Siku Isiyo na Jina: 11

Comments ...
Siku Isiyo na Jina 11

​Ilipoishia....
​Ngube alitazama dirisha ambalo sekunde chache zilizopita lilisikika likivunjika kwa kishindo, lakini sasa lilikuwa imara na halikuonyesha dalili yoyote ya ufa wala mchubuko. Angel, yule yule aliyedhaniwa kuwa muuguzi mnyonge kutoka Siaya, alisimama mbele ya kikosi hatari cha Risasi Tatu akiwa na tabasamu la dharau. Aliwaeleza wazi kuwa hahitaji ulinzi wao na wala hawapaswi kupokea tena maagizo kutoka kwa Mike Gonard, bali sasa watafanya kazi chini yake, kisha akatoweka kimajabu chumbani humo na kuwaacha Ngamba, Ngombo na Ngube wakiwa wameduwaa.
​Huko Moscow nchini Urusi, Abdul alikuwa amezinduka na kujikuta amefungwa kwa kamba ngumu za nailoni kwenye kiti kizito cha chuma. Jasusi huyo aliyejifanya polisi alikuwa ameingizwa mkenge na Angel feki ambaye sasa alikuwa amevalia suti nyeusi ya kijasusi. Angel huyo alimdhihaki Abdul na kumuacha chumbani humo huku akimwekea bomu la kutegwa lenye saa iliyokuwa ikihesabu sekunde za kuelekea mauti yake.
​Wakati huo huo, mahali pasipojulikana kina kirefu chini ya bahari, Manu na MCA Adrian Sirya walikuwa bado wamefungiwa kwenye chumba chao cha kioo na chuma. Huku Adrian akiwa amekata tamaa, Manu alikuwa na mpango mwingine. Kutoka kwenye mshono wa suruali yake, Manu alikuwa ametoa kipande kidogo sana cha plastiki kilichobeba micro-processor ya siri aliyoiunda yeye mwenyewe. Alikisogeza kipande hicho kwenye mwanya wa paneli ya kielektroniki ya mlango wao. Taa nyekundu ikaanza kupepesuka. Manu alikuwa ameanza safari ya kufungua kaburi lao la maji, hakuwa na habari kwamba, kule nje, Angel aliyekuwa anapigania kumuokoa, hakuwa anahitaji kuokolewa na mtu yeyote yule.

​Endelea...
​Taa ndogo nyekundu iliyokuwa inapepesuka juu ya mlango wao ilitoa mlio mdogo sana uliofichwa na sauti ya mawimbi ya nje, tiiih, kisha ikabadilika na kuwa ya rangi ya kijani.
​Adrian alibaki ametoa macho, asiamini kile anachokiona. Mlango mzito wa chuma uliokuwa tegemeo la Khumalo Thembi na Romeo kuwafungia, uliteleza na kufunguka kimya kimya kama vile ulikuwa unasubiri amri kutoka kwa Manu.
​Manu aliinua mkono kumpa Adrian ishara ya kubaki kimya. Alichungulia kwenye korido ndefu iliyokuwa na mwanga hafifu wa bluu. Hakukuwa na mlinzi yeyote kwa wakati huo. Hili lilikuwa kituo kinachotegemea zaidi ulinzi wa mifumo ya kompyuta na ulinzi wa kiasili wa kuwa chini ya maji, kuliko walinzi wa kibinadamu.
​"Nifuate kwa tahadhari, ukikanyaga sakafu hakikisha unatumia ncha za vidole, sitaki mwangwi," Manu alinong'ona. Adrian alitikisa kichwa, woga ukiwa bado umemjaa lakini imani yake kwa Manu ikiwa imeongezeka mara dufu.
​Waliteleza kwenye korido hiyo kama vivuli. Baada ya kupita milango mitatu iliyofungwa, Manu alisimama ghafla mbele ya mlango ulioandikwa 'Server Room - Access Restricted'.
​Kwa kutumia kilekile kifaa chake kidogo, Manu aliingilia mfumo wa mlango huo na kuufungua. Ndani, chumba kilikuwa na baridi kali sana kikisheheni makabati makubwa ya kompyuta zilizokuwa zikihifadhi data za kituo kizima. Manu alikimbilia kwenye kompyuta kuu, vidole vyake vikaanza kucheza kwenye keyboard kwa kasi ya ajabu.
​"Unafanya nini, Manu? Si tutafute njia ya kutokea juu?" Adrian aliuliza kwa hofu huku akichungulia mlangoni, akihofia Khumalo Thembi kutokea muda wowote.
​"Kutoroka bila kujua tuko wapi ni sawa na kujitupa kwenye taya za papa," Manu alijibu huku macho yake yakisoma mistari ya data iliyokuwa ikishuka kwa kasi kwenye skrini. "Kwanza, nahitaji ramani ya jengo hili. Pili, nahitaji kujua mifumo yao ya ulinzi. Tatu..." Manu alinyamaza ghafla, uso wake ukionyesha mshtuko mzito.
​"Nini mbaya?" Adrian alisogea karibu.
​"Hawa watu hawajengi tu 'Clones'... Adrian, huu mtandao umeunganishwa moja kwa moja na ngome kuu ya Naibu Rais Rihadh Gahag. Na baya zaidi... kuna shehena ya kalamu kama ile yangu inatengenezwa hapa! Wanaiba teknolojia yangu kuunda jeshi la majasusi wasioonekana," Manu alikunja ngumi kwa hasira. Kisha akabonyeza kitufe cha kuhifadhi taarifa hizo kwenye kile kifaa chake. "Sasa najua pa kutokea. Kuna chombo kidogo cha majini (Submersible) upande wa mashariki wa kituo hiki. Twende haraka.

​Chumba cha Hoteli – Moscow, Urusi
​Sauti ya tii... tii... tii... ilikuwa ikizidi kuongezeka kasi chini ya kiti alichofungiwa Abdul. Taa nyekundu ya bomu hilo dogo ilikuwa ikimulika usoni mwake kama jicho la shetani linalomsubiri ameze roho yake.
​Abdul aliangalia chini kwa tabu. 00:45. Sekunde arobaini na tano zilibaki kabla chumba hicho hakijageuka majivu. Jasho jembamba lilitiririka kutoka usoni mwake na kuingia machoni, lakini hakuwa na muda wa kufuta.
​Kama kulikuwa na kitu kimoja alichojivunia Abdul, ni mafunzo yake magumu ya kuvumilia maumivu ya kifo aliyopitia ughaibuni. Alijua kamba za nailoni haziwezi kukatika kwa kuvutwa tu; jinsi anavyojivuta ndivyo zinavyozidi kumkaba. Alihitaji kulegeza mkono wake mmoja hata kama itamgharimu kiungo.
​Alivuta pumzi nzito sana, akauelekeza mkono wake wa kulia kwenye pembe kali ya chuma cha kiti kwa nyuma. Kwa kutumia nguvu zake zote za mwili, na huku akiuma meno kuzuia kelele zisimtoke, Abdul alipindua kidole chake cha gumba (thumb) kwa nguvu dhidi ya chuma kile.
​Crrrack! Sauti ya mfupa ulioteguka ilisikika chumbani humo. Maumivu makali kama ya kupigwa na shoti ya umeme yalipita mwili mzima wa Abdul. Lakini kidole kilipoteguka, kiganja chake kilipungua upana. Kwa kutumia damu iliyokuwa inatoka kwenye mchubuko kama kilainishi, alitelezesha kiganja chake taratibu na kukitoa kwenye kitanzi cha ile kamba ngumu.
​00:15... 00:14... 00:13...
​Akiwa ameutumia mkono ulioteguka kidole kwa taabu, alifungua kamba za mkono wa kushoto na kisha miguu. Alijitupa sakafuni na kutazama lile bomu. Lilikuwa bomu la kidijitali lililounganishwa na nyaya tatu; nyekundu, nyeusi, na ya njano.
​Abdul, akijua mbinu nyingi za walipuaji kutoka Mashariki ya Kati, alijua kwamba kukata waya uliounganishwa na saa (timer) si suluhisho, bali ni lazima akate waya unaopeleka moto kwenye baruti yenyewe.
​00:05... 00:04...
​Hakusita, alivuta kwa nguvu waya wa njano kwa kutumia meno yake.
​Saa ilisimama kwenye 00:01.
​Chumba kilijawa na ukimya wa kutisha. Abdul alianguka chali sakafuni akihema kwa nguvu, kifua chake kikipanda na kushuka. Alijishika mkono wake wa kulia na kukirudisha kidole chake cha gumba mahali pake kwa kishindo, Pwaah! Akasimama taratibu, macho yake yakiwaka moto wa kisasi usiomithilika. Yule Clone aliyemuacha hapo alifanya kosa moja kubwa; hakuhakikisha Abdul amekufa.
​"Utanikoma. Wewe si Angel. Wewe ni shetani aliyevalia ngozi ya mwanamke," Abdul alinong'ona kwa sauti iliyojaa chuki, huku akiokota koti lake tayari kuingia mitaa ya Urusi kumsaka Ninja huyo.

​Mitaa ya Moscow – Karibu na Kanisa la Saint Basil
​Baridi ya usiku ya Urusi ilikuwa kali, lakini Angel aliyekuwa akitembea mitaani alionekana kutojali kabisa. Alikuwa amevalia koti jeusi refu lililoficha suti yake ya kijasusi ya ndani. Macho yake makali yalikuwa yakitazama minara maarufu ya Kanisa la Mtakatifu Basil kwa mbali.
​Angel aliinua mkono na kubonyeza kifaa kidogo kilichokuwa sikioni mwake, mawasiliano yakafunguka kwa njia ya usimbaji (encrypted channel) kuelekea chini ya Bahari ya Hindi.
​"Romeo," Angel aliongea kwa sauti baridi. "Abdul ameondolewa. Sidhani kama atakuwa na uwezo wa kuleta shida tena. Nimewaweka Risasi Tatu chini ya udhibiti wangu."
​Sauti nzito, iliyobadilishwa kimtandao ya Romeo ilisikika sikioni mwake. "Kazi nzuri sana. Sasa, fuatilia mawimbi ya ile kalamu iliyoko hapo Moscow. Kuna mzigo tunauhitaji kabla Henessa na watu wake hawajautia mikononi. Usifanye makosa."
​"Sijawahi kufanya makosa," Angel alijibu kwa kujiamini na kukata mawasiliano.
​Angel alitoa simu yake maalum ambayo ilikuwa na ramani inayomulika alama moja ya kijani inayosogea. Alama hii ilikuwa ni signal ya moja ya zile kalamu za siri za Manu. Angel hakujua kwamba, harakati hizi alizokuwa anazifanya ndizo haswa zilizomfanya Mafaa Henessa amuone kupitia kompyuta yake kule Palestina akiwa kama "Ninja" anayepanda na kushuka dari la kanisa hilo usiku huu.
​Mchezo ulikuwa umefika patamu. Wakati Manu alikuwa akiiba ramani na kutafuta njia ya kutoroka chini ya bahari, Angel aliyekuwa Urusi alikuwa akijipanga kutikisa ulimwengu wa ujasusi akifuata kalamu ya siri. Na Abdul, akiwa ameponyoka mauti ya sekunde moja, alikuwa nyuma yake kama mzimu unaotafuta damu.

Itaendelea...
... views
Advertisement

Comments ()