HADITHI: MALAIKA MWEUSI
FINAL EPISODE
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500
ILIPOISHIA:EPISODE 9
Marry White alipowaamuru waniache akavua nguo zake na kubakia na 'skin tight' iliyombana vyema na kuanza upya mpambano.
Mwanzo tulipigana vilivyo kila mtu alionyesha uwezo wake, lakini kwa vile nilikuwa nimepigana kwa kipindi kirefu nilikuwa nimechoka sana. Hali ile ilimpa nafasi Marry White kunipa kipigo mpaka nikapoteza fahamu.
SASA ENDELEA...
Nilipozinduka nikijikuta nimefungwa kwenye nguzo yenye umbile la msalaba nikiwa mtupu kama nilivyozaliwa. Mazingira yaliyokuwepo kuokoka kwangu kulitegemea miujiza ya Mungu tu na si kitu kingine.
Kwani sikuwa na mtu aliyekuwa ananifuatilia au kunilinda nilikuwa peke yangu mahali pale. Nilikuwa nimefungwa kwa kamba madhubuti hata kama ingekuwa meli isingeyumba.
Nilikuwa nasikia baridi kali na muda wote huo mvua ilikuwa inaendelea kunyesha, ilionesha ubaridi wa kukaribia alfajiri, eneo lile hapakuwepo na mtu zaidi yangu.
Nilijiuliza ina maana pale ndio uwanja wa damu aliposema Marry White, sehemu niliyoelezwa na Kallo kuwa hutumika kutoa adhabu za kuchuna ngozi na kucharangwa mashoka kama buchani.
Moyo wangu ulishtuka baada ya kuliona gogo kubwa linalo fanana na yale yanayotumika katika mabucha, lilikuwa na michirizi ya damu. Kwa vile macho yangu yalikwisha kuzoea hali ya hewa niliweza kuona mafuvu na vipande vya mifupa ya binadamu.
Kufikia hapo moyo ulikufa ganzi na kujua nimekwisha sikuwa na ujanja, nilijua lazima ningekufa kifo cha kukatwa shingo na shoka au kuchunwa ngozi na kisha mwili kuliwa na mamba.
Kwa kweli kilichobakia ilikuwa ni kuomba Mungu ashushe miujiza yake kama alivyowashushia mitume wake kutoka enzi za akina Ibrahim baba wa imani, Musa, Yakubu, Daniel, Mkombozi wetu Yesu Kristo na Mtume Muhammad.
Japo ilikuwa ni vigumu sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano, lakini nilijipa moyo kwamba yote kwa Bwana yawezekana. Baridi ilikuwa kali hadi mwili niliusikia umekufa ganzi na kiu kilikuwa kikali na njaa niliisikia kama tumboni kulikuwa na msasa.
Suala la njaa sikuitilia maanani zaidi ya uhai wangu ambao sikuwa na uhakika nao. Katika kitu kilichouumiza moyo wangu kushindwa kutimiza dhamira yangu ya kutokomeza udhalimu na kuwakomboa watoto waliokuwa katika hatari ya kutokomezwa kwa kuchunwa ngozi na kunyonywa damu.
Ningejisikia fahari kubwa kufa baada ya kutimia dhamira yangu lakini ndivyo hivyo,
nilikuwa nimekata tamaa kwani nilijua siku zote mwanadamu hupanga yake na Mungu hupanga yake. Lakini niliamini kitu kimoja kwamba, Mungu kwa uwezo wake baada ya kifo changu atamwinua mwingine kama alivyo niinua mimi ili amalizie kazi niliyoianzisha.
Nikiwa katikati ya mawazo mazito, mara nilisikia mingurumo ya gari nilipo nyanyua macho yangu niliyaona magari zaidi ya manne yakielekea sehemu niliyokuwepo. Matatu yalikuwa ya wazi yaliyojaa askari wenye silaha nzito na moja lilikuwa kawaida Toyota Land Cruiser.
Waliteremka watu zaidi ya 12 waliokuwa na silaha wote walizielekeza kwangu, watatu walipanda juu na kunifungua kamba na kisha waliniteremsha chini.
Nilikuwa kama gaidi au siku Osama atakapokamatwa na Marekani, jinsi nilivyokuwa chini ya ulinzi mkali. Nilivishwa koti refu nzito, na kulivaa mwili ulikuwa hauna nguvu hata kutembea nilitembea kwa shida.
Niliingizwa garini na safari ilianza kutoka kwenye uwanja ule wa damu, nikiwa ndani ya gari nilifunguliwa pingu na kupewa onyo kali:
"Sikiliza we malaya ukileta ujanja mwili wako tutageuza ubao wa shabaha."
Ilionyesha ni jinsi gani walivyoniogopa kwani nilikuwa chini ya ulinzi mkali huku mitutu zaidi ya sita ilikuwa imenielekea mimi. Gari liliendeshwa kwa kasi kwa mwendo wa nusu saa tulifika eneo moja ambalo lilikuwa na jengo lililoonyesha bado halijamalizika vizuri vilevile kulikuwa na milio ya jenereta ikionyesha jengo lile halikuwa na umeme.
Niliingizwa ndani ya lile jengo na kupelekwa moja kwa moja kwenye jengo la mikutano. Ndani ya ule ukumbi nilimkuta Marry White na washirika wenzake wote.
Niliingizwa hadi kwenye meza kubwa tukawa tunatizamana na wale mumiani, nikiwa mtupu kama nilivyozaliwa, niliamriwa niketi nami nilitee amri.
Marry White uso wake uliokuwa umekunjamana kwa hasira aliniuliza swali lilelile la awali:
"Nafikiri sasa tutaelewana haya jibu swali langu kwa nini umenitia hasara?"
"Una swali jingine au hilohilo?" nami nilimjibu kwa swali.
"Ninayo mengi lakini jibu kwanza hili."
"Uliza jingine hili nilishalijibu awali."
Jibu langu lilimzidisha hasira Marry White alinyanyuka na kunifuata pale nilipo kuwa na kunishika sehemu za mdomoni na kuanza kunibana kwa nguvu:
"Thereza nitakuumiza jibu swali langu," maumivu yalipozidi nilimuomba aniachie.
"Haya nijibu."
"Ukinieleza kwa nini ulitaka kuniua na mimi nitakuwa na jibu kwa sasa sina jibu hata ukinikata kichwa.”
"Sikiliza binti utaongea katika mazingira magumu kitu ambacho sipendi kikutokee," alinichimba mkwara.
"Nasema sina jibu zaidi ya nililokuuliza jibu unalo wewe mwenyewe."
"John naona huyu binti analeta utani hebu mwite Zimwi Shetani na Roho ya Chuma."
Yule jamaa mwenye mwili mkubwa alitoka kuelekwa nje ya jengo, mara aliporudi alikuwa ameongozana na watu wawili wenye miili ya kutisha mmoja mfupi alikuwa hana tofauti na mzee Ole wa kwenye gazeti la Sani ungemuona ungejua ni yeye au pacha wake.
Walipofika walisimama mbele ya Marry White na washirika wake waliinama kuonyesha wameitikia wito. Walikuwa na miili ya kutisha iliyogawanyika walikikuwa vifua wazi chini walivalia chupi za ngozi ya chui.
"Zimwi Shetani," Marry White aliita.
"Naam Malkia."
"Nataka umuonyeshe huyu binti kuwa sisi si watu wa mchezo."
''Sawa Malkia."
Kusikia vile niliingiwa na woga na mwili ulianza kutetemeka ile hali Marry White aliiona na kuniambia:
"Unaogopa nini we si unajifanya umemaliza? Basi leo ndio utaijua sababu iliyomfanya kuku asikojoe."
Zimwi Shetani alikuwa ameweka shoka yake begani, shoka ya mpini wa chuma ilionekana ina makali ya kutisha.
"Mleteni mtu wa mfano aone kama atakataa kujibu jinsi tutakavyo mfanya huyo wa mfano."
Aliondoka kijana mmoja na kurudi na mtu aliyekuwa amefungwa kitambaa usoni alipofikishwa mbele na alifunguliwa kitambaa. Alionekana mtu aliyejikatia tamaa machozi yalimtoka muda wote tangu alipofikishwa pale mbele. Sio siri nilimuonea huruma na kuyasahau yalio mbele yangu.
Zimwi shetani alitoka nje na kurudi na gogo kubwa la kubebwa na watu zaidi ya wanne tena walioshiba. Lakini mwanaume wa shoka alilibeba peke yake , duniani wapo viumbe wanaotisha mmojawapo ni yule mbaba.
Lile gogo liliwekwa mbele kisha yule mtu alilazwa juu ya lile gogo, kabla ya kulazwa alivuliwa nguo zote na kubakia mtupu. Zimwi Shetani alipaka unga mweupe mikononi ilionyesha kama poda kisha alichukua lile shoka lililokuwa pembeni na kulipunga hewani.
Ulikuwa kama mchezo vile wakati Zimwi Shetani alipoliteremsha shoka lake kwenye mwili wa yule mtu aliyelazwa juu ya gogo. Mwanzo niliona kama utani lakini aliporudia pigo la pili nilipiga kelele na kufumba macho sikuangalia kilichooendelea zaidi ya kusikia kishindo cha shoka.
Shoka lilipotulia nilifumbua macho, mmh..kama kuna binadamu wenye roho mbaya basi yule mbaba ni namba moja. Juu ya gogo kulikuwa na vipande vya nyama ya mtu na pale pote palikuwa pametapakaa damu iliyomchafua yule zimwi shetani sehemu za tumbo kifua na usoni.
Nilijikuta naingiwa na woga wa ajabu lakini nilijikaza kikie ili kuficha woga wangu. Marry White alinigeukia na kunieleza:
"Nafikiri mfano hai umeuona sasa chaguo moja ucharangwe kama nyama au ujibu maswali yangu kwa ufasaha," alisema yale huku watumishi wake wakikusanya nyama za yule mtu aliyeuawa kikatili na kuziweka kwenye mfuko wa plastic.
Swali nilisikia lakini moyoni niliapa kuwa sitamjibu vizuri maswali yake kwa kujua kama nitamjibu lazima atapata faida na kisha kuniua. Niliona bora nife kuliko kumpa faida mshenzi mumiani mkubwa. Alipoona simjibu alinifuata tena na kunishika sehemu za mdomo na kuniuliza:
"Utanijibu hunijubu?"
Sikumjibu kitu, nilikaa kimya hali iliyompandisha hasira na kuanza kunipiga ngumi za usoni zilizozidisha hasira zilizonitoa damu puani na mdomoni nilisikia sehemu za pembeni ya mdomo zimechanika. Lakini vilevile sikujibu nilikaa kimya.
Alipotaka kuniuliza tena nilimtemea mate usoni yaliyochanganyikana na damu, Marry White alinipiga teke lililonirusha kwa nyuma na kuniacha uchi nilimsikia akisema:
"Zimwi shetani hebu fanya kazi yako naona analeta utani."
MWISHO.
Your Thoughts