MWISHO WANGU

 SIMULIZI FUPI - MWISHO WANGU


Nilidhani kubadilisha ndoto zangu na kuvurugikiwa ilihitaji miaka mingi jambo hilo kutokea. Nilidhani kuisha kwa uzuri wangu na kila nilichokianzisha toka nilipokuwa mdogo ilihitajika miaka mingi kama ile niliyokuwa nayo sasa. Nilikuwa msichana mdogo sana na mwenye ndoto kubwa ambazo tayari sasa zilikuwa zimetimia. Kuwa na magari ya kifahari na familia yenye furaha ndicho kitu nilichokiwaza katika muda wote wa maisha yangu. Hatima ya maisha yetu anayeijua ni Mungu na kamwe huwezi kumuona na kumuomba muda zaidi maisha yafikapo tamati, kila kitu huvurugika pale jioni ya maisha yako ifikapo. Milango ya ndoto zako hufungwa na giza nene hutanda mbele, fimbo ya kukuongoza njia hupotea. Mwanga hufifia na woga hukusonga.


Hiyo ndiyo hali iliyonipata, machozi na jasho vikanitoka, aliyekuwa awe msaada wangu akanikimbia na kunisahau. Hata wale niliowadharau mwanzoni na kuwaona hawawezi kuwa chochote kwangu wala kunipa msaada nilitamani sasa wajitokeze lakini haikuwa hivyo. Msichana mrembo nikageuka kuwa kituko mbele ya jamii, maringo yangu yote na elimu yangu havikunisaidia kupata huruma ya wanajamii. Jina nililopewa toka utotoni lilikuwa ni Yasmin, ila kwa mapenzi na upendo mkubwa kwa Tony niliamua kubadilisha dini na kuitwa Anjela. Lakini mapenzi yangu kwa huyu mwanaume yalifanya niringe na kujidai, nilimpenda sana, alikuwa ni mtanashati alikuwa ni mwanaume mwenye pesa zake na niliamini alikuwa akinipenda. Maisha mazuri tuliyoishi mimi na yeye yalinifanya niwaone majirani zangu kama takataka, Tony alinikataza kabisa kujumuika nao na mimi sikuona haja hiyo ya kuwa karibu nao. Niliishi kivyangu, hata marafiki zangu niliwakwepa baada ya kufunga ndoa na Tony, nia yangu ni kujiepusha nao ili wasijewakamzoea Tony.


 Nilimpenda sana Tony wangu. Kwa shida na raha ndio nadhiri tulioiweka kanisani, ndugu wakachukia kwakuwa tu nilikubali kubadili dini, nikajipa moyo kwakuwa mwanzo nimeshaujua. Maisha mzuri, kazi nzuri, mume mzuri na hatimaye furaha yangu ikatimia baada ya kupata watoto mapacha, watoto waliokuja kubadilisha mwonekano wa familia na mategemeo yangu. Leticia na Lucrecia ndo majina ya watoto wetu. Walikuwa wazuri sana, watoto wa kike niliowaota siku nyingi sana, wakwe zangu wakaja kunipa hongera, tukasafiri na Tony hadi Irkepusi huko kwenye kreta ya Ngorongoro ili watoto wakamuone mzee Ole Senteu ambaye ndiye babu yao. Tony alikuwa ni Mmasai, alikuwa ni moja kati ya wamasai wasomi na walioishi maisha ya kimjini sana.


Mimi nilikutana na Tony chuo kikuu cha Dar es Salaam kipindi yeye akiwa anasoma uhandishi wa elektroniki, alikuwa kijana mrefu na mtanashati, sikukwazwa na masikio yake au ndonya kwenye paji la uso wake, nilipenda lafudhi yake na haswa alipokuwa akiongea kingereza. Tulipenya misitu na mabonde mpaka irkepusi na tulifanikiwa kufika, vichanga vikafanyiwa mitambiko na tukaruhusiwa kurudi Dar kuendela na maisha Mzee Ole Senteu akamuasa mwanae awe mwangalifu wa watoto, akamsihi anipende na kuniheshimu. Nasaha zikamkaa Tony na nyumbani tukarudi. Tony aliyenipenda sasa alikuwa hasafiri tena, alikuwa akiwahi kurudi nyumbani na aliwapenda sana watoto kuliko mimi. Alikuwa ni mtu wa safari kwa kipindi kabla sijajifungua lakini baada ya hapo hakutaka kusafiri. Mara zote alikuwa nyumbani akiwabeba watoto wake.


Nilimpenda sana mume wangu, nilimpenda kuliko chochote. Asubuhi ilikuja na usikuwa ukafata, riadha na matarajio yangu yakaanza kuota mbawa, watoto wakakua na sasa wakaweza kusema baba na mama, siku zikaenda na miaka nayo ikatutupa mkono. Tony na safari, safari na Tony, Tony anakwenda Uingereza na watoto wanakaa hata miezi sita. Akirudi utasikia anakwenda Ngorongoro huko umasaini, namwambia Tony twende wote Tony hataki ananambia niende kazini na nikae na nyumba nirudipo. Watoto wakajengwa kisaikolojia na hawakuwa tena wakiniita mama, wao kila mara wakawa wanamuwaza baba yao tu, eti tena wananiita AUNT ANJELA, mh! ndo walivyofundishwa na baba yao.


 Miaka minne ikakatika Tony akawapeleka watoto shule ya bweni iliyoko Kenya, nikabakizwa bila watoto,. Nani ataamini kuwa eti toka nilipojifungua mpaka watoto wanakua na kwenda shule sijawahi kufanya mapenzi na Tony? Yeye kila wakati amechoka, injinia yuko kazini hata usiku.


Hisia zangu zikaporomoka na mawazo yakaujaza uso wangu. Akili ikagoma kama mshale wa saa, sina tena wa kumwelezea matatizo yangu. Mawifi niliowategemea wakawa wakali kila mara wananiambia nampa kaka yao presha. Nikaanza kujuta kuitwa Anjela. Bado moyo wa kuwa na Tony kama zamani nilikuwa nao, nilijua tu siku moja Tony atakuja kuwa kama mwanzo pale ambapo kazi zitaisha. Sina rafiki tena, mtaani nilikuwa naringa kama nimeolewa na mfalme, hakuna mwingine zaidi ya mimi. Tony akaniambia niache kazi hataki kuona nikiwa nahangaika na kazi tena. Nikamkatalia, akaingia ndani na kuchukua vyeti vyangu vyote akachoma moto. “Nimekuambia ukae hapa nyumbani kama hutaki tafuta pa kwenda, unahangaika nini wakati pesa ipo, nini cha kukufanya uangaike kuamka saa 11 asubuhi eti unakwenda kazini wakati mimi nafanyakazi? Kaa nyumbani wanangu wanarudi toka shule uwahudumie na unihudumie na mimi, hiyo ndio kazi ya mama yoyoo.” Tony akanikoromea kwa ile lafudhi ya kimasai. Akawa mbogo na mori zikataka kumpanda, mwanamke kumbishia mwanaume kwenye kabila lao haikuwa sahihi, kile kitendo cha mimi kukataa kuacha kazi yeye alikichukulia ni kama dharau.


Lakini haikuwa hivyo, haikuwa rahisi kwa yeye kuchukulia kuwa kawaida kwakuwa tayari alishakasirika. Wakati ananigombeza akaja kaka yake wakawa wanazungumza “yero subai” Tony akamsalimu na kaka yake bado akishangaa inakuwaje nilikuwa naongea na mume wangu huku nimesimama, “Yeba, Keiya” akaitika yule shemeji yangu, Tony akiwa bado anatetemeka mikono kwa sababu ambayo haikuwa kubwa akaitikia tena “Shidai”, Ole Itutu akaniangalia na kunipengea kamasi, Tony akalisikia na kugeuka, nilikuwa nalia lakini Tony hakufanya chochote. Wakaingia ndani na mimi nikaketi pale chini nikijililia. Nikatamani nimpigie Cesilia simu lakini ningeanzia wapi? Marafiki niliowatelekeza kwa kumpata mume leo ningeanzaje. Niajikaza tu, wanangu wakarudi kwa likizo baada ya kuwa shuleni muda mrefu sana, nikajua watakuwa wamebadilika na kuanza kumpenda mama yao, lakini haikuwa hivyo. Walikuwa ni watoto wa kizungu. Wakaja na kuniona kama vile mimi ni mfanyakazi wa ndani, wakanijibu watakavyo na Tony akawa anawaangali tu, sikuwa na mamlaka na wanangu.


Siku ya tatu toka waje Tony akaniambia anawapeleka watoto umasaini ili wakajifunze mila na lugha ya kimasai. Sikuafiki hilo, tuligombana sana na Tony, nia haikuwa mimi kuwakataza watoto kwenda umasaini, hapana, nia yangu ni kwamba nilihitaji kukaa na wanangu angalau nijaribu kuwaonyesha kuwa mimi ndo mama na wanatakiwa wanithamini.


Mawazo yalikuwa ndiyo sehemu ya maisha niliyojichagulia. Kiu ya wanangu ilizidi kuwa kubwa kwani baada ya wao kwenda umasaini sikuwaona tena na niliambiwa kuwa wamesharudishwa shule. Tony alikuwa ni Mnyama kuliko hata Khajat wa kwenye hadithi fulani niliyowahi kuisoma, maumivu yangu yalilingana na Nadia kwenye hadithi ya mwandishi mashuhuri aliyeitwa George.


Nikawa mpweke, lakini bora basi watoto waondoke ila Tony awe karibu na mimi, hiyo ilikuwa ndoto ya mchana, safari za Tony zikazidi, mwaka wa tano Tony hataki kufanya mapenzi na mimi eti amechoka. Nikapekuwa makabrasha yake, nikakuta risiti za ada za shuleni walikokuwa wanasoma wanangu. Nikapekuwa na kukuta namba za simu za ile shule, nikapiga simu kwenye ile shule ndipo nilipopagawa. “hallo” simu ilipokelewa na mwanamke aliyeonekana kabisa kuwa alikuwa anatarajia nimuongeleshe kwa lugha ya kwao. “Am calling from Tanzania, I was asking to speak to my daughters. (napiga simu toka Tanzania, nilikuwa naomba kuongea na binti zangu)” nikajaribu kwa upole na unyenyekevu kuomba japo nisikie sauti ya wale watoto ambao hawakuwa wakimpenda mama yao. “madam am sorry its 6pm now the pupils have already went home. (Madam samahani kwasasa ni saa 12 jioni na wanafunzi wameshakwenda nyumbani)” mwe! Yule dada akanijibu kama vile alikuwa anashangaa. Nikataja mpaka majina ya wanangu ila yule dada akaniambia wao hawana mtoto anayekaa bweni, akaniambia watoto wamechukuliwa na mama yao ambaye ndiye anayewaleta na kuwapitia arudipo kazini.


Nikaomba namba ya yule mama na nikampigia lakini akaniambia nikae mbali na watoto wake. Nikajaribu kumwambia majina ya wanangu kama ndo hao akanijibu ndio hao ila nimuulize Tony nani mama wa wale watoto, nikamsihi anipe niongee na wale watoto, akawaita na nikasikia sauti ya Leticia ikiitikia abee mama, sikuwahi kusikia mwanangu akiniitikia vile, kisha alimwambia njoo umsalimie Aunt Anjela, ila mtoto akasema baba amesema tusipende kuongea na Aunt Anjela..niliumia sana. Nikashangaa na kutahamaki kwanini Tony anifanyie vile.


Kesho yake nikatoroka nyumbani kwakuwa alikuwa amesafiri, nikapanda ndege asubuhi mpaka Nairob nchini Kenya, nikawasiliana na yule mwalimu na akanielekeza shule ilipo, nikaenda na watoto walikuwa bado hawajaletwa kwakuwa walikuwa wanaingia darasani saa 7 siku hiyo. Nikakaa na baadaye niliona gari likiwashusha wanangu, nikawakimbilia, ooh mungu wangu watoto wakasimama hawakutaka kunitazama, wakageuka na kuangalia nyuma, nikashangaa sana Tony kutoka kwenye ile gari na kuja kwa haraka, hakuniuliza kitu, alinipiga kupita kiasi mbele ya wale watoto, yule mwanamke aliyekuwa naye kwenye gari alitoka na kuja pale kisha akamwambia Tony aniache.


“Tony mume wangu, muache tu, hiyo inamtosha.” Yule mwanamke akaonekana kufurahia kilichonitokea.


“We dada, mimi ni mwanamke mwenzio, nilipata shida miezi tisa kubeba watoto hawa na zaidi nimewalea na wewe leo hii unashiriki kunitenga na wanangu, mchukue Tony ila niachie wanangu.” Yule dada akanipandisha na kunishusha. Akanitemea mate na kuondoka. Jamani mimi ni binadamu au takataka. Nikanyanyuka na watu walikuwa wengi pale, damu zilikuwa zikinitoka puani. Nikamuomba mtu anionyeshe hospitali ilipo nikaenda wakanitibu pale na kunifunga vidonda vile kisha nilielekea uwanja wa ndege na kupanda ndege ya kuja dar.



Nilipofika Dar nilikwenda kufata gari yangu niliyokuwa nimeiegesha kwenye maegesho ya pale uwanjani na kuondoka. Nilikuwa nalia kama mtoto. Nikafika ubungo mataa nikiwa mbele kabisa nasubiri foleni iruhusu, machozi yakaujaa uso wangu, nikaona taa ya kijani, kumbe haikuwa ya kijani, ilikuwa ni nyekundu ila niliona vibaya, nikaondoa gari na kukutana na Lori la mizigo. Nilikuja kushtuka wiki mbili mbele, nilikuwa mwenyewe hospitalini, miguu yangu yote ilikuwa imekatwa kuanzia kwenye magoti kushuka chini, nikalia sana. Nikauliza kama kuna mtu amekuja kuniangalia nikaambiwa kuna mtu alipiga simu akasema atakuja kuniona lakini hajawahi kuja. Nikauliza namba iliyopiga wakanijulisha ilikuwa namba ya Tony. Tony hakuja mpaka karibu naruhusiwa ndipo alikuja, akajifanya kunipa pole. Madaktari wakamwambia atoe milioni nne niwekewe miguu ya bandia ila alisema hana pesa.


Nikasema akachukue kwenye akaunti yangu lakini Tony akajibu kuwa ameshazitumia kwenye kitu kingine na kwamba hakuna haja ya kumuhudumia kiwete. Tony akamuhamishia yule mwanamke nyumbani na mimi akanipa chumba kingine. Hiyo haijatosha Tony hakutaka hata kuniogesha, eti akamleta kijana wa kiume awe ananihudumia na kuniogesha. Mh! nilikaa mpaka wiki mbili na nguo moja, sikuweza kujisogeza kwakuwa sikuwa na nguvu, alininyang’anya simu na kunifungia ndani.


Kuna siku nilikuja kuona huo ni ujinga, nikajiburuta mpaka sebuleni, Tony alikuwa amelala sakafuni na yule mwanamke wakichezeana, nilikuwa na kisu nimekificha, niliposogea taratibu nikakipenyeza kile kisu kifuani kwa Tony na kukichomoa haraka, wakati yule mwanamke anataka kukimbia nilivuta dera lake na hapo alianguka nikamchoma kisu cha tumbo na kurudia mara nane, nilirudi tena na kumchoma Tony kisu mara ishirini.


LEO HII NIKO HAPA NASUBIRI RAIS AWEKE SAHIHI KWENYE HATI YA MAHAKAMA ILI NINYONGWE,,,niliishi na watu vibaya naomba kila mtu anisamehe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.