A Reject Kayumba 2024: 03

Comments ...
banner

​A REJECT KAYUMBA 2024.
​NA: Emmanuel Charo.
WhatsApp: +254796273110

​SEHEMU YA 3

​Ilipoishia...
Asubuhi ya leo hali ilikuwa tofauti kwa Abdul alichangamka kiasi cha kuwashangaza wazazi wake. Aliingia ndani ya darasa lao mpya darasa la saba na kuona rafiki zake wote hilo liliongeza furaha yake lakini hakuiona nywila ya maisha yake, Almas, chotara wa kiyemen na Mmijikenda ambaye Abdul hakuona kasoro yoyote kwake.
​Endelea...
​Abdul aliketi kwenye dawati lake lililokuwa mstari wa tatu kutoka mbele. Macho yake yalikuwa yakitazama mlangoni kila sekunde. Wanafunzi waliendelea kuingia, wengine wakikumbatiana kwa furaha ya kuonana baada ya likizo ndefu ya Disemba, lakini kwake, kelele zote hizo zilikuwa kama upepo tu.
​Ghafla, harufu nzuri ya marashi laini ilipita karibu yake. Almas aliingia darasani. Hakika Mungu alitumia muda wake kumuumba binti huyu. Nywele zake ndefu za asili zilikuwa zimesukwa vizuri, na tabasamu lake lilikuwa na uwezo wa kuyeyusha hata moyo wa jiwe. Abdul alihisi mapigo yake ya moyo yakienda mbio. Alitaka kunyanyuka amsalimie, lakini ujasiri ulimuisha, akabaki ameganda kama sanamu.
​Paaap! Kofi jepesi lilitua kwenye bega la Abdul, likimshtua na kumtoa kwenye dimbwi la mawazo. Aligeuka kwa hasira lakini hasira hizo ziliyeyuka mara moja alipomuona rafiki yake wa kufa na kupona. Alikuwa ni Emmanuel, au kama walivyopenda kumuita, Manu.
​"Oya mwanangu, mwaka mpya huu, bado tu unamkodolea macho Almas kama unatazama runinga?" Manu alisema huku akivuta kiti na kukaa kwenye dawati lilelile alilokaa Abdul.
​Abdul alitabasamu kwa aibu. "Acha zako Manu. Nilikuwa naangalia tu jinsi darasa lilivyopangwa."
​Manu aliangua kicheko kidogo. Manu alikuwa ni kijana mkimya kwa watu asiowajua, lakini mchangamfu sana akiwa na Abdul. Tofauti na Abdul ambaye alikuwa na umbo kubwa kidogo na kupenda sifa za hapa na pale, Manu alikuwa mwembamba, mwenye macho makali yanayochunguza kila kitu. Kwenye mikono ya Manu, kulikuwa na saa ya kidijitali aliyokuwa akiifungua na kuifunga kwa kutumia bisibisi ndogo aliyoibeba kama pambo.
​"Sawa bwana mkubwa, lakini ukichelewa kutoa neno, wajanja watabeba," Manu alimtania huku akiunganisha nyaya ndogo za saa yake.
​"Hakuna anayeweza kumsogelea Almas wakati mimi nipo. Wewe unanijua vizuri," Abdul alijibu kwa kujiamini, japo ndani ya moyo wake alikuwa akitetemeka.
​Mwalimu wa hisabati, Bwana Kazungu, aliingia darasani. Darasa lilizizima na kila mwanafunzi akasimama kutoa heshima. Baada ya salamu, Bwana Kazungu hakuchelewesha muda, aliandika swali gumu la Algebra ubaoni. Lilikuwa swali la kidato cha kwanza lakini alipenda kuwapima wanafunzi wake wa darasa la saba ili kuona akili zao zimeamka vipi baada ya likizo.
​"Nani anaweza kutatua fumbo hili?" Mwalimu Kazungu aliuliza huku akizungusha macho darasani.
​Ukimya ulitawala. Wanafunzi wengi walikwepa macho ya mwalimu. Abdul, akitaka kuonyesha umwamba mbele ya Almas ambaye alikuwa amekaa madawati mawili mbele yao, alinyosha mkono haraka.
​"Haya Abdul, njoo ubaoni," Mwalimu alisema.
​Abdul alisimama kwa mbwembwe na kuelekea ubaoni. Alichukua chaki, akatazama lile swali, kisha akaanza kukokotoa. Lakini kadiri alivyokuwa akiandika, ndivyo namba zilivyokuwa zikimchanganya. Baada ya dakika mbili, alikwama kabisa. Wanafunzi walianza kunong'ona. Abdul aligeuka na kumtazama Almas, alimuona binti huyo akiwa ameinamisha kichwa kama anamsikitikia. Aibu ilimjaa Abdul.
​"Inaonekana likizo imekulaza akili Abdul. Nenda kakae," Mwalimu Kazungu alisema kwa sauti ya kukatisha tamaa.
​Abdul alirudi kwenye kiti chake akiwa amejawa na hasira na aibu.
​"Mwalimu, naweza kujaribu?" Sauti tulivu ya Manu ilisikika.
​"Njoo Emmanuel."
​Manu alisimama taratibu. Hakuwa na mbwembwe. Alifika ubaoni, akachukua chaki, na ndani ya sekunde thelathini, alikuwa amepanga namba kwa mfuatano wa kimantiki na kupata jibu sahihi. Hakukokotoa tu, bali alielezea njia fupi zaidi ya kupata jibu ambayo hata Mwalimu Kazungu aliishia kutikisa kichwa kwa mshangao.
​"Safi sana Emmanuel! Makofi kwake!" Mwalimu Kazungu aliongoza darasa kumpigia makofi.
​Manu alipokuwa akirudi kwenye kiti chake, macho yake yaligongana na ya Almas. Almas alimpa Manu tabasamu pana sana, tabasamu ambalo Abdul alilitamani asubuhi yote.
​Abdul alihisi kitu kikimchoma moyoni. Haikuwa chuki, maana Manu alikuwa rafiki yake wa dhati, lakini ulikuwa ni wivu. Wivu wa jinsi Manu anavyofanya mambo magumu yaonekane mepesi sana. Wivu wa jinsi akili ya Manu inavyong'aa bila hata yeye kutumia nguvu.
​"Umeua mwanangu," Abdul alimpongeza Manu alipoketi, lakini sauti yake ilificha uchungu aliohisi ndani.
​"Ni swali dogo tu lile, ulikosea kanuni tu mwanzoni," Manu alisema kwa unyenyekevu huku akirudisha umakini kwenye saa yake aliyokuwa akiitengeneza.
​Wakati wa mapumziko ulipofika, Abdul alikusanya ujasiri wake. Alimfuata Almas aliyekuwa amesimama peke yake karibu na bustani ya maua ya shule.
​"Mambo Almas," Abdul alisalimia, sauti yake ikitetemeka kidogo.
​"Poa Abdul. Pole kwa lile swali la hesabu, mwalimu alikuwa anatuonea tu," Almas alimjibu kwa sauti nyororo iliyomfanya Abdul asahau aibu yote aliyopata.
​"Ah, kawaida ile. Niliamua kumpa Manu nafasi tu aonekane," Abdul alijidai, akijaribu kufunika udhaifu wake. "Hivi... nilikuwa nafikiria... nikusindikize nyumbani leo jioni?"
​Almas alitabasamu, kisha akatazama upande ambao Manu alikuwa amesimama mbali kidogo akichezea redio ndogo. "Sijui... labda kama mtakuwa wote na Manu. Yule rafiki yako ana akili sana."
​Kauli ile ilikuwa kama mkuki kwenye moyo wa Abdul. Alitikisa kichwa kwa tabu na kukubali. Uhasama baridi ulikuwa umeanza kujengeka bila wao kujua. Urafiki wao ulikuwa unaelekea kwenye mtihani mgumu sana; mtihani ambao baadaye ungewafanya wawe maadui wakubwa kwenye idara nyeti za kijasusi.
​ITAENDELEA...
... views
Advertisement

Comments ()