ya kitajiri wewe pangu pakavu tia mchuzi. Kingine ambacho kinafanya usiweze kabisa kumpa ni kuwa Colin ana mchumba na mipango  ya harusi ipo karibuni sasa huyo Colin  yupi wa kukuona?”

“Mama nina uhakika kwa asilimia mia Colin kunioa,” Cecy alisema kwa kujiamini.

“Wee mtoto una wazimu? Au kuna mganga kakudanganya, maana siku hizi ushirikina hauna mtoto wala mzee.”

“Mama katu mapenzi sitayaendelea kwa mganga, ila nitayapigania kwa  nguvu zote.”

“Kipi hasa kinakupa jeuri ya kusema hivyo?”

“Ipo siku nitakwambia lakini amini ndoa ya Colin na Mage haipo ila mimi ndiye mke wake.”

“He he he heee, usinichekeshe miye, kwa nini unasema hivyo?” mama Cecy alicheka mpaka machozi yakamtoka.

“Mage hampenzi Colin.”

“We umejuaje?”

“Ni historia ndefu mama.”

Cecy alianza kumhadithia mama yake sababu ya kuamini siku moja Colin atakuwa mpenzi japokuwa hajawahi kumtamkia kitu kama hicho hata siku moja.

 Alianza toka siku ya kwanza kumuona Colin, Mage msichana aliyetoka katika familia ya kimaskini elimu yake ya darasa la saba shuleni alikuwa mmoja wa wasichana waburuza mkia.

Baada ya kufeli kwenye mtihani wa mwisho aliamua kufanya biashara ya ndizi kwa kupita mtaani kuuza.  Japokuwa alikuwa maskini lakini alijipenda sana.

Baada ya kuuza ndizi siku za mwanzo alinunua nguo nzuri ambazo alizivaa kila alipozunguka mkaani kuuza ndizi zake.

 Kitu kilichopelekea apendwe na  wateja wengi kutokana na umaridadi wake na heshima kwa wote akiwemo mama Colin ambaye alikuwa mnunuzi wake mkubwa.

Nyumba ya mama Colin ilikuwa ndiyo iliyokuwa ikinunua ndizi nyingi kitu kilichomfanya Cecy aongeze mtaji. Mama Colin alitokea kumpenda sana na kumwita mkwe.

Siku moja alipitisha ndizi kama kawaida bila kujua kama nyumba ile ina kijana mzuri aliyekuwa nje amerudi baada ya kumaliza masomo yake. Baada ya kufika nje ya geti alibonyeza kengele na mlinzi  alimfungulia mlango na kuingia ndani. 

“Mwambie mama mkwe leo nimeleta ndizi za ukweli,” alimwambia mlinzi aliyekuwa amemzoea sana.

“Mamkweee,” Cecy alipaza sauti kama kawaida yake kila alipofika.

Mara alitoka mama Colin akiwa katika muonekano wa mtoko.

“Ha! Ma mkwe safari ya wapi tena?”

“Nampeleka mchumba wako mjini.”

“Muongo, yupo wapi?”

“Yupo ndani anakuja.”

“Amekuja lini?”

Siku zote Cecy alipokuwa akipeleka ndizi alitaniwa na mama Colin kwa kuitwa mkwe japokuwa hakuwahi kumuona huyo mwanaume. Kila siku alikuwa na hamu ya kumuona japokuwa alikuwa akitaniwa.

“Jana usiku na ndege.”

“Waawooo,” Cecy aliruka juu kama anamfahamu.

Ghafla alinyamaza baada ya kumuona mvulana mzuri tena mtanashati akitoka ndani. Alibakia kama kapigwa shoti ya umeme kwa jinsi alivyosimama kwa mshangao kidole mdomoni.

“Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?” mama Colin alitania.

“Nimemuona mzuri tena mrembo,” Colin alisema huku akimtazama Cecy aliyekuwa bado amesimama.

“Cecy umemuona Colin?”

“Ndi..ndi..yo,” Cecy alipatwa na aibu na kushindwa kuzungumza.

“Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini.”

“Sawa mkwe.”

Mama Colin alifungua pochi na kutoa noti ya elfu tano na kumpatia Cecy, wakati huo Colin alikuwa akilisimamisha gari pembeni ya mama yake. Mama Colin alifungua mlango wa gari wa nyuma na kuingia. 

“Bai  mchumba,” Colin alimuaga Cecy aliyekuwa ameingiwa aibu.

“Bai,” Cecy alisema huku akiangalia pembeni kwa aibu.

Geti lilifunguliwa na gari lilitoka nje kuelekea mjini na kumuacha Cecy akitoa ndizi kwa msichana wa kazi kisha alitoka na kuendelea kufanya biashara kama kawaida.

                                                 ****

Safari ya mama Colin na mwanaye ilikuwa kwenda nyumbani  kwao Mage msichana aliyemchagua kuwa mke wa mwanaye.  Alimuona siku moja alipokuwa na mama yake walipokutana na shoga yake Super Market, wakati akiwa katika manunuzi ya bidhaa muhimu.

“Ha! Shoga  za siku?” Mama Colin alimsemesha mama Mage.

“Nzuri shoga, za kupotezana?”

“Mmh! Nzuri, vipi Colin bado hajarudi?”

“Anarudi mwezi kesho mwishoni.”

“Shikamoo,” Mage alimwamkia mama Colin.

“Marahaba, hujambo mama?”

“Sijambo.”

“Monika, binti yako?” mama Colin alimuuliza shoga yake.

“Ndiyo amemaliza chuo kikuu Mlimani anasubiri ajira.”

“Nimempenda sana, unafaa kuwa mke wa Colin.”

“Tena wataendana wasomi kwa wasomi,” mama Mage aliunga mkono.

“Anaitwa nani?”

“Mage,” Mage alijibu mwenyewe.

Tokea siku ile wakawa wakiwasiliana hata kutembelea huku wakisubiri muda wa Colin kurudi toka masomoni ili wapange mipango ya ndoa. Mama Colin alimpenda sana Mage kwa umbile lake nzuri na heshima aliyoionesha siku zote kwake. Naye mama Mage alifurahi mwanaye kuolewa na Colin kutokana na kumfahamu vizuri.

Siku Colin aliyofika hakutaka kuwajulisha, kesho yake alimpeleka nyumbani kwao Mage bila taarifa ili wafanye surprise. Familia ya kina Mage ilikuwa ikikaa Kigamboni walikwenda hadi kwao na kupiga honi nje ya geti. Wakati wote huo Colin alikuwa  hajui anakwenda wapi.

Baada ya geti kufunguliwa Colin aliliingiza gari ndani na kwenda kulipaki kwenye maegesho. Mama Mage alitoka nje baada ya kusikia gari likingia ndani na kujiuliza nani amekwenda kwake bila taarifa. Alishtuka kumuona mama Colin akiteremka kwenye gari.

“Waawooo jamani, ha! Colin siamini jamani karibu mwanangu,” alikuwa akimfuata mama Colin kumkumbatia lakini aligeuza  baada  ya kumuona Colin na kwenda kumkumbatia.

Colin alijikuta akishangaa baada ya kuteremka kwenye gari na kujiuliza pale ni wapi na yule aliye mfurahia na kumkumatia ni nani.

“Asante, shikamoo.”

“ Marahaba karibu sana mwanangu,” mama Mage alisema kwa furaha huku amemshika mabegani Colin na kumtazama.

Aliwapokea wageni na kuingia nao ndani kwenye sebuleni, baada ya kukaa alimwita Mage kwa sauti kubwa.

“Mageee.”

“Abee mama,” sauti ya Mage ilitoka chumbani.

“ Njoo mara moja.”

“Nakuja.”

Mage alikuja mbio bila kujua anaitiwa nini, alipofika alishtuka kumuona mama Colin.

“Ha! Mama mkwe.”

“Nimejaa tele,” mama Colin alijibu kwa tabasamu pana.

“Shikamoo.”

“Marahaba.”

“Mambo?” Mage alimsabahi Colin bila kumjua.

“Poa za hapa?”

“Nzuri,” Mage alijibu huku akishtuka na kujiuliza yule kama ndiye Colin, ili kupata uhakika aliomba msamaha na kutoka mara moja.

“Jamani samahanini nakuja mara moja.”

“Bila samahani,” alijibu mama Colin.

Alichepua mwendo na kwenda upande wa vyumba huku akimwambia mama yake.

“Mama njoo mara moja.”

“Jamani samahanini nakuja mara moja.”

“Hakuna tatizo,” mama Colin alijibu.

Baada ya mama Mage  kuondoka kumufuata mwanaye, mama Colin alimsemesha mwanaye kwa sauti ya chini.

 “Mchumba unamuonaje?”

“Yupo vizuri.”

“Umempenda?”

“Sana.”

“Nimefurahi kuona chaguo langu amelikubali.”

“Mama wee kiboko unajua kuchagua.”

Mama Mage baada ya kufika kwa mwanaye aliyekuwa amesimama upande wa vyumba.

“Vipi?” alimuuliza mwanaye.

“Safi, eti mama yule si Colin?”

“Ndiyo.”

“Mamaaa! Kwa nini hukuniambia mapema nijiandae anaweza kuniona sijipendi.”

“Walaa mbona umependeza, vipi umempenda?”

“Ndiyo,” Mage alikubali huku akinyanyua kichwa.

“Basi turudi.”

“Naona aibu ngoja nikaoge na kubadili nguo.”

Mama Mage aliwarudia wageni wake ili kuwapatia kinywaji kabla ya kuanza mazungumzo.



Mage msichana mwenye elimu ya chuo aliyekuwa na shahada ya Uhusiano, baada ya kuachana na mama yake alikwenda chumbani kwake ili kujiandaa kuonana na wageni. Kwanza alikwenda kuoga kisha alibadili nguo ambayo aliamini ni sahihi kwa ajili ya kumpokea mgeni wake.

Alijipulizia manukato ya bei mbaya aliyonunuliwa na baba yake alipokwenda Ufaransa kikazi. Alisimama mbele ya kioo kikubwa cha ndani  na kujitazama kisha kujigeuza kila pembe. Baada ya kuridhika na gauni alilovaa alikisogelea kioo na kujitazama jinsi Mungu alivyomuumba kwa uzani unaolingana, alijikuta akitokwa machozi ( siri ya machozi yake soma katika muendelezo wa hadithi hii.)

Aligundua kuna mapungufu kichwani mwake,  alikwenda mpaka kwenye dresing table na kukaa kwenye kiti kidogo kisha alivuta droo na kutoa wanja.  Alipaka wanja mwembamba ulioongeza uzuri wa sura yake.

Alichukua heleni ndogo na kuvaa kisha alichukua cheni yake ndogo ya dhahabu na kuivaa, kidani chenye jila lake kilikaa kwenye mfereji ya matiti yaliyojaa na kumfanya apendeze zaidi. 

Mage aliamini mpaka pale alikuwa amekamilika  kwenda mbele ya wageni wake ambao walikuja mahususi kwa ajili yake. Alikwenda kwenye kabati na kutoa kiatu cha kisigino kifupi cha rangi ya machungwa kilichoendana na linda la chini la gauni lake alilovaa lenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na weupe kwa mbali.

Hakika Mage  alikuwa amependeza kama malkia aliyekuwa tayari kuonana na mfalme. Alitembea kwa madaha toka chumbani kwake kuelekea sebuleni palipokuwa na wageni.

 Harufu ya manukato yake yalitangulia kabla yake. Colin na mama yake waligeuza macho kuangalia upande wa chumba na kukutana na Mage aliyetokeza akiwa amependeza mara dufu na awali alivyokuwa.

Moyo wa Colin alipasuka vipande na kuwa hoi taabani kwa uzuri wa Mage msichana chaguo la mama yake. Alijikuta akijiuliza hali ile mama yake ni mwanamke amejua kuchagua binti mrembo kama yule, je, angekuwa mwanaume angekuwa na uwezo gani wa kuchangua wanawake warembo.

Mama Colin alitulia kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme hata kukapua macho alishindwa kutokana na uzuri wa Mage mkwewe mtalajiwa.

“Wageni karibu  sana huyu mnayemuona ndiye Magreth halisi.”

“Asante, tunashukuru kukutambua,” Colin alijitahidi kuitikia japo mwili ulipoteza ujasiri wa kiume baada ya kuingiwa baridi la mshtuko.

“Mama zangu samahanini  namuomba mgeni wangu,” Mage alisema huku akisogea kwa Colin na kumshika mkono.

Colin alinyanyuka na kukiacha kinywaji chake juu ya meza ndogo, lakini Mage alikichukua na kukishika mkono wa kushoto huku wa kulia akimshika mkono Colin na kuondoka naye kuelekea nyuma ya nyumba kwenye bustani.

Walivyokuwa wakitembea wazazi wao waliwasindikiza kwa macho mpaka walivyopotea kwenye macho yao. Waligeuka na kutazamana kisha walitabasamu.

“Yaani walivyopendeza nilitamani leo ndiyo iwe siku ya sendoff ya mwanangu,” mama Mage alisema kwa hisia kali.

“Kila kitu kina wakati wake, kilichonifurahisha mimi jinsi walivyoonekana kupenda. Wasiwasi wangu huenda Mage asingempenda Colin.”

“Isingekuwa rahisi, Colin ni mmoja wa vijana wazuri ambao Mungu kawajalia. Nitajivunia kuwa na mkwe kama yeye, nitatembea kifua mbele.”

Upande wa pili Mage alimpeleka Colin mpaka kwenye bustani.

“Karibu kwenye kiti mgeni wangu,” Mage alimkaribisha kwenye kiti cha uvivu na meza ndogo katikati ya kuwekea vinywaji. Mage kabla ya kukaa alikumbuka amesahau kinywaji chake.

“Sorry Colin nakuja nimesahau kinywaji changu,”  Mage alisema  huku akigeuka ili arudi ndani.

“Mage,” Colin alimwita Mage aliyeanza kwenda ndani.

“Abee,” Mage alitikia huku akigeuka kumsikiliza Colin.

“Kinywaji hiki kinatutosha.”

“Mbona kidogo hakitutoshi.”

“Kinatutosha, kwangu wewe ni zaidi ya kinywaji.”

“Colin nimefurahi kufahamu hilo.”

Mage alirudi na kukaa pembeni ya Colin, baada ya kukaa Colin alibeba glasi iliyokuwa na kinywaji na kumnywesha Mage ambaye alisogeza mdomo kuipokea.

Baada ya kumeza funda ya juisi alimumunya midomo yake mipana na kusema:

“Colin, leo ni siku yetu ya kwanza kuonana lakini umenifanya nikuone mwenyeji katika moyo wangu. Nasikia fahari kuwa mkeo,” Mage huku akimtazama kwa macho yake makubwa kidogo yaliongezwa uzuri na wanja aliojipaka.

“Nashukuru kwa hilo,” Colin alijibu huku akiachia tabasamu pana.

“Lakini nina wasiwasi mmoja ambao umekuwa ikisumbua mawazo yangu na kuukosesha amani moyo wangu,” Mage alisema huku uso wake ukionesha uzuni.

“Wasiwasi wa nini Mage?” 

Colin aliuliza huku akijiweka vizuri kitini na kuiweka glasi ya juisi juu meza kisha alipeleka mkono kwenye nywele fupi za kipilipili na kuzichezea kitu kilichofanya Mage mwili umsisimke.

“Najua ndiyo siku yako ya kwanza kuniona, siamini kama Colin unanipenda kama ninavyokupenda?”

“Mage toka nilipoelezwa nimepatiwa mchumba moyo wangu ulikuwa taabuni kutaka kukuona. Nilikuumba akilini kwa kila umbile na kukupamba kwa rangi nyingi.

“Amini Mage kila nilichokiwaza moyoni mwangu kilikuwa uongo. Nilichokiona ni zaidi ya vyote nilivyoviwaza,” Colin alisema huku amemshika mabegani Mage na kumtazama usoni kwa jicho la huruma. 

“Vitu gani hivyo Colin?” Mage aliuliza huku akijitahidi kuyatoa macho nje kama anaweza kuyaona maneno kwa macho.

“Kila umbile  na sura niliyoiwaza ambayo niliamini huenda moja wapo litakuwa yako  imekuwa kinyume kabisa.”

“Mmh! Colin, kwa nini?”

“ Mage we ni mzuri wa wazuri mrembo wa warembo. Najiona kiumbe mwenye bahati kama nitakuwa mume wako,” Colin alisema akiwa ameyakaza macho kuonesha anachokizungumza hatanii. 

“Siamini, Colin siamini,” Mage alisema mikono ameshika kifuani huku machozi yalinitoka.

“Mage huamini nini?”

“Inawezekana Colin unalitamani umbile langu lakini si mapenzi ya dhati toka moyoni mwako,” Mage alisema huku machozi yakimtoka na kuweka michirizi kwenye mashavu.

“Mage amini nakupenda kama ugonjwa wa shinikizo la damu linavyochukuwa uhai wa mtu ghafla.”

“Colin sijui wewe ni mwanaume wa aina gani,” Mage alijisema huku akijitahidi kutengeneza tabasamu ndani ya machozi.

“Kwa nini mpenzi?”

“Maneno yako yamekuwa na sumaku yenye nguvu ya ajabu kuweza kunasa chuma kilichomo moyoni mwangu.”

“Sijakuelewa mpenzi.”

“Ameweza kuuteka moyo wangu na kukubali kuwa mateka wako. Colin nakuamini, usiniache katikati ya bahari nitakufa maji boya langu ni wewe. Maumivu ya mapenzi ni zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi.”

“Amini Mage nakuahidi kuwa mume mwema.”

“Nami nakuahidi kuwa mke mwema.”

Baada ya hapo mazungumzo yaliendelea kila mmoja kuitaka kumjua mwenzake kiundani mpaka muda ulipofika wa kuondoka.

 Colin akiwa mtu mwenye furaha na mama yake waliondoka na kuwaacha Mage na mama yake nje baada ya kuwasindikiza wageni. Walirudi ndani mtu na mama yake wakishikana mikono.

  Walipoingia ndani Mage  alimuuza swali mama yake.

“Mama, kweli Colin atanioa?” alimuuliza huku akimkazia macho.

“Mbona umeniuliza hivyo, kwani mmezungumza nini?”

“Amenihakikishia atanioa.”

“Sasa wasiwasi wako nini?”

“Mama anaweza kuwa na mwanamke mwingine na kuniacha njia panda kama alivyofanya Hans. Najiona nimefanya haraka sana kumkubali Colin bila kujua historia yake. Safari hii sitakubali kuumizwa mara mbili lazima nitanyongwa tu,” Mage alisema kwa hisia kali.

“Kwa hiyo ukigundua Colin ana mwanamke mwingine utamuua?”

“Siwezi kumuua Colin bali mwanamke wake.”

“Lakini Hans alikuwa akikupenda tatizo wazazi wake ndiyo waliomchagulia mwanamke mwingine.”

“Mama, Hans hakuwa ananipenda ni muongo mkubwa.”

“Kwa nini?”

“Alisema anamuoa yule mwanamke hatakaanaye atamuacha, mwezi jana nilimekutana na yule mwanamke akiwa mjamzito.”

“Ndiyo basi tena, nawe umepata wako tena kijana mzuri msomi mwenzako.”

“Mama bado inaniuma sana, niliutoa mwili wangu kwa Hans kwa kujua ndiye atakaye kuwa mume wangu. Mama sijui mwanaume yeyote zaidi ya Hans, nilijitunza kwa ajili yake matokeo yake alinidanganya ataachana na yule mwanamke aliyelazimishwa kuoa.

“Nilimuamini lakini mwezi ulioisha nilijikuta nikimchukia Hans baada ya kumuona yule mwanamke mjamzito. Imeniuma sana mama nakuahidi sitamsamehe Hans na sitakubali kuchezewa tena na Colin nitakufa mimi au yeye,” Mage alibadili uzuri wake wote ulipotea alikuwa kama akipigana na mtu.

“Mage mwanangu, ya Hans tuliyazungumza tukayamaliza.”

“Mama hujui kiasi gani nilivyoumizwa na Hans kuoa, lakini alinituliza na kusema kuwa ataachana na mpenzi wake ili anioe. Lakini nilichokiona  niliwaza mbali sana mama.

“Leo nakupa siri niliyoificha moyoni, siku niliyokutana na mke wa Hans mjamzito, nilinunua vidonge na pombe kali ambavyo nilipanga kunywa usiku ili asubuhi ukiamka ukute mzoga.

“Usiku ulipoingia niliandaa vitu vyote kwa ajili ya kuutoa uhai wangu, kabla ya kufanya tendo lile nilikumbuka kauli ya profesa mmoja wakati tupo chuoni, kuwa thamani yangu haipo kwa mtu mmoja bali ya ulimwengu mzima kwa hiyo nisipoteze uhai wangu kwa kosa la makusudi bali niitazame thamani yangu mbele ya jamii.

“Mama nililia sana na kuchukua vitu vyote na kwenda kuvitupa. Huwezi kuamini nimchukia Hans kama kifo. Ujio wa Colin umenishtua na kuona kama maumivu mengine yanakuja.”

“Mage mwanangu naiamini familia ya kina Colin, uzuri mama yake kakuchagua.”

“Mamaa! Ngoja tuone.”

Mage alisema huku akielekea chumbani kwake. 

                                    ***

Cecy baada ya kufanya biashara yake ambayo iliisha mapema na kurudi nyumbani akiwa mwenye furaha. Mama yake alijua furaha ile ni kwa ajili kumaliza bishara mapema kumbe sivyo. Usiku ulipoingia  aliwahi kula, baada ya kuoga alipanda kitandani mapema. 

Kitendo kile kilimshtua mama yake na kuamini mwanaye  labda anaumwa. Mama Cecy baada ya kumaliza kazi zake alimfuata mwanaye chumbani aliyekuwa amejilaza chali mikono ameilalia kwa nyuma.

 Mpaka anaingia chumbani Cecy alikuwa ametulia macho kayaelekeza juu. Mama yake alitulia akimuangalia na kumuona mwanaye yupo katika lindi la mawazo jambo ambalo halikuwa kawaida kuliona kwa mwanaye. 

Baada ya muda alimuona akitabasamu na kujikuta akitazama juu labda kuna kitu mwanaye anakitazama na kumfurahisha, lakini hakuona kitu. Alijiuliza kipi kilichomfanya mwanaye awahi kitandani kisha kutulia akitazama juu na kutabasamu.

Baada ya kutabasamu alimuona alishika mikono kifuani na kusema kwa sauti ya chini ambayo mama yake aliisikia.

“Cecy mimi,mmh! Sijui?”

Baada ya kusema vile aligeukia ukutani na kumpa mgongo mama yake aliyekuwa amesimama mlangoni bila kumuona. 

“Cecy..Cecy,” mama yake alimwita.

“A..a..bee,” Cecy  aliitikia huku akigeuka kumtazama mama yake na kumshangaa kumuona amesimama mlangoni.

“Vipi mama?” alimuuliza bila kunyanyuka zaidi ya kujigeuza.

“Unajua leo sikuelewi kabisa.”

“Kivipi?” Cecy alijibu huku akikaa kitako.

“Umewahi kupanda kitandani si kawaida yako, nimefika muda nimekuona akitazama juu na kutabasamu peke yako. Kisha unazungumza peke yako una nini leo mwanangu?”

“Mama nipo kawaida, siku azilingani.”

“Kipi kilichokupa furaha leo.”

“Mama nawaza  kama siku moja nitaolewa na mwanaume mzuuuri mwenye uwezo tena mwenye mapenzi ya dhati nitafurahi sana.”

“Utapata tu mwanangu, Mungu nawezi kutunyima vyote.” 

“Asante mama yangu kunipa moyo.”

“Lakini huna tatizo lolote?”

“Sina mama yangu.”

“Haya mwanangu usiku mwema.”

“Na wewe pia mama yangu.”

Mama Cecy aliondoka na kurudi chumbani kwake kulala na kumuacha mwanaye akirudi kujilaza kama mwanzo macho yake yakiangalia juu.

Alijikuta akikumbuka kauli ya mama Colin baada ya kutoka ndani, mwanaume mzuri ambaye alikuwa na kila sababu ya kujivunia kama akiwa mumewe au mpenzi wake.

Alikumbuka jinsi alivyoshtuka baada ya kumuona Colin. Kauli ya mama Colin ilijirudia kichwani mwake. 

“Colin umemuona mchumba wako niliyekuandalia?” 

“Nimemuona mzuri.”

“Cecy umemuona Colin?”

“Ndi..ndi..yo,” Cecy alikumbuka alipipata kigugumizi na kuugua ugonjwa wa mapenzi ghafla.

“Sasa mkwe, msichana wa kazi atachukua ndizi sisi tuna safari ya mjini.”

“Sawa mkwe.”

Cecy alijiuliza kauli ile ya mama Colin ilikuwa na ukweli gani kutokana na kuona  kuolewa na Colin sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano.

“Mbona sielewi, kweli Colin atanioa au ananitania, mbona hakukataa mbele ya mama yake, na kwa nini mama yake aendelee kuniita mkwe?”

Cecy alijiuliza bila kupata jibu la moja kwa  moja. Lakini wasiwasi wake ikawa kwenye hali zao yeye muuza ndizi anazurura mitaani na mwenzake mtoto wa kitajiri.

“Watakuwa wananitania,” alisema kwa sauti ya kakata tamaa na kugeukia ukutani kuutafuta usingizi.


ITAENDELEA...

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.