WAKILI WA MOYO O2

WAKILI WA MOYO 02


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

SIMU: +255713 646500


ILIPOISHIA 01


“Mmh! Sikumualika si unajua watu waliokuja hapa mwenye hadhi zao, hivyo angekuwa tofauti na wengine.”

“Mimi nilimualika.”

“Sasa Colin... yule msichana atavaa nini ili alingane na hadhi ya sherehe hii. Inawezekana kabisa John kamzuia getini kutokana na hadhi ya sherehe yako.”

“Kama atakuwa amefanya hivyo atakuwa hakutenda haki kwa vile mimi ndiye niliyemualika.”

SASA ENDELEA...


“Achana naye, si muhimu kama sherehe yako,” mama Colin alijibu kwa mkato huku akichukua glasi ya kinywaji na kupeleka mdomoni.

“Hapana,” Colin alisema huku akielekea getini.

Mama yake hakushughulika naye alimuacha aende, alipofika getini alimuuliza John kama amemuona Cecy.

“Sijamuona, sizani kama anaweza kuja kwenye sherehe ya watu wazito kama hii. Kila mmoja kaja na gari la kifahari,  msichana mmoja ndiyo kaja na gari la kukodi, muuza ndizi kama Cecy atakaa wapi?” John alisema kwa dharau.

“John au umemkatalia?” Colin alimuuliza huku akimkazia sauti na macho.

“Hapana bosi,”John aliingiwa hofu.

“Sasa kesho aje aseme umemzuia jihesabu huna kazi.”

“Sijamuona kwa kweli, kama akifika nitamruhusu aingie.”

Wakati Colin akirudi ndani, Cecy alikuwa akitoka msalani na kukutana uso kwa uso. Kwa vile Colin alikuwa na hasira alimuona msichana mrembo lakini akili yake haikumtambua. 

Baada ya kusalimiana alimchangamkia kama wageni wengine na kutaka kuelekea ukumbini.

“Colin jamani ndiyo nini?” Cecy alimsemesha. 

Sauti ya Cecy ilimshtua Colin na kugeuka na kujikuta akitazamana na msichana mrembo.

“Mungu wangu, nini wewe Cecy?” Colin alishtuka.

“Naam, ni mimi,” Cecy alisema kwa sauti ya kike huku akishika mkono mmoja kiunoni na kunesa kwa madaha na macho kuyarembua.

“Yaani huwezi kuamini, natoka nje kukuuliza.”

“John kasemaje?”

“Cecy ulivyopendeza umetuchanganya wengi, kuanzia mama mpaka John getini amekusahau, anasema hajakuona.”

“Jamani! Ndizi ni kazi lakini umbile kazi ya Muumba, ninyimwe kila kitu? Nimemkosea nini Mungu?” Cecy alisema kwa sauti ya kinanda na kumfanya Colin aamini kama si kutangaza uchumba basi yeye angekuwa chaguo lake.

“Basi nimefurahi kukuona pia hongera umependeza sana na karibu sana.”

“Asante.”

“Wacha niwahi sherehe inanisubiri mimi.”

“Hakuna tatizo tupo pamoja.”

“Nilisahau kamsalimie mama ajue upo.”

“Sawa.”

Cecy baada ya kuagana na Colin alikwenda mpaka alipokuwa amekaa mama Colin na kumsemesha.

“Shikamoo ma’ mkwe,” alimsalimia huku akipiga magoti kwa heshima.

“Ha! Cecy mkwe wangu jamani, nisamehe sana nilikusahau nawe umependeza sana.”

“Ni kawaida yangu.”

“Karibu mkwe.”

“Asante, nipo mbele.”

“Hakuna tatizo.” 

Mama Colin alimsindikiza mpaka anakaa na kutikisa kichwa na kujisemea moyoni: “Cecy msichana mzuri sana.”

Sherehe iliendelea kila mmoja akiifurahia huku Mc akieleza kila hatua iliyokuwa ikiendelea. Ilifika wakati wa kukata keti, kama kawaida Mage ndiye aliyekata keki na kumlisha kisha Colin kumlisha Mage. 

Kisha keki ilikatwa vipande kisha Colin alipita kila meza ya wageni na kumlisha mojamoja huku akipiga naye picha. Baada ya zioezi lile alimwambia mpigapicha ahakikishe anampiga Cecy picha zaidi ya ishirini za mikao tofauti na kumpelekea.

 Mpiga picha alifanya kama alivyoelekezwa kwa kumfuata Cecy na kwenda naye kumpiga picha tofauti.

Baada ya zoezi la kulishana keki kumalizika, Colin aliomba kipaza sauti na kuzungumza machache kuhusiana na sherehe yake kwa kuwashukuru wageni waalikwa.

“Kwanza namshukuru wazazi wangu kunizaa kwa mama yangu mzazi kunilea na baba yangu aliyetangulia mbele ya haki. Pia nawashukuru wageni waalikwa kwa kufika katika sherehe ya kuzaliwa kwangu.

“Leo ni siku muhimu na maalumu katika historia ya maisha yangu, kitakacho kifanya ni hatua moja kuelekea katika maisha yangu ya kujitegemea. Wazazi wangu na wageni waalikwa natumia siku ya yangu ya kuzaliwa ili kumtambulisha mchumba wangu kwa kumvisha pete.”

Kauli ile ilifanya moyo wa Cecy ilipuke pa! Na kufanya mapigo ya moyo kwenda kwa kasi. Alijiuliza kauli ile anayoisikia ni ya kweli au anaota ndotoni. Akili yake ilipata jibu la kupewa nguo nzuri na kualikwa kwenye sherehe ile. Aliiona ndoto yake ya mchana kuwa mke wa Colin ilikuwa ikitimia muda si mrefu. 

Alitulia akijipa ujasiri ili kunyanyuka kwenda kuvishwa pete mbele ya umati ule akiitwa. Colin aliendelea kuzungumza huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa mkebe wenye pete ya uchumba. 

“Jamani naomba mpenzi wangu wa moyo ambaye anatarajiwa kuwa mama wa watoto wangu asogee mbele.”

Kauli ilimfanya Cecy atake kunyanyuka akiamini kabisa yeye ndiye mchumba wa Colin. Kabla hajanyanyuka kwenda mbele alishangaa kumuona Mage msichana aliyetoka naye ndani akisogea mbele akiwa ameshika kifuani asiamini kilichosemwa.

Baada ya kufika hapo Mc alichukua kipaza sauti na kuongoza zoezi lile. 

Wakati huo Cecy alikuwa ameingiwa ganzi mwilini na kuona kama Colin kumuita kwenye sherehe ile ilikuwa amemtendea unyama. Alijiuliza kitu gani alichomtendea Colin mpaka kumfanyia ukatiri kama ule. Alijitahidi kuzuia hali ile kwa kushika mkono kifuani kuzuia mapigo yaliyokuwa yakienda kasi huku kijasho chembamba kikimtoka.

Wakati wa kuvishwa Mage pete kilikuwa kipindi kigumu kwa Cecy, ilikuwa sawa na kupasuliwa moyo wake kwa kisu butu bila ganzi. Bila kujielewa presha ilimpanda alishindwa kuizuia na kujikuta akiona kiza kizito mbele yake , alipiga kelele. “Mungu wangu.”  alijikuta akinguka chini kama mzigo na kuwashtua waliokuwa wamekaa naye karibu.       

Tukio lile lilizua taharuki na kusababisha sherehe kusimama, wakati huo zoezi la pete lilikuwa limeisha. Colin na mama yake walishtuka kusikia aliyeanguka ni Cecy.

Walikimbia eneo la tukio na kumkuta amezungukwa na watu.

“Vipi?” waliuliza kwa sauti ya mshtuko.

“Hata sijui, nilimuona akishika kifuani na kuhema kwa kasi kisha kufumba macho. Nilipotaka kumuuliza  nilimsikia akisema Mungu wangu na kushangaa kumuona akianguka chini. Nilijitahidi kumuwahi nilichelewa tayari alikuwa ameanguka chini,” alisema dada mmoja aliyekuwa amekaa meza moja na Cecy.

“Labda ana kifafa?” mmoja alichangia.

“Hapana kile si kifafa, kwa jinsi nilivyomuona si kifafa,” alijibu aliyekaa naye meza moja.

“Kifafa gani kisicho na povu,” mwingine aliongezea.

“Jamani tumuwahishe hospitali,” mama Colin alisema.

“Mama we’ baki na wageni acha mimi nimpeleke,” Colin alisema huku akipiga magoti na kushika kichwa cha Cecy aliyekuwa ametulia kama amelala.

“Hapana Colin wewe baki na wageni kumbuka sherehe ni ya kwako pia umemaliza kumvisha mchumba wako pete muda mfupi, hivyo unatakiwa kuwa naye karibu. Endeleeni na sherehe mimi ninatosha.”

Colin alikubaliana na mama yake, yeye alibaki na kuendelea na sherehe na mama aliyemchukua  Cecy na kumuwahisha hospitali.

                                     ***

Cecy baada ya kufikishwaa hospitali alichukuliwa vipimo na kuoneka hana tatizo kubwa ila presha ilikuwa juu. Lilifanyika zoezi kuishusha mara moja na kurudi katika hali ya kawaida.

“Nafikiri tatizo siyo kubwa sana, baada ya kumaliza drip nitamruhusu,” daktari alisema.

“Itachukua muda gani?”

“Si muda mrefu mtaondoka naye.”

Mama Colin alitoka na kukaa kwenye makochi huku amekasirika na kulaumu kitendo cha mwanaye kumualika msichana yule ambaye hakuwa na hadhi ya sherehe ile na kufikia kuharibu starehe yake kwa kuacha shughuli ya mwanaye kwa ajili ya msichana dhalili kama yule.

Alipanga kupiga marufuku ukaribu wa Cecy na Colin kwa vile aliuona unataka kwenda ndivyo sivyo. Yeye alitengeneza utani ambao ulimtia wasiwasi kwa mwanaye kuamini ni kweli, akiwa katikati ya mawazo daktari alimshtua:

“Mama mgonjwa wapo yupo tayari unaweza kumchukua.”

Alinyanyuka na kwenda wadini alipomkuta Cecy amekaa kitandani.

“Vipi mkwe?”

“Nashukuru sijambo.”

“Tatizo nini?”

“Hata najua! Nimejikuta nikiona kiza ghafla,” Cecy alipindisha ukweli.

“Imeisha wahi kukutokea?”

“Hata siku moja, hata mimi najishangaa, ila samahani mkwe kwa kuharibu sherehe ya mwanao.”

“Ujaharibu kitu sherehe inaendelea kama kawaida.”

“Naomba uniende nyumbani.”

“Hapana nitakupeleka.”

Alimchukua na kumuwahisha kwao ili yeye ageuke awahi sherehe. Alipomfikisha alimpa elfu hamsini kwa ajili ya kujiangalizia hali yake.

“Mkwe ugua pole.”

“Asante ma’ mkwe.”

Cecy aliagana na mama Colin na kwenda kugonga mlango, mama yake aliyekuwa hana amani na moyo wake toka aondoke mwanaye kwenda kwenye sherehe za usiku. 

Muda wote alikuwa macho, mwanaye alipogonga aliwahi kufungua.

“Umerudi mwanangu?” 

“Ndi..ndi..ndiyo mama.” 

Kauli ya Cecy iliyochanganyikana kigugumizi na kilio ilimshtua.

“Cecy nini mama?”

“Ningejua  nisingeenda,” alisema sauti ya kilio. 

“Kwa nini?”

“Yaani wameniita kuniumiza! Nimewakosea nini?”

“Kukuumiza! Kivipi?”

“Mama yaani sijawahi kuumizwa moyo wangu kama leo, najua unaniona mtoto mdogo lakini nina hisia kama mtu mwingine, mama inaumaa,” Cecy alisema kwa uchungu huku akishika mkono kifuani.

“Kuna nini mbona uniweki wazi?” mama yake alishtuka.

“Mama Colin wa kuniita kunionesha mchumba wake?”

“Kukuonesha kivipi?”

Cecy alimweleza kila kitu kilivyokuwa katika sherehe, mama yake alishtuka na kusema:

“Mwanangu unataka kujiua bure, nilikueleza na mapema tajiri na sisi kina pangu pakavu wapi na wapi?”

“Kwa nini mama yake ananiita mkwe wakati mwanaye ana mwanamke mwingine?” Cecy aliuliza macho yakijaa machozi.

“Kuna siku alikutamkia suala la uhusiano kati yake na wewe?”

“Hapana.”

“Sasa kuumia huko kumetoka wapi?”

“Mama! Nampenda sana Colin.”

“Ulimwambia unampenda?”

“Nilikuwa naona aibu.”

“Siku zote moyo ni mfungwa wa mapenzi hasa kumpenda asiyejua anapendwa mdomo wako ndiyo wakili wa kuutetea moyo wako. Bila hivyo upendo wako utateketea kama mwanga wa mshumaa mchana wa jua kali, hakuna atakayeuona mwanga wake.” 

“Mama, Colin alionesha ananipenda.”

“Nilikueleza toka zamani ule  ni utani tu wala hakuna ukweli wowote.”

“Kwa kitendo walichonifanyia siendi tena kwao kuuza ndizi.”

“Mwanangu nikueleze mara ngapi kila kitu kinatokana na baraka za Mungu. Muombe yeye ndiye atakayekuchagulia mwanaume  wa maisha yako.”

“Asante mama kwa kunitia moyo.”

“Basi badili nguo kisha uoge ule ulale.”

“Mama hata hamu ya kula ninayo, wacha tu nikalale.”

Cecy aliingia chumbani kwake kulala na kumwacha mama yake akiwa amesimama na kuyafikiria yote aliyoelezwa  na mwanaye. Alimuonea huruma kwa kujiingiza kwenye mapenzi ya kumpenda mtu mwenye mpenzi mwingine anayempenda.

Kingine kibaya ilikuwa hali yao duni ambayo ilikuwa tofauti na matazamo ya familia yenye fedha kuwaangalia matajiri na wasomi wenzao. Alijiuliza kwa hali iliyomtokea mwanaye iliyopelekea kupatwa na presha kupelekea kukimbizwa hospitali itachukua muda gani kumtoa.

Aliamini ingemtesa mwanaye kwa kipindi kirefu na kumfanya akose amani ya moyo wake. Lakini aliamini atampatia ushauri nasaha utakaomrudisha katika hali ya kawaida. Aliachana na mawazo yale na kwenda chumbani kwake kulala.



Cecy siku ile ilikuwa mbaya katika siku alizowahi kuishi, aliyakumbuka maneno ya mama yake kuhusu Colin kumtamkia mpenzi wake zaidi ya utani wa uchumba.

 Kwa vile kichwa kilikuwa kikimuuma, alimeza dawa za usingizi na kupanda kitandani kuitafuta siku ya pili.

                                         ***

Wakati hayo yakiendelea, Colin na Mage walikuwa kwenye furaha ya ajabu. Mage hakuamini tukio lililotokea usiku ule la kuvalishwa pete ya uchumba mbele ya watu.

Kilikuwa kitu kikubwa sana katika maisha yake, pamoja na kupendana sana na Hans kwa muda mrefu lakini hakikufanyika kitu kama kile. 

Aliamini Colin alikuwa mwamaume aliyeletwa kwake na Mungu kwa kuonesha ana mapenzi ya dhati na yeye.

“Colin asante sana mpenzi wangu,” Mage alisema huku akiitazama pete yake ya kito cha Tanzanite kidoleni kwake.

“Kawaida tu, nina vitu vingi vya kukufanyia mpenzi wangu,” Colin alijibu huku akichezea vidole vya mikono ya Mage.

“Colin nakuahidi kuwa mke mwema.”

“Nashukuru, nataka harusi yetu isichukue muda mrefu.”

“Hujui tu, ukitaka sasa hivi nipo tayari hata unioe bure kwa vile upendo wa kweli ni ghari kuliko kuitafuta fedha. Nakuhitaji kuliko kitu chochote chini ya jua.”

 Mage alisema huku machozi yakimtoka akikumbuka alichofanyiwa na mpenzi wake Hans, mwanaume aliyeamini ndiye wake wa kufa na kuzikana. 

 Lakini kilichotokea kilikuwa kinyume na matarajio yake, kiliufanya moyo wake kuingia wasiwasi wa kumkosa hata yule.

“Mage usilie nataka ulie kwa furaha ukiwa nami si kwa huzuni,” Colin alimwambia Mage huku akichezea vidole vyake na macho yake kutazama usoni kwake.

“Nina wasiwasi naweza kutendwa tena, Colin ukinitenda nitakufa mwenzio nakuona wewe ndiye uliyeshika uhai wangu,” Mage alisema kwa sauti iliyohitaji huruma.

“Nakuhakikishia furaha yako itapitia mikononi mwangu.”

“Kweli Colin?” Mage aliuliza huku ametoa macho.

“Amini nakupenda sana Mage, wewe ni ua la moyo wangu sitachoka kulitunza na kulimwagilizia ili liendelee kustawi na kuchanua.”

“Asante Colin, nami nitahakikisha chaguo la mama yako hutajutia maishani mwako. Hazina yote ya mapenzi nahamishia kwako.”

“Asante mpenzi wangu nami nitakuwa benki yenye usalama kwa ulichokiweka kila sekunde kinaongezeka faida ya upendo.”

“Nimefurahi kusikia hivyo, nina imani kovu la kutendwa litaondoka.”

“Niamini nikisemacho, kwa vile nami nahitaji furaha yangu itoke kwako.”

“Asante mume wangu mtarajiwa,” Mage alisema huku akimkumbatia Colin kwa mahaba mazito.

Baada ya sherehe, Mage alikataa kuondoka na mama yake na kulazimisha kubaki na Colin.

“Mage mwanangu muda wa kuwa karibu na Colin bado.”

“Hapana mama, alichokifanya leo ni zaidi ya ndoa. Naomba uniache nina mengi ya kuzungumza naye usiku wa leo.”

“Mama Mage mwache mtoto abakie na mwenziye, bado wana mengi ya kuongea wakiwa karibu,” mama Colin aliingilia kati na kufanya mama Mage kukubaliana na mzazi mwenzie kumuacha Mage alale na Colin siku ile.

                                                   ****       

 Cecy alishindwa kutoka kwao kwa siku mbili, muda mwingi aliitumia kuwaza na kujiona ni kiumbe kwenye mkosi ambaye hakufaa kuishi katika dunia ile. Alijiona hana thamani yoyote kutokana na kukosa kila kitu ambacho mwanadamu alitakiwa kuwa nacho.

Maisha yao yalitawaliwa na umaskini wa kutupa, elimu nayo ilikuwa duni ya shule za kata, kwake alichombulia ni kujua kusoma na kuhesabu zaidi ya hapo hakuna alichokijua.

 Kingine kibaya ambacho ndicho kilichomuuliza sana kukosa haki ya kupenda kwa vile tu hana elimu pia anatoka katika familia duni. Japokuwa hakuwa msomaji wa vitabu lakini alikuwa akipenda kusikiliza vipindi vya usiku hasa vinavyohusu mapenzi na uhusiano. 

Alikuwa muumini mzuri wa vipindi hivyo kwa kujifunza vitu vingi,  aliweza kujua thamani ya kuwa mwanamke pia mapenzi hayahitaji mtaji wa fedha wala elimu bali hisia za mtu ambazo hupokelewa na mtu mwingine na kuwa kama ncha mbili zinasababisha umeme zikiungana ndipo  umeme hupatikana.

Siku zote mada zile zilimfanya ajiamini na kuamini anaweza kuwa na mpenzi wa aina yoyote mwenye hadhi yoyote kwa hali yake duni na elimu yake ileile. Alichojifunza kingine msichana kuwa msafi wakati wote hata kama anauza karanga hakutakiwa kijifuja na kutembea na nguo chafu au kutojijali.

Cecy aliamini kupendwa na watu wengi huku biashara yake ukiuzika sana ilikuwa ni kutokana na kujipenda kwa kununua nguo nzuri na muda wote kuwa msafi. Lakini kitendo alichofanyiwa na Colin kilimvunja nguvu na kuona hakuwa na sababu ya kupoteza fedha zake kununua nguo na vipodozi, kwa vile hakuona umuhimu wake zaidi kurudia maisha ya zamani ya kuvaa nguo nzuri siku jumapili atakapokwenda kanisani tu lakini siku nyingine alivaa hovyo. 

Kitendo cha kutokwenda kwenye biashara kilimshtua sana mama yake na kutaka kujua kulikoni.

“Mwanangu kwa nini huendi kwenye biashara?”

“Mama yaani sijui nitatembeaje najisikia aibu  naona kama kila mtu anajua kilichonitokea siku ile.”

“Mwanangu, kilichotokea ni siri yako kwa vile hakuna aliyejua moyoni unawaza nini.”

“Ni kweli, lakini moyo unaniuma sana mama.”

“Kuumwa moyo ni kujitakia kwa vile Colin hakukutamkia wala wewe hukumtamkia kipi kikuumize.”

“Kwa nini aliniita kwenye sherehe yake?”

“Kama walivyoitwa wengine.”

“Mmh! Sawa, lakini nimeapa sitapeleka tena ndizi kwa mama Colin.”

“Hiyo ni juu yako, lakini kumbuka katika sehemu uliyokuwa na uhakika wa fedha ni katika nyumba ile. Siku zote usiingize mapenzi kwenye biashara.”

“Siwezi..siwezi mama watanionaje?”

“Wakuoneje, kwani wao wanajua nini juu ya kuanguka kwako?”

“Hata kama hawajui siendi,” Cecy alishikilia msimamo wake.

“Siwezi kukulazimisha kwa vile wateja wale sikukutafutia uliwatafuta mwenyewe.”

Cecy alipanga kuendelea na biashara yake mwisho wa wiki huku akisimamia msimamo wake wa kutopeleka ndizi kwa mama Colin.

                                                        ***

Upande wa Colin alishtushwa na ukimya wa Cecy  kutoonekana kwa siku tatu nyumbani kwao kupeleka ndizi. Akiwa chumbani kwake alichukua picha alizopigwa Cecy na kuzitazama.

 Aliusifia uwezo wa mpiga picha kwa kumpiga picha nzuri za tofauti, alituza macho na kuangalia uzuri wa asili wa Cecy.

“Hakika binti huyu ni mrembo,” alisema kwa sauti ya chini na kurudia tena picha moja baada ya nyingine.

Alitabasamu na kuamini wazo lake la kuanzisha kampuni ya mitindo litafanikiwa kwa kukusanya mabinti wenye uzuri wa asili wasiotumia madawa ya ngozi kama Cecy ambao angewatumia katika maonesho ya mitindo mbalimbali huku akiuza nguo.

Japokuwa elimu ya Cecy ilikuwa darasa la saba, kwa umri wake aliamini akisoma twisheni ya Kingereza kwa kipindi anajiandaa kufungua kampuni angekuwa amepiga hatua katika kuzungumza na kusoma Kingereza vizuri.

Alijikuta akitoka sebuleni na picha ya Cecy mkononi hadi alipokuwa amekaa mama yake.

“Mama mbona mchumba haonekani siku hizi?”

“Colin, wa nini kwani siku ambazo hakuja tumekosa ndizi?” mama yake alimuuliza huku akiondoa macho kwenye gazeti na kumtazama mwanaye.

“Hapana mama kumbuka alipata matatizo siku ya sherehe yangu huenda amezidiwa.”

“Daktari alisema hakuwa na ugonjwa wowote alichopata ni mshtuko tu.”

“Lakini kumbuka toka apate tatizo lile hatujamuona kuleta ndizi.”

“Hata tukimuona atatusaidia nini?”

“Mamaaa! Mbona majibu yako kama yanaonesha chuki.”

“Colin, mimi na wewe nani anamjua sana Cecy?”

“Wewe.”

“Sasa kipi kinakufanya kutaka kuyajua mambo yake?”

“Kwa kawaida mtu ambaye alikuwa akituletea biashara atoweke ghafla lazima nihoji.”

“Hiyo picha ya nani?”

“Ya Cecy.”

“Ya Cecy! Imefikaje kwako..hebu.” 

Mama Colin alisema huku akinyanyuka na kumfuata alipokuwa amesimama mwanaye na kuichukua picha ya Cecy aliyokuwa amekaa pozi tata. Aliitazama kwa muda kisha alimuangalia mwanaye na kumuuliza.

“Hii picha umeitoa wapi?”

“Kwa nini unaniuliza hivyo?”

“Colin mwanangu sasa nimejua sababu ya Cecy kuja kwenye sherehe yako, yaani unajifanya unampenda Mage kumbe  upo na Cecy.”

“Mamaa!” Colin alimshangaa mama yake kusema kauli ile.

“Nasema hivi sitaki kukuona na uchafu huu na tena nitakwenda kumkomesha.”

“Mama mbona unanihukumu bila kuniuliza?” Colin alizidi kumshangaa mama yake.

“Nikuulize nini, yaani uchafu huu sitaki kuuona,” alisema huku akiichana picha ya Cecy na kuvitupa vipande chini na kumwita msichana wa kazi kuja kuvizoa.

“Mama unafanya nini, nilikueleza nini kuhusu production yangu?”

“Production na mapenzi yako na msichana mchafu maskini tena mbumbumbu hainiingia akilini,” mama yake alisema huku akibinua midomo.

“Mama Cecy si mpenzi wangu bali niliamini kwa muonekano wake pamoja na wasichana wengine wa muonekano kama wake angenisaidia katika kampuni yangu kufanya vizuri.”

“Sitaki mazungumzo mengi nataka uvunje uhusiano wako na Cecy au nitamfanyia kitu kibaya ili nikanyogwe hawezi kuharibu mipango ya maisha yangu.”

“Mama sina mpango wowote na Cecy ulipoelekea sipo,” Colin alimshangaa mama yake.

“Naomba uondoke mbele yangu.”

Colin hakusema kitu aliondoka na kurudi chumbani kwake, alipofika alizichukua picha zote za Cecy na kuzificha kwa kuamini kwa jinsi alivyopendeza hata Mage angeziona angejua lazima ana uhusiano naye.

Kitendo cha Colin kuwa na picha ya Cecy pia kumkaribisha kwenye sherehe ya kuzaliwa kwake, kiliamsha hasira za mama yake na kujikuta akimchukia Cecy ambaye aliamini kabisa mwanaye anampenda kuliko Mage. 

Alinyanyuka na kutoka nje akiwa mwenye hasira hadi kwenye gari. Aliingia na kuondoka nalo kuelekea nyumbani kwao na Cecy ili kwenda kumkomesha aachane na mwanaye.

 Aliendesha gari kwa kasi mpaka nyumbani kwao na Cecy. Alipofika aliteremka bila kufunga mlango na kwenye anapoishi Cecy na mama yake. Alimkuta mama yake akitengeneza samaki wa biashara.

“Cecy yupo wapi?” aliuliza kwa hasira hata bila salamu.

“Dada yangu hata bila salamu?” mama Cecy alisema kwa sauti ya upole.

“Haikusaidii kitu, huyo kiinyago wako yupo wapi?” 

“Tatizo nini mzazi mwenzangu?”

“Sina shida ya maswali namtaka Cecy.”

“Amekwenda kwenye biashara zake.”

“Ooh! Kumbe ndiyo janja yake mwambie nimeisha mbaini. Akija mwambie sitaki kuvuruga maisha ya mwanangu nasema amkome.”

“Kwani kafanya ni...” alikatwa kauli.

“Ee..ee, nimesema amkome kama ana tabia ya kenge basi damu itamtoka maskioni.”

“Mbo..mbona ..si..si.”

“Nimesema nikisikia tena usije kunilaumu, mwambie mwanao amkome mwanangu kama alivyokoma kunyonya ziwa lako.”

Baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka na kumuacha mama Cecy ameganda kama sanamu asielewe chochote zaidi ya kashfa walizomiminiwa na mama Colin.

 Alilitizama gari liliondoka kwa kutimua vumbi mpaka lilipopotea kwenye macho yake.

“Maama, ” alishtuliwa na kauli ya Cecy aliyetokea nyuma ya nyumba akiwa na beseni tupu baada ya kumaliza ndizi.

Mama yake aligeuka na kumtazama mwanaye aliyegundua kulegwa kwa machozi kwa mama yake ambaye uso wake ulipoteza furaha.

“Mamaa! Kuna nini?” Cecy alishtuka.

“Mwanangu umaskini mbaya,” mama yake alisema huku akielekea kukaa kwenye kizingiti cha nyumba.

“Kwa nini mama?”

“Umemfanya nini mama Colin?”

“Kivipi?”

Mama yake alimweleza yaliyotokea muda mfupi, Cecy alishtuka sana kusikia habari zile.

“Mama yaani ndiyo kasema hivyo! Hayo mapenzi na mwanaye yameanza lini?”

“Sijui.”

“Mama namfuata sasa hivi anieleze kuja kututukana bila sababu, kama umaskini wetu tumeridhika nao.”

“Hapana mwanangu mwenye nguvu mwache apite.”

“Si kwa hilo, wameniumiza bado wananifuatafuata,” Cecy alisema kwa sauti ya kilio.

“Wee waache.”

“Mama tukiwaacha watatuzoea, nimeacha kwenda kwao bado tu hawajaridhika mama niache akanithibitishie alichokisema. Ni kweli nampenda Colin lakini hatujatamkiana mambo ya mapenzi yeye kayatoa wapi?” Cecy alisema kwa jazba.

“Mwanangu jasho la mnyonge haliendi joshi.”

“Sawa, lakini Mungu yupo.”

Cecy aliweka beseni lake na kwenda chumbani kwake akiwa amefura kwa hasira. Moyoni alijiapia siku akikutana na mama Colin siku hiyo atamkosea adabu kwa dharau aliyoifanya nyumbani kwao.


Familia mbili zilikutana kupanga tarehe ya harusi ya watoto wao. Kila mmoja alitaka kufanyika harusi ya kifahari kutokana na watoto wao kuwa wa kwanza kuoa na kuolewa katika familia zao.  

Baada ya makubaliano ya tarehe ya ndoa, waliwataarifu watoto wao kilichokuwa kikiendelea juu ya ndoa yao.  Mara moja zilisambazwa taarifa kwa ndugu na jamaa kwa kupewa kadi na wengine kuhudhulia vikao vya maandalizi ya harusi vilivyoanza mara moja. 

Mage alipanga picha zake za harusi kuzisambaza katika mitandao yote ili kumuonesha Hans naye ana watu wanaompenda kwa dhati kuliko yeye aliye upasua moyo wake kwa kisu butu bila ganzi.

Wakiwa katika Mgahawa wa Samakisaki Mlimani City walipokutana Mage na shoga yake kipenzi Brenda kwa ajili ya kula raha. Wakiwa wanakula piza na juisi, baada ya kutafuna kipande cha piza na kusukumia na juisi ya embe, alisema: 

“Brenda yaani sijui siku ya harusi yangu itakuwaje?”

“Mage, litakuwa bonge la harusi ambalo halijawahi kutokea jijini. Mama yako alivyopania, sijui!”

“Yaani, baada ya ndoa wakati tupo honey moon nitazisambaza picha za harusi mitandao yote ili kuwakonga wavimba macho walionicheka baada ya Hans kuoa.”

“Najua Hans ataumia sana,”Brenda alisema huku akikata kipande cha piza.

“Aumie nini wakati amefurahia, lakini Mungu yupo, kisasi changu kwake hakijaisha ningekuwa na uwezo ningemmwagia tindi kali,” Mage alisema huku akikunja uso kwa hasira.

“Magee! Tindi kali ya nini ikiwa tayari umepata mtu mwenye mapezi ya kweli?”

“Brenda hujui tu jinsi nilivyoumia kwa kitendo cha Hans kunihalibia ndoto zangu za maisha.”

“Mage bado unampenda Hans!”

“Aah, wapi!”Mage aliruka kimanga.

“Muongo unampenda na akitokea leo haki ya nani ndoa hakuna,” Brenda alimwambia shoga yake akiwa amemkazia macho.

“Haitatokea hata siku moja, labda jua litoke Magharibi  kwenda Mashariki.”

“Unajikomba tu, lakini upo na Colin kama bodi lakini injini ni Hans.”

“Mawazo yako, kwanza tuachane na mambo ya Hans tuzungumzia harusi yangu.”

“Kama kweli umedhamilia kuolewa na Colin basi litakuwa bonge la harusi.”

Wakiwa katika ya mazungumzo simu Brenda iliita, alipoangalia alikuta namba ngeni alipokea.

“Haloo.”

“Haloo Brenda.”

“Abee, nani mwenzangu?”

“Yaani nawe umenichukia kama shoga yako, Brenda nimekukosea nini?”

Sauti ile ilimshtua na kugundua anazungumza na Hans.

“Jamani shemu mambo mengi si unajua  mitihani ilitukamata.”

“Pamoja na mitihani, lakini umenitenga shemeji yangu!”

“Siwezi kukutenga.”

“Naomba msaada wa kunikutanisha na Mage, kuna tetesi zimeniumiza moyo wangu. Usishangae wakati wowote ukisikia kifo changu.”

“Brenda unazungumza na nani?” Mage aliingilia kati mazungumzo kwa kusimama na kusogea kwa Brenda.

“Mage hebu subiri,”Brenda alimtuliza Mage na kuendelea kuzungumza.

“ Kipi tena kitasababisha kifo chako, unaumwa?”

“Heri ningeumwa kuliko ukatili anaonifanyia shoga yako. Anajua mimi na yeye tumetoka wapi na tuliahidiana nini. Kweli Mage unakubali kuolewa na mwanaume mwingine tofauti na mimi?” Hans alisema kwa sauti ya huzuni. 

“Hans utakuwa unakosea kusema hivyo, wewe ndiye uliyesababisha yote. Ulikuwa ukifahamu Mage alikuwa akikupenda kiasi gani na unajua nini kilimpata baada ya wewe kufunga ndoa.”

“Najua, lakini nilimweleza kila kitu.”

“Mbona ulikwenda kinyume?”

“Nilikuwa na sababu yangu ambayo Mage alitakiwa kunisikiliza na kuelewa sababu ya mimi kufanya vile wala asingefikia huko.”

“Hans usimlaumu Mage kwa vile naye kafanya kama wewe.”

“Kivipi?”

“Mume katafutiwa na mama yake.”

“Duh! Haijawahi kutokea.”

“Basi imetokea.”

“Basi naomba anipe nafasi ya kuzungumza naye kwa dakika chache.”

“Sidhani kama anaweza kupata nafasi kwa muda huu wa maandalizi ya harusi.”

“Najua, ila nilikuwa nataka kuzungumza naye hata dakika kumi kabla ya ndoa yake.”

“Hans, hiki si kipindi cha kuzungumza chochote na Mage, unaweza kuivuruga ndoa yake.”

“Siwezi, nataka tu nizungumze naye ili akiolewa ajue mimi si adui yake.”

“Mmh! Nitafikisha ujumbe.”

“Naomba shemeji yangu unikutanishe na Mage nitakupa zawadi yoyote unayotaka.”

“Sawa shemu.”

“Nashukuru kwa kunisikiliza pia wewe ni daraja muhimu kati yangu na Mage.”

“Nimekuelewa.”

Brenda alikata simu na kumgeukia shoga yake aliyekuwa na kumuhemuhe cha kutaka kujua Hans alikuwa akisemaje.

“Vipi mzushi alikuwa akisemaje?”

Brenda alimweleza mazungumzo yote waliyozungumza na Hans.

“Mmh! Anataka kuniambia nini?”

“Sijui, ninyi ndiyo unajua mlizungumza nini katika ahadi ya penzi lenu.”

“Uhuu!” Mage alishusha pumzi na kusema:

“Brenda unanishauri nini?”Mage alionekana kama ametahayari kusikia taarifa za Hans.

“Kwa vile upo katika hatua nzuri ya harusi, huu si muda wa kuzungumza na Hans unaweza kuharibu kila kitu ukakosa bara na pwani,” Brenda alimtaadhalisha rafiki yake.

“Eti eeh, sijui Hans anataka kuniambia nini?”

“Achana naye.”

“Mmh! Sawa.”

Kwa vile muda uliokuwa umekwenda sana, kila mmoja aliingia kwenye gari lake kurudi nyumbani.

                                       ***

Brenda alipofika nyumbani kwao alikwenda kuoga na kupata chakula kisha alijifungia chumbani kwake na kuwasha Ipad yake na kuanza kuchati na marafiki zake kwenye  Twiter na Skype. 

Akiwa anaendelea kuchati  simu yake iliita, namba ilikuwa ngeni aliipokea.

“Haloo.”

“Haloo Brenda.”

“Abee, nani?”

“Brenda unaniuliza nani wakati tumetoka kuzungumza muda si mrefu.”

“Hans?” Brenda aliuliza.

“Ndiyo.”

“Unasemaje?”

“Brenda samahani sana.”

“Bila samahani.”

“Naomba unikutanishe leo na Mage.”

“Hans, si tumeisha ongea?”

“Hapana Brenda, kuna kitu cha muhimu sana nataka nizungumza naye kabla siku ya kesho.”

“Samahani Hans, nipo Bagamoyo sitarudi leo.”

“Naomba hata umpigie simu ili anisikilize hata kwa sekunde tano tu.”

“Hans kwanza samahani, hapa nipo na boy friend yangu, ana wivu sana naomba tuzungumze kesho,” Brenda alidanganya. 

“Samahani, ila utakacho kisikia  kesho usishangae najua Mage atafurahi.”

“Unataka kufanya nini Hans?”

“Nilitakiwa kumweleza Mage mwenyewe, kwa heri.”

Hans alikata simu na kumfanya Brenda abakie na simu mkononi kama anatazama kitu cha kumshangaza, alijikuta akijuliza.

“Hans anataka kufanya nini? Au anataka kujiua? Mmh! Ngoja nimweleze Mage maana sasa imekuwa kazi. Lakini kipi cha ajabu Mage akiolewa? Kwani alitaka akae vile mpaka lini? Hivi Hans anashida na Mage au anataka kumvuruga maisha tu?”

Brenda alijikuta akiwaza peke yake, wakati huo simu aliyopiga ilikuwa ikiita. Ilipokelewa upande wa pili.

“Haloo shoga lete stori,” Mage alipokea.

“Mmh! Mtu wako ananisumbua sana.”

“Nani?”

“Hans.”

“Kakupigia tena?” Mage alishtuka.

“Ndiyo.”

“Brenda achana naye, kwa nini unamsikiliza?”

“Mage siwezi kumkatia simu kwa vile sina ugomvi naye.”

“Yaani hivi najiandaa kwenda kwa Colin, tulikuwa tunachati tukaona haitoshi, tukaongea vilevile tukaona haitoshi, nimeamua kwenda kabisa kuonana uso kwa macho.”

“Duh!”

“Brenda, nimeamini Colin ananipenda sana.”

“Sasa ndiyo utulie.”

“Brenda, lazima nitulie Colin kaniahidi vitu vingi sana baada ya ndoa nina imani ndoto zangu nilizoziota kwa Hans zitakuwa mara kumi.”

“Basi ndiyo hiyo mtu wako wa roho ya Mungu anatapatapa kama mfa maji.”

“Kwani alikuwa akisemaje?”

Brenda alimweleza yote aliyoelezwa na Hans na alivyomdanganya, Mage baada ya kumsikiliza alishusha pumzi na kusema:

“Kwani Hans anataka kuniambia nini?” Mage aliuliza.

“Akwambie nini! Yule muharibifu, huu si muda wa kumsikiliza, ukirogwa kumsikiliza tu ndoa huna.”

“Mmh! Nimekuelewa japo moyo unatamani kumsikiliza ili nijue anataka kusema nini?”

“La kusema hakosi, anaweza kukuvuruga akili na ndoa yako ukaiona chungu. Najua bado unampenda sana Hans, kama utampa nafasi narudia tena ndoa hakuna,” Brenda alimtaadhalisha Mage.

“Hata siku moja, labda siyo Mage mimi, siwezi kuumizwa mara ya tatu mbili zinatosha.”

“Basi ndiyo hivyo kuwa makini na Hans, kwa nini muda wote akae kimya, kusikia unataka kuolewa ndiyo ajifanye anakupenda sana.”

“Nimekuelewa basi wacha niwahi kwa mahabuba wangu.”

“Mambo si hayo.”

Brenda alikata simu na kuendelea kuchati na mashoga zake.

                                                                    ***

Sauti ya simu kuita ilimshtua Brenda aliyekuwa bado amelala, alipoangalia ilikuwa namba ngeni, aliipokea.

“Haloo.”

“Haloo, nazungumza na Brenda?”

“Ndiyo, nani mwenzangu?”

“Naitwa Ndubi rafiki mkubwa wa Hans.”

“Ndiyo Ndubi.”

“Kuna habari siyo nzuri.”

“Habari gani?”

“Hans amepata matatizo makubwa sana, nilijaribu kumpigia Mage simu yake haipatikani nikaona nikupigie wewe ili umjulishe.”

“Mmh! Matatizo gani?”

“Jana usiku wamevamiwa nyumbani kwake na majambazi,  mkewe na mwanaye wameuawa na yeye hatujui kama yupo hai.”

“Mungu wangu! Yupo wapi kwa sasa?”

“Yupo hospitali ya muhimbili chumba cha wagonjwa mahututi.”

“Mungu wangu! Ngoja nimjulishe Mage.”

“Itakuwa vizuri.”

Baada ya simu kukatwa Brenda alimpigia simu Mage aliyekuwa bado yupo kwa mchumba wake Colin. Baada ya simu kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.

“Haloo Brenda mbona unaharibu pozi za watu,” Mage alisema kwa utani.

Brenda hakupoteza muda alimweleza taarifa aliyopokea asubuhi ile, taarifa ile ilimshtua sana Mage.

“Mungu wangu! Yupo wapi?”

“Mihimbili.”

“Nakuja sasa hivi twende.”

“Noo, tutakutana hospitali.”

Mage alinyanyuka kitandani na kupitia nguo zake na kuvaa bila kuoga, hakutaka kumwamsha Colin aliyekuwa bado amepitiwa usingizi. Alitoka hadi kwenye gari lake na kuondoka kuelekea muhimbili kumuona Hans. Njia nzima alijilaumu kukataa kusikiliza wito wa Hans kwa kuamini kuna kitu  cha muhimu alitaka kumweleza.

Alijiuliza Hans alitaka kumweleza nini na kwa nini alilazimisha waonane usiku wa jana yake kisha asubuhi  asikie habari kama zile za kushtusha. 

“Mungu wangu kama Hans atakuwa amekufa atakufa na kinyongo, sikutakiwa kuwa katili kiasi kile. Japokuwa sikuwa tayari  kurudiana naye lakini nilitakiwa kumsikiliza.”

Mage alikuwa kwenye lindi la mawazo juu ya  Hans kuwa katika hali ile. Alijikuta akitokwa na machozi kumlilia. Alijiuliza kama ndiye yeye angekuwa mke wa Hans na tukio lile likatokea ina maana angekufa yeye.

Kutokana na mawazo mengi alijikuta akiendesha gari pasipo umakini, alifunga breki mbele ya gari lililosimama baada taa nyekundu kuwaka za makutano ya barabara ya Oceon na Upanga. Alikanyaka breki kwa nguvu zote huku akifumba macho na kuuma meno. Gari lilisota na kwenda kujigonga kidogo kwenye Land Cruser  la Mwarabu.

Kelele za breki zilifanya watu wote kugeuka kuangalia, askari wa barabarani alifika lakini Mwarabu hakutaka kesi kwa vile gari lake halikuharibika sehemu yoyote. Aliliruhusu na kumfuata  Mage kumuuliza:

“Vipi mbona hivyo?”

Mage alishindwa kumjibu kwa vile presha ilikuwa juu na uso ulikuwa umejaa machozi. Askari hakutaka kumuhoji kitu alimruhusu kuondoka. Mage aliondoa gari kuingia barabara ya Upanga kuelekea Muhimbili kumuona Hans.

Njia nzima Mage alikuwa akilia, alikumbuka maisha aliyoishi na Hans, mwanaume akiyempenda kuliko kitu chochote chini ya jua. Waliishi maisha ya mapenzi kama njiwa, kila mmoja alimpenda mwenzake penzi la glasi halikuwa na kificho kila mmoja aliamini anapendwa na mwenzake.

Alikumbuka ahadi ya Hans alipomwambia kumuacha yeye ni sawa na roho kuachana na mwili. Alimuhakikisha yeye ndiye mwanamke wa maisha yake. Baada ya Hans kuozwa kwa shinikizo la wazazi, walikubaliana avumilie ili baadaye amuache mwanamke wa kulazimishwa ikiwa pamoja na kuitozaa naye. 

Lakini Hans alionekana kugeuka pale alipopata mtoto ndani ya ndoa yake tofauti na walivyokubaliana kutozaa na yule mwanamke na kwenda kinyume na kumfanya naye akubali kuolewa na Colin.

Alijiuliza nani aliyefanya kitendo kile, alijikuta akitengeneza mawazo ya kijiunga kuwaza labda mpango ule kaufanya Colin kutokana na wasiwasi wa kurudiana na Hans.

“Nikigundua Colin kama ndiye aliyemuua mpenzi wangu, nitamchukia mpaka kufa na nitakuwa shahidi namba moja kuhakikisha na yeye ananyongwa,” Mage aliwaza.  

Alipofika Muhumbili alisimamisha gari na kuelekea kwenye wadi ya wagonjwa mahututi. Nje ya wadi aliikuta familia ya Hans, hakuna aliyemjali japokuwa alionekana amevimba macho kutokana  kumlilia Hans.

Alipojaribu kuingia wadini alikatazwa na kuamua kusimama pembeni peke yake, baada ya muda shoga yake Brenda alifika na kwenda aliposimama.

“Vipi shoga?”

“Yaani mama Hans kanifukuza kama mbwa!”

“Kwa nini?”

“Hata sijui wakati anafahamu mimi na mwanaye tulikuwa vipi.”

“Kwa hiyo hujui hali ya Hans?”

“Sijui chochote.”

Mara simu ya Mage iliita alipoangalia ilikuwa ikitoka kwa Colin, aliitazama na kukunja uso bila kuipokea. Brenda aliyekuwa  akimtazama usoni alimuuliza.

“Simu ya nani?”

“Achana nayo,” alijibu kwa mkato.

“Mmh!”

Baada ya muda simu iliita tena, Brenda alishtuka kuona jina la Colin bila kupokelewa.

“Shoga mbona hupokei?”

“Achana naye.”

“Ha! Wewe si ulikuwa kwa Colin na umeondokaje?”

“Sijamuaga nimemuchana bado amelala.”

“Unajua unacho kifanya unaiweka ndoa yako njia panda.”

“Kwani asiponioa nitapungukiwa nini?” Mage alijibu huku akibinua midomo.

“Mage, usipoteze muda wa Colin, kuamini unampenda kumbe upo naye kivuli tu.”

“Brenda mwenye uamuzi wa kumpenda nani ninao mimi.”

“Kwa hiyo Colin si chaguo lako?”

“Brenda huu si wakati wa kuzungumzia Colin zaidi ya kujua hali ya Hans ndiye aliyetuleta hapa.”

“Mmh! Sawa.”


Colin baada ya kushtuka usingizini alijua mpenzi wake yupo msalani au bafuni, lakini muda ulikatika bila kuonekana. Alikwenda msalani kumtafuta huku akimwita bila kupata jibu. Alitoka hadi nje na kumuuliza mlinzi.

“John umemuona shemeji yako?”

“Ametoka asubuhi sana, hakukuaga?”

“Ameniacha nimelala.”

“Tena alionekana kama analia nilijua mmegombana.”

“Hata sielewi kitu.”

Colin alimpigia simu mchumba wake, lakini iliita bila kupokelewa. Alirudia zaidi ya mara tatu vilevile haikupokelewa. Alijiuliza Mage amepatwa na nini, wasiwasi wake labda kwao kumetokea tatizo. Aliingia ndani na kuvaa pensi na fulana chini alivaa ndala na kuingia kwenye gari kuelekea Kigamboni kwa kina Mage ili ajue amepatwa na nini.  

Alikimbiliza gari, kutokana na foleni aliamua gari lake kulipaki Posta ya zamani na kuchukua bodaboda ili awahi kuifika. Baada ya kuvuka alichukua nyingine iliyo mpeleka nyumbani kwao Mage. 

Alimlipa dereva na kuingia ndani ya geti, alipofika sebuleni alimkuta msichana wa kazi akifanya usafi.

“Habari Sofi?”

“Nzuri shemu, shikamoo.”

“Marahaba, vipi Mage yupo?”

“Sijamuona toka asubuhi.”

“Mama.”

“Yupo chumbani kwake.”

“Kaniitie.”

Colin alibakia sebuleni kumsubiri mama Mage, baada ya muda alitokea na kushangaa kumuona Colin katika hali ile.

“Vipi baba, kwema?” 

“Kwema, sijui hapa.”

“Hapa hatujambo, mwenzio yupo wapi?”mama Mage alimuulizia mwanaye baada ya kumuona Colin peke yake.

“Nimeshtuka kitandani sikumkuta, nimempigia simu haipokelewi, nikawa na wasiwasi na kuamua kuja huku.”

“Hapa sijamuona, atakuwa amekwenda wapi? Mmh! Basi atakuwa kwa Brenda tu.”

Colin alipiga simu kwa mara nyingine lakini haikupokelewa, alirudia mara mbili vilevile haikupokelewa baadaye ikazimwa kabisa.

“Mama simu haipokelewi niliporudia imezimwa kabisa.”

“Mmh! Atakuwa wapi mtoto huyu la..”

Mama yake alinyamaza baada ya kumuona mwanaye akiingia, wote walipeleka macho kwake. Walishtuka kumuona macho yake yamevimba kuonesha alikuwa akilia.

 Aliwapita bila kuwasemesha na kuelekea chumbani kwake kitu kilichomshtua mama Mage na kumuuliza Colin.

“Colin umemfanya nini mwanangu?”

“Mama sijamfanya kitu, si umuulize mbele yangu.”

Mama Mage alimfuata mwanaye chumbani na kumkuta amejilaza kwa kulilia tumbo.

“Mage.”

“Abee.”

“Kuna nini?”

“Hans ana hali mbaya asishangae kusikia amefariki.”

“Amefanya nini?”

“Amevamiwa na majambazi, mke wake na mwanaye wameuawa.”

“Mungu wangu! Ndipo unapotoka?”

“Ndiyo, mama.”

“Mbona hukumuaga mwenzio?”

“Ningemuaga nakwenda wapi?”

“Na mbona umempita bila kumsalimia.”

“Nitamweleza nini?”

“Kwa hiyo itakuwaje?”

“Mwambie aondoke siwezi kuzungumza naye chochote kwa sasa.”

“Magee, unajua Colin ni nani yako?”

“Mchumba wangu na mume wangu mtalajiwa, lakini kwa leo naomba aniache nitamtafuta mwenyewe.”

“Mage, unajua unanitafutia lawama, Colin atatuelewa kweli?”

“Mama tumia kila uwezavyo ili Colin aondoke nitamtafuta.”

“Unanitia kwenye ubaya, Mage unaibomoa ndoa yako kwa mikono yako, unapoteza uaminifu kabla ya ndoa.”

“Mama ndoa ni zawadi toka kwa Mungu, kama si riziki yangu siwezi kuilazimisha.”

“Mmh! Sawa wacha nikajaribu,” mama Mage alitoka chumbani na kumwacha mwanaye amejilaza huku akiwa na mtihani wa kumweleza Colin ili aondoke bila kuhoji kitu. 

Colin alibakia sebuleni akiwaza kipi kimempata mchumba, alijiuliza alikwenda wapi asubuhi ile mchumba wake kama hakurudi nyumbani na kwa nini ameonekana analia kipi kimemsibu. Alibakia kusubiri kwa hamu kujua kipi kimemsibu mchumba wake, ambaye aliamini ndiye moyo wake yeye alibakia na mwili tu. 

Mama Mage alirudi hadi sebuleni, Colin aliyekuwa ametazama juu akiwa mwingi wa mawazo kutokana na kilichotokea asubuhi ile. Aliposikia sauti ya  miguu ikisogea alipokuwa amekaa aliyahamisha macho yake na kumuona mama Mage, alijikuta akinyanyuka kama anampokea mheshimiwa.

“ Vipi mama?”

“Mmh! Safi tu,” Mama Mage alijibu huku akijitahidi kutengeneza uso wa mbuzi ili aweze kutengeneza mambo hasa kutokana kuwa mzazi.

“Vipi Mage alikuwa wapi na amepatwa na nini?” Colin aliuliza akiwa amemkazia macho.

“Mmh! Si..si..au fanya hivi, baba wewe nenda nyumbani mpenzi wako kuna mambo yao ya kitoto si unajua baba mwenzio bado mdogo?”

“Ndiyo najua, lakini amepatwa na nini na alikwenda wapi bila kuniaga ikiwa hawa wewe hujui?”

“Mwanangu, wala hakuna jambo la kutisha, u..u..najua mwenzio, baba eeh, hebu kwanza hili tuliache jioni mwenyewe atakueleza kila kitu,” mama Mage alijitahidi kubadili mazungumzo.

“Sawa mama, lakini Mage ni mchumba  wangu ninatakiwa kujua kila kitu chake, sasa hivi ni mke wangu, tumetenganishwa na ndoa tu ambayo haipo mbali. Hivi nirudi nyumbani namweleza mama nilichokikuta hapa kisha naulizwa  kimetokana na nini nitajibu nini?” Colin alitetea hoja yake.

“Mwanangu ngoja nikutoe wasiwasi, mwenzio alikwenda kwa shoga yake sijui nini anamdai, basi wametibuana ndiyo maana yupo vile,” mama alitengeneza uongo.

“Sasa mama kama ni hivyo kwa nini hataki kuzungumza na mimi?”

“Colin mwanangu, mi mkubwa naomba uondoke ili jioni uzungumze vizuri na mwenzako. Atakachokuambia hata wewe utacheka.”

“Mmh! Sawa, basi mi’ naondoka.”

Colin alisema huku akinyanyuka kuelekea nje, alipofika nje alikodi bodaboda hadi Kivukoni  ambako alivuka upande wa pili na kukodi bodaboda nyingine hadi kwenye gari lake na kuingia ndani.

Kabla ya kuondoka alitulia mikono aliweka juu usukani na macho aliangalia mbele, alikuwa kama anaona lakini alizama kwenye mawazo na kujiuliza Mage alikwenda wapi bila kuaga na kwa nini amerudi akilia kipi kimempata alipokwenda na mwisho alijiuliza kwa nini amekataa kuzungumza naye.

Baada ya kukosa majibu ya maswali yake aliondoa gari kuelekea nyumbani, alitembea mwendo wa kawaida huku akili yake ikiwa haijakaa sawa. Alipofika katika makutano ya barabara ya Kawawa na Morogoro macho yake yalishtuka kumuona msichana mmoja akiuza ndizi.

Sura yake haikuwa ngeni machoni mwake lakini mavazi yalifanya macho yapingane na akili yake. Sura ilikuwa ya Cecy lakini mavazi yake yalikuwa machakavu na mwili ulimvaa vumbi kwa ajili ya kutembea  barabarani kwa miguu kuuza ndizi. Kwa vile alikuwa kwenye foleni alituliza macho yake kwa binti yule ambayo yalimwambia ni Cecy.

Wakati anataka kuondoa gari alisikia mtu akimwita.

“Cecy leta ndizi mbili.”

Kwa vile taa ziliruhusu aliliondoa gari na kwenda kulipaki kituo cha mafuta cha Magomeni, alilizima na kutoka nje, kwa vile Cecy alikuwa amevuka barabara kwenda kuuza ndizi maeneo ya Hospitali. Alimtuma kijana mmoja aliyekuwa akiuza miwa.

“Samahani mkubwa, naomba kwamwambia yule msichana alete ndizi kumi.”

Yule kijana alimfuata Cecy aliyekuwa ametua beseni lake chini akiuza ndizi, alipofika alimwambia.

“Dada peleka ndizi kumi kwenye lile gari.”

“Kumi hazitafika zitabaki sita.”

“Mpelekee zote.”

“Sawa, ngoja nichukue hela.”

Baada ya kuuza alibeba beseni lake na kuvuka barabara mpaka kwenye gari, kioo cha gari kilikuwa kimepandishwa kidogo hivyo hakumuona aliyekuwa kwenye gari. Aligonga kioo kidogo ili auze ndizi.

“Kaka.”

Colin aliteremsha kioo na kufanya Cecy amuone vizuri kitu kilichomfanya ashtuke.

“Ha! Colin?” mshtuko alioupata ulifanya adondoshe beseni  la ndizi.

Hakuliokota alibakia amesimama mpaka Colin alipoteremka kwenye gari na kuokota ndizi  zote kisha alimshika mkono Cecy.

“Cecy.”

“Abee,” Cecy aliitikia huku machozi yakimtoka na mwili kumtetemeka.

“Unalia nini mchumba?”

“Colin mimi si mchumba wako, mchumba wako Mage,” Cecy alijibu kwa ukali kidogo.

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Mama yako amechotufanya kwa ajili yako, Colin lini nilikutamkia nakupenda?”

“Hujawahi hata siku moja.”

“Kwa nini mama yako amefunga safari ya kuja kunituka kuwa naingilia ndoa yako na kutudhalilisha kwa ajili ya umaskini wetu. Colin maskini hapendi?”

“Anapenda.”

“Ni kweli Colin nakupenda zaidi ya kukupenda, nailaumu nafsi yangu kuchelewa kukueleza ukweli kuwa nakupenda. Najua haikuwa bahati yangu unayetaka kumuoa ndiye chaguo la moyo wako. Kipi kilichomtuma mama yako kuja kunitukana na kutudhalilisha  bahati yake sikumkuta najua ningemfanya nini!” Cecy alisema kwa sauti ya  hasira.

“Lini?”

Cecy alimtajia siku na kukumbuka siku  ambayo Colin alikumbuka ndiyo siku aliyokamata picha kumbe alikwenda kumtukana Cecy bila kutaka kuujua ukweli.

“Cecy samahani sana, pia pole kwa kushindwa kuujua upendo wako.”

Alimweleza ukweli juu ya uchumba wake na Mage alivyotengenezwa na mama yake.

“Kwa hiyo Mage si chaguo lako ni la mama yako?”

“Hapana, mwanzo lilikuwa chaguo la mama baada ya kumuona nilikubaliana naye na ndiyo tulipanga kuoana.”

“Kwa hiyo siku ile uliniita kuja kunidhalilisha na kuumiza moyo wangu?”

“Hapana nilikualika kama wageni wengine, pia nina mpango mkubwa sana kwako ambao utakusaidia kimaisha.”

“Colin mpango ambao naukubali kwako labda niwe mkeo lakini zaidi ya hapo usijisumbue,” Cecy alisema kwa sauti ya kike kwa kujiamini.

Colin alijitahidi kumwelewesha sababu ya picha zake na kipi alichokipanga juu yake.

“Hivi leo hii nifanye kazi kwenye kampuni yetu mama yako atakubali anajua sisi ni wapenzi, kuna kazi?”

“Kwanza hebu nieleze sababu ya wewe kuwa kwenye hali hii?” Colin alimuuliza huku akiangalia mavazi na hali aliyokuwa nayo Cecy.

“Sina thamani haya ndiyo maisha niliyoyachagua ili mama yako akiniona asiwe na wasiwasi na ndoa yako.”

“Cecy nitakutafuta tuzungumze akili yako ikitulia.”

“Usijisumbue.”

“Lazima nijisumbue kwako kwa vile kuna kitu ndani yako nilichokiona.”

“Colin niache nirudi nyumbani.”

“Unakaa wapi nikupeleke.”

“Colin unataka mama yako aje kuchoka pagala letu, aliona picha ikawa vile vipi anione kwenye gari lako?”

“Hawezi, na ungeniambia alichokifanya ningempa ukweli, tabu ya kina mama wa kiswahili wazungu hawajali vitu vya kijingakijinga.”

“We nenda tu.”



Colin alimbembeleza sana Cecy, kwa vile naye alikuwa akimpenda akiingia kwenye gari na kurudishwa nyumbani kwao.  Walipomfikisha Colin naye aliteremka na kuongozana hadi kwa kina Cecy ambako kulikuwa na nyumba ya vyumba viwili na sebule. Lakini nyumba ilikuwa ya hali ya chini bati zake zilikuwa na kutu na juu waliweka mawe ili kuzuia bati lisiezuliwe na upepo. 

Cecy baada ya kufika eneo la kwao alishukuru na kuanza kuelekea nyumbani, lakini Colin alimsemesha.

“Cecy mbona unaniacha mgeni?”

“Colin nashukuru umenileta, lakini naomba usifike nyumbani.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Nimekueleza mara ngapi kuhusu mama yangu, unataka mama yako aje akitie moto kibanda chetu.”

“Cecy suala la kuhusu mama yangu niachenie mimi, naomba nimsalimie mama mara moja.”

“Mmh! Sawa.”

Waliongozana Cecy na Colin hadi nyumbani kwao ambako alitambulishwa kwa mama yake na kumfanya mama Cecy ashtuke.

“Ha! Wewe ndiye unayenyanyasa mwanangu?”

“Kumnyanyasa kivipi mama?”

Mama Cecy alimweleza mateso yote ya mwanaye juu yake na jinsi mama yake alivyokwenda kuwatukana huku akitishia maisha ya Cecy kama ataharibu ndoa yake na Mage. Colin baada ya kusikilia maneno yale aliyarudia maneno ya Cecy juu ya mapenzi yake kwake.

Ashangaa kuona penzi la Cecy kwake lilikuwa wazi kwa mama yake lakini mhusika mkuu alikuwa hajui kitu zaidi ya kumuona Cecy kama msichana mzuri lakini hakuwa na uwezo wa kumtamkia chochote kutokana na mama yake kumtafutia mwanamke aoe ambaye kwa upande wake aliungana na uchaguzi wa mama yake.

“Mzazi wangu, kwanza niwaombeni radhi kwa yote yaliyotokea kwa mama yangu kuja kuwatukana bila sababu. Naweza kusema labda makosa nimefanya mimi kwa kutomjulisha nini nilichotaka kukifanya na Cecy. 

“Najua mama yangu alimpenda Cecy lakini si kuwa mke wa mwanaye bali msichana mzuri anayejiheshimu. Inawezekana kigezo cha elimu ndicho kilichomfanya mama yangu amtafute Mage, nina imani kama Cecy angekuwa na elimu kama ya Mage basi angekuwa chaguo la kwanza la mama.

“ Wasiwasi mkubwa wa mama ilianzia siku alipomuona Cecy kapendeza naweza kusema aliwashinda wote waliokuwa kwenye sherehe yangu. Kilichomshtua mama yangu kunikuta na picha ya Cecy aliyokuwa amependeza sana. Aliamini kabisa ni mpenzi wangu hivyo kujihami kabla mambo hayajaharibika kutokana na harusi yetu kuandaliwa kwa fedha nyingi sana. 

“Lakini hakutakiwa kuchukua uamuzi aliochukua bila kuniuliza mimi japokuwa nilimweleza sababu ya kuwa na picha ile. Ila napenda kuwaeleza kitu kimoja kuwa sitauacha upendo wa Cecy upitee hivihivi najitolea kumsomesha ili aongeze elimu na ujuzi.

Baada ya elimu hiyo nitafanya naye kazi ndani na nje ya nchi ambayo naamini itamweka katika maisha mazuri na ramani ya dunia. Pia nitahakikisha naijenga nyumba yenu katika hadhi ya kisasa pia mama nitakufungulia mradi ili muendeshe maisha yenu,” Colin alieleza nia yake nzuri kwa Cecy na mama yake.

“Asante bab..”

“Mama nani kamwambia sisi tuna shida ya vitu hivyo? Kama kilichonitesa nimekikosa, sihitaji kitu kingine toka kwako,” Cecy alimkatisha mama yake na kumjia juu Colin kwa kauli yake.

“Cecy mimi na wewe nani mwenye kosa, ulilolisema leo ungelisema mapema situngefika huku,” Colin alijitetea.

“Muongo! Colin  hata ningesema ingekuwa sawa na kazi bure kwa vile tayari mama yako aliisha kuchagulia mwanamke,” Cecy alisema kwa hisia kali.

“Kabla ya kutoa uamuzi ningechagua.”

“Mimi na Mage unampenda nani?”

“Nawapenda wote, ila kwa sasa Mage kwa vile ndiye tupo katika mipango ya ndoa.”

“Kwa kauli hiyo naomba tukomane kila mtu ashike hamsini zake ukinikuta njiani nipite kama nguzo ya umeme,” Cecy alisema kwa hasira.

“Cecy kuwa na adabu, heshimu anachokisema mwenzako...Baba kama una nia hiyo ifanye faida hataiona leo, lakini baadaye atakushukuru.”

“Sawa mama nimekuelewa, Cecy punguza hasira nina nia nzuri na wewe, uzuri wako nitaulinda na baadaye utakuingia fedha nyingi na kumsaidia mama. Utauza ndizi mpaka lini?”

Cecy hakujibu kitu aliinama chini, Colin alimsogelea na kumbembeleza kitu kilichomfanya Cecy aangue kilio na kusema:

“Colin nisamehe kwa yote, hujui kiasi gani penzi lako lilivyouathiri moyo wangu, najua nilikupenda bila kushauriana na moyo wangu. Mnaweza kuniona mdogo lakini nami nina hisia za mapenzi kama wengine,” Cecy alisema huku akimtazama Colin kwa macho yaliyojaa machozi.

“Najua Cecy, isingekuwa mipango ya harusi ningeza kufanya chochote ili ujue nauthamini upendo wako.”

“Sawa Colin nimekuelewa.”

Kwa vile muda ulikuwa umekwenda Colin aliaga kuwahi nyumbani baada ya kuondoka bila kuaga. Alikwenda kwenye gari na kuwaletea laki moja, walimshukuru naye aliondoka kuelekea nyumbani. Njiani alijikuta akimuwaza Cecy msichana mdogo lakini alikuwa jasiri kuzielezea hisia zake japo aliamini mama yake asingemkubali kutokana na uduni wa maisha na kukosa elimu.

Kwa upande mwingine aliamini kabisa kutokana na kasi ya mabadiliko duniani Mage ndiye mwanamke sahihi kwake. Kwani aliamini maisha ni zaidi ya mapenzi kwa vile maisha yakiwa vizuri kila kitu kinakwenda. Aliamini kwa umbile adimu la Cecy angeweza kuifanya kazi yake vizuri ya maonesho ya mavazi.

Kitu kikubwa aliamini Cecy kama atapata twisheni ya kingereza ataweza kuongeza uwezo wake hata kusafiri nchi za nje kufanya kazi ya maonesho ya mavazi pia kupata tenda ya kupamba majarida. Aliamini akimtumia vizuri Cecy kampuni yake itafika mbali na yeye kujitengezea kipato kikubwa.

Alipanga kuwekeza fedha nyingi kwa Cecy baadaye angevuna fedha nyingi kwa kuamini alikuwa na kitu cha ziada ambacho wasichana wengi hawakuwa nacho. Japokuwa alikuwa na wasiwasi na kikwazo cha mama yake, lakini kwa vile yupo kikazi alijua mama yake angemuelewa tu.

Alipanga ndani ya wiki mbili nyumba ya kisasa ya kina Cecy iwe imesimama huku akimtafutia twisheni nzuri ili kuijua lugha haraka. Alipanga kufungua duka mbele ya nyumba yao ambalo litawafanya waingize kipato kila siku. Kutokana na kuzama kwenye mawazo ya kumuwaza Cecy alijikuta akimsahau Mage mpaka alipofika kwao.

                                                                  ***

Alipoingia ndani alikutana na mama yake ambaye alishangaa kumuona mwanaye akiteremka kwenye gari.

“Colin unatoka wapi?”

Colin ilibidi amweleze mama yake kilichotokea, baada ya kumsikiliza alimuuliza:

“Colin mwanangu umemfanya nini mtoto wa watu?”

“Mama sijamfanya kitu chochote kama nilivyokueleza.”

“Mage si mjinga kulia tu na kukataa kuzungumza na wewe wakati mlikuwa pamoja?”

“Yaani sijui kitu labda uulize wewe utapata jibu.”

“Nitauliza, lakini Colin kuna kitu unanificha haiwezekani Mage aondoke bila kukuaga kisha akatae kuzungumza na wewe wakati usiku mmelala pamoja?”

“Mama piga simu uulize labda utagundua kitu.”

“Mmh! Sasa nimepata jibu,” mama Colin alisema huku akitikisa kichwa kama kakumbuka kitu.

“Jibu gani?”

“Colin lazima kuna kitu Mage amegundua kuhusu wewe na Cecy, nasema hivi ndoa ikivunjika Cecy atanitambua.”

“Mama unamuonea bure mtoto wa watu, toka siku ile ya sherehe sijaonana na Cecy,” Colin alidanganya.

“Muongo umemkataza asilete ndizi ili mkutane sehemu nyingine. Colin Mage akinieleza kuwa amegundua una uhusiano na msichana mwingine pagala lao nakwenda kulitia moto sasa hivi.”

“Mama kwa nini unanihukumu kwa kosa nisilofanya, nimekueleza piga simu uulize unaanza kutengeneza mawazo yako. Cecy amekukosea nini mpaka kumchukuia hivyo, ni wewe ndiye uliyekuwa naye karibu?”

Mama Colin hakusema kitu aliingia ndani kuchukua simu ili ampigie Mage kujua amepatwa na nini.

                                                               ***  

Baada ya Colin kuondoka  mama Mage alimfuata mwanaye chumbani aliyekuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo juu ya hali ya Hans na familia yake ilivyomtenga na kumuona kama kinyesi. Moyo ulimuuma na kujua hakukuwa na haja ya yeye kwenda hospitali pia kumuacha mchumba wake mumewe mtarajiwa akiwa amelala na kuondoka bila kumuaga.

Alijilaumu kwa kitendo chake cha kumpita Colin bila kumsemesha, alijiuliza atamfikiliaje. Alijiuliza ndoa yake ikivunjia na ijulikane sababu ya Hans mwanaume asiye na mapenzi naye ataiweka wapi sura yake. Lakini alijiuliza angesimama na kuzungumza na Colin angemwambia anatoka wapi na kwa nini hakumuaga?

Akiwa katika dimbwi la mawazo mama yake aliingia na kumkuta amezilaza chali huku ameukumbatia mto wake na wacho yake alikuwa akiangalia darini.

“Mage..Mage.”

“A..a..bee.”

“Mbona sikuelewi mwanangu?”

“Mama nahitaji msaada wako najua nimechanganya madawa.”

“Nikusaidie nini?”

“Sijui Colin atanielewaje maana nilichomfanyia si kitu kizuri.”

“Kwa kweli hatua tuliyofikia huku vikao vikienda vizuri  halafu mwenzako abadili uamuzi sijui sura zetu tutaziweka wapi?”

“Hapo ndipo ninapochanganyikiwa, mama kitendo walionifanyia familia ya kina Hans sitawasahau.”

“Umeona eeh, nilikueleza toka zamani familia ile ilikuwa haikupendi kama ungeolewa na Hans ndoa yako isingedumu. Mungu amekuletea mwanaume wa maisha yako unamchanganya.”

“Mama nimeisha fanya kosa naomba msaada wako, nitamweleza nini Colin anielewe.”

“Wala usiwe na wasi kamwambie kuwa ulimtuma Brenda cheni ambayo ulipanga kumpatia kama surprise umekuta hajaitengeneza na kujikuta umekasirika na kuanza kulia.”

“Mmh! Atanielewa? Naona kama utetezi mwepesi.”

“Walaa, ye anajua ulikuwa kwa Brenda, nilimwambia kuna kitu mmeshindwa kuelewana ndiyo maana ulirudi katika hali ile.”

“Mmh! Basi ngoja nifanye hivyo.”

Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya iliita ilikuwa ikitoka kwa mama Colin.

“Mkweo,” mama Mage alisema.

“Mmh! Lazima ataulizia kilichotokea.”

“Ngoja nimsikilize,” alisema huku akibofya cha kupolelea na kuweka simu sauti ya nje.

“Haloo mama Colin.”

“Eeh! Dada kuna nini huko?”

“Kwani vipi?”

“Naona Colin ananichanyanyia maneno wala simuelewi.”

“Wala hakuna kitu cha kutisha bali mkweo aliudhiwa na shoga yake, lakini kwa sasa yupo sawa na wakati wowote atakuja huko.”

“Mmh! Afadhali maana nilikuwa na wasiwasi.”

“Wa nini?”

“Nilijua Colin kisha mtibua mkwe wangu.”

“Walaa, sema mkweo ana hasira za kitoto kitu kidogo analia kama kafiwa.”

“Basi nikuacheni muendelee na mambo mengine.”

Baada ya simu kukatwa mama Mage alimgeukia mwanaye na kumwambia.

“Unaona ulivyotaka kumsababishia matatizo mwenzako?”

“Mama lazima niende sasa hivi najua mpenzi wangu hayupo kwenye hali nzuri.”

“Fanya hivyo na...” mama Mage alinyamaza baada ya mlango kugongwa.

“Unasemaje?” aliuliza kwa sauti.

“Kuna wageni.”

“Nakuja,” mama Mage alitoka nje kwenda kumsikiliza mgeni.

Alitoka hadi getini na kukutana wa wanaume wawili na mwanamke mmoja, aliwatazama walikuwa wageni kwake.

“Karibuni.”

“Asante.”

Aliwakaribisha hadi sebuleni, baada ya kuketi mama Mage alitaka kujua wana shida gani.

“Ndiyo jamani mna shida gani?”

“Sisi ni maafisa wa polisi,” walitoa vitambulisho vyao.

“Ndiyo, mna shida gani?”

“Tuna imani hapa ndipo anaishi Magreth Chogo.”

“Ndiyo.”

“Yupo?”

“Mna shida gani?”

Kabla hajajibu Mage alitoka chumbani ili awaone wageni ni kina nani, askari mmoja baada ya kumuona alijua ni Mage alibahatisha kwa kumwita jina.

“Mage.”

“Abee.”

“Upo chini ya ulinzi,” alisema askari wa kike.

“He! Kwa kosa gani?” Mage alishtuka. 

“Kutokana na tukio lililomtokea mpenzi wako wa zamani.”


ITAENDELEA



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.