
A REJECT KAYUMBA 2024.
NA: Emmanuel Charo.
WhatsApp: +254796273110
SEHEMU YA 4
Almas alitabasamu, kisha akatazama upande ambao Manu alikuwa amesimama mbali kidogo akichezea redio ndogo. "Sijui... labda kama mtakuwa wote na Manu. Yule rafiki yako ana akili sana."
Kauli ile ilikuwa kama mkuki kwenye moyo wa Abdul. Alitikisa kichwa kwa tabu na kukubali. Uhasama baridi ulikuwa umeanza kujengeka bila wao kujua. Urafiki wao ulikuwa unaelekea kwenye mtihani mgumu sana; mtihani ambao baadaye ungewafanya wawe maadui wakubwa kwenye idara nyeti za kijasusi.
Endelea...
Safari ya elimu iliendelea kuteleza, na ule utoto wa shule ya msingi ulibaki kuwa kurasa za kumbukumbu. Maisha yaliwatawanya kiasi, lakini hatima ilikuwa na mipango yake. Abdul alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu akisomea masuala ya usalama na uhusiano wa kimataifa, huku mwili wake ukiwa umejengeka kimichezo na kumpa muonekano wa kijana aliye tayari kwa medani za kivita. Manu pia alikuwepo chuoni hapo, lakini alikuwa katika ulimwengu wake wa pekee, akizama zaidi kwenye sayansi ya kompyuta, usimbaji, na udukuzi wa mifumo.
Ilikuwa ni katika mazingira haya ya chuo kikuu ambapo maisha ya Abdul yaligongana na kijana mwingine aitwaye Rahim.
Rahim alikuwa kijana mtanashati, mkimya kwa asili lakini mwenye akili ya kipekee. Alitoka mkoa tofauti na akina Abdul, akiwa ametupwa chuoni hapo chini ya shinikizo kali la baba yake, Daktari Karim, ili asomee udaktari. Lakini tofauti na matarajio ya baba yake, moyo wa Rahim haukuwa kwenye stethoscope wala madawa; mapenzi yake yalikuwa kwenye kompyuta. Udaktari kwake ulikuwa ni kama kifungo.
Siku moja, wakati wa mapumziko kwenye viwanja vya chuo, Abdul alimkuta Rahim akiwa ameinamia kompyuta yake mpakato chini ya mti, akijaribu kudukua mfumo wa Wi-Fi wa chuo. Udadisi ulimfanya Abdul amsogelee na kuanza kumuuliza maswali. Hilo lilikuwa tundu la sindano lililopitisha urafiki wao. Ndani ya muda mfupi, Abdul na Rahim wakawa marafiki wa kufa na kupona, wakishirikiana katika mambo mengi ya kimasomo na maisha ya ujana. Abdul alijikuta akimuelewa sana Rahim, na mara nyingi alimuahidi kumuunganisha na rafiki yake wa utotoni, Manu, ili ampe mbinu za kiwango cha juu za udukuzi.
Siku moja jioni, wakiwa wamekaa kwenye mkahawa wa chuo wakinywa kahawa, Abdul alikuwa akiperuzi picha kwenye simu yake. Uso wake ulionyesha tabasamu lililochanganyikana na unyonge alipoitazama picha ya Almas.
"Kuna nini mwanangu? Mbona unatabasamu na kununa kwa wakati mmoja?" Rahim aliuliza huku akisogeza kiti chake.
Abdul alishusha pumzi nzito na kumgeuzia Rahim ile simu. "Huyu hapa. Anaitwa Almas. Nimempenda tangu tukiwa darasa la saba. Ni msichana mzuri sana, nywila ya maisha yangu. Lakini... ni kama nimekwama. Sijawahi kupata ujasiri wa asilimia mia kumteka jumla, na kuna nyakati nahisi kama anamuona Manu kuwa bora zaidi yangu."
Rahim aliitazama ile picha kwa makini, kisha akakunja uso kwa mshangao. "Subiri kidogo... huyu si Almas binti wa Kiyemeni? Asili ya kwao ni wale wa upande wa pili kule?"
Abdul alishtuka. "Unamjua?"
Rahim aliangua kicheko kidogo. "Namjua sana! Licha ya kuwa tunaishi sehemu tofauti, asili yetu ya Kiyemeni huwa inatukutanisha sana kwenye shughuli za kifamilia, harusi, na mambo ya kidini. Almas ni msichana anayejiheshimu sana, na nina ukaribu naye wa kindugu kutokana na familia zetu."
Macho ya Abdul yaling'aa kwa matumaini mapya. Hakuamini kama dunia ni ndogo kiasi hicho. Kijana aliyekutana naye chuoni ndiye alikuwa na ufunguo wa moyo wa binti aliyemkosesha usingizi miaka nenda rudi.
"Rahim, mwanangu... lazima unisaidie," Abdul alisema kwa msisitizo, akimshika Rahim mkono. "Nifanye nini kumpata? Wewe unamjua vizuri, unajua tamaduni zenu na nini anapenda."
Rahim alitabasamu na kumrudishia Abdul simu yake. "Ondoa shaka, Abdul. Wewe ni rafiki yangu. Almas anapenda mwanaume anayejiamini, mwenye msimamo, na anayeheshimu asili. Tatizo lako wewe unatumia nguvu nyingi badala ya akili. Nitakupa siri za kumteka, na nitamwambia maneno mawili matatu mazuri kukuhusu. Nikimuweka sawa, uwanja utakuwa wako."
Kuanzia siku hiyo, Rahim aligeuka kuwa daraja la mapenzi kati ya Abdul na Almas. Kwa kutumia ushawishi wake kama kijana wanayeheshimiana kitamaduni, Rahim alianza kumsifia Abdul mbele ya Almas kila walipowasiliana. Alimpa Abdul mbinu za jinsi ya kuvaa, maneno ya kutumia, na hata zawadi ndogondogo zenye maana kubwa kulingana na asili yao.
Mbinu hizi zilifanya kazi kama uchawi. Almas alianza kumuona Abdul kwa jicho tofauti kabisa. Ule uoga wa Abdul ulitoweka, akijiamini kwa sababu alikuwa na 'nywila' halisi iliyotoka kwa Rahim. Haikuchukua muda mrefu, Almas alikubali kuwa mpenzi rasmi wa Abdul, jambo ambalo lilimpa Abdul furaha isiyoelezeka na kumfanya amuone Rahim kama ndugu wa damu.
Hata hivyo, wakati furaha ikitawala upande wa Abdul, kulikuwa na wingu jeusi lililokuwa likitanda upande wa pili. Manu, ambaye pia alikuwa chuoni hapo na ambaye moyo wake bado ulikuwa ukimpigia Almas tangu utotoni, alikuwa bado hajajua kuhusu mchezo huu uliochezwa nyuma ya mgongo wake. Bomu la uhasama lilikuwa likisubiri muda tu wa kulipuka.
Itaendelea
