BANGUZI 1

Emmanuel Lee
By -
0

 RIWAYA: BANGUZI

NA: HASSAN O MAMBOSASA



_____SEHEMU YA KWANZA_____



Jicho lisilo kavu wala kuwa na unyevu sana ndani yake, analo hata kwenye hali hiyo bado halikuweza kupotea. Mboni za rangi ya nyeusi zililipamba, ambalo lilizungukwa na kope ndefu ziso na matunzo tofuati na ilivyozoelekea na watu wa umri aliyo nao. Uso wake mwembamba mrefu wa wastani, wenye pua isiyochongoka sana pamoja na midomo midogo ambayo ilionekana kuanza kumpauka. Haikuacha kudhihirisha kwamba huyu aliwahi kuwa mnyange, tena angeweka vikolombwezo usoni mwake angebaki mrembo daima.


Mabinti wengi wa rika hilo hupenda kuendelea kuonekana ni wapo kwenye 'fomu' ila kwa huyu haikuwa hivyo. Nywele zilibaki kutibuka tu ingawa zilioneshwa zinapewa matunzo ya kila siku ndani ya maisha yake. Alipo amevaa nguo nadhifu, akiwa ameketi kitako kitandani, macho ameyakodoa kuelekeza mbele pasipo kupepesa. Haikuchukua muda basi chozi humtoka, laiti ungelimwona ungalisema ya kwamba ni analia. Ila haikuwa hivyo, mtu mwenye kufikia hali hii hawezi kuwa na simanzi ya namna hiyo labda arejewe kidogo na jambo lililomfanya akawa namna hiyo ndiyo anaweza kuangusha chozi.


Mwanadamu daima akikodoa jicho muda mrefu pasipo kupepesa, basi chozi humnyemelea. Ndiyo ilivyo kwa binti huyo, hakuchezesha macho yake ndiyo maana ikawa namna hiyo. Hata waliyopo mbele yake wanaomtazama tu anavyotokwa na chozi, walihisi yu ndani ya huzuni kali ila haikuwa hivyo.

Mwanamke mtu mzima aliyejipara haswa, pamoja na mabinti wawili waliyovuka umri wa kupevuka wakikimbilia mvuko wa umri wendawazimu walibaki wakimtazama Msichana huyo ambaye sura yake imelandana na zao. Walimwonea huruma kwa hali aliyo nayo, kiasi cha kushindwa kusema kile kimsibucho hadi kufikia awe namna hiyo.


"Mama hivi Dada atapona kweli, miaka miwili sasa yupo hivi?", Mmoja kati ya Mabinti hao aliuliza swali.


"Na wewe Spora maswali gani hayo ya kuniuliza, atapona kweli unamaanisha nini? Huamini kama atapona, yaani unakosa imani kwenye jaribio dogo kama hili", Mama huyo alimkaripia Bintiye.


"Si hivyo Mama ninaumia mno kumwona dada yangu yupo kwenye hali hii, natamani sana arejee kama mwanzo. Nampenda sana dada yangu" Spora aliyekemewa hapo awali kwa kutoa kauli ya kukatisha tamaa, alisema kisha akaenda kuketi jirani na Dada yake.


Alimshika kichwa chake na kukilaza begani mwake, Binti kama yeye aliyemzidi umri naye anatii amri na kujiegemeza akiwa yu kimya tu haongei chochote. Msichana aliyesalia baada ya kuliona hilo chozi lilimdondoka, anajifuta huku akimtazama Dada yake kwa simanzi kuu. Hali hiyo ilipelekea Mama yake kumwambia, "Eliza usilie mwanangu dada yako bado mzima huyu, atapona tu tuombe Mungu tu ingawa tumehangaika naye". Eliza aliposikia hivyo alisema, "Ila Mama inauma sana naamini Mama Jeta kafanya ushirikina tu si bure kisa anamchukia Dada yetu".


"Elizaaa! Hebu kuwa wa kisasa mwanangu, bado na wewe upo kwenye imani za kishirikina. Ingekuwa ni imani hizo maombi yote aliyofanyiwa si angekuwa mzima hivi sasa. Amini huo ni mtihani wa Mungu, msitake kuniliza na mimi hapa kwa maneno hayo. Siamini mama kama yule anaweza kufanya haya haswa akijua jinsi mwanae nilivyokuwa nikimwona kama mwanangu, kama kumchukia binti yangu ni haki yake kuwa hivyo, mwacheni awe vile Gina dada yenu alikosea sana. Ila hawezi kufikiaa hatua ya kufanya vile," Mama huyo alisema huku akifikicha macho yake ambayo yalianza kulengwa na machozi.


Alipoweka kituo tu kwenye maneno yake, alitoka humo chumbani, akiwaacha mabinti zake pekee. Muda huo kitendo cha kuondoka, Binti mkubwa asiyeongea wala kufanya chochote, alishuka kitandani na kusimama wima ghafla. Eliza na Spora wakabaki wanatazama tu kwani hawakutaraji suala kama hilo, aliganda namna hiyo huku akipeleka macho kwenye kioo cha kujipamba kilichopo kwenye kabati meza ya vipodozi. Alikishangaa haswaa kionesha taswira hicho, hadi mdogo wake mmojawapo akashindwa kustahimili akamwita.


"Dada Gina", Spora aliita ila hakupokea mrejesho wowote ule kutoka kwa Binti huyo.

Mrembo huyu asiye na matunzo alipokitazama kioo hicho, ghafla alijiwa na kumbukumbu ya ajabu kichwani mwake. Muziki wa kizazi kipya anaanza kuusikia masikioni mwake, hajakaa sawa anasikia mayowe ya wasichana ambao waliashiria wazi kupagawishwa na mwenendo wa ala maalum pamoja na sauti zitokazo kwenye spika maalum. Anajikuta akizungusha shingo kutoka upande mmoja kwenda mwingine, akiwatafuta hao wanaocheza hivyo ni kina nani. Hakuweza kuona mtu yeyote, anajiona yu ndani ya kuta nyeupe tupu tu huku sauti hizo zikizidi kuvuma masikioni mwake. Aliporejesha macho kwenye kioo ambacho kimezongwa na vidopozi, anajiona akiwa ameweka nywele kwa mtindo wa kupendeza. Uso wake ukiwa umepambwa vilivyo, kifuani akiwa na mkufu wa dhahabu.


Kitendo cha kuliona pambo hilo, lisilosimama wala kusimikwa. Aliweka mkono shingoni mwake ambapo muda huo hakukuwa na kitu, hali ilimfanya ajipapase mara kadhaa kwani hakuamini kama kioo kile kichomwonesha akiwa na mkufu kiwe kinamdanganya. Loh! Masikini ya Mungu, Gina hakuwa akijitambua wala kuweza kumaizi hiyo ni sehemu ya kumbukumbu zilizopita ambazo zimelundikana kichwani mwake. Akifanya hayo wadogo zake walishaanza kuhisi kitu, walipaza sauti kumwita mama yao. Yeye wala hakuwa na habari na wito wa nguvu kwa mzazi wake wa kike, alibaki kaduwaa vilevile tu huku hana habari na chochote kile.


Mama alifika hima baada ya kusikia kuitwa huko, alimkuta Gina bado akikidolea macho kioo hicho. Akijitazama, hakuwa na furaha usoni mwake ila kwenye kioo anajiona ni mwenye furaha huku akiyumba kwa madaha kuendana na dundo wa muziki unaosikika masikioni mwake. Hajakaa sawa kupitia kioo anamwona banati mwingine aliyependeza haswa akiwa amevaa gauni jekundu akija kumkumbatia hapo kwenye kioo huku akipiga yowe kwa kunogewa na muziki. Kitendo hiko kinamfanya ajawe na tabasamu haswa, mara ghafla muziki ukazimika ghafla masikioni mwake. Yowe zito la Binti akiomba msaada linafuatia, hali hiyo inamfanya kwa haraka ashtuke na kurudi nyuma kwa ghafla huku akipiga kelele kisha kilio kinafuatia.


"Gina! Gina!", Mama yake anaitwa huku akihangika kumtuliza kutokana na kilio hicho alichokianzisha, ila inakuwa haina msaada wowote ule. Mama huyo alipoona hali ni tete aliagiza, "Wewe Eliza hebu funika hicho kioo na kanga, Spora leta vidonge vyake pale kwenye kabati tumpe alale".


Mabinti kwa pamoja walikimbia kwenda huko walipotumwa, kila mmoja anatimiza agizo lake kwa wakati husika. Gina anapewa dawa ambayo inamfanya atulie, analala papo hapo na kuwaacha jamaa zao wakimtazama kwa masikitiko makuu.


****


Siku iliyofuata asubuhi eneo jingine kabisa lenye mchanganyiko wa watu, alionekana mwanamke aliyevaa suti za kisasa za kike zenye mfumo wa suruali. Akipishana na watu kwa tabu, huyo aliingia upande ambao una mabanda mengi yaliyobanana ambayo huuzwa vitu mbalimbali za vyumbani. Alitembea huku akipita mabao kadhaa yenye vitunguu, nyanya na baadhi ya viungo hadi akafika kwenye eneo lenye kuuza njegere pamoja na maharage mabichi. Hapo ndipo aliweka kituo, akapeleka macho kumtazama Mchuuzi.


"Karibu Dada", Alilakiwa.


"Asante Kaka yangu, njegere mnauzaje?"


"Njegere kipimo kidogo ni shilingi 1000 na kikubwa ni shilingi 3000"


"Nipatie kipimo kikubwa viwili" Mwanamke huyo alisema hivyo anahisi kuguswa begani mwake, anapogeuka anaishia kusema, "Waaaoh! Spora mdogo wangu". Anakumbatiana na msichana ambaye alimgusa bega.


"Haya za masiku we mtoto, yaani mmekuwa adimu nyinyi", Alianza kuongea na Spora.


"Nzuri tu, Dada tupo si unajua da Gina hali ndiyo ileile ndiyo maana hatuonekana muda wote tupo naye"


"Mungu wangu namhurumia sana shosti wangu Gina, Mama nimemwambia hali ile ilianza vipi na nikamshauri cha kufanya ila naona amekikatia tamaa ndiyo hali inakuwa vile"


"Da Heriety kwani uliongea naye vipi mama"


"(Akipokea njegere zilizopo kwenye mfuko laini, huku akimpatia Muuzaji pesa yake) Wadogo zangu unajua bila ya maneno ya Jeta na kile alichokisababisha ndiyo chanzo cha yote yale, msamaha wa yule mama ndiyo kila kitu. Gina alikosea tena sana, ndiyo kosa lake linalomfanya awe vile. Najua nyote hamkuwahi kusikia yote kiupana, ila mimi niliyesoma naye na kukaa naye chumba kimoja hosteli shuleni hadi chuoni ndiyo ninajua hilo. Anahitaji msamaha sana wa Mama Jeta kwa niaba ya Jeta"


"Mh! Hebu da Heriety hebu subiri ninunue vitu maramoja hapahapa, unieleze", Spora aliagiza kwa haraka kile kilichomleta sokoni huko, alipomaliza akamtazama Heriety aliyekuwa akimsubiri kama alivyopenda. Alisogea naye hadi mbali na eneo lenye watu kisha akamwambia, "Dada najua wewe ndiyo unayejua mengi sana kuhusu dada yangu kipindi yupo chuo kuliko hata mama yetu. Maana wewe umesoma naye toka Kidato cha tano hadi chuo, niambie kipi kimemsibu hadi akawa vile. Sikupata kukisikia kisa kile chote"


"Ni kweli Spora mimi ndiye niliyesoma naye Gina, ninayajua mengi ambayo mengi sikuyaweza kuyazungumza kwa mama yako kwani yanatuhusu sisi mabinti tu. Hata kama mama naye ni mwanamke ila mengine, ilinibidi niyaache tu ili kumsitiri shoga yangu. Spora mdogo wangu, mwanzo wa histori haya yalianza tukiwa 'form five' ambapo watu watatu ndiyo chanzo cha Gina kuwa vile. Kevi, Jeta na Allice. Laiti kama isingekuwa uwepo wa hao basi hii leo Gina angekuwa na maisha mazuri kama sisi"


"Kwani ilikuwaje?"


"Ni hadithi ndefu sana, ila ukae ukijua mwanzo wa yote yalianza kupikika tukiwa kidato cha tano. Yakaja kuharibika siku ya 'graduation' yetu usiku ule yaani keshatunukiwa cheti chake cha Degree ndiyo yanamkumba hayo. Yamepelekea kidonda kisichoponda, yaani dondandugu kila kukicha linakuwa. Kama manvyomuona pale alipofikia, mwanzo alikuwa mkaaji kimya tu na si mwongeaji na mambo mengine akifanya ila leo hii hafanyi chochote".


"Dada unanieleza juu juu tu wala huniambii ilikuwaje"


"Spora mdogo wangu, inahitaji muda mwingi sana wa kutulia maana ni kisa kirefu hichi si kama unavyofikiri tukikaa hapa na kukianza sidhani kama tutakimaliza. Yaani hapa tutatumia muda wetu ila hakitoisha, nafikiri leo ni ijumaa na kesho ni jumamosi siku ya mapumziko. Siku ya kesho hiyo ninawaalika kwangu kupata chakula cha jioni, naamini tutapata muda mzuri wa kuzungumza kwani mume wangu amesafiri hivi sasa. Kwa hapa haitowezekana, tuombe uzima hiyo kesho mjue kila kitu kuhusu dada yenu"


"Sawa dada, ngoja nikuache mimi niwahi nyumbani. Kesho nitakuja na Eliza huko"


"Karibuni wadogo zangu, mtanikuta"


****

Post a Comment

0Comments

Your Thoughts

Post a Comment (0)