HADITHI: MALAIKA MWEUSI
EPISODE 2
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500
ILIPOISHIA EPISODE 1
Wakati wanateremsha mwili wa marehemu na kuuweka kwenye machela Anderson alikuwa amefika eneo lile alikisogelea kitanda alipokifikia wakati huo vijana wake walikuwa tayari kukisukuma, aliamua kuifunua shuka ili aione sura ya marehemu.
Anderson alishtuka na kupiga ukulele:
“Aaah!” nguvu zilimuishia baada ya kuiona sura ya marehemu alianguka chini na kupoteza fahamu.
SASA ENDELEA...
Vijana wa Anderson walistushwa na hali ilivyotokea kwa bosi wao ilibidi wauguzi wafanye kazi ya ziada kumuhudumia Mr Anderson kwani alikuwa amepoteza fahamu.
Wakati huo mzee chuma mr Anderson alikuwa anakuja mbio kumuwahi mtoto wake.
“Vipi jamani?” aliuliza mzee Chuma.
“Mzee, amepata na mshituko baada ya kuiona sura ya marehemu aliyelazwa hapo juu ya kitanda”.
“Kwani ni mwili wa nani?.
“Hata sisi hatujui!’
Mzee Chuma aliuendea ule mwili pembeni ya kitanda upande wa kichwani na kufunua shuka, alipoiona ile sura alipiga kelele mara moja naye alianguka chini na kuzirai.
Kitendo kile kilimshtua kila mmoja aliyekuwepo pale, walijiuliza yule marehemu ana uhusiano gani na wale watu wawili.
Baada ya kupata huduma ya kwanza Anderson alikuwa wa kwanza kupata fahamu kabla ya baba yake. Mmoja wa vijana wake walimuliza bosi wake.
“Vipi bosi kuna nini mboma mnazidi kutuacha njia panda?”
“Huu ni mwaka wetu.”
“Una maana gani?”
Kabla ya machungu kuishaya kufiwa na mke na mtoto nafiwa na mama yangu mzazi na kidonda kikiwa bado ni kibichi nafiwa na mdogo wangu kipenzi huu ni mkosi gani sijui?”
“Ina maana huyu ni mdogo wako?”
“Enhee huyu ni mdogo wangu anayenifuata kwa mara ya pili.”
“Ooh, pole sana.”
“Asante, mpelekeni kwa uchunguzi zaidi na taarifa zake mtaniletea, na pia wengine mjigawe kwa ajili ya maandalizi ya mazishi kwani swala hili lazima lifanywe upesi.”
Anderson na baba yake walirudishwa nyumbani tayari kwa matanga ya vifo vya ghafla vya mama na mdogo wake.
Lilikuwa ni pigo kubwa maishani mwake, watu aliowategemea kwa mengi likiwemo suala la kusimamia ndoa yake na Malaika Mweusi ndio walikuwa wamefariki.
Alijiuliza maswali mengi ya kumweleza Malaika Mweusi kuhusu kifo cha mama yake aliyempenda kupindukia. Hata alipoondoka alimuahidi mkwewe lazima amletee zawadi ambayo hataisahau maishani mwake.
Alizidi kujiulliza kama alivyomweleza vifo vya mkewe na mwanaye tena muda ulikuwa umepita nusura azirai itakuwaje ikiwa atamweleza vifo vya mama yake na mdogo wake.
Anderson akiwa katikati ya mawazo mara simu yake ya mkononi iliita aliichomoa mkononi na kuangalia namba na kugundua ni Malaika Mweusi. Ghafla mapigo ya moyo yalibadili mwelekeo na kwenda kasi. Kama ungekuwa karibu yake ungesikia mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakidunda.
Aliishika ile simu na kuanza kutetemeka, alijiuliza kuwa ataanzaje kumweleza misiba ile miwili. Simu iliita mpaka inakatika akiwa bado ameshikilia, baada ya simu kukatika ndipo akashtuka.
“Ohh shit,” alisema kwa hasira.
Mara iliita tena na safari hii aliipokea na kuzungumza.
“Hallo.”
“Ohh my sweet heart vipii? Mbona hupokei simu au una mtu mwingine? Usiache nikafa kwa presha bure hebu nieleze kwa nini hupokei simu au umeshanichoka… yaaa…ni..”
Malaika Mweusi hakumaliza alianza kulia upande wa pili kitu kilichozidi kumpa ugumu Anderson.
“Si…si hivyo nini najua unipeni.”
“Hapana Malaika wangu hakuna kitu ninachokipenda kama pendo lako nipo tayari kufa ili nisikupoteze wewe ua la moyo wangu, kato la kiu yangu, baridi la joto langu.”
“Sasa kama ni hivyo kwa nini umechelewa kupokea simu mpaka unanipa presha bure?”
“Kuna tatizo?”
“Tatizo tatizo gani tena Yahillah?”
“Mama amepatwa na ajali.”
“Mungu wangu nisaidie aja wako, ajali imetokana na nini na vipi hali yake inaendeleaje?”
“Presha ilimpata ghafla akaendesha moja kwa moja akagonga mti hali yake si nzuri na hajapata kauli mpaka sasa tangu apate ajali.”
“Ooh maskini nakufa mie…sasa mpaka muda huu mmempa msaada gani?”
“Yupo kwenye matibabu ya hali ya juu na madaktari wanahangaikia kuokoa maisha yake.. wewe kwa sasa upo wapi?”
“Nipo Dubai kesho asubuhi nitarejea ili nije kumuuguza mama. .ooh maskini kipenzi changu mama mkwe wangu. Mungu ampe afueni ili apone haraka mwambie mama nampenda sana,” maneno ya Malaika yalikuwa kama mkuki kwa Anderson lakini alijikaza kiume ili asijulikane.
“Kwa hiyo dear nikutegemee kesho?”
“Yaani ingekuwa ni uwezo wangu nisingekuja leo hiihii ila naomba uendelee kunijulisha maendeleo ya mama.”
“Sawa, ngoja nikuache ujiandae na safari.”
“Sawa mpenzi usiku mwema, samahani hapo kwani uko hospitali au nyumbani?”
“Mmh nipo nyumbani nimerudi muda sasa hivi.”
“Ok usiku mwema.”
“Nawe pia, bai.”
Baada ya ukata simu Anderson alishusha pumzi ndefu kama ameshusha mzigo mzito, alijiuliza kuwa akija akikuta kuna msiba sijui itakuwaje au naye ndio presha itampanda liwe pigo la tatu takatifu.
Usiku kucha akupata usingizi akipanga mipango ya kumpokea Malaika Mweusi na namna ya kumweleza kifo cha mkwewe na mdogo wake bila ya upata mshituko wowote ambao utaleta madhara yeyote. Mpaka kunakucha alikuwa macho akipanga hili na lile ambayo yote aliyaona hayafai.
Saa 12.00 alfajiri alikuwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere zamani Dar es Salaam International Air port kumsubiri kipenzi chake Malaika Mweusi.
Malaika Mweusi aliwasili hapo uwanjani saa moja na dakika kumi na kulakiwa na mumewe mtarajiwa Anderson.
Baada ya kukumbatiana na kupigana mabusu na kujuliana hali katika siku zile walizopoteana machoni, swali la Malaika lilimchanganya Anderson.
“Enhe, mpenzi vipi hali ya mama?”
“Mmh hajambo kidogo,” alijibu kwa sauti ya chini.
“Mbona una sita kuna mabadiliko yeyote ya hali yake tangu jana?”
“Aaah! kidogo afadhali.”
“Sasa mpenzi breki ya kwanza ni hospitali kwa mama mkwe.”
“Hapana mpenzi kwanza tuanzie nyumbani kisha hospitali.”
“Hapana, haiwezekani, kwani kuna nini tukienda moja kwa moja hospitalini?”
“Si unajua asubuhi kunakuwa na masuala ya usafi. hivyo haitakuwa vema ni bora tusubiri kidogo.”
“Bora usafi unikute palepale lakini siwezi kwenda nyumbani mpaka nikamuone mama, tafadhali nipeleke hospitali alipolazwa,” Malaika alikuwa mbishi.
Anderson hakuwa na ujanja ilibidi atafute njia nyingine ya kumdanganya ili warudi nyumbani na mambo yote atayajua akikapo huko.
“Ni hivi mpenzi mama yupo nyumbani ndipo anapopata matibabu.”
“Mbona sikuelewi, mara hospitali mara nyumbani nishike lipi sasa?”
“Nyumbani si unajua tena mpenzi nimechanganyikiwa.”
“Pole sana mama anauma sana siwezi kueleza jinsi nilivyoumia.”
Walikubaliana kwenda moja kwa moja hadi nyumbani ambapo ni ukweni. Wakiwa njiani Anderson alikuwa na mawazo ya hali ya Malaika Mweusi atakapogundua mkwewe si mgonjwa bali ni marehemu.
Gari lilisimamishwa mbele ya geti la nyumba wa wazazi wa Anderson na baada ya kufunguliwa waliingia na gari ndani. Mazingira ya pale yalimshangaza haikuwa hali ya ugonjwa bali ni msiba. Wakati wakiteremka kwenye gari Malaika alimuliza Anderson.
“Dear kuna nini kinaendelea mbona sielewi?”
“Uuu…unajua…mama..ma..mama”
“Mama kafanya nini tena mpenzi? Mbona sikuelewi?”
“A..a..me..me.”
“Niambie ukweli mama amefanya nini..mbona unielezi ukweli mama amefanya nini?”
“Samahani mpenzi …mama amefariki.”
“Aaa maskini roho yangu.”
Malaika mweusi alianguka chini na kuzirai, ilibidi ifanywe kazi ya kumwagia maji ya baridi ili kurudisha fahamu zake na baada ya kurudiwa na fahamu alianza kulia tena bila ya kujua msiba si wamama mkwe tu bali na shemeji yake. Taarifa za msiba zilisababishwa akimbizwe hospitali lakini hali yake ilikuwa nzuri kwa muda mfupi na kurudishwa msibani.
Malaika aliamua gharama zote za mazishi ziwe juu yake, yalikuwa ni majeneza yote mawili ya gharama kubwa ambapo kila moja lilikuwa milioni moja na nusu yalikuwa yamenakshiwa kwa dhahabu. Mazishi yalikwenda vizuri na yalifanyika kwenye ua wa nyumban.
Baada ya mazishi ya tofauti makaburi hayakufukiwa na badala yake, juu ya kaburi kiliwekwa kioo kikubwa, yalikuwa ni mazishi ya aina yake yaliyoachwa simulizi midomoni mwa watu.
“Baada ya mazishi Malaika Mweusi alitaka kujua kifo cha shemeji yake kimetokana na nini?”
“kutokana na maelezo aliyoyaacha mwenyewe aliamua kujiua baada ya kugunduakuwa ameatrhirika.”
“Si kweli,” Malaika alikataa.
“Una maana gani?” Anderson aliuliza.
“Kwa nini ukubali kirahisi namna hiyo?”
“Kwa nini usiamini?”
“Labda watu wamemuua na kushinikisha amekufa maji.”
“Maneno yako yanaweza kuwa na ukweli ndani yake lakini kuna ugumu kwani hati ya mwandiko ni wa mdogo wangu na mwandiko wake naufahamu vizuri.”
“Au mmemnyanya paa?”
“Waala, yaani jana ndio nimejua ameathirika.”
“Sasa mpenzi mipango yetu tuisimamishe mpaka hapo tutakapo panga baadaye.”
“Lakini tusichelewe si unajua majonzi juu ya majonzi sina mwingine wa kuniliwaza ila ni wewe?’
“Hilo nalielewa ndio maana nipo pamoja na wewe katika kipindi chote kigumu cha majonzi kwani lako ndio langu.”
“Ndiyo maana nikakuita Malaika Mweusi uliyeletwa duniani kwa ajili ya kunifariji mtu kama mimi.”
“My sweet hivi sasa sisafiri tena hadi nihakikishe upo katika hali yako ya kawaida.”
“Sawa mpenzi.”
Malaika Mweusi alikuwa karibu na Anderson safari ile alilala siku zote kwa mchumba wake lakini ilikuwa kama kawaida yake kuondoka saa kumi alfajiri. Anderson alipenda kujua shughuli za Malaika Mweusi.
“Ni kweli nakupenda na ni vizuri kuelewa utajiri wangu umetokana na nini, lakini ni haraka sana kwa kuwa tupo pamoja taratibu utanielewa tu.”
“Kwa nini usinieleze tatizo ni nini?”
“Utanipenda?”
“Hilo halina kificho.”
“Unaniamini?”
“Nakuamini kwa asilimia mia moja.”
“Hapana hunipendi.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Kwa nini tubishane kwanye jambo ambalo liko wazi?”
“Basi mpenzi nimekuelewa.”
“Si hivyo darling kama hatuaminiani au hauko tayari kunisikiliza kuna umuhimu gani wa kuwa pamoja?”
“Usifike huko mpenzi nimekuelewa naomba unisamehe sipendi kukudhi kwani itakuwa sawa na kuiudhi nafsi yangu.”
Anderson alijikuta hana kauli ya kuhoji chochote cha Malaika Mweusi kitu ambacho kilimtatiza. Japokuwa hakuna alichokikosa kutoka kwa Malaika Mweusi, alipata kila alichotaka huku akilelewa kama yai.
Malaika Mweusi alionyesha mapenzi ya dhati kwa Anderson na kuwa karibu naye katika kipindi chote cha majonzi alimpa ahadi nyingi tu watakapofunga ndoa yao ahadi zilizomtia wazimu Anderson.
Mara nyingi Malaika alipokuwa akienda kulala kwa Anderson alikwenda bila mkoba wake, kitu ambacho Anderson alikuwa amekizoea. Ilikuwa ni jambo la ajabu siku moja Malaika alipokwenda kulala akiwa na mkoba wake, kitu kilichomfanya Anderson kukosa usingizi kwa kutaka kuchunguza kulichokuwa ndani ya mkoba kwani haikuwa kawaida.
Alimtegea Malaika Mweusi alipokuwa amelala kwenye usingizi mzito, aliuchukua mkono wake aliokuwa ameuweka juu ya kifua chake aliuweka juu ya mto na kunyanyuka taratibu hadi kwenye mkoba uliokuwa juu ya droo ya kitanda.
Mawazo yake yalimtuma Malaika anajishughulisha na biashara haramu iliyompa fedha nyingi kwani ni vigumu kwa msichana mdogo kama yule kuwa na pesa kiasi kile ni kazi au biashara ya dawa za kulevya.
Kwa mafunzo yake ya kijeshi aliweza kujitoa kwa Malaika bila kujijua, aliuchukua ule mkoba na kuufunga taratibu kwa tahadhari kubwa.
Ndani ya mkoba ule kulikuwa na pesa nyingi packeti mbili za glovu, kichupa kidogo cha pafyumu kilichokuwa nusu kilichokuwa na marashi ya Kirusi, alijiuliza zile glovu za nini. Kabla hajafanya kitu Malaika alishtuka usingizini kwa haraka Anderson aliingia na ule mkoba chini ya uvungu wa kitanda.
Malaika mweusi alipoangalia pale kitandani alijiona yupo peke yake aliamua kumuita Anderson kwa sauti ya kati.
“Sweetie..”
Anderson alikaa kimya chini ya uvungu huku akijiuliza maswali mengi kuhusu vile vitu vina maana gani, aliona wazi kabisa Malaika anajihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Hofu ilimuingia endapo Malaika atagundua yupo uvunguni? Tena na mkoba wake atamuelewaje.
Malaika baada ya kushtuka usingizini alijiuliza mpenzi wake yupo wapi alimwita tena.
“Sweetie uko wapi?”
Hakuwa na jibu, aliangalia saa yake ndogo ya mkononi ilimuonyesha ni saa tisa na nusu usiku. Alijinyanyua na kujipekecha macho kutokana na usingizi alijua lazima Anderson atakuwa msalani alipitia taulo lake na kwenda msalani.
Anderson aliutumia muda ule kutoka uvunguni mwa kitanda na kurudisha mkoba ulipokuwa na kujilaza kitandani na kujifanya kukoroma.
Malaika alipotoka kuoga alishtuka kumuona Anderson kitandani akiwa katika usingizi mzito. Alijiuliza alipoamka alikuwa na usingizi mzito kichwani uliomfanya ashindwe kumuona. Alijikuta akishindana na mawazo yake kwani alikuwa na uhakika aliamka usingizini Anderson hakuwa kitandani.
Alijua yupo msalani vilevile alishangaa kutomkuta kama alivyotarajia na cha kushangaza zaidi alipotoka kuoga alimkuta kitandani tena kwa usingizi mzito.
Aliyapuuza mawazo yake kwani aliona yanampotezea wakati, hakuwa na haja ya uendelea kulala pale. Alikwenda hadi kitandani wakati huo Anderson alijifanya yupo kwenye usingizi mzito na kumshika mgongoni huku akimtingisha taratibu akimuita.
“Sweet….sweet,” Anderson hakushtuka mapema mpaka alipomuita zaidi ya mara sita na kujifanya anashtuka.
“Eeeh.” Aliitikia huku akijifanya kujigeuza kitandani.
“Sweet” Malaika Mweusi alirudi tena.
“Naam,” aliitika bila kufumbua macho.
“Mi’ ndio naondoka.”
“Kwani saa hizi ni saa ngapi?”
“Kumi kasoro.”
“Kumi kasoro mbona ni usiku sana?” aliuliza huku akifumbua macho na kujifanya kupiga miayo.
“Aah, nimeamua kuondoka tu.”
“Nikusindikize?”
“Hapana we endelea kulala tu.”
Malaika Mweusi alipitia mkoba wake bila kuchunguza alimbusu Anderson na kutoka nje. Nje alisikia sauti ya gari likiondoka. Anderson alikaa kitandani baada ya Malaika kuondoka akiwa na mawazo mengi juu ya vitu alivyovikuta kwenye mkoba. Chupa ya manukato, chupa ya dawa ya sindano yenye maji meupe, bomba la sindano na glovu.
“Hapana kuna haja ya kufuatilia nyendo zake lazima kesho niwape kazi vijana wangu kufuatilia miradi yote iliyo chini ya msichana mdogo lakini mwenye utajiri wa kutisha,” alijisemea kwa sauti ya chini.
Swali lingine lilikuwa ni kuhusu Malaika Mweusi kuondoka ghafla usiku huku akionyesha kitu kama hasira. Alijiuliza inawezekana amepekua mkoba wake na kugundua jambo? Alijua kama itakuwa hivyo basi uhusiano kati yao utaingia ufa au kufa kabisa kwani ni msichana aliyeonyesha msimamo wa hali ya juu.
Alfajiri ilimkuta akiwa macho alioga na kwenda ofisini kwake mapema, kitu kilichomshtua Secretari wake hata vijana wake pia. Hakupoteza muda aliwaita vijana wake na kuwapa jukumu la kufuatilia miradi yote iliyopo chini ya leseni ya TEMA na kuchunguza pia inashughulika na nini ikiwa ni pamoja na kuwahoji kwa siri baadhi ya wafanyakazi na majibu aliyataka jioni ile.
Vijana walitawanyika na kuanza kazi ile mara moja, wengine walianza kwenye miradi wote inayofahamika wengine kwenye ofisi ya kodi ya mapato huku wengine wakiingia kwenye mtandao ili kujua TEMA inashughulika na nini katika mtandao wa www.mate.com.tz.
***
Majira ya saa moja jioni Mr Anderson alikutana na vijana wake ili kumpa majibu ya kazi alizowatuma.
“Vipi jamani za kutwa?”
“Nzuri tu bosi.”
“Eeh mambo yamekwendaje?”
“Si mabaya sana tumepata baadhi ya dondoo nina imani unaweza kupata mwanga wa kitu unachokitaka.”
“Sawa mmefikia wapi?”
“Bosi baada ya kutugawa tumefanya uchunguzi wetu wa kina na kila mmoja akiwa na jukumu lake nina imani kila mmoja wetu mambo yake yamekwenda vizuri,” Alisema Aziz.
“Baada ya kila mmoja kupata alichokidodosa tulikutana pamoja kabla ya kukuletea jibu moja litakalokuwa limejitosheleza,” Aliongezea Suzana aliyekuwa kiongozi.
“Sawa nawasikiliza.”
Taarifa ilionyesha kuwa miradi iliyopo chini ya leseni ya TEMA ni mingi ambayo yote ipo chini ya msichana mmoja mdogo jina lake Tereza Maria Magdalena, anamiliki shule za kimataifa sita, nne zipo jiji la Arusha na moja Mwanza, pia anamiliki viwanda vitano viwili za dawa za binadamu na mifugo kimoja cha plastiki kwa ajili ya kutengenezea bidhaa za maji, biskuti na juisi ambavyo amevitenga mahsusi kwa ajili ya wanawake wajane wenye maisha magumu.
Pia ana hospitali mbili kubwa hapa jijini inayotoa huduma kwa gharama pia alitenga sehemu maalum kwa ajili ya magonjwa ya ukimwi ili afanye kazi nyepesi ambazo hazitawachosha sana. Amejenga vituo ishirini kwa ajili ya kulelea watoto yatima ambavyo vina shule ndani, ni msichana anayeishi katika mazingira ya kawaida hajaolewa.
“Mmedodosa vyanzo vyake vya pesa?”
“Inaonyesha pesa nyingi anapata kwa wafadhili, kuna mashirika zaidi ya ishirini yanatoa pesa zaidi ya dola milioni elfu moja ili kuboresha shughuli zote za kujitolea kama watoto yatima, kuanzisha mfuko wa kuwahudumia wagonjwa wa ukimwi ikiwa ni pamoja na kugawa dawa bure ambazo hununua kwa pesa zake.
“Siku zote NGO’s za nje zinatafuta watu au vikundi vyenye kutoa msaada kwa jamii na kuiongezea nguvu.”
“Miradi mingi ameiongeza baada ya kupata fedha kutoka kwa wafadhili nje kabla ya pesa za wafadhili hizo za kuanzia ametoa wapi?”
“Ukweli hapo hatukupata habari za pesa zake za kuanishia hiyo miradi aliipata wapi.”
“Ok kazi si mbaya ila kesho nataka kupata jibu kuwa pesa za kuanzia alizipata vipi.” “Asante nashukuru kwa kazi nzuri tutaonana kesho.”
Aliagana na vijana wake na kujirudisha nyumbani huku akiwa na mawazo kuhusu utajiri wa kutisha wa Malaika Mweusi. Ni msichana wa ajabu anayeonyesha ni jinsi gani anajali binadamu wenzake ukweli usiopingika kuwa msichana Tereza ni Malaika mwenye umbile la kibinaadamu.
Ni msichana mwenye huruma na mapenzi ya kweli lakini je, chanzo cha utajiri wake kimetokana na nini? Mara nyingi watu wengi wenye roho nzuri walio mstari wa mbele kusaidia jamii misaada yao huwa kama kinga ya kulinda maovu yao lakini nyuma yao ni uozo unaotapisha na kutotamani kuuona wala kusikia.
Anderson alijua kesho yake ni lazima atajua ukweli juu ya chemchemi ya utajiri wa Malaika Mweusi unatokana na nini pia vitu alivyoviona kwenye mkoba vilikuwa na maana gani. Alijikuta akijilaumu ni kwa nini asimulize lakini angeanzia wapi na ni nani aliyempa ruksa ya kupekua mkoba wake bila ya idhini ya mhusika.
Akiwa sebuleni alijikuta kila achokiwaza hakupata jibu kamili, hata usingizi ulivyomchukua hakujua alishtushwa usingizini na sauti ya Malaika Mweusi.
“Sweetie.. vipi ulalaji gani huo kama si askari?”
“Aah! Hivi umekuja muda mrefu, kwani sasa hivi ni saa ngapi?”
“Ni saa tatu kasoro.”
“Mungu wangu kumbe nimelala bila ya kujijua!”
”Pole sana shughuli ya leo ilikuwa nzito nini?”
“Si sana.”
“Ushakula?”
“Bado nilikuwa nakusubiri wewe.”
“Muongo ulijiua nakuja saa ngapi?”
Muda wote hata kama ingekuwa ni alfajiri ningekusubiri tu.”
Walijikuta wakiangua kicheko pamoja na kwenda kuoga, waliporudi walikwenda kwenye mgahawa wa karibu kupata chakula na waliporudi walilala.
Kama kawaida Anderson alipanga kuwa Malaika Mweusi atakapolala atafanya uchunguzi wa kina pamoja na kuandika majina ya chupa zile mbili ili awapelekee wataalam wa maswala ya kemikali.
Kama kawaida alijifanya amelala Malaika Mweusi alipitiwa na usingizi, muda mrefu aliangalia saa ya ukutani akisubiri ifike saa saba ya nusu au nane aamke. Alijitahidi kuwa macho hadi saa sita na nusu aliamua kujinyoosha kidogo na usingizi ukampitia. Aliposhituka macho yake yalikuwa juu ya saa kubwa ya ukutani ikimuonyesha ni kuwa saa nane na nusu saa moja zaidi ya muda aliopanga.
Kitandani alikuwa peke yake alijiuliza Malaika Mweusi amekwenda wapi au msalani. Alisubiri kwa robo saa hakumuona na na alipomuangalia msalani pia hakuwepo. Alijikuta akijiuliza atakuwa amekwenda wapi alizunguka nyumba nzima lakini hakumuona ufunguo ulikuwepo mlangoni na mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.
Anderson aliingiwa na wasiwasi inawezekanaje mtu atoke ndani bila ya kufungua mlango au Malaika Mweusi si binadamu wa kawaida ni jinni. Akiwa kati kati ya mawazo, mara simu yake ililia alipofuata kwenye kitanda na kwenda kuichukua namba zilizokuwa za ofisi. Moyo ulimlipuka usiku kama ule simu ya nini tena na aliinyanyua na kuanza kuongea.
“Enhe lete habari?”
“Bosi habari ni mbaya.”
“John Masu na Mustachi wameuawa.”
“Wameuawa na nani na vifo vyao vimetokana na nini?”
“Bosi usiombe, vita iliyotokea saa moja na nusu iliyopita sijawahi kuiona toka nijiunge na kazi ya jeshi.”
“Ilikuwaje?”
“Tulifanikiwa kuwazingira wauaji waliokuwa wamevamia kanisa shida yao ubwa ilikuwa kumuua Mchungaji Marco Gin.”
“Kwa kuwa tuliwazingira vizuri tulijitahidi kupambana nao na kufanikiwa kuwatia mikononi sita kati ya kumi, tulijua ndio mwisho wao.
“Huwezi kuamini ni vijana wadogo sana hata umri miaka kumi na tano bado tena ni watoto wa kike wazuri lakini wote wana ujuzi wa hali ya juu wa kutumia siraha za aina zote.
“Tukiwa tunasheherekea ushindi mara kuna gari mbili zilifunga breki mbele yetu bila ya kutarajia walianza kutumimia risasi wakiongozwa na wanawake mmoja hatari sana kwa kuwa tulikuwa tumejisahau aliua watu wetu wawili palepale Mustach na John….Masu alimuwahi yule mwanamke alionyesha amevaa nguo nyeusi tupu ya kitambaa cha mpira mwili mzima.
Alimuwahi risasi ya begani ambayo nina uhakika atakuwa amemuua lakini mfuasi wa yule mwanamke alimuwahi risasi iliyohitimisha idadi ya wenzetu watatu.”
“Shughuli bado pevu na kanisani hawakudhuru mtu?”
“Wamekufa walinzi wanane pia wamemjeruhi mchungaji Marco Gin.”
“Vipi hali yake?”
“Bado mbaya.”
“Ok nakuja.”
Wakati anajiandaa mara simu iliita iliingia namba ngeni machoni mwake alipokea na kuongea.
“Haloo… haloo...eeh ndiyo mimi…eti unasema Malaika Mweusi amefanya nini? Hapana…hapana haiwezekani…lazima nije nishuhudie mwenyewe kama ni kweli itakuwa pigo la tatu takatifu,” taarifa zile zilimchanganya Anderson alichanganyikiwa alijikuta anapanda gari na taulo tena kifua wazi.
Taarifa za Malaika Mweusi zilimchanganya kwa kiasi kikubwa na kujiona kiumbe mwenye mkosi mapigo ya moyo yalimtingisha lakini mke wangu na mwanangu na sasa wamemuua kipenzi changu Malaika Mweusi nani sasa atakuwa amebaki kama si mimi mwenyewe?” Anderson alizungumza mwenyewe huku akiendesha gari kuelekea kwenye tukio.
Aliwaza mengi baada ya kupata taarifa za Malaika Mweusi. Akiwa njiani alijigundua kuwa yupo kifua wazi na amevaa taulo tu, hilo hakujali alisimamisha gari mbele ya mapokezi ya Muhimbili na kwenda moja kwa moja mapokezi huku akihema utafikiri alikuwa anatembea kwa miguu na wala hakupanda gari.
“Samahani ndugu kuna taarifa zozote za kipolisi zilizofikishwa hapa?”
“Ndio..ndio.. mzee.”
“Ya kwanza kuna maiti zimeletwa kutoka kwenye eneo la kanisa.”
“Na nyingine?”
“Maiti ya msichana iliyookotwa barabarani.”
“Ooh Mungu wangu ipo wapi?.... ni bora nikaishuhudia mimi mwenyewe.”
“Mzee maiti itakaa wapi zaidi ya monchwari?”
Mr Anderson aliishiwa na nguvu alijikuta anakaa chini, vijana waliokuwepo hospitali walianza kumshangaakumuona bosi wao katika hali ile.
“Vipi bosi mbona upo katika hali hii?”
“Nyie acheni tu mbona mwaka huu wangu?”
“Nini tena bosi?”
“Si shemeji yenu.”
“Nani? Malaika wako?”
“Kuna nani zaidi yake?”
“Kafanya nini?”
“Amekufa…..
Hakumalizia kusema mzee mzima alianza kulia mbele ya vijana wake.
“Utani huo bosi muda si mrefu uliniambia kuwa upo na mamaa kabla ya lile sheshe la maeneo ya kanisani, vipi amevamiwa akiwa nyumbani?”
“Ni historia ya ajabu ngoja niende mochwari nikaishuhudie hiyo maiti kama ni ya Malaika Mweusi.”
Kutokana na kuishiwa nguvu vijana wake walimsaidia kuingia chumba cha maiti ili ashuhudie. Walikwenda hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, mhudumu baada ya kufika alipoulizwa kuhusu kupokea maiti ya mwanamke alisema:
“Kwa kweli nimepokea maiti nyingi sana leo za wanawake sasa sijui mnamhitaji nani labda tumtafute kwa pamoja.”
“Hamna tabu.”
Anderson alijibu huku wakiingia katika chumba cha maiti na kuanza kufungua dro moja hadi nyingine za kuhifadhi maiti zilizoigizwa siku hiyo. Maiti zote walizoziona zilizokuwa ndani ya chumba ajabu hawakuiona ya Malaika Mweusi.
Ilibidi wamuulize vizuri yule mhudumu wa mochwari.
“Mbona bado maiti moja?”
“Maiti gani hiyo?”
“Kati ya zilizoingia usiku huu.”
“Ni hizi tu hakuna nyingine.”
“Hapana bado moja.”
“Labda kama iliingia kabla yangu hebu tuangalie kwenye kitabu.”
Waliongozana moja kwa moja hadi kwenye kitabu cha maiti waliingia usiku ule lakini pia maiti ya Malaika Mweusi haikuwepo ili kumridhisha roho yake waliangalia maiti zote zilizokuwepo bila ya kujali maiti nyingine ambazo zilikuwa zinatisha sana kutokana na majeraha.
Lakini maiti ya Malaika Mweusi haikuwepo, ilibidi kijana wake amulize.
“Kwani bosi, taarifa za kifo ulizipata wapi na kutoka kwa nani?”
“Kuna mtu alinipigia simu akinijulisha kuwa mwili wa Malaika Mweusi umeokotwa ukiwa umelowa damu nyingi kifuani.”
“Alikueleza amepelekwa wapi?”
“Amesema hapahapa Muhimbili.”
“Sasa mbona haupo au yupo wodini?” alitoa wazo.
“Tangu lini maiti akawekwa wodini?” Anderson aliuliza.
“Una uhakika gani kama amekufa labda wingi wa damu tu inawezekana yupo hai au atakuwa amepoteza fahamu wakajua amefariki.”
“Kwa hiyo unaniambia twende wodini tukaulize?” Anderson aliuza swali kama mtoto mdogo.
“Ndio maana yake.”
Waliongozana pamoja hadi wodini na kuliza kama kuna majeruhi yeyote aliyeingizwa usku ule.
“Ni wengi waliovamiwa na majambazi, wapo waliopatwa na ajali pia kuna mwanamke mmoja aliyeokotwa inaonekana alijeruhiwa vibaya na risasi.”
“Eeh, ndiye huyo yupo wapi?” Anderson alirukia.
“Taratibu mzee yupo katika chumba cha wagonjwa mahututi huwezi kuonanana naye kwa sasa.”
“Lakini yupo katika hali gani?”
“Sikudanganyi yupo katika hali mbaya sana kupona kwake ni majaliwa ya Mungu.”
“Mungu wangu sijui itakuwaje!”
“Kwani mzee ni nani yako?”
“Mke wangu.”
“Ina maana haya yote yanatokea alikuwa anatoka wapi?”
“Si wakati wake sasa cha msingi ni kujua hali ya mgonjwa kwanza.”
“Kwa leo hatuna jibu njoo kesho utapata habari kamili za mgonjwa.”
“Jamani hata kumuona kidogo?”
“Sasa itasaidia nini?”
“Angalau nimuone kwa macho roho yangu iamini.”
Anderson aliongozwa na daktari hadi kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kushuhudia Malaika Mweusi akiwa amelala kitandani akipumua kwa msaada wa mashine maalum pia alikuwa ameongezewa damu.
Malaika alikuwa sawa na maiti kwani alikuwa hajui kinachoendelea, Anderson hakuwa na jinsi ilibidi aende nyumbani ili arejee kesho yake kufuatilia hali ya kipenzi chake.
****
Siku ya pili kabla ya kwenda hospitali ili kujua hali ya Malaika Mweusi hata hivyo jibu alilopewa halikuwa na tofauti na la jana kwani hali yake bado ilikuwa ni mbaya sana alikuwa bado anatumia mashine ya kupumulia.
Anderson alirudi ofisini alikuwa mnyonnge kutokana na hali ya kipenzi chake kuwa bado mbaya. Akiwa ofisini alijawa na mawazo mengi juu ya mkasa mzima na mazingira yaliyompata Malaika hadi kufikia kukumbwa na dhahama ile alijiuliza kwa nini aliondoka bila kuaga na gari lake lipo wapi. Baada ya muda mfupi simu yake iliita alinyanyua na kuongea.
“Habari za asubuhi bosi.”
“Nzuri tu.”
“Si kweli, pole sana.”
“Bado sijapoa, ulikuwa unasemaje?”
“Vijana wapo tayari kuonana na wewe.”
“Ooh, wambie waingie.”
Mara mlango uligongwa, vijana saba wa kazi waliingia ambao idadi yao walikuwa kumi lakini wenzao watatu walikufa kwenye mshikemshike wa usiku kuamkia jana yake.
“Habari za asubuhi,” aliwasabahi baada ya kuwaruhusu kukaa chini.
“Nzuri bosi sijui wewe?”
“Zangu ni mbaya kama mlivyosikia.”
“Pole sana inavyoonekana muuaji amepania.”
“Mimi wasiwasi wangu bado kidogo kumtia mikononi hivyo anajiamini ili kukutisha lakini nakuahidi sitaacha kumtafuta hadi damu ya mwisho”.
“Bosi usemayo ninakuunga mkono ni wasiwasi wake tu ndio maana anafanya vitu vya kukutisha,” kijana wake mmoja aliunga mkono.
“Sasa ni hivi, wanne nendeni mkafanye mipango ya mazishi, wawili mtakaa mmoja ndani ya hospitali na wengine nje ili kulinda Malaika wangu asipate shambulio jingine. Mimi na Lyasi tutaongozana hadi kanisani tukapate maelezo ya mchungaji Father Marco Gin labda tutapata picha yeyote.. haya tutawanyikeni tutaonana msibani.”
Anderson baada ya kugawa kazi kwa vijana wake alielekea kanisa kuu la WALIJITOA KWA AJILI YA MUNGU. Moja ya makanisa makubwa sana nchini japokuwa ni geni lilikuwa na tofauti na yanayotangulia kwa muda mfupi ilikusanya waumini wengi kutokana na mfumo mzima wa usambazaji wa neno la Mungu.
Ndiyo kanisa lililokuwa linaongoza kwa msaada na promotion kwa vijana wengi kwenda nje ya nchi kufanya kazi. Pia lilitoa misaada kwa vijana wengi wanawake wajane bila usahau waathirika wa ugonjwa wa ukimwi.
Kanisa lililoongozwa na mchungaji Marco Cin raia wa Marekani lakini aliishi sana nchini Italia ni mtu aliyekuwa na umaarufu mkubwa. Kwa muda wa miaka saba aliweza kufungua matawi mengi nchini mjini na vijijini makanisa ya WALIOJITOA KWA AJILI YA MUNGU yalisambaa nchi nzima.
Jina la Marco Cin lilikuwa kubwa ndani na nje ya nchi kwani alikuwa ni mtu mwenye huruma na mwenye kujali utu wa watu. Alikuwa ni mtu anayeheshimika serikalini.
Kila sehemu walipofungua kanisa sehemu hiyo ilipata maendelea kama huduma za maji, shule, hospitali na huduma za umeme wa jua la solar power.
Sehemu zote hizo vijana wote walipata nafasi za kufanya kazi nje ya nchi hata waliokuwa hawana elimu jambo lililowafanya vijana wengi kwenda katika kanisa hilo.
Mchungaji Marco Cin alifungua miradi mingi ya vijana ili kuwapunguzia ukali wa maisha. Akiwa njiani na kijana wake Anderson alibadilishana naye juu ya wimbi la mauaji yaliyogubika jiji.
“Hivi Lyasi unaweza kujua haya mauaji yanafanywa na mtu mmoja au kikundi cha watu?”
“Yoye mawili yanawezekana.”
“Sasa inamaana haya mauaji ni ya kisasi au?”
“Sidhani kama kuna kisasi cha aina gani hiyo.”
“Sasa unadhani ni nini?”
“Nina wasiwasi mauaji haya yanafanywa na watu tofauti na si mtu mmoja.”
“Unadhani ni kwa nini?”
“Hilo ni swali gumu mkuu ndio maana tunaangaika kutafuta tatizo ili tujue kiini cha matatizo yote.”
Mara simu ya Anderson ililia alipoangalia ilikuwa ya kiofisi aliipokea na kuongea.
“Haloo.. en’hee..lete habari.”
“Bosi gari la Malaika Mweusi limekutwa Kibaha likiwa na alama za risasi na michirizi ya damu maeneo ya mlango wa dereva.”
“Inawezekana wezi walimpora?”
“Ni kweli kabisa mkuu wazo lako halitofautiani na langu kwani inawezekana waliamua kuliacha baada ya upasukiwa na gurudumu moja.”
“Kwa sasa gari hilo lipo wapi?”
“Lipo Kibaha katika kituo cha polisi.”
“Sawa nitalifuata baadae baada ya kupata maelezo kwa mchungaji.”
“Sawa mkuu tunaendelea na uchunguzi zaidi.”
Anderon alikata simu na kumgeukia kijana wake.
“Hivi Lyasi suala la kutaka kuuawa kwa mtu kama Father Gin mtu aliyejitoa kwa ajili ya watu leo hii anataka kuuawa bila ya sababu mbona kama sielewi.”
“Mkuu hii ishu lazima kuna watu hawapendezwi na huduma anazozitoa kwa jamii, siku zote si watu wote wanaopenda maendeleo ya watu.”
“Ni kweli Lyasi lakini ukweli tutaupata kwa mchungaji.”
Wakati huo gari lao lilikuwa limesimama mbele ya lango la kuingilia katika kanisa la WAUMINI WALIOJITOA KWA MUNGU. Baada ya mahojiano na walinzi wa getini waliruhusiwa kuingia ndani. Walipaki gari lao kuelekea kwenye ofisi za kanisa, walipokewa na sister wa kizungu aliyekuwa mapokezi.
“Ooh, karibuni sana,” aliwakaribisha kwa unyenyekevu.
“Asante.”
“Niwasaidie nini?” Anderson alijitambulisha na yule sister alimueleza.
“Mr Anderson subirini kidogo kaeni hapo kwenye kochi..sijui mnatumia kinywaji gani cha moto au baridi?” Walikaribishwa kwenye makochi.
“Asante hatuhitaji kwa sasa.”
“Hapana hii ni kwa ajili yenu hiki ni kinywaji kwa ajili wageni wanaomsubiri Father.”
“Sawa sista tuletee chochote”.
Waliletewa kinywaji baridi, baada ya robo saa walielezwa na yule sister:
“Mchungaji yupo tayari nendeni kwenye chumba cha wageni.”
Alitokea sister mwingine na kuwaongoza hadi kwenye chumba cha maongezi.
Walipoingia ndani walimkuta Father akiwa kwenye kibaiskeli cha matairi manne.
“Ooh! Mr Anderson, karibuni sana.”
Kabla hajajibu simu yake iliita.
“En’heee ndiyo mimi….eti… acha utani Malaika amefanya nini?... ameibiwa hospitalini? Hii kali nakuja sasa hivi. Anderson ilibidi amuage mwenyeji wake Father Gin.
“Vipi ofisa kuna habari gani, naona kama zimekushitua sana?”
“Aaa..a. samahani Father ni habari za kikazi tu nitarudi baadaye.”
“Ooh! Bwana awafikishie salama ili tuonane tena.”
“Asante Father.”
Anderson aliondoka na kijana wake Lyasi kuwahi Muhimbili kupata taarifa rasmi za kutoweka kwa Malaika Mweusi katika mazingira tata.
“Lyasi sasa huu ni mchezo, ina waana watu wote walikuwa wapi mpaka aibiwe?”
“Ndiyo suala la kushangaza mkuu.”
“Unajua Lyasi naona kama utani vile yaani atoweke katika hali kama ile ina maana wale wauaji hawakuridhika baada ya kusikia hakufa?”
“Mkuu mbona kama kitendawili, inavyoonekana hawakutaka kumuibia gari bali nikumuua.”
“Unajua Lyasi kama Malaika Mweusi akiuawa mimi ndiye nitakuwa nimechangia kifo chake,” alisema Anderson.
“Kwa nini mkuu?”
“Baada ya kifo cha mke wangu na mwanangu nilipotaka kumuoa Malaika Mweusi alikataa kwa kuhofia naye anaweza kuuawa.”
“Sasa wewe unahusika kivipi?”
“Nimeshindwa kumlinda vijana wangu safari hii mmeniangusha,” Anderson alisema kwa masikitiko.
“Si hivyo tulijaribu kumlinda kwa karibu sana lakini kwa Malaika Mweusi ilikuwa vigumu kumlinda.”
“Kwa nini?”
“Kwani anaweza kuwapotoea katika mazingira ya ajabu mnabaki mnaulizana amepita wapi!”
“Kuwapotea kivipi?”
“Siku moja baada ya kutoka hapa kwako tulimfuatilia hadi kwenye maegesho ya magari Kinondoni lakini cha kushangaza ndani ya gari alitoka bibi kizee kikongwe ambaye aliingia kwenye gari lingine na kuondoka.”
“En’he ikawaje?”
“Basi mkuu tuliilinda lile gari ili kujua Malaika Mweusi ataenda wapi lakini cha kushangaza hakuonekana kutoka hadi kunakucha na tulipokwenda kwenye lile gari hatukumkuta!!”
“Mmh! Ipo shughuli.”
“Acha hiyo bosi kuna siku moja alituacha hoi watu wote.”
“Ilikuwaje?”
“Kama kawaida alipotoka kwako siku hiyo ilikuwa ni mchana kwa bahati mbaya gari lake liligongana na gari kwa nyuma tena eneo lenyewe lilikuwa na trafic ilibidi amtoe kwenye gari na kumpeleka kituoni.
“Mmh?”
“Tuliona si vyema mama mtarajiwa afikishwe kituoni ni lazima angetuuliza tunafanya kazi gani.”
“Mkamfanyaje sasa?”
“Tulilipita lile gari lilikuwa limembeba Malaika, tulisimamisha trafiki alituelewa na kumuachia, lakiini kilichotokea kilikuwa kama mazingaombwe.”
“Nini kilitokea?”
“Mkuu hakuwa Malaika Mweusi lakini wanafanana sana kwa umbo na sura kopi raiti. Hakuna kutofautisha.”
“Kwa nini msihoji yupo wapi?”
“Tulimhoji mkuu.”
“Akasemaje?”
“Akasema kuwa tumemuacha kwenye gari na tulipokwenda tulimkuta.”
“Hamuoni hapo mlifanya uzembe?”
“Najua utasema uzembe kumlinda Malika Mweusi ni kazi ngumu kwa kweli hatumuelewi vizuri.”
“Kivipi?”
“Anabadilika kama kinyonga.”
“Habadiliki chochote pupa yenu tu kutokuwa makini kwa yale mnayotumwa.”
Wakati huo alikuwa anasimamisha gari mbele ya hospitali ya Muhimbili. Aliteremka harakaharaka na kukimbilia wodini. Alikutana na dokta Bon Mandi ambaye alionekana hajatulia vizuri.
“Vipi Dokta?”
“Hili mzee ni tukio la kigaidi.”
“Una maana gani?”
“Yaani madaktari wote wameleweshwa kwa kupuliziwa dawa.”
“Na mgonjwa?”
“Mzee nikueleze mara ngapi hili ni tukio la kijasusi baada ya kuwalewesha wote na kumuiba mgojwa”
“Wewe ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nipo chumba cha upasuaji, dokta Mbilinyi aliponiletea taarifa kuwa mgonjwa ametoweka.”
“Yeye alijuaje?”
“Dokta Fanuel alikuwa anatoka alimtumia ujumbe kuwa akiingia aende kumjulia hali mgonjwa, alipokwenda wodini alishangaa kuwaona wauguzi wote wakiwa wamejilalia na mgonjwa hakuwepo ndipo aliponiita chumba cha upasuaji na kunieleza yaliyojitokeza.”
“Mpaka sasa mmechukua hatua gani?”
“Tumeitalifu polisi nao wamekuja kufanya uchunguzi wao na kuchukua maneno mawili matatu.”
“Hakuna aliyekufa?”
“Hakuna mheshimiwa.”
“Sawa nitarudi baadaye kupata taarifa zaidi.”
“ Anderson alirudi ofisini na kuanza kuwasema vijana wake.”
“Jamani naona wazi kazi imetushinda ni bora kila mtu akashike jembe akalime sioni umuhimu wa sisi kuwepo hapa zaidi ya kuitia hasara serikali.”
“Bosi hii ngoma ni nzito si ya kitoto kama tunavyofikiria adui tunayepambana naye ana utaalamu wa hali ya juu hivyo sasa hivi si muda wa kufanya kazi kwa kufuatana fuatana kila mtu ahangaike kivyake na kwa mbinu nyingine kabisa ni wazi adui yetu anatuelewa vizuri sana mpaka udhaifu wetu na ndio maana anatuzidi maarifa.
“Sasa kwa mawazo yangu kila mmoja atoweke kijijini na arudi baada ya mwezi mmoja ataleta taarifa kwa wakati wake atakaporudi …..sijui hapo mnasemaje?”
“Wazo lako ni zuri sana kesho baadhi ya watu nitawapa pesa ya kujikimu na kutoweka kijijini kila mtu aje kivyake na kuanza kazi mara moja.”
Anderson aliagana na vijana wake na kurudi nyumbani alipofika nyumbani alishangaa kukuta barua imebandikwa mlangoni kwake. Aliichukua na kuingia nayo ndani kabla hajaisoma ile barua aliyoingia nayo ndani ilikuwa imeandikwa:
Anderson ukaidi wako ndiyo umesababisha lkifo cha Malaikwa Mweusi sasa hili ni onyo usiingilie yasiyo kuhusu ukaidi wako utakufanya kila siku upoteze roho za watu na mwisho wake itakuwa roho yako. Bado tunaipenda hatupendi kuiona inapotea kwa jambo la kuacha kila yamkute basi yakazua mwenyewe siku zote akumulikae wewe mchome kabisa, wacha walinywe wamelikoroga wenyewe.
Ndimi apendaye maisha yako.
Anderson baada ya kuisoma ile barua alishusha pumzi na kujiona sawa na mtu aliye jangwani anayeonekana kwa uwazi. Aliona jinsi adui zake walivyo mzunguka kila kona kuliko yeye anavyowafuata usiku na mchana bila ya kuwaelewa wapo wapi.
Vita aliiona ni nzito aliifananisha na mpiganaji aliyefungwa kitambaa machoni na kupigana na mtu anayeona tena ana nguvu za ziada.
Lakini alijipa moyo kuwa anamtafuta muuaji wake hadi tone la mwisho la damu yake. Hakuona hasara kwani mama yake mdogo wake mkewe, mwanaye na kipenzi chake Malaika mweusi hawapo, akuona ubaya naye kuwafuata.
***
Siku ya pili alikwenda kanisa la WALIOJITOLEA KWA AJILI YA MUNGU ili apate mawili matatu kwa Father Gin.
Kama kawaida alikaribishwa na sister wa Kiswahili na kuletewa kinywaji baridi, wakiwa katikati ya vinywaji alikuja sister mwingine na kuwaomba waongozane hadi chumba cha maongezi na baada ya salamu zilipita kama dakika ishirini hivi ndiyo Father Gin alitokea akiwa kwenye kiti chake cha magurudumu(wheel chair) alipowaona tu aliwakaribisha kwa furaha.
“Ooh! Wapendwa karibuni sana.”
“Asante Father.”
“Za tokea jana, safari yenu ilikuwa yenye amani?”
“Ndiyo Father Gin.”
“Ooh, karibu sana.”
“Asante samahani Father.”
“Bila ya samahani.”
“Tulikuwa tunaomba kupata maelezo yako kutokana na sakata la juzi.”
“Kwa kweli siwezi ulieleza kwa undani zaidi kwa kuwa mengine siyajui ninachokumbuka nilitoka kwenye gari ili niwaangalie vijana waliokuwa wamelewa lakini baadaye niligundua hawajalewa bali dhamira yao ilikuwa ni kufanya mauaji.”
“Unafikiri nani mlengwa wa mauaji hayo?”
“Sijui labda ni mimi.”
“Unakumbuka sura zao?”
“Ni vigumu kwani ilikuwa ni usiku wa giza.”
“Pole sana Father Mungu atakusaidia upone haraka.”
”Amen, nanyi pia ila nitawaombea wote waliofanya unyama huu Mungu awarudishe kwani awana tofauti na kipofu anayehitaji msaada wa kuongozwa hata bwana yetu Yesu Kristo amefundisha kusamehe kwani wengi wetu hatujui tutendalo.”
“Ni kweli lakini watu hawa wakikamatwa ni lazima wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”
“Hiyo ndiyo hukumu ya sheria.”
“Unasema baada ya kukugundua watu hao si walevi ulifanya nini?”
“Kwa kweli nilichelewa nilihisi maumivu upande wa bega la kulia na kilichoendelea sikujua mpaka nilipojikuta nipo Hospitali.”
“Pole sana Father Gin ila tutakapokuwa na shida na wewe tutarudi tena.”
“Hakuna tatizo karibuni sana Bwana atawaongoza mfike salama.”
Anderson aliagana na Father Gin na kuelekea ofisini kwake akiwa hajapata mwanga wowote wa kumsaidia katika uchunguzi wake.
Njiani alijawa na mambo mengi na moja ni kifo cha Malaika Mweusi ilikuwa ni vigumu kukubaliana adui yake kuwa ndiye mhusika mkubwa wa mauaji yote. Lakini mauaji yalianza kabla ya kuanza upelelezi pia alijua kurudi nyuma ni sawasawa na kusaliti jeshi.
Mwezi ulikatika bila ya matukio yoyote ya mauaji, mji ulikuwa shwari lakini Anderson muda wote roho ilikuwa juu safari hii kuwa ni nani atakayefuata kufa. Vijana nao waliangaika huku na huko kutafuta taarifa zozote zitakazo wasaidia jeshi kuwatia mikononi watuhumiwa.
Kilichomshangaza juu ya taarifa za vitisho toka kwa mtu anayejiita mtetezi wa haki za binaadamu siri zote za vijana wake zilikuwa hadharani japo kila mmoja alirudi kwa wakati wake.
Alijiuliza ina maana muuaji amekuwa na uwezo gani wa kujua siri yao. Kidogo alianza kuuona ugumu wa kumtia mikononi muuaji, lakini hiyo haikumkatisha tamaa ya kuendelea na uchunguzi wake kwani hakuwa tayari kusalimu amri.
MWAKA MMOJA BAADAYE
Anderson akiwa amekwisha kata tama ya kumkamata muuaji wake, kipindi chote cha mwaka mzima kilikuwa shwari amani ilijirudia hapakuwa na taarifa za mauaji kitu kilichomfanya Anderson na vijana wake kulala usingizi. Siku zote alijipa matumaini adui yake amesitisha mauaji baada ya kuona yupo mbioni kutiwa nguvuni na askari wa upelelezi.
Taarifa zilizomfikia zilimtibua akili yake kuwa nyumba zote na vituo vya mafuta vinavyomilikiwa na tajiri mmoja wa kiarabu vimelipuliwa na mabomu na kusabaabisha hasara kubwa pamoja na kupoteza maisha ya watu zaidi ya mia moja akiwemo tajiri na familia yake.
Kazi aliiona ni nzito mbele yake kweli kimya kingi kilikuwa na mshindo mkubwa.
Kama kawaida vijana wake waliendelea na upelelezi wao naye alichukua maelezo muhimu ambayo aliyafanyia kazi.
Aliamua kurudi nyumbani kwani tukio lile lilimshtua sana hakutegemea, aliendesha gari lake hadi kwenye baa na kuagiza kinywaji baridi ili kutuliza akili yake ambayo nusura ipasue kichwa kutokana na mawazo.
Baada ya kuridhika na kinywaji chake aliingia ndani ya gari lake na kuondoka kuelekea nyumbani kujipumzisha akijua wazi kuwa hana ujanja wowote wa kumkwepa muuaji anayemfahamu kama kiganja cha mkono.
Alifika kwake majira ya saa tatu na nusu usiku alishangaa kukuta taa ndani inawaka huku kukiwa na sauti ya muziki ukilia. Alijiuliza ina maana wakati anaondoka asubuhi alisahau kuzima taa na bila kuzima redio.
Lakini hata hivyo akili yake ilishindana na mawazo yake kwani alikuwa na uhakika kuwa alipoondoka asubuhi alizima taa na kuzima redio. Baada ya kupaki gari lake alikwenda hadi mlangoni alitoa ufunguo na kufungua. Alipoingia sebuleni alishangaa hali aliyoikuta, ilikuwa na usafi wa hali ya juu alijiuliza ni nani aliyefanya usafi ule.
Kilichomshangaza zaidi ni kuwa funguo za nyumba alikuwa nazo yeye na marehemu Malaika Mweusi. Alijiuliza maswali mengi atakuwa nani, muziki wa taratibu uliendelea kulia chumbani mlango ulikuwa umeegeshwa tu aliusukuma na kuingia ndani.
Alishtuka kumkuta mwanamke amelala kitandani akiwa amevaa night dress alikuwa amempa mgongo amelala kifudifudi huku akiwa ameukumbatia mto alijiuliza kuwa huyu mwanamke atakuwa nani, tangu afariki Malaika Mweusi hakuwa na uhusiano na kiumbe chochote cha kike.
“Mmh!… atakuwa nani….mbona kama a..a..ana..fa..fanana…. hapana….. haiwezekani kuwa yeye sasa ni nani au jini nipige kelele…mmh! Ngoja,” alijikuta akiwaza vitu vingi.
Kwa ujasiri mkubwa alisogea kitandani kwa mwendo wa kunyata, alisimama pembeni ya kitanda huku akitetemeka na kumshika bega aliyelala ili amuulize. Pombe zote zilimtoka.
Anderson alipotaka kumgusa yule mwanamke aliyekuwa amelala kitandani roho ilisita. Alimwangalia kwanza usoni ili ajue ni nani hasa, huku akihema kwa hofu ya kutaka kujua ni nani, alizunguka upande wa pili wa kitanda yule mwanamke alipokuwa ameelekeza uso wake, baada ya kumuona alijikuta akipingana na mawazo yake.
''Mmmh haiwezekani...haiwezekani hawezi kuwa ni yeye huu lazima utakuwa ni mzimu wake...sijui nifanyaje.''
Akiwa katikati ya mawazo mara yule mwanamke alijigeuza na kufumbua macho yake yalikutana sawia na ya Anderson.
"Ooh! My sweet! Umerudi?! Karibu sana mpenzi wangu my husband to be'',alisema yule mwanamke ambaye hakuwa mwingine bali ni Malaika Mweusi.
''Hapana si wewe,'Anderson aling`aka.
''Kusema sio mimi una maana gani?''
''Wewe ni mzimu!''
''My sweet Ander mbona sikuelewi? Kwa nini unanifananisha na mzimu?''
''Wewe ni kivuli cha mzimu wa mpenzi wangu Malaika Mweusi!''
''Ni nani amekueleza kuwa nimekufa?''
''Hao waliokuua''
''Anderon mimi sijafa kama hao watu wanavyonizushia.”
''Kama hujafa ulikuwa wapi?!''
''Ni historia ndefu inahitaji nafasi zaidi ya kuzungumza, maadam tuko pamoja utanielewa vizuri na utajua baada ya kupigwa risasi na kutoroshwa hospitali nilikuwa wapi katika kipindi cha mwaka mzima.”
''Pamoja na maelezo yako yanalingana na ukweli lakini mimi bado sikuamini.”
''Naomba uniamini mimi si mzimu bali ni yule Malaika wako aliye hai na wala si kivuli cha mfu,” Malaika kwa sauti tamu.
Malaika Mweusi alinyanyuka kitandani alipokuwa amekaa na kumfuataAnderson amkumbatie lakini Anderson aliruka nyuma kwa hofu.
''Mpenzi usiniogope mimi ni yuleyule malaika wako.'' Alizungumza huku akimshika mabega Anderson na mkono mmoja akiuzungusha shingoni ili amkumbatie.
''Mpenzi hawakuwahi kuniua niliokolewa, onyesha furaha kuniona au ulipenda nife? Haya basi nitakunywa sumu mbele yako ili ushuhudie kifo changu na wala hutaona mzimu wangu.''
''Nina imani hutaona huo mzimu wangu unaoufikiria, nifanye nini ili unielewe? Mimi mzima,naona sina budi kuiaminisha akili yako kuwa mimi si mfu hadi utakapoiona maiti yangu mbele yako.”
Kauli ile ilimshitua Anderson, wakati huo Malaika Mweusi alikuwa akijitoa kifuani kwake. Kwa muda mfupi machozi yalilowesha shati la Anderson.
Hali ya Malaika Mweusi ilimchanganya ilibidi awe mpole kwani hali aliyoionyesha ilimtisha.
“Si hivyo Malaika wangu lilikuwa ni jambo la ajabu kwa mtu aliyejua umekufa kisha baada ya mwaka nikuone ukiwa hai.”
''Ni kweli kama ulielezwa hivyo lazima uwe na wasiwasi, ni kweli nilinusa mauti baada ya kupigwa risasi begani na watu walionipora gari yangu lakini Mungu mkubwa ameokoa maisha yangu.”
''Basi yameisha mpenzi wangu karibu sana jisikie kama uko kwako kwa mara nyingine tena,” Anderson aliyasema huku akimkumbatia Malaika Mweusi aliyejilaza kifuani.
***
Malaika Mweusi akiwa amerudi tena kwa mara nyingine baada ya mapumziko Anderson alitaka kujua ilikuwaje mpaka tukio lile likamkuta baada ya kuondoka bila ya kuaga tena katikati ya usiku mkubwa kama ule.
''Unajua mpenzi mapenzi yangu mazito kwako ndiyo yaliyosababisha yanikute yaliyonikuta.”
''Una maana gani kusema hivyo?”
''Nilikuwa nimelala nilipigiwa simu kuwa kama nitaendelea kulala humu ndani basi tutakufa wote nyumba ilikuwa imetegwa kwa bomu.”
''Ni nani aliyekupigia simu?''
“Kwa kweli simjui.”
“Wewe uliamini vipi na kwanini hukunieleza.”
''Alinitisha kuwa kama nitachelewa bomu lingelipuka muda uleule.”
“Uliamini vipi?”
''Kutokana na matukio yanayoendelea kutokea upande wako.”
''Kwa nini hukunieleza?”
“Lazima pangetokea ubishi kati ya mimi na wewe hivyo ingefanya tupoteze muda na kufanya nyumba yetu ilipuliwe na kupoteza maisha yetu hatuna ujanja zaidi ya mimi kuondoka.”
''Ee’he baada ya kuondoka nini lilitokea?”
''Inavyoonesha muuaji hataki kukudhuru bali kuiteketeza familia yako na watu waliokuzunguka shida yake ni kunitoa pale na kuniua.”
“Ikawaje baada ya kutoka kwangu.”
“Nikiwa naelekea kwangu mara gari mbili zilinipita na kusimama mbele yangu kitu kilichonifanya na mimi nisimame kwani hapakuwa na njia ya kupita.”
" Mara nilisikia milio ya risasi ikipigwa kwenye gari langu kabla sijaamua nini cha kufanya nilipigwa risasi ya bega. Kutokana na kuvuja damu nyingi pamoja na jeraha walijua nimeua ndipo waliponitoa garini na kunitupa chini na kuondoka na gari langu zaidi ya hapo sikujua nini kilichoendelea mpaka miezi miwili ndipo nilipopata fahamu na kujua hapa ni wapi.
“Nilijua nipo hospitali lakini sikujua ni wapi wakati huo nilikuwa napata huduma ya hali ya juu. Nilirudishwa kwenye hospital ya dini inayomilikiwa na shirika moja la kidini. Nilielezwa kuwa pale ni nchini Kenya niliokotwa kwenye gari lililokuwa lipo kama gari la wagonjwa baada ya lile gari kupata ajali na wahusika kukimbia.
“Baada ya kupona nilirudishwa Tanzania nilipofika tu niliamua kwenda kuishi nchini Marekani nilikuwa na mawazo mengi juu yako nilijua kuwa nilikuacha kwenye hali mbaya na maswali mengi kichwani mwangu.
“Kwa kweli niliamua kurudi nchini nakuamua kama kufa bora tufa wote ndio maana nimeamua kurudi mikononi mwako sitaogopa vitisho vyovyote nakuahidi mpenzi kwanzia leo hii nitakuwa kifuani kwako sitaachana na wewe hadi kifo,” Malaika alisema kwa hisia kali.
''Mpenzi kwanza pole kwa yote yaliyokukuta nina imani Mugu yuko ndani yako hivyo hutapungukiwa na kitu na maisha yako bado ni marefu Mungu atuhepushe na mabaya yote.”
Penzi la Anderson na Malaika Mweusi lizaliwa upya, tabia ya Malaika Mweusi ilikuwa ile ile ya kuondoka usiku wa manane. Baada ya muda walikwenda kumtembelea baba mzaa chema akiwa na kipenzi chake Malaika Mweusi.
Siku hiyo aliongea mengi pamoja na mipango ya harusi yao ambayo walipanga kufanya miezi mitatu ijayo. Pia siku ile ilihitimmishwa usiku na Malaika kumpa penzi zito Anderson lililomrusha akili na kujiuliza alikuwa wapi siku zote kumpa penzi tamu kama lile.
Hata asubuhi Malaika alipoamka ili amuage sauti yake ilitoka kivivu kwani mwili wake ulikuwa umechoka kwa patashika ya usiku. Baada ya Malaika kuondoka aliendelea kujilaza kwa uchovu.
***
MlLIO wa simu ulimshtua mkuu wa upelelezi aliyekuwa katikati ya usingizi, alipotupa macho yake kwenye saa ndogo iliyokuwa juu ya droo ya kitanda ilimuonyesha kuwa ni saa tisa na robo usiku ikiwa ni nusu saa tangu amsindikize Malaika Mweusi.
Aliinyanyua simu yake iliyokuwa pembeni ya mto aliokuwa ameulalia, ilimuonesha ni simu maalumu kutoka ofisini, mara nyingi simu hiyo hutumika kwa ajili ya dharura hasa pale panapotokea matatizo yasiyokuwa ya kawaida.
Alibofya kitufe cha kupokelea simu na kuzungumza kwa sauti ya uchovu kwani shughuli ya usiku haikuwa ya kitoto iliyongonyesha mwili. Mwanaume yeyote asingeweza kujizuia kutangaza ndoa kwa binti anayetoka katika familia ya kitajiri. Akizungumza kwa sauti ya kivivu :
“Ndiyo nakupata leta habari.”
“Afande mambo yameharibika .“
“Wapi tena?”
" Hakimu ."
"Ooh Mungu wangu!.. hii sasa inatisha ! tukutane ofisini sasa hivi."
Anderson alikwenda bafuni kuoga haraka haraka na kubadili nguo, wakati akitoka nje aliuona mkoba wa Malaika Mweusi ukiwa juu ya kochi.
Wakati akitoka aliwaza sana kuhusu ile pochi ya Malaika Mweusi.
" Aah kumbe jana alisahau pochi yake sio mbaya ataukuta jioni. "
Alikwenda hadi kwenye banda la gari yake na kulichukua tayari kwa safari ya ofisini. Saa yake ya mkononi ilimuonyesha kuwa ni 11:35 alfajiri. Akiwa njiani aliwaza mambo mengi kuhusu vifo vya kutisha vya mfululizo ni vifo ambavyo vinamchanganya yeye na vijana wake.
Alipofika ofisini alimkuta ofisa mpelelezi na vijana wake wakiwa wameashafika ofisini. Alipoingia wote walisimama baada ya kukaa aliwaamuru nao wakae chini.
"Ndio jamani leteni habari."
" Mkuu kama uliovyosikia yule hakimu ameuwawa si chini ya saa sita zilizopita. "
" Saa sita ina maana ilikuwaje hadi ikachelewa kujulikana?"
"Inavyo semekana amekutwa amekutwa amekufa katika gari lake ambalo lilkuwa limeegeshwa pembeni mwa barabara."
"Ni nani aliyegundua mwili wa marehemu kwenye gari?"
"Ni askari wa dori ambao walikuwa wanakipita kila mara lile gari, walipoamua kulichunguza ndipo walipogundua ni mwili wa hakimu.”
"Lakini ni lazima tukubali kuwa tumefanya uzembe wa hali ya juu kutokana na kifo cha hakimu."
" Kwa kweli bosi sidhani kama tumehusika pamoja na muuaji kutoa vitisho miezi miwili iliyopita nina imani tulimpa tahadhari na kumwelekeza sehemu na muda anaotakiwa kuwa nje ya nyumba yake nina imani kifo chake amekitengeneza yeye mwenyewe."
“Sawa lakini muuaji ni nani? hivi vifo vinahusiana na nini?"
" Sidhani lakini la muhimu tuwahoji wale ndugu wa yule bwana, inasemekana hakuwatendewa haki na muuaji alihidi pindi hakimu akipandisha , basi sheria itamuhukumu yeye."
“'Lakini si tuliwahoji mapema wao wakasema hawana uhusiano wowote wala tarifa yoyote kutoka kwa muuaji?"
" Kwani mara ya mwisho hakimu alikuwa wapi?"
"Job Pub"
"Sawa, kuna umuhimu wa kuwahoji watu waliokuwepo pale JobPub ili kujua kuwa aliondoka saa ngapi na aliongozana na nani."
" Sawa mkuu tutaifanya kazi hiyo."
" Haya majibu nayataka kabla ya saa moja usiku sawa jamani?"
Mkuu wa upelelezi Anderson aliagana na vijiana wake na kuondoka kurudi nyumbani huku akiwa amejawa na mawazo mengi kuhusu mauaji ya kutisha, alijiuliza muuaji ni nani.
“Kama kamuua hakimu kwa ajili ya kupandisha sheria na hao wengine vifo vyao vimet okana na nini, kikiwemo cha mkewe na mwanaye mpenzi Gift.”
Alijiapiza kuwa siku atakayo mtia mikononi muuaji huyo ama zake au za muaji. Alipofika nyumbani alikuwa amechoka akili na mwili, alijitupa kwenye kochi na usingizi mzito ukamchukua. Alishtuka usingizini majira ya jioni na kujiona amelala muda mrefu na ilikuwa imebaki nusu saa tu akutane na vijana wake kumpa taarifa za hakimu aliyeuwawa usiku wa kuamkia siku hiyo.
Kama kawaida alikwenda kuoga na kubadili nguo tayari kwenda ofisini, kilichiomvutia wakati anataka kutoka ni mkoba wa Malaika Mweusi. Aliangalia saa yake ilimuonyesha bado dakika ishirini, alijua ni muda wa dakika kama tano hivi kwa mwendo wa gari angefika ofisini.
Aliamua kuipekua ile pochi ili ajue kuna vitu gani pengine angegundua siri yoyote kuhusu msichana yule kutokana na siku moja kukutana na vitu vilivyo mchanganya kwenye pochi ya Malaika. Alijua kuwa ule ndio wakati wa kufanya uchunguzi wa kina .
Dakika kumi zingemtosha kufanya upekuzi wa harakaharaka , ndani ya lile pochi alikuta na cheni isiyopungua thamani ya shilingi milioni mbili na nusu simu ya mkononi aina ya samsung yenye thamani ya shilingi milioni moja na nusu lakini ilikuwa haina laini.
Katika kimfuko kidogo alikuta kijitabu kidogo (note book) alikifungua nakuanza kukisoma karatasi moja baada ya jingine. Ilionyesha namna ya miradi yake mingi yenye thamani ya mamilioni ya shilingi. Aliendelea kusoma kalatasi za mbele alikut5ana na majina ya watu yaliyoandikwa na wino wa bluu.
Lakini asilimia kubwa ya majina hayo yalikuwa yamezungushiwa wino mwekundu na majina mawili tu ndiyo yaliyo kuwa hayajazungushiwa wino mwekundu.
Majina yale yaliushtua moyo wake na kusababisha mwili wote kusisimka na jasho jembamba likimvuja juu ya paji la uso. Aliyarudia yale majina zaidi ya mara tano na jibu likuwa lilelile alichokisoma machoni mwake kilikuwa sahihi.
Yalikuwa ni majina baadhi ya wale wote waliouwawa na kumchanganya na kushindwa kumtambua muuaji na mbele ya majina yale kulikuwa na tarehe na siku mauaji yaliyofanyika. Ndani ya majina yale kulikuwepo jina la marehemu mama yake, siku na tarehe aliyouwawa , japo alijuwa mama yake alikufa kwa ajali ya gari.
Jina jingine lilikuwa la mdogo wake aliyeuwawa katika mazingira ya kutatanisha. Mwili wake ulikutwa kwenye bwawa la maji machafu.
Pia tarehe ya vifo vya mkewe na mwanaye vilivyotokea siku moja ambavyo vilimuuma sana na kumchanganya akili kwani mkewe aliuawa kikatili kupasuliwa matumbo na sehemu za siri na kisha kupigiliwa kipande cha mti.
Alikumbuka alivyouapia mwili wa mkewe na mwanaye siku za kuuaga kwamba atamtafuta muuaji na kutia hatiani kwa mkono wake mwenyewe.
Alijikuta katika mawazo mengi juu ya kile kitabu cha majina na Malaika Mweusi vina uhusiano gani.
Ajiuiiza kama atakuwa amehusika na vifo vile au la, hakukubaliana na akili yakekuwa Malaika Mweusi anahusika kwa vile alikuwa ni msichana aliyemuamini na kumuona kuwa ndiye aliyeziba pengo la marehemu mkewe hadi akafikia hatua ya kumtambulisha kwa wazazi wake ambao nao waliwapa baraka zote ili wafunge ndoa.
Kile kitabu kiliichanganya a kili yake, kwani hata mama yake kabla ya kifo chake alionyesha mapenzi mazito kwa Malaika Mweusi na alimsifia mwanaye kwa chaguo lake zuri la msichana mzuri mwenye tabia njema.
Alijikuta akisema kwa sauti :
"Hapana haiwezekani Malaika Mweusi akafanya hivi ila nina imani atakuwa anamjua muuaji lazima nipate ukweli kupitia kwake."
Jasho lilikuwa linamtoka chapachapa kama alifungiwa katika chumba chenye joto kali aliendelea kusoma kile kitabu na majina ya mwisho mawili yaliyobaki ambayo hayakuwa yamezungushiwa wino mwekundu, lilikuwepo jina la baba yake mzazi alijikuta akibwatuka.
“Ha! Na baba?" Tarehe iliyopo mbele ya jina la baba yake ilikuwa ni siku ileile alisema tena kwa sauti:
"Hapana haiwezekani na baba tena hapana."
Alitoa simu yake ya mkononi na kubonyeza namba za baba yake ili kumjulisha awe makini kwani kifo kilikuwa kinamnyemelea. Alipopiga iliita bila kupokelewa mpaka ikakatika. Alijikuta akitoka kwa mwendo wa kuruka hadi katika gari lake na kuliondoa katika mwendo wa kasi mithili ya ndege za kivita ili kuwahi kuokoa maisha ya baba yake.
Ndani ya dakika ishirini alikuwa anaelekea kwa baba yake, aliachana na njia kuu na kufuata njia ndogo kuelekea kwa wazazi wake. Kwa vile njia ilikuwa ni ya kupita gari moja mbele yake kulikuwa na gari limeharibika.
Hata bila ya kuchomoa funguo ya gari aliteremka na kuanza kukimbia kuelekea kwa baba yake, njiani alikutana na mwanamke kama Malaika Mweusi, lakini hakumjali zaidi ya kuwahi kuokoa maisha ya baba yake. Nyumba ya baba yake ilikuwa giza aliingia ndani ya geti na kwenda moja kwa moja hadi ndani, alimuita baba yake lakini hakukukuwa na majibu.
Alikwenda hadi sebuleni na kuwasha taa ilikuwa tupu na hakukuwa na mtu yeyote, alielekea chumbani kwa baba yake.
Mlangoni alikutana na michirizi ya damu lakini chumbani kwa baba yake kulikuwa na giza. Ile damu ilimfanya aione hali ya hatari mbele yake
Alitoa bastola na kuingia kwa tahadhari kubwa alipapasa ukutani na kufanikiwa kuwasha taa hakuamini macho yake palepale alishuhudia mwili wa baba yake ulikuwa umelazwa kitandani ukiwa mtupu kama alivyozaliwa.
Sehemu zake za siri zilikuwa zimetenganishwa na kisu kilikuwa kimemchoma katikati ya moyo wake, macho yalikuwa yamemtoka akionyesha kuwa amekufa kwa mateso makali. Damu ilikuwa mbichi na mwili wake ulikuwa bado una joto. Chumba chote kilikuwa kinanuka damu mbichi.
Anderson aliuvamia mwili wa baba yake na kulalia na huku akiendelea kuapa atamshikisha adabu aliyetenda kosa hilo. Alitoka harakahara ili aanze msako wa Malaika Mweusi ili apate ukweli wa vifo vyote. Lakini alikataa katakata muuaji anaweza kuwa mpenzi wake.
Kwa vile nguo zake zilikuwa zimetapakaa damu ya baba yake aliwapigia simu vijana wake waje kuchukua mwili wa marehemu baba yake kuupeleka hospitali.
****
Anderson alipokuwa njiani anarudi nyumbani alijawa na mawazo mengi juu ya ile note book ya Malaika Mweusi ina uhusiano gani na mauuaji yaliyotokea. Akili na mawazo vilishindana na alichokuwa anafikiria, aliwaza:
“Hivi kile kitabu kina maana gani? Inawezekana Malaika Mweusi akawa ni muuaji? …. Hapana …..Si Malaika atakuwa ni mtu mwingine ….. lakini muuaji anamjua sina budi kuyaweka mapenzi pembeni nimbane anieleze muaji ni nani.”
Alisimamisha gari mbele ya nyumba yake na kuwahi kile kitabu ili apate ushaidi… kama kawaida mlango ulikuwa umerudishwa na taa ilikuwa ikiwaka huku muziki mwororo ukilindima kwa mbali.
Hakuwa na swali la kujiuliza kuwa ni nani, alijua atakuwa ni Malaika. Harakaharaka aliwahi mezani kile kitabu lakini hakikuwepo. Alijilaumu kwa kuacha ushidi na kukimbilia eneo la tukio. Akiwa ameshika kiuno na nguvu zimemwishia baada ya kufanya uzembe wa hali ya juu kuacha ushaidi ambao ungemsaidia kumbana Malaika.
Mara alitokea Malaika Mweusi akiwa amejifunga taulo akionyesha anatoka kuoga.
“Ooh! My husband to be huyooo,” akiwa anamfuata kumkumbatia alishtuka kuona nguo za mpenzi wake zina damu.
“ Ha! Sweet nini tena hiki?” Malaika alikuliza kwa mshangao.
“Unamuuliza nani, hujui?”
“Kama ningekuwa najua nisingekuuliza hebu nijulishe nini kimekusibu mume wangu? “
“Naomba kile kitabu kilichokuwa juu ya meza.”
“kitabu gani?”
“Ulichokichukuwa .“
“Mbona sikijui sweet”
“Utanieleza majina yaliyokuwemo kwenye kitabu chako yanahusiana vipi na mauaji yote ya raia wasio na hatia na familia yangu yote.”
“Sweet upo sawa mbona naona kama umelewa mbona maneno yako siyaelewi? “
“Eti? “
Kofi zito lilitua kwenye shavu la kushoto la Malaika Mweusi lililompeleka chini.
“ Nataka kitabu na maelezo ya mauaji yote yaliyotokea la sivyo wewe utawafuata hao waliotangulia.”
“Mpenzi mimi sijui lolote utaniumiza bure. “
“Aha unafanya masihara eeh na damu za watu basi leo utanijua mimi ni nani ?”
Alimfuta pale chini Malaika Mweusi alipokuwa amelala na kumnyanyua juu na kumuuliza kwa ukali.
“Utanipa kitabu hunipi?”
“Kitabu kipi na nikitoe wapi?” Malaika bado aliendelea kukataa.
Anderson alimuongeza kofi jingine lililomtoa damu puani na mdomoni. Siku zote unapotaka kumuua nyani usimuangalie usoni. Alimfuata tena pale chini na kumnyanyua.
“Nieleze nani kamuua baba yangu?”
“Sijui.”
“Teddy nitakuumiza sema ukweli,” Anderson mapenzi yote kwa Malaika yaliisha.
“Sijui lolote wewe fanya upendavyo hata ukitaka kuniua niuue.“
Kauli ile ilimzidi kumuongezea hasira Anderson alimtikisa kwa nguvu na kumsukumia ukutani Malaika Mweusi alijigonga kichwani na kupasuka.
Damu nyingi zilimtoka akiwa mtupu na kumlaza kwenye zulia wakati huo alikuwa amelegea na kuhema kwa mbali.
Aliwapigia simu vijana wake waje kumchukua, mara ghafla umeme ulikatika kwa dakika moja na uliporudi Malaika Mweusi hakuwepo.
Itaendelea
Your Thoughts