MALAIKA MWEUSI EPISODE 1

 




Hadithi: MALAIKA MWEUSI

SEHEMU: 01

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

SIMU: 0713 646500


                               MALAIKA MWEUSI.


Alikuwa amepiga goti pembeni ya mwili wa mama yake ambaye alikuwa amefariki muda mfupi tu kutokana na kipigo cha mumewe, ambaye ni baba wa kufikia wa msichana Thereza. Huku akiwa analia kwa uchungu alimuahadi mama yake kuwa lazima atalipa kisasi kwa wale waliomtendea unyama. Kwa kusoma kwa bidii ili siku moja awe hakimu au mwanasheria awafunge wote wanaonyanyasa wanawake na kuwabaka. Lakini dhamira yake ilikatishwa kwa kuachishwa shule akiwa darasa la sita na kuuzwa kwa mtu ili awe mtumishi wa ndani! Je, msichana Thereza atatimiza ahadi yake aliyo ihaidi mbele ya mwili wa marehemu mama yake? Ungana na mtunzi mahiri Ally Mbetu katika riwaya hii ya kusisimua. 


                                                         ****

MLIO wa simu ulimshtua mkuu wa upelelezi aliyekuwa katikati ya usingizi. Aliyatupia macho yake kwenye saa ndogo iliyokuwa juu ya droo ya kitanda, ilimuonyesha kuwa ni saa 10:15 za usiku nusu saa tangu amsindikize rafiki yake wa kike aliyembatiza jina la Black Angel, yaani Malaika Mweusi. 

Aliinyanyua simu yake iliyokuwepo pembeni ya mto aliokuwa ameulalia, alipoichukua simu ilimuonyesha ni simu maalumu kutoka ofisini. Mara nyingi simu hiyo hutumika kwa ajili ya dharura tu. Hasa pale panapotokea matatizo yasiyokuwa ya kawaida.

Alibofya kifute cha kupokelea simu na kuzungumza kwa sauti ya uchovu, kutokana na shughuli ya usiku haikuwa haba, ilimnyong’onyesha mwili.

Shughuli ya Malaika Mweusi ilimfanya atangaze ndoa na msichana huyo aliyetokea kumuamuni kupita kiasi, hasa kutokana na tabia yake ya upole, ucheshi na roho ya huruma. Vitu ambavyo wanawake wengi hawana zaidi ya kuwa na kimojakimoja, pia Malaika Mweusi alijaliwa sura na umbile la kuvutia.

Mwanaume yeyote asingeweza kujizuia kutangaza ndoa kwa binti huyo aliyeonekana kutoka kwenye familia ya kitajiri. Akizungumza kwa sauti ya kivivu, Mkuu huyo wa upelelezi bwana Anderson: 

“Ndiyo nakupata, lete habari.”

“Afande, mambo yameharibika,” sauti ya upande wa pili ilisema.

“Wapi tena?” Aliuliza huku akiiweka sawa akili yake.

“Yule hakimu.”

“Ooh! Mungu wangu, hii sasa inatisha nakuja sasa hivi ofisini.”

Bwana Anderson alikwenda bafuni kuoga haraka haraka na kubadili nguo, wakati alitoka nje aliona mkoba wa Malaika Mweusi ukiwa juu ya kochi. Aliwaza sana kuhusu ule mkoba wa Malaika Mweusi na kusema kwa sauti ya chini:

“ Aah! Kumbe jana aliacha mkoba wake, siyo mbaya ataufuata jioni.”

Alikwenda hadi kwenye banda la gari na kulichukua tayari kwa safari ya ofisini. Saa yake ya mkononi ilimuonyesha kuwa ni saa 11:35. Akiwa njiani akiwaza mambo mengi kuhusu vifo vya kutisha vya mfululizo, vifo  ambavyo vimemchanganya yeye na vijana wake. Alipofika ofisini alimkuta maofisa upelelezi na vijana wake wakiwa wameshafika ofisini. Alipoingia ofisini wote walinyanyuka, baada ya kukaa aliwaamuru nao wakae chini.

“Mnaweza kukaa,” baada ya kuketi alisema.

“Ndiyo,  leteni habari,” alisema huku akitembeza macho kila kila mmoja aliyekuwemo mule ndani.

“Afande kama ulivyosikia yule hakimu ameuawa, inavyoonekana ameuawa si chini ya saa sita zilizopita.” Alisema afisa upelelezi.

“Saa sita! Ilikuwaje akachelewa kujulikana?”

“Inavyosemekana amekutwa amekufa katika gari lake ambalo lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara.”

“Nani aliyegundua mwili wa marehemu kwenye gari?”

“Askari wa doria ambao walikuwa wanalipita kila mara ile gari, walipoamua kulichunguza ndipo walipogundua mwili wa hakimu.” 

“Lazima tukubali tumefanya uzembe wa hali ya juu kutokana na kifo cha hakimu.”

“Bosi sidhani kama tumehusika, pamoja na muuaji kutoa vitisho miezi miwili iliyopita. Nina imani tulimpa Hakimu tahadhari na kumweleza sehemu na muda anaotakiwa kuwa nje ya nyumba yake. Kwa kukiuka masharti yetu  kifo chake amekitengeneza yeye mwenyewe.”

“Mmh! Sasa muuaji ni nani, hivi vifo vinafanana? sidhani lakini la muhimu tuwahoji wale ndugu wa yule bwana aliyefungwa na kusababisha vitisho vya muuaji. Maelezo ya awali yalionesha  Hakimu alipindisha sheria na mwisho wa siku ilimuhukumu mwenyewe.”

“Lakini si tuliwahoji mapema wao wakasema hawana uhusianao wowote wala taarifa yoyote kutoka kwa muuaji.”

“Unajua hii inatisha, eti muuaji anajiita mtetezi wa haki za binaadamu.”

“Kwani kwa mara ya mwisho hakimu alikuwa wapi?”

“Job Pub.”

“Okay, kuna umuhimu wa kuwahoji watu waliokuwepo pale Job Pub ili kujua kuwa aliondoka saa ngapi na aliongozana na nani.”

“Sawa bosi, tutaifaanya kazi hiyo.”

“Haya majibu niyapate kabla ya saa moja  usiku, sawa jamani?”

Mkuu wa upelelezi Anderson aliagana na vijana wake na kuondoka kurudi nyumbani huku akiwa amejawa na mawazo mengi kuhusu mauaji ya kutisha yaliyokuwa yakiendelea huku muuaji akionekana ni mtaalamu wa hali ya juu. Alijiuliza muuaji ni nani? Kama kamuua hakimu kwa ajili ya kupindisha sheria na hao wengine vifo vyao vimetokana na nini? Kikiwepo cha mkewe na mwanaye kipenzi Gift?

Alijiapiza kuwa siku atakayomtia mikononi huyo muuaji ama zake au za muuaji. Alipofika nyumbani alikuwa amechoka akili na mwili, alijitupa kwenye kochi na usingizi mzito ukamchukua. 

 Anderson alishtuka usingizini majira ya jioni na kujiona amelala kipindi kirefu, muda uliobaki ilikuwa nusu saa akutane na vijana wake kumpa taarifa ya hakimu hiyo. Kama kawaida alikwenda kuoga na kubadili nguo tayari  kwenda ofisini.

Wakati anataka kutoka mkoba mweusi wa Malaika Mweusi ulimgusa na kuhisi kuna kitu cha muhimu kukiangalia kwenye mkoba wa binti anayeonekana mtoto wa tajiri. Aliangalia saa yake ilimuonyesha bado dakika ishirini akijua ni muda wa dakika tano hivi kwa mwendo wa gari atawahi ofisini.                                                                                                       Hamu ya kujua kuna nini katika mkoba ule ilimfanya kuupekua ili ajue kuna vitu gani. Aliamini huenda angegundua siri yoyote ya msichana huyo kutoka familia ya kitajiri. Kwa dakika kumi alijua zinatosha kufanya upekuzi wa haraka haraka.

Alipofungua pochi, ndani  alikutana na cheni isiyopungua thamani ya shilingi milioni moja na nusu na simu ya mkononi aina ya Sum sung yenye thamani ya shilingi milioni moja na laki saba, lakini ilikuwa haina line. Katika mfuko mdogo wa ile pochi alikuta kijitabu kidogo “note book.” 

Alikifungua na kuanza kukisoma karatasi moja baada ya nyingine, ilionyesha kuwa ni msichana mwenye miradi mingi ya mamilioni ya shilingi. Aliendelea kusoma karatasi za mbele alikutana na majina yameandikwa majina ya bluu.

Lakini asilimia kubwa ya majina hayo yalikuwa yamezungushiwa wino mwekundu na majina mawili tu ndiyo yalikuwa hayajazungushiwa wino  mwekundu. 

Majina yale yalimshtua moyo wake na kusababisha mwili kusisimka na jasho jembamba kumvuja juu ya paji la uso. Aliyarudia zaidi ya mara tano na jibu lilikuwa lilelile, alichokisoma machoni mwake kilikuwa sahihi.

Yalikuwa ni majina ya baadhi ya watu waliouawa katika matukio yaliyomchanganya akili  na kushindwa kumtambua muuaji. Mbele ya majina yale yalikuwa na tarehe sahihi ya mauaji yaliyofanyika. Ndani ya majina yale lilikuwepo jina la marehemu mama yake mzazi, siku na tarehe aliyouawa, japo mama yake alijua amekufa kwa ajali ya gari. 

Jina lingine lilikuwa la mdogo wake aliyeuawa kwenye mazingira ya kutatanisha. Mwili wake ulikutwa kwenye bwawa la mji machafu chuo kikuu. Pia tarehe ya kifo cha mkewe na mwanaye ilionekana siku moja na tarehe ilikuwa ileile. Kifo kilichomuuma sana na kumchanyanya akili.

Mkewe aliuawa kikatili kwa kuchunwa ngozi sehemu za siri na kisha kupigiliwa kipande cha mti. Kilikuwa kifo cha mateso makubwa, maiti yake ilikatwa ikiwa imelaliwa na mwanaye ikiwa inavuja damu mwili mzima.

 Vifo vya mkewe na mwanaye vilimuuma sana hasa alipouona mwili wa mkewe livyoharibika vibaya hasa sehemu za siri. Aliapa mbele ya ya mwili wa mkewe na mwanaye  siku ya kutoa heshima za mwisho kwamba atamfafuta muuaji na kumtia hatiani kwa mkono wake mwenyewe.  

Alijikuta katika mawazo mengi kuhusu kile kitabu cha majina na Malaika Mweusi kina uhusiano gani? Alijiuliza kama atakuwa amehusika na vifo vile au la. Hakukubaliana na akili yake kuwa Malaika Mweusi ndiye muuaji.

Alimuamini na kumwona ndiye atakayeziba pengo la marehemu mkewe hadi akafikia hatua ya kumtambulisha kwa wazazi wake ambao nao wakawapa baraka zote ili wafunge ndoa. 

Kile kitabu kilimchanganya sana akili yake, Mama yake kabla kifo chake alionyesha mapenzi mazito kwa Malaika Mweusi na alimsifia mwanaye kwa chaguo lake zuri la msichana mzuri mwenye tabia njema.

Alijikuta akisema kwa sauti: 

“Hapana haiwezekani Malaika Mweusi kuwa muuaji, lazima atakuwa anamjua muuaji, lazima nipate ukweli kupitia kwake.”

 Jasho lilikuwa linamvuja chapachapa kama aliyefungiwa kwenye chumba cheye joto kali. Aliendelea kusoma kitabu majina ya mwisho mawili yaliyobaki ambayo hayakuwa yamezungushiwa wino mwekundu. Katika majina hayo lilikuwepo jina la baba yake mzazi,  yalizidi kumchanganya, alijikuta akibwatuka:

“Ha! Na babaa, nooo..nooo.”

 Tarehe iliyokuwa  mbele ya jina la baba yake ilikuwa ni siku ileile, alisema tena kwa sauti:

“Hapana haiwezekani na baba tena, hapana.”

 Alitoa simu yake ya mkononi na kubofya namba ya baba yake ili kumjulisha awe makini kwani kifo kilikuwa kinamnyemelea. Lakini alipopiga ilikuwa inaita tu bila kupokelewa mpaka ikakatika. Alijikuta akitoka ndani kwa mwendo wa kuruka hadi katika gari lake na kuliondoa katika mwendo wa kasi mithili ya ndege za kivita kuwahi kwa baba yake. 

Ndani ya dakika tano alikuwa anaelekea kwa baba yake, aliiacha barabara kuu na kuingia ndogo inayoelekea kwa baba yake, mbele yake kulikuwa na gari limeharibika.

Kwa haraka aliteremka kwenye gari bila ya kuchomoa funguo wala kufunga  mlango na kuanza kukimbia kuelekea kwa baba yake. 

Njiani alikutana na mwanamke kama Malaika Mweusi, lakini hakumjali zaidi ya kuwahi kuokoa maisha ya baba yake. Nyumba ya baba yake ilikuwa giza, aliingia ndani ya geti na kwenda moja kwa moja hadi ndani. Alimwita baba yake kwa sauti ya juu, lakini hakukukuwa na majibu lolote. Sebule ilikuwa kimya pia  giza.

 Alipowasha taa alishangaa kukuta ukumbi mtupu hakukuwa na mtu yeyote, alielekea chumbani kwa baba yake. Mlangoni alikutana na michirizi ya damu lakini chumbani kwa baba yake kulikuwa na giza. Ile damu ilimfanya aione hali ya hatari mbele yake 

Alitoa bastola na kuingia kwa tahadhari kubwa alipapasa ukutani na kufanikiwa kuwasha taa. 

Hakuamini macho yake, alishuhudia mwili wa baba yake ulikuwa umelazwa kitandani ukiwa mtupu kama alivyozaliwa. Sehemu zake za siri zilikuwa zimetenganishwa na kisu kilikuwa kimemchoma katikati ya moyo wake, macho yalikuwa yamemtoka akionyesha amekufa kwa mateso makali.

Damu ilikuwa mbichi na mwili wake ulikuwa bado una joto. Chumba chote kilikuwa kinanuka damu mbichi. Anderson aliuvamia mwili wa baba yake na kuukumbatia huku akiendelea kuapa atamshikisha adabu aliyetenda kosa lile.

Alitoka harakahara ili aanze msako wa Malaika Mweusi ili apate ukweli a vifo vyote. Lakini alikataa katakata muuaji anaweza kuwa Malaika Mweusi. Kwa vile nguo zake zilikuwa zimetapakaa damu ya baba yake alipapigia simu vijana wake waje kuchukua mwili wa marehemu baba yake kuupeleka hospitali.

 Akiwa njiani aliwaza sana uhusu vifo vyote hasa vinavyoihusu familia yake kama wameuawa wote aliyebaki ni yeye na kama asipomuwahi muuaji basi atamuua yeye. 

“Hivi Malaika Mweusi anaweza kuwa muuaji?.....inawezekana maana nimemuona eneo la tukio sasa hivi, kwani ana siri gani inayomfanya afanye hivyo?” Mr. Anderson alijikuta akizungumza peke yake. Hakuamini mtu aliyemuamini na kumbatiza jina la Malaika Mweusi awe muuaji, kama ni kweli alihusika hakuwa Malaika Mweusi bali Shetani Mweusi. 



                                           *******

Alianza kukumbuka siku ya kwanza walipoanza kufahamiana na Malaika Mweusi ilikuwa ni siku ambayo alikuwa amechanganyikiwa kutokana na zaidi ya miezi miwili kutokutulia nyumbani kutokana na mfululizo wa matukio ya vifo vya watu kila kukicha watu waliuawa na muuaji hakuonekana. 

Kwanza yalikuwa mauaji ya mzungu mmoja aliyekuwa msimamizi wa uchimbaji wa madini. Kabla hajajua kinachoendelea vikatokea vifo vya kutisha vya wazungu wengine sita ambao waliuawa kinyama kwa kupigwa risasi nyingi miilini. Hali ile ilitishia jiji na kufanya kikosi cha upelelezi na jeshi zima la polisi uwa katika wakati mgumu wa kuhangaika huku na huko kuwasaka wauaji wenye mbinu za kijasusi.

Kutokana na kuwa bize katika suala la kutafuta muuaji usiku na mchana bila mafanikio hali ilimfanya Anderson kutokuwa karibu na mkewe. Kitendo cha kutolala kila siku nyumbani na mkewe na kutopata muda wa kuzungumza, kwa muda mwingi, kuwa bize na shughuli za serikali. Hali iliyosababisha mkewe amjie juu na kumuomba achague moja kazi ama mke.

Pamoja na kumwambia mkewe umuhimu wake kwa taifa lake, kuwa yeye ni mtumishi wa watu. Lakini mkewe hakumuelewa na kutishia  endapo ataendelea hivyo basi yeye atarudi nyumbani kwao.

 Anderson alifikiri kuwa ni utani, siku moja aliporudi kutoka kwenye msako wa muuaji hakumkuta mkewe alikuwa amerudi kwao, alijikuta amechanganyikiwa. Muuaji hakumtia mkononi na mkewe ndio amekimbia na alipokwenda kwao alimkatalia katakata huku akimwuliza:

“Huyo muuaji ameshampata?”

“Bado.”

“ Kama bado unanifuatia nini?”

“Sikiliza mke wangu muuaji na ndoa yetu ni vitu viwili tofauti kila kitu kina nafasi  yake.”

“Kwa hiyo muuaji amechukua nafasi zote au sio? Basi mimi nakuachia umsake huyo muuaji ni mtu mwenye mbinu za hali ya juu hivyo kumtia mikononi ni vigumu itachukua muda mrefu.” 

“Mimi kurudi nyumbani sitaki chagua moja uachane na kazi hiyo ya kumsaka muuaji au la mimi niendelee kubaki nyumbani.”

“Mke wangu elewa kazi ndiyo inayotuweka mjini, sasa nikiacha unataka tukae tunatazamana, tutakula mawe?”     

"Ina maana hiyo kazi nzito umeanza leo, tuna miaka minne sijaona kitu kama hicho basi watu wote walioolewa na watu kama ninyi hawafurahii maisha ya ndoa?”

“Hapana mambo haya hutokea kwa msimu hivyo nivumilie.”

“Siwezi, we endelea sijakuzuia, najiona sina tofauti na mlinzi wa nyumba, mara simu ililia Anderson alilipokea ilikuwa inamjulisha kifo cha meneja wa wa kampuni ya mafuta jijini ambaye amekutwa ofisini kwake.

Anderson alijikuta katika kipindi kigumu, alijiuliza atamwelezaje mke wake juu ya ujumbe alioupata muda ule. 

“Unashangaa shangaa nini?” Mkewe alimuuliza.

“Aah! Kawaida.”

“Wee nenda,” mkewe alisema baada ya kuigundua simu ilikuwa ya kazi. 

“Sawa….. sasa tutaongea vizuri nikirudi mpenzi.”

 “Sawa, lakini hakikisha unampata muuaji ama sivyo uzi ni uleule, bai,” mkewe alimuaga huku akishikilia msimamo wake.

Anderson aliingia katika gari na kuelekea eneo la tukio, alijikuta katika kipindi kigumu maishani mwake toka atoke tumboni kwa mama yake. Kazi aliipenda ndiyo inamfanya aitwe mwanaume na mkewe vile vile anampenda ni zaidi ya kazi kwani ndiye pumbazo la moyo wake suruhisho la mawazo yake. 

Ule usemi wa mwili mmoja wa mke na mume, mkewe Sarah aliudhinisha kwani alikuwa mshauri mwema wa mumewe. Alimlea kama mwanawe na mtoto wao wa kike Gift. 

Hali ya mkewe kubadilika ilimchanganya, alikuwa na haki ya kulalamika, mwezi wa pili hajalala ndani kwa kusaka muuaji. Heri angempata kuliko kuwa kama anazurula bila mpango.

Anderson alifika kwenye eneo la tukio kwenye ofisi moja iliyopo katikati ya jiji, alikuta umati wa watu wengi. Alijipenyeza katikati yao na kukutana na kijana wake walipanda juu ya ghorofa ya tatu.

Waliingia na kumkuta mtu mmoja mwenye umbo kubwa aliyevaa kinadhifu akiwa amelalia meza akitokwa na povu lililochanganyika na damu. Walimnyanyua na lile povu liliochanganyika na matapishi yenye damu lilichuruzika chini ya meza.

Anderson baada ya kumchunguza yule mtu aliwaamuru vijana wake kumpeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi. Alimchukua secretari wa meneja aliyeuawa, na aliondoka naye kwa mahojiano zaidi.

Walipofika ofisini alikuwa na mahojiano mafupi na secretari.

“Binti una muda gani katika ofisi ambayo imetokea mauaji?” 

“Ni mwaka na miezi mitano sasa.”

“Unazifahamu vizuri tabia za bosi wako?”

“Kuzifahamu kivipi?”

“Yaani muundo wa maisha yake kwa ujumla.”

“Si sana.”

“Nieleze unavyomfahamu.”

“Bosi ni mtu mpole, mcheshi na alikuwa anajali wafanyakazi wote tulio chini yake.”

“Unaweza kunieleza kifo cha bosi wako kimetokana na nini?”

“Kwa kweli sijui.”

“Ni nani aliyegundua bosi wako ameshafariki?”

“Mimi.”

“Uligundua kivipi?”

“Wakati nampelekea kahawa kama ilivyo kawaida yake, muda ukifika ni lazima nimpelekee. Nilishangaa kumkuta bosi kalalia meza na povu lililochanyanyika na damu lilimtoka mdomoni.”

“ Baada ya kuona hivyo ulifanya nini?”

“Nilipiga kelele ya woga iliyowafanya wafanyakazi wenzangu waje kuangalia kuna nini, ndipo ilipojulikana kuwa amefariki na kuamua kujulisha chombo cha usalama.”

“Ni nani aliyeingia ofisini kwake kwa mara ya mwisho?”

“Mmh! Sina uhakika sana…Aaaha,  sawa ni msichana mmoja hivi.”

“Unamkumbuka sura yake?”

“Hapana alikuwa amevaa hijabu iliyomfunika uso na alikuwa akizungumza lafudhi ya Kiunguja.”

“Alichukua muda gani?”

“Mmh! Sina kumbukumbu sidhani kama alitoka, maana nina uhakika sikumuona akitoka. Hata muda wa kumpelekea kahawa nilijua bado yupo nilibeba vikombe viwili, ajabu sikumkuta na kukuta bosi katika hali kama vile nilivyoeleza.” 

“Unadhani ni muda gani alipita toka yule msichana aingie na wewe kupeleka kahawa?”

“Zaidi ya saa tatu.”

“Saa tatu! Mazungumzo gani ambayo hukuyatilia wasi wasi?”

“Saa tatu mbona ni chache, huzungumza na wateja zaidi ya saa sita.”

“Sawa, unaweza kwenda lakini uwe tayari muda wowote tunakuhitaji.”

“Sawa muheshimiwa,” yule secretari aliruhusiwa kuondoka. 

Anderson aliongozana na baadhi ya vijana wake kuelekea hospitali kwa ajili ya majibu ya kifo cha meneja. Alipofika alipata maelezo kuhusiana na kifo cha meneja wa kampuni ya mafuta. Dokta alimweleza kuwa kifo cha meneja kimetokana na kupuliziwa dawa ya sumu iliyoharibu mapafu na kifua.

Kwa mara ya kwanza Anderson aliona kazi ya upelelezi ni ngumu, kumtafuta mtu asiyemjua na mtu mwenyewe awe na ujuzi wa hali ya juu anayefanya mauaji yake kwa mpangilio wa hali ya juu. Wakati anatoka hospitali alikuwa ni mwingi wa mawazo juu ya mauaji yale alijiuliza maswali yasiyo na majibu.

“Kwa nini muuaji ameamua kufanya vile, lazima ipo sababu  yake au ndiyo kiasasi? Na kama kisasi kwa nini asitoe taarifa kwenye vyombo husika ili wabaya wake wakamatwe na kufunguliwa mashtaka? Mbona mauaji yenyewe yanachanganya? Mmh! Kazi ya upelelezi ni ngumu kumtafuta mtu usiyemjua inawezekana kabisa anakufahamu na kula naye meza moja. 

Mmh! Kweli huu ni mwaka wangu, muuaji ananichanganya na mke wangu aishi vituko vinavyotishia maisha ya ndoa yangu. Kitu kisichowezekana eti niamue kuacha kazi  tutakula mawe?”

Anderson anazidi kuchanganyikiwa, ili kutuliza mawazo aliamua kuingia katika ukumbi mmoja wa starehe wa Puzzo Hill Hotel na kutafuta meza moja ya pembeni mwa ukumbi uliokuwa umejaa watu. Lakini kuna meza moja ilikuwa tupu watu ndiyo kwanza walikuwa wamenyanyuka.

Alipoketi kitini alionekana mtu mwenye mawazo mengi, mikono ilikuwa shavuni. Hata mhudumu alipofika kumsikiliza mbele yake hakumuona. 

“Samahani kaka nikusaidie nini?”

“Ooh! Samahani dada yangu nilikuwa mbali nisaidie safari mbili.”

”Sawa kaka yangu punguza mawazo, kama huna kampani mimi nipo kwa ajili yako.” 

“Asante dada yangu nitakapohitaji nitakujulisha.” 

Yule mhudumu alifuata bia huku sehemu zake za nyuma akizitingisha, naye hakuwa haba Mungu alimjalia. Anderson aliyekuwa katikati ya mawazo hakukiona alichokifanya muhudumu yule. Baada ya kumuagiza alizama tena ndani ya dimbwi la mawazo kwa kurudisha mikono yake shavuni.

“Samahani mpenzi kinywaji hiki,” mhudumu alishtuka zaidi ya mara mbili, Anderson alizipiga zote mbili kama tarumbeta kisha akaagiza nyingine mbili. Nazo alizipiga kama tarumbeta zilipofika sita aliagiza nyingine mbili ambazo alikunywa taratibu muda huo sasa ulikuwa majira ya saa moja usiku.

                                                                 ***

 Anderson aliamka siku ya pili yake na kugundua sehemu alipolala si nyumbani kwake ilikuwa sehemu ngeni. Alipepesa macho yake, alishtuka kuona pembeni yake amelala binti mwenye urembo wa shani. Kama yule binti angekuwa mweupe na uzuri ule basi angejua ni jini. 

Binti aliyelala pembeni yake alikuwa na uso wa kitoto yaani ‘baby face’. Alikuwa amepitiwa na usingizi wa fofofo, Anderson alianza kujiuliza: 

“Hapa ni wapi?” 

Alipepesa macho yake na kugundua pale ni nyumba ya wageni, alijiuliza amefikaje pale, kutoka  alipofunga ndoa na mkewe hajawahi kulala nje, pasipokuwa na sababu za kikazi wala kuwa na uhusiano na mwanamke yeyote zaidi ya mkewe mama Gift.

Alijiuliza yule mwanamke ni nani mbona hamtambui ilibidi avute hisia za jana ilivyokuwa. 

“Mmh! Jana nilipotoa hospitali nilikwenda Puzzo Hill Hoteli..Ehe nimekumbuka, niliagiza vinywaji.. eeh.. sawa.. aliingia msichana aliyeushtua moyo wangu aliyekuja moja kwa moja ahadi kwenye meza yangu na kuniambia nikae naye.

”Oooh sawa nilimkubalia na kuanza kunywa pamoja, mmh nina imani hapo ndipo mwisho wa kumbuumbu zangu. Lakini kilichoendelea sikujua cha kushangaza nimeshituka alfajili hii na kujikuta nipo hotelini na mtu nisiyemjua wala kuwa na uhusiano naye.

“Hizi pombe sasa zinanipeleka pabaya Mungu wangu! Sijui nimefanya nae ngono? Na  kama nimefanya sijui kama nimetumia kinga huu ndiyo mwanzo wa kuambukizwa ukimwi.”

“Vipi umeamka zamani,” Sauti tamu mithili ya kinubi cha mtume Daudi alichotumia kumbembeleza mfalme Sauli, ilipenya wenye ngoma za masikio ya Anderson na kumfanya alishtuka kutoka kwenye lindi la mawazo. 

“Eeeh!”

“Pole sana kaka yangu, inawezekana kuna jambo linakutatiza lililokuchanganya akili yako, tena si dogo ni kubwa,” alisema yule binti huku akitambaza mikono yake laini mgongoni kwa Anderson.

Habari zile zilizidi kumchanganya ilibidi amuulize yule binti kwa ukali.

“Hizi habari zangu umezijuaje? Wewe ni nani na hapa ni wapi na nimefikaje?”

 “Aah! Kaka yangu unaniuliza kwa ukali hivyo au wema wangu kwako umekuwa mbaya? Basi nisamehe kwa wema wangu.” 

Kauli tamu ya binti mrembo ilimfanya Anderson kuwa mpole. 

“Samahani dada yangu, sikuwa na nia hiyo kauli yangu imekuwa kali naomba nisamehe kwa hili.” 

“Basi kaka yangu jana nilipoingia ukumbini, sehemu zote zilikuwa zimejaa watu ila meza uliyokuwa umekaa peke yako ilikuwa na nafasi ndipo nilipokuja kukuuliza kama una mtu ulinijibu kuwa uko peke yako kwa sauti ambayo ilionyesha umeshaanza kulewa.

“Tulijumuika pamoja na tukaanza kunywa kwa pamoja huku ukinikataza nisilipe utalipa wewe. Tulipokuwa tukiendelea kunywa ulionekana ni mtu mwenye mawazo mengi. Ilikuwa haipiti dakika mbili lazima ujifyonye na kila nilipokuwa nikikuuliza, ulinijibu we acha tu.

“Sikujua una maswahibu gani kilichonishangaza zaidi ni unywaji wako wa pombe wa kupita kiasi. Hata nilipojaribu kukukataza ulinikaripia nikuache la sivyo utanifukuza.”

“Nilikuacha unywe utakavyo, ukinywa mpaka ukawa ujielewi na kulala juu ya meza, nikawa sina jinsi siwezi kukuacha peke yako unaweza kuiibiwa na vibaka vitu vyako si unajua jinsi vibaka wanavyo watamani walevi. 

“Ilibidi nikunyanyue kwa shida mpaka nje kwenye gari lako, kwani nilikuwa nalijiua wakati unateremka garini nami nilikuwa naingia. Nilipokupapasa nilikukuta na funguo ya gari na pesa shilingi laki mbili na ishirini. Nilikukokota hadi kwenye gari na kukupeleka sehemu ambayo utapumzika kwa amani hadi asubuhi hii uendelee na shughuli zako.”

“Mmh! Siamini wewe ni msichana wa ajabu hii ni hoteli gani na gari langu liko wapi?”

“Hapa ni Biski Hill Hotel, Hoteli ya kitalii iliyo pembeni mwa bahari yenye ufukwe mwanana na gari lako lipo salama kwenye maogesho ya magari ya hoteli hii.”

“Siamini wewe ni kiumbe wa ajabu lazima nilipe fadhila zako.”

“Hapana sikukutendea wema ili unilipe fadhila, bali ni msaada kama msamaria mwema.”

“Sawa, suruali yangu ipo wapi?”  Mr Anderson aliuliza.

 Yule msichana alimletea, aliingiza mkono mfukoni na kuhesabu fedha zake na kuzikuta sawasawa pia simu yake ilikuwemo, alichukua laki moja na kumpa yule msichana kama asante. 

“Hapana kaka yangu ukinipa siku nyingine nitachukua siyo leo.”

Wakati huo yule binti alikuwa akinyanyuka kutoka kitandani na kuelekea bafuni kuoga alipotoka bafuni alivaa nguo zake na kumuaga.

“Samahani kaka wacha nikuache uendelee kupumzika,” yule binti aliupitia mkoba wake ili aondoke, Anderson alitaka kumfahamu vizuri. 

“Samahani mrembo, unaitwa nani?”

“Naitwa Teddy”.

“Ooh! Jina zuri kutokana na vitu ulivyonitendea sina budi kukubatiza jina lingine.”

“He! Lipi tena hilo?” 

“Nakuomba nikuite ‘Black Angel’ Malaika Mweusi.”

 “Sidhani kama ninalingana na hilo jina,” Teddy alisema huku akibinua midomo kike.

 “Siku zote kioo cha kujifahamu ni yule aliye pembeni yako wewe mwenyewe hata siku moja huwezi kujijua,” Anderson alisema huku akimtamaza yule binti.

 “Nakushukuru kwa jina hilo, langu umelijua sijui wewe unaitwa nani?”

“Naitwa Anderson.”

 “Nakushukuru kaka yangu kwa kulijua jina lako, nilikuwa na hamu ya kujua nini kilichokusibu lakini muda hauniruhusu ila siku yoyote Mungu akijalia tutaonana.”

 ”Hapana Malaika wangu, nina mengi ya kuzungumza kila nikikuangalia  sipati jibu. Hivyo nakuomba jioni ya leo tukutane Puzzo hoteli.”

”Sawa basi tukutane saa 12:00 jioni tuwe na ahadi za uhakika japokuwa wengi wanakasumba kusema za kizungu, ina maana mzungu akichelewa atakuwa na ahadi za Kiswahili?”

“Inaonekana u muelewa sana, kwa kugundua kasumba iliyotutawala wengi.”

 Anderson aliagana na Mailaka Mweusi, alipotaka kumsindikiza alitakataa. 

“Kwa nini nisikusindikize?” Anderson alihoji.

“Hapana usisumbuke kuna usafiri hapo nje unanisubiri,” Malaika Mweusi aliondoka na kumwacha Anderson bado akiwa kitandani amejifunga shuka.

Baada ya Malaika Mweusi kuondoka Anderson alibakia na maswali mengi kichwani juu ya msichana yule aliyetoka muda  mfupi na kukiacha chumba kikinukia manukato ya bei mbaya. Alimshangaa yule msichana alikuwa wa aina gani, wasichana wengi jijini hujiuza ili kujikimu na ugumu wa maisha. Lakini ilikuwa tofauti na tena kwa tofauti kubwa. Alikuwa na uwezo wa kuchukua kila kitu hata gari, lakini kila kitu amekikuta kipo katika hali nzuri, ilikuwa ajabu kubwa kwake.

Aliomba jioni ifike haraka ili aweze kuonana na binti wa ajabu aliyemfananisha na Malaika Mweusi. Aliona hakuna muda wa kuendelea kuwa pale alinyanyuka na kwenda bafuni kuoga ili akirudi nyumbani kubadili nguo ili aingie ofisini kumtafuta muuaji ambaye ameichanganya akili yake kila kukicha na bila ya kumsahau. 

Mke wake aliyempa masharti ya kutorudi nyumbani mpaka awe amempata muuaji sharti lililompa wakati mgumu. Lakini vitu alivyofanyiwa na Malaika Mweusi vilimpunguzia mawazo yake aliyaelekeza kwake alimuona ni msichana wa ajabu.

Kutwa nzima alifanya kazi lakini akili yake yote ilikuwa kwa Malaika Mweusi msichana wa ajabu ambaye akuwahi kumuona katika maisha yake yote. Ilipotimu saa kumi jioni alirudi nyumbani alijiandaa kwa ajili ya kukutana na Malaika Mweusi.

 Anderson alivalia nguo zenye hadhi ya juu na kujipulizia pafyumu ya bei mbaya ambayo huitumia mkewe ili aonekane mtu wa hali ya juu. Alijitazama kwenye kioo na kujiona amependeza kwani nguo zilikuwa zimemkaa vyema, alitazama saa yake ya ukutani iliyomuonyesha ni saa kumi na moja na robo alijua muda ule utamtosha kufika Puzzo Hoteli.

Alikwenda kwenye banda la gari na uchukua gari lake tayari kwenda Puzzo Hoteli kwa ajili ya kuonana na Malaika Mweusi binti wa ajabu ambaye alimfanya asiamini kama kweli aliyoyafanya  yanatendeka katika dunia ya sasa ambayo asilimia kubwa ya akina dada wamekuwa na roho ya kinyama. 

Kwa hali aliyomkuta angeibiwa kila kitu ikiwa pamoja na gari lake. Majira ya saa kumi na mbili kasoro dakika tano aliwasili eneo la Puzzo Hotel, alipepesa macho yake huku na kule ili atafute sehemu nzuri ya kuegesha gari lake na baada ya muda aliiona sehemu nzuri ya kuegesha gari lake. 

Akiwa katika harakati za kupaki gari lake mara gari dogo aina ya Mitsubishi Pajero nyeusi ilipita na kwenda kusimama mbele yake, akiwa anasubiri lile gari limpishe aliteremka binti mrembo katika lile gari.

 Anderson alijikuta anapigwa na bumbuwazi na woga wa kumtawala alijikuta akijisemea moyoni. Yule msichana alipiga hatua za alipiga hatua za taratibu kwenda alipo.

 Ile ilimpa nafasi ya kumsoma vizuri yule mrembo sura na umbile lake alianza kumwangalia toka nywele zake za rasta ndogondogo zilizoishia mgongoni na usoni alivaa miwani ndogo ya mviringo iliyobebwa na pua ndogo ya kitusi, midomo yake midogo ambayo ilionekana kama iliumbwa kwa matumizi ya vitu laini na vinywaji baridi. 

Akiwa bado anamkazia macho  yule msichana aliyekuwa amemuelekea alikutana na tabasamu lililozidisha uzuri wa binti aliyekuja mbele yake ambaye alionesha kama anamfahamu lakini kwake alikuwa mgeni.

Lilikuwa tabasamu tamu lililonakshiwa na mwanya mwembamba lililopoteza mawasiliano katika ubongo wa Anderson. Yule msichana alikuwa amevalia brauzi cha rangi ya jani la mgomba iliyoishia juu ya kitovu na kuliacha tumbo lake dogo wazi kidogo, chini alivaa sketi yenye rangi kama kiblauzi iliyoishia kidogo juu ya makalio kutokana na kupasuliwa kwa nyuma na nyuma alikuja amejaaliwa kiasi hakika mwenyezi Mungu alimpendelea kwa kila kitu. 

Shingoni alikuwa na cheni tatu za dhahabu hesabu ya haraka haraka zilikuwa na thamani ya milioni mbili kasoro, masikioni kila sikio lilitobolewa matundu matano na kila tundu lilikuwa na hereni ya dhahabu, vidoleni kila kidole kilikuwa na pete ya dhahabu ya miundo tofauti mkono mmoja ulikuwa na bangili ya dhahabu na mwingine ulikuwa na saa ndogo vilevile ya dhahabu, mdomo ulikuwa na meno mawili ya dhahabu.

 Tabasamu ya yule binti nusra lisimamishe mapigo ya moyo katika mwili wa Anderson. Akiwa bado ameshangaa kama kaona meli barabarani yule binti mrembo alipita upande wa pili wa mlango wa gari la  Anderson na kufungua mlango baada ya kuingia alifunga mlango.

 Aliona kama yupo ndotoni baada ya kuona ule mlango unafunguliwa na yule msichana mwenye uzuri wa ajabu aliyevaa vitu vyenye mamilioni ya pesa. 

“Eeeh…unataka lifti?’ Aliuliza huku akimtupia jicho la wizi.

“Anderson vipi?” yule msichana alisema kwa sauti tamu na laini. “Unasemaa….Umejuaje jina langu?” Anderson alimshangaa yule mrembo.

“Unanitania au unasema kweli?” binti mrembo aliuliza.

 “Si utani, we nani na umejuaje jina langu?”

 “We umekuja kukutana na nani hapa?”

 “Swali lile lilimshtua Anderson alituliza akili na kumuangalia yule binti aliyekaa pembeni yake ambaye kipindi hicho alikuwa amevua miwani yake. Taratibu sura yake ilianza kumjia na kugundua ni Malaika Mweusi lakini huyu ni mzuri mara dufu lakini harufu ya manukato yalimfanya abahatishe.

 “Ina maana wewe ni Malaika wangu?”

“Ndio mimi wala si mwingine,” Malaika alijibu huku akilegeza sauti. 

“Umebadilika kwa asilimia mia.” 

“Si kweli, sura na umbile lilelile kilichobadilika ni mavazi.”

 “Malaika Mweusi umependeza sana, hongera sana unastahili pongezi zangu.”

“Nashukuru, sasa ni hivi geuza gari tuelekee tulipolala jana, ni sehemu inayofaa kwa mazungumzo,” Malaika alimweleza   Anderson.

 Anderson aligeuza gari na kwenda Biski Hoteli, waliposhuka Biski Hoteli walikwenda moja kwa moja hadi mapokezi. Chumba kimoja kilikuwa laki mbili na nusu moja za Kitanzania. Mr Anderson aliingiza mkono mfukoni ili atoe malipo ya chumba lakini Malaika Mweusi alimkataza.

 “Hapana nitalipa mimi,” Malaika Mweusi alifungua mkoba wake na kutoa noti kumi za kumikumi na kulipa. Walipewa chumba kimoja chenye kila kitu, walipoingia chumbani Malaika Mweusi alikaa kitandani na Anderson alikaa kwenye sofa. Malaika Mweusi alihama kutoka kwenye kitanda na kumsogelea karibu na Anderson, wakati huo Anderson alionekana mtu mwenye mawazo mengi. 

“Vipi Mr Anderson naona uko mbali?”

 “Ha…ha..pana tuko pamoja.” 

“Nina imani huu ni muda mzuri wa kuzungumza lililokusibu jana,” Malaika Mweusi alisema huku akitembeza kikono yake kwenye kifua cha Mr Anderson.

“Halina umuhimu sana tuachane nalo.”

 “Hapana Anderson nipo hapa kwa ajili yako nimeacha kazi zangu naomba ujali muda wangu na pia ni muhimu mimi kuwa hapa,” Malaika Mweusi alisema kwa msisitizo. Anderson hakupenda mambo yake yatoke nje wala siri ya kazi yake. Akabaki katikati ya mawazo, Malaika Mweusi alimstua.  

“Mr. Anderson naona huna la kuongea?” Malaika Mweusi alinyanyuka na kutaka kuondoka. 

“Hapana usiondoke na nitakueleza,” Anderson alinyanyuka na kumshika mkono Malaika.

Wakati huo Malaika Mweusi alikuwa ameshachukua mkoba wake ili aondoke,  Anderson alimshika mkono na kumrudisha kwenye sofa. 

“Samahani Malaika wangu sina nia ya kukuudhi bali linataka maelezo ya kina.” 

“Ndio maana nikaamua kuondoka kwa vile sina msaada kwako wala umuhimu wowote,” Malaika alijibu kwa hasira kidogo.

“Hapana Malaika wangu sina maana hiyo wewe ni mtu ninaye kuona una umuhimu wa kipekee kuliko hata hao niliokuwa nao muda mrefu. Wewe kwa ufupi inaonyesha jinsi gani unanijali sina budi nikueleze kilichonisibu.

“Usinieleze kwa kukulazimisha haitakuwa vizuri bali kwa hiari yako.”

“Nitakuelewa kwa hiyari yangu.”

“Haya nieleze.”

Anderson alimweleza masahibu yote yanayomzonga ubongo wake hadi hatua ya kuichukia dunia na kujuta kwa nini amezaliwa mwanaume. Alikuwa amechanganywa na mauaji yaliyokuwa yakitikisa jiji kwa takribani miezi miwili na nusu. Akiwa katika mtihani mzito wa kumsaka muuaji mkewe naye alimjia juu kwa kitendo cha kukosekana nyumbani usiku na mchana na muuaji haonekani kila moja lilimchanganya sana.

“Nashindwa Malaika wangu nifanye nini, muuaji amenichanganya akili nyumbani nako mke wangu anazidi kunichanganya ati niache kazi, unafikiri nitakuwa mgeni wa nani utaishi vipi bila kazi?” Anderson kwa mara ya kwanza alijikuta anitoa siri ya kazi yake kosa lilikuwa kubwa kumuamini usiyemjua.

Malaika Mweusi baada ya kumsikiliza kwa kina alimsogelea Anderson aliyekuwa ameweka mikono shavuni akionesha wazi kuwa amekosa ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwa mbele yake.

Malaika Mweusi aliuweka mkono wake mgongoni kwa Anderson na kuongea kwa sauti yake tamu mithili ya kinubi cha mfalme Daudi, aliongea kwa sauti ya chini:

“Pole sana Anderson kweli mzigo uliokuwa mbele yako ni mzito sana unahitaji msaada mkubwa... sasa ni hivi….”




Malaika Mweusi alizungumza huku akimpapasa Mr Anderson shingoni na kumfanya asisimke huku aliendelea kuzungumza:

“Ni hivi suala moja nitajaribu kulitatua lakini jingine liko nje ya uwezo wangu.”

“Lipi hilo?”

“La mkeo.”

 “Utanisaidiaje?” Anderson aliuliza huku akigeuka kumtazama Malaika aliyeonesha hana wasiwasi.

“Unajua siku zote kila kitu kina nafasi yake, kazi ina nafasi yake na mkeo ana nafasi yake vilevile, kwa hiyo unaweza kupanga muda wako vizuri tu. Utashangaa kazi inakwenda na huku ukifurahia maisha yako ya nyumbani kama kawaida.

“Lazima uelewe kutokana na ugumu wa kazi yako lazima mwezi wako awe pozeo la yote yanayokuchanganya siku nzima,” Malaika alisema kwa sauti ya upole.

“Ungekuwa wewe ungefanyaje?” Anderson aliuliza akitegemea msaada wa Malaika.

“Swali zuri, ningekuwa mimi tena una nafasi ya juu wewe ndio top kuanzia asubuhi unadili na kazi za serikali lakini jioni unakuwa na mamaa ili kupoteza akili kwa ajili ya kupanga mikakati kwa kazi inayofuata. 

“Ni wazi inaichosha sana akili yako huna muda kuiacha akili yako ipumzike kwa kufurahi na mkeo na mwanao, kitu kitakacho kufanya usahau matatizo ya mbele.”

“Sawa kuna matatizo yanatokea usiku unafikiri nitaacha kwenda?”

“Matukio ya usiku ni siku moja moja lakini imekithiri na kuwa kero kwenye ndoa hata mimi nisingekubali miezi miwili na nusu unanusa nyumbani na kuondoka mkeo ana haki, ni kweli kabisa unaweza kuzipunguza kazi zisizo na umuhimu.

“Haya tangu tuanze kumtafuta muuaji hata fununu yake hujaipata  zaidi ya kujigeuza walinzi wa sungusungu.’’ Malaika alisema kwa utulivu tofauti na umbile na umri wake.

“Nimesikia nitajaribu.’’

“Si kujaribu anza kutekeleza sasa, mfuate mkeo ikiwezekana ukitoka hapa mweleze kama nilivyokueleza nakutakia muafaka mwema. Ila  suala la kumpata muuaji hilo lipo nje ya uwezo wangu, nina imani umenielewa?”

“Nimekuelewa Malaika wangu nitatekeleza yote uliyonieleza.”

Kwa vile muda ulikuwa umekwenda, Anderson na Malaika Mweusi waliongozana na kutoka nje ya Hotel ili kurudi mjini.

“Naomba nikupeleke kwako.”

“Hapana we nenda tu, mimi nina usafiri wangu nitafika sasa hivi ila mwisho wa wiki tukutane nijue umeutumiaje ushauri wangu.”

Anderson na Malaika Mweusi waliagana ilikuwa ni majira ya saa mbili usiku. Aliamua apitilize moja kwa moja hadi Sinza kwa mkewe mama Gift ili warudi nyumbani.

Alipofika alimweleza mkewe jinsi atakavyoutenga muda wake wa kazi na muda wa kukaa na familia yake kama alivyoelezwa na Malaika Mweusi. Mkewe alimjibu:

“Kama itakuwa hivyo mimi sina kipingamizi ila ukienda kinyume na haya unayonieleza basi nikiondoka tena usinifuate, sawa umenielewa?”

“Ndiyo mke wangu.”

Alimchukua mke wake na kurudi naye nyumbani Mikocheni walipokuwa wakiishi na familia yake.

                                                           ****

  Anderson alijitahidi kupanga muda wake wa kazi na wa kukaa na familia yake, kitu kilichorudisha upendo katika nyumba yake kama zamani. Alizidi kumuona Malaika Mweusi kiumbe cha ajabu kutokana na uwezo mkubwa wa kutatua tatizo lililokosa ufumbuzi kwa watu aliowaamini wenye busara.

Hakuamini msichana mdogo kama yeye kuwa na moyo wa busara na huruma uliojaa upendo, alipanga siku atakayokutana naye tena lazima ampe zawadi kubwa. 

Alipanga zawadi gani itakayolingana na wema wake ambayo amgeiona nzuri kwake. Kumpa pesa ingekuwa utani kutokana na yule mwanamke kuonesha ana uwezo mkubwa kuliko yeye pengine mara kumi yake, aliamua kumuuliza mwenyewe anahitaji zawadi gani toka kwake.

 Ilikuwa siku ya jumapili walikutana pale Puzzo Hoteli na kuongozana wote hadi Biski Hoteli. Wakiwa njiani kuna kitu kilikuwa kinagonga kwenye gari kila lilivyokuwa likienda kitu ambacho kilimkera Malaika Mweusi akabidi aulize:

“Anderson nini kinachogonga chini ya gari?”

“Aah! kuna matatizo kwenye Propela shafti.”

“Kwa nini usipeleke gereji?”

“Ugonjwa wake ni pesa nyingi kidogo na sasa sina pesa nasubiri mwisho wa mwezi.”

“Kwani kiasi gani?”

“Ni pesa nyingi kwani kuna spea mpya inatakiwa kununuliwa na matengenezo yake ni kama laki nne kasoro.”

“Sawa,” Malaika Mweusi alimjibu na kukaa kimya hadi walipofika Biski Hoteli. 

 Anderson kwa kuwa aliona hakukuwa na kitu kingine zaidi ya mazungumzo tu ya kawaida hakutaka kupoteza pesa kwa kuchukua chumba alionelea bora waongelee palepale kwenye gari au waende kwenye mchanga na kuzungumza.

“Kwani tatizo ni nini kama ningekuwa sina uwezo wa kulipia chumba nisingekueleza tuje huku,” Malaika alipingana naye.

“Hapana pamoja na hayo mimi naona maongezi yetu hayana haja sana ya kuongelea chumbani bora kama tungekuwa wape..,”  Anderson hakumalizia.

“Nimekuelewa vizuri sana pengine labda kukushinda wewe mwenyewe lazima uwe mwelewa siku zote, ila samahani kama kauli yangu itauudhi. Wewe ni mume wa mtu sipendi kutia dosari ndoa yako ndio maana nachukua chumba ili tuongee kwa mapana zaidi.”

“Huoni kuwa ni pesa nyingi  unazitumia bila sababu?”

“Pesa kazi yake ni matumizi ndio maana zinatafutwa ili zitumiwe, pesa kwangu si tatizo au ushanichoka sema tu usipindishe pindishe maneno kama safari ya nyoka?” Malaika alimuuliza akiwa amemkazia macho.

“Malaika wangu sina maana hiyo bali lazima nami nionyeshe ni jinsi gani ninavyokujali hata katika matumizi yako au hupendi ushauri wangu?” Anderson alimuuliza kwa sauti ya upole.

“Hapana, nauhitaji sana kwani umenizidi vitu vingi sikupati hata kimoja moja lakini hili halina tatizo na suala kuwa wapenzi mbona sisi ni wapenzi, siku zote hakuna urafiki bila kupendana sisi ni marafiki na pia wapenzi au mmeshazoea wapendanao wote lazima wafanye ngono?” Malaika aliuliza kwa sauti ya upole.

Anderson alikubali na kufanya waongozane wote hadi Hotelini kama kawaida Malaika Mweusi alilipia chumba.

Walipofika chumbani Malaika alitaka kujua wamefikia wapi na mkewe.

“Eeh! Lete stori, mmefikia wapi na mkeo? Ulinieleza kuwa anaitwa mama Gift eeh?”

“Ndio mama Gift.”

 Anderson alimshukuru kwa ushauri wake na nasaha alizompa zilizorudisha furaha katika nyumba yake.

“Ooh, siamini kumbe nami naweza kuokoa nyumba za watu basi muda si mrefu nitafungua kituo cha ushauri nasaha,” Malaika alisema huku akionesha aibu na kumfanya achanue kama tausi bustanini na kuuongeza uzuri wake mara dufu.

“Nami nitakitangaza kila kona,” Anderson aliongezea.

Mara simu ya Anderson ikaita, naye alipokea na kuongea mara akasema:

”Hebu subiri,” Anderson alitoa pochi yake na kuchambua baadhi ya vitu fulani na kutoa business card na kuanza kumsomea mtu wa upande wa pili.

Wakati anaitoa ile business card, picha yake ya kipande ilidondoka chini ambayo Malaika Mweusi aliokota na kuangalia wakati huo Anderson alimaliza kuzungumza na simu. 

Malaika mweusi alitazama ile picha na kupiga kelele ya mshituko.

“Haa! Huyu ndio mkeo?”

“Eeh, mbona umestuka baada ya kumuona una mfahamu?”

“Hapana ni mzuri sana unajua kuchagua.”

“Hakushindi wewe.”

“Ananishinda tena kwa mbali ndio maana yeye ameolewa na mimi bado nazurula.”

“Naamini ulikuwa umejificha kama ningekuona wewe nisingethubutu kuoa mwanamke mwenye kiburi kama huyu.”

“Na huyu ndiye mtoto wenu?”

“Eeh, ndio Gifti mwenyewe huyo.” 

Ilikuwa ni picha ndogo ya pamoja ya familia ya Mr. Anderson yeye na familia yake. 

“Sasa lini nitamuona wifi?”

“ Kwa kuwa tupo pamoja tutapanga siku ya kumuona.”

“Sawa nitafurahi kumfahamu wifi pamoja na mtoto wetu.”

Baada ya mazungumzo, kabla ya kutoka Malaika Mweusi alimuliza Anderson kuwa anahitaji kiasi gani cha pesa kwa ajili ya matengenezo ya gari lake.

“Laki nne kasoro,” Malaika Mweusi alifungua mkoba na kutoa laki nne taslimu.

“Nina imani tutakapokutana gari likuwa zima?”

“Asante sana, sijui nikushukuru vipi, sina cha kukupaa,” Teddy alizidi kumchanganya Anderson.

“Vipo vingi,” Teddy alijibu huku akitabasamu.

“Kimojawapo?”

“Ipo siku nitakwambia ni kipi.”

“Kipi mpenzi?” Anderson alitaka kujua.

“Ooh! Mbona umefika mbali, wewe ni mume wa mtu, naheshimu ndoa yako sitaki ndoa yako ivunjike, tutaendelea kuwa marafiki tu na usidhani kutaka msaada kwako ni kutaka penzi kwako la hasha bali moyo wangu umekutunuku hilo wazo litoe mawazoni,” Teddy alimkatisha tamaa Anderson.

“Sasa ni lini utaniambia kitu hicho?”

“Nilishakwambia nitakujulisha lini tena kitu hicho hakina gharama.”

“Sawa ngoja nisubiri ingawa umeniachia fumbo zito.”

“Tena imekuwa vizuri nimekumbuka kuanzia kesho nitakuwa na safari ambayo itaniweka mbali kwa wiki mbili nitakaporudi nitakujulisha.”

“Sawa japo sipendi kujua unaenda wapi.”

“Nami natarajia kukuta ndoa yako inashamiri, sitaki kusikia mkeo amerudi nyumbani kwao.”

“Sidhani, wewe nenda salama Mungu akijali tutaonana sio siri umeshaniambukiza ugonjwa wa mazoea moyo wangu huwa taabani nisipokuona hata sijui kwa nini?”

“Umenishiba, hata mimi mgonjwa juu yako ungekuwa ujaoa sijui….” Hakumaliza na kujikuta walicheka kwa pamoja huku wakigonganishiana mikono. Waliagana na kama ilivyokuwa kawaida kwa kutangulia Anderson na kumuacha Malaika Mweusi.

                                                     ******

Siku ya pili tangu walipoagana na rafiki yake wa karibu aliyemteka mawazo yake Malaika Mweusi, msichana mwenye fumbo la ajabu kwake. Anderson baada ya shughuli zake za kawaida za wiki nzima aliamua kutoka na familia yake kwenye ufukwe mwanana wa Biski Beach ili kupumzisha misukosuko ya wiki nzima ya kumtafuta muuajia ambaye kwa wiki mbili alikuwa ametulia na kuacha swali kwake safari ile angefanya mauaji wapi au kamaliza kampeni yake.

Akiwa na familia yake mkewe na mtoto wake Gift walijiandaa kutoka majira ya saa sita alasiri, wakati huo mkewe alikuwa akijipodoa kwenye meza ya kujipodoa. Mara simu yake iliita na alipoziangalia namba zilikuwa ngeni kwake alijiuliza kabla ya kupokea ni nani, wasiwasi wake huenda mambo yameharibika.

Kilichomshangaza namba zote zinazopigwa katika simu yake hutoa jina, namba ile wanaoijua ni wachache na majina yao yamo kwenye simu. 

Alijiuliza sijui anatakuwa ni nani na anataka nini tena katika muda ambao anahitaji kupumzika na familia yake, aliamua kupokea kwa ukali kidogo akihoji:

“Haloo, nani? Na unataka nini?” aliuliza kwa ukali kidogo.

“Samahani wewe ni Mr Anderson?” sauti ya kike iliuliza.

“Wewe ni nani?” hakumjibu alimuuliza swali.

“Kabla ujajua mimi ni nani kwanza nijue wewe ni Mr, Anderson?”

“Hii namba kakupa nani?”  Anderson hakujibu zaidi ya kuongeza swali lingine.

“Mzee huu muda si wakulizana maswali mengi kuchelewa kwako ni kuendelea kuharibu mambo,” kauli ilimtaadhalisha.

“Una maana gani kusema hivyo?” alishtuka kidogo.

“Mimi ni msamalia mwema si lazima ujue ni nani aliyenipa namba yako, ukija katika eneo la tukio tutaelewana vizuri,” kauli ya upande wa pili ilizungumza kwa taratibu na kujiamini.

“Tukio! Tukio gani tena hilo?” moyo ulimpasuka kwa kujua mambo yameiva.

“Mzee, kuna vijana watatu wameingia katika moja ya ofisi tumewatilia mashaka huenda ndio wauaji wenyewe wanaofanya mauaji jijini.”

  “Ooh! Ni eneo gani hilo?”

    “Ni maeneo ya Jengo la Ushirika, Mnazi Mmoja pembeni kuna jengo moja lenye ghorofa mbili. Wameingia humo ndani  fanyeni haraka mkichelewa tu mtakuta watu wameuawa.”

 “Ooh! Ishakuwa tabu, sasa hii ni kazi gani isiyokuwa na mapumziko?” Anderson alizungumza peke kwa sauti.

“Vipi tena mume wangu ?” mama Gift aliuliza.

  “Kuna tukio limetokea mnazi mmoja  karibu na jengo la ushirika. “

    “Sasa ndio itakuwaje?”

     “Hakuna kitakachoharibika nyie jiandaeni kama kawaida ngoja niwajulishe vijana wangu waende katika tukio  ili tuedelee na safari yetu.”

 Anderson aliwajulisha vijana wake  kuwa wakutane  katika eneo la Mnazi Mmoja kwenye jengo lililo pembeni na Ushirika  tayari kulivamia. Alimwacha mkewe akiwa analalama hakusikiliza  lawama za mkewe  aliingia kwenye gari na safari ya kuelekea Mnazi mmoja ilianza.

Alikwenda kwa mwendo wa kasi  ya kuruka alitumia dakika kumi na mbili  kufika katika eneo la tukio  na kuwakuta vijana wake  wakiwa tayari wameshafika  mara moja walilitafuta jengo lililoelezwa limevamiwa. 

 Hali katika eneo la Mnazi Mmoja ilikuwa shwali hakukuwa na dalili yoyote  ya kuwepo tukio lolote la hatari. Ilibidi wawahoji  baadhi ya watu waliokuwepo kwenye eneo lile  lakini kila mmoja habari ile ilikuwa mpya kwake. Walijaribu kuzunguka katika eneo lote  bila kuona dalili zozote za hatari.

“Bosi hebu mpigie basi huyo mtu atuelekeze vizuri.”

Alipojaribu kupiga namba ilikuwa haipatikani.

Anderson aliwachagua vijana wake  zaidi ya watano waendelee kulinda  katika eneo lile na yeye alirudi nyumbani  kumwahi mkewe ambaye alijua lazima safari yenyewe ataisusa.

 Ilikuwa imepita saa moja  tangu aondoke nyumbani kwake kwenda kwenye tukio aliendesha gari kwa mwendo wa kasi ili kumuwahi mkewe  alijua akifika tu hata ndani haiingii zaidi ya kumpigia honi  na kuondoka.

 Alifika nyumbani kwake majira saa kumi na robo  hakuwa na haja ya kuingia ndani alipofika tu alipiga honi ili mkewe atoke na kuondoka. Alipiga honi zaidi ya mara kumi lakini mkewe hakutoka alijua amesusa ilibidi ateremke garini amfuate ndani, sio  siri tabia mkewe zilimchosha, jambo ndogo lazima asuse na kuwa kubwa hata kama lina umuhimu.

Aliteremka kwenda ndani, mlango wa sebuleni ulikuwa umeegeshwa aliusukuma kuingia moja kwa moja ndani huku akimuita mkewe.

“Sweet ... Ma Sweet heart, Mama Gifti upo wapi mpenzi au ndio umesusa? Njoo mpenzi nimerudi mumeo sijachelewa najua umeshajiandaa twende basi mpenzi au umerudi ndani kulala?”

Sebuleni hapakuwepo mtu alijua wapo chumbani alikwenda moja kwa moja hadi chumbani, mlango wa chumbani nao ulikuwa umesindikwa aliusukuma na kuingia ndani. Picha aliyoiona machoni mwake hakutarajia kuiona maishani mwake mpaka anakufa. Alijiuliza yupo ndotoni au wapi, alijikuta akisema kwa sauti ya juu: 

“Hapana…hapana...haiwezekani,” alisema huku akishika mikono kichwani. Kilichokuwa mbele yake kilikuwa ni kweli, mwili wa mke wake ulikuwa umelazwa kitandani ukiwa mtupu kama alivyozaliwa akiwa ameuawa kifo cha kinyama.

Kilikuwa kifo cha kinyama na cha ukatili wa hali ya juu alikuwa amelazwa chali mwili wote ukiwa umechanwachanwa na matumbo yote yakiwa yapo nje, sehemu za siri zikiwa zimeharibiwa vibaya zilikuwa zimechanwachanwa na sehemu za siri zilikuwa zimewekwa kipande cha mti.

 Kilikuwa ni kifo cha unyama wa hali ya juu na pembeni yake alikuwa mwanae Gifti akiwa amelalia kifuani kwa mama yake naye alikuwa ameuwawa pia. Ilionyesha kuwa Gifti alikufa kwa kunyongwa kwa kamba au mshipi kwani alikuwa hana jeraha lolote mwilini Anderson alijikuta nguvu zikimwishia na kujibweteka chini pwaaa! Huku nguvu zikimuishia kabisa. 

Alilia kama mtoto mdogo akiwalilia mke na mtoto wake Gitfi, lakini alijikuta akijisemea ni upumbavu kulia kama mwanamke kwani adui anaweza kuwa yumo humo ndani na anaweza kunimaliza kirahisi.

Alijikaza kiume na alichukua bastola yake mkononi, alinyanyuka kutoka pale chini alipokuwa amejibweteka na kuanza kuanza kumsaka mbaya wake kwa taadhari kubwa. Alizunguka kila kona bila kumuona mtu yeyote aliamua kurudi ndani kuifadhi miili ya marehemu mkewe na mtoto wake Gifti zilizokuwa zimejitandaza katika kitanda kizima huku akiwa ametapakaa damu nyingi na kuchuruzika kwenye sakafu.

Aliunyanyua mwili wa mtoto wake Gifti na kuulaza pembeni ya mama yake huku mwili wake ukimtetemeka na jasho likimvuja kama maji mwili mzima. Aliuchunguza mwili wa mtoto wake na kugundua kuwa ulikuwa na jeraha shingoni likionesha kuwa amenyongwa na mshipi.

Aliuchukua mwili wa mkewe na kuufunika vizuri alinyanyua simu na kuwajulisha vijana wake yaliyomsibu. Vijana wake waliwasili haraka kumpa msaada bosi wao, miili ya marehemu wote ilipeleka Hospitali ya taifa ya Muhimbili na vijana wengine walifanya usafi sehemu zote zenye damu.

Anderson alionyesha kuwa mtu mwenye mawazo mengi juu ya tukio lile zito la kutisha. Alijawa na mawazo juu ya mbinu za hali ya juu wanazotumia wauaji, ikiwemo kumuondoa nyumbani na kupata nafasi ya kuitelekeza familia yake.

Alijikuta akijiuliza muuaji ni nani na kwanini ameamua kuua familia yake au ni kwa sababu ameanza uzijua nyendo zake. Amefanya vile ili umtisha. Lakini alijiapiza kwa hali yoyote ile atahakikisha anamtia mikononi, iwe isiwe. Aliweka nadhiri kumsaka muuaji hadi tone la mwisho la damu yake.


                    ****

Mazishi ya mkewe na mtoto wa mkuu wa upelelezi Anderson yalifanyika kwa heshima zote. Kabla ya maziko wakati wa kuaga miili ya marehemu Anderson alimuahidi mkewe kwa sauti kubwa mbele ya kadamnasi:

“Ewe mke wangu na mwanangu mpenzi nendeni mkiwa mmeniachia jeraha kubwa moyoni mwangu nakuahidi damu yenu aitapotea bure. Nakuhakikishia muuaji nitamtia mkononi na kulipiza mara dufu kwa hili alilowafanyia. Eeh! Mungu wapokee na uwape makazi mazuri ili siku moja tukutane

“Ooh! Maskini ni nini nilichomkosea huyu muuaji mpaka afanye unyama wa kikatili namna hii. Eeeh! Mke wangu….Ooh! Mwanangu kipenzi Gifti, zawadi nilizopewa na Mungu baba  leo inapotea kama kibatari kilichozimika kwenye upepo mkali.”

 Anderson nguvu zilimwisha na kujitupa juu ya majeneza na mke wake na mtoto wake. Alilia kama mtoto mdogo kila alipofikilia kifo cha mkewe alikuwa anajiuliza kama muuaji ameona ameanza kugundua mbinu zake. Kwa nini awaue mkewe na mtoto wake ni bora angemuua yeye mwenyewe kuliko unyama alioufanya.

Kuua familia yake anakuwa hajafanya kitu chochote kwani ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto si  kuuzima bali ni kuzidisha moto uwake kwa nguvu.

                                                          ***


Wiki moja baada ya kifo cha mkewe na mtoto wake akiwa ofisini alikuwa ni mwingi wa mawazo kuhusu mbinu za muuaji. Alifikiria ujumbe ambao hupenda kuwaachia wauaji. Maneno ambayo hupenda kuyatumia ni ‘Mtetezi wa Haki za Binaadamu, Mshahara wa Dhambi ni Mauti, Hukumu baada ya Hukumu, na alioachiwa kwa mkewe kuwa ALINIMULIKA MIMI NIMEMCHOMA. 

Alijuliza haya maneno yana maana gani ni wazi inaonyesha si muda mrefu muuaji atamtia mikononi kitendo cha muuaji cha kuteketeza familia yake ni dalili za mfa maji ambaye ameanza kutapatapa.

Akiwa bado kwenye lindi la mawazo  simu yake ililia, alichukua juu ya meza aliziangalia zile namba kwa makini kwani zilikuwa ni ngeni kwake namba zile zilimfanya aingiwe na hofu ilikuwa ni sawa na kutonesha kidonda kilichoanza kupona.

Simu kama ile wiki iliyopita ilipoteza familia yake, alipandisha pumzi juu na kuzishusha ili kujipa ujasiri na baadaye alibonyeza kitufe cha kupokea na kuongea kwa ukali:

“Haloo nani mwenzangu?”

 “Aah! Anderson mbona kila wakati unakuwa mkali  hivi hata wifi anapata nafasi ya  kucheka na wewe?”  Ilikuwa ni sauti tamu ya kinubi cha mtume Daudi ya rafiki wake wa karibu Malaika Mweusi ambaye walipotezana kwa takribani wiki mbili kwa kuwa   alikuwa safari nje ya nchi.

“Aaah! Samahani Malaika wangu umerudi lini?”

“Leo hii nina hamu kubwa ya kukuona rafiki yangu mpenzi nina imani wifi hajambo na mtoto wenu kipenzi Gift pia, nina matumaini ndoa yenu inashamiri na kuleta furaha isiyo na kifani.”

Kauli ile iliuchoma moyo wa Anderson ilikuwa ni kama kutonesha donda lililokwishaanza kupona. Jibu lilikuwa zito sana kutoka mdomoni kwake,  kitu kilichomshtua Malaika Mweusi upande wa pili.

 “Vipi mbona kimya nasikia ukivuta pumzi  na kuzishusha au hupendi kuonana na mimi, basi samahani,” Malaika Mweusi alikata simu  Anderson alikurupuka kama anatoka usingizini.

 “No..no..hapana Malaika wangu sikuwa na maana hiyo wakati huo simu ilikuwa imekatwa. Kwa  haraka alimpigia simu Malaika Mweusi  aliipokea upande wa pili.

“Eeh! Unasemaje?”

 “Samahani Malaika wangu  sina maana uifikiriayo.”

    “Kufikiria  nini Anderson?”

     ”Kuwa labda sipendi kuonana na wewe Malaika, ni mambo mazito yamenipata sina msaada wowote nina imani wewe ndiye tegemeo langu la pekee.  Kwanza nina shukuru kukutana nawe  nipo chini ya miguu yako Malaika wangu, ni mtu wa pekee  duniani unayeweza angalau kwa asilimia tano kunipa faraja maana najiona nipo katikati ya dunia na mbingu,” Andarson alibembeleza.

“Anderson mbona unanitisha una nini?” Malaika alishtuka.

“Ni mengi ya kuzungumza na wewe tukikutana, nahitaji msaada wako mkubwa kwa muda huu.” 

“Sawa basi tukutane palepale pa siku zote muda uleule tafadhali jali wakati,  usijali kila kitu nitalipia mimi.”

“Sawa Malaika wangu usiache kuja nakutegemea kuliko kitu chochote duniani kwa sasa.”

“Sawa Anderson lazima nifike usihofu nipo kwa ajili yako,” Malaika alimtoa hofu.

“Nitafurahi kama utafika.”’

“Usihofu nisubiri au nitawahi ili kukuonyesha jinsi ninavyokujali.”

Kwa vile muda ulikuwa umeisha Anderson alitoka ofisini na kurudi nyumbani tayari kwa kujiandaa kukutana na Malaika Mweusi. Baada ya kujiandaa aliingia garini na kuelekea Biski hoteli, aliwasili robo saa kabla ya muda waliopangaa kukutana, alitafuta eneo zuri na kuegesha gari lake aliteremka na kuhakikisha gari lake lipo kwenye usalama alielekea hotelini.

Akiwa anaelekea mapokezi alishtukia anashikwa bega alipogeuka alikutana na harufu kali ya manukato apendayo ujipulizia Malaika Mweusi alipogeuza shingo alilakiwa na tabasamu lililonakshiwa na meno madogo meupe yenye mwanya mwembamba. 

“Ooh! Vizuri, kumbe tumewahi pamoja karibu sana,” ilikuwa ni sauti tamu ya Malaika Mweusi. 

“Jambo nililonalo ni zito hivyo linatakiwa umakini na kujali muda,” Aderson alisema akielekea mapokezi.

“Asante, twende zetu moja kwa moja nimeshalipia mapema na ufunguo ninao.”

Waliongozana moja kwa moja hadi kwenye chumba ambacho Malaika alikuwa amelipia.

Sura ya Anderson ilikuwa imezongwa na lindi la mawazo yaliyokosa ufumbuzi. Kama kawaida Malaika Mweusi alifikia kitandani na Anderson alikaa kwenye kochi.

Kabla hawajaanza chochote kilichowapelekea pale chumbani, mara mlango ulipogongwa, alikuwa ni mhudumu alileta vinywaji na Malaika alivipokea na kufunga mlango kwa ndani. 

Aliruhdi hadi kochini akiwa na glasi mbili za vinywaji na kukaa pembeni ya  Anderson.

“Karibu,” alimkabidhi glasi moja.

“Asante,” alijibu huku akiipokea na kugongesha glasi kutakiana afya njema.

Baada ya kimya kifupi Malaika kwa sauti ya upole aliuvunja ukimya ule.

“Ndiyo Mr. Anderson nipo hapa kwa ajili yako, nipo tayari kukusaidia kwa kadri ya uwezo wangu,” maneno ya Malaika yalimpa faraja Anderson.

Kwa ujasili mkubwa alianza kumhadithia kuanzia mwanzo hadi mwisho yaliyomsibu wiki moja iliyopita. Simulizi lile lilimshtua sana Malaika Mweusi na kuangua kilio kilichomshtua hata Anderson.

“Malaika mbona unanivunja nguvu? Wakati wewe ndiye niliyekutegemea unaonyesha udhaifu sasa unafikiri nani atanisaidia?”

“Anderson inauma ni unyama wa aina gani huo, mkeo amekosa nini mpaka apewe adhabu kubwa namna hiyo, inauma…inauma….mtoto Gift amekosa nini? Mtu kama  huyu si wa kuhurumiwa hata kidogo,” wakati huo Malaika Mweusi alikuwa analia akiwa kajitupa chini.

Ilibidi Anderson afanye kazi ya ziada kumbembeleza:

“Malaika wangu wewe ndiye niliyekuwa nakutegemea, unalia hivyo nani atakaye nisaidia?”

“Inauma sana wacha nilie nikamue uchungu uliopo moyoni mwangu ili niweze kujua nini nitakachokusudia,” baada ya kimya ndipo Malaika Mweusi alipoanza kusema:

“Ni kweli inaniuma sana lakini cha kufanya kwanza kabisa kabla ya yote nakuahidi nitashirikiana na wewe katika kipindi chote cha majonzi nitakuliwaza na kukufariji,” Malaika alisema huku akinyanyuka alipokuwa amekaa.

“Hilo nashukuru sana, je, la huyu muuaji utanisaidia vipi?”

“Sipendi kukudanganya suala la polisi mimi sijui chochote lakini kuna umuhimu wa kuwatumia hata Interpool (polisi wa kimataifa) nina imani ninyi kazi iliyopo mbele yenu naona imewazidi na siku zinakatika na mauaji yanaongezeka kila kukicha. Ni vizuri kusema umeshindwa ili upate msaada.”

Malaika alitumia muda mwingi kuongea na Anderson baada ya kikao chao kilichowarudisha katika fikira nyingine ambazo ndizo zingekuwa suluhu ya matatizo ya Anderson. 

Hata hivyo kila mmoja alikuwa na fikra tofauti ndani ya  moyo wake kutokana na ukaribu wao waliokuwanao.  Anderson hisia zake zilikuwa katika mapenzi yaani wako bibi na bwana.

Alijikuta akiongeza mapenzi kwa Malaika Mweusi na kumwona ndiye mwanamke anayefaa kuziba pengo la mkewe, kwani alionekana kuwa msichana aliyesimama kidete kumliwaza muda wote wa matatizo.

Kilichomshangaza ni tofauti ya mawazo yake, alihisi labda pamoja na kupenda lakini Malaika Mweusi alishindwa kumweleza kwa sababu alikuwa akijua kwamba yeye ni mume wa  mtu.

Lakini alijua huo ndio ulikuwa muda mzuri wa Malaika Mweusi kulionyesha penzi kwake. Hata hivyo aliishia kuona penzi la kirafiki kama la dada na kaka.

                                                            *** 

Siku zote Anderson alipokuwa na Malaika Mweusi hasa sehemu za faghara, mikao na nguo alizovaa zilimfanya awe na matumaini kuwa Malaika Mweusi anamwonyesha alivyojirahisi kwake. Siku zilikatika bila mabadiliko yoyote katika uhusiano wao.


MIEZI 6 BAADA YA VIFO VYA FAMILIA YA ANDERSON.

Siku moja wakiwa faragha Mr Anderson hakuamini masikio katika mazungumzo yake na Malaika Mweusi. 

“ Anderson,” Malaika Mweusi alimwita akiwa amemchanulia tabasamu pana.

“Unasemaje Malaika wangu?”

“Utakaa hivi hadi lini?”

“Una maana gani?”

“Lazima uoe ili kuondoa mawazo ya matatizo yaliyonikuta, lazima uwe na mwenza ambaye atafungua ukurasa mpya.”

 Anderson alijua sasa wazo lake la kumpenda Malaika Mweusi  limepata jibu.

“Ni kweli kabisa Malaika wangu, sijui utanisaidiaje?”

“Tafuta mwanamke ili ufungue ukurasa mpya yaliyopita yamepita , imebaki historia.” Malaika alisema huku akimuangalia kwa jicho la huruma.

“Ni kweli Malaika wangu, na nina imani wewe unajua nani ni chaguo langu.”

“Ni vigumu, mimi si mnajimu wala hujawahi kunidokeza nani anaweza kuwa chaguo lako baada ya kifo cha kipenzi chako mama Gift.”

“Wamjua wazi ila hutaki kumweka bayana na…”

“Ni kweli simjui, hebu nifumbue macho nami nimjue wifi yangu atakayeziba pengo la wifi yangu mama Gift.”

“Ni kweli humjui?” Anderson alimuuliza akiwa amemkazia macho.

“Simjui, kwa nini nikukatalie?”

Anderson mdomo ulikuwa mzito kumtamka huyo mwenza mtarajiwa, Malaika Mweusi alipoona amepata kigiugumizi alimuliza.

“Vipi  Anderson mbona umekuwa bubu ghafla?”

“Hapana, basi kesho tukikutana utamjua vizuri hata nikikueleza utashangaa.”

“Anderson… nikueleze mara ngapi kuwa mtu huyo simjui au kuna mtu ulimuonyesha ukafikiri kuwa ni mimi? Katu sijui.”

“Utamjua tu,” Mr Anderson alimtoa wasiwasi.

“Ni vizuri na mimi nimjue wifi yangu mtarajiwa ili nikupe maksi, lakini nakuamini mjuzi wa kuchagua wasichana warembo. Ina maana huna hata picha yake?” swali lile lilizidi kumchangaya sana  Anderson roho ilimwambia kwani  nini asimweleze ukweli  kuliko kuyaficha maumivu yake.

Alipandisha pumzi na kuzishusha kitu kilichomfanya Malaika Mweusi amwangalie usoni na kupandisha macho yake kwenye uso wa Anderson ambaye alipopeleka macho yake kwenye uso wa Malaika yalikutana na  kuona aibu.  Ilibidi aangalie pembeni Malaika Mweusi alimsogelea karibu na umshika bega.

“Una nini, mbona umebadilika?”

“Aah! Wacha tu,” alipoteza ujasili wa kiume.

“Hapana nipo hapa kwa ajili yako kwa hiyo usihofu nieleze tu nipo tayari kukusaidia kwa vile wewe ni mtu muhimu sana maishani mwangu.”

“U…naaa…jua,” bado Mr Anderson alipata kigugumizi

“Simjui ndio maana nataka unieleze nimjue wifi yangu.”

“Kweli unanipenda?” aliuliza swali badala ya kujibu swali.

“Hilo si swali bali upendo wangu kwako upo wazi hauhitaji maswali,” Malaika alijibu kwa sauti tamu huku akimuangalia kwa jicho la huruma. 

“Upo tayari kunisikiliza?”

“Nimekusikiliza mara ngapi hadi hili linishinde kusikiliza.”

“Malaika wangu,” Anderson alimwita kwa sauti ya upole.

“Unasemaje?”

“Nakupenda sana Malaika wangu.”

“Hata mimi naelewa ndio maana nipo pamoja nawe baada ya kuelewa ulivyo na umuhimu kwenye maisha yangu.”

“Sasa mbona unielewi?” aliongea kwa sauti nyonge sana.

“Kwa lipi?”

“Kuhusu upendo wa dhati juu yako, unafikiri ni nani atakayeziba pengo la mke wangu mama Gift kwa asilimia mia kama si wewe!”

Malaika Mweusi alivyosikia vile alishituka na kuuliza kama kwamba hajasikia. 

“Eti unasemaje?”

“Ni kweli kabisa kuwa wewe ndiye chaguo langu sina mwingine zaidi ya hapo sitaoa tena mwingine maishani mwangu.”

“Mmh! Mbona unanipa mtihani mkubwa nisio uweza kujibu.”

“Mtihani gani huo, kwani umeolewa?”

“Hapana.”

“Una mchumba?”

“Hapana.”

“Rafiki wa kiume?”

“Sina.”

“Sasa Malaika wangu ugumu upo wapi?”

“Sikiliza Anderson chaguo lako lilikuwa zuri ambalo hata mimi ningeweza kulipokeakwa mikono miwili lakini…”

“Lakini nini tena Malaika wangu, elewa moyo wangu wote umeubeba wewe.”

“Anderson aliyoyasema ni sawa lakini kuna vitu vinanipa ugumu wa mimi kuwa mkeo.”

“Vitu gani?”

“Unaelewa vizuri kuwa uhusiano wetu umeanza muda mrefu kabla ya kifo cha mkeo.”

“Hilo naelewa sasa tatizo ni nini?”

“Kama ulivyonieleza kifo  cha mkeo kilivyokuwa.”

“Naelewa lakini mbona unapindisha si useme kipingamizi kingine lakini nina imani hakuna kipingamizi ni wazi ulikuwa hunipendi bali unanidanganya tu, nafikiri hiki ndicho kipindi cha kudhihirisha mapenzi yetu bayana.”

“Unajua Anderson unaongea tu bila ya kufikiri unachokisema   kimesimama upande gani.”

“Una maana gani?”

“Mimi kama nitaolewa na wewe watu watafikiri mambo mengi kuhusu kifo mkeo labda tumemuua ili tuishi pamoja.”

“Hivi nani duniani aliyewahi kuzuia mwanadamu asizunguze anayotaka kusema. Ukisikiliza maneno ya watu unachelewa maendeleo, kwanza nani anajua  uhusiano wetu?”

“Ina maana katika dunia hii tupo wawili tu?”

“Hapana ila sidhani kama watafikiri hivyo, huo ni wasiwasi wako tu japo waswahili wanasema jino la pembe si dawa ya pengo lakini kwangu wewe si jino la pembe ni jino jipya linaloota na kuziba pengo.”

“Usemavyo sikatai lakini tatizo jingine huoni kama utanioa utakuwa umeniingiza kwenye matatizo?”

“Matatizo gani tena?”

“Nina imani bado muuaji atataka kuiteketeza familia yako, huoni kuwa uhai wangu utakuwa umeuweka sokoni?”

“Nakuhakikishia kuwa kosa nililofanya awali sitarudi tena nitakulinda kama mboni ya jicho langu sidhani kama muuaji atanisogelea tena.”

“Mmh! Sawa.”

“Sawa nini, mbona uniweki sawa?”

“Nimekubali.”

“Aah! Siamini…Siamini Malaika wangu, nimeamini kuwa wewe si mtu wa kawaida bali Malaika uliyeubwa kwa ajili yangu ili kunipa faraja,” Anderson alimkumbatia Malaika Mweusi na kumbeba juu juu hadi kitandani.

Alimuomba Malaika Mweusi siku ileile wakalale nyumbani kwake.

“Hapana mpenzi sina budi kulitamka  neno mpenzi kutoka uvunguni mwa moyo wangu,” Malaika alisema kwa sauti ya kinanda.

“Kwa nini honey tusiende nyumbani kwako ili ukapazoee kabla ya harusi?”

“Ni haraka sana, lakini nimeshakukabidhi  moyo wangu hivyo siku zote mambo mazuri hayataki haraka.”

“Hapana lazima niwe na haraka mimi kwako kama msafiri aliye jangwani aliyedondosha chupa ya maji na kuteswa na kiu kwa kipindi kirefu bila matumaini ya kupata maji. Ghafla anakiona kisima chenye maji sidhani kama atasubiri.”

“Maneno yako yana ukweli wa asilimia mia, lakini siku zote subira waswahili wanasema ni dhahabu.”

 “Sawa nimekubali, basi wiki endi hii nitakupeleka kwa wazazi wangu nina imani ndio siku itakayokuwa maalum wa sherehe fupi ya kuvishana pete ya uchumba na mipango ya ndoa ianze mara moja.”

“Nina furaha sana tena sana kufahamiana na familia yako.” 

Ilikuwa ni siku ya furaha kwa watu wawili  Anderson pale alipopata tulizo la moyo wake lililokuwa likimpa kimuhemuhe usiku na mchana. Naye Malaika Mweusi alikuwa na furaha kubwa kumpata yule aliyemuota usiku na mchana kuwa siku moja atakuwa mumewe wa ndoa.

                                                 ***

Ilikuwa ni siku maalum iliyoandaliwa kwa vitu viwili muhimu kwa wakati mmoja, moja kutambulishwa kwa Malaika Mweusi kwa wazazi wa Anderson pili kuvishwa pete ya uchumba. Malaika Mweusi alimpitia Mr Anderson kwake akiwa kwenye gari  lake la kifahari aina ya Range Rover Vogue sport ya rangi nyeusi.

Hakuwa yule Malaika Mweusi aliyependa kuvaa mavazi yanayomweka nusu uchi na mapambo ya gharama, la hasha huyu alikuwa  mwingine kabisa.

Alikuwa amevalia vazi refu la kitenge cha rangi ya njano na nyeusi kilichoshonwa kwa ustadi mkubwa na kilemba chake na mkoba wa ngozi ya pundamilia, hakika alipendeza sana. Ukimwangalia harakaharaka ungesema ameteremka kutoka Lagos Nigeria au DR Congo.

Vazi alilolivaa hupendelewa kuvaliwa na wanawake matajiri nchini Nigeria au wafanya biashara wa Kikongomani. Chini alivaa viatu virefu vya ngozi ya pundamilia vilivyofanana na rangi ya mkoba wake. Shingoni alivaa mkufu mpana wa dhahabu. Hakuvaa mingi kama kawaida yake na mkononi hakuvaa bangili ya dhahabu aliivaa saa yake ndogo ya dhahabu.

Hakika Malaika Mweusi alipendeza sana machoni mwa mtu yeyote alionekana msichana  mrembo mwenye heshima anayefaa kupelekwa kwa wakwe. Anderson alipomwona Malaika Mweusi alichanganyikiwa kwani kila siku alimuona mwanamke mpya.

“Malaika Mweusi! Hakika mwenyezi Mungu lazima nimpe shukrani zangu kwa kumuumba mrembo asiye na mapungufu yeyote ya sura, umbo na hata tabia hongera sana umependeza,” Anderson alimsifia akiwa amechanganyikiwa na urembo wake.

“Asante kwa kunisifia lakini sikushindi wewe ulivyopendeza kwenye suti nzito, hali hii  tunaenda kutambulishana je, itakuwaje siku ya harusi yetu, Anderson mpenzi na mimi sina budi kumshukuru mwenyezi Mungu kunichagulia mume  bora, unajua nilichokupendea?”

“Sijui Malaika wangu hebu niondoe tongotongo zililotanda kwenye ubongo wangu.”

“Si tupo pamoja habari hizi zinataka kituo kwa vile tuna safari ambayo tunasubiriwa kwa hamu kubwa kama ulivyonieleza huu si wakati wake fanya twende tuwahi tusije onekana kama tuna ahadi za ubabaishaji na kuwafanya wazazi wako kupunguza maksi.”

“Sawa mpenzi wacha tuwahi japokuwa unaniweka roho juu kama kiuno cha mnazi juu sipo na chini pia sipo nipo katikati.” 

“Ushaanza, tangu lini mnazi ukawa na kiuno? Ninyi ndio mnaosema eti nyoka ana kiuno.”

Walicheka kwa pamoja na kuingiaa ndani ya gari la Malaika Mweusi alikuwa anaendesha mwenyewe kuelekea nyumbani kwa wazazi wa Anderson. Walipofika walipokewa kwa shangwe na vifijo walifika sebuleni ambako palikuwa pamepambwa kwa maua ilionyesha kuwa ni siku maalum iliyoandaliwa kwa shughuli maalum.

Sebuleni kulikuwa na wageni wasiopungua kumi na mbili ila wazazi wa Anderson walikuwa ndani baada ya mgeni kufika na kutulia ndio walipokwenda kuitwa.

Baba na mama Anderson walitoka wakiwa wameongozana pamoja, wakati wanaingia Malaika mweusi alikuwa ameinama  alinyanyua uso wake baada ya kusikia sauti ya mama mkwe wake mtarajiwa.

“Ooh! Karibu sana mwanangu!”

 Macho ya Malaika Mweusi alikutana juu ya macho ya mama mkwe wake,   wakati huo alikuwa ananyanyuka ili amlaki mama mkwe wake mtarajiwa. Alijikuta akipatwa na mshtuko wa ajabu na kupiga ukelele mdogo.

“Ooh! Mungu wangu!” alijikuta akirudi tena chini kwenye kochi wakati huo alikuwa ameshikilia kifua chake kuonyesha amepatwa na hofu, kitu kilichomfanya mama Anderson abaki amesimama kama sanamu.

Watu waliokuwepo pale walikuwa na mshangao Anderson naye alipigwa na butwaa asijue nini kilichotokea. Baba na mdogo wake ilibidi wamfuate Malaika Mweusi aliyekuwa akihema kwa shida. Walipofika pale alipokuwa amekaa na kumuuliza.

“Nini tatizo mama?”

 Malaika kabla ya kujibu alinyanyua uso wake na na kukutana tena na sura za watu wawili baba na mkwe wake na shemeji yake mdogo wa  Anderson. Alishtuka zaidi kitu kilichozidi kuwashangaza wote waliokuwa pale.

Ilionyesha kuna kitu kilimtisha pale ndani na kupatwa na mshtuko. Anderson ambaye alikuwa amesimama pembeni ya mlango walioingilia wazazi wake alishangazwa na hali aliyojitokeza kwa mchumba wake. Alitoka pale mlangoni na kwenda moja kwa moja kwa mchumba wake ambaye muda mchache  angemvisha pete ya uchumba na kuwa mke wake mtarajiwa. 

Alijipenyeza katikati alipokuwa mdogo wake na baba yake mdogo waliokuwa wamepigwa na butwaa kwa kile alichokionyesha Malaika Mweusi, alimshika mabega na kumwita:

“Malaika wangu kulikoni mbona hivyo?”

Baada ya kusikia sauti ya Anderson alinyanyua kichwa ili kuhakikisha kuwa ni yeye. Alipitisha mikono yake nyuma ya shingo ya Anderson na kumkumbatia na kilio cha kuvuta makamasi kwa ndani.



“Malaika wangu hebu nitoe kizani nini kilichokusibu muda mfupi ulikuwa na furaha lakini ghafla umebadilika baada ya kuiona familia yangu?”

“Hapana mpenzi sivyo ufikiliavyo,” Malaika alisema kwa sauti ya kilio.

“Kama si hivyo ni nini kimekusibu?”

Alijitoa mikono ya Anderson, kwanza alimfuta machozi na kupangusa kamasi nyembamba kwa kitambaa cha mkononi. Kisha alikohoa ili kutengeneza sauti yake na kuzungumza kwa sauti ya chini kidogo inayomuwezesha mtu yeyote aliyekuwepo sebuleni kumsikia.

“Kwanza niombe radhi kwa hali niliyoionyesha kila mmoja ana shauku ya kutaka kujua kilichonisibu. Haikuwa nia yangu bali hali hii imejitokeza ghafla bila ya mimi kutarajia, Naweza kusema kweli dunia ni watu wawiliwawili.

“Yaani marehemu mama yangu anafanana sana na mama mkwe,  si kwa umbile bali hata sauti utafikiri walizaliwa mapacha. Wakati nanyanyua macho nionane na mama mkwe wangu nilipigwa na mshituko wa ajabu na kuona kama mama yangu mzazi amefufuka na siyo siri katika vitu nilivyovipenda ni mama yangu mzazi. Nilimpenda zaidi ya kitu chochote hasa kwa malezi na mapenzi mazito  aliyonileana. 

“Alipofariki ilikuwa ni pigo ambalo liliniumiza siku hadi siku kila nimkumbukapo marehemu mama yangu majonzi hunianza upya huwa kama nachubua kidonda ambacho kilianza kupona. Kwa kweli nilipomuona mama mkwe ilikuwa ni jeraha jingine la moyo wangu kwa hilo naomba baba, mama na shemeji yangu na wote mliokusanyika mnisamehe sana haikuwa nia yangu.”

Malaika mweusi baada ya kusema sababu iliyomfanya atokewe na hali ile  huku akilia. Alikwenda moja kwa moja hadi kwa mama mkwe wake na kumkumbatia. Mama mkwe naye alimpokea na kumkumbatia na kumpa pole.

“Pole sana mwanangu kazi ya Mungu haina makosa….je, baba yupo?”

“Hapana sina, kwani mpaka mama anafariki nilikuwa simjui baba yangu.”

“Ooh! Pole sana, nani aliyekulea mpaka ukafikia hatua hii?”

“Ni walimwengu tu.” Malaika Mweusi aliondoka kwa mama na kwenda kwa baba mkwe wake na kumtaka kumshika miguu.

“Baba naomba unisamehe.” lakini alimuwahi kabla ajainama na kumnyanyua.

“Hapana mama huna kosa lolote jisikie huru kwa lolote lile hapa ni kwenu.”

“Asante kwa hilo wazazi wangu”.

Aliwageukia wageni walikwa na kuwaomba msamaha ambao nao hawakuliona kosa lake na walimpa pole kwa mkasa wake mzito. Baada ya muda Malaika Mweusi alijitajidi kurudi katika hali yake ya kawaida na shughuli zote zilikwenda kama walivyopangwa.

 Alitambulishwa kwa ndugu na jamaa na wazazi wake wa Anderson na kuhitimisha kwa sherehe fupi lakini iliyofana vilivyo ya kuvishana pete ya uchumba. Baada ya sherehe Anderson na mchumba wake, mkewe mtarajiwa walikaa kikao kabla ya kuondoka kuzungumzia masuala ya harusi.

Japokuwa Anderson alitaka harusi ifanyike ndani ya mwezi mmoja, lakini Malaika Mweusi alitaka iwe baada ya miezi mitatu ili naye apate muda wa maandalizi kwa kuwaalika marafiki wake walio nje ya nchi. Wazo la Malaika lilipitishwa na baada ya kikao waliondoka pamoja siku hiyo  alilala kwa Anderson.  Ilipofika saa kumi na nusu usiku aliondoka.

                                                  ****

Tokea siku ile ikawa ni mazoea kwa Malaika Mweusi kulala na  saa kumi na nusu huondoka. Kila alipotaka kusindikizwa alikataa kitu ambacho kilichoanza kumtilia wasiwasi Anderson.

“Malaika.”

“Unasemaje my sweet?”

“Unajua tabia yako ya kuondoka alfajiri kila unapokuja kulala hapa inanitia wasiwasi.”

“Wasiwasi wa nini?”

“Labda kuna mume mwenzangu.”

“Hilo ni wazo potofu, lakini siwezi kukukataza kuwaza hivyo lazima unionee wivu, kama ningekuwa na bwana kwako ningekuja kufanya nini. Nilitaka kuja kwako baada ya kunioa lakini nimekubali kwa sababu  ya upendo wa dhati  kwako. Umeniomba nije nilale kwako nimekubali tena kwa muda wa siku uipendayo kwa vile bado hatujaoana huu ni utaratibu wangu wa kuondoka alfajiri ili asubuhi unikute nipo nyumbani kwangu najua huwezi kuamini lakini huo ndio ukweli sina mwanaume yeyote zaidi yako ili ukweli utaupata utakapo nioa.”

“Mmh sawa,” alijibu Anderson kwa unyonge.

“Usihudhunike mpenzi hizi ni zako dhabibu utazila taratibu  hakuna wa kukuibia.” Malaika Mweusi alimpiga busu Anderson na kuondoka na kumuacha akimkodolea macho.

                                                              ***** 

Mahusianao kati ya Malaika Mweusi na familia ya Anderson yalikuwa makubwa kitu kilichojenga mapenzi mazito kutoka ndani ya familia na kumsifu mtoto wao kwa kuchagu msichana mwenye upendo na huruma.

Kwa muda mfupi alitoa msaada mkubwa ikiwa ni pamoja kumaliza nyumba ya wakwe zake na kuwanunulia gari dogo la kutembelea kila mmoja aliomba siku ifike ili ndoa halali ifungwe.

Anderson alitaka kujua utajiri wa mchumba wake ameupata wapi wakati ni msichana mdogo tena yatima aliyelelewa na wasamalia wema. Hatua hiyo ilikuja baada ya kuonyeshwa mikataba.

“Najua utashangaa mpenzi baada ya kuona utajiri wangu wa kutisha nikiwa jijana mdogo na kuongoza vitu vyote hivi hili ni jambo linalotaka nafasi..si unakumbuka siku nilikueleza nilikupendea nini?”

“Ndio nakumbuka.”

“Basi vitu vyote navitafutia siku ili nikueleze kwa kituo, si haya tu kuna mengi yaliyo chini ya moyo wangu ambayo siku hadi siku yananiumiza akili yangu.

“Ni siku gani isiyokuwa na jina?”

“Ni baada ya ndoa yetu.. unajua bado ni muda gani tufunge pingu za maisha?”

 “Mwezi mmoja na siku kama ishirini hivi.”

“Vizuri siku ya kesho nitakuwa na safari yangu ya mwisho ya kibiashara kabla ya harusi yetu vilevile nitatumia safari hiyo kufanya mambo makubwa wawili. Moja kumtambulisha mtu ambaye atakuwa anafuata bidhaa kwani baada ya ndoa sitatoka mbali nawe ili tuweze kuonja raha ya ndoa au sio dear?”

“Mimi sina cha kuongea.”

“Pili kufanya shoping kwa kwa ajili ya harusi yetu nataka nikakununulie bonge la suti ya gharama ilingane na harusi yetu itakayoacha kumbukumbu kwenye ubongo wa watu.”

“Sawa lakini usikae sana kuondoka kwako ni sawa na kunyang’anywa blanketi kwenye baridi kali.”

“Si wewe tu bali imebidi ndio maana baada ya harusi nitahakikisha sibanduki kwako nina imani wivu wangu ni maradufu zaidi ya marehemu mke wako mama Gift.”

Malaika Mweusi aliondoka kuelekea Uingereza, Marekani, Asia na Falme za Kiarabu, katika uwanja wa ndege aliagwa na mumewe mtarajiwa na familia nzima ya Anderson baba, mama na ndugu na jamaa zake.

Kabla ya kupanda ndege aliagana na kila mmoja wao kwa kukumbatiana naye na wa mwisho aliagana na mumewe mtarajiwa kwa kukumbatiana kwa muda huku kila mmoja machozi yakimtoka kwa sauti iliyojaa majonzi alisema:

“Japo moyo unaniuma kutengana kwa muda lakini imebidi kutokana na sababu maalum lakini cha muhimu ni kuniombea dua niende salama na nirudi salama ili tusheherekee harusi yetu na nanyi bakini salama mkiendelea na mipango ya harusi nina imani baada ya wiki mbili au tatu nitakuwa nimerudi kabla ya harusi au itanilazimu nikatize ziara yangu.”

Machozi yalimtoka Malaika Mweusi wakati akiagana na ndugu wa familia ya mumewe mtarajiwa, baada ya muda aliingia kwenye Gulf Air na kuondoka nchini alimuacha  Anderson kama kinda la ndege lililoachwa kwenye kiota na mama yeke.

Wiki mbili baada ya Malaika Mweusi kuondoka kwenda kwenye ziara yake ya kibiashara Anderson aliendelea na mipango ya harusi yao wakati huo mauaji jijini yalikuwa yamepoa japokuwa uchunguzi haukufanikiwa kumtia mikononi muuaji.

Muda wote alikuwa akiwasiliana na kipenzi chake kipya Malaika Mweusi lakini wiki moja baada ya Malaika Mweusi kuondoka alimjulisha Anderson namba yake mpya kuwa amepoteza simu yake hivyo atamjulisha kwa namba mpya ili waendelee kuwasiliana. 

Malaika kupoteza simu yake alikuwa akiwasiliana na mchumba wake kwa yeye kumpigia kila siku  usiku. Siku zilikatika kama tatu bila ya mawasiliano kitu kilichomtia hofu Anderson na kujiuliza kulikoni mbona kimya cha ghafla ni kitu gani kimemsibu mchumba wake.

Alipokuwa ofisini kama kawaida yake alipokea simu ya baba yake mzee Chuma.

“Ndiyo baba, shikamoo.”

“Marahaba aisee njoo nyumbani haraka sana.”

“Kuna nini?”

Anderson habari zile zilimchanganya sana, aliingia kwenye gari akiwa na mawazo mengi juu ya simu ile ya baba yake.  Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi hadi Mbezi mwisho kwa wazazi wake alipofika alifungua geti na kuingia ndani moja kwa moja hadi ndani.

Ndani alilakiwa na vilio vilivyoonyesha kuna tukio lisilokuwa la kawaida wote walipomuona walimvamia kwa kilio.

“Jamani kulikoni?!”

“Ooh! Mama yako hatunaye,” aliambiwa na baba yake ambaye macho yake yalikuwa yamembadilikana kuwa mekundu kwa kulia na mkononi alishikilia kitambaa kwa ajili ya kujifutia machozi na kamasi.

“Eti unasema mama kafanyaje?” Anderson aliuliza kama hakusikia.

“Mama yako amefariki.”

“Amefanya nini, ameuawa?”

“Hapana amepata ajali amegonga mti wakati anakwenda shambani.”

“Una uhakika hajauawa?”

“Ni kweli taarifa zilitufikia na askari wa usalama barabarani.”

“Mwili wake upo wapi?”

“Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.”

“Kuna umuhimu wa kwenda sasa hivi.”

Aliongozana na baba yake hadi hospitali muhimbili kuchukua majibu ya kifo cha mama yake. Majibu yalionyesha kuwa amekufa kwa ajili ya kupata presha wakati anaendesha gari iliyosababisha ashindwe kuliongoza gari vizuri na kwenda kugonga mti.

Wakati anatoka hospitali na baba yake mara simu yake iliita. Ilikuwa ni simu ya kiofisi ambayo alipokea huku roho ikimdunda. 

“Ndiyo lete habari.”

“Mkuu kuna maiti moja imekutwa imekufa maji kwenye bwawa la maji machafu chuo kikuu. Marehemu  kandika ujumbe kwenye kikaratasi kuwa amejiua kwa sababu amejigungua kuwa ameathirika, maelezo yake tumeyakuta kwenye mfuko wake yaliyozungushiwa na karatasi ya nailoni ili usilowane.

“Kwa sasa hivi mpo wapi?”

“Tunakaribia hospitali ya Muhimbili.”

“Vizuri hata mimi nipo hapahapa mama yangu amefariki kwa ajali ya gari.”

Vijana wa Anderson waliwasili katika hospitali ya muhimbili harakaharaka walichukua machela kwa ajili ya marehemu tayari kumpeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Wakati wanateremsha mwili wa marehemu na kuuweka kwenye machela Anderson alikuwa amefika eneo lile alikisogelea kitanda alipokifikia wakati huo vijana wake walikuwa tayari kukisukuma, aliamua kuifunua shuka ili aione sura ya marehemu.

 Anderson alishtuka na kupiga ukulele:

“Aaah!” nguvu zilimuishia baada ya kuiona sura ya marehemu alianguka chini na kupoteza fahamu.


Itaendelea...


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.